Dondoo za Mapishi na Lishe

Jinsi ya kupika Wali Wa Samaki Na Mboga

VIPIMO VYA SAMAKI

Samaki wa sea bass vipande – 1 1/2 LB (Ratili)
Kitunguu saumu(thomu/galic) -1 Kijiko cha supu
pilipili mbichi iliyosagwa – 1 Kijiko cha chai
Bizari ya manjano au ya pilau – 1/2 Kijiko cha chai
Paprika ya unga au pilipili ya unga – 1 kijiko cha chai
Chumvi – Kiasi
Ndimu
Mafuta – 3 Vijiko vya supu

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Roweka samaki kwa viungo hivyo vyote kwa muda wa robo saa hivi.

Washa oven moto wa 400F.
Kisha weka samaki katika trea na choma kwa muda wa dakika 15 na weka moto wa juu dakika za mwisho ili ipate rangi nzuri.
Ikishaiva epua na itakuwa tayari kuliwa.

VIPIMO VYA MBOGA

Gwaru (green beans) – 1 LB
Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha supu
Karoti – 4-5
Chumvi – Kiasi
Bizari ya manjano – 1/2 Kijiko cha chai
Pilipili manga – 1/4 kijiko cha chai
Mafuta ya zaituni – Kiasi

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Kata kata karoti na toa sehemu ya mwisho za binzi.
Weka mafuta katika sufuria kisha kaanga karoti na gwaru
Kisha weka moto mdogo na funika ili ziwive na sio kuvurujika.
Karibu na kuiiva tia thomu kaanga kidogo,tia bizari ,chumvi na pilipili manga.
Ikisha changanyikana vizuri epua na tayari kuliwa na wali na samaki.

Mapishi ya Muhogo Na Mbatata Za Nazi Kwa Nyama Ngombe

Vipimo – Mahitaji Ya Nyama

Nyama ya n’gombe ya mifupa – 3 lb

Tangawizi mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Kitunguu thomu – 1 kijiko cha supu

Bizari ya pilau/jira/uzile (cumin) – 1 kijiko cha supu

Ndimu – 1

Kitunguu kilokatwakatwa (chopped) – 1 cha wastan

Pilipili mbichi – 3 Zilizosagwa

Chumvi – Kiasi

Vipimo – Muhogo Na Mbatata/Viazi

Muhogo menya na ukate vipande pande – 2

Mbatata/Viazi menya ukate vipande vikubwa kiasi – 5 kiasi

Tui la nazi zito – 1 gilasi

Nyanya ilokatwakatwa au kusagwa – 1

Kitunguu kilokatwakatwa (chopped) – 1 kiasi

Bizari ya mchuzi – kiasi

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha nyama kisha weka katika pressure cooker au sufuria.
Tia viungo vyote vya nyama uchanganye vizuri, kisha ikorogekoroge mpaka maji yake yakaribie kukauka. Usifunike.
Tia maji kiasi ya kuivisha nyama na kubakisha supu yake kiasi ya kuivisha muhogo na mbatata. Muda wa kuivisha nyama inategemea nyama yenyewe na kama unatumia pressure cooker ni takriban dakika 35-40. Ikiwa sufuria ya kawaida utakuwa unaikoroga.
Mimina ndani ya supu, muhogo, mbatata, nyanya, kitunguu, bizari ya mchuzi, chumvi.
Acha ichemke uive muhogo na viazi.
Tia tui la nazi, changanya vizuri acha kwenye moto dakika chache tu.
Epua ikiwa tayari. Tolea na achari.

Mapishi mazuri ya Chapati za maji

Mahitaji

Unga wa ngano (plain flour) ( 1/4 kilo)
Yai (egg 1)
Sukari (sugar 1/4 kikombe cha chai)
Chumvi (salt 1/4 kijiko cha chai)
Hiliki (ground cardamon 1/4 kijiko cha chai)
Maji kiasi
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Tia unga kwenye bakuli, kisha weka sukari, chumvi, hiliki na maji kiasi. Kisha koroga mpaka mchanganyiko wako uwe mzito. Baada ya hapo tia yai na ukoroge tena. hakikisha mchanganyiko hauwi mzito sana au mwepesi sana.Baada ya hapo onja kama kila kitu kimekolea. Injika chuma cha kupikia chapati (fry-pan) jikoni katika moto wa wastani. Baada ya hapo tia nusu kijiko cha chakula cha mafuta katika fry-pan na kisha yatandaze. Hakikisha chuma kinapata moto na weka upawa mmoja wa unga wa chapati na uutandaze mpaka uwe flat. Baada ya hapo subiri mpaka chapati ikauke juu na kisha igeuze upande wa pili tia mafuta kijiko 1 kikubwa cha chakula kwa upande wa chini na wa juu kisha uanze kuikandamiza kwa juu na kijiko ili iweze kuiva vizuri kwa chini. Ikisha kuwa ya rangi ya brown igeuze na upike upande wa pili kiasi kisha iipue na uiweke kwenye sahani yenye kitchen towel ili kukausha mafuta. Rudia hii process kwa unga wote uliobakia. Na chapati zitakuwa tayari

Mambo ya msingi kufahamu kuhusu Lishe

Nini maana ya lishe?

• Lishe yahusu mafunzo ya chakula na jinsi miili yetu inavyotumia chakula kamakichocheo cha ukuaji, kuzaana na utunzaji wa afya.
• Lishe inajumuisha mchakato wa utoaji virutubishi vinavyohitajika kwa afya, ukuaji, kuendelea na kuishi.

Umuhimu wa lishe bora

Lishe bora ni muhimu katika mambo yafuatayo

• Utoaji nishati ili kuishi, uwepo wa mwendo, utendaji kazi, na joto.
• Ukuaji, uendeleaji, ujengaji mwli, urejeshaji na utengenezaji wa seli na mikusanyika ya seli hizo (tishu)
• Ufanyaji michakato ya kikemia kama vile uyeyushaji chakula, umetaboli na utunzaji mwili.
• Kinga dhidi ya magonjwa, upigaji vita maambukizi na uponaji magonjwa.
• Ili afya njema iweze kudumishwa, mlo wa kila siku lazima ukamilishe shughuli nne zilizotajwa hapo awali. Vyakula vinavyokamilisha moja au zaidi ya shughuli tatu huitwa virutubishi.

Virutubishi

Aina za irutubishi vikuu tunavyohitaji kwa wingi. Hivi ni:

• kabohaidreti (vyakula vya wanga, sukari na vyakula vya ufumwele):
• mafuta yatokanayo na wanyama – haya yapo ya aina kadhaa
• Protini- kuna mamia ya aina mbalimbali za protini.
• Maji.

Virutubishi vidogovidogo tunavyohitaji kwa kiwango kidogo. Kuna aina nyingi ya hivi bali vile vinavyoelekea kukosekana kwenye mlo ni:

• madini – madini ya chuma (angalia Kisanduku cha 6, ukurasa 16), madini ya joto na zinki.
• vitamnini – vitamini A, vitamini za kundi B (ikiwemo folate) na vitamini C. Kama chakula chaweza kuwa chanzo bora cha kirutubishi au la hutegemea:
• Kiwango cha kirutubishi katika chakula. Vyakula vyenye viwango vingi vya virutubishi vidogovidogo kulinganisha na viwango vyake vya nguvu huitwa vyakula ‘vilivyosheheni virutubishi’ (nutrient-rich) au wakati mwingine huitwa vyakula vyenye ‘ujanzo mwingi’ wa virutubishi (nutrient dense). Vyakula hivi hupendwa kwa kuwa hutoa virutubishi vyote vinavyohitajika. Kiambatisho hiki kinaorodhesha vyakula vinavyotoa viwango muhimu vya virutubishi mbalimbali.
• Kiwango cha chakula kinachotumika mara kwa mara.

Mapishi – Fish Finger

Leo tunaangalia mapishi ya fish finger ( sijui kama unaweza kusema kidole cha samaki)!, Ni mlo mzuri hasa kuliwa kama kitafunio au mboga ya pembeni.

Mahitaji

500g Fileti ya samaki
120g Chenga za mkate
100g Unga wa ngano
Mayai 2
Ndimu 1
Kitunguu saumu 1
Kotmiri
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Menya vitunguu saumu kisha visage

Katakata fileti kwa muundo wa mraba (kama vidole) kisha paka mchanganyiko wa vitunguu saumu

Kata ndimu na kamulia kwenye fillet yako

Weka chenga za mkate kwenye bakuli kisha uchanganye chumvi kiasi na kata kata kotmiri majani 3 na uchanganye pamoja.

Kwenye bakuli lingine weka mayai na uyapigepige yawe kama uji mzito

Weka unga kwenye bakuli jingine.

Chukua kipande cha fillet kiweke unga kidogo kisha kizamishe kwenye yai na baada ya hapo kizamishe kwenye mchanganyiko wa chenga za mkate. Fanya hivyo kwa vipande vyote.

Weka mafuta kwenye kikaago na subiri yachemke kisha weka fillet zako vizuri na zikaange pande zote hadi zimekuwa rangi ya brown ( hakikisha moto sio mkali sana).

Epua na weka pembeni mafuta yote yakauke

Weka kwenye sahani tayari kwa kula.

Jinsi ya kupika Viazi Vya Nazi Kwa Nyama

Mahitaji

Viazi – 3lb

Nyama – 1lb

Kitunguu – 1

Nyanya – 2

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha chai

Manjano – ½ kijiko cha chai

Curry powder – ½ kijiko chai

Nyanya kopo – 1 kijiko cha chai

Pilipili ya unga – kiasi upendavyo

Chumvi – kiasi

Kidonge cha supu – 1

Tui la nazi – 1 kopoau zaidi

Mtindi ukipenda – 3 vijiko vya supu

Kotmiri – kiasi ya kupambia

Nazi ya unga – 4 vijiko vya supu

Mafuta – 2 vijiko vya supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Kata nyama vipande vipande kisha chemsha na chumvi mpaka iive.
Menya maganda viazi na ukate slice kubwa weka pembeni
Kata kata kitunguu kisha kaanga na mafuta mpaka vibadilike rangi
Tia thomu, bizari ya manjano, pilipili ya unga, nyanya kopo
Kata kata nyanya nzima vipande vidogo tia na kidonge cha supu.
Kisha tia viazi, nyama na tui la nazi finika mpaka viazi viwive lakini visiwe vikavu.
Tia mtindi na nazi ya unga kama vijiko 4 vya supu iache motoni kidogo kisha pakua, tupia kotmiri juu na itakuwa tayari kuliwa.

Mapishi ya wali wa Kiafrika Mangaribi

Mahitaji

Mchele (rice vikombe 2 na 1/2)
Vitunguu (onion 2)
Nyanya ya kopo (tin tomato kopo 1)
Tangawizi (ginger paste kijiko 1 cha chakula)
Kitunguu swaum (garlic paste kijiko 1 cha chakula)
Paprika (kijiko 1 na 1/2 cha cha chai)
Pilipil (scotch bonnet pepper 1)
Curry powder (kijiko 1 cha chai)
Maggi cubes 3(unaweza kutumia yenye ladha ya chicken, beef au vegetable. Inategemea unasevu na mchuzi wa aina gani)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Loweka mchele kwa muda wa dakika 10.Katakata vitunguu kisha weka pembeni, saga pamoja nyanya ya kopo,pilipili, tangawizi na kitunguu swaum kisha weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu vikiiva tia curry powder, maggi cubes, chumvi na paprika na uchanganye vizuri. Kisha tia mchanganyiko wa nyanya na uupike mpaka uive. Baada ya hapo tia mchele na maji na uupike mpaka ukaribie kuiva kisha ugeuze na umalizie kwa kutia njegere na umalizie kuupika mpaka uive. baada ya hapo utakuwa tayari kuseviwa na mboga yoyote kama kuku, nyama, samaki au assorted meat (Mchanganyiko wa utumbo, makongoro na nyama), Hapo mimi nili-save na mchuzi wa kuku wa kienyeji.

Mapishi ya Ugali Mchuzi Wa Samaki Nguru Wa Nazi Na Bamia Za Kukaanga

Vipimo Vya Ugali:

Unga wa mahindi/sembe – 4

Maji – 6 takriban

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chota unga kidogo katika kibakuli uchanganye na maji kidogo .
Weka maji mengineyo katika sufuria kwenye moto.
Changanya na mchanganyiko mdogo ufanya kama uji.
Kisha kidogo kidogo unaongeza sembe huku unakoroga na kuusonga ugali hadi uive.

Vipimo Vya Mchuzi Wa Samaki Wa Nazi

Samaki nguru – 5 vipande

Pilipili mbichi ilosagwa

Kitunguu maji kilosagwa – 1 kimoja

Nyanya ilosagwa – 2

Haldi/tumeric/bizari ya manjano – ¼ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Ndimu – 2 kamua

Tui la nazi zito – 2 vikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Baada ya kumuosha samaki, weka katika sufuria.
Tia chumvi, ndimu, pilipili mbichi ilosagwa.
Tia vitunguu na nyanya zilosagwa
Mkaushe kwa hivyo viungo, akianza kukauka tia tui la nazi.
Acha kidogo tu katika moto tui liwive mchuzi ukiwa tayari.

Vipimo Vya Bamia

Bamia – ½ kilo takriban

Nyanya kopo – 1 kijiko cha chai

Methi/uwatu/fenugreek seeds ilosagwa – 1 kijiko cha chai

Dania/corriander ilosagwa – ½ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Mafuta – 1 kikombe cha kahawa

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata bamia kwa urefu.
Weka mafuta katika karai, kisha tia bizari zote na nyanya kopo, kaanga kidogo.
Tia bamia endelea kukaanga, kisha acha katika moto mdogomdogo ufunike.
Kila baada ya muda funua karai ukaange bamia hadi ziwive zikiwa tayari.

Jinsi ya kupika Biskuti Za Njugu/Matunda Makavu (Rock Cakes)

Viambaupishi

Unga 4 Vikombe

Sukari 10 Ounce

Siagi 10 Ounce

Mdalasini ya unga 2 vijiko vya chai

Matunda makavu/njugu (kama lozi,
Zabibu, maganda ya chungwa,
Cherries na kadhalika 4 ounce

Maziwa ya maji 4 Vijiko vya supu

Jinsi ya kuandaa na kupika

1) Chukua siagi na sukari koroga na mixer mpaka iwe kama cream.

2) Tia vanilla mdalasini, tia yai moja mix tena endelea kuongeza yai lingine mpaka umalize yote, changanya mpaka iwe laini kama sufi (fluffy)

3) Tia unga na baking powder na dried fruits, changanya na mwiko.

4) Chota mchanganyiko na kijiko cha soup weka kwenye treya ya kupikia tandaza na uma ili upate matundu juu ya biskuti.

5) Pika (bake) kwenye oven lenye moto wa 375 F. kwa muda wa dakika 15 hivi huku unazitazama tazama.

Mapishi ya chipsi

Mahitaji

Viazi (potato) 1/2 kilo
Mafuta ya kukaangia (veg oil)
Chumvi

Matayarisho

Menya viazi kisha vioshe na vikaushe maji yote kwa kutumia kitchen towel.Baada ya hapo katakata katika shape ya chips uzipendazo either nyembamba au nene kisha zikaushe tena maji na uzitie chumvi. Baada ya kuzitia chumvi tu zitie kwenye mafuta ya kukaangia straightaway (hakikisha mafuta yasiwe ya moto sana kwani utazibabua) Zipike upande mmoja ukiiva geuza upande wa pili. Baada ya hapo endelea kuzipika uku ukiwa unazigeuzageuza mpaka kwa nje ziwe light brown na crisps.Baada ya hapo zitoe na uziweke kwenye kitchen towel ili zichuje mafuta na zitakuwa tayari kwa kuliwa.

JINSI YA KUANDAA VILEJA

MAHITAJI

Unga wa mchele – 500g

Samli – 250g

Sukari – 250g

Hiliki iliyosagwa – 1/2 kijiko cha chai

Arki (rose flavour) – 1/2 kijiko cha chai

Baking powder – 1 kijiko cha chai

Mayai – 4

Maji ya baridi – 1/2 kikombe cha chai

MAANDALIZI

Saga sukari iwe laini kiasi, changanya unga wa mchele, baking powder, hiliki na sukari.
Pasha moto samli mpaka iwe nyepesi kama maji mimina kwenye ule mchanganyiko wa unga wa mchele, kisha uchanganye pamoja na arki.
Ongeza mayai yaliopigwa endelea kuchanganya mpaka unga umeanza kuchanganyika vizuri.
Ongeza maji ya baridi sana kama nusu kikombe tu ili uchanganyike vizuri.
Kata kwa design unayotaka viwe vinene visiwe kama cookies za kawaida kama ilivyo kwenye picha na ukipenda utaweka kidoto kwa kutumia zaafarani katikati ya kileja kama inavyoonesha hapo juu.
Choma kwa moto wa baina ya 300F na 350F kwa dakika 15 mpaka 20 visiwe vyekundu toa na tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Samaki wa kupaka

Mahitaji

Samaki (Tilapia 2)
Nyanya ya kopo (Tomato tin 1)
Kitunguu (Onion 1)
Tangawizi (ginger kiasi)
Kitunguu swaum (garlic clove )
Mafuta (Vegetable oil)
Pilipili (scotch bonnet pepper 1)
Tui la nazi zito (coconut milk 2 vikombe vya chai)
Curry powder 1/2 cha kijiko cha chai
Binzari nyembamba ya unga (ground cumin 1/2 kijiko cha chai
Binzari manjano (turmaric 1/2 kijiko cha chai
Chumvi (salt)
Limao (lemon 1)
Giligilani (fresh coriander)

Matayarisho

Marinate samaki na chumvi, limao, kitunguu swaum, tangawizi kwa muda wa masaa 6 au zaidi. Baada ya hapo wakaange au waoke katika oven mpaka waive ila usiwakaushe sana. Baada ya hapo saga pamoja nyanya ya kopo, kitunguu maji, kitunguu swaum na tangawizi. Kisha bandika huo mchanganyiko jikoni na upike mpaka ukauke maji kisha tia mafuta, binzari zote, curry powder, chumvi na pilipili na upike kwa muda wa dakika 5. Baada ya hapo tia maji kidogo (kama 1/2 kikombe) pamoja na tui la nazi. Acha uchemke mpaka tui liive na mchuzi ubakie kiasi. Baada ya hapo waweke samaki kwenye sufuria ya kuokea na kisha umwagie huo mchuzi juu ya hao samaki na owaoke (bake) kwa muda wa dakika 20. Ukisha toa kwenye oven katakata giligilani na utie kwenye hao samaki na hapo watakuwa tayari kwa kuliwa. unaweza kuwala na wali, ugali au chapati

Mapishi ya Sambusa za nyama

Mahitaji

Nyama ya kusaga (minced beef 1/4 kilo)
Vitunguu maji vilivyokatwakatwa(diced onion 2 vikubwa )
Kitunguu swaum/ tangawizi (garlic and ginger paste 1 kijiko cha chakula)
Chumvi (salt)
Pilipili iliyokatwakatwa (scotch bonnet 1)
Limao (lemon 1/2)
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Cinnamon powder 1/4 kijiko cha chai
Coriander powder 1/4 kijiko cha chai
Cumin powder 1/4 kijiko cha chai
Unga wa ngano (all purpose flour kidogo)
Manda za kufungia (spring roll pastry)
Giligilani (fresh coriander kiasi)
Mafuta ya kukaangia

Matayarisho

Changanya nyama na limao, chumvi, pilipili,kitunguu swaum, tangawizi na spice zote, kisha pika katika moto wa kawaida mpaka nyama iive na maji yote yakauke. Baada ya hapo kabla hujaipua nyama tia vitunguu na giligilani na uvipike pamoja kwa muda wa dakika 2 na uipue weka pembeni na uache viipoe. Baada ya hapo tia unga kidogo katika bakuli nauchanganye na maji kidogo kupata uji mzito kwa ajili ya kugundishia manda. Baada ya hapo tia nyama katika manda na kisha zifunge kwa kugundishia na unga wa ngano.Ukisha maliza kuzifunga zote zikaange mpaka ziwe za brown na uzitoe. Na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Borhowa

Mahitaji

Daal (lentils) nyekundu au/na kijani – 1 Kikombe kikubwa

Bizari ya manjano ya unga – 1/2 Kijiko cha chai

Pili pili ya unga – 1/2 kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Maji ya ndimu – 3 Vijiko vya supu

Kitunguu – 1 kiasi

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 Kijiko cha chai

Bizari ya unga (cummin powder) – 1 Kijiko cha chai

Mafuta ya kukaangia – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha daal kwa kutoa mawe ikiwa yapo, kisha osha na roweka dakika 15 hivi.
Kisha chemsha kwa kutia maji, bizari ya manjano, chumvi, pili pili ya unga na maji ya ndimu hadi iive na kuvurujika.
Halafu chukua kisufuria na kaanga kitungu, kisha thomu na mwisho tia bizari ya pilau.
Kisha mimina mchanganyiko wa kitunguu kwenye sufuria ya daal (iliyokwisha iiva)na uchanganye na iwache motoni kidogo itokote.
Ukipenda mimina mchanganyiko kwenye blenda na usage mpaka iwe laini.
Tia kwenye bakuli na itakuwa tayari kuliwa na wali na samaki ukipenda

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About