Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Half cake (Keki)

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) kikombe 1na 1/2
Sukari (sugar) 1/4 kikombe
Barking powder 1/2 kijiko cha chai
Magadi soda (bicarbonate soda) 1 kijiko cha chai
Mafuta 2 vijiko vya chai
Mafuta ya kukaangia
Maji ya uvuguvugu kiasi

Matayarisho

Changanya unga na vitu vyote (kasoro mafuta ya kuchomea) kisha ukande (hakikisha unakuwa mgumu) Baada ya hapo sukuma na ukate shape uipendayo (hakikisha unakata vipande vinene kiasi na sio kama mandazi) Baada ya hapo ziweke sehemu yenye joto na uache ziumuke. Zikisha umuka zikaange katika moto mdogo ili ziive mpaka ndani. Zikisha iva zitoe na uziweke katika kitchen towel ili zichuje mafuta. Ziache zipoe na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kutengeneza Labania Za Maziwa

MAHITAJI

Maziwa ya unga – 2 vikombe

Sukari – 3 vikombe

Maji – 3 vikombe

Unga wa ngano – ½ kikombe

Mafuta – ½ kikombe

Iliki – kiasi

MAPISHI

Paka sinia mafuta kabla ya kupika labania
Katika sufuria chemsha maji na sukari pamoja na iliki mpaka inate vizuri
Kisha mimina mafuta koroga
Halafu mimina unga wa ngano na ukoroge haraka haraka
Kisha tia unga wa maziwa, endelea kukoroga usiwe na madonge mpaka uwe rangi ya browni isiokoleza.
Kisha mimina mchanganyiko kweye sinia uliyoipaka mafuta, iwache ipoe na kata kata upendavo na itakuwa tayari.

Jinsi ya kupika Donati

Viamba upishi

Unga
2 Magi (kikombe kibuwa cha chai)

Sukari
1/3 Kikombe cha chai
Mayai 5

Siagi 4 Vijiko vya chakula

Hamira 1 Kijiko cha chakula

Baking Powder 1 Kijiko cha chai

Vanilla 1 Kijiko cha chai

Hiliki zilizosagwa 1 Kijiko cha chai

Sukari ya laini ya unga

(icing sugar) 1 Magi

Jinsi ya kuandaa na kupika

Unavunja mayai, unatia sukari, hamira, baking powder, vanilla na hiliki ikisha unapiga kwa kutumia mchapo wa kupigia keki. Unapiga mchanganyiko kwa muda wa dakika tano.

Unatia siagi kwenye sufuria na unaiyayusha na kuipasha moto mpaka iwe moto ikisha unaimimina kwenye mchanganyiko na unapiga tena kwa dakika mbili tu.

Unatia unga kwenye sinia au bakuli kubwa ikisha unamimina ule mchanganyiko kwenye unga na unaukanda kutumia mkono, mpaka ulainike.

Ukiona unga mwingi basi ongeza maziwa kidogo mpaka uwe sawa, na ukiona unga mwepesi sana basi unaweza kuongeza unga kidogo pia mpaka ukae sawa mfano wa unga wa maandazi.

Sukuma na ukate madonge kama unavyoyaona hapo juu. Tumia kifuniko cha chupa kwa kukatia kiduara kidogo katikakti ya madonge.
Ukimaliza kukata madonge yote, yaweke kidogo yavimbe halafu teleka mafuta na uyachome.
Ukitoa kwenye mafuta yachuje moto na kabla ya kupoa yawe moto moto yarovye kwenye icing sugar na uhakikishe yote yameenea sukari juu.
Ukimaliza tia kwenye sahani acha zipowe na zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika Biskuti Ya Keki Kavu kwa kizungu Shortcake

Viamba upishi

Unga 2 Magi (vikombe vya chai)

Sukari iliyosagwa 2/3 Magi (kikombe cha chai)

Siagi   220 g

Unga wa mchele ½ Magi

Yai 1

Vanilla 1 kijiko cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Changanya vitu vyote hivyo kwenye bakuli mpaka unga ushikamane.

2. Paka mafuta treya ya kuchomea kisha utandaze kwenye treya ya 20cm kwa 30 cm au (8 in kwa 12 in)

3. Choma kwenye moto 325˚C kwa muda wa saa nzima au mpaka ibadilike kuwa rangi ya dhahabu.

4. Epua acha ipoe kisha kata vipande kama mstatili, weak kwenye sahani tayari kunywewa na chai.

Mapishi – Kisamvu cha Karanga

Mapishi yetu leo ni kisamvu cha kuchanganya na karanga. Karibu.

Mahitaji

Majani ya kisamvu
Karanga nusu kikombe
kitunguu kimoja
nyanya mbili
karoti moja
mafuta na chumvi kiasi

Matayarisho

1. Osha kisamvu chako vizuri kisha katakata vipande vidogo vidogo

2. Unaweza kutwanga kwa kutumia kinu au kuchemsha kidogo na kisha kusaga kwa kutumia mashine. Ukitumia mashine uwe makini usije ukasaga sana ukaharibu.

3. Kaanga karanga kidogo na kisha zisage ziwe unga unga.

4. Chemsha kisamvu chako hadi kiive.

5. Katakata kitunguu, karoti na na nyanya

6. Anza kuunga kisamvu kwa kukaanga vitunguu, weka karoti na kisha nyanya na vikishaiva weka kisamvu na koroga pamoja kisha weka karanga. Acha vichemke kwa muda na unaweza pia weka na nazi tui la kwanza.

7. Baada ya muda mfupi epua na kitakiwa tayari. Waweza kula kwa ugali, wali, chapati, makande n.k

Jinsi ya kupika Pilau ya Nyama ya Kusaga Na Mboga Mchanganyiko

Mahitaji

Mchele – 2 Mugs

Viazi – 3

Nyama ya Kusaga – 1 Pound

Mboga mchanganyiko za barafu – 1 Mug

(Frozen vegetable)

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi – 2 vijiko vya supu

Garam masala – 1 kijiko cha supu

Nyanya – 1

Kitungu maji – 1

Mdalasini nzima – 1 vijiti

Karafuu – 3 chembe

Pilipili mbichi – 1

Chumvi – kiasi

Maji – 2 ½ Mugs

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele na uroweke kiasi kutegemea aina ya mchele.
Katakata viazi kaanga katika mafuta, toa weka kando.
Tia mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu maji mpaka kigeuke rangi ya hudhurungi (brown).
Tia nyama ya kusaga, thomu na tangawizi, pilipili, bizari zote na chumvi. Kaanga hadi nyama iwive.
Katakata nyanya uliyokatakata itie katika mchanganyiko wa nyama na endelea kukaanga kidogo tu.
Tia mboga ya barafu (frozen vegetables)
Tia maji, kidonge cha supu.
Yatakapochemka tia mchele.
Punguza moto uwe mdogo funika kwa muda wa ½ saa hadi wali ukauke na uwive. Utakuwa tayari kuliwa.

Mapishi ya Wali Wa Nazi Wa Adesi, Bamia Na Mchuzi Wa Kamba

Mahitaji

Mchele – 2 vikombe

Adesi -1 ½ vikombe

Nazi ya unga – 1 Kikombe

Maji (inategemea mchele) – 3

Chumvi – Kiasi

Vipimo Vya Bamia:

Bamia – ½ kilo

Vitunguu maji – 2 vya kiasi

Nyanya iliyosagwa – 1 kubwa

Nyanya ya kopo – 2 vijiko vya chai

Pilipili manga – ½ kijiko cha chai

Mafuta – 3 vijiko vya chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika:

Wali wa adesi

Osha na roweka mchele na adesi .
Chuja nazi kwa vikombe 3 vya maji tia chumvi kisha weka jikoni.
Tui la nazi likishachemka tia mchele na adesi pamoja. Punguza moto, funika wali upikike kwa moto mdogo mpaka ukauke vizuri.

Bamia

Katakata bamia vipande vya kiasi/ Katakakata vitunguu weka kando.
Katika sufuria tia mafuta na kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi.
Tia nyanya ilosagwa na nyanya ya kopo na pilipili manga na chumvi.
Kisha Tia bamia punguza moto mdogo mdogo mpaka ziwive.

Vipimo: Mchuzi Wa Kamba

Kamba – 1Lb

Vitunguu vilokatwa katwa – 2

Nyanya ilokatwa katwa – 2

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 Kijiko cha chai

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 Kijiko cha chai

Bizari ya mchuzi (curry powder) – ½ Kijiko cha chai

Haldi – bizari ya manajano – ½ kijiko cha chai

Nyanya ya kopo – ½ Kijiko cha chai

Ndimu – 1

Chumvi – Kiasi

Mafuta ya kukaangia – 2 Vijiko vya supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Kaanga vitunguu kidogo hadi vilainike,
Tia nyanya, thomu na piilipili mbichi. Endelea kukaanga, tia nyanya ya kopo, chumvi, bizari zote.
Tia tia kamba na huku unakoroga mpaka wabadilike rangi na kuwiva. Kamulia ndimu na mchuzi uko tayari.

Mapishi ya Boga La Nazi

Vipimo

Boga la kiasi – nusu yake

Tui zito la nazi 1 ½ gilasi

Sukari ½ kikombe

Hiliki ½ kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Menya boga kisha katakata vipande vya kiasi.
Weka katika sufuri tia maji kiasi ya kuchemshia na kuwiva bila ya kubakia maji mengi.
Changanya tui na sukari na hiliki kisha mimina juu ya boga wacha katika moto dakika chache tu bila ya kufunika.
Epua mimina katika chombo likiwa tayari.

Mambo ya msingi kufahamu kuhusu Lishe

Nini maana ya lishe?

• Lishe yahusu mafunzo ya chakula na jinsi miili yetu inavyotumia chakula kamakichocheo cha ukuaji, kuzaana na utunzaji wa afya.
• Lishe inajumuisha mchakato wa utoaji virutubishi vinavyohitajika kwa afya, ukuaji, kuendelea na kuishi.

Umuhimu wa lishe bora

Lishe bora ni muhimu katika mambo yafuatayo

• Utoaji nishati ili kuishi, uwepo wa mwendo, utendaji kazi, na joto.
• Ukuaji, uendeleaji, ujengaji mwli, urejeshaji na utengenezaji wa seli na mikusanyika ya seli hizo (tishu)
• Ufanyaji michakato ya kikemia kama vile uyeyushaji chakula, umetaboli na utunzaji mwili.
• Kinga dhidi ya magonjwa, upigaji vita maambukizi na uponaji magonjwa.
• Ili afya njema iweze kudumishwa, mlo wa kila siku lazima ukamilishe shughuli nne zilizotajwa hapo awali. Vyakula vinavyokamilisha moja au zaidi ya shughuli tatu huitwa virutubishi.

Virutubishi

Aina za irutubishi vikuu tunavyohitaji kwa wingi. Hivi ni:

• kabohaidreti (vyakula vya wanga, sukari na vyakula vya ufumwele):
• mafuta yatokanayo na wanyama – haya yapo ya aina kadhaa
• Protini- kuna mamia ya aina mbalimbali za protini.
• Maji.

Virutubishi vidogovidogo tunavyohitaji kwa kiwango kidogo. Kuna aina nyingi ya hivi bali vile vinavyoelekea kukosekana kwenye mlo ni:

• madini – madini ya chuma (angalia Kisanduku cha 6, ukurasa 16), madini ya joto na zinki.
• vitamnini – vitamini A, vitamini za kundi B (ikiwemo folate) na vitamini C. Kama chakula chaweza kuwa chanzo bora cha kirutubishi au la hutegemea:
• Kiwango cha kirutubishi katika chakula. Vyakula vyenye viwango vingi vya virutubishi vidogovidogo kulinganisha na viwango vyake vya nguvu huitwa vyakula ‘vilivyosheheni virutubishi’ (nutrient-rich) au wakati mwingine huitwa vyakula vyenye ‘ujanzo mwingi’ wa virutubishi (nutrient dense). Vyakula hivi hupendwa kwa kuwa hutoa virutubishi vyote vinavyohitajika. Kiambatisho hiki kinaorodhesha vyakula vinavyotoa viwango muhimu vya virutubishi mbalimbali.
• Kiwango cha chakula kinachotumika mara kwa mara.

Mapishi ya Pilau Ya Kuku Kwa Mchele Mpya

Mahitaji

Mchele – 1 kilo

Kuku – 1

Vitunguu – 3

Viazi/mbatata – 5

Jira/bizari ya pilau nzima – 3 vijiko vya supu

Mdalasini – 1 kijiti

Pilipili manga – 1 kijiko cha supu

Hiliki – 3 chembe

Karafuu – 5 chembe

Kitunguu saumu(thomu/galic) kilosagwa – 3 vijiko vya supu

Tangawizi mbichi ilosagwa – 3 vijiko vya supu

Mafuta ya kupikia – ½ kikombe

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Baada ya kumsafisha kuku na kumkatakata, mchemshe kwa chumvi na ndimu, kijiko kimoja cha kitunguu thomu/somu na tangawizi yote..
Menya viazi, katakata vipande vya kiasi.
Katakata vitunguu maji kisha kaanga kwa mafuta katika sufuria ya kupikia pilau.
Tia bizari zote isipokuwa hiliki.
Saga hiliki kisha tia pamoja na kitunguu thomu/somu ukaange kidogo.
Mimina kuku na supu yake ikichemka kisha tia mchele na viazi.
Koroga kisha acha katika moto mdogomdogo wali uwive kama kawaida ya kupika pilau.

Mapishi ya wali wa Kiafrika Mangaribi

Mahitaji

Mchele (rice vikombe 2 na 1/2)
Vitunguu (onion 2)
Nyanya ya kopo (tin tomato kopo 1)
Tangawizi (ginger paste kijiko 1 cha chakula)
Kitunguu swaum (garlic paste kijiko 1 cha chakula)
Paprika (kijiko 1 na 1/2 cha cha chai)
Pilipil (scotch bonnet pepper 1)
Curry powder (kijiko 1 cha chai)
Maggi cubes 3(unaweza kutumia yenye ladha ya chicken, beef au vegetable. Inategemea unasevu na mchuzi wa aina gani)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Loweka mchele kwa muda wa dakika 10.Katakata vitunguu kisha weka pembeni, saga pamoja nyanya ya kopo,pilipili, tangawizi na kitunguu swaum kisha weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu vikiiva tia curry powder, maggi cubes, chumvi na paprika na uchanganye vizuri. Kisha tia mchanganyiko wa nyanya na uupike mpaka uive. Baada ya hapo tia mchele na maji na uupike mpaka ukaribie kuiva kisha ugeuze na umalizie kwa kutia njegere na umalizie kuupika mpaka uive. baada ya hapo utakuwa tayari kuseviwa na mboga yoyote kama kuku, nyama, samaki au assorted meat (Mchanganyiko wa utumbo, makongoro na nyama), Hapo mimi nili-save na mchuzi wa kuku wa kienyeji.

Mapishi ya tambi za kukaanga

Kupika tambi ni kama ifuatavyo

VIAMBA UPISHI

Tambi pakti moja

Sukari ¾ kikombe cha chai

Mafuta ½ kikombe cha chai

Iliki kiasi

Maji 3 Vikombe vya chai

Vanilla / Arki rose 1-2 Tone

Zabibu Kiasi (Ukipenda)

JINSI YA KUPIKA TAMBI ZAKO

1. Zichambue tambi ziwe moja moja.

2. Mimina mafuta kwenye sufuria yakisha pata moto mimina
tambi,zigeuzegeuze mpaka zibadilike rangi na kuwa brown.

3. Punguza mafuta kwa kuyachuja na zirudishe jikoni.

4. Nyunyizia iliki zilizosagwa koroga kidogo na mimina maji na tia arki
na acha zichemke mpaka maji yakikaribia kukauka mimina sukari
koroga kidogo na punguza moto.
5. Kisha tia zabibu ukipenda, zifunike ili zikaukie vizuri.

6. Zikishakauka pakua kwenye sahani tayari kwa kuliwa

Kidokezi: Itategemea na aina za Tambi unazopika kwa kukisia maji, kama utaona hazijaiva unaweza kuongeza maji kidogo.

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Kamba Wa Nazi, Kisamvu Na Kachumbari Ya Papa Mkavu

Vipimo – Ugali

Maji – 4 vikombe kiasi inategemea na unga wenyewe.

Unga wa sembe – 2 vikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Tia maji kiasi katika sufuria, weka motoni, yakipata moto korogea unga wa sembe kiasi na ufanye uji mzito uache uchemke vizuri huku ukikoroga.
Chota kibakuli kimoja cha uji huo weka pembeni kisha mimina unga wote uliobaki upigepige uchanganyike vizuri kwenye uji huo mpaka ushikamane
Punguza moto anza kuusonga taratibu huku ukiongeza ule uji ulioweka pembeni kidogo kidogo mpaka uone sasa umeshikamana vizuri.
Endelea kusonga mpaka ulainike kisha mimina kwenye bakuli au sahani iliyolowanishwa na maji kisha upete pete huku ukiugeuza geuza mpaka ukae shepu nzuri ya duara.Weka tayari kwa kuliwa.

Vipimo – Mchuzi wa kamba wa nazi

Kitunguu – 1

Nyanya – 2

Kamba waliomenywa – 1 Kilo

Pilipili mbichi iliyosagwa – ½ kijiko cha chai

Kitunguu saumu na tangawizi ilivyosagwa – 1 kijiko cha supu

Nazi nzito iliyochujwa – 1 kikombe

Bizari ya mchuzi – ½ kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Ndimu – Nusu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha na osha kamba vizuri kisha mtie katika sufuria. Katia kitunguu, nyanya, tia chumvi, pilipili mbichi ya kusaga, thomu na tangawizi, bizari ya mchuzi na ndimu. Tia maji kidogo kiasi acha ichemke.
Watakapoiva na karibu kukauka, mimina tui la nazi taratibu koroga kiasi
Punguza moto aacha ichemke kidogo ukiwa mchuzi tayari.

Vipimo – Kisamvu

Kisamvu – 2 vikombe

Kunde mbichi zilizochemshwa – 1 kikombe

Kitunguu – 1

Nazi nzito iliyochujwa – 1 vikombe

Chumvi – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka kisamvu katika sufuria, katia kitunguu, tia chumvi, maji kidogo acha kichemke.
Huku ikichemka mimina kunde mbichi zilizochemshwa acha zipikikie kidogo mpaka kisamvu kikaribie kukauka na kunde kuiva.
Mimina nazi nzito punguza moto acha ichemke kidogo, mimina kwenye bakuli tayari kwa kuliwa.

Vipimo – Kachumbari Ya Papa

Papa mkavu (au nguru) – kipande

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Muoshe papa vizuri atoke mchanga kisha mchome kwenye jiko la mkaa au unaweza kumtia kwenye treya kisha kwenye oven kwa moto wa 350 kwa dakika 15 mpaka 20.
Akikauka mchambue chambue weka kando.
Tengeneza kachumbari, kwa kukata kitunguu, nyanya na pilipili mbichi, tia ndimu na chumvi.
Changanya na papa mkavu uliyemchambu ikiwa tayari.

Jinsi ya kupika Wali Wa Samaki Na Mboga

VIPIMO VYA SAMAKI

Samaki wa sea bass vipande – 1 1/2 LB (Ratili)
Kitunguu saumu(thomu/galic) -1 Kijiko cha supu
pilipili mbichi iliyosagwa – 1 Kijiko cha chai
Bizari ya manjano au ya pilau – 1/2 Kijiko cha chai
Paprika ya unga au pilipili ya unga – 1 kijiko cha chai
Chumvi – Kiasi
Ndimu
Mafuta – 3 Vijiko vya supu

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Roweka samaki kwa viungo hivyo vyote kwa muda wa robo saa hivi.

Washa oven moto wa 400F.
Kisha weka samaki katika trea na choma kwa muda wa dakika 15 na weka moto wa juu dakika za mwisho ili ipate rangi nzuri.
Ikishaiva epua na itakuwa tayari kuliwa.

VIPIMO VYA MBOGA

Gwaru (green beans) – 1 LB
Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha supu
Karoti – 4-5
Chumvi – Kiasi
Bizari ya manjano – 1/2 Kijiko cha chai
Pilipili manga – 1/4 kijiko cha chai
Mafuta ya zaituni – Kiasi

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Kata kata karoti na toa sehemu ya mwisho za binzi.
Weka mafuta katika sufuria kisha kaanga karoti na gwaru
Kisha weka moto mdogo na funika ili ziwive na sio kuvurujika.
Karibu na kuiiva tia thomu kaanga kidogo,tia bizari ,chumvi na pilipili manga.
Ikisha changanyikana vizuri epua na tayari kuliwa na wali na samaki.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About