Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Biriani Ya Kuku Wa Kuchoma Wa Tanduri

Mahitaji

Mchele – 4 vikombe

Kuku – 1

Vitunguu – 3

Nyanya/tungule – 4

Zabibu kavu – ½ kikombe

Tangawizi na kitunguu (thomu/galic) – 2 vijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Mtindi (yoghurt) – 2 kijiko cha supu

Masala ya tanduri – 2 vijiko vya supu

Pilipili manga – 1 kijiko cha chai

Hiliki – ½ kijiko cha chai

Mdalasini – kijiti kimoja

Ndimu – 3 vijiko vya supu

Chumvi – kiasi

Zaafarani (saffron) – 1 kijiko cha chai

Mafuta – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Kuku:

Baada ya kumsafisha kuku, mkate vipande vikubwa vikubwa kiasi upendavyo, muoshe mchuje atoke maji.
Katika bakuli, tia tangawizi, kitunguu thomu ilosagawa, pilipili mbichi ilosagwa, chumvi, ndimu, mtindi, masala ya tanduri na uchanganye vizuri, kisha mtie kuku na uchanganye tena na acha arowanike kwa muda wa kiasi saa au zaidi.
Panga kuku katika sinia ya kuchoma ndani ya oveni. Kisha mchome (grill) hadi awive, mtoe acha kando. Mwagia juu yake masala yatakayobakia katika sinia baada ya kumchoma.

Namna Ya Kutayarisha Masala Ya Nyanya:

Weka mafuta katika karai, tia vitunguu ulivyokatakata, kaanga hadi vianze kugeuka rangi.
Tia nyanya ulizokatakata, tia pilipili manga, hiliki, mdalasini, chumvi, na zabibu. Kaanga kidogo tu yakiwa tayari.

Namna Ya Kutayarisha Wali:

Osha na roweka mchele wa basmati.
Roweka zaafarani kwa maji ya moto kiasi robo kikombe weka kando.
Chemsha maji, tia chumvi, kisha tia mchele uive nusu kiini.
Mwaga maji uchuje mchele kisha rudisha katika sufuria au sinia ya foil. Nyunyizia zaafarini, na rudisha katika moto upike hadi uive kamili.
Epua, kisha pakua wali katika sahani au chombo upendacho, mwagia juu yake masala ya nyanya. Kisha weka vipande vya kuku ulivyochoma, biriani ikiwa tayari

Mapishi ya Biriani Ya Samaki Nguru, Njegere Na Snuwbar (UAE)

Mahitaji

Mchele wa basmati – 4 cups

Samaki nguru (king fish) – 7 vipande au zaidi

Kitunguu – 5

Nyanya/tungule – 3

Njegere – 1 kikombe

Snuwbar (njugu za pine) – 1 kikombe

Viazi – 2 kata kata mapande makubwa

Tangawizi mbichi – 1 kijiko cha supu

Kitunguu saumu – 1 kijiko cha supu

Pilipili nyekundu – 1 kijiko cha chai

Bizari ya biriani/garama masala – 1 kijiko cha supu

Namna Ya Kupika:

Kaanga samaki mbali kwa viungo upendavyo umkoleze vizuri. Au choma (bake/grill) katika oveni ukipenda.
Weka mafuta katika sufuria, tia vitunguu kaanga hadi vigeuka rangi. Gawa sehemu mbili.
Sehemu moja bakisha katika sufuria kisha tia tangawizi mbichi na kitunguu thomu ukaange.
Tia nyanya kaanga kisha tia bizari zote endelea kukaanga, tia njegere, njugu za snuwbar na ndimu kavu.
Tia viazi ulivyokwishakaanga, na vitunguu vilobakia.
Tia mapande ya samaki, changanya na masala bila ya kumvuruga samaki.
Chemsha wali kisha mwagia juu yake, funika upike ndani ya oveni au mkaa hadi wali uive kama unavyopika kawaida ya biriani.
Epua pakua huku ukichanganya na masala ya samaki.

Mapishi ya Half cake (Keki)

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) kikombe 1na 1/2
Sukari (sugar) 1/4 kikombe
Barking powder 1/2 kijiko cha chai
Magadi soda (bicarbonate soda) 1 kijiko cha chai
Mafuta 2 vijiko vya chai
Mafuta ya kukaangia
Maji ya uvuguvugu kiasi

Matayarisho

Changanya unga na vitu vyote (kasoro mafuta ya kuchomea) kisha ukande (hakikisha unakuwa mgumu) Baada ya hapo sukuma na ukate shape uipendayo (hakikisha unakata vipande vinene kiasi na sio kama mandazi) Baada ya hapo ziweke sehemu yenye joto na uache ziumuke. Zikisha umuka zikaange katika moto mdogo ili ziive mpaka ndani. Zikisha iva zitoe na uziweke katika kitchen towel ili zichuje mafuta. Ziache zipoe na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika mboga ya majani ya mashona nguo

Viamba upishi

Mashonanguo mkono 1
Tui la nazi kikombe 1
Karanga zilizosagwa kikombe ½
Mafuta vijiko vikubwa 4
Kitunguu 1
Nyanya ndogo 2
Chumvi kiasi

Hatua

• Chambua mashona nguo mateke, osha na katakata.
• Menya osha na katakata kitunguu.
• Osha, menya na katakata nyanya.
• Kaanga karanga, ondoa maganda na saga zilainike.
• Kuna nazi na chuja tui.
• Kanga kitunguu, weka nyanya na koroga mpaka zilainike.
• Weka mashona nguo na chumvi kisha koroga sawa sawa,
funikiakwa dakika 5 -10.
• Changanya tui la nazi na karanga, ongeza kwenye hizo mboga
ukikoroga kwa dakika 5, punguza moto ili ziive taratibu.
• Onja chumvi na pakua kama kitoweo.
Uwezekano
Changanya mnavu, mgagani, mashonanguo kidogo ki¬dogo au
mboga nyingme.
Tumia maziwa au krimu badala ya tui la nazi.
Weka nyama au dagaa au samaki au mayai badala ya – karanga.

Jinsi ya kupika Wali Wa Karoti Na Nyama

Viambaupishi: Wali

Mchele 3 Magi

Mafuta 1/4 kikombe

Karoti unakata refu refu 3

Vitunguu maji kata vikubwa vikubwa 1 kikubwa

Pilipli manga 1/2 kijicho chai

Hiliki 1/2 kijiko chai

Karafuu ya unga 1/4 kijiko cha chai

Mdalasini wa unga 1/2 kijiko cha chai

Zaafarani (ukipenda) roweka katika maji 1 kijiko cha chai

Zabibu kavu (ukipenda) 1/4 kikombe

Chumvi kiasi

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Kwenye sufuria tia mafuta na kaanga karoti kidogo.

2. Tia vitunguu kisha tia bizari zote.

3. Tia maji kiasi (kutegemea aina ya mchele) na chumvi

4. Tia mchele upike uwive.

5. Karibu na kuwvia tia zabibu ukipenda.

6. Funika endelea kuupika hadi uwive.

Viambaupishi kwa Nyama

Nyama 2 Ratili (LB)

Chumvi Kiasi

Mafuta 1/4 kikombe

Kitunguu (kata virefu virefu) 1 Kikubwa

Pilipili mboga kubwa 2

(ukipenda moja nyekundu moja kijani)

unazikata vipande virefu virefu.

Figili mwitu (celery) kata vipande Miche miwili

virefu virefu

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Chemsha nyama hadi iwive

2. Ikaange kwa mafuta hadi iwe nyekundu

3. Weka vitunguu, pilipili mboga na figili mwitu

4. Kaanga kidogo tu kama dakika moja.

Tofauti kati ya yai la kuku wa kienyeji na la kuku wa kisasa

Kilishe mayai yote ni sawa. Virutubishi vinavyopatikana kwenye yai la kuku wa kienyeji kama protini, vitamini A, madini ya chuma na virutubishi vya aina nyingine, ndivyo hivyo vinavyopatikana pia kwenye yai la kuku wa kisasa.

Tatizo linaweza kutokea pale ambapo wafugaji wa kuku wa kisasa hawafuati taratibu za ufugaji na pengine hawawapi kuku vyakula muhimu wanavyohitaji au wanawapa dawa na vyakula visivyo bora kiafya, hivyo wakati mwingine kiini cha yai la kuku wa kisasa huonekana kupungua rangi ya njano kuliko kiini cha yai la kuku wa kienyeji.

Mtu anashauriwa kula yai bila kujali ni la kuku gani, kwa kutegemea ni yai lipi linapatikana kwa urahisi. Lakini nivizuri kula mayai ambayo yapo salama.

Mapishi – Kisamvu cha Karanga

Mapishi yetu leo ni kisamvu cha kuchanganya na karanga. Karibu.

Mahitaji

Majani ya kisamvu
Karanga nusu kikombe
kitunguu kimoja
nyanya mbili
karoti moja
mafuta na chumvi kiasi

Matayarisho

1. Osha kisamvu chako vizuri kisha katakata vipande vidogo vidogo

2. Unaweza kutwanga kwa kutumia kinu au kuchemsha kidogo na kisha kusaga kwa kutumia mashine. Ukitumia mashine uwe makini usije ukasaga sana ukaharibu.

3. Kaanga karanga kidogo na kisha zisage ziwe unga unga.

4. Chemsha kisamvu chako hadi kiive.

5. Katakata kitunguu, karoti na na nyanya

6. Anza kuunga kisamvu kwa kukaanga vitunguu, weka karoti na kisha nyanya na vikishaiva weka kisamvu na koroga pamoja kisha weka karanga. Acha vichemke kwa muda na unaweza pia weka na nazi tui la kwanza.

7. Baada ya muda mfupi epua na kitakiwa tayari. Waweza kula kwa ugali, wali, chapati, makande n.k

Jinsi ya kupika Pilau Ya Nyama Ya Ng’ombe Na Nyanya

Viambaupishi

Mchele (Basmati) 3 vikombe

Nyama ya ngo’mbe 1 kg

Pilipili boga 1 kubwa

Nyanya 2 kubwa

Vitunguu maji 2 vikubwa

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa 1 kijiko cha supu

Tangawizi 1 kijiko cha chai

Ndimu 1

Mafuta ya kupikia ½ kikombe

Mdalasini ½ kijiko cha chai

Binzari nyembamba 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ½ Kijiko cha chai

Hiliki ½ Kijiko cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

Loweka mchele wako katika chombo

Chukuwa nyama na ioshe vizuri na itie thomu, tangawizi, ndimu, pilipili manga na chumvi kiasi

Iweke jikoni hadi ikauke maji na kuwa imewiva huku ukiikaanga kaanga kwa hayo hayo mafuta yake hadi kuwa rangi ya hudhurungi

katakata Vitunguu na nyanya weka pembeni

Chukua pilipili boga, thomu, tangawizi na visage katika mashine ya kusagia

Weka sufuria pembeni na utie mafuta, subiri yapate moto

Kisha tia vitunguu na vikaange hadi kuwa hudhurungi na tia nyanya

Kisha mimina mchanganyiko wako ulio usaga wa pilipili boga, thomu na tangawizi

Koroga kwa dakika kadhaa Kisha mininia nyama uliyokuwa tayari, maji kiasi na chumvi wastani na subiri maji hayo yachemke

Weka mchele humo na koroga kiasi na onja chumvi kama ipo sawa au kama ndogo unaweza kuongeza

Funika na punguza moto na uache uive taratibu

Baada ya kukauka maji kabisa basi ugeuze na subiri tena kwa dakika kama mbili na tayari kuliwa.

Jinsi ya kupika Vileja

VIPIMO

Unga wa mchele 500g

Samli 250g

Sukari 250g

Hiliki iliyosagwa 1/2 kijiko cha chai

Arki (rose flavour) 1/2 kijiko cha chai

Baking powder 1 kijiko cha chai

Mayai 4

Maji ya baridi 1/2 kikombe cha chai

NAMNA YA KUTAYRISHA NA KUPIKA

1. Saga sukari iwe laini kiasi, changanya unga wa mchele, baking powder, hiliki na sukari.

2. Pasha moto samli mpaka iwe nyepesi kama maji mimina kwenye ule mchanganyiko wa unga wa mchele, kisha uchanganye pamoja na arki.

3. Ongeza mayai yaliopigwa endelea kuchanganya mpaka unga umeanza kuchanganyika vizuri.

4. Ongeza maji ya baridi sana kama nusu kikombe tu ili uchanganyike vizuri.

5. Kata kwa design unayotaka viwe vinene visiwe kama cookies za kawaida kama ilivyo kwenye picha na ukipenda utaweka kidoto kwa kutumia zaafarani katikati ya kileja kama inavyoonesha hapo juu.

6. Choma kwa moto wa baina ya 300F na 350F kwa dakika 15 mpaka 20 visiwe vyekundu toa na tayari kwa kuliwa

Jinsi ya kupika Keki Ya Maboga

Viamba upishi

Unga wa ngano vikombe vikubwa 3
Boga lililopondwa kikombe 1
Baking powder vijiko vidogo
Sukari kikombe kikubwa 1
Blue band kikombe ½
Vanilla kijiko kidogo 1
Mayai 2
Maji kiasi/ maziwa
(kama nilazima)

Hatua

• Osha boga, Kata, ondoa mbegu, kisha kata vipande vikubwa, chemsha na maji mpaka vilainike.
• Kwangua boga la ndani ukiacha maganda na ponda sawasawa.
• Chekecha unga (kila kikombe 1, vijiko vidogo 2 vya baking powder) kwenye bakuli kubwa.
• Ongeza blue band na changanya sawasawa na vidole.
• Ongeza sukari na changanya.
• Ongeza mayai na koroga na mwiko.
• Ongeza boga lililopondwa na koroga njia moja mpaka ilainike.
• (Kama haikulainika ongeza yai /mayai au maziwa/ maji kidogo).
• Ongeza vanilla na koroga.
• Paka mafuta chombo cha kuokea au sufuria kisha chekecha unga kidogo wa ngano.
• Mimina rojo la keki kwenye sufuria au chombo cha kuokea.
• Oka kwenye oven au tumia sufuria na weka mkaa wa moto juu na chini moto kidogo mpaka iive.
• Jaribu kuchoma kisu katikati, kama ni kavu keki imeiva, epua, pozesha kata tayari kwa kula, kama kitafunio.

Mapishi ya Biriani Nyepesi Kupika Ya Samaki

Vipimo

Mchele wa pishori (basmati) – 4

Vitunguu katakata – 3

Nyanya (tungule) katakata vipande vikubwa – 3 -5

Pilipili boga la kijani (capsicum) katakata

Supu ya kitoweo au vidonge vya supu – 1

Bizari mchanganyiko Garama masala – 5-7

Pilipili mbichi ya kusaga – Kiasi

Zaafarani ya maji (flavor) – 1 kijiko cha chakula

Mafuta ya kupikia – ¼ kikombe

Samaki wa kukaanga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Roweka mchele kiasi nusu saa kisha chemsha mchele kwa supu uive nusu kiini. Mwaga maji chuja.
Wakati mchele unapikika, weka mafuta katika sufuria kubwa ya kupikia wali, kaanga vitunguu mpaka vigeuke rangi ya hudhurungi.
Tia nyanya na vitu vinginevyo vyote kaanga kidogo tu.
Mwaga wali katika sufuria na nyunyizia zaafarani kisha changanya na masala vizuri.
Funika upike katika oven (bake) au juu ya stovu moto mdogo mdogo kiasi dakika 15- 20.
Epua ikiwa tayari, pakua kwenye sahani kisha tolea kwa samaki wa kukaanga.

Jinsi ya Kupika skonzi

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour 2 vikombe vya chai)
Sukari (sugar 1/2 kijiko cha chakula)
Chumvi (salt 1/2 kijiko cha chai)
Hamira (yeast 1/2 kijiko cha chakula)
Baking powder 1/2 kijiko cha chai
Siagi (butter 1/4 ya kikombe cha chai)
Maziwa (fresh milk 3/4 ya kikombe cha chai)(unaweza kutumia maji badala ya maziwa)

Matayarisho

Pasha maziwa yawe ya uvuguvugu kisha weka pembeni, pia yeyusha siagi na uweke pembeni.Baada ya hapo tia kila kitu kwenye bakuli la kukandia kasoro maziwa, na uchanganye vizuri kisha tia maziwa kidogo kidogo katika mchanganyiko huo kisha ukande. Ukimaliza uweke kwenye sehemu ya joto na uache uumuke. Ukisha umuka utawanyishe katika madonge saba Kisha .pakaza mafuta au siagi katika chombo cha kuokea kisha yapange hayo madonge katika hicho chombo na uyaache yaumuke tena (kwa mara ya pili). Baada ya hapo pakaza mafuta juu ya hayo madonge na uyaoke (bake) katika oven (moto 200°C ) kwa muda wa dakika 25 na hapo scones au maskonzi yatakuwa tayari

Mapishi ya Borhowa

Mahitaji

Daal (lentils) nyekundu au/na kijani – 1 Kikombe kikubwa

Bizari ya manjano ya unga – 1/2 Kijiko cha chai

Pili pili ya unga – 1/2 kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Maji ya ndimu – 3 Vijiko vya supu

Kitunguu – 1 kiasi

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 Kijiko cha chai

Bizari ya unga (cummin powder) – 1 Kijiko cha chai

Mafuta ya kukaangia – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha daal kwa kutoa mawe ikiwa yapo, kisha osha na roweka dakika 15 hivi.
Kisha chemsha kwa kutia maji, bizari ya manjano, chumvi, pili pili ya unga na maji ya ndimu hadi iive na kuvurujika.
Halafu chukua kisufuria na kaanga kitungu, kisha thomu na mwisho tia bizari ya pilau.
Kisha mimina mchanganyiko wa kitunguu kwenye sufuria ya daal (iliyokwisha iiva)na uchanganye na iwache motoni kidogo itokote.
Ukipenda mimina mchanganyiko kwenye blenda na usage mpaka iwe laini.
Tia kwenye bakuli na itakuwa tayari kuliwa na wali na samaki ukipenda

Jinsi ya kupika Biskuti Za Tende

Viamba upishi

Unga 4 Vikombe vya chai

Sukari ya laini (icing sugar) 1 Kikombe cha chai

Baking powder 2 Vijiko vya chai

Mayai 2

Siagi au margarine 1 Kikombe cha chai

Vanilla 1 Kijiko cha chai

Maziwa ya kuchanganyia kiasi

Tende iliyotolewa koko 1 Kikombe

ufuta (sasame) kiasi 1/4 kikombe

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Changanya unga, siagi, baking powder, na sukari katika mashine.

2. Kisha tia mayai, vanilla na halafu maziwa kidogo kidogo hadi mchanganyiko ushikamane.

3. Gawanya madonge mawili na usukume kama chapati, lakini sio nyembamba sana.

4. Tandaza tende robo ya duara na unyunyize ufuta duara zima: kisha kunja hadi mwisho na ukate kate, kisha upange katika trei ya kuvumbika.

5. Vumbika (bake) moto wa 350°F kwa muda wa dakika 20 au hadi vigeuke rangi na viwive.

6. Zikisha iiva ziache zipowe na zitakuwa tayari kuliwa.

Shopping Cart
2
    2
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About