Dondoo za Mapishi na Lishe

Jinsi ya kupika Labania Za Maziwa

Viamba upishi

Maziwa ya unga 2 vikombe

Sukari 3 vikombe

Maji 3 vikombe

Unga wa ngano ½ kikombe

Mafuta ½ kikombe

Iliki kiasi

Jinsi ya kuandaa na kupika

Paka sinia mafuta kabla ya kupika labania
Katika sufuria chemsha maji na sukari pamoja na iliki mpaka inate vizuri
Kisha mimina mafuta koroga
Halafu mimina unga wa ngano na ukoroge haraka haraka
Kisha tia unga wa maziwa, endelea kukoroga usiwe na madonge mpaka uwe rangi ya browni isiokoleza.
Kisha mimina mchanganyiko kweye sinia uliyoipaka mafuta, iwache ipoe na kata kata upendavo na itakuwa tayari.

Jinsi ya kupika Wali Wa Sosi Ya Tuna

Viambaupishi

Sosi Ya tuna

Tuna (samaki/jodari) 2 Vikopo

Vitunguu (kata kata) 4

Nyanya zilizosagwa 5

Nyanya kopo 3 Vijiko vya supu

Viazi (vilivyokatwa vipande vidogo – cubes) 4

Dengu (chick peas) 1 kikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic)&Tangawizi iliyosagwa 1 Kijiko cha supu

Hiliki 1/4 kijiko cha chai

Mchanganyiko wa bizari 1 kijiko cha supu

Chumvi kiasi

Pilipili manga 1 Kijiko cha chai

Vipande cha Maggi (Cube) 2

Wali

Mchele 3 Vikombe vikubwa (Mugs)

Mdalasini 2 Vijiti

Karafuu chembe 5

Zaafarani kiasi

*Jirsh (Komamanga kavu au zabibu kavu -raisins) 1/2 Kikombe

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Kosha Mchele na roweka.

2. Kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi (brown) chuja mafuta uweke kando.

3. Kaanga viazi, epua

4. Punguza mafuta, kaanga nyanya.

5. Tia thomu/tangawizi, bizari zote, vipande vya Maggi, nyanya kopo, chumvi.

6. Mwaga maji ya tuna iwe kavu, changanyisha kwenye sosi.

7. Tia zaafarani kidogo katika sosi na bakisha ya wali.

8. Chemsha mchele pamoja na mdalasini na karafuu.

9. Karibu na kuwiva, chuja maji utie katika chombo cha kupikia katika jiko (oven)

10. Nyunyizia zaafarani, mwagia vitunguu, viazi, na dengu juu ya wali.

11. Mwagia sosi ya tuna na pambia jirshi (au zabibu).

12. Funika wali na upike katika jiko moto wa 450º kwa muda wa kupikika wali.

* Jirsh (komamanga) kavu zioshwe vizuri kutoa vumbi au tumia zabibu kavu (raisins)

Jinsi ya kupika Vileja Vya Tambi

Viambaupishi

Tambi (vermiceli Roasted) Mifuko 2

Siagi 4 Vijiko vya supu

Maziwa (condensed) 300Ml

Lozi zilizokatwakatwa 1 kikombe

Zabibu kavu 1 Kikombe

Arki (essence) 1 Kijiko cha supu

Jinsi ya kuandaa na kupika

1) Weka karai kwenye moto kiasi

2) Tia siagi

3) Tia tambi uzikaange usiachie mkoni mpaka ziwe rangu ya dhahabu.

4) Weka lozi na zabibu huku unakoroga

5) Tia maziwa na huku unakoroga usiachie mkono.

6) Tia arki

7) Epua karai, tumia kijiko cha chai kwa kuchotea na utie kwenye kikombe cha kahawa nusu usikijaze.

8) Kipindue kwenye sahani utoe kileja.

9) Fanya hivyo mpaka umalize vyote.

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Nazi Wa Nyanya Chungu/Mshumaa/Ngogwe Na Bamia, Mboga Ya Matembele Na Samaki Wa Kukaanga

Vipimo Vya Ugali

Unga wa mahindi – 4

Maji – 6 kiasi kutegemea na aina ya unga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka maji katika moto.

Tia unga kidogo katika kibakuli, koroga ufanye uji.

Maji yakichemka tia kwenye maji uwe uji.

Ujii ikiiva punguza kidogo tia unga kidogokidogo na usonge ugali. Ikiwa unga ni mgumu utaongeza maji ya ule uji ulopunguza usonge hadi uive ukiwa tayari.

Vipimo Vya Mchuzi Wa Nazi Kwa Nyanya Chungu/Mshumaa/Ngogwe Na Bamia

Nyanya chungu/mshumaa/Ngogwe – 7

Bamia – 10

Kitunguu maji – 2

Nyanya/tungule – 2

Tui la nazi jepesi – 2 viwili

Tui la nazi zito – 2

Chumvi – kiasi

Ndimu – 2 mbili kamua

Bizari manjano/haldi/turmeric – ½ kijiko cha chai

Pilipili mbuzi – 3

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata kitunguu maji na nyanya vipande vidogodogo sana kisha weka katika sufuria.

Iache ichemke kwa maji yake ya nyanya, ikishachemka tia maji kidogo kama robo kikombe.

Tia nyanya chungu, bamia na koleza ndimu, chumvi.

Iache ichemke. Inapokuwa tayari imeiva tia tui jepesi endelea kuacha katika moto huku unakoroga kidogo kidogo.

Tui jepesi likipungua kiasi chake, tia tui zito, kisha usiachie mkono koroga ikichemka kidog kiasi cha kuiva tui mchuzi tayari.

Vipimo Vya Mboga Ya Matembele

Matembele – 5 mafungu

Mafuta – ¼ kikombe

Kitunguu maji kilokatwakatwa – 1

Nyanya/tungule – 4

Chumvi – 1

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Punguza miche ya matembele kwa kuikata ncha kisha osha majani yake. Acha yachuje maji .
Weka mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu maji na nyanya hadi viivie.
Tia mboga, Iache ichemke kwa maji yake hadi iive. Ukiona bado haikuiva tia maji kidogo tu.
Ukipenda unatia ndimu kiasi cha kipande kimoja ukamue .

Samaki Wa Nguru Wa Kukaanga

Samaki Wa Nguru – 4 vipande

Kitunguu saumu(thom/galic) na tangawizi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi – 4

Ndimu – 2 kamua

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Mwoshe samaki kisha mtie kitunguu thomu, tangawizi ilosagwa, chumvi, pilipilimbichi ilosagwa, ndimu na bizari ya samaki.
Mwache akolee viungo kwa muda kidogo.
Makaange katika mafuta hadi aive akiwa tayari.

Jinsi ya kuandaa Vileja Vya Karanga

MAHITAJI

Mayai 5

Sukari 450gm (1 lb)

Unga wa Ngano 1 kg

Siagi 450gm (1 lb)

Baking powder ½ Kijiko cha chai

Unga wa Custard Vijiko 2 vya chakula

Karanga za kusaga 250gm

Jam ½ kikombe

MAANDALIZI

Chukua bakuli la kiasi, weka sukari na siagi.
Changanya sukari na siagi kwa kutumia mashine ya kukorogea keki (cakemixer), mpaka sukari ichanganyike na siagi.
Vunja yai moja moja na weka kiini chake kwenye mchanganyiko wa sukari na siagi, endelea kuchanganya mpaka ichanganyike vizuri. Hifadhi ute wa mayai ndani ya kibakuli.
Mimina unga wa ngano ndani ya mchanganyiko wako huku ukichanganya Changanya unga wa custard na baking powder.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Vichovye viduara ndani ya ute wa yai kisha zimwagie unga wa karanga na kuzipanga kwenye tray ya kuchomea.
Weka dole gumba kati kati ya kila kiduara na uweke jam.
Washa jiko (oven) 350F na uchome vileja vyako kwa dakika 20.
Toa vileja vyako vipoe na uviweke ndani ya sahani tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Pilau Ya Nyama Na Mtindi

MAHITAJI

Nyama iliyokatwa vipande – 1 Ratili(LB)

Mchele Basmati – 2 Magi

Chumvi ya wali – kiasi

Kitungu kilichokatwa katwa – 1 kikubwa

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi – 1 kijiko cha supu

Mtindi (yogurt) – ½ kikombe

Mchanganyiko wa bizari ya pilau ya tayari – 2 vijiko vya supu

Mafuta kidogo yakukaangia

Rangi ya manjano (ukipenda)

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Osha mchele na roweka nusu saa .

Weka mafuta katika sufuria na kaanga vitungu mpaka viwe rangi ya hudhurungi (brown).

Tia thomu na tangawizi na ukaange kidogo.

Kisha weka bizari ya pilau halafu nyama huku unakaanga hadi nyama isiwe nyekundu tena.

Tia maji gilasi 1½- 2 ichemke mpaka nyama iwive na karibu kukauka.

Mimina mtindi na iachie moto mdogo ikauke kidogo.

Kwenye sufuria nyingine chemsha mchele pamoja na chumvi na mafuta kidogo mpaka uive.

Mimina wali juu ya nyama, kisha nyunyiza rangi (ukipenda) kama vile wali wa biriani na ufunike kwa dakika kumi hivi.

Changanya wali na nyama pamoja ikiwa tayari kuliwa.

Mapishi ya Pilau Ya Sosi Ya Soya Na Mboga

Viambaupishi

Kuku (mkate mkate vipande) 1

Mchele wa Basmati (rowanisha) 3 magi

Mdalasini 1 mchi mmoja

Vitunguu maji (vilivyokatwa vyembamba) 6

Mchanganyiko wa mboga za barafu 1 magi

(karoti, mahindi, njegere)

Kabichi (iliyokatwa katwa nyembamba) 1 magi

Pilipili mbichi (iliyosagwa) 3

Pilipili boga iliyokatwa vipande vidogo vidogo 1

Pilipili manga 1 kijiko cha chakula

Chumvi 1 kijiko cha chakula

Sosi ya soya (soy sauce) 5 vijiko vya chakula

Kotmiri iliyokatwa katwa 1 magi

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa 2 vijiko vya chakula

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Tia mafuta ndani ya karai. Yakipata moto kiasi, mimina vitunguu maji na mdalasini 1 mzima kaanga. Itachukua muda kidogo. Kaanga mpaka viwe rangi ya hudhurungi (brown). Viepue na uweke kando.

2. Ndani ya sufuria kubwa, mimina kuku, chumvi, thomu na tangawizi, sosi ya soya, pilipili manga, pilipili mbichi, chemsha mpaka kuku awive na maji yakauke.

3. Changanya vitunguu ulivyokaanga, kabichi, pilipili, mboga, kotmiri, mchanganyiko wa mboga za barafu na weka kwa muda wa dakika tano au kumi. Tia na mafuta kidogo uliyokaangia vitunguu .

4. Chemsha mchele na chumvi uwive kama kawaida ya kupika wali wa kuchuja. Ukishauchuja umwagie katika masala ya kuku.

5. Nyunyizia mafuta kidogo uliokaangia vitunguu.

6. Weka moto mdogo mpaka wali ukishawiva. Uchanganye ukiwa tayari kwa kuliwa.

KIDOKEZO:

Unaweza kuupika wali huo ndani ya jiko, yaani badala ya kutia masala kwenye sufuria ukayatia katika bakuli au treya ya jiko (oven), kisha ukamwagia wali uliouchuja humo na kuupika kaitka moto wa 400-450 Deg kwa muda wa dakika 15-20.

Jinsi ya kupika Biskuti Nyembamba (Wafer Bar) Za Chokoleti Na Njugu

MAHITAJI

Wafer Powder/gram wafer (unga wa biskuti uliosagwa wa tayari) – vikombe 2

Maziwa ya Mgando Matamu ya Kopo – 2 vikombe

Nazi iliyokunwa – ½ Kikombe

Chokoleti vipande vipande – 1 Kikombe

Njugu vipande vipande – ½ Kikombe

Siagi – 227 g

MAPISHI

Yeyusha siagi motoni kisha changanya na unga wa wafer acha kidogo motoni
Mimina katika treya unayochomea itandaze vizuri, kisha mimina maziwa juu yake pamoja na njugu vipande , nazi iliyokunwa na vipande vya chokoleti.
Choma (bake) kwenye oveni kwa moto wa 350ºC kwa dakika 20.
Katakata tayari kwa kuliwa

Mapishi ya chipsi

Mahitaji

Viazi (potato) 1/2 kilo
Mafuta ya kukaangia (veg oil)
Chumvi

Matayarisho

Menya viazi kisha vioshe na vikaushe maji yote kwa kutumia kitchen towel.Baada ya hapo katakata katika shape ya chips uzipendazo either nyembamba au nene kisha zikaushe tena maji na uzitie chumvi. Baada ya kuzitia chumvi tu zitie kwenye mafuta ya kukaangia straightaway (hakikisha mafuta yasiwe ya moto sana kwani utazibabua) Zipike upande mmoja ukiiva geuza upande wa pili. Baada ya hapo endelea kuzipika uku ukiwa unazigeuzageuza mpaka kwa nje ziwe light brown na crisps.Baada ya hapo zitoe na uziweke kwenye kitchen towel ili zichuje mafuta na zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika Pilau Ya Nafaka Na Nyama Ya Kusaga

Viambaupishi

Mchele 3 vikombe

Nyama ya kusaga 1 LB

Mchanganyiko wa Nafaka (upendavyo) 1 kikopo

(maharagwe, njegere, mbaazi, na kadhalika)

Vitunguu maji kata vipande vipande 3 vya kiasi

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi 2 vijiko vya supu

Mafuta ½ Kikombe

Mchanganyiko wa bizari (Garam Masala) 2 vijiko vya chai

Vipande vya supu (Maggi cubes) 3

Maji (inategemea mchele) 5

Chumvi Kiasi

Jinsi ya kuandaa na kupika

1) Osha mchele na roweka.

2) Weka mafuta katika sufuria na kaanga vitunguu mpaka viwe brown.

3) Tia Thomu na tangawizi, kaanga kidogo.

4) Weka nyama ya kusaga, chumvi na garam masala, endelea kukaanga mpaka nyama iwive.

5) Mwaga maji yaliomo katika kopo la nafaka na utie nafaka pekee humo.

6) Tia maji na vipande vya supu (Maggi cubes) huku unavivuruga, koroga kidogo.

7) Tia mchele, koroga kidogo.

8) Funika na pika kwa moto mdogo mpaka karibu na kukauka ukikorogoka kidogo. (kama unavyopika pilau ya kawaida)

9) *Epua uipike katika moto wa oven 350-400 Deg kwa muda wa dakika 15.

*Kama sufuria uliyotumia sio ya kupikia katika oven, mimina katika chombo chochote kinachotumika kwa oven kama bakuli la pyrex au treya za foil.

10) Pakua katika sahani na iko tayari kuliwa.

Mapishi ya Half cake (Keki)

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) kikombe 1na 1/2
Sukari (sugar) 1/4 kikombe
Barking powder 1/2 kijiko cha chai
Magadi soda (bicarbonate soda) 1 kijiko cha chai
Mafuta 2 vijiko vya chai
Mafuta ya kukaangia
Maji ya uvuguvugu kiasi

Matayarisho

Changanya unga na vitu vyote (kasoro mafuta ya kuchomea) kisha ukande (hakikisha unakuwa mgumu) Baada ya hapo sukuma na ukate shape uipendayo (hakikisha unakata vipande vinene kiasi na sio kama mandazi) Baada ya hapo ziweke sehemu yenye joto na uache ziumuke. Zikisha umuka zikaange katika moto mdogo ili ziive mpaka ndani. Zikisha iva zitoe na uziweke katika kitchen towel ili zichuje mafuta. Ziache zipoe na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya wali wa Kiafrika Mangaribi

Mahitaji

Mchele (rice vikombe 2 na 1/2)
Vitunguu (onion 2)
Nyanya ya kopo (tin tomato kopo 1)
Tangawizi (ginger paste kijiko 1 cha chakula)
Kitunguu swaum (garlic paste kijiko 1 cha chakula)
Paprika (kijiko 1 na 1/2 cha cha chai)
Pilipil (scotch bonnet pepper 1)
Curry powder (kijiko 1 cha chai)
Maggi cubes 3(unaweza kutumia yenye ladha ya chicken, beef au vegetable. Inategemea unasevu na mchuzi wa aina gani)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Loweka mchele kwa muda wa dakika 10.Katakata vitunguu kisha weka pembeni, saga pamoja nyanya ya kopo,pilipili, tangawizi na kitunguu swaum kisha weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu vikiiva tia curry powder, maggi cubes, chumvi na paprika na uchanganye vizuri. Kisha tia mchanganyiko wa nyanya na uupike mpaka uive. Baada ya hapo tia mchele na maji na uupike mpaka ukaribie kuiva kisha ugeuze na umalizie kwa kutia njegere na umalizie kuupika mpaka uive. baada ya hapo utakuwa tayari kuseviwa na mboga yoyote kama kuku, nyama, samaki au assorted meat (Mchanganyiko wa utumbo, makongoro na nyama), Hapo mimi nili-save na mchuzi wa kuku wa kienyeji.

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Tangawizi

MAHITAJI

Unga – 2 Vikombe

Cocoa ya unga – 1 Kijiko cha supu

Sukari ya hudhurungi – 1 Kikombe

Siagi – ¾ Kikombe

Yai – 1

Molasses – ¼ Kikombe

Baking soda – 2 vijiko vya chai

Mdalasini wa unga – 1 kijiko cha chai

Tangawizi mbichi – 1 kijiko cha supu

Karafuu ya unga – ½ kijiko cha chai

Chumvi ½ kijiko cha chai

Vanilla ½ kijiko cha chai

MAANDALIZI

Katika bakuli, chunga unga, baking soda, chumvi na cocoa. Weka kando.
Washa oven lipate moto huku unatayarisha biskuti.
Katika bakuli jengine, mimina siagi na sukari upige kwa mashini ya keki hadi mchanganyiko uwe laini kama dakika mbili.
Mimina molasses na yai ndani ya mchanganyiko wa siagi na sukari uchanganye vizuri.
Mimina unga kidogo kidogo huku unachanganya na mwiko hadi unga wote umalizike.
Mimina mdalasini, karafuu na tangawizi, changanya vizuri.
Weka mchanganyiko wako ndani ya friji kama masaa mawili. (Ukipenda unaweza kuhifadhi mchanganyiko wako ndani ya mfuko wa freezer na uoke siku nyengine.)
Tengeneza viduara vidogo vidogo.

Chovya kila kiduara katikati sukari, kisha panga kwenye treya ya kuoka

Rudisha viduara katika friji kama nusu saa.

Oka katika oven 350ºF kwa muda wa dakika 15.

Toa biskuti kwenye oven na uache zipoe kama dakika kumi.
Panga kwenye sahani tayari kuliwa.

Namna ya kutengeneza Visheti Vya Nazi Na Njugu (Sudani)

VIAMBAUPISHI

Unga – 3 mug za chai

Samli – ½ mug ya chai

Maziwa – 1¼ mug ya chai

Baking powder – 2 vijiko vya chai

VIAMBAUPISHI VYA MJAZO

Njugu zilizomenywa vipande vipande – 2 vikombe cha chai

Sukari – ½ kikombe cha chai

Iliki – 1 kijiko cha chai

Nazi iliyokunwa – 2 vikombe vya chai

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 2 vikombe vya chai

Maji – 1 kikombe cha chai

Ndimu – 1

JINSI YA KUVIANDAA

1-Changanya unga na samli kisha tia baking powder na maziwa. Ukande ulainike kisha

uwache kama dakika 5 uumuke.

2-Kwenye bakuli nyingine changanya njugu, sukari na iliki.

3-Kata madonge madogo dogo sukuma kila donge duara jembamba, kisha tia kijiko cha mchanganyiko wa njugu juu yake ifunikie juu yake na ibane pembeni.

4-Panga kwenye treya isiyoganda (non stick) kisha choma kwenye oven kwa moto wa chini

(bake) 350° C kwa dakika kama 15-20.

5-Chemsha maji na sukari katika sufuria ndogo kisha tia ndimu acha ichemke mpaka inatenate unapoigusa.

6-Kwenye sahani ya chali mimina nazi iliyokunwa.

7-Vibiskuti vikiwa tayari vya motomoto chovea kwenye shira kisha zungushia katika nazi iliyokunwa,

panga kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About