Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Biskuti Za Mtindi/Yoghurt

MAHITAJI

Chenga za biskuti – 3 gilasi

Mtindi (yogurt) – 1 Kopo (750g)

Maziwa ya unga – 1 gilasi

Siagi – 10 Vijiko vya supu

Sukari – ½ gilasi

Lozi zilizomenywa vipande vipande – ½ gilasi

Nazi iliyokunwa – ½ gilasi

Vanilla – 1 Kijiko cha supu

MAPISHI

Katika mashine ya kusagia (blender), tia mtindi, sukari, siagi na vanilla na usage pamoja hadi ichanganyike.
Mimina katika bakuli la kiasi.
Tia vitu vilivyobakia na uchanganye vizuri.
Mimina kwenye treya ya kuchomea na uvumbike katika oveni moto wa 350° hadi ishikamane na kuwa tayari.
Iaache ipoe kisha katakata vipande na tayari kwa kuliwa.

Baada yakuwa imeshaiva, ukipenda unaweza kupakiza jamu au karameli ya tayari kwa juu, kisha ukarudisha kwenye oveni moto wa juu kidogo kwa ladha nzuri zaidi

Jinsi ya kupika Magimbi Kwa Nyama Ya Ng’ombe

Vipimo

Majimbi (Eddoes) kiasi 6 au 7

Nyama ng’ombe ½ kilos

Tangawizi ilosagwa 1 kijiko cha kulia

Haldi (bizari manjano/turmeric) ½ kijiko cha chai

Tui zito la nazi vikombe 2

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha nyama kisha weka chumvi, bizari ya manjano, tangawizi mbichi, ukaushe kwanza katika sufuria kwa kukaanga kaanga.
Ikianza kukauka, weka maji funika uchemshe iwive.
Menya majimbi ukate kate na uweke katika sufuria nyengine.
Mimina supu na nyama katika majimbi uchemshe yawive majimbi.
Mwisho weka tui zito la nazi uchanganye vizuri kisha weka katika moto kidogo tu bila kufunika yakiwa tayari.

Jinsi ya kupika Roast ya biringanya na mayai

Mara nyingi biringanya hutumika kama kiungo cha nyongeza katika mchuzi. Hata hivyo, kiungo hiki kinaweza kupikwa chenyewe na kutoa mchuzi wenye ladha ya kipekee.

Baadhi ya wapishi wameweza kubuni aina hii ya upishi ambayo huweza kupikwa kwa dakika tano tu na kukupa chakula kitamu chenye ladha ya kuvutia.

Uzuri wa chakula hi ni kwamba kinaweza kuliwa wakati wowote na kwa chakula chochote kulingana na matakwa ya mlaji.

Kwa mujibu wa wataalamu wa maswala ya mapishi, biringanya ni miongoni mwa vyakula vyenye mapishi mengi kama ilivyo kwa mchele.
Hapa tutaenda kuona jinsi ya kupika roast ya biringanya na mayai.

Mahitaji:

Biringanya 2 kubwa
Nyanya 4 kubwa
Kitunguu maji kilichosagwa kijiko 1 cha mezani
Mayai 2
Mafuta ya mzeituni vijiko vitatu vya mezani
Chumvi kiasi
Pilipili 1 (kama unatumia)
Hoho 1
Karoti 1
Kitunguu swaumu kilichosagwa 1
Kotimili fungu 1

Maadalizi:

Chukua biringanya ioshe vizuri na kasha katakata vipande vidogo vidogo.
Osha na menya nyanya hapafu katakata. Fanya hivyo kw akaroti na hoho pia.
Weka mafuta kwenye sufuria na weka jikoni kwenye moto kiasi
Yakishachemka maji na kasha weka kitunguu maji na kasha swaumu huku ukikaanga taratibu.
Weka hoho na karoti huku ukiendelea kukaanga. Baada ya hapo weka nyanya na baadae chumvi. Funika hadi ziive kabisa na kasha weka majani ya kotimili.
Weka biringanya. Acha vichemke hadi viive. Koroga ili kuruhusu mchanganyiko wako uchanganyike vizuri.
Kwa kuwa biringanya ina majimaji huhitaji kuweka maji ya ziada, weka pilipili.
Acha kwa muda wa dakika tatu hadi dakika tano. Pasua mayai na kisha miminia huku ukikoroga taratibu. Fanya hivyo hadi yaive kabisa na kuwa mchuzi mzito. Roast yako ya biringanya iko tayari kwa kuliwa
Unaweza kula aina hii ya mboga na mikate, maandazi na hata ugali

Mapishi – Kisamvu cha Karanga

Mapishi yetu leo ni kisamvu cha kuchanganya na karanga. Karibu.

Mahitaji

Majani ya kisamvu
Karanga nusu kikombe
kitunguu kimoja
nyanya mbili
karoti moja
mafuta na chumvi kiasi

Matayarisho

1. Osha kisamvu chako vizuri kisha katakata vipande vidogo vidogo

2. Unaweza kutwanga kwa kutumia kinu au kuchemsha kidogo na kisha kusaga kwa kutumia mashine. Ukitumia mashine uwe makini usije ukasaga sana ukaharibu.

3. Kaanga karanga kidogo na kisha zisage ziwe unga unga.

4. Chemsha kisamvu chako hadi kiive.

5. Katakata kitunguu, karoti na na nyanya

6. Anza kuunga kisamvu kwa kukaanga vitunguu, weka karoti na kisha nyanya na vikishaiva weka kisamvu na koroga pamoja kisha weka karanga. Acha vichemke kwa muda na unaweza pia weka na nazi tui la kwanza.

7. Baada ya muda mfupi epua na kitakiwa tayari. Waweza kula kwa ugali, wali, chapati, makande n.k

Jinsi ya kupika Vileja Vya Tambi

Viambaupishi

Tambi (vermiceli Roasted) Mifuko 2

Siagi 4 Vijiko vya supu

Maziwa (condensed) 300Ml

Lozi zilizokatwakatwa 1 kikombe

Zabibu kavu 1 Kikombe

Arki (essence) 1 Kijiko cha supu

Jinsi ya kuandaa na kupika

1) Weka karai kwenye moto kiasi

2) Tia siagi

3) Tia tambi uzikaange usiachie mkoni mpaka ziwe rangu ya dhahabu.

4) Weka lozi na zabibu huku unakoroga

5) Tia maziwa na huku unakoroga usiachie mkono.

6) Tia arki

7) Epua karai, tumia kijiko cha chai kwa kuchotea na utie kwenye kikombe cha kahawa nusu usikijaze.

8) Kipindue kwenye sahani utoe kileja.

9) Fanya hivyo mpaka umalize vyote.

Jinsi ya kutengeneza Muhogo Wa Nazi Na Samaki Wa Kukaanga

Mahitaji

Muhogo – 3

Tui La Nazi – 2 vikombe

Chumvi – kiasi

Pilipili mbichi – 2

Mafuta – 1 kijiko moja

Kitunguu maji – 1 kidogo

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chambua muhogo ukatekate au tumia iliyo tayari.
Chemsha muhogo katika sufuria kwa maji kidogo na chumvi, funika uive muhogo.
Karibu na kukauka maji tia tui, kitunguu maji ulichokatakata na pilipili mbichi.
Unaupika moto mdogo mdogo hadi ukauke tayari kuliwa na samaki au kitoweo chochote kingine

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Tende

MAHITAJI

Unga – 4 Vikombe vya chai
Sukari ya laini (icing sugar) – 1 Kikombe cha chai
Baking powder – 2 Vijiko vya chai
Mayai – 2
Siagi au margarine – 1 Kikombe cha chai
Vanilla -1 Kijiko cha chai
Maziwa ya kuchanganyia – kiasi
Tende iliyotolewa koko – 1 Kikombe
ufuta (sasame) kiasi 1/4 kikombe

MAANDALIZI

Changanya unga, siagi, baking powder, na sukari katika mashine.
Kisha tia mayai, vanilla na halafu maziwa kidogo kidogo hadi mchanganyiko ushikamane.
Gawanya madonge mawili na usukume kama chapati, lakini sio nyembamba sana.
Tandaza tende robo ya duara na unyunyize ufuta duara zima: kisha kunja hadi mwisho na ukate kate, kisha upange katika trei ya kuvumbika.
Vumbika (bake) moto wa 350°F kwa muda wa dakika 20 au hadi vigeuke rangi na viwive.
Zikisha iiva ziache zipowe na zitakuwa tayari kuliwa.

Jinsi ya kupika Mishkaki ya kuku

Kidali cha kuku 1 kikubwa
Swaum,tangawizi 1 kijiko cha chai
Limao 1/2
Pilipili ya unga 1/2 kijiko cha chai
Curry powder 1/2 kijiko
Paprika 1/2 kijiko cha chai
Hoho jekundu 1/2
Hoho la njano 1/2
Kitunguu 1/2
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Katakata kuku ktk vipande vya mishkaki ya kawaida kisha vimarinate na vitu vyote, kasoro hoho na kitunguu.Ni vizuri kuziacha either usiku mzima au kwa masaa machache ili spice ziingie vizuri. Baada ya hapo katakata hoho na vitunguu vipande vya wastani kiasi. Baada ya hapo Taarisha vijiti vya mishkaki kisha tunga nyama pamoja na hoho na vitunguu kisha nyunyuzia mafuta na kisha uzichome kama mishkaki ya kawaida. Itakapoiva itakuwa tayari kwa kuliwa na chochote upendacho kama ndizi za kuchoma, viazi na n.k.

Jinsi ya kupika Baklawa Za Pistachio Na Lozi

VIAMBAUPISHI

Philo (thin pastry) manda nyembamba – 1 paketi

Siagi – ¼ Kikombe cha chai

Baking powder – 2 Vijiko vya chai

Pistachio/ lozi – 2 vikombe vya chai

Mafuta – ½ Kikombe

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 2 Vikombe vya chai

Maji – 2 ½ Vikombe vya chai

ndimu – ½ kijiko cha chai

JINSI YA KUANDAA

Tafuta treya iliyokuwa sawa na ukubwa wa hizo manda nyembamba (philo) au zikate hizo manda kwa ukubwa wa treya (mraba au mstatili)
Kisha yeyusha siagi changanya na mafuta.
Kisha panga manda moja pakaza mafuta juu yake kisha weka manda nyingine juu yake kisha pakaza mafuta tena weka manda nyingine juu yake, endelea kufanya hivyo mpaka ziwe kama sita au saba kisha nyunyizia pistachio na lozi halafu panga tena manda na mafuta manda na mafuta tena sita au saba kisha nyunyizia tena pistachio na lozi.
Panga namna hivyo mpaka treya ijae inapofika manda ya mwisho kata vipande vya mraba vidogodogo humo humo kwenye treya kisha nyunyizia mafuta yaliyobaki.
Washa moto wa oven 350°F kwa muda wa dakika 20 au hadi rangi ibadilike kidogo (isikauke sana)
Chemsha syrup yako kama shira ya majimaji lakini isiwe nzito sana ikishakuwa tayari mwisho tia ndimu acha ipoe kidogo kisha miminia juu ya treya yote halafu malizia kunyunyizia pistachio na lozi zilizobaki.
Zikishakuwa tayari zipange kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

ANGALIZO

Ukishatoa treya kwenye oven wacha ipoe kidogo na syrup yako pia wacha ipoe kidogo kabla hujamimina, ukitia ya motomoto zitalainika.
Manda nyembamba za baklawa zinauzwa tiyari madukani kwenye pakiti.

Mapishi – Fish Finger

Leo tunaangalia mapishi ya fish finger ( sijui kama unaweza kusema kidole cha samaki)!, Ni mlo mzuri hasa kuliwa kama kitafunio au mboga ya pembeni.

Mahitaji

500g Fileti ya samaki
120g Chenga za mkate
100g Unga wa ngano
Mayai 2
Ndimu 1
Kitunguu saumu 1
Kotmiri
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Menya vitunguu saumu kisha visage

Katakata fileti kwa muundo wa mraba (kama vidole) kisha paka mchanganyiko wa vitunguu saumu

Kata ndimu na kamulia kwenye fillet yako

Weka chenga za mkate kwenye bakuli kisha uchanganye chumvi kiasi na kata kata kotmiri majani 3 na uchanganye pamoja.

Kwenye bakuli lingine weka mayai na uyapigepige yawe kama uji mzito

Weka unga kwenye bakuli jingine.

Chukua kipande cha fillet kiweke unga kidogo kisha kizamishe kwenye yai na baada ya hapo kizamishe kwenye mchanganyiko wa chenga za mkate. Fanya hivyo kwa vipande vyote.

Weka mafuta kwenye kikaago na subiri yachemke kisha weka fillet zako vizuri na zikaange pande zote hadi zimekuwa rangi ya brown ( hakikisha moto sio mkali sana).

Epua na weka pembeni mafuta yote yakauke

Weka kwenye sahani tayari kwa kula.

MAPISHI YA LADU

VIAMBAUPISHI

Unga – 6 vikombe

Samli – ½kikombe

Baking Powder – ½kijiko cha chai

Maziwa- 1 kikombe

Maji -Kisia kiasi kama unga bado mzito

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 5 vikombe

Maji – 2 1/2 vikombe

Vanilla – 2 vijiko vya chai

Rangi ya orange – 1 kijiko cha chai

Iliki ya unga – 1 Kijiko cha chai

MAANDALIZI

Changanya unga wa dengu, samli, baking powder pamoja na maziwa katika mashine ya keki (cake mixer).
Ukisha changanya angalia kama mchanganyiko wako umekua mwepesi kidogo kuliko wa keki, kama bado mzito basi ongeza maji kiasi.
Kisha weka mafuta kiasi kwenye karai,weka na samli kikombe kimoja, weka kwenye moto wa kiasi.
Mafuta yakisha pata moto, chukua kijiko kikubwa cha matundu chota mchanganyiko wako na kijiko cha kawaida tia kwenye kijiko cha matundu. Hakikisha kijiko cha matundu kiwe juu ya karai ili mchanganyiko wako uchuruzike ndani ya mafuta yalio pata moto.
Pika ndani ya mafuta mpaka iwive, ila usiache ikawa brown.
Toa mchanganyiko ulowiva tia ndani ya shira uliyo pika. Hakikisha shira iwe imepoa kabla ya kutia mchanganyiko huo.
Endelea kupika mchanganyiko wako mpaka uishe, kila ukitoa katika mafuta hakikisha unatia ndani ya shira.
Ukishamaliza wote kanda huo mchanganyiko ulokua ndani ya shira mpaka uone shira yote imekauka (yaani iwe imeingia ndani ya mchanganyiko).
Tupia zabibu kavu na lozi zilizo katwa, changanya na mkono.
Wacha mchanganyiko katika bakuli, funika na foil mpaka siku ya pili.
Siku ya pili chukua mchanganyiko kiasi katika mkono tengeneza mviringo (round).

MAANDALIZI YA SHIRA

Katika sufuria, tia sukari, maji, iliki, vanilla na rangi.
weka kwenye moto wacha ichemke mpaka itowe povu (bubbles) juu.
Kisha toa povu, wacha shira kwenye moto kama dakika 3.
Hakikisha shira yako iwe inanata kiasi kwenye vidole, lakini iwe nyepesi kidogo kuliko shira ya kaimati.

Jinsi ya kupika Vileja

VIPIMO

Unga wa mchele 500g

Samli 250g

Sukari 250g

Hiliki iliyosagwa 1/2 kijiko cha chai

Arki (rose flavour) 1/2 kijiko cha chai

Baking powder 1 kijiko cha chai

Mayai 4

Maji ya baridi 1/2 kikombe cha chai

NAMNA YA KUTAYRISHA NA KUPIKA

1. Saga sukari iwe laini kiasi, changanya unga wa mchele, baking powder, hiliki na sukari.

2. Pasha moto samli mpaka iwe nyepesi kama maji mimina kwenye ule mchanganyiko wa unga wa mchele, kisha uchanganye pamoja na arki.

3. Ongeza mayai yaliopigwa endelea kuchanganya mpaka unga umeanza kuchanganyika vizuri.

4. Ongeza maji ya baridi sana kama nusu kikombe tu ili uchanganyike vizuri.

5. Kata kwa design unayotaka viwe vinene visiwe kama cookies za kawaida kama ilivyo kwenye picha na ukipenda utaweka kidoto kwa kutumia zaafarani katikati ya kileja kama inavyoonesha hapo juu.

6. Choma kwa moto wa baina ya 300F na 350F kwa dakika 15 mpaka 20 visiwe vyekundu toa na tayari kwa kuliwa

Mapishi ya Wali, samaki wa nazi na kisamvu

Mahitaji

Mchele
Kisamvu kilichotwangwa
Samaki
Mbaazi
Nyanya chungu
Vitunguu
Nyanya ya kopo
Tangawizi
Kitunguu swaum
Vegetable oil
Curry powder
Tui la nazi (kopo 2)
Chumvi
Pilipili
Limao

Matayarisho

Safisha samaki kisha wamarineti na kitunguu swaum, tangawizi, pilipili, chumvi na limao kwa muda wa masaa 3.Baada ya hapo wakaange na usiwakaushe sana na uwaweke pembeni kwa ajili ya kuungwa.Katakata vitunguu maji, saga tangawizi na kitunguu swaum. Baada ya hapo injika sufuria ya mchuzi jikoni na mafuta kiasi ya kupikia, mafuta yakisha pata moto, tia vitunguu maji na vikaange mpaka viwe vya rangi ya brown. kisha tia kitunguu swaum na tangawizi.kaanga kidogo kisha tia nyanya ya kopo moja na ufunike. acha mpaka nyanya ziive. Kisha tia chumvi na curry powder na uache ikaangike kwa muda wa dakika 2 kisha tia samaki na nyanya chungu nakisha kamulia nusu ya limao. Geuza mpaka mchanganyiko uchanganyike vizuri kisha tia tui la nazi kopo moja na uache ichemke mpaka mchuzi uive.

Baada ya hapo chemsha kisamvu pamoja na mbaazi Kikisha iva, kaanga kitu na nyanya pembeni mpaka ziive kisha tia kisamvu. geuza mchanganyiko mpaka uchanganyike vizuri kisha tia tui la nazi na chumvi na aacha ichemke mpaka tui liive kisha ipua.malizia kwa kupika wali ambapo utachemsha maji kisha tia mafuta,chumvi na mchele na uupike mpaka uive kisha sevu na mboga ulizopika na mlo wako utakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika Biriyani Ya Nyama Ng’ombe

Viambaupishi Vya Masala

Nyama vipande – 3 LB

Mtindi – ½ kopo

Kitunguu (thomu/galic) – 1½ kijiko cha supu

Tangawizi – 1½ kijiko cha supu

Nyanya – 2

Pilipili mbichi – kiasi

Nyanya kopo – 4 vijiko vya supu

Vidonge supu – 2

Pilipili nyekundu paprika – kiasi

Bizari zote saga – 2 vijiko vya supu

Viazi – 4

Mafuta – 2 mug

Samli – ½ kikombe

Vitungu – 6

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika masala

Kwenye sufuria tia nyama, saga nyanya na thomu, pilipili mbichi, tangawizi. Mimina kwenye nyama na mtindi, tia na nyanya kopo, bizari paprika, vidonge vya supu, chumvi kisha changanya vyote pamoja weka motoni.
Katika sufuria nyengine tia mafuta na samli kaanga vitungu mpaka viwe rangi ya hudhurungi toa weka pembeni.
Kanga viazi weka pembeni.
Chukua mafuta kidogo uliyokangia tia kwenye nyama acha katika moto wa kiasi mpaka nyama iwive na maji ya punguke.
Tia viazi na vitunguu vivunje vunje tia ndani ya nyama acha moto mdogo.

Vipimo Vya Wali

Mchele – 5 mug

Maji – kiasi

Chumvi – kiasi

Mafuta uliyokaanga vitungu – kiasi

Rangi ya biriani – ¼ kijiko cha chai

*Zafarani – ½ kijiko cha chai

*roweka rangi na zafarani

Namna Ya Kutarisha Na Kupika Wali

Osha mchele roweka muda wa saa.
Chemsha maji kama magi 10 hivi na chumvi tia mchele.
Uache uchemke ukishaiva kiini nusu, mwaga maji chuja.
Mimina juu ya nyama tia rangi na mafuta kwa juu funika.
Aacha kidogo katika oveni kwa muda wa dakika 20 hivi kisha epua ikiwa tayari.

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About