Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Biriani Ya Samaki Nguru, Njegere Na Snuwbar (UAE)

Mahitaji

Mchele wa basmati – 4 cups

Samaki nguru (king fish) – 7 vipande au zaidi

Kitunguu – 5

Nyanya/tungule – 3

Njegere – 1 kikombe

Snuwbar (njugu za pine) – 1 kikombe

Viazi – 2 kata kata mapande makubwa

Tangawizi mbichi – 1 kijiko cha supu

Kitunguu saumu – 1 kijiko cha supu

Pilipili nyekundu – 1 kijiko cha chai

Bizari ya biriani/garama masala – 1 kijiko cha supu

Namna Ya Kupika:

Kaanga samaki mbali kwa viungo upendavyo umkoleze vizuri. Au choma (bake/grill) katika oveni ukipenda.
Weka mafuta katika sufuria, tia vitunguu kaanga hadi vigeuka rangi. Gawa sehemu mbili.
Sehemu moja bakisha katika sufuria kisha tia tangawizi mbichi na kitunguu thomu ukaange.
Tia nyanya kaanga kisha tia bizari zote endelea kukaanga, tia njegere, njugu za snuwbar na ndimu kavu.
Tia viazi ulivyokwishakaanga, na vitunguu vilobakia.
Tia mapande ya samaki, changanya na masala bila ya kumvuruga samaki.
Chemsha wali kisha mwagia juu yake, funika upike ndani ya oveni au mkaa hadi wali uive kama unavyopika kawaida ya biriani.
Epua pakua huku ukichanganya na masala ya samaki.

Mapishi ya Mitai

VIAMBAUPISHI

Unga wa ngano – magi 2 (vikombe vikubwa)

Hamira kijiko 1 cha chai

Sukari Vijiko 2 vya supu

Maziwa ¾ Magi

Siagi Vijiko 2 vya supu

Mafuta ya kukaangia kiasi

VIAMBAUPISHI:SHIRA

Sukari ¾ Kikombe

Maji ¾ Kikombe

Illiki ya unga kiasi

Zafarani kiasi

JINSI YA KUPIKA

Katika bakuli, changanya vipimo vyote pamoja na ukande unga usiwe mgumu wala laini sana uwe kiasi.
Kisha fanya donge moja na iache pahali penye joto mpaka iimuke.
Halafu weka mafuta ya kukaangia kwenye moto.
Sukuma donge hadi liwe duara sio nyembamba sana, kisha katakata kama maandazi.
Mafuta ya kisha pata moto choma mittai hukuunazigeuza hadi ziwive na kugeuka rangi.
Katika sufuria tia vipimo vya shira na iache ichemke isiwe nzito sana.
Mimina mitai kwenye shira na uzipepete, kisha weka kwenye sahani na zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kuandaa Vileja Vya Tambi

MAHITAJI

Tambi (vermiceli Roasted) Mifuko 2

Siagi – 4 Vijiko vya supu

Maziwa (condensed) 300Ml

Lozi zilizokatwakatwa – 1 kikombe

Zabibu kavu – 1 Kikombe

Arki (essence) – 1 Kijiko cha supu

MAPISHI

Weka karai kwenye moto kiasi
Tia siagi
Tia tambi uzikaange usiachie mkoni mpaka ziwe rangu ya dhahabu.
Weka lozi na zabibu huku unakoroga
Tia maziwa na huku unakoroga usiachie mkono.
Tia arki
Epua karai, tumia kijiko cha chai kwa kuchotea na utie kwenye kikombe cha kahawa nusu usikijaze.
Kipindue kwenye sahani utoe kileja.
Fanya hivyo mpaka umalize vyote.

Mapishi ya viazi mbatata Vya Nazi Kwa Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Mbatata / viazi – 2 kilo

Nyama ng’ombe – ½ kilo

Kitunguu maji – 2

Tungule/nyanya – 2

Nazi /tui zito – 2 vikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic) ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Tangawizi mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

pilipili shamba/mbichi ilosagwa – kiasi

Mdalasini – 1 kipande

Bizari ya manjano – ½ kijiko cha chai

Bizari ya pilau/jiyrah/cummin – ½ kijiko cha chai

Ndimu/limau – 1

Namna Ya Kupika:

Chemsha nyama kwa kutia; chumvi, tangawizi, kitunguu thomu, mdalasini, na bizar zote.

Ipike nyama mpaka iwive na ibakishe supu yake kidogo.

Changanya tui la nazi pamoja na supu ilobakia.

Panga mbatata katika sufuria.

Tia nyama

Mwagia vitunguu na nyanya ulizotayarisha, tia pilipili.

Mwagia supu ulochanganya na tui

Funika upike mpaka viwive .

Tia ndimu

Mapishi ya Sponge keki

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) 100g
Sukari (sugar) 100g
Siagi isiyokuwa na chumvi (unsalted butter) 100g
Mayai (eggs) 2
Vanila 1 kijiko cha chai
Chumvi pinch
Warm water 3 vijiko vya chakula

Matayarisho

Kwanza washa oven moto wa 200 C. Baada ya hapo saga butter na sukari mpaka viwe laini kisha tia mayai na uendelee kusaga mpaka vichanganyike vizuri kisha tia unga, vanila, chumvi na na maji na usage mpaka upate uji usiokuwa mzito sana au mwepesi sana. Baada ya hapo utie kwenye baking tin na u bake kwa muda wa dakika 25 na mpaka cake yako iive yani juu na chini iwe ya brown na ukidumbukiza kijiti katikati kinatoka kikiwa clean. Baada ya hapo itoe kwenye tin na uiache ipoe. Ikisha poa itakuwa tayari kwa kuliwa.

Virutubishi, kazi zake katika mwili na vyanzo vyake

Virutubishi

ni viini vilivyoko kwenye chakula ambavyo vinauwezesha mwili kufanya kazi zake, karibu vyakula vyote huwa na kirutubishi zaidi ya kimoja ila hutofautiana kwa kasi na ubora. Kila kirutubishi kina kazi yake mwilini na mara nyingi hutegemeana ili viweze kufanya kazi yake kwa ufanisi. Hakuna chakula kimoja chenye virutubishi vya aina zote isipokuwa maziwa ya mama kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto, ni mhimu kula vyakula vya aina mbalimbali ili kuwezesha mwili kupata virutubishi mchanganyiko vinavyohitajika.

Aina za virutubishi vinavyohitajika mwilini

  1. Kabohaidreti / vyakula vya wanga
  2. Mafuta ya Wanyama na Mimea
  3. Protini
  4. Vitamini na Madini
  5. Maji

Kabohaidreti / vyakula vya wanga

Kabohaidreti / vyakula vya wanga huvipa mwili nguvu inayoihitajika kujiendesha. Vyakula
hivi vyaweza kuwa sahili au changamani. Hii inahusu jinsi ambavyo chakula chaweza
kubadilisha sukari katika mwili. Vyakula vya wanga na sukari huvipa mwili nguvu
inayohitajika kuufanya upumue na kuendelea kuishi, kuwa na mwendo na utoaji joto, na kwa
ukuaji na utengenezaji wa mkusanyiko wa seli (tishu). Baadhi ya wanga na sukari
hubadilishwa kuwa mafuta mwilini.
Ufumwele utokanao na kabohaidreti hufanya kinyesi kiwe laini na kingi na huondoa kemikali
za sumu, na hivyo hufanya matumbo yawe na afya njema. Hupunguza uyeyushaji na
ufyonzaji wa virutubishi katika vyakula, na husaidia kupunguza unene.

Vyanzo vya kabohaidreti

Vyanzo vikuu vya kabohaidreti ni:

• Nafaka

– Mahindi/ugali
– Serena
– Mtama
– Mchele
– Unga wa ngano

• Mizizi ya vyakula vya wanga

– Viazi vitamu
– jimbi
– Viazi mviringo
– Muhogo mbichi
– Unga wa muhogo
– Ndizi

Mahitaji ya kabohaidreti mwilini

– Mahitaji hutofautiana kutegemea na umri, jinsi, jinsia, shughuli, hali ya kiafya
– Kula mara tatu au zaidi kwa siku.

Mafuta ya Wanyama na Mimea

Mafuta ya wanyama na mimea kwenye chakula na tishu ya shahamu kwenye miili yetu huwa
na shughuli nyingi

Kazi za mafuta ya wanyama kwenye mwili

• Virutubishi: mafuta ya wanyama hutoa tindikali za mafuta muhimu, ambazo
huhitajika katika ukuaji wa kawaida kwa watoto wachanga na watoto wengine na
kwa uzalishaj wa michanganyiko ya aina ya kihomoni inayorekebisha upeo mpana
wa shughuli za kimwili na kukufanya uwe mwenye afya njema.
• Usafirishaji: mafuta ya wanyama hubeba mafuta ya miyeyusho ya vitamini (A, D,
E, na K) na kurahisisha ufyonzaji wake.
• Ufahamu: mafuta ya wanyama huchangia kwenye harufu nzuri na ladha ya
chakula.
• Umbile la asili: mafuta ya wanyama hufanya chakula (hususan nyama na vyakula
vya kukaushwa) kuwa nyororo.
• Ukinaishaji: mafuta ya wanyama hukipa chakula ukinaishaji, hivyo hujikuta
umeshiba na kutosheka kwa muda mrefu baada ya chakula.
• Mafuta ya wanyama ni chanzo cha utoaji wa mkusanyiko wa kalori. Hili ni jambo
jema unapokuwa kwenye safari ndefu, itumiayo nguvu nyingi, ukiwa umebeba
chakula chako.

Mafuta ya wanyama mwilini hufanya yafuatayo:

• Mafuta ni muundo mkuu wa mwili wa kuhifadhi nishati (ambazo ni muhimu wakati wa
ugonjwa au kupungua kwa ulaji chakula)
• Mafuta hutoa sehemu kubwa ya nishati inayotumika kwenye kufanyiza kazi misuli.
• Mafuta hukinga viungo vya ndani na kuhami miili yetu dhidi ya hali za joto
zinazopitiliza mipaka.
• Mafuta huunda malighafi kuu ya utando wa seli (hususan seli za ubongo na za
mishipa ya fahamu)
• Mafuta hugeuzwa kuwa aina nyingi za homoni (ikiwemo homoni za mambo yahusuyo
mapenzi)
Mafuta ki kitu kizuri! Isipokuwa tu pale uzuri unapozidi kiwango ndipo kunapokua na tatizo.

Aina za mafuta:

mafuta yaliyokolea dhidi ya yale yasiyokolea
Kama ambavyo kuna aina kuu mbili za kabohaidreti, kuna aina kuu mbili za mafuta
kutegemea na mfumo wake wa kikemia; mafuta yaliyokolea na yale ambayo hayajakolea.
Aina hizi za mafuta zina athali tofauti kabisa kwa afya yako.

1. Mafuta yaliyokolea

• Huwa na kawaida ya kuongeza lehemu “mbaya” kwenye damu na kuongeza
uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo.
• Mafuta yaliyokolea huwa na kawaida ya kuganda kwenye hali ya joto la kawaida.
• Hupatikana kwa wingi kutokana na vyanzo vya mafuta ya wanyama.
Vyanzo vya mafuta yaliyokolea
• Siagi, malai, mafuta ya nyama ya ngómbe, ngozi ya kuku, mafuta ya maziwa yenye
malai, jibini, aisikirimu, siagi, samli, mafuta ya nguruwe/ya kupikia, mafuta
yatokanayo na nyama, mawese mekundu, na nazi.
• Yaliyopo nje ya utaratibu: mafuta ya nchi za joto (ikiwemo ya nazi na mawese) yana
kiwango kikubwa cha mafuta yaliyokolea.

2. Mafuta yasiyokolea

• Mafuta yasiyokolea ni aina ya mafuta ambayo kwa ujumla yanahusishwa na afya bora.
• Yana kwaida ya kushusha viwango vya lehemu na kupunguza hatari za magojwa ya
moyo.
• Mafuta yasiyokolea huwa na kawaida ya kuwa ya mmiminiko katika joto la kawaida.
• Hupatikana kwa wingi kutokana na mimea.
Vyanzo vya mafuta yasiyokolea
• Mafuta yatokanayo na mboga za majani, mizeituni, miparachichi, njugu, mafuta ya
karanga, maharagwe meupe, mbegu za alizeti, mbegu za ufuta na aina nyingine za
mbegu, mafuta ya samaki na soya.
• siagi, samli, mafuta ya nguruwe/ya kupikia, maziwa yenye malai, jibini, mafuta
yatokanayo na nyama, mawese mekundu, na nazi.

Kuna mafuta yatokanayo na kuchujwa kwa mafuta ya mbogamboga na kugandishwa. Mafuta
haya huishia kuwa na tabia za mafuta yaliyokolea. Mafuta haya pia hayapashwi kutumiwa
kwa wingi.

Vyanzo ni:

• majarini, mafuta ya nguruwe, vyakula vya kukaangwa, donati, keki, biskuti, aiskrimu.

Mahitaji ya mafuta mwilini

Mahitaji ya mafuta huelezewa kama ‘ni asilimia ya mahitaji yote ya nishati’. Kiwango chote
cha asilimia ya nishati kinachopashwa kitokane na mafuta katika mlo bora uliokamilika ni
kama ifuatvyo:
• Asilimia 30-40 kwa watoto hadi kufikia miaka miwili kwenye milo ya nyongeza
• Asilimia 15-30 kwa watoto wakubwa na wengi wa watu wazima; kwa watu wazimu
wenye afya – hadi asilimia 35 inakubalika.
• Angalau asilimia 20 hadi 30 kwa akina mama wenye umri wa kuweza kuzaa (15-45).

Protini

Protini ni zana za ujenzi wa misuli yetu, viungo na baadhi ya vitu vingi vinavyotengeneza
miili yetu. Hutoa tindikali muhimu za amino zitumiwazo na mwili kutengeneza misuli ya tishu.
Mwili unahitaji protini na kalori kila siku.
Unapokosa kupata kalori na protini za kutosha kila siku, mwili wako hutumia akiba yake
kufidia pengo la ukosefu wa nishati. Hali hii huinyima mwili wako kalori unazohitaji kuufanya
uwe na afya bora na hivyo kusababisha kupungua kwa uzito.

Vyanzo vya protini

Protini yaweza kupatikana kwenye vyakula vya wanyama na mimea.

1. Vyanzo vitokanavyo na wanyama

• Nyama, kuku/mabata n.k., samaki, mayai, jibini, maziwa na mtindi.
• Vyakula hivi vinachukuliwa kuwa kama ‘kamili’ au ‘vyenye kiwango cha juu’cha
protini kwa kuwa vina aina zote za ‘tindikali muhimu za amino’. ‘Muhimu”inamaanisha
lazima vitumiwe kwenye milo yetu; miili yetu haiwezi kuzitengeneza.

2. Vanyzo vitokanavyo na mimea

• Bidhaa zitokanazo na soya, (tofu, tempeh), maziwa ya soya na mazao mengine
yatengenezwayo na soya), maharagwe, mbegu na njugu.
• Viwango vidogo vya protini vinapatikana vilevile kwenye mikate, mahindi /ngano, na
aina nyinge ya nafaka, na mbogamboga pia.
• Vyanzo hivi vya protini vinachukuliwa kama ‘si kamili’kwa kuwa vinakosa moja au
zaidi ya tindikali muhimu za amino.
• Protini ya maharagwe meupe ndiyo ya kipekee. Haya yanachukuliwa kuwa ni kamili.

Mahitaji ya protini mwilini

Mahitaji hutofautiana kulingana na umri, jinsi, jinsia, na shughuli.

Vitamini na Madini

• Vitamini husaidia mwili kugeuza chakula kuwa nishati na tishu.
• Kuna aina 13 za vitamini kwa ujumla: Vitamini A; vitamini B; vitamini B mchanganyiko
unayojumuisha vitamini B1, Vitamini B2, Viamnini B3 vitamin, B6, Vitamini C, Vitamin
B12 tindikali ya pantotheniki (pantothenic acid), na biotini (biotin); na vitamini C, D, E,
na K.
• Madini yanahitajika katika ukuaji na utunzaji wa miundo ya mwili. Yanahitajika pia
katika kutunza juisi za uyeyushaji chakula na mimiminiko iliyopo ndani na
kandokando mwa seli.
• Madini hayatokani na mimea wala wanyama. Mimea hupata madini kutokana na maji
au udongo, na wanyama hupata madini kwa kula mimea au wanyama wanaokula
mimea.
• Vitamini na madini hujulikana pia kama vyakula vya ujenzi na ulinzi wa mwili.
• Vijirutubishi ambavyo havipatikani kwa wingi na ambavyo husababisha matatizo
mengi yatokanayo na utapiamlo wa ukosefu wa vijirutubish duniani ni kama
vifuatavyo; madini ya joto, zinki, vitamini A, chuma na folate.

Vyanzo vya Vitamini na Madini

• Mboga jamii ya machungwa, kama vile viazi vitamu vya njano na karoti, matunda jamii
ya machungwa kama vile, embe, papai, na mawese mekundu ni vyanzo vizuri sana
vya vitamini A.
• Matunda mengi yatokanayo na jamii ya michungwa na mboga zisizoivishwa sana
huwa na vitamini C.
• Mboga za kijani kibichi hutupatia folate na kiasi cha vitamini A.
• Mbogamboga nyingi (mf. nyanya, vitunguu) hutoa vijirutubishi muhimu vya nyongeza
viwezavyo kukinga mwili dhidi ya magonjwa sugu kama ya mioyo.
• Njia bora ya kuhakikisha tunapata vijirutubishi na ufumwele wa kutosha ni kula aina
mbalimbali za mbogamboga, matunda na nafaka zisizokobolewa kila siku.
• Nyama, viungo vya ndani vya wanyama na maini ya aina zote ni chanzo kizuri sana
cha vitamini A.

Mahitaji ya vitamin na madini mwilini

• Vitamini na madini vinahitajika kwa viwango vidogo vidogo.
• Mahitaji hutegemea umri, jinsi na kiwango cha shughuli, na ulaji wa aina mbalimbali
za matunda, mbogamboga na nafaka zisizokobolewa.

Maji

Maji ni kirutubishi muhimu sana. Hakika, zaidi ya nusu ya mwili ni maji. Unaweza kuishi bila
ya chakula kwa wiki kadhaa, bali hauwezi kuishi zaidi ya wiki moja bila ya maji.
Mwili unahitaji maji ili kufanya kazi.

Umuhimu wa maji mwilini

• Kuhifadhi joto la mwili;
• Kusafirisha virutubishi mwilini;
• Kuvifanya viungo viwe na unyevunyevu;
• Kuyeyusha chakula;
• Kuondoa uchafu mwilini;
• Kupoza mwili.
(Fikiria matumizi ya maji unapojenga nyumba; bila ya maji: saruji, mchanga na zege
havitakuwa na matumizi yeyote).

Vyanzo vya maji mwilini

• Maji yenyewe
• Juisi za matunda
• Supu
• Maziwa
• Uji
• Vinywaji visivyo na kafeini (vinywaji vyenye kafeini na kileo vina madawa ya
kuongeza mkojo (diuretics) inayosababisha upotevu wa maji mwilini)

Mahitaji ya maji mwilini

Lita 1.5 au glasi 8 kwa siku.

Jinsi ya kupika Mkate

Mahitaji

Unga wa ngano ( self risen flour) kikombe 1 na 1/2
Hamira (yeast) 1 kijiko cha chai
Sukari (sugar) 1 kijiko cha chakula
Chumvi (salt) 1/2 kijiko cha chai
Siagi iliyoyeyushwa (melted butter) 1 kijiko cha chakula
Maji ya uvuguvugu ( warm water) kiasi

Matayarisho

Changanya vitu vyote katika bakuli kubwa kisha aanza kukanda mpaka upate donge laini.Baada ya hapo liweke hilo donge kwenye bakuli la plastic na weke katika sehemu yenye joto ili unga uumuke. Hakikisha unga unaumuka zaidi (yani unaji double size) unaweza kuchukua kama saa 1 na nusu hivi. Baada ya hapo ukande tena na uache uumuke tena kwa mara ya pili, Ukisha umuka pakaza butter katika baking tin (chombo cha kuokea) na upakaze mkate butter kwa juu,kisha uoke katika oven kwa muda wa dakika 30 (katika moto wa 200C) (hakikisha juu na chini unakuwa wa brown Na hapo mkate wako utakuwa tayari

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Cornflakes

MAHITAJI

Unga – 1 Kikombe

Sukari ya kusaga – 3/4 Kikombe

Siagi – 125 gms

Yai – 1

Baking powder – 1/2 kijiko cha chai

Zabibu kavu – 1/2 kikombe

Cornflakes iliyovunjwa (crushed) – 2 Vikombe

Vanilla – 1 kijiko cha chai

MAANDALIZI

Tia kwenye mashine ya kusaga (blender) au mashine ya keki, siagi, yai na vanilla uchanganye hadi ichanganyike vizuri.
Tia baking powder, zabibu na unga na changanya vizuri.
Paka siagi sinia ya kupikia ya oveni.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Weka cornflakes katika sahani ya chali (flat) na zungusha viduara humo kisha upange katika sinia ya oveni.
Pika katika moto wa 350ºF kwa muda wa dakika 20-25 hadi vigeuke rangi na viwive.

Mapishi ya Biskuti Za Jam

VIAMBAUPISHI

Unga 2 ½ gilasi

Sukari ¾ gilasi

Samli 1 gilasi

Mayai 2

Baking powder 2 kijiko vya chai

Vanilla 1 ½ kijiko cha chai

Maganda ya chungwa 1

MAPISHI

Tia kwenye machine ya kusagia (blender) mayai, sukari, vanilla, samli na maganda ya chungwa, saga vizuri.
Tia unga kwenye bakuli pamoja na baking powder, mimina vitu ulivyosaga kwenye bakuli, changanya.
Punguza unga uliochanganya kidogo weka pembeni.
Unga uliobakia tia kwenya tray ya kuchomeya, utandaze vizuri, tia jam juu yake.
Chukua la kukwaruzia carrot (grater) ukwaruze unga uliuopunguza juu ya jam.
Choma kwa muda dakika 20 moto wa 180 C.

Acha ipowe kidogo, zikate vipande vya mraba (square) Tayari kwa kula.

Jinsi ya kuandaa Vileja Vya Karanga

MAHITAJI

Mayai 5

Sukari 450gm (1 lb)

Unga wa Ngano 1 kg

Siagi 450gm (1 lb)

Baking powder ½ Kijiko cha chai

Unga wa Custard Vijiko 2 vya chakula

Karanga za kusaga 250gm

Jam ½ kikombe

MAANDALIZI

Chukua bakuli la kiasi, weka sukari na siagi.
Changanya sukari na siagi kwa kutumia mashine ya kukorogea keki (cakemixer), mpaka sukari ichanganyike na siagi.
Vunja yai moja moja na weka kiini chake kwenye mchanganyiko wa sukari na siagi, endelea kuchanganya mpaka ichanganyike vizuri. Hifadhi ute wa mayai ndani ya kibakuli.
Mimina unga wa ngano ndani ya mchanganyiko wako huku ukichanganya Changanya unga wa custard na baking powder.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Vichovye viduara ndani ya ute wa yai kisha zimwagie unga wa karanga na kuzipanga kwenye tray ya kuchomea.
Weka dole gumba kati kati ya kila kiduara na uweke jam.
Washa jiko (oven) 350F na uchome vileja vyako kwa dakika 20.
Toa vileja vyako vipoe na uviweke ndani ya sahani tayari kwa kuliwa.

Madhara ya nyama nyekundu kwa mtu mwenye VVU

Kuna nyama za aina mbili, nazo ni nyama nyeupe na nyama nyekundu.

Nyama nyeupe

Hizi ni nyama zitokanazo na samaki, kuku, ndege wa aina zote, bata, wadudu

Nyama nyekundu

Hutokana na ng’ombe, mbuzi, kondoo,nguruwe na wanyama wa porini.

Nyama ina virutubishi vingi muhimu kwa afya ya binadamu kama protini, vitamini na madini. Madini ya chuma yanayopatikana kwenye nyama ni rahisi sana kusharabiwa (kufyonzwa) mwilini na ni muhimu kwa kuongeza wekundu wa damu.
Uwezo wa miili ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kuyeyusha chakula na kusharabu (kufyonza) virutubishi hupungua. Utumiaji wa nyama nyekundu kwa wingi unaweza kuwaletea matatizo hasa katika uyeyushwaji tumboni kwani nyama nyekundu si rahisi kuyeyushwa ukilinganisha na nyama nyeupe.

Hata hivyo katika nchi yetu watu walio wengi wanatumia nyama kwa kiasi kidogo sana na mara chache. Si vyema watu hawa waache kabisa nyama nyekundu. Jambo la muhimu ni kutumia njia mbalimbali ili kuifanya nyama hii iyeyushwe kwa urahisi tumboni.

Namna ya kusaidia uyeyushwaji ni pamoja n a : –

• Kutafuna vizuri au kutumia nyama ya kusaga (kwa wanaoipata).
• Kupika nyama na viungo vinavyosaidia kulainisha kama vile papai bichi, limao, vitunguu saumu n.k.
• Kula nyama pamoja na papai

Kwa hiyo, kwa anayepata nyama nyekundu kwa wingi, kupunguza kiasi cha nyama hiyo na kuongeza kiasi cha nyama nyeupe. Na kwa yule asiyepata nyama nyeupe, apatapo nyama nyekundu asiache kutumia kwani ina umuhimu mwilini mwake.

MAANA YA MANENO YANAYOTUMIKA KATIKA MASUALA YA LISHE

1. Chakula

ni kitu chochote kinacholiwa au kunywewa na kuupatia mwili virutubishi mbalimbali Chakula huupatia mwili nguvu, kuulinda na kuukinga dhidi ya maradhi mbalimbali .Mfano wa chakula ni ugali, wali, maharagwe, ndizi, viazi, mchicha, nyama, samaki.

2. Lishe

ni mchakato unaohusisha hatua mbalimbali za jinsi mwili unavyokitumia chakula kilicholiwa, hatua hizi ni kuanzia chakula kinapoliwa, jinsi mwili unavyokisaga na kukiyeyusha, umetaboli, na hatimaye virutubishi kufyonzwa na kutumika mwilini.

3. Virutubishi

ni viini vilivyoko kwenye chakula ambavyo vinauwezesha mwili kufanya kazi zake, karibu vyakula vyote huwa na kirutubishi zaidi ya kimoja ila hutofautiana kwa kasi na ubora. Kila kirutubishi kina kazi yake mwilini na mara nyingi hutegemeana ili viweze kufanya kazi yake kwa ufanisi. Hakuna chakula kimoja chenye virutubishi vya aina zote isipokuwa maziwa ya mama kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto, ni mhimu kula vyakula vya aina mbalimbali ili kuwezesha mwili kupata virutubishi mchanganyiko vinavyohitajika.

4. Mlo kamili

ni ule ambao hutokana na chakula mchanganyiko kutoka katika makundi yote ya chakula na una virutubishi vyote muhimu kwa ajili ya lishe na afya bora. Mlo huu unapoliwa kwa kiasi cha kutosha kulingana na mahitaji ya mwili angalau mara tatu kwa siku huupatia mwili virutubisho vyote muhimu.

5. Ulaji unaofaa

hutokana na kula chakula mchanganyiko na cha kutosha (mlo kamili) ili kukidhi mahitaji ya mwili. Ulaji unaofaa pia huzingatia matumizi ya kiasi kidogo cha chumvi, mafuta, sukari, ulaji wa nyama nyekundu kwa kiasi kidogo. Ni muhimu kuzingatia ulaji wa mboga mboga, matunda, na vyakula vya jamii ya kunde kwa wingi ili kudumisha uzito wa mwili unaotakiwa na kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

6. Nishati- lishe

ni nguvu inayopatikana baada ya virutubishi (kabohaidreti, mafuta) kuvunjwa vunjwa mwilini. Mwili huitumia nguvu hiyo kufanya kazi mbalimbali Kama kulima, kutembea, kupumua, kuziweka seli za mwili katika hali inayotakiwa n.k.

7. Kalori au kilo kalori

ni kipimo kinachotumika kupima nishati -lishe

8. Makapi mlo

ni sehemu ya chakula ambayo mwili hauwezi kuyeyusha lakini ni muhimu katika uyeyushwaji wa chakula. Mfano wa vyakula venye makapi mlo kwa wingi ni mboga za majani, matunda( maembe, machungwa, mapera, machenza, mafenesi, unga usiokobolewa( dona) na vyakula vya jamii ya kunde.

9. Lehemu

ni aina ya mafuta yanayopatikana hasa kwenye vyakula vya asili ya wanyama na pia hutengenezwa mwilini. Lehemu inayotokana na vyakula ikizidi mwilini huleta madhara ya kiafya. Vyakula venye lehemu kwa kiasi kikubwa ni pamoja na maini, figo, mayai, nyama iliyonona kama nundu, nyama ya nguruwe yenye mafuta, mkia wa kondoo, samli, siagi, ngozi ya kuku n.k.

10. Utapiamlo

ni hali ya kupungua au kuzidi kwa baadhi ya virutubishi mwilini ambapo husababisha lishe duni au unene uliozidi.

11. Antioxidants

ni viini ambavyo vina uwezo wa kukinga seli za mwili zisiharibiwe na chembe chembe haribifu (free radicals) ambazo huweza kusababisha saratani. Viini hivyo huungana na chembechembe hizo haribifu na kuzidhibiti ili zisisababishe madhara. Mifano ya antioxidants ni pamoja na beta-carotene, lycopene, vitamin C, E, na A.

Mapishi ya Bilinganya

Mahitaji

Bilinganya 2 za wastani
Nyanya kubwa 1
Kitunguu maji 1 kikubwa
Swaum 1/2 kijiko cha chai
Limao 1/4
Pilipili ya unga 1/2 kijiko cha chai
Parpika 1/4 kijiko cha chai
Pilipili mtama 1/4 kijiko cha chai
Curry powder1/4 kijiko cha chai
Chumvi kiasi
Coriander
Olive oil

Matayarisho

Katakata bilinganya slice nyembamba kisha ziweke pembeni. Baada ya hapo kaanga kitunguu maji mpaka kiwe cha brown kisha tia swaum na spice zote, zikaange kidogo kisha tia nyanya na chumvi kiasi. Pika nyanya mpaka iive na itengane na mafuta. Baada ya hapo tia mabilinganya na ukamulie limao kisha punguza moto na uyafunike na mfuniko usioruhusu kutoa mvuke ili yaivie na huo mvuke. Baada ya hapo yaonje kama yameiva na malizia kwa kutia fresh coriander na baada ya hapo yatakuwa tayari kwa kuliwa. kwa kawaida mi hupendaga kuyalia na wali na maharage badala ya kachumari kwahiyo nakuwa naitumia hiyo kama kachumbari

Jinsi ya kupika Labania Za Maziwa

Viamba upishi

Maziwa ya unga 2 vikombe

Sukari 3 vikombe

Maji 3 vikombe

Unga wa ngano ½ kikombe

Mafuta ½ kikombe

Iliki kiasi

Jinsi ya kuandaa na kupika

Paka sinia mafuta kabla ya kupika labania
Katika sufuria chemsha maji na sukari pamoja na iliki mpaka inate vizuri
Kisha mimina mafuta koroga
Halafu mimina unga wa ngano na ukoroge haraka haraka
Kisha tia unga wa maziwa, endelea kukoroga usiwe na madonge mpaka uwe rangi ya browni isiokoleza.
Kisha mimina mchanganyiko kweye sinia uliyoipaka mafuta, iwache ipoe na kata kata upendavo na itakuwa tayari.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About