Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Supu Ya Maboga

Viamba upishi

Blue band vijiko vikubwa 2
Maziwa vikombe 2
Royco kijiko kikubwa 1-2
Pilipili manga (unga) kijiko cha 1
Chumvi kiasi Maji lita 2-3
Boga kipande ½
Viazi mviringo 2
Vitunguu 2
Karoti 2
Nyanya 2

Hatua

• Menya boga, viazi, karoti, nyanya na kwaruza weka kwenya sufuria kubwa.
• Menya, osha na katakata vitunguu kisha ongeza kwenye mboga.
• Ongeza maji na chumvi chemshwa mpaka vilainike.
• Pekecha ikiwa jikoni na moto kidogo
• Ongeza blue band, maziwa royco na pilipili manga ukikoroga kwa dakika 5.
• Onja chumvi na pakua kama supu.
Uwezekano
Tumia siagi badala ya margarine.

Mapishi ya wali Wa Nazi Kwa Mchuzi Wa Nyama Ng’ombe Na Mchicha

Wali Wa Mpunga

Mchele wa mpunga – 4 Vikombe

Tui la nazi – 6 vikombe

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele kisha

Bandika tui jikoni likichemka tia mchele na chumvi.

Funika uchemke, tui likikauka wacha moto mdogomdogo hadi wali uive ukiwa tayari. Ikiwa unatumia mkaa unapalia juu yake.

Mchuzi wa nyama Ng’ombe

Nyama – 1 kilo

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi ilosagwa -2 viijiko vya supu

Viazi/mbatata – 2

Kitunguu maji kilokatwakawa (slice ndogo) – 2

Nyanya/tungule – 4

Nyanya kopo – 3 vijiko vya supu

Majani ya mchuzi/mvu – 3 msongo (bunches)

Bizari ya mchuzi (simba 2) – I kijiko cha chai

Ndimu – 1 kamua

Mafuta – ¼ kikombe

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka nyama katika sufuri, tia kijiko kimoja cha kitunguu thomu na tangawizi, chumvi, ndimu na chemsha nyama hadi iwive na ibakie supu yake kidogo.
Weka mafuta katika sufuri nyingine, kaanga kitunguu. Vinapogeuka rangi tia majani ya mchuzi endelea kukaanga hadi vigeuke rangi ya hudhurungi (golden brown)
Tia nyanya/tungule, viazi/mbatata, endelea kukaanga mpaka nyanya ziive.
Tia nyama na supu yake kisha tia nyanya ya kopo, kotmiri, bizari ya mchuzi, chumvi uache mchuzi kidogo katika moto hadi viazi viive vikiwa tayari.

Mboga Mchicha

Mchicha – 4 michano/vifungu

Kitunguu – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 3

Nyanya/tungule – 2

Tui la nazi zito – 1 kikombe cha chai

Chumvi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mboga iache ichuje maji.
Ikatekate kisha weka katika sufuria.
Katika kitunguu maji, kitunguu thomu kisage au kikatekate kidogodogo (chopped), nyanya.
Weka jikoni ipikike kwa maji yake na mvuke.
Tia tui endelea kuweka katika moto mdogomdogo hadi ikaribie kukauka ikiwa tayari.

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Chumvi

VIAMBAUPISHI

Unga – 3 Vikombe vya chai

Siagi – 250 gms

Baking powder – 3 Vijiko vya chai

Mayai – 2

Chumvi – 1 kijiko cha chai

Maziwa – 1/2 Kikombe

Pilipili manga ya unga 1 Kijiko cha chai

MAANDALIZI

Katika bakuli la kusagia (blender) au mashine ya keki, tia siagi, chumvi na mayai, piga mpaka iwe kama malai (cream).
Tia Unga, baking powder, pilipili manga.
Tia maziwa.
Kata usanifu (design) unayotaka na sokota au kunja kwa usanifu unaopenda.
Pika (bake) katika moto wa 350º C – usiviache vikawa rangu ya udongo (brown) sana.

Jinsi ya kupika mkate wa sembe

Mahitaji:

Unga sembe glass 1
Unga ngano glass 1
Sukari glass 1 (unaweza kupunguza kidogo)
Maziwa glass 1
Mafuta 1/2 glass
Mayai 4
Iliki iliosagwa 2tbs
Bp 2tbs

Jinsi ya kupika:

Saga sukari yako uweke kwenye bakuli safi pamoja na mayai. Tumia mashine ya cake kusagia hadi ifure/ivimbe.
Weka mafuta saga, weka maziwa saga, weka unga wa ngano na bp(bp imix kwenye unga kabla kumimina kwenye mchanganyiko) changanya vizuri halafu malizia kwa kuweka unga sembe na iliki usage vizuri.

Chukua trey au sufuria safi weka baking paper Mimina mchanganyiko wako na uoke.

Ukiwiva utoe na uwache upoe. Mkate wa sembe utakua tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya wali wa mboga

Mahitaji

Wali uliopikwa (cooked rice) kiasi
Hoho la kijani (green pepper) 1/2
Hoho jekundu (red pepper) 1/2
Carrot 1
Kitunguu kikubwa (onion) 1
Njegere (pears) 1/2 kikombe cha chai
Mayai (eggs) 2
Uyoga (mushroom) 2 vikombe vya chai
Soy source 2 vijiko vya chakula
Chumvi (salt) kiasi
Mafuta (veg oil) 3 vijiko vya chakula

Matayarisho

Katakata hoho, kitunguu,na uyoga vipande vikubwa kiasi(chunks) kisha katakata carrot zisiwe nene au nyembamba sana. Baada ya hapo weka mafuta katika katika frying pan yako isiyoshika chini acha yapate moto kisha tia uyoga na ukaange mpaka uive.Baada ya hapo tia vegetable zote na uzikaange pamoja na uyoga kwa muda wa dakika 2, kisha katika hiyohiyo frying pan zisogeze vegetable zako pembeni (ili kupata nafasi ya kukaangia mayai).Yakaange mayai katika hiyo sehemu yakiisha iva yavuruge na kisha yachanganye pamoja na vegetable na kisha tia chumvi kidogo sana. Baada ya hapo malizia kwa kutia wali na soy source kisha koroga vizuri mpaka mchanganyiko wako wote uchanganyike vizuri (hakikisha wali unapata moto na vegetable haziivi sana) . Na baada ya hapo chakula chako kitakuwa tayari.

Jinsi ya kupika pizza ya mboga mboga na cheese

MAHITAJI

1 kilo unga wa ngano
240 ml maji ya vugu vugu
2 olive oil kijiko kikubwa cha chakula
2 asali kijiko kidogo cha chai
1 chumvi kijiko kidogo cha chai
1 hamira ya chenga kijiko kidogo cha chai

JINSI YA KUPIKA

Chukua bakuli weka maji ya uvugu vugu, amira ya chenga, asali na chumvi kisha koroga ichanganyike vizuri acha itulie kwa dakika 10.
Kisha chukua olive oil na unga wa ngao mimina kidogo kidogo changanya mpaka ichanganyike safi kabisa kisha anza kukanda kama mchanganyiko wa chapati au maandazi.
Baada ya mchanganyiko wako kua mgumu safi kabisa funika bakuli lako na mfuko wa plastiki au cling film kwa muda wa saa 1 katika joto la chumba na mchanganyiko wako utaumuka baada ya muda huo. kisha ukandamize mchanganyiko huo wa unga na kua flati kama mwanzo.
Kata mafungu matano hadi saba ya ujazo sawa inategemea na ukubwa wa piza unaopenda we mlaji kisha sukuma umbo la duara.
Tengeneza mchuzi mzito wa nyanya kisha weka juu ya kitako cha piza na kuitandaza vizuri kwenye pizza yako kama unavyopaka siagi kwenye mkate. Usisahau kuweka chumvi na sukari kidogo katika mchuzi wa nyanya ili kukata uchachu.
Katakata nyanya, kitunguu, pili pili hoho, na bilinganya na kuziweka juu ya pizza yako kwa mpangilio ukitanguliza biringanya, ikifuatiwa na pili pili hoho, kitunguu maji na nyanya.
Kisha chukua mozarella cheese ikwaruze katika mkato mdogo rahisi kuyeyuka kwa kutumia kwaruzo la karoti linafaa.
kisha chukua mkwaruzo wa mozarella cheese na unyunyizie juu ya hizo mboga.
Weka pizza yako kwenye sahani ya bati au pizza pan ili isaidie kuiva upande wa chini.
Weka pizza yako kwenye oven ambayo imeshawashwa na ina joto 400 – 450 F. Choma kwa dakika 20 hadi 25 iwe kaukau na rangi ya kahawia pia cheese itakua imyeyuka na kusambaa vizuri juu ya pizaa.

NB: Unaweza weka mchanganyiko wa nyama yeyote ile kama salami, nyama ya ngombe, nyama ya kuku au samaki kwa kufata maelekezo sawa sawa na hii piza ya mboga, tofauti yake itakua huweki mboga unaweka nyama.

Mapishi ya Wali, samaki wa nazi na kisamvu

Mahitaji

Mchele
Kisamvu kilichotwangwa
Samaki
Mbaazi
Nyanya chungu
Vitunguu
Nyanya ya kopo
Tangawizi
Kitunguu swaum
Vegetable oil
Curry powder
Tui la nazi (kopo 2)
Chumvi
Pilipili
Limao

Matayarisho

Safisha samaki kisha wamarineti na kitunguu swaum, tangawizi, pilipili, chumvi na limao kwa muda wa masaa 3.Baada ya hapo wakaange na usiwakaushe sana na uwaweke pembeni kwa ajili ya kuungwa.Katakata vitunguu maji, saga tangawizi na kitunguu swaum. Baada ya hapo injika sufuria ya mchuzi jikoni na mafuta kiasi ya kupikia, mafuta yakisha pata moto, tia vitunguu maji na vikaange mpaka viwe vya rangi ya brown. kisha tia kitunguu swaum na tangawizi.kaanga kidogo kisha tia nyanya ya kopo moja na ufunike. acha mpaka nyanya ziive. Kisha tia chumvi na curry powder na uache ikaangike kwa muda wa dakika 2 kisha tia samaki na nyanya chungu nakisha kamulia nusu ya limao. Geuza mpaka mchanganyiko uchanganyike vizuri kisha tia tui la nazi kopo moja na uache ichemke mpaka mchuzi uive.

Baada ya hapo chemsha kisamvu pamoja na mbaazi Kikisha iva, kaanga kitu na nyanya pembeni mpaka ziive kisha tia kisamvu. geuza mchanganyiko mpaka uchanganyike vizuri kisha tia tui la nazi na chumvi na aacha ichemke mpaka tui liive kisha ipua.malizia kwa kupika wali ambapo utachemsha maji kisha tia mafuta,chumvi na mchele na uupike mpaka uive kisha sevu na mboga ulizopika na mlo wako utakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Wali Wa Karoti Na Kuku Wa Kukaanga

Vipimo Vya Wali

Mchele wa Basmati/Pishori – 1 kilo moja

Vitunguu maji – 3

Karoti – 2

Siagi – 3 vijiko vya supu

Kidonge cha supu (stock) – 1 kimoja

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Ósha mchele uroweke kama saa moja au mbili
Katakata vitunguu vipande vidogodogo (chopped) weka kando.
Kwaruza karoti (grate) weka kando.
Tia siagi katika sufuria ya kupikia wali, weka katika moto iyayuke
Kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi kiasi tu.
Tia maji kiasi ya kupikia wali, changanya na kidonge cha supu.
Yakichemka tia mchele, koroga, funika uweke moto mdogo mdogo.
Kabla ya maji kukauka tia karoti changanya wali kisha funika uive kama unavyopika pilau.

Vipimo Vya Kuku Wa Kukaanga

Kuku alokatwakatwa – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi ilosagwa – 2 vijiko vya supu

Bizari ya mchanganyiko/garam masala – kijiko cha supu

Mtindi/Yoghurt – 1 kijiko cha supu

Ndimu – 1

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kukaangia – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Ukishamuosha kuku, mchuje atoke maji yote.
Changanya viungo vyote katika kibakuli kidogo.
Changanya pamoja na kuku kisha acha akolee viungo (marinate) kwa muda wa masaa mawili takriban.
Weka mafuta katika karai na kaanga kuku, akiwiva yu tayari kuliwa na wali.

Mapishi mazuri ya Chapati za maji

Mahitaji

Unga wa ngano (plain flour) ( 1/4 kilo)
Yai (egg 1)
Sukari (sugar 1/4 kikombe cha chai)
Chumvi (salt 1/4 kijiko cha chai)
Hiliki (ground cardamon 1/4 kijiko cha chai)
Maji kiasi
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Tia unga kwenye bakuli, kisha weka sukari, chumvi, hiliki na maji kiasi. Kisha koroga mpaka mchanganyiko wako uwe mzito. Baada ya hapo tia yai na ukoroge tena. hakikisha mchanganyiko hauwi mzito sana au mwepesi sana.Baada ya hapo onja kama kila kitu kimekolea. Injika chuma cha kupikia chapati (fry-pan) jikoni katika moto wa wastani. Baada ya hapo tia nusu kijiko cha chakula cha mafuta katika fry-pan na kisha yatandaze. Hakikisha chuma kinapata moto na weka upawa mmoja wa unga wa chapati na uutandaze mpaka uwe flat. Baada ya hapo subiri mpaka chapati ikauke juu na kisha igeuze upande wa pili tia mafuta kijiko 1 kikubwa cha chakula kwa upande wa chini na wa juu kisha uanze kuikandamiza kwa juu na kijiko ili iweze kuiva vizuri kwa chini. Ikisha kuwa ya rangi ya brown igeuze na upike upande wa pili kiasi kisha iipue na uiweke kwenye sahani yenye kitchen towel ili kukausha mafuta. Rudia hii process kwa unga wote uliobakia. Na chapati zitakuwa tayari

Jinsi ya kuandaa Biriani Na Sosi Ya Nyama Ya Mbuzi

Mahitaji

Nyama Ya Mbuzi – 1 Kilo

Mchele – 4 Magi

Vitunguu – 3

Nyanya – 2

Nyanya kopo – 3 vijiko vya chai

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 2 vijiko vya supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Garam Masala (mchanganyiko wa bizari) – 2 vijiko vya supu

Hiliki – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Mafuta – ½ kikombe

Zaafarani au rangi za biriani za kijani na manjano/orenji

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Sosi Ya Nyama

Changanya nyama na thomu, pilipili, chumvi na nusu ya garam masala. Tia katika treya ya oveni uipike nyama (Bake) hadi iwive. Au iwivishe kwa kuichemsha.
Katika kisufuria kingine, tia mafuta (bakisha kidogo ya wali) kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi, kisha tia nyanya, nyanya kopo, bizari zote nyingine zilizobakia.

Namna Ya Kupika Wali

Mchele – 4 magi

Mdalasini – 1 kijiti

Hiliki – 3 chembe

Kidonge cha supu – 1

Chumvi

Osha na roweka mchele wa basmati.
Tia maji katika sufuria uweke jikoni. Tia kidonge cha supu, mdalasini, hiliki na chumvi .
Yakichemka maji tia mchele, funika upike hadi nusu kiini kisha uchuje kwa kumwaga maji.
Tia mafuta kidogo katika mchele na zaafarani iliyorowekwa au rangi za biriani kisha rudisha mchele katika sufuria ufunike na upike hadi uwive.
Pakua wali katika sahani kisha mwagia sosi ya nyama juu yake, pambia kwa kukatika nyanya, pilipili mboga na figili mwitu (Celery) au mboga yoyote upendayo.

Mapishi ya Wali Wa Tambi Na Kuku Wa Sosi Ya Mtindi

Vipimo Vya Wali

Mchele – 3 vikombe

Tambi – 2 vikombe

Mafuta – ¼ kikombe

Chumvi

Vipimo Vya Kuku

Kuku kidari (boneless) aliyekatwa katwa vipande – 1 Kilo

Kitunguu maji kilichokatwa katwa – 2

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Paprika – 1 kijiko cha supu

Masala ya kuku (tanduri au yoyote) – 1 kijiko cha supu

Ndimu – 2 vijiko vya supu

Mtindi (yoghurt) au malai (cream) – 1 kikombe

Mafuta – ¼ kikombe

Majani ya kotmiri (coriander) – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Wali:

Osha Mchele, uroweke.
Tia mafuta katika sufuria, kaanga tambi zilizokatwakatwa hadi zigeuke rangi kuwa nyekundu.
Tia mchele endelea kukaanga kidogo.
Tia maji kiasi cha wali kupikika kama unavyopika pilau. Kiasi cha maji kinategemea aina ya mchele
Funika katika moto mdogo mdogo hadi uive ukiwa tayari.

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Kuku

Katika bakuli, changanya vitu vyote isipokuwa mtindi na kitunguu.
Tia mafuta katika karai, kisha tia kitunguu ukaange muda mdogo tu, usikiache kugeuka rangi.
Tia kuku na masala yake, endelea kukaanga, kisha tia mtindi au malai ufunike apikike na kuiva vizuri.
Nyunyuzia kotmiri iliyokatwakatwa ikiwa tayari kuliwa na wali wa tambi.

Jinsi ya kupika Pilau ya Mpunga Na Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Mpunga – 4 vikombe

Nyama – 1 kilo moja

Kitunguu maji – 3

Mbatata/viazi – 7 vidogodogo

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi ilosagwa 3 vijiko cha supu

Bizari nzima/ya pilau/uzile/cumin – 3 vijiko vya supu

Mdalasini – 3 vipande

Hiliki – 7 punje

Pilipili manga nzima – 1 kijiko cha supu

Chumvi kiasi

Mafuta – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele weka kando
Katakataka vitunguu slice ndogo ndogo.
Weka mafuta katika sufuria kisha ukaange vitunguu pamoja na mdalasini, hiliki pilipilimanga.
Vitunguu vikigeuka rangi unatia kitunguu thomu na tangawizi.
Tia supu kidogo na nyama, kisha tia bizari ya pilau/uzile, na viazi/mbatata.
Maliza kutia supu yote, na ikiwa ni kidogo ongeze maji kiasi cha kuivisha mchele. kisha tia mchele ufunike hadi wali uwe tayari.
Ikiwa unatumia mkaa palia juu yake, ikiwa hutumii uache uive kwa moto mdogo mdogo.

Jinsi ya kupika Visheti

Viamba upishi

Unga 2 Vikombe

Samli au shortening ya mboga 2 Vijiko vya supu

Maziwa ¾ Kikombe

Iliki Kiasi

Mafuta ya kukarangia Kiasi

Shira

Sukari 1 Kikombe

Maji ¾ Kikombe

Vanila ½ Kijiko cha chai

Zafarani (ukipenda) Kiasi

Jinsi ya kupika na kuandaa

Katika kisufuria pasha moto maziwa na wakati huo huo chemsha Samli katika kisufuria kengine.
Tia unga katika bakuli na iliki, kisha mimina samli iliyochemka na huku unachanganya, kisha tia maziwa na uwendele kuchanganya vizuri isiwe na madonge, ikiwa maziwa haitoshi ongeza maji kidogo.
Kisha uwache unga ukae mahali pa joto kwa muda wa dakika 10 hivi.
Halafu fanya viduara vidogo vidogo, kisha finyiza kwenye greta yenye vishimo vidogo ili upate umbo kama kwenye picha.
Kisha karanga kwenye mafuta yaliyopata moto hadi vibadilike rangi ya dhahabu, kisha viepue vichuje mafuta.
Chemsha shira, ikiwa tayari mimina visheti na upepete na kuzichanganya zipate shira kote.
Weka kwenye sahani na zitakuwa tayari kwa kuliwa na kahawa.

Mapishi ya Wali Wa Kukaanga Kwa Kidari Cha Kuku (Chicken Breast) Wa Kukausha

Viambaupishi

Vipimo vya Wali:

Mchele 3 vikombe

*Maji ya kupikia 5 vikombe

*Kidonge cha supu 1

Samli 2 vijiko vya supu

Chumvi kiasi

Hiliki 3 chembe

Bay leaf 1

Viambaupishi: Kuku

Kidari (chicken breast) 1Kilo

Kitunguu 1

Tangawizi mbichi ½ kipande

Kitunguu saumu(thomu/galic) 7 chembe

Pilipili mbichi 3

Ndimu 2

Pilipilimanga 1 kijiko cha chai

Mdalasini ½ kijiko cha chai

Jira/Cummin ya unga 1 kijiko cha chai

Maji ¼ kikombe

Jinsi ya kuandaa na kupika

Wali:

Osha na roweka mchele kisha weka sufuria katika moto tia samli ipashe moto.

Tia hiliki, bay leaf, kaanga, kisha tia mchele ukaange kidogo.

Tia maji, chumvi na kidonge cha supu, upike wali kama unavyopika pilau.

*Maji kisia kwa kutegemea mchele ulivyo.

  • Unaweza kutumia supu yoyote badala ya kidonge.

Kuku:

Katakata kidari cha kuku vipande vya kiasi, weka katika sufuria, tia ndimu, bizari zote, chumvi.

Katakata kitunguu vipande vidogodogo, pilipili, na kitunguu thomu (chopped), tia katika kuku.

Chuna tangawizi mbichi tia katika kuku. Changanya vitu vyote vizuri.

Tia maji kiasi ¼ kikombe tu kiasi cha kumkaushia kuku. Weka katika moto mpike huku unageuzageuza. Anapokaribia kukauka epua akiwa tayari kuliwa na wali (na saladi upendayo)

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About