Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Pilau Ya Nyama Ng’ombe Karoti Na Zabibu

Vipimo – Nyama

Nyama ng’ombe ya mifupa ilokatwa vipande – 1 kilo

Tangawizi na thomu (somu/garlic) ilosagwa – 2 vijiko vya supu

Bizari mchanganyiko/garama masala – 1 kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Vipimo – Wali

Mchele – 4 glass

Mbatata/viazi menya katakata – 3 kubwa

Vitunguu katakata – 5

Kitunguu thomu kilosagwa (garlic/somu) – 1 kijiko cha supu

Hiliki ya unga – 1 kijiko cha chai

Bizari nzima ya pilau/cumin – 1 mti

Samli au mafuta – 2 Vijiko vya supu

Karoti zilokatwakatwa nyembamba – 6-7

Zabibu – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katika sufuria weka mafuta kijiko kimoja cha supu tia nyama na viungo vyake.
kaushe katika moto hadi ikaribie kukauka kisha tia maji kiasi cha kuivisha na kubakisha supu ya mchele.
Katika sufuria ya kupikia weka samli au mafuta ishike moto.
Tia mbatata/viazi kaanga, tia vitunguu kaanga kidogo.
Tia kitunguu thomu, hiliki, bizari ya pilau endelea kukaanga hadi viwe rangi ya brown kidogo.
Tia mchele kaanga kidogo, kisha mimina nyama na supu yake. Funika wali uwive.
Weka kikaangio katika moto, tia samli kijiko kimoja kisha tia karoti na zabibu, kaanga kwa sekunde chache tu kwa ajili ya kulainisha karoti na zabibu.
Utakapopakuwa wali, pambia juu karoti na zabibu.

Mapishi ya choroko

Mahitaji

Choroko kikombe 1 na nusu
Nazi kopo 1
Kitunguu kikubwa 1
Nyanya 1/2 kopo
Swaum 1 kijiko cha chai
Curry powder 1 kijiko cha chai
Chumvi kiasi
Olive oil
Pilipili nzima

Matayarisho

Loweka choroko usiku mzima kisha zichemshe mpaka ziive na ziweke pembeni. Baada ya hapo saga pamoja nyanya, kitunguu, na swaum kisha vipike mpaka maji yote, baada ya hapo tia mafuta na curry powder, pika mpaka nyanya zitoe mafuta kisha tia choroko,tui la nazi, maji nusu kikombe,pilipili na chumvi, kisha koroga vizuri na uache ichemke. Pika mpaka tui la nazi litakapoiva na rojo ibakie kidogo sana, kisha ipua na mboga yako itakuwa tayari kwa kuliwa. Mi huwa napenda kuila na wali ila hata na ugali au chapati inaenda pia.

Mapishi ya Biriani Nyepesi Kupika Ya Samaki

Vipimo

Mchele wa pishori (basmati) – 4

Vitunguu katakata – 3

Nyanya (tungule) katakata vipande vikubwa – 3 -5

Pilipili boga la kijani (capsicum) katakata

Supu ya kitoweo au vidonge vya supu – 1

Bizari mchanganyiko Garama masala – 5-7

Pilipili mbichi ya kusaga – Kiasi

Zaafarani ya maji (flavor) – 1 kijiko cha chakula

Mafuta ya kupikia – ¼ kikombe

Samaki wa kukaanga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Roweka mchele kiasi nusu saa kisha chemsha mchele kwa supu uive nusu kiini. Mwaga maji chuja.
Wakati mchele unapikika, weka mafuta katika sufuria kubwa ya kupikia wali, kaanga vitunguu mpaka vigeuke rangi ya hudhurungi.
Tia nyanya na vitu vinginevyo vyote kaanga kidogo tu.
Mwaga wali katika sufuria na nyunyizia zaafarani kisha changanya na masala vizuri.
Funika upike katika oven (bake) au juu ya stovu moto mdogo mdogo kiasi dakika 15- 20.
Epua ikiwa tayari, pakua kwenye sahani kisha tolea kwa samaki wa kukaanga.

Mapishi ya Tende Ya Kusonga Ya Lozi Na Cornflakes

VIAMBAUPISHI

Tende zilizotolewa kokwa – 1 Kilo

Cornflakes – 1 ½ kikombe

Lozi Zilokatwa katwa – 1 kikombe

Siagi – ¼ kilo

MANDALIZI

Mimina tende na siagi kwenye sufuria bandika motoni moto mdogo mdogo mpaka zilainike. Kwa muda wa dakika 10.
Isonge kidogo kwa mwiko au kuikoroga ichanganyike vizuri.
Changanya Cornflakes na lozi kwenye tende mpaka zichanganyika vizuri.
Pakaza treya au sinia mafuta au siagi kidogo.
Mimina mchanganyiko wa tende, zitandaze vizuri na ukate vipande saizi unayopenda. Zikiwa tayari kuliwa kwa kahawa.

Jinsi ya kupika Biskuti Za Ufuta Na Jam

Viamba upishi

Unga 2 Viwili

Sukari ya kusaga 1/4 Kikombe

Siagi 250 gms

Jam kisia

Ufuta Kisia

Vanilla 1 kijiko cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Tia kwenye mashine ya kusaga (blender) au mashine ya keki, siagi, yai, sukari na vanilla uchanganye hadi ichanganyike vizuri.

2. Tia baking powder, na unga na changanya kwa mkono vizuri.

3. Paka siagi sinia ya kupikia ya oveni.

4. Tengeneza viduara vidogo vidogo.

5. Bonyeza kila kiduara katikati kwa kidole, kisha weka jam, halafu juu yake paka mayai na unynyuzie ufuta.

6. Pika katika moto wa chini 350ºF kwa muda wa dakika 20-25.

7. Tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya wali kuku wa Kisomali

Mahitaji ya wali

Mchele – 3 vikombe

Vitunguu (viliokatwa vidogo vidogo) – 2

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 kijiko cha chai

Bizari ya pilau – 1 kijiko cha supu

Mdalasini – 1 kijiti

Hiliki – 3 chembe

Pilipili manga nzima – chembe chache

Siagi – Vijiko 2 vya supu

Chumvi – kiasi

Mahitaji kwa kuku

Kuku kidari (Breast) kata vipande vipande – 2 LB

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Kotmiri iliyokatwa ndogo ndogo – kiasi

Bizari ya pilau (cummin au jiyrah) – 1 kijiko cha chai

Pilipili kubwa tamu la kijani – 1

Pilipili kubwa tamu nyekundu – 1

(zikate vipande vipande)

Karoti iliyokunwa – 1 – 2

Chumvi – Kiasi

Mapishi ya Wali:

Roweka mchele kwa muda fulani kutegemea mchele
Katika sufuria tia mafuta na kaanga vitunguu hadi vibadilike rangi kidogo.
Tia thomu iliyosagwa, mdalasini, bizari ya pilau, hiliki, pilipili manga na chumvi, kaanga kidogo.
Tia mchele kaanga kidogo, kisha tia maji ya moto kiasi kutegemea na aina ya mchele kama kawaida ya kupika wali kama pilau.
Tia sigai, funika upikike wali hadi uwive.

Mapishi ya Kuku:

Mchanganye kuku pamoja na thomu/tangawizi iliyosagwa, chumvi, pilipili mbichi.
Katika karai tia mafuta yapate moto vizuri.
Mtie kuku, bizari ya pilau (jiyrah) na ukaange, karibu na kuiva tia vitunguu.
Tia mapilipili makubwa, kotmiri, na kaanga kwa dakika moja tu uzime moto na epua weka kando.

JINSI YA KUANDAA VILEJA

MAHITAJI

Unga wa mchele – 500g

Samli – 250g

Sukari – 250g

Hiliki iliyosagwa – 1/2 kijiko cha chai

Arki (rose flavour) – 1/2 kijiko cha chai

Baking powder – 1 kijiko cha chai

Mayai – 4

Maji ya baridi – 1/2 kikombe cha chai

MAANDALIZI

Saga sukari iwe laini kiasi, changanya unga wa mchele, baking powder, hiliki na sukari.
Pasha moto samli mpaka iwe nyepesi kama maji mimina kwenye ule mchanganyiko wa unga wa mchele, kisha uchanganye pamoja na arki.
Ongeza mayai yaliopigwa endelea kuchanganya mpaka unga umeanza kuchanganyika vizuri.
Ongeza maji ya baridi sana kama nusu kikombe tu ili uchanganyike vizuri.
Kata kwa design unayotaka viwe vinene visiwe kama cookies za kawaida kama ilivyo kwenye picha na ukipenda utaweka kidoto kwa kutumia zaafarani katikati ya kileja kama inavyoonesha hapo juu.
Choma kwa moto wa baina ya 300F na 350F kwa dakika 15 mpaka 20 visiwe vyekundu toa na tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Wali Wa Karoti Na Kuku Wa Kukaanga

Vipimo Vya Wali

Mchele wa Basmati/Pishori – 1 kilo moja

Vitunguu maji – 3

Karoti – 2

Siagi – 3 vijiko vya supu

Kidonge cha supu (stock) – 1 kimoja

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Ósha mchele uroweke kama saa moja au mbili
Katakata vitunguu vipande vidogodogo (chopped) weka kando.
Kwaruza karoti (grate) weka kando.
Tia siagi katika sufuria ya kupikia wali, weka katika moto iyayuke
Kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi kiasi tu.
Tia maji kiasi ya kupikia wali, changanya na kidonge cha supu.
Yakichemka tia mchele, koroga, funika uweke moto mdogo mdogo.
Kabla ya maji kukauka tia karoti changanya wali kisha funika uive kama unavyopika pilau.

Vipimo Vya Kuku Wa Kukaanga

Kuku alokatwakatwa – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi ilosagwa – 2 vijiko vya supu

Bizari ya mchanganyiko/garam masala – kijiko cha supu

Mtindi/Yoghurt – 1 kijiko cha supu

Ndimu – 1

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kukaangia – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Ukishamuosha kuku, mchuje atoke maji yote.
Changanya viungo vyote katika kibakuli kidogo.
Changanya pamoja na kuku kisha acha akolee viungo (marinate) kwa muda wa masaa mawili takriban.
Weka mafuta katika karai na kaanga kuku, akiwiva yu tayari kuliwa na wali.

UNYONYESHAJI BORA WA MAZIWA YA MAMA

• Maziwa ya mama pekee ndio chakula na kinywaji cha mtoto bora zaidi kwa watoto kwa miezi sita ya kwanza.
• Ni jambo la muhimu sana kunyonyesha watoto wachanga kwa muda wa miezi minne na uendelee kunyonyesha hadi mtoto atakapofikisha mwaka mmoja na kuendelea.

• Mtoto akifikisha miezi sita ndio wakati muafaka wa kumpa vyakula vya nyongeza vilivyotayarishwakatika hali ya usafi.

• Onana na mnasihi akushauri kuhusu muda na jinsi ya kumuanzishia mtoto wako vyakula vya nyongeza

• Vyakula vya ngogeza viwe ni vya mchanganyiko wa makundi yafuatayo ya chakula:- vyakula vya nafaka, venye asili ya nyama, mbogamboga na matunda, mafuta na sukari (kiasi). Lisha kila chakula kwa siku kadhaa kwa kufuatanisha kabla hujaaza chakula chengine kipya.

• Usimuachilie mtoto alale kama chupa ya maziwa ingali mdomoni, ili kuepukana na kuoza kwa meno na madhara ya.

• Watoto wanaopewa maziwa ya mama pekee hawaugui mara kwa mara, na wakiugua, makali ya ugonjwa hupungua na hupona mapema kwa sababu yale maziwa ya mwanzo ya njano yenye viini vingi vya kumkinga dhidi ya magonjwa.

Jinsi ya kupika Cookies Za Jam Ya Peach Na Raspberry

MAHITAJI

Unga kikombe 1 ½

Siagi ½ kikombe

Sukari ½ kikombe

Yai 1

Vanilla 1 kijiko cha chai

Jam ya peach na raspberry

MAANDALIZI

Wash oven moto wa takriban 180 – 190 Deg F
Piga siagi na sukari katika mashine mpaka iwe laini na nyororo (creamy) kisha weka yai na vanilla.
Tia unga kidogo kidogo uchanganye kwa mwiko wa mbao (wooden spoon).
Pakaza mkononi unga uchukue vidonge ubonyeze kufanya vishimo vya kuwekea jam.
Panga katika treya uliyopakaza siagi.
Tia nusu yake jam ya peach na nusu jam ya raspberry
Bake katika oven kiasi robo saa mpaka ziwive na kugeuka rangi ya brown light.
Epua vikiwa tayari

Mapishi ya Wali Wa Kichina Wa Kamba Na Kuku

MAHITAJI

Mchele wa pishori (basmati) – 4

Nyama ya kuku bila mafupa – 1 Lb

Kamba saizi kubwa – 1Lb

Mchanganyiko wa mboga – njegere, karoti,

mahindi, maharage ya kijani (spring beans) – 2 vikombe

Figili mwitu (Cellery) – 2 mche

Vitunguu vya majani (spring onions) – 4-5 miche

Kebeji – 2 vikombe

Pilipili ya unga nyekundu – 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ya unga – 1 kijiko cha chai

Sosi ya soya – 3 vijiko vya supu

Mafuta – 1/4 kikombe

Chumvi – kiasi

MAPISHI

Osha na roweka mchele.
Tia kamba chumvi na pilipili nyekundu ya unga. Tia mafuta vijiko viwili katika kikaango (frying pan), kaanga kamba kidogo tu, weka kando.
Katakata kuku vipande vidogo vidogo, tia chumvi na pilipili manga. Kaanga kaTika kikaango (ongeza mafuta kidogo) Weka kando.
Katika karai, tia mafuta kidogo kama vijiko vitatu vya supu, tia kamba na kuku, tia mboga za mchanganyiko, sosi ya soya na chumvi, kaanga kidogo. (Kama mboga sio za barafu) itabidi uchemshe kidogo.
Katakata kebeji, figili mwitu (cellery) na vitunguu vya majani (spring onions) utie katika mchaganyiko. acha kwa muda wa chini ya dakika moja katika moto.
Chemsha mchele, tia mafuta kidogo au siagi, chumvi upikie uive nusu kiini, mwaga maji uchuje.
Changanya vyote na wali rudisha katika sufuria au bakuli la oveni, funika na upike kwa moto wa kiasi kwa muda wa dakika 15-20 takriban.
Epua na upakue katika sahani ukiwa tayari kuliwa.

Jinsi ya kutengeneza Fagi Ya Kumumunyuka Mdomoni

VIAMBAUPISHI

Maziwa mazito matamu (condensed milk) – 2 vibati

Sukari – 1 kikombe

Samli 1 ½ kikombe

Vanilla 2 kifuniko cha chupa yake

Hiliki ilosagwa – 2 vijiko vya chai

Sinia kubwa ya bati Paka samli

MAANDALIZI

Changanya maziwa, sukari na samli katika sufuria isiyogandisha chakula (non-stick) uweke katika moto.
Koroga huku ikipikika hadi ianze kugeuka rangi na kuanza kuachana. Usiache mkono kuroga isije kufanya madonge.
Tia hiliki na vanilla, endelea kuipika.
Itakapogeuka rangi vizuri mimina katika sinia na haraka uitandaze kwa mwiko huku ukiuchovya katika maji na kuendelea kuitandaza hadi ikae sawa kote.
Pitisha kisu kuikataka ili ikipoa iwe wepesi kuitoa vipande.

Kila inapozidi kupoa na kukaa ndipo fagi inakauka na kumumunyuka.

Mapishi ya wali wa Kiafrika Mangaribi

Mahitaji

Mchele (rice vikombe 2 na 1/2)
Vitunguu (onion 2)
Nyanya ya kopo (tin tomato kopo 1)
Tangawizi (ginger paste kijiko 1 cha chakula)
Kitunguu swaum (garlic paste kijiko 1 cha chakula)
Paprika (kijiko 1 na 1/2 cha cha chai)
Pilipil (scotch bonnet pepper 1)
Curry powder (kijiko 1 cha chai)
Maggi cubes 3(unaweza kutumia yenye ladha ya chicken, beef au vegetable. Inategemea unasevu na mchuzi wa aina gani)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Loweka mchele kwa muda wa dakika 10.Katakata vitunguu kisha weka pembeni, saga pamoja nyanya ya kopo,pilipili, tangawizi na kitunguu swaum kisha weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu vikiiva tia curry powder, maggi cubes, chumvi na paprika na uchanganye vizuri. Kisha tia mchanganyiko wa nyanya na uupike mpaka uive. Baada ya hapo tia mchele na maji na uupike mpaka ukaribie kuiva kisha ugeuze na umalizie kwa kutia njegere na umalizie kuupika mpaka uive. baada ya hapo utakuwa tayari kuseviwa na mboga yoyote kama kuku, nyama, samaki au assorted meat (Mchanganyiko wa utumbo, makongoro na nyama), Hapo mimi nili-save na mchuzi wa kuku wa kienyeji.

Mapishi ya Haliym Ya Nyama Mbuzi -Bokoboko La Pakistan

Mahitaji

Nyama ya mbuzi au ng’ombe ya mafupa – 2 LB

Mchanganyiko wa dengu (hadesi, mchele, chooko, ngano, dengu n.k au nunua ya tayari iliyokwisha changanywa – 2 Vikombe

Kitungu maji (vikate vidogo) – 1

Mafuta – ¼ Kikombe

Nyana kata ndogo ndogo – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawazi iliyosagwa – 1 Kijiko cha supu

Bizari ya haliym – 2 vijiko vya supu

Nyanya ya kopo – 2 vijiko vya supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chemsha nyama na chumvi ½ kijiko mpaka iive, toa mafupa.
Chemsha mchanganyiko wa dengu mpaka ziive.
Katika sufuria weka mafuta, kaanga vitunguu vilainike, tia thomu na tangawizi, bizari ya haliym, nyanya ya kopo. Kaanga mpaka iwive.
Tia nyama iliyowiva na supu yake kidogo.
Tia mchanganyiko wa dengu tia kwenye mashine ya kusaga (blender), saga na ile supu ya nyama isagike vizuri
Mimina kwenye sufuria changanya, tia ndimu kidogo, acha moto mdogo mdogo kwa muda wa dakika 15.
Tia katika bakuli, pambia kwa vitunguu vilivyokaangwa vya rangi ya hudhurungi vikavu, pilipili mbichi (ukipenda) na kotmiri, ikiwa kuliwa.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About