Dondoo za Mapishi na Lishe

Jinsi ya kupika Wali wa hoho

Wali wa hoho ni chakula maalum kinachotumika katika hafla au sherehe. Ni chakula chenye ladha nzuri na kina muonekano wa kuvutia kinapokuwa mezani tayari kwa kuliwa.

Mara nyingi huandaliwa kama zawadi katika harusi hususan kwa watu wa pwani. Kwa kuwa zawadi hiyo au maarufu kama kombe huwa kuna vyakula vingi, ikiwamo chakula hiki ambacho hufanya kombe kuwa na muonekano wa kupendeza.

Mbali na kuliwa kama kombe chakula hiki kinaweza kuandaliwa kama mlo wa usiku.

Mahitaji:

β€’ Mchele Β½ kg
β€’ Nyanya 3
β€’ Mafuta ya kupika ΒΌ kikombe cha chai
β€’ Chumvi kiasi
β€’ Kitunguu swaumu kilichosagwa kijiko 1 cha mezani
β€’ Kitunguu maji kilichosagwa kijiko 1 cha mezani
β€’ Hoho 4
β€’ Nyama ya kusaga ΒΌ
β€’ Tangawizi kijiko 1 cha chakula
β€’ Limao au ndimu kipande

Maadalizi:

β€’ Chukua mchele uoshe vizuri kasha chuja maji
β€’ Chukua nyama ya kusaga na kamulia ndimu, weka chumvi na tangawizi, changanya vizuri na weka jikoni.iache ichemke hadi ikauke maji yote.
β€’ Chukua maji na kiasi cha robo tatu lita chemsha na weka pembeni
β€’ Chukua sufuria kavu yenye uwezo wa kupika kiasi cha kilo moja
β€’ Weka mafuta ya kupika kiasi cha vijiko vitatu na acha yapate moto
β€’ Weka vitunguu maji, menya nyanya na katakata halafu weeka katika sufuria hiyo.
β€’ Weka chumvi na kanga hadi vilainike kabisa
β€’ Baada ya kuiva weka vitunguu swaumu na baadaye mchele
β€’ Koroga hadi uchanganyike na weka nyama. Endelea kukoroga, baada ya hapo weka maji kiasi cha kuivisha mchele huo. Acha vichemke hadi vikaukie.
β€’ Palia mkaa juu yake au kama unatumia jiko la gesi au umeme weka kwenye oven hadi maji yakauke kabisa.
β€’ Baada ya hapo chukua hoho na kasha kata upande wa juu kama vifuniko. Kasha ondoa matunda ya ndani yake. Funika na kasha zipange kwenye sufuria yenye maji na chumvi na mafuta kidogo kiasi cha kijiko kimoja. Chemsha jikoni hadi ziive.
β€’ Baada ya kuiva, chukua hoho zako na kasha chota wali kw akutumia kijiko kasha jaza katika kila hoho na weka kwenye sahani tayari kwa kuliwa.
β€’ Unaweza kupamba na salad ukipenda.

Jinsi ya Kupika Kalmati

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour 2 vikombe vya chai)
Hamira (yeast kijiko 1 cha chai)
Sukari (sugar 2 vikombe vya chai)
Hiliki (cardamon 1/4 ya kijiko cha chai)
Maji kikombe1 na 1/2
Mafuta

Matayarisho

Changanya unga, hamira, maji na mafuta kijiko 1. Koroga vizuri mpaka upate uji mzito usiokuwa na madoge Baada ya hapo uache uumuke kisha zichome kalmati katika moto wa wastani. Baada ya hapo tia sukari, hiliki na maji 1/2 kikombe katika sufuria na ichemshe uku unakoroga mpaka iwe tayari.(ukitaka kujua kama iko tayari chovya mwiko kisha gusa na vidole utaona iko kama nta au gundi) Baada ya hapo tia kalmati na uzichange pamoja mpaka zikolee kisha zitoe na uziache mpaka zipoe tayari kwa kuliwa.

Madhara ya kula yai bichi

Yai bichi linaweza kuwa na vijidudu viitwavyo kwa kitaalamu β€œSALMONELLA” vinavyoweza kusababisha tumbo kuuma, kichefuchefu na pia kuharisha.
Vijidudu ya β€œSalmonella” vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa watoto, wazee na wale wenye hali dhaifu ya kimwili kama wagonjwa wa UKIMWI.

Pia yai bichi lililowazi linaweza kuwa zalio zuri la vimelea vya maradhi mbalimbali. Inashauriwa kupika yai mpaka liive kabisa, na kuhakikisha kwamba hakuna ute unaoteleza.

Kama ni yai la kuchemsha, lichemshwe kwa dakika kumi zaidi baada ya maji kuchemka. Pia ni muhimu kuhakikisha kwamba vyombo vilivyotumika k u k o rogea yai bichi vinaoshwa kwa maji na sabuni kabla ya kuvitumia tena kwa matumizi mengine ili kuepuka maradhi.

Mapishi ya Maini ya kuku

Mahitaji

Maini ya kuku 1/2 kilo
Vitunguu vikubwa 2
Hoho 1
Pilipil 1
Limao 1/2
Swaum/tangawizi 1 kijiko cha chai
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Safisha maini weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu,swaum na tangawizi pamoja (hakikisha vitunguu visiwe vya brown), kisha tia maini, curry powder, pilipili, chumvi ,hoho na limao kisha changanya vizuri na ufunike. Pika mpaka maini yaive na hakikisha yanakuwa na rojo kidogo. Baada ya hapo ipua na yatakuwa tayari kwa kuliwa na chochote upendacho kama vile chapati, chips, ugali, wali.

Jinsi ya kuandaa Ndizi Mbichi Za Supu Ya Nyama Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi mbichi – Kisia

Nyama ng’ombe – Β½ kilo

Pilipili ya kusaga – 1 kijiko cha chai

Tangawizi ya kusaga – 2 vijiko vya supu

Thomu (garlic/saumu) – 1 kijiko cha supu

Bizari mchuzi – 1 kijiko cha chai

Nazi ya unga (ukipenda kuongezea) – 2 vijiko cha supu

Chumvi – Kiasi

Ndimu – 1 kamua

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka nyama ng’ombe katika sufuria, tia tangawizi, thomu, pilipili mbichi, bizari, chumvi. Roweka kidogo ukipenda kisha ikaushe yenyewe kwa maji yake
Ongezea maji ya kiasi yasizidi mno, kisha funika na chemsha.
Menya ndizi, ukatekate.
Nyama ikikaribia kuiva, weka ndizi uendelee kupika mpaka viive vyote.
Tia nazi ya unga kidogo tu ukipenda. Koleza kwa bizari mchuzi, pilipili, na ndimu
Epua mimina katika chombo cha kupakulia zikiwa tayari.

Jinsi ya kutengeneza Rock-cakes Za Njugu Na Matunda Makavu

Mahitaji

Unga – 4 Vikombe

Sukari -10 Ounce

Siagi – 10 Ounce

Mdalasini ya unga – 2 vijiko vya chai

Matunda makavu/njugu (kama lozi, Zabibu, maganda ya chungwa, Cherries na kadhalika – 4 ounce

Maziwa ya maji – 4 Vijiko vya supu

Maandalizi

Chukua siagi na sukari koroga na mixer mpaka iwe kama cream.
Tia vanilla mdalasini, tia yai moja mix tena endelea kuongeza yai lingine mpaka umalize yote, changanya mpaka iwe laini kama sufi (fluffy)
Tia unga na baking powder na dried fruits, changanya na mwiko.
Chota mchanganyiko na kijiko cha soup weka kwenye treya ya kupikia tandaza na uma ili upate matundu juu ya biskuti.
Pika (bake) kwenye oven lenye moto wa 375Β F. kwa muda wa dakika 15 hivi huku unazitazama tazama.

Jinsi ya kuandaa Pilau ya sosi ya soya, nyama na mboga

Mahitaji

Nyama isiyokuwa na mifupa – 1 Β½ Lb(ratili)
Mchele wa Basmati (rowanisha) – 3 Magi
Vitunguu maji – 2
Mchanganyiko wa mboga za barafu – 1 Magi
(karoti, mahindi, njegere)
Pilipili Mbichi – 3
Pilipili mboga kijani na nyekundu – 1
Pilipili manga – Β½ kijiko cha chai
Chumvi – Kiasi
Sosi ya soya (soy sauce) – 5 Vijiko vya supu
Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 Kijiko cha supu
Mchanganyiko wa bizari (garam masala) – 1 Kijiko cha supu
Kotmiri iliyokatwa – Β½ Kikombe
Mafuta ya kukaangia – Kiasi

Namna Ya Kutaarisha

Ndani ya sufuria, tia mafuta yakipata moto kaanga vitunguu mpaka ziwe rangi ya hudhurungi.
Kisha tia nyama iliyokatwa vipande vidogo vidogo pamoja na maji ya kiasi na viungo vyote isipokuwa mchele, mboga zote na kotmiri. chemsha mpaka nyama iwive na maji yakauke.
Halafu changanya na mboga na iwache kwa muda wa dakika kumi kisha tia kotmiri na umimine kwenye bakuli au treya ya oveni na uweke kando.
Chemsha mchele na chumvi uwive kama kawaida ya kupika wali wa kuchuja, kisha umwagie juu ya ile treya ya nyama.
Nyunyizia mafuta na sosi ya soya na ipike katika oveni moto wa 350Β° kwa muda wa dakika 20 hivi.
Ukishawiva, uchanganye ukiwa tayari kwa kuliwa

Mapishi ya Pilau Ya Adesi Za Brown Karoti Na Mchicha Kwa Samaki Wa Salmon

Vipimo

Mchele vikombe 3

Karoti 1 ikune (grate)

Mchicha katakata kiasi

Adesi za brown

Kitunguu katakata (chopped)

Supu ya kitoweo chochote upendayo au vidonge vya supu 2

Garama masala (bizari mchanganyiko) kijiko 1 cha kulia

Samli ΒΌ kikombe

Chumvi kiasi

Vipimo Vya Samaki Wa Salmon

Samaki wa Salmon vipande 4 vikubwa

Tangawizi mbichi ilosagwa kijiko 1 cha kulia

Thomu (garlic/saumu) kijiko 1 cha kulia

Chumvi kiasi

Bizari ya mchuzi kijiko 1 cha kulia

Ndimu 1 kamua

Nyanya 2 kata slice kubwa kubwa

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Samaki wa Salmon

Changanya viungo vyote upake katika samaki.
Weka katika treya na panga slice za nyanya juu yake.
Oka (grill/choma) katika oven umgeuze samaki upande wa pili.
Akiwa tayari epua.

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Wali

Roweka mchele kiasi kutegemea aina ya mchele. Tumia basmati (pishori)
Roweka adesi kisha zichemshe katika maji ya kiasi. Chuja maji adesi na maji yatakayobakia tumia katika kupikia pilau hii.
Kaanga vitunguu katika samli iliyoshika moto kwenye sufuria ya kupikia.
Vikianza kugeuka rangi tia karoti, mchicha, adesi, bizari mchanganyiko kisha kaanga kidogo.
Tia mchele ukaange kidogo kisha tia supu au maji pamoja na kidonge cha supu.
Tia chumvi ukoroge funika upike kama pilau.
Epua upakue katika sahani utolee kwa samaki wa salmon

Jinsi ya kutengeneza Wali Wa Dengu Kwa Samaki Wa Kukaanga

Mahitaji

Mchele wa basmati – 3 Vikombe

Dengu – 2 vikombe

Viazi – 3 vikubwa

Kitunguu – 2 kubwa

Nyanya – 2

Pilipili mbichi kubwa – 3

Pilipilimanga – Β½ kijiko cha chai

Garama Masala (bizari mchanganyiko) -1 kijiko cha chai

Supu ya vidonge (stock cubes) – 2 vidonge

Chumvi – kiasi

Mafuta – ΒΌ kikombe

Zaafarani – 1 kijiko cha chai

Samaki wa kukaanga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Dengu kama sio za tayari kwenye kopo, roweka na zichemshe hadi ziwive

Maandalizi ya Masala Ya Dengu:

Zaafarani – iroweke katika maji ya dafu dafu (warm) ya chini ya robo kikombe weka kando.
Osha mchele, roweka.
Menya viazi na vitunguu, katakata vitunguu, na nyanya , weka kando.
Katakata viazi vipande vidogo vidogo kwa umbo la mchemraba (cubes).
Katika sufuria tia mafuta yakipata moto, tia viazi ukaange kidogo kwa moto mdogo mdogo hadi kukaribia kuwiva, toa weka kando.
Kaanga vitunguu hadi vigeuka rangi ya hudhurungi isiyokoza (light brown) kisha tia nyanya ukaange kidogo.
Tia vidonge vya supu (stock cubes) uvivuruge katika mchanganyiko, katakata pilipili mbichi kwa urefu tia, uendelee kukakaanga. Tia bizari, chumvi.
Zima moto, changanya dengu na viazi katika mchanganyiko huo.

Mapishi ya Wali:

Chemsha mchele kama kawaida ya kupika wali mweupe, kiini kiwe kimewiva nusu yake.
Chuja maji kisha changanya katika mchanganyiko wa dengu.
Nyunyizia zaafarani, uchanganye wali na mchanganyiko kidogo tu.
Funika acha uive katika mtoto mdogo mdogo au tia katika oveni hadi uive kama kawaida ya kupika wali.
Pakua katiha sahani na tolea na samaki yoyote wa kukaanga.

Mapishi ya Viazi vitamu na kachumbari

Mahitaji

Viazi utamu 3
Nyanya 2 kubwa
Kitunguu
Tango
Limao
Chumvi
Pilipili
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Menya viazi na kisha vikate katika vipande. Tia mafuta kwenye chuma cha kukaangia, yakisha pata moto tia viazi nauviache vikaangike mpaka upande mmoja uwe wa brown na kisha geuza upande wa pili na upike mpaka uwe wa brown. Vikisha iva ipua na uweke kwenye kitchen towel ili vikauke mafuta.
Kachumbali: Katakata vitunguu katika bakuli na kisha tia chumvi kwa ajili ya kuondoa ukali wa vitunguu. Baada ya hapo vioshe mpaka chumvi yote iishe. osha nyanya, Pilipili tango na kisha katakata slice nyembamba na uchanganye na vitunguu. Baada ya hapo tia chumvi, kamulia limao na uchanganye zote pamoja .Baada ya hapo viazi na kachumbali vitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kuandaa biskuti za Siagi Na Jam

MAHITAJI

Unga – 2 Vikombe
Sukari ya icing – 1 Kikombe
Siagi – 250 gm
Yai – 1
Vanilla – 2 Vijiko vya chai
Baking powder -1 Kijiko cha chai
Jam – ΒΌ kikombe
Lozi – ΒΌ kikombe

JINSI YA KUPIKA

Koroga siagi na sukari katika mashine ya keki (cake mixer) mpaka iwe laini (creamy).
Tia yai na vanilla koroga mpaka mchanganyiko uwe laini kama sufi.
Tia unga na baking powder changanya na mwiko.
Chota mchanganyiko kwa mkono (kiasi cha kijiko kimoja cha supufanya duara kisha weka kwenye treya ya kupikia.
Bonyeza kila kiduara katikati kwa kidole, kisha weka jam na tupia lozi zilizomenywa na kukatwa katwa.
Pika (bake) katika oven moto wa 375Β° F kama muda wa dakika 15 hivi huku unazitazama tazama

Mapishi ya Wali Wa Nyanya Wa Kukaanga

Vipimo

Mchele basmati, pishori – 3 vikombe

Vitunguu katakata – 2

Nyanya/tungule katakata – 5 takriban

Viazi/mbatata menya katakata – 3 kiasi

Thomu (saumu/garlic) ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Bizari mchanganyiko – 1 kijiko cha kulia

Hiliki ya unga – Β½ kijiko cha chai

Kidonge cha supu – 2

Chumvi – kisia

Mafuta – Β½ kikombe

Maji ya moto au supu – 5 takriban

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha na roweka mchele
Katika sufuria weka mafuta yashike moto, tia viazi, vitunguu ukaange.
Vikianza tu kugeuka rangi tia thomu na bizari, hiliki, endelea kukaanga kidogo.
Tia nyanya kaanga lakini usiache zikavurugika sana.
Tia mchele ukaange chini ya dakika moja.
Tia maji ya moto, na kidonge cha supu au supu yoyote kiasi cha kufunika mchele yazidi kidogo.
Koroga vichanganyike vitu, kisha funika upike kama pilau.
Pakua ikiwa tayari, tolea kwa samaki wa kukaanga au kitoweo chochote kile

Mapishi ya Chai ya maziwa, mandazi, uyoga na mayai

Mahitaji

Mandazi (angalia jinsi ya kupika katika recipe ya mandazi ya nyuma)
Uyoga (mashroom kikombe 1 cha chai)
Mayai (eggs 4)
Hoho (greenpepper 1/4 ya hoho)
Nyanya (fresh tomato 1)
Kitunguu (onion 1/4 ya kitunguu)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)
Hiliki nzima (cardamon 4)
Masala ya chai (tea masala 1 kijiko cha chai)
Pilipili mtama iliyosagwa (ground black pepper 1/4 ya kijiko cha chai)
Maziwa (fresh milk 1 kikombe cha chai)
Majani ya chai (tea leaves)
Maji kiasi.
Sukari (sugar)

Matayarisho

Jinsi ya kupika chai, weka maziwa, maji kiasi,hiliki, masala ya chai, pilipili mtama na majani katika sufuria. Chemsha kwa muda wa dakika 10 na chai itakuwa tayari.
Jinsi ya kupika mayai, weka mafuta kiasi katika fry pan na utie vitunguu, vikaange kidogo kisha tia nyanya, chumvi na hoho. Pika kwa muda wa dakika 4 kisha tia mayai na uyaache yaive mpaka yakauke kisha geuza upande wa pili na uyapike mpaka ya ive kisha ipua.
Jinsi ya kupika uyoga, weka mafuta kidogo katika fry pan kisha tia uyoga na chumvi na ukaange mpaka uive katika moto wa wastani. Ukisha iva breakfast yako itakuwa teyari kwa kuseviwa.

Jinsi ya kutengeneza Cookies Za Tende Na Tangawizi

MAHITAJI

Unga vikombe vikombe 4

Baking soda 1 kijiko cha chai mfuto

Siagi 400 gms

Sukari Β½ kikombe

Tende chambua ukatekate ifikie ΒΎ kikombe

Tangawizi ya unga vijiko 2 vya chai

Vanilla 1 kijiko cha chai

Yai 1

Maziwa mazito vijiko 2 vya kulia.

MAANDALIZI

Changanya siagi na sukari katika mashine usage mpaka iwe laini nyororo.
Tia yai uchanganye vizuri
Tia tende na vanilla, tangawizi uchanganye vizuri.
changanya unga na baking soda kisha, mimina kidogo kidogo huku unachanganya kwa kijiko cha ubao (mwiko).
Unga ukiwa mzito ongeza vijiko 2 vya maziwa. Fanya viduara upange katika treya uliyopakaza siagi kisha uchome (bake) katika over moto mdogo wa kiasi dakika 15 vigeuke rangi viwive.
Epua vikiwa tayari

Shopping Cart
19
    19
    Your Cart
    🏠 Home πŸ“– Reading πŸ–ΌοΈ Gallery πŸ’¬ AI Chat πŸ“˜ About