Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Sambusa za nyama

Mahitaji

Nyama ya kusaga (minced beef 1/4 kilo)
Vitunguu maji vilivyokatwakatwa(diced onion 2 vikubwa )
Kitunguu swaum/ tangawizi (garlic and ginger paste 1 kijiko cha chakula)
Chumvi (salt)
Pilipili iliyokatwakatwa (scotch bonnet 1)
Limao (lemon 1/2)
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Cinnamon powder 1/4 kijiko cha chai
Coriander powder 1/4 kijiko cha chai
Cumin powder 1/4 kijiko cha chai
Unga wa ngano (all purpose flour kidogo)
Manda za kufungia (spring roll pastry)
Giligilani (fresh coriander kiasi)
Mafuta ya kukaangia

Matayarisho

Changanya nyama na limao, chumvi, pilipili,kitunguu swaum, tangawizi na spice zote, kisha pika katika moto wa kawaida mpaka nyama iive na maji yote yakauke. Baada ya hapo kabla hujaipua nyama tia vitunguu na giligilani na uvipike pamoja kwa muda wa dakika 2 na uipue weka pembeni na uache viipoe. Baada ya hapo tia unga kidogo katika bakuli nauchanganye na maji kidogo kupata uji mzito kwa ajili ya kugundishia manda. Baada ya hapo tia nyama katika manda na kisha zifunge kwa kugundishia na unga wa ngano.Ukisha maliza kuzifunga zote zikaange mpaka ziwe za brown na uzitoe. Na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi – Saladi ya Matunda

Matunda ni mojawapo wa kundi la vyakula, ni muhimu sana kwa afya bora. Matunda yakitengenezwa vizuri yanavutia sana na yanakuwa ni chakula kizuri sana.

Mahitaji

Embe iliyoiva kiasi
Nanasi
Tango
Tikiti maji
Zabibu
Papai

Matayarisho

1. Ondoa maganda kwenye embe, nanasi, tango, papai na tikiti maji kisha kata kata vipande vidogo vidogo vya mraba

2. Changanya vipande vya matunda kwenye bakuli safikisha weka na zabibu zilizotolewa kwenye kikonyo chake.

3. Weka kwenye friji yapate ubaridi kidogo

4. Saladi yako tayari kwa kuliwa

Waweza kula saladi hii kama mlo wa kati au kama mlo kamili wa usiku.

Mapishi ya samaki aina ya salmon

Mahitaji

Salmon fillet 2
Potatao wedge kiasi
Lettice kiasi
Cherry tomato
Limao 1
Swaum
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Mmarinate samaki na chumvi, swaum na nusu ya limao kisha muweke pembeni, baada ya hapo washa oven kisha tia potato wedge zikisha karibia kuiva anza kumpika samaki, tia mafuta kidogo sana kama kijiko kimoja cha chai hivi katika frypan isiyoshika chini yakisha pata moto kiasi muweke samaki wako (upande wenye ngozi chini kwanza) Mpike mpaka uone rangi ya kahawia kwa chini kisha mgeuze upande wa pili, uku samaki wako akiwa anaendelea kuiva, tayarisha salad yako kwa kusafisha lettice na nyanya kisha zichanganye pamoja kisha tengeneza salad dressing pembeni , kamua limao kisha tia olive oil na chumvi kidogo, Baada ya hapo samaki na potato wedge vitakuwa vimeiva, andaa mlo wako na utakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi – Kisamvu cha Karanga

Mapishi yetu leo ni kisamvu cha kuchanganya na karanga. Karibu.

Mahitaji

Majani ya kisamvu
Karanga nusu kikombe
kitunguu kimoja
nyanya mbili
karoti moja
mafuta na chumvi kiasi

Matayarisho

1. Osha kisamvu chako vizuri kisha katakata vipande vidogo vidogo

2. Unaweza kutwanga kwa kutumia kinu au kuchemsha kidogo na kisha kusaga kwa kutumia mashine. Ukitumia mashine uwe makini usije ukasaga sana ukaharibu.

3. Kaanga karanga kidogo na kisha zisage ziwe unga unga.

4. Chemsha kisamvu chako hadi kiive.

5. Katakata kitunguu, karoti na na nyanya

6. Anza kuunga kisamvu kwa kukaanga vitunguu, weka karoti na kisha nyanya na vikishaiva weka kisamvu na koroga pamoja kisha weka karanga. Acha vichemke kwa muda na unaweza pia weka na nazi tui la kwanza.

7. Baada ya muda mfupi epua na kitakiwa tayari. Waweza kula kwa ugali, wali, chapati, makande n.k

Mapishi ya Dagaa wa nazi, nyanya chungu na bamia

Mahitaji

Dagaa waliokaushwa (dried anchovy 2 kikombe cha chai)
Bamia (okra 5)
Nyanya chungu (garden egg 5)
Tui la nazi (coconut milk 1 kikombe cha chai)
Nyanya (fresh tomato 2)
Kitunguu (onion 1)
Curry powder 1/2 ya kijiko cha chai
Turmeric powder 1/2 kijiko cha chai
Limao (lemon 1/2)
Chumvi (salt kiasi)
Pilipili (scotch bonnet 1)
Mafuta (veg oil)

Matayarisho

Safisha dagaa na uwaweke pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu vikianza kuwa vya brown tia dagaa wakaange kidogo kisha tia chumvi, pilipili, curry powder, turmeric, bamia na nyanya chungu, koroga vizuri mpaka mchanganyiko wote uchanganyike vizuri kisha tia nyanya na ufunike. Pika mpaka nyanya iive kisha kamulia limao,na pia hakikisha nyanya chungu na bamia zimeiva kidogo(usiache mpaka ziive sana manake zitavurugika pindi utakapotia tui la nazi) kisha malizia kwa kutia tui la nazi na uache lichemke mpaka rojo ibakie kidogo. Hakikisha nyanya chungu na bamia zimeiva ndo uipue. Na hapo dagaa wako watakuwa tayari kwa kuliwa na wali au ugali.

Mapishi ya Wali Wa Zaafarani Na Kuku Wa Kupaka

Vipimo

Wali:

Mchele – 3 Vikombe

Kitunguu kiichokatwa – 1

Pilipili boga nyekundu iliyokatwa vipande – 1

Mafuta – ¼ Kikombe

Zaafarani – 1 kijiko cha chai tia kwenye kikombe na maji robo roweka

Chumvi – 1 kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katika sufuria, tia mafuta, kaanga kitunguu mpaka kiwe kidogo rangu ya udongo (brown)
Tia pili pili boga.
Tia mchele, kaanga kwa muda wa dakika 3, tia zaafarani na chumvi.
Tia supu uliyochemshia kuku iwe imoto.
Pika wali katika moto mdogo hadi uwive.

Kuku

Kuku Mzima -1

Mayai ya kuchemsha – 6

Namna Ya Kupika Kuku

Mchemshe kuku mzima na chumvi mpaka uhakikishe ameiva vizuri.
Mtowe na muweke pembeni. Supu yake tumia katika wali kama ilivyo hapo juuu.
Chemsha mayai, menya na kata vipande viwili kila yai moja weka kando

Vipimo Vya Sosi Ya Kuku Ya Nazi

Kitunguu – 1

Nyanya iliyokatwa vipande – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi – 1 kijiko cha supu

Garam Masala – ½ kijiko cha supu

Bizari ya manjano – ½ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Pilipili masala ya unga – ½ kijiko cha chai

Nyanya ya kopo – 1 kijiko cha supu

Nazi ya unga – 1 kikombe

Maji ya ukwaju – ¼ kikombe cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Tia Mafuta vijiko 2 vya supu katika sufuria
Kaanga kitunguu maji mpaka kiwe rangi ya udongo (brown).
Tia thomu na tangawizi.
Tia nyanya nzima iliyokatwa katwa.
Tia garam masala, manjano, pilipili ya unga, nyanya ya kopo, kaanga vizuri.
Changanya kwenye sufuria na ukwaju. Iache ichemke vizuri.
Changanya nazi ya unga na maji vikombe viwili.
Mtie kuku mpike vizuri na hilo tui.
Mtie kwenye oveni kidogo.

Kupakuwa katika Sinia

Pakuwa wali kwanza katika sinia
Muweke kuku juu ya wali.
Pambia mayai

Mapishi ya Tende Ya Kusonga Ya Lozi Na Cornflakes

VIAMBAUPISHI

Tende zilizotolewa kokwa – 1 Kilo

Cornflakes – 1 ½ kikombe

Lozi Zilokatwa katwa – 1 kikombe

Siagi – ¼ kilo

MANDALIZI

Mimina tende na siagi kwenye sufuria bandika motoni moto mdogo mdogo mpaka zilainike. Kwa muda wa dakika 10.
Isonge kidogo kwa mwiko au kuikoroga ichanganyike vizuri.
Changanya Cornflakes na lozi kwenye tende mpaka zichanganyika vizuri.
Pakaza treya au sinia mafuta au siagi kidogo.
Mimina mchanganyiko wa tende, zitandaze vizuri na ukate vipande saizi unayopenda. Zikiwa tayari kuliwa kwa kahawa.

Mapishi ya Pilau Ya Nyama Ya Ng’ombe Na Nyanya

Vipimo

Mchele (Basmati) – 3 vikombe

Nyama ya ngo’mbe – 1 kg

Pilipili boga – 1 kubwa

Nyanya – 2 kubwa

Vitunguu maji – 2 vikubwa

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Tangawizi – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 1

Mafuta ya kupikia – ½ kikombe

Mdalasini – ½ kijiko cha chai

Binzari nyembamba – 1 kijiko cha chai

Pilipili manga – ½ Kijiko cha chai

Hiliki – ½ Kijiko cha chai

Namna ya kutayarisha na Kupika

Roweka mchele wako katika chombo

Chukuwa nyama na ioshe vizuri na itie thomu, tangawizi, ndimu, pilipili manga na chumvi kiasi

Iweke jikoni hadi ikauke maji na kuwa imewiva huku ukiikaanga kaanga kwa hayo hayo mafuta yake hadi kuwa rangi ya hudhurungi

Katakata Vitunguu na nyanya weka pembeni

Chukua pilipili boga, thomu, tangawizi na visage katika mashine ya kusagia

Weka sufuria pembeni na utie mafuta, subiri yapate moto

Kisha tia vitunguu na vikaange hadi kuwa hudhurungi na tia nyanya

Kisha mimina mchanganyiko wako ulio usaga wa pilipili boga, thomu na tangawizi

Koroga kwa dakika kadhaa Kisha mininia nyama uliyokuwa tayari, maji kiasi na chumvi wastani na subiri maji hayo yachemke

Weka mchele humo na koroga kiasi na onja chumvi kama ipo sawa au kama ndogo unaweza kuongeza

Funika na punguza moto na uache uive taratibu

Baada ya kukauka maji kabisa basi ugeuze na subiri tena kwa dakika kama mbili na tayari kuliwa.

Mapishi ya Biriani la nyama ya ng’ombe

Mahitaji

Nyama ya ng’ombe (beef 1/2 kilo)
Mchele (rice 1/2 kilo)
Vitunguu (onion 2)
Viazi (potato 2)
Vitunguu swaum (garlic 3 cloves)
Tangawizi (ginger)
Nyanya ya kopo (tomato 1/2 ya tin)
Curry powder (1/2 kijiko cha chai)
Binzari nyembamba ya kusaga (cumin 1/2 kijiko cha chai)
Binzari manjano (tarmaric 1/2 kijiko cha chai)
Mafuta (vegetable oil)
Chumvi (salt)
Rangi ya chakula (food colour)
Giligilani (fresh coriander)
Maziwa ya mgando (yogurt kikombe 1 cha chai)
Hiliki nzima (cardamon 3cloves)
Karafuu (clove 3)
Pilipili mtama nzima (black pepper 5)
Amdalasini (cinamon stick 1)

Matayarisho

Katakata nyama kisha ioshe na uiweke kwenye sufuria kisha tia kitunguu swaum, tangawizi, nyanya, curry powder, binzari zote, chumvi na maziwa ya mgando kisha bandika jikoni ichemke mpaka nyama iive na mchuzi ubakie kidogo.Baada ya hapo kaanga viazi na uweke pembeni, kisha kaanga vitunguu na mafuta mpaka viwe ya brown na kisha uvitie viazi vitunguu, na mafuta yake katika nyama. Koroga na uache uchemke kidogo kisha ipua na utie fresh coriander iliyokatwa na hapo mchuzi wako utakuwa tayari.
Baada ya hapo loweka mchele wako kwa muda wa dakika 10, kisha chemsha maji yatie chumvi, hiliki, karafuu, pilipili mtama na abdalasin na mafuta. Yakisha chemka tia mchele na uache uchemke mpaka ukauke maji yakisha kauka tia rangi ya chakula na uanze kugeuza ili ichanganyike na wali wote. Baada ya hapo ufunike na uache mpaka uive. Na baada ya hapo biriani litakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika Mseto Kwa Mchuzi Wa Samaki Wa Nazi

Vipimo vya mseto

Tanbihi: Kiasi ya vipimo inategemea wingi wa watu, unaweza kupunguza au kuongeza. Hiki ni kiasi cha watu 6 takriban.

Chooko – 3 Vikombe

Mchele – 2 Vikombe

Samli – 2 vijiko Vya supu

Chumvi – kiasi

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Safisha na kosha chooko utoe taka taka zote.
Osha mchele kisha roweka pamoja na chooko kwa muda wa saa au zaidi.
Pika chooko na mchele ukiongeza maji inapohitajika, tia chumvi, funika pika moto mdogo mdogo huku unakoroga kwa mwiko kila baada ya muda huku unaponda ponda.
Karibu na kuwiva na kupondeka tia samli endelea kupika hadi karibu na kukauka. Epua.

Samaki

Vipande vya samaki (nguru) – 6 – 7 (4LB)

Kitunguu saumu na tangawizi iliyosagwa – 2 vijiko vya supu

Pilipili ya unga nyekundu – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa ukipenda – 1 kijiko cha chai

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Ndimu – kiasi

Mafuta ya kukaangia – kiasi

Namna Ya Kutaysha Na Kupika

Changanya thomu/tangawizi, pilipili, bizari, chumvi pamoja na ndimu iwe masala nzito.
Paka vipande vya nguru kwa masala hayo weka akolee dakika kumi hivi.
Kaanga vipande vya nguru katika mafuta madogo kwenye kikaango (fyring pan) uweke upande.

Mchuzi Wa Nazi

Vitunguu maji – katakata vidogodogo – 4

Nyanya zilizosagwa (crushed) – 3- 4

Nyanya kopo – 1 kijiko cha chai

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Bizari ya mchuzi – 1 kijiko cha chai

Bamia zilizokatwa ndogo ndogo – 2 vikombe

Chumvi – kiasi

Ndimu – 2 vijiko vya supu

Tui la nazi – 3 Vikombe au 800 ml

Namna Ya Kupika

Katika karai au sufuria, tia mafuta ukaange vitunguu hadi vianze kugeuka rangi.
Tia nyanya zilizosagwa, nyanya kopo, uendelee kukaanga, kisha tia bizari, chumvi.
Tia nazi na mwisho tia bamia uache ziwive kidogo tu.
Tia vipande vya samaki vilivyokwisha kaangwa.
Tayari kuliwa na mseto upendavyo.

Vidokezo:

Bizari nzuri kutumia ni ya ‘Simba Mbili’ inaleta ladha nzuri katika mchuzi.
Ni bora kupika mchuzi kwanza kabla ya mseto kwani mseto ukikaa kwa muda unazidi kukauka.

Mapishi ya Bokoboko La Kuku

Mahitaji

Ngano nzima (shayiri) – 3 Vikombe

Kuku – ½ (3 LB takriban)

Thomu na tangawizi iliyosagwa – 1 kijko cha supu

Pilipili manga ya unga – ½ kijiko cha chai

Jiyrah (cumin/bizari ya pilau) – ½ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Kidonge cha supu – 1

Samli ya moto – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Roweka ngano (shayiri) tokea usiku au muda wa masaa.
Katakata kuku mtie katika sufuria, tia maji kiasi viungo vyote. Mchemeshe awive na ibakie supu yake.
Toa kuku, toa mifupa na umchambue chambue vipande vidogo vidogo.
Chemisha ngano (shayiri) kwa kufunika sufuria hadi iwive na kukauka maji.
Tia supu ya kuku katika ngano (shayiri), na kuku uliyemechambua. Tia kidonge cha supu.
Tia samli nusu (bakisha nusu) kisha songa mchanganyiko uchanganye hadi ivurugike kuku na ngano (shayiri) vizuri.
Mimina katika sahani, mwagia samli imoto ilyobakia likiwa tayari.

Mapishi ya Pilau Ya Nafaka Na Nyama Ya Kusaga

VIAMBAUPISHI

Mchele – 3 vikombe

Nyama ya kusaga – 1 LB

Mchanganyiko wa Nafaka upendazo; maharagwe, njegere, mbaazi n.k 1 mug

Vitunguu maji kata vipande vipande – 3 vya kiasi

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi – 2 vijiko vya supu

Mafuta – ½ Kikombe

Mchanganyiko wa bizari (Garam Masala) – 2 vijiko vya chai

Vipande vya supu (Maggi cubes) – 3

Maji (inategemea mchele) – 5

Chumvi – Kiasi

MAPISHI

Osha mchele na roweka.
Weka mafuta katika sufuria na kaanga vitunguu mpaka viwe brown.
Tia Thomu na tangawizi, kaanga kidogo.
Weka nyama ya kusaga, chumvi na garam masala, endelea kukaanga mpaka nyama iwive.
Mwaga maji yaliomo katika kopo la nafaka na utie nafaka pekee humo.
Tia maji na vipande vya supu (Maggi cubes) huku unavivuruga, koroga kidogo.
Tia mchele, koroga kidogo.
Funika na pika kwa moto mdogo mpaka karibu na kukauka ukikorogoka kidogo. (kama unavyopika pilau ya kawaida)
*Epua uipike katika moto wa oven 350-400 Deg kwa muda wa dakika 15.
*Kama sufuria uliyotumia sio ya kupikia katika oven, mimina katika chombo chochote kinachotumika kwa oven kama bakuli la pyrex au treya za foil.
Pakua katika sahani na iko tayari kuliwa.

Kupima lishe au afya ya mtu

Njia za kupima Afya

Njia mbalimbali hutumika kupima hali ya lishe, njia hizi ni;

1. Vipimo vya umbile la mwili

2. Vipimo vya maabara

3. Kuchukua historia ya ulaji na maradhi

Vipimo vya umbile la mwili

Baadhi ya vipimo ambavyo vinaweza kutumika kutoa tahadhari kuhusu magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza ni;

1. Uwiano wa uzito na urefu au Body Mass Index (BMI).

2. Mzunguko wa kiuno.

3. Uwiano wa mzunguko wa kiuno na nyonga.

4. Kulinganisha uzito na umri.

Uwiano wa uzito na urefu au Body Mass Index (BMI).

Hiki ni kipimo kinachotumika kuangalia uwiano wa urefu na uzito wa mtu, ni muhimu kuchukua vipimo kwa usahihi.Uwiano wa uzito katika Kilogramu na urefu katika mita hupatikana kwa kutumia kanuni ifuatayo:

BMI= uzito (Kg)/Urefu2 (m2)

BMI huwa na viwango mbalimbali vilivyowekwa na shirika la Afya duniani (WHO) kutafsiri hali ya lishe ya mtu ambavyo ni

1. BMI chini ya 18.5 = uzito pungufu.

2. BMI kati ya 18.5 mpaka 24.9= uzito unaofaa.

3. BMI kati ya 25.0 mpaka 29.9 = unene uliozidi.

4. BMI ya 30 au zaidi = unene uliokithiri au kiribatumbo.

Mahitaji ya chakula mwilini hutegemea umri, jinsi, hali ya kifiziolojia (kama ujauzito na kunyonyesha), hali ya kiafya, kazi na mtindo wa maisha. Uzito wa mwili hutegemea na chakula unachokula, pamoja na shughuli unazofanya, mara nyingi unene hutokana na kula chakula kwa wingi.
Unene uliokithiri unachangia kwa kiwango kikubwa kupata magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, magonjwa ya moyo, shinikizo kubwa la damu, na saratani. Uzito uliozidi unapaswa kupunguzwa ili kuepuka magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza

Jinsi ya kupunguza unene uliozidi

1. Tumia mafuta kwa kiasi kidogo kwenye chakula

2. Epuka kula vyakula vyenye mafuta mengi hususani vinavyopikwa kwa kudumbukizwa kwenye mafuta, au vinavyokaangwa kwa mafuta mengi.

3. Epuka matumizi ya vinywaji au vyakula venye sukari nyingi

4. Epuka asusa zenye mafuta mengi au sukari nyingi kati ya mlo na mlo.

5. Ongeza vyakula venye makapi- mlo kwa wingi kama matunda, mboga mboga na nafaka zisizokobolewa.

BMI haitumiki kwa wanawake wajawazito, BMI haitumiki kwa watoto na vijana walio na umri chini ya miaka 18, BMI haitumiki kwa watu wasioweza kusimama vyema, waliovimba miguu, na wanawake wanaonyonyesha katika miezi sita ya mwanzo baada ya kujifungua.

Mapishi ya Viazi vitamu na kachumbari

Mahitaji

Viazi utamu 3
Nyanya 2 kubwa
Kitunguu
Tango
Limao
Chumvi
Pilipili
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Menya viazi na kisha vikate katika vipande. Tia mafuta kwenye chuma cha kukaangia, yakisha pata moto tia viazi nauviache vikaangike mpaka upande mmoja uwe wa brown na kisha geuza upande wa pili na upike mpaka uwe wa brown. Vikisha iva ipua na uweke kwenye kitchen towel ili vikauke mafuta.
Kachumbali: Katakata vitunguu katika bakuli na kisha tia chumvi kwa ajili ya kuondoa ukali wa vitunguu. Baada ya hapo vioshe mpaka chumvi yote iishe. osha nyanya, Pilipili tango na kisha katakata slice nyembamba na uchanganye na vitunguu. Baada ya hapo tia chumvi, kamulia limao na uchanganye zote pamoja .Baada ya hapo viazi na kachumbali vitakuwa tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About