Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya chipsi na samaki wa kuchoma

Mahitaji

Viazi ulaya (baking potato 5 vya wastani)
Parprika 1 kijiko cha chai
Pilipili mtama ilyosagwa (ground black pepper 1 kijiko cha chai
Kitunguu swaum cha unga (garlic powder 1 kijiko cha chai)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)
Marination za samaki (angalia kwenye recipe ya samaki ya nyuma)

Matayarisho

Osha viazi na maganda yake kisha vikaushe na uvikate vipande vya wastani. Kwa kila kiazi toa vipande 6. Kisha vitie kwenye bakuli na utie parpika, pilipili mtama ya unga, kitunguu swaum cha unga, chumvi na mafuta kama vijiko 2 vya chakula. Changanya pamoja na kisha uvibake katika oven kwa muda wa dakika 25. Hakikisha vinakuwa rangi ya brown. Vikisha iva vitoe.
Wamarinate samaki, na uwaoke kisha wasevu na potato wedges tayari kwa kuliwa
(Jinsi ya kupika samaki, angalia katika recipe za nyuma)

Mapishi ya Mchuzi wa kambale

Mahitaji

Kambale 2
Nazi kopo 1
Nyanya kopo 1
Vitunguu 2
Curry powder 1 kijiko cha chai
Turmaric 1/2 kijiko cha chai
Binzari nyembamba ya unga 1/2 kijiko cha chai
Swaum/ tangawizi 1 kijiko cha chakula
Giligilani kiasi
Limao 1/2
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Loweka samaki katika maji ya moto kwa muda wa muda wa nusu saa.Baada ya hapo Saga pamoja nyanya, vitunguu, swaum na tangawizi kisha vibandike jikoni na uvipike mpaka maji yote yakauke kisha tia mafuta. Pika mpaka nyanya zitengane na mafuta kisha tia spice zote.Zipike kwa muda mdogo kisha tia tui la nazi, maji kiasi, samaki, pilipili nzima, chumvi na kamulia limao. Pika mpaka tui la nazi litakapoiva na samaki pia wawe wameiva na mchuzi ubakie kiasi. Baada ya hapo ipua kisha tia giligilani iliyokatwa na mchuzi utakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuulia kwa chochote kile upendacho. Mi hupendaga kuulia na ugali mlaiiini au na wali pia.

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Ya Keki Kavu (Shortcake)

VIAMBAUPISHI

Unga – 2 Magi (vikombe vya chai)

Sukari iliyosagwa – 2/3 Magi (kikombe cha chai)

Siagi – 220 g

Unga wa mchele – ½ Magi

Yai -1

Vanilla – 1 kijiko cha chai

MAANDALIZI

Changanya vitu vyote hivyo kwenye bakuli mpaka unga ushikamane.
Paka mafuta treya ya kuchomea kisha utandaze kwenye treya ya 20cm kwa 30 cm au (8 in kwa 12 in)
Choma kwenye moto 325˚C kwa muda wa saa nzima au mpaka ibadilike kuwa rangi ya dhahabu.
Epua acha ipoe kisha kata vipande kama mstatili, weak kwenye sahani tayari kunywewa na chai.

NYONGEZA

Kwa unga huo huo unaweza kutengeneza vibiskuti vya duara duara.

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Cornflakes

MAHITAJI

Unga – 1 Kikombe

Sukari ya kusaga – 3/4 Kikombe

Siagi – 125 gms

Yai – 1

Baking powder – 1/2 kijiko cha chai

Zabibu kavu – 1/2 kikombe

Cornflakes iliyovunjwa (crushed) – 2 Vikombe

Vanilla – 1 kijiko cha chai

MAANDALIZI

Tia kwenye mashine ya kusaga (blender) au mashine ya keki, siagi, yai na vanilla uchanganye hadi ichanganyike vizuri.
Tia baking powder, zabibu na unga na changanya vizuri.
Paka siagi sinia ya kupikia ya oveni.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Weka cornflakes katika sahani ya chali (flat) na zungusha viduara humo kisha upange katika sinia ya oveni.
Pika katika moto wa 350ºF kwa muda wa dakika 20-25 hadi vigeuke rangi na viwive.

Mapishi ya Biskuti Za Jam

VIAMBAUPISHI

Unga 2 ½ gilasi

Sukari ¾ gilasi

Samli 1 gilasi

Mayai 2

Baking powder 2 kijiko vya chai

Vanilla 1 ½ kijiko cha chai

Maganda ya chungwa 1

MAPISHI

Tia kwenye machine ya kusagia (blender) mayai, sukari, vanilla, samli na maganda ya chungwa, saga vizuri.
Tia unga kwenye bakuli pamoja na baking powder, mimina vitu ulivyosaga kwenye bakuli, changanya.
Punguza unga uliochanganya kidogo weka pembeni.
Unga uliobakia tia kwenya tray ya kuchomeya, utandaze vizuri, tia jam juu yake.
Chukua la kukwaruzia carrot (grater) ukwaruze unga uliuopunguza juu ya jam.
Choma kwa muda dakika 20 moto wa 180 C.

Acha ipowe kidogo, zikate vipande vya mraba (square) Tayari kwa kula.

Mapishi ya Biriani Nyepesi Kupika Ya Samaki

Vipimo

Mchele wa pishori (basmati) – 4

Vitunguu katakata – 3

Nyanya (tungule) katakata vipande vikubwa – 3 -5

Pilipili boga la kijani (capsicum) katakata

Supu ya kitoweo au vidonge vya supu – 1

Bizari mchanganyiko Garama masala – 5-7

Pilipili mbichi ya kusaga – Kiasi

Zaafarani ya maji (flavor) – 1 kijiko cha chakula

Mafuta ya kupikia – ¼ kikombe

Samaki wa kukaanga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Roweka mchele kiasi nusu saa kisha chemsha mchele kwa supu uive nusu kiini. Mwaga maji chuja.
Wakati mchele unapikika, weka mafuta katika sufuria kubwa ya kupikia wali, kaanga vitunguu mpaka vigeuke rangi ya hudhurungi.
Tia nyanya na vitu vinginevyo vyote kaanga kidogo tu.
Mwaga wali katika sufuria na nyunyizia zaafarani kisha changanya na masala vizuri.
Funika upike katika oven (bake) au juu ya stovu moto mdogo mdogo kiasi dakika 15- 20.
Epua ikiwa tayari, pakua kwenye sahani kisha tolea kwa samaki wa kukaanga.

Mapishi ya wali mtamu Wa Nazi Kwa Maharage Na Samaki Nguru Wa Kukaanga

Vipimo

Wali:

Mchele mpunga – 4 Vikombe

Tui la nazi – 6 vikombe

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele weka kando.
Bandika tui jikoni likichemka tia mchele na chumvi.
Funika uchemke, tui likikauka wacha moto mdogomdogo hadi wali uive ukiwa tayari. Ikiwa unatumia mkaa unapalia juu yake.

Maharage Ya Nazi

Maharage – 3 vikombe

Tui la nazi zito – 1 kikombe

Tui la nazi jepesi – 1 kikombe

Kitunguu maji – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) kilosagwa -1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chemsha maharage mpaka yaive.
Katiakatia kitunguu maji na tia thomu, tia na tui jepesi kikombe kimoja.
Tia tui zito endelea kuweka katika moto mdogomdogo hadi yakaribie kukauka yakiwa tayari.

Samaki Nguru Wa Kukaanga

Samaki Wa Nguru – 4 vipande

Kitunguu saumu(thomu/galic) & tangawizi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi – 4

Ndimu – 2 kamua

Bizari ya samaki -1 kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Mwoshe samaki kisha mtie kitunguu thomu, tangawizi ilosagwa, chumvi, pilipilimbichi ilosagwa, ndimu na bizari ya samaki.
Mwache akolee viungo kwa muda kidogo.
Makaange katika mafuta hadi aive akiwa tayari.

Jinsi ya kupika Wali wa hoho

Wali wa hoho ni chakula maalum kinachotumika katika hafla au sherehe. Ni chakula chenye ladha nzuri na kina muonekano wa kuvutia kinapokuwa mezani tayari kwa kuliwa.

Mara nyingi huandaliwa kama zawadi katika harusi hususan kwa watu wa pwani. Kwa kuwa zawadi hiyo au maarufu kama kombe huwa kuna vyakula vingi, ikiwamo chakula hiki ambacho hufanya kombe kuwa na muonekano wa kupendeza.

Mbali na kuliwa kama kombe chakula hiki kinaweza kuandaliwa kama mlo wa usiku.

Mahitaji:

• Mchele ½ kg
• Nyanya 3
• Mafuta ya kupika ¼ kikombe cha chai
• Chumvi kiasi
• Kitunguu swaumu kilichosagwa kijiko 1 cha mezani
• Kitunguu maji kilichosagwa kijiko 1 cha mezani
• Hoho 4
• Nyama ya kusaga ¼
• Tangawizi kijiko 1 cha chakula
• Limao au ndimu kipande

Maadalizi:

• Chukua mchele uoshe vizuri kasha chuja maji
• Chukua nyama ya kusaga na kamulia ndimu, weka chumvi na tangawizi, changanya vizuri na weka jikoni.iache ichemke hadi ikauke maji yote.
• Chukua maji na kiasi cha robo tatu lita chemsha na weka pembeni
• Chukua sufuria kavu yenye uwezo wa kupika kiasi cha kilo moja
• Weka mafuta ya kupika kiasi cha vijiko vitatu na acha yapate moto
• Weka vitunguu maji, menya nyanya na katakata halafu weeka katika sufuria hiyo.
• Weka chumvi na kanga hadi vilainike kabisa
• Baada ya kuiva weka vitunguu swaumu na baadaye mchele
• Koroga hadi uchanganyike na weka nyama. Endelea kukoroga, baada ya hapo weka maji kiasi cha kuivisha mchele huo. Acha vichemke hadi vikaukie.
• Palia mkaa juu yake au kama unatumia jiko la gesi au umeme weka kwenye oven hadi maji yakauke kabisa.
• Baada ya hapo chukua hoho na kasha kata upande wa juu kama vifuniko. Kasha ondoa matunda ya ndani yake. Funika na kasha zipange kwenye sufuria yenye maji na chumvi na mafuta kidogo kiasi cha kijiko kimoja. Chemsha jikoni hadi ziive.
• Baada ya kuiva, chukua hoho zako na kasha chota wali kw akutumia kijiko kasha jaza katika kila hoho na weka kwenye sahani tayari kwa kuliwa.
• Unaweza kupamba na salad ukipenda.

Mapishi ya Mlenda wa bamia na nyanya chungu

Mahitaji

Bamia (okra) 20
Nyanya chungu (garden eggs) 5
Magadi soda (Bicabonate soda) 1/4 ya kijiko cha chai
Nyanya (fresh tomato) 1
Chumvi (salt) kidogo
Pilipili 1/4

Matayarisho

Osha bamia, nyanya chungu na nyanya kisha vikatekate katika vipande vidogovidogo. Baada ya hapo vitie kwenye sufuria na vitu vyote vilivyobakia na kisha tia maji kidogo.Chemsha mpaka bamia na nyanya chungu ziive na vimaji vibakie kidogo sana. Baada ya hapo ziponde na mwiko kidogo kisha zikoroge na uipue na mlenda utakuwa tayari kwa kuliwa na ugali.

Mapishi ya Mchemsho wa ndizi na nyama

Mahitaji

Ndizi mbichi 6
Nyama ya ng’ombe (nusu kilo)
Viazi mviringo 2
Kitunguu swaum
Tangawizi
Kitunguu maji
Nyanya 1 kubwa
Mafuta (vegetable oil)
Chumvi
Limao
Pilipili

Matayarisho

Chemsha nyama na limao, kitunguu swaum, tangawizi chumvi na maji kiasi mpaka nyama iive, Hakikisha unaiacha na supu kiasi kwa ajili ya kuwekea kwenye ndizi.Kisha katakata nyanya na vitunguu na uweke pembeni .Menya ndizi na viazi kisha zichemshe pamoja na vitunguu, nyanya, maji kidogo, mafuta na uhakikishe haziivi kabisa. Baada ya hapo tia nyama na supu yake, pilipili mzima na chumvi na uache uchemke mpaka ndizi na viazi viive.Na baada ya hapo mchemsho wako utakuwa tayari kwa kuliwa

Jinsi ya kutengeneza saladi

Mahitaji

Tango 1/2
Kitunguu 1/2
Cherry tomato 8
Lettice kiasi
Green olives kidogo
Black olives kidogo
Hoho jekundu 1
Carrot
Giligilani kidogo

Salad dressing
Yogurt 1/2 kikombe
Swaum 1/2 kijiko cha chai
Limao 1/2
Pilipili ya unga 1/4 kijiko cha chai
Chumvi kidogo
Olive oil kiasi

Matayarisho

Osha vitu vyote kisha vikaushe maji. Baada ya hapo ktk bakuli kubwa katakata, lettice, tango,hoho, kitunguu,giligilani na kisha ikwangue carrot na utie bila kusahau nyanya zote pamoja na olives.Baada ya hapo ichanganye vizuri, kisha tengeneza salad dressing kwa kuchanganya vitu vyote vilivyo (kwenye list ya salad dressing) kisha koroga vizuri.Baada ya hapo ichanganye na salad.Na hapo salad yako itakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuila na chochote upendacho kama vile chips, nyama choma au au chakula kikuu.

Namna ya kupika Vitumbua

Vitumbua ni aina ya vitafunwa vya chai ambavyo hutengenezwa kwa kutumia unga wa mchele. Kiasili vitumbua ni chakula ambacho hupendelewa sana na watu wa pwani. Na mara nyingi wamekuwa wakipika kwa kuchanganya na nazi ili kuvifanya view na ladha nzuri zaidi

Mahitaji:

Unga wa mchele ½ kg
Sukari vijiko 4 vya mezani
Tui bubu la nazi
Mafuta ya kupikia
Unga wa hiliki ½ kijiko cha chai
Hamira kijiko 1 cha chai
Chuma cha vitumbua

Maandalizi:

Chukua unga wa mchele na weka kwenye bakuli au sufuria ya kilo moja
Weka hamira kisha weka sukari kisha miminia tui katika mchanganyiko wako
Weka hiliki koroga hadi view uji mzito
Acha uji huo kwa muda wa saa moja hadi uumuke, mara nyingi kuumuka kunategemea na hali ya hewa,
Baada ya hapo weka mafuta kijiko kimoja cha chakula kila kishimo acha yapate moto Kisha kaanga virumbua vyako

Mapishi ya Wali Wa Kukaanga Kwa Nyama Mbuzi Ilichomwa Ya Sosi Ya Ukwaju

Vipimo Vya Wali

Mchele Basmati – 4 vikombe

Vitunguu vya majani (Spring onions) – 5 miche

Pilipili mboga nyekundu (capsicum) – 1

Pilipili mboga manjano (capscimu) – 1

Nyanya kubwa – 1

Supu ya kidonge – 2

Siagi – 2 vijiko vya supu

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele kisha roweka kiasi masaa matatu takriban.
Katakata vitunguu majani, mapilipili boga, nyanya vipande kiasi.
Weka siagi katika sufuria ya kupikia, weka katika moto iyayuke.
Tia vitunguu majani, mapilipili boga, nyanya, kaanga kidogo tu.
Tia mchele kaanga kidogo, kisha tia maji kiasi ya kuivisha mchele.
Tia supu ya kidogo au supu yoyote, funika wali upikike moto. mdogodogo.

Vipimo Vya Nyama Mbuzi Na Sosi Ya Ukwaju

Nyama mbuzi mapande makubwa kiasi – 7/8 vipande

Kitunguu saumu(thomu/galic) kilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Ukwaju mzito ulokamuliwa – 1 kikombe cha chai

Jiyra/cummin/bizari pilau – 1 kijiko cha chai

Nyanya kopo – 2 vijiko vya supu

Siki – 2 vijiko vya supu

Mafuta – ½ kikombe cha chai

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Changanya vitu vyote pamoja katika kibakuli kidogo.
Weka nyama katika bakuli kubwa kisha tia mchanganyiko wa sosi, ubakishe sosi kiasi pembeni.
Roweka kwa muda wa masaa 3 – 5
Panga nyama katika bakuli au treya ya kuchomea katika oven.
Pika (bake) kwa moto wa kiasi kwa muda wa saa takriban.
Karibu na kuiva, epua, zidisha kuichangaya na sosi ilobaki.
Rudisha katika jiko uendelee kuipika muda kidogo tu.
Epua ikiwa tayari, weka juu ya wali uliopakuwa kisha mwagia sosi ya nyanya pilipili (chilii tomato sauce) ukipenda.

Mchemsho wa samaki na viazi

Mahitaji

Samaki mbichi (1)
Viazi mbatata (3)
Nyanya (1)
Kitunguu maji
Limao
Kitunguu saumu
Tangawizi
Chumvi
Pilipili
Vegetable oil

Matayarisho

Safisha samaki kisha mmarinate na tangawizi, kitunguu swaum, chumvi na limao kwa muda wa masaa mawili. Baada ya hapo menya viazi na uvikate vipande vidogo kisha vioshe na viweke kwenye sufuria yenye maji kiasi kwa ajili ya kuvichemsha. Viinjike jikoni na uviache vichemke kwa dakika 7. Vikisha chemka tia samaki, katia kitunguu,pilipili, chumvi, limao, vegetable oil na nyanya na uache supu ichemke mpaka samaki na viazi vitakapoiva. baada ya hapo supu itakuwa tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About