Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Samaki Wa Kuchoma

Vipimo Vya Ugali

Unga wa mahindi – 4 vikombe

Maji – 6 kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Tia maji kiasi katika sufuria wacha yachemke hasa

Tia unga kidogo kidogo huku ukikoroga mpaka ukamatane

Punguza moto huku ukiendelea kuusonga

Endelea kusonga kwa dakika kadhaa mpaka uanze kuchambuka

Kisha mimina kwenye bakuli au sahani na itakuwa tayari

Vipimo Ya Upishi Wa Mchuzi Wa Samaki Wa Kuchoma Wa Nazi

Samaki:

Samaki wa Nguru – kiasi vipande 5 – 6

Pilipili mbichi – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 5 chembe

Tangawizi mbichi – 1 kipande

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha supu

Pilipili nyekundu ya unga – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 3 kamua

Chumvi – kiasi

Ukipenda mkate samaki vipande kiasi.
Saga vipimo vyote vinginevyo katika mashine. Mchanganyiko ukiwa mzito ongezea ndimu
Changanya pamoja na samaki upake vizuri vipande vya samaki
Acha kwa muda wa nusu saa vikolee mchanganyiko
Panga samaki katika treya ya kupikia ndani ya oveni, kisha mchome (grill) samaki huku ukigeuza hadi viwive.
Epua weka kando.

Kuandaa Mchuzi:

Nyanya/tungule – 3

Kitunguu – 2

Bizari ya manjano/haldi – ¼ kijiko cha chai

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Tui la nazi zito – 3 vikombe

Chumvi – kiasi

Katakata vitunguu na nyanya vidogodogo (chopped) weka kando

Weka mafuta katika karai au sufuria, kaanga vitunguu hadi vianze kugeuka rangi

Tia nyanya kaanga pamoja na tia bizari ya njano/haldi .

Tia tui la nazi, chumvi koroga .

Mwishowe tia vipande vya samaki na rojo lake litakalobakia katika treya, mchuzi uko tayari

Jinsi ya kutengeneza Pilau Ya Kuku

Mahitaji

Mchele wa basmati – 3 vikombe

Kuku – ½

Viazi – 4

Vitunguu – 2

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa – 2 vijiko vya supu

Binzari ya pilau nzima – 1 Kijiko cha chakula

Binzari ya pilau – ½ kijiko cha chai

Pilipili manga nzima – ½ kijiko cha chai

Karafuu nzima – 8

Iliki nzima – 6

Mdalasini nzima – 5 vijiti

Pilipili mbichi iliyosagwa – 2

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kupikia – ¼ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika:

Osha mchele na roweka kwa muda kutegemea na aina ya mchele.
Kata kuku vipande upendavyo, safisha kisha mchemshe kwa chumvi, pilipili iliyosagwa, thomu na tangawizi.
Akiwiva kuku, mtoe weka kando, bakisha supu katika sufuria.
Katika sufuria, kaanga vitunguu hadi vigeuke rangu ya hudhurungi.
Tia thomu na tangawizi na binzari zote kaanga kidogo
Kisha tia viazi kanga kidogo kisha tia kisha tia vipande vyako vya kuku na supu acha ichemke kidogo kisha tia maji ukisie kutokana na mchele unaotumia.
Mwisho tia mchele koroga uchanganye na vitu vyote acha ichemke kiasi kisha funika na punguza moto mpaka uive (huku ukiugeuzageuza)
Ukishakuwa tayari pakua kwenye sahani tayari kwa kula na salad na pilipili.

Jinsi ya kupika Mitai

VIAMBAUPISHI

Unga wa ngano 1 1/2 Kikombe

Baking powder 1 Kijiko cha chai

Baking soda ¼ Kijiko cha chai

Chumvi ½ kijiko cha chai

Sukari 1 kijiko cha supu

Hamira 1/2 Kijiko cha supu

Yai 1

Maziwa ½ Kikombe

Mafuta ya kukaangia

VIAMBAUPISHI:SHIRA

Sukari 1 Kikombe

Maji ½ Kikombe

Iliki au Mdalasini ¼ kijiko cha chai (ya unga)

MAANDALIZI NA JINSI YA KUPIKA

1. Kwenye bakuli, changanya pamoja unga, baking powder, baking soda, chumvi, sukari na hamira.

2. Katika kibakuli, piga mayai na maziwa pamoja.

3. Changanya mchanganyiko wa mayai na wa unga ; na ukande kama unga wa maandazi.

4. Ikisha fura, sukuma unga kama wa maandazi na ukate mitai .

5. Pasha moto mafuta na uchome hadi iwe rangi ya dhahabu, upande zote mbili.

6. Ipikie shira lakini isiwe nzito .

7. Tia mitai na upepete hadi sukari ienee kote na zitakuwa tayari kuliwa.

Mchemsho wa samaki na viazi

Mahitaji

Samaki mbichi (1)
Viazi mbatata (3)
Nyanya (1)
Kitunguu maji
Limao
Kitunguu saumu
Tangawizi
Chumvi
Pilipili
Vegetable oil

Matayarisho

Safisha samaki kisha mmarinate na tangawizi, kitunguu swaum, chumvi na limao kwa muda wa masaa mawili. Baada ya hapo menya viazi na uvikate vipande vidogo kisha vioshe na viweke kwenye sufuria yenye maji kiasi kwa ajili ya kuvichemsha. Viinjike jikoni na uviache vichemke kwa dakika 7. Vikisha chemka tia samaki, katia kitunguu,pilipili, chumvi, limao, vegetable oil na nyanya na uache supu ichemke mpaka samaki na viazi vitakapoiva. baada ya hapo supu itakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Wali Wa Kichina Wa Kuku Na Mboga Mchanganyiko

Vipimo

Mchele wa basmati/pishori – 4 vikombe vikubwa (mugs)

Kuku – 2

Vitnguu vya kijani (sprin onions) katakata – 5 miche

Maharage machanga (spring beans) katakata – kiasi kujaza mug moja

Pilipili boga la (capsicum) katakata – 1

Karoti katakata vipande virefu – 1

Kitunguu thomu (garlic) kuna (grate) – 1 kubwa

Tangawizi mbichi kuna (grate) – 1 kubwa

Sosi ya soya (soy sauce) – 2 vijiko vya supu

Kidonge cha supu – 1

Mafuta ya kupikia – ¼ kikombe cha chai

Chumvi – kiasi

Pilipili manga – 1 kijiko cha supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha kuku vizuri, katakata vipande, weka katika sufuria, tia chumvi, pilipili manga, mfunike, umkaushe motoni huku ukimgeuza geuza.

Roweka mchele kisha uchemshe uive nusu. Chuja maji, tia siagi kidogo ili usigandane.

Weka karai ya kupika mboga (wok) au sufuria kisha tia mafuta yashite moto.

Tia kitunguu thomu, tangawizi, kaanga kidogo.

Tia mboga zote, ulizokatakata.

kaanga kidogo, kisha tia sosi ya soya na kidonge cha supu. Usizipike sana mboga mpaka zikalainika mno. Sababu zitaiva katika mchele

Changanya kuku na mboga kisha changanya vyote katika mchele, urudishe katika moto.

Funika upike hadi uive kamilifu.

Pakua kwenye sahani.

Mapishi ya Pilau Ya Nyama Na Mtindi

MAHITAJI

Nyama iliyokatwa vipande – 1 Ratili(LB)

Mchele Basmati – 2 Magi

Chumvi ya wali – kiasi

Kitungu kilichokatwa katwa – 1 kikubwa

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi – 1 kijiko cha supu

Mtindi (yogurt) – ½ kikombe

Mchanganyiko wa bizari ya pilau ya tayari – 2 vijiko vya supu

Mafuta kidogo yakukaangia

Rangi ya manjano (ukipenda)

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Osha mchele na roweka nusu saa .

Weka mafuta katika sufuria na kaanga vitungu mpaka viwe rangi ya hudhurungi (brown).

Tia thomu na tangawizi na ukaange kidogo.

Kisha weka bizari ya pilau halafu nyama huku unakaanga hadi nyama isiwe nyekundu tena.

Tia maji gilasi 1½- 2 ichemke mpaka nyama iwive na karibu kukauka.

Mimina mtindi na iachie moto mdogo ikauke kidogo.

Kwenye sufuria nyingine chemsha mchele pamoja na chumvi na mafuta kidogo mpaka uive.

Mimina wali juu ya nyama, kisha nyunyiza rangi (ukipenda) kama vile wali wa biriani na ufunike kwa dakika kumi hivi.

Changanya wali na nyama pamoja ikiwa tayari kuliwa.

Mapishi ya Ndizi Za Supu Ya Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi – 15 takriiban

Nayma ya ng’ombe – 1 kilo

Kitunguu maji – 1

Nyanya – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) kilosagwa – 1 kijiko cha supu

Tangawizi mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi ilopondwa – 2

Jira/cummin/bizari ya pilau ilosagwa – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 1

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chemsha nyama kwa ndimu, chumvi na tangawizi mbichi na kitunguu thomu.
Menya ndizi na zikatekate vipande kiasi, weka katika sufuria.
Katakata kitunguu na nyanya utie katika ndizi.
Tia jira na chumvi.
Nyama ikiwiva mimina pamoja na supu yake ufunike ndizi ziwive na kuwa tayari kuliwa.
Ukipenda tia pilipili mbuzi zichemke pamoja na ndizi.

Jinsi ya kuandaa Wali Wa Hudhurungi Na Kabeji

VIPIMO VYA WALI

Mchele wa hudhurungi (brown rice)

na (wild rice kidogo ukipenda)Osha na Roweka – 2 Vikombe

Kitungu maji – 1 Kiasi

Kitunguu saumu – 1 Kijiko cha supu

Bizari ya manjano – 1/2 Kijiko cha chai

Mdalasini nzima – 1 kijiti

Iliki iliyosagwa – 1/4 Kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Pilipili manga – 1/4 Kijiko cha cha

Mafuta – 2 Vijiko vya supu

Majani ya Bay(bay leaves) – 1

Mbegu ya giligilani iliyoponwa (coriander seeds) – 1 Kijiko cha chai

Supu ya kuku ya vidonge – 1

Maji ya wali – 4 vikombe

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Kaanga kitungu, kabla ya kugeuka rangi tia thomu.
Kisha weka bizari zote na ukaange kidogo.
Tia mchele kisha maji na ufunike upike katika moto mdogo.
Na ikishawiva itakuwa tayari kwa kuliwa na kabeji na kuku wa tanduuri.

VIPIMO VYA KABEJI

Kabeji iliyokatwa katwa – 1/2

Karoti iliyokwaruzwa – 1-2

Pilipili mboga kubwa – 1

Figili mwitu (celery) iliyokatwa – 1 au 2 miche

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa – 1 Kijiko cha supu

Pilipili mbichi – 1

Kisibiti (caraway seed) – 1/4 Kijiko cha chai

Bizari ya manjano ya unga = 1/2 Kijiko cha chai

Giligani ya unga – 1 Kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Kitungu maji kilichokatwa -1

Kotmiri – upendavyo

Mafuta ya kukaangia – Kiasi

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Kwenye sufuria kaanga kitungu, figili mwitu kisha tia thomu na pilipili zote.
Halafu tia bizari zote na ukaange kidogo.
Kisha weka kabeji na chumvi, ufunike moto mdogo ilainike kidogo na sio sana
Tia karoti na usiwache motoni sana, kisha zima moto na inyunyizie kotmiri juu.

Jinsi ya Kupika Kalmati

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour 2 vikombe vya chai)
Hamira (yeast kijiko 1 cha chai)
Sukari (sugar 2 vikombe vya chai)
Hiliki (cardamon 1/4 ya kijiko cha chai)
Maji kikombe1 na 1/2
Mafuta

Matayarisho

Changanya unga, hamira, maji na mafuta kijiko 1. Koroga vizuri mpaka upate uji mzito usiokuwa na madoge Baada ya hapo uache uumuke kisha zichome kalmati katika moto wa wastani. Baada ya hapo tia sukari, hiliki na maji 1/2 kikombe katika sufuria na ichemshe uku unakoroga mpaka iwe tayari.(ukitaka kujua kama iko tayari chovya mwiko kisha gusa na vidole utaona iko kama nta au gundi) Baada ya hapo tia kalmati na uzichange pamoja mpaka zikolee kisha zitoe na uziache mpaka zipoe tayari kwa kuliwa.

Mapishi – Kisamvu cha Karanga

Mapishi yetu leo ni kisamvu cha kuchanganya na karanga. Karibu.

Mahitaji

Majani ya kisamvu
Karanga nusu kikombe
kitunguu kimoja
nyanya mbili
karoti moja
mafuta na chumvi kiasi

Matayarisho

1. Osha kisamvu chako vizuri kisha katakata vipande vidogo vidogo

2. Unaweza kutwanga kwa kutumia kinu au kuchemsha kidogo na kisha kusaga kwa kutumia mashine. Ukitumia mashine uwe makini usije ukasaga sana ukaharibu.

3. Kaanga karanga kidogo na kisha zisage ziwe unga unga.

4. Chemsha kisamvu chako hadi kiive.

5. Katakata kitunguu, karoti na na nyanya

6. Anza kuunga kisamvu kwa kukaanga vitunguu, weka karoti na kisha nyanya na vikishaiva weka kisamvu na koroga pamoja kisha weka karanga. Acha vichemke kwa muda na unaweza pia weka na nazi tui la kwanza.

7. Baada ya muda mfupi epua na kitakiwa tayari. Waweza kula kwa ugali, wali, chapati, makande n.k

Mapishi – Fish Finger

Leo tunaangalia mapishi ya fish finger ( sijui kama unaweza kusema kidole cha samaki)!, Ni mlo mzuri hasa kuliwa kama kitafunio au mboga ya pembeni.

Mahitaji

500g Fileti ya samaki
120g Chenga za mkate
100g Unga wa ngano
Mayai 2
Ndimu 1
Kitunguu saumu 1
Kotmiri
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Menya vitunguu saumu kisha visage

Katakata fileti kwa muundo wa mraba (kama vidole) kisha paka mchanganyiko wa vitunguu saumu

Kata ndimu na kamulia kwenye fillet yako

Weka chenga za mkate kwenye bakuli kisha uchanganye chumvi kiasi na kata kata kotmiri majani 3 na uchanganye pamoja.

Kwenye bakuli lingine weka mayai na uyapigepige yawe kama uji mzito

Weka unga kwenye bakuli jingine.

Chukua kipande cha fillet kiweke unga kidogo kisha kizamishe kwenye yai na baada ya hapo kizamishe kwenye mchanganyiko wa chenga za mkate. Fanya hivyo kwa vipande vyote.

Weka mafuta kwenye kikaago na subiri yachemke kisha weka fillet zako vizuri na zikaange pande zote hadi zimekuwa rangi ya brown ( hakikisha moto sio mkali sana).

Epua na weka pembeni mafuta yote yakauke

Weka kwenye sahani tayari kwa kula.

Mapishi ya Koshari Na Sosi Ya Kuku

Vipimo Vya Koshari

Mchele – 2 vikombe

Makaroni – 1 kikombe

Dengu za brown – 1 kikombe

Vitunguu vilokatwakatwa (chopped) – 2

Nyanya ziilokatwakatwa (chopped) – 4

Nyanya ya kopo – 1 kijiko cha supu

Kitunguu saumu(thomu/galic) ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ya unga – 1 kijiko cha chai

Mdalisini kijiti – 1

Bizari ya pilau (cumin seeds) – 1 kijiko cha supu

Hiliki – 2 chembe

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Chumvi – kiasi

Vipimo Vya Kuku

Kuku – 3 LB

Kitunguu saumu(thomugalic) na tangawizi – 1 kijiko cha supu

Mtindi (yoghurt) – 1 kijiko cha supu

Pilipili ya masala nyekundu – 1 kijiko cha chai

Bizari upendazo – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 1

Vitunguu slesi vilokaangwa – 3

Namna Kutayarisha Kuku

Kata kuku vipande vikubwa kiasi, osha, weka kando achuje maji.
Changanya vipimo vya kuku pamoja katika kibakuli.
Changanya pamoja na kuku, roweka muda wa kiasi nusu saa au zaidi.
Mchome (grill) kuku hadi aive weka kando.

Namna ya Kutayarisha Koshari

Tia mafuta katika sufuria, kaanga vitunguu hadi viive kuwa rangi hudhurungi.
Tia thomu ,mdalisini, bizari ya pilau na hiliki kaanga tena kidogo.
Tia nyanya, pilipili zote, nyanya kopo, chumvi changanya vizuri ukaange kidogo.
Epua sosi acha kando.
Chemsha dengu pamoja na kidonge cha supu ziive nusu kiini na ibakie supu yake. Muda wa kuchemsha dengu inategemea aina yake.
Tia mchele uchanganyike, funika, pika hadi uive vizuri pamoja na dengu
Chemsha makaroni hadi yaive , epua chuja maji.
Changanya pamoja wali wa dengu na macaroni.
Pakua katika sahani, kisha weka juu yake kuku aliyechomwa, mwagia vitunguu vilokaangwa, kisha mwagia sosi.

Mapishi ya Biskuti Za Mtindi/Yoghurt

MAHITAJI

Chenga za biskuti – 3 gilasi

Mtindi (yogurt) – 1 Kopo (750g)

Maziwa ya unga – 1 gilasi

Siagi – 10 Vijiko vya supu

Sukari – ½ gilasi

Lozi zilizomenywa vipande vipande – ½ gilasi

Nazi iliyokunwa – ½ gilasi

Vanilla – 1 Kijiko cha supu

MAPISHI

Katika mashine ya kusagia (blender), tia mtindi, sukari, siagi na vanilla na usage pamoja hadi ichanganyike.
Mimina katika bakuli la kiasi.
Tia vitu vilivyobakia na uchanganye vizuri.
Mimina kwenye treya ya kuchomea na uvumbike katika oveni moto wa 350° hadi ishikamane na kuwa tayari.
Iaache ipoe kisha katakata vipande na tayari kwa kuliwa.

Baada yakuwa imeshaiva, ukipenda unaweza kupakiza jamu au karameli ya tayari kwa juu, kisha ukarudisha kwenye oveni moto wa juu kidogo kwa ladha nzuri zaidi

Mapishi ya Sponge keki

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) 100g
Sukari (sugar) 100g
Siagi isiyokuwa na chumvi (unsalted butter) 100g
Mayai (eggs) 2
Vanila 1 kijiko cha chai
Chumvi pinch
Warm water 3 vijiko vya chakula

Matayarisho

Kwanza washa oven moto wa 200 C. Baada ya hapo saga butter na sukari mpaka viwe laini kisha tia mayai na uendelee kusaga mpaka vichanganyike vizuri kisha tia unga, vanila, chumvi na na maji na usage mpaka upate uji usiokuwa mzito sana au mwepesi sana. Baada ya hapo utie kwenye baking tin na u bake kwa muda wa dakika 25 na mpaka cake yako iive yani juu na chini iwe ya brown na ukidumbukiza kijiti katikati kinatoka kikiwa clean. Baada ya hapo itoe kwenye tin na uiache ipoe. Ikisha poa itakuwa tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart
4
    4
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About