Dondoo za Urembo na Mitindo

Jinsi ya kuondoa kitambi Kitaalamu

Hapo zamani kidogo tuliona na tulishuhudia watu wakisema ya kwamba mwanaume ambaye ana kitambi ndiye ambaye mwenye fedha, hiyo ni imani ambayo ilijengeka katika fikra na mitazamo yetu. Lakini katika karne hii mambo yamebadilika baada ya kuona baadhi ya madaktari wakieleza kwa kina ya kwamba kuwepo matumbo makubwa tanatokana na uwepo wa mafuta mengi katika kuta za tumbo.

Na mafuta hayo pindi ambao yanazidi huwa na athari sana kiafya, athari hizo za kiafya hupelekea mtu kuweza kupata magonjwa mbalimbali kama vile shinikizo la damu na magonjwa mengine mbalimbali.

Hivyo ili kuepukana na athari hizo zitokanazo na kitambi nakusihi ufanye yafuatayo:

1. Chakula

Huu ni msingi mwingine muhimu sana katika harakati za kupunguza unene na tumbo, kwa kifupi unahitaji kuzingatia yafuatayo:

 1. Kula mboga za majani kwa wingi kwani husaidia sana kiafya.
 2. Kunywa maji mengi sana
 3. Weka chakula cha kukutia hamu mbali na nyumba yako
 4. Kula vyakula ambavyo vitatumika kwa kiwango kikubwa katika kujenga mwili wako ila epuka kula vyakula vyenye mafuta kwa wingi.

2. Mazoezi ya viungo husaidia kupunguza tumbo.

Kwa kiwango kikubwa Unaweza kufanya mazoezi ya aina nyingi ili kupunguza tumbo. Mazoezi yoyote ya nguvu yatapunguza mafuta ya mwili wako pamoja na mafuta ya ndani (visceral fat).
Mazoezi ambayo nayazungumzia ni mazoezi ambayo yanasaidia kukata tumbo kwa kiwango cha juu sana. Mazoezi haya kwa karne hii ya teknolojia yapo wazi katika video mbalimbali.

Hivyo jaribu kutafuta video mbalimbali ambazo zitakusaidia kwa kiwango kikubwa katika kukata tumbo.

3. Hakikisha unapata usingizi Wlwa kutosha kwa siku.

Kupata usingizi kwa muda mzuri kumeonyesha kuwa na mchango katika kudhibiti kiwango cha mafuta katika mwili wa binadamu. Katika utafiti mmoja, watu waliopata usingizi kwa saa 5 hadi 7 kwa siku katika kipindi cha miaka 5, walionyesha kuwa na mafuta mwilini kidogo zaidi ukilinganisha na wale waliopata usingizi kwa pungufu ya saa 5 kwa siku.

Hivyo hakikisha unatenga muda wa kupumzika hasa pale unapokuwa una usingizi.

Faida na namna ya kutumia mafuta ya Zaituni Olive Oil kwenye nywele

Faida ya Mafuta Ya Zaituni Olive Oil kwenye nywele.

1. Yanasaidia kufanya mzunguko wa damu kufanya kazi vizuri kwenye ngozi ya kichwa na kupenyeza hadi kwenye shina ya nywele kisha kuifanya nywele inayoota kuwa imara

2. Yanasaidia kupambana na mba kwenye ngozi ya kichwa

3. Yanasaidia uzalishwaji wa mzizi au shina ya nywele

4. Yanasaidia uzalishwaji wa melanin ambayo inafanya kazi ya kutoa rangi ya nywele inayotakiwa.

5. Yanasaidia kuifanya nywele isiwe kavu sana.

NAMNA YA KUZIHUDUMIA NYWELE:

Unaweza kuchanganya na Mdalasini pamoja na Asali.

1. Olive oil vijiko 2 vya chakula

2. Asali kijiko 1 cha chakula

3. Mdalasini kijiko 1 cha chai

Pasha moto olive oil kisha changanya vyote kwa pamoja pakaa kwenye nywele acha kwa muda wa dakika 20 kisha osha nywele zako na upakae mafuta zikishakauka.

Ninashauri utumie mafuta haya kwenye nywele na ngozi ni mazuri sana. Ukiwa na mba pakaa kwenye ngozi mba itaisha na muwasho utaondoka.

Uvaaji wa Tai kulingana na Umbo lako

Kuna mambo mengi ya kufanya ili tuwe watu wa kuvutia kila wakati.Mpangilio wa mavazi hufanya mtu kuonekana maridadi. Kama wewe ni mvaaji wa tai unapovaa unazingatia mambo yapi? Na je unafunga tai yako kwa namna inayokubalika?

Wengine huwa hawafahamu jinsi ya kufunga tai na hivyo kuleta mushkeri wakati wa kuvaa tai na kusababisha tai kukaa upande. Unapoamua kuvaa tai na shati ambalo halijanyooshwa ambalo linakuwa kwenye mikunjo au kuvaa tai na ndala unakuwa umeua maananzima na kulivunjia heshima vazi hili.

Tai ni vazi lawatu walio maridadi kama huwezi kuwa maridadi basi vazi hili halikufai kabisa.
Unapovaa taa unatakiwa kuzingatia aina ya umbo lako kama wewe ni mnene vaa tai inayoendana na mtu mnene na kama wewe ni mwembamba basi vaa tai inayoendana na mtu mwembamba.

Kuna wengine huvaa tai zinazofika magotini na kuwa kichekesho anapopita mtaani
Tai ni vazi ambalo huongeza heshima na hadhi ya mvaaji cha muhimu ni jinsi gani unavaa tai yako na ikiwezekana jaribu kumechisha tai na suruali kwa vile ili tai upendeze ni laima iendane na nguo unayovaa.

Ni vyema ukahakikisha kuwa unakuwa na tai zenye rangi tofauti ambazo zitaendana na nguo unazovaa.

Jinsi ya Kujaza nywele kwa njia za Asili

Zingatia mambo haya yafuatayo;

 1. Chukua parachichi kubwa moja, asali vijiko vitatu na kiini cha yai.
 2. Osha nywele zako kwa shampoo na uzikaushe.
 3. Ponda ponda parachichi mpaka lilainike kabisa. Chukua vijiko vitatu vya asali na kiini cha yai kisha changanya yote kwa pamoja.
 4. Paka mchanganyiko huo kaa nao kwa muda wa dakika 15 kisha osha.
 5. Fanya hivyo kwa muda wa wiki moja hadi mbili na utaweza kuona matokeo mazuri katika nywele yako

Njia za kutunza nywele zako

Suala la kutunza nywele za asili wengi hutamani japokuwa ukweli kwamba kuna changamoto kadhaa, lakini kwa mtu aliye makini anao uwezo wa kupata kilicho bora katika nyewle zake. Leo tunaangazia vitu vya kufanya ili kukuza na kutunza nywele za asili.

Kwanza kabisa unapaswa kuzikubali nywele zako na kuzipenda , jambo hilo litapelekea mahusiano mazuri, kuelewa tatizo la nywele zako na kuanza kuchukua hatua taratibu ya kuzipatia uvumbuzi tatizo hilo.

Pili, unapaswa kufanya usafi wa kina wa ngozi na nywele zenyewe kwasababu endapo nywele zitaachwa chafu, basi ule uchafu unaziba matundu ya nywele na kuzuia njia kama vile ambavyo matundu ya uso yakiziba unapata chunusi.

Tatu, ni kulinda unyevu wa nywele . pale zinapooshwa, yale mafuta asilia ya kuzilinda huondoka na uchafu. Nywele inabaki ikiwa na udhaifu fulani maana haiwezi hata kushikilia hayo maji yaliyoo vizuri na zikikauka zinakuwa kavu sana. Ni vizuri kabla hazijakauka vizuri, zikafanyiwa ‘condition’ , kwa zile nywele ambazo ni nyepesi na chache pia kuna bidhaa zinasaidia kutunza vizuri unyevu na hivyo kuwa na afya nzuri.

Hatua nyingine ni ya kupaka mafuta kichwani, kwani mafuta yana umuhimu mno katika ukuaji wa nywele na mafuta mazuri ni ya nazi ambayo yamewafaa baadhi ya watumiaji wengi .

Njia nyingine ni ya kuzichambua vizuri nyele kabla ya kuzichana, hapa mtu anatakiwa kuwa na subira na nywele zake , asifanye pupa kuzichana na ikiwezekana aziloweshe maji kidogo halafu ndipo azichane kwa chanuo kubwa lenye upana wa kutosha (wide toothed comb) ili kuzipa afya na kuepuka kujiumiza wakati wa kuzichana.

Pia mtu anayetunza nywele za asili anatakiwa kupunguza matumizi ya vitu vyenye moto katika nywele zake kama vile pasi ya nywele na vingine kama hivyo. Nywele zinatakiwa zichanwe kawaida na ziachwe zikauke zenyewe kwa hewa bila kuzilazimisha.

Jinsi ya kuchagua rangi sahihi wakati wa Kujipodoa

YAPO mambo mabalimbali katika tasnia ya urembo hasa katika vipodozi yanayopaswa kuzingatiwa katika kuboresha muonekano wa mtu.
Moja ya mambo hayo ni ujuzi na uelewa wa kutumia rangi katika kujipodoa kwani ni wanawake wachache wenye ujuzi huu.
Katika makala hii, nitakuelezea namna ya kuchanganya na kutofautisha rangi za vipodozi, lengo likiwa ni kuboresha muonekano wako.

Uchanganyaji wa rangi za vipodozi ni muhimu sana kwani katika kujipodoa, rangi zote za vipodozi unavyopaka zinatakiwa zioane ili kuleta muonekano ulio sawa na wa kueleweka.

Kwanza kabisa unatakiwa uwe makini katika kuoanisha rangi za vipodozi pamoja na rangi ya ngozi yako, hivyo katika hili unatakiwa kuwa na ujuzi maalumu ili usije ukafanya makosa na kuharibu muonekano wako.

Pia inabidi ufahamu hatua za upakaji vipodozi ili usije ukafanya vipodozi vingine visionekane katika uso wako.

Namna ya kuoanisha na kutofautisha rangi

Siku zote vipodozi vyako lazima viendane na mavazi yako ili kuleta maana zaidi kwa mfano, mara nyingi rangi ya mdomo ‘lipstick’ huendana na vazi lako wakati shedo ‘eye shadow’ zinatofautiana.

Kwa nguo za pinki

Katika mavazi haya, unatakiwa kupaka rangi ya mdomo yenye rangi ya pinki ambayo itaendana sawasawa na mavazi yako huku ukichanganya na shedo ‘eyeshadow’, inaweza kuwa ya rangi ya bluu ili kuitofautisha na mavazi yako, hapo utakuwa sawa katika kanuni za urembo.

Vazi la kijani

katika vazi hili unatakiwa kupaka rangi ya mdomo yenye rangi ya kahawia huku ukichanganya na shedo ya rangi ya kijani au kahawia iliyoingiliana na pinki au rangi ya machungwa.

Kwa vazi la njano au kahawia

Katika vazi hili unatakiwa kupaka ‘lipstick’ ya rangi ya kahawia iliyokolea, kwa upande wa shedo waweza kupaka ya rangi ya dhahabu.

Kwa vazi la bluu

Katika vazi hili unatakiwa kupaka ‘lipstick’ yenye rangi ya pinki huku ukipaka shedo ya rangi ya bluu kwa mtindo huu utakuwa mwenye kuvutia siku zote.

Mambo ya kuzingatia kama una ngozi yenye Mafuta

Ngozi yenye mafuta kwa kawaida huwa inang’ara, nene na yenye rangi iliyotitia. Mara nyingi ngozi yenye mafuta mengi sana huwa na chunusi nyingi na vipelepele na mara nyingine huwa na chunusi zenye vichwa vyeusi. Katika aina hizi za ngozi mafuta hutokana na tezi za sebaceous na kuzalisha mafuta zaidi ya kiwango kinachotakiwa. Mafuta hayo husambaa katika ngozi na kuifanya iwe na mafuta mafuta.

Mafuta katika mwili yanatengenezwa na ‘sebaceous glands’,kwa hiyo kuna baadhi ya watu wana sebaceous glands ambazo zinatengeneza mafuta kwa wingi sana na hivyo kufanya ngozi zao kung’aa kwa sababu ya hayo mafuta mengi.

Sebaceous gland zipo kwa wingi usoni(face) shingoni(neck), kifuani, kichwani na mgongoni, ndiyo maana hayo maeneo yanakuwa na mafuta kwa wingi.

Sababu zinazosababisha ngozi kuwa na mafuta:

 1. Kurithi.
 2. Lishe.
 3. Kiwango cha homoni mbalimbali mwilini.
 4. Ujauzito.
 5. Vidonge vya kuzuia mimba.
 6. Baadhi ya vipodozi.
 7. Hali ya hewa ya joto.

Namna ya kutunza ngozi zenye mafuta

Faida kubwa ya kuwa na ngozi yenye mafuta ni kuwa haizeeki kwa haraka ikilinganishwa na aina nyinginezo za ngozi. Miongoni mwa mambo yanayosaidia ili kuitunza ngozi yenye mafuta na kuiepusha na chunusi na hali isiyopendeza ni:-

Ngozi yenye mafuta inahitajia kusafishwa vyema kwa maji ya moto na sabuni ili kuzuia vinyweleo visizibwe na mafuta.

Epusha vifaa vigumu visikwaruze uso wako na kupelekea ngozi kubanduka, kwani suala hilo husababisha tezi za mafuta kufanya kazi zaidi ili kujaza sehemu iliyopotea ya mafuta.

Epuka kutumia vipodozi ambavyo huifanya ngozi yako ipoteze maji au kukauka. Kwani husababisha sehemu ya juu ya ngozi inyauke, na hivyo kusababisha mafuta kuziba vinyweleo na kupelekea kutokea vichwa vyeusi.

Jitahidi kuitunza vyema ngozi yako na kuisafisha vizuri. Jaribu kuosha uso mara mbili au tatu kwa siku. Usioshe mara nyingi kwani kufanya hivyo huufanya uso kutoa mafuta zaidi.

Chagua kile unachosafishia kwa makini, jiepushe kutumia cream nzito nzito au vifaa vugumu wakati wa kuosha uso wako. Ni bora utumie sabuni za kawaida zisizokuwa na madawa. Unaweza kutumia lotion ya kuua bacteria au sabuni zisizo na dawa nyingi (lightly medicated), au sabuni zenye madini mbalimbali. Ni bora usioshe au kutumia lotion au michanganyiko yenye alkoholi.

Tumia maji ya moto au ya vuguvugu wakati unaosha uso wako.

Wakati unapoosha uso wako, ukande kwa kutumia ncha za vidole, jiepushe kupaka sabuni moja kwa moja usoni, inaweza kuganda na kuzuia vinyweleo kuziba.

Kutumia mask za udongo (clay) na tope (mud) husaidia katika ngozi za aina hii. Ni bora utumie mask mara moja au mbili kwa wiki.

Jitahidi kutumia vipodozi vya uso ambavyo vimetengenezwa kwa ajili ya ngozi yenye mafuta.

Jinsi ya kuvaa viatu mbalimbali inavyotakiwa na ili upendeze

Viatu ni kinga kwa ajili ya kuhifadhi miguu. Vile vile viatu ni vazi ambalo linaongeza urembo na nakshi kwa mvaaji. Viatu vipo vya aina mbalimbali na vinavaliwa kulingana na mahali na mavazi yanayoambatana navyo. Tuangalie baadhi ya aina za viatu na wapi hasa na vipi vikitumika vinapendeza zaidi.

1.Viatu vya ngozi vya kufunika

Viatu vya kufunika vipo virefu sana, vyenye urefu wa wastani na vifupi kabisa. Mara nyingine haviwi vya ngozi kabisa bali ni kama vina plastiki na pia vingine huwa na uwazi mdogo kwa mbele.Viatu virefu zaidi mara hupendeza zaidi kuvaliwa kwenye sherehe na kanisani. Unaweza kuvaa kazini kama kazi yako haikulazimu kutembea tembea maana vitachosha miguu yako na kupunguza ufanisi.

Viatu vyenye urefu wa wastani unaweza kuvaa popote iwe kazini, kanisani, kwenye sherehe n.k. Viatu vya chini kabisa vinakuwa vyenye matumizi zaidi wakati unamatembezi mengi. Havifai sana kuvaa kwenye sherehe za usiku hasa kama unavaa nguo maalumu ya usiku. Vinafaa sana kwa mjamzito hasa katika miezi ya mwisho.

2.Viatu vya wazi virefu

Viatu hivi vipo vya aina mbili, vyenye rangi za mng’ao na ambavyo ni mahususi kwa sherehe za usiku na vyenye rangi ngumu ambavyo waweza kuvaa kazini au kanisani. Viatu hivi vinapendeza kuvaliwa na nguo yoyote ila ikiwa ya urefu wa wastani ni nzuri zaidi maana huwezesha kuonekana urembo na uzuri wote wa kiatu. Viatu hivi vinakuja katika mitindo mbalimbali na unachagua ule ambao wewe unaupendelea zaidi mfano vyenye visigino vyembamba, visigino vinene au aina ya ‘wedges’.

3.Viatu vya wazi vifupi

Viatu hivi ni vizuri sababu vinawezesha miguu kupumua na ku’relax’. Viatu hivi vipo vya aina tofauti tofauti na vinafaa sana kuvaliwa kwa matembezi ya jioni, wakati wa safari ndefu, wakati ukiwa na mizunguko mingi na pia hata kazini au kanisani pale unapokuwa umevaa nguo za kawaida (casual). Havivutii sana kuvaliwa na suti au nguo ya usiku. Pia mara nyingi viatu vya chini hupendezea kuvaliwa na nguo ndefu( hasa casual) na viatu virefu hupendeza zaidi kwa nguo yenye urefu wa wastani.

4.Viatu vya muda maalumu

Hivi ni viatu ambavyo vinavaliwa wakati wa kazi maalumu kama wakati wa kazi za mashambani, mgodini, wakati wa michezo au wakati wa baridi kali.

Ni vyema na inapendeza kama unauwezo uwe na viatu vya aina mbalimbali angalau aina tatu. Mfano viatu vyeusi vya urefu wa wastani, viatu vya usiku vya wazi, viatu vya chini vya kufunika na vya wazi.

Matumizi ya Asali kwenye Urembo wa ngozi na Nywele

Asali hutumika kulainisha Ngozi

Asali ina asili ya kuvuta unyevu kutoka kwenye hewa na kuipa ngozi uwezo wa kuhifadhi unyevu hivyo ni faida kwa mtu mwenye ngozi kavu.

Jinsi ya kuandaa
Chukua asali mbichi kijiko kimoja cha chai kisha paka usoni, kaa nayo kwa dakika 15 hadi 20 kisha safisha uso wako.

Asali katika kusafisha ngozi, kutibu na kuzuia chunusi

Kutokana na uwezo wa asali katika kuua bacteria na kuvuta uchafu katika matundu ya ngozi asali itakusaidia kutatua tatizo la chunusi.

Jinsi ya Kuandaa
Chukua asali mbichi Kijiko kimoja cha chakula changanya na mafuta ya nazi vijiko viwili changanya mchanganyiko uwe mlaini kisha paka usoni huku ukisugua taratibu kwa kufanya kama viduara huku ukiepuka kufikisha machoni. ukimaliza kusugua uso na mchanganyiko wako osha uso wako.

Jinsi ya kuandaa kama kisafisha ngozi, exfoliator
Changanya kijiko kimoja asali na kijiko kimoja baking soda. tumia mchanganyiko huu kusugua ngozi yako. Asali inaongeza lishe na chembe chembe kuzuia madhara yanayotokana na sumu za hewani zinazozeesha ngozi. Baking soda inasaidia kusafisha matundu ya ngozi.

Asali inasaidia ngozi iliyoungua na jua kujirudi na kung’aa.

Jinsi ya kutumia asali katika nywele
Asali inatibu nywele kavu zilizopauka, na kulainisha ngozi kavu ya kichwa na kutibu muwasho kichwani.

Jinsi ya kufanya
Changanya kijiko kikubwa cha asali na maji ya uvuguvugu kisha paka kichwani Acha kwa muda wa saa 1 iwe kama conditioner kisha safisha nywele zako.

Unaweza kuchanganya asali kiasi cha kijiko kimoja mpk viwili katika maji vikombe vitano kisha safishia nywele zako taratibu, yaani yapitishe tu hayo maji kwenye nywele zako ambazo ni safi.

Tahadhari: Asali kwa kiasi kikubwa hupausha weusi wa nywele kutokana na Hydrogen Peroxide inayopatikana ndani ya asali.

Ni vema ukatumia asali mbichi kujihakikishia faida za asali katika mwili wako.
Iwapo unavutiwa na matumizi ya kitu cha asili katika urembo wako unaweza kuongeza kitu hicho katika kitu kingine unachotumia mfano katika steaming yako au scrub unayotumia.

Mambo ya Kuzingatia Kama una ngozi Kavu na Kuepuka kuwa na ngozi kavu

Ngozi kavu inaweza kukufanya ukose raha kutokana na kuwasha mara kwa mara, lakini pia kupauka hii inaweza kusababisha mikunjo ya ngozi na hata kupatwa na vidonda katika ngozi. Ngozi kavu husababishwa na baridi lakini pia unaweza ukawa umezaliwa nayo tu upo hivyo. kama una ngozi ya aina hii basi haya ni mambo matatu ya kuyaepuka kufanya.

Kuoga maji ya moto kwa muda mrefu

Epuka kuoga maji ya moto mara kwa mara kunaweza kufanya yale mafuta natural yanayo moisturize mwili kukauka, ili kuepuka tatizo hili ni vyema ukatumia maji ya uvuguvugu au baridi katika kuoga au kunawa mwili wako.

kutumia vipodozi vyenye Alcohol Nyingi

Alcohol nyingi husababisha ngozi kuzidi kuwa kavu, wakati wa kwenda kununua vipodozi vyako hakikisha unasoma maelezo na kujua kiasi cha alcohol kilichopo kama ni nyingi usichukue chukua yenye kiasi kidogo.

Kuosha Ngozi Na Sabuni Mara Kwa Mara Na Kusugua Kwa Nguvu

Kuosha ngozi mara nyingi sana na sabuni ni njia ya mojawapo ya kupata ngozi kavu. Ngozi kavu iliyokasirika huathirika zaidi na maambukizi ya bakteria kwa sababu kuosha mara nyingi huondosha safu za kinga ya ngozi yako.

Shopping Cart