Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Wali Wa Kichina Wa Kamba Na Kuku

MAHITAJI

Mchele wa pishori (basmati) – 4

Nyama ya kuku bila mafupa – 1 Lb

Kamba saizi kubwa – 1Lb

Mchanganyiko wa mboga – njegere, karoti,

mahindi, maharage ya kijani (spring beans) – 2 vikombe

Figili mwitu (Cellery) – 2 mche

Vitunguu vya majani (spring onions) – 4-5 miche

Kebeji – 2 vikombe

Pilipili ya unga nyekundu – 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ya unga – 1 kijiko cha chai

Sosi ya soya – 3 vijiko vya supu

Mafuta – 1/4 kikombe

Chumvi – kiasi

MAPISHI

Osha na roweka mchele.
Tia kamba chumvi na pilipili nyekundu ya unga. Tia mafuta vijiko viwili katika kikaango (frying pan), kaanga kamba kidogo tu, weka kando.
Katakata kuku vipande vidogo vidogo, tia chumvi na pilipili manga. Kaanga kaTika kikaango (ongeza mafuta kidogo) Weka kando.
Katika karai, tia mafuta kidogo kama vijiko vitatu vya supu, tia kamba na kuku, tia mboga za mchanganyiko, sosi ya soya na chumvi, kaanga kidogo. (Kama mboga sio za barafu) itabidi uchemshe kidogo.
Katakata kebeji, figili mwitu (cellery) na vitunguu vya majani (spring onions) utie katika mchaganyiko. acha kwa muda wa chini ya dakika moja katika moto.
Chemsha mchele, tia mafuta kidogo au siagi, chumvi upikie uive nusu kiini, mwaga maji uchuje.
Changanya vyote na wali rudisha katika sufuria au bakuli la oveni, funika na upike kwa moto wa kiasi kwa muda wa dakika 15-20 takriban.
Epua na upakue katika sahani ukiwa tayari kuliwa.

Mapishi ya Pilau Ya Nyama Ya Ng’ombe Na Nyanya

Vipimo

Mchele (Basmati) – 3 vikombe

Nyama ya ngo’mbe – 1 kg

Pilipili boga – 1 kubwa

Nyanya – 2 kubwa

Vitunguu maji – 2 vikubwa

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Tangawizi – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 1

Mafuta ya kupikia – ½ kikombe

Mdalasini – ½ kijiko cha chai

Binzari nyembamba – 1 kijiko cha chai

Pilipili manga – ½ Kijiko cha chai

Hiliki – ½ Kijiko cha chai

Namna ya kutayarisha na Kupika

Roweka mchele wako katika chombo

Chukuwa nyama na ioshe vizuri na itie thomu, tangawizi, ndimu, pilipili manga na chumvi kiasi

Iweke jikoni hadi ikauke maji na kuwa imewiva huku ukiikaanga kaanga kwa hayo hayo mafuta yake hadi kuwa rangi ya hudhurungi

Katakata Vitunguu na nyanya weka pembeni

Chukua pilipili boga, thomu, tangawizi na visage katika mashine ya kusagia

Weka sufuria pembeni na utie mafuta, subiri yapate moto

Kisha tia vitunguu na vikaange hadi kuwa hudhurungi na tia nyanya

Kisha mimina mchanganyiko wako ulio usaga wa pilipili boga, thomu na tangawizi

Koroga kwa dakika kadhaa Kisha mininia nyama uliyokuwa tayari, maji kiasi na chumvi wastani na subiri maji hayo yachemke

Weka mchele humo na koroga kiasi na onja chumvi kama ipo sawa au kama ndogo unaweza kuongeza

Funika na punguza moto na uache uive taratibu

Baada ya kukauka maji kabisa basi ugeuze na subiri tena kwa dakika kama mbili na tayari kuliwa.

Mapishi ya Bokoboko La Kuku

Mahitaji

Ngano nzima (shayiri) – 3 Vikombe

Kuku – ½ (3 LB takriban)

Thomu na tangawizi iliyosagwa – 1 kijko cha supu

Pilipili manga ya unga – ½ kijiko cha chai

Jiyrah (cumin/bizari ya pilau) – ½ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Kidonge cha supu – 1

Samli ya moto – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Roweka ngano (shayiri) tokea usiku au muda wa masaa.
Katakata kuku mtie katika sufuria, tia maji kiasi viungo vyote. Mchemeshe awive na ibakie supu yake.
Toa kuku, toa mifupa na umchambue chambue vipande vidogo vidogo.
Chemisha ngano (shayiri) kwa kufunika sufuria hadi iwive na kukauka maji.
Tia supu ya kuku katika ngano (shayiri), na kuku uliyemechambua. Tia kidonge cha supu.
Tia samli nusu (bakisha nusu) kisha songa mchanganyiko uchanganye hadi ivurugike kuku na ngano (shayiri) vizuri.
Mimina katika sahani, mwagia samli imoto ilyobakia likiwa tayari.

Jinsi ya kutengeneza Nangatai

MAHITAJI

Unga wa ngano – 2 – 2 ¼ Vikombe

Siagi – 1 ½ Kikombe

Sukari – 1 Kikombe

Yai – 1

Vanilla -Tone moja

Baking Powder -kijiko 1 cha chai

Chumvi – Kiasi kidogo (pinch)

Unga wa Kastadi – 2 Vijiko vya supu

MATAYARISHO

Changanya vitu vyote isipokuwa unga.
Tia unga kidogo kidogo mpaka mchanganyiko uwe sawa.
Kisha fanya duara ndogo ndogo uzipange kwenye treya na utie rangi katikati.
Halafu zichome katika moto wa 300°F kwa muda wa dakika 20 – 25 na zisiwe browni .
Kisha panga kwenye sahani tayari kuliwa na chai.

Mapishi – Kisamvu cha Karanga

Mapishi yetu leo ni kisamvu cha kuchanganya na karanga. Karibu.

Mahitaji

Majani ya kisamvu
Karanga nusu kikombe
kitunguu kimoja
nyanya mbili
karoti moja
mafuta na chumvi kiasi

Matayarisho

1. Osha kisamvu chako vizuri kisha katakata vipande vidogo vidogo

2. Unaweza kutwanga kwa kutumia kinu au kuchemsha kidogo na kisha kusaga kwa kutumia mashine. Ukitumia mashine uwe makini usije ukasaga sana ukaharibu.

3. Kaanga karanga kidogo na kisha zisage ziwe unga unga.

4. Chemsha kisamvu chako hadi kiive.

5. Katakata kitunguu, karoti na na nyanya

6. Anza kuunga kisamvu kwa kukaanga vitunguu, weka karoti na kisha nyanya na vikishaiva weka kisamvu na koroga pamoja kisha weka karanga. Acha vichemke kwa muda na unaweza pia weka na nazi tui la kwanza.

7. Baada ya muda mfupi epua na kitakiwa tayari. Waweza kula kwa ugali, wali, chapati, makande n.k

Mapishi ya Maini ya ng’ombe

Mahitaji

Maini (Cow liver) 1/4 kilo
Vitunguu (chopped onion) 2
Nyanya (chopped tomato) 1
Kitunguu swaum/tangawizi (ginger /garlic paste) 1 kijiko cha chai
Mafuta ya kupikia
Chumvi
Coriander
Curry powder 1 kijiko cha chai
Limao (lemon) 1/4
Pilipili (scotch bonnet ) 1

Matayarisho

Safisha maini na ukate vipande vidogovidogo na uweke pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu kidogo(visiwe vya brown) kisha tia ginger/ garlic paste,carry powder kaanga kidogo kisha tia nyanya. Kaanga nyanya mpaka zitoe mafuta kisha tia chumvi, pilipili na vimaji kidogo. Acha vichemke kidogo kisha tia maini na uyapike mpaka yaive. Malizia kwa kukamulia limao na kutia coriander kisha ipua na hapo yatakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kutengeneza Bisikuti Za Kaukau Na Kahawa (Cocoa Coffee Biscuits)

MAHITAJI

Maji baridi – kikombe 1

Biskuti za kawaida – paketi 2

Kaukau (cocoa) – vijiko 3 vya kulia

Kahawa ya unga – kijiko 1 cha kulia

Njugu mchanganyiko zilokatwakatwa – kikombe 1

Sukari – kiasi upendavyo

MAANDALIZI

Changanya maji na kaukau na kofi na sukari
Katakata biskuti kisha tia paketi moja na nusu uchanganye vizuri.
Kisha nusu ya biskuti zilobakia katakata vipande vikubwa na weka juu ya mchanganyiko, kisha changanya kidogo tu.
Weka katika foil paper na zungusha (roll)
Kisha fungua umwagie njugu au mkassaraat zilosagwa
Kisha roll katika foil paper na uweke katika freezer mpaka igande
Kisha kata kata slices na iko tayari

Mapishi ya Biriyani Ya Kuku

Vipimo

Mrowanishe kuku na viungo hivi kwa muda mdogo tu

Kuku (Mkate kate Vipande) – 4 LB

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi – 2 Vijiko vya supu

Chumvi – kiasi

Pilipili nyekundu ya unga – 1 Kijiko cha supu

Bizari ya manjano (Haldi au Tumeric) – 1 Kijiko cha chai

Bizari ya pilau ya powder (Jeera) – 1 Kijiko cha chai

Gilgilani powder (Dania) – 1 Kijiko cha chai

Ndimu – 1 Kijiko cha supu

Mchele na vitu vya Masala:

Mchele (Basmati mzuri) (rowanisha) – 7 cups

Mafuta ya kupikia – kiasi

Vitunguu Vilivyokatwa – 8

Nyanya iliyokatwa katwa – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi – 1 Kijiko cha supu

Garam Masala -1 Kijiko cha supu

Hiliki powder – ½ Kijiko cha chai

Tomatoe paste – 1 Kijiko cha supu

Pilipili mbichi zipasue katikati – 4

Chumvi – kiasi

Mtindi – 4 Vijiko vya supu

Kotmiri iliokatwa (Chopped) – ½ Kikombe

Mafuta ya kunyunyuzia katika wali – 3 Vijiko vya supu

Zaafarani au rangi ya biriani – kiasi

Namna Ya Kutaarisha Na Kupika

Weka kuku aliyerowanishwa na viungo vyake katika Foil tray au chombo chocote utakachomwagia wali humo humo na kupikia biriani, kisha mchome (Bake) mpaka awive na awe mkavu kiasi.

Wakati kuku anapikika, kaanga vitunguu katika karai au sufuria mpaka viwe brown na epua nusu yake weka kando.

Punguza mafuta yabakie kiasi tu, ongeza Thomu na tangawizi, na viungo vyote vya hapo juu isipokuwa Mtindi na kotmiri, endelea kukaanga hadi tomatoe zilainike.

Ongeza chumvi, malizia mwisho kwa kutia mtindi, kotmiri na vile vitunguu ulivyoweka kando. Masala yako tayari.

Mwagia masala juu ya kuku uliyekwishmpika changanya vizuri.

Chemsha Mchele uwive nusu, chuja na mwagia juu ya masala.

Nyunyiza mafuta kidogo juu ya mchele na zaafarani au rangi ya biriani.

Bake katika moto wa 350 – 400 kwa muda wa 15 – 20 minutes. Biriyani imekuwa tayari kuliwa.

Mtindi wa kutolea Biriyani:

Mtindi – 1 kikombe

Pilipili mbichi – 1 ndogo

Kitunguu saumu(/galic) thomu – chembe mbili

Nanaa – kiasi

Chumvi – chembe tu

Weka kwenye Blender na uchanganye, kisha mimina katika bakuli

Mapishi ya Bilinganya

Mahitaji

Bilinganya 2 za wastani
Nyanya kubwa 1
Kitunguu maji 1 kikubwa
Swaum 1/2 kijiko cha chai
Limao 1/4
Pilipili ya unga 1/2 kijiko cha chai
Parpika 1/4 kijiko cha chai
Pilipili mtama 1/4 kijiko cha chai
Curry powder1/4 kijiko cha chai
Chumvi kiasi
Coriander
Olive oil

Matayarisho

Katakata bilinganya slice nyembamba kisha ziweke pembeni. Baada ya hapo kaanga kitunguu maji mpaka kiwe cha brown kisha tia swaum na spice zote, zikaange kidogo kisha tia nyanya na chumvi kiasi. Pika nyanya mpaka iive na itengane na mafuta. Baada ya hapo tia mabilinganya na ukamulie limao kisha punguza moto na uyafunike na mfuniko usioruhusu kutoa mvuke ili yaivie na huo mvuke. Baada ya hapo yaonje kama yameiva na malizia kwa kutia fresh coriander na baada ya hapo yatakuwa tayari kwa kuliwa. kwa kawaida mi hupendaga kuyalia na wali na maharage badala ya kachumari kwahiyo nakuwa naitumia hiyo kama kachumbari

Jinsi ya kutengeneza Wali Wa Dengu Kwa Samaki Wa Kukaanga

Mahitaji

Mchele wa basmati – 3 Vikombe

Dengu – 2 vikombe

Viazi – 3 vikubwa

Kitunguu – 2 kubwa

Nyanya – 2

Pilipili mbichi kubwa – 3

Pilipilimanga – ½ kijiko cha chai

Garama Masala (bizari mchanganyiko) -1 kijiko cha chai

Supu ya vidonge (stock cubes) – 2 vidonge

Chumvi – kiasi

Mafuta – ¼ kikombe

Zaafarani – 1 kijiko cha chai

Samaki wa kukaanga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Dengu kama sio za tayari kwenye kopo, roweka na zichemshe hadi ziwive

Maandalizi ya Masala Ya Dengu:

Zaafarani – iroweke katika maji ya dafu dafu (warm) ya chini ya robo kikombe weka kando.
Osha mchele, roweka.
Menya viazi na vitunguu, katakata vitunguu, na nyanya , weka kando.
Katakata viazi vipande vidogo vidogo kwa umbo la mchemraba (cubes).
Katika sufuria tia mafuta yakipata moto, tia viazi ukaange kidogo kwa moto mdogo mdogo hadi kukaribia kuwiva, toa weka kando.
Kaanga vitunguu hadi vigeuka rangi ya hudhurungi isiyokoza (light brown) kisha tia nyanya ukaange kidogo.
Tia vidonge vya supu (stock cubes) uvivuruge katika mchanganyiko, katakata pilipili mbichi kwa urefu tia, uendelee kukakaanga. Tia bizari, chumvi.
Zima moto, changanya dengu na viazi katika mchanganyiko huo.

Mapishi ya Wali:

Chemsha mchele kama kawaida ya kupika wali mweupe, kiini kiwe kimewiva nusu yake.
Chuja maji kisha changanya katika mchanganyiko wa dengu.
Nyunyizia zaafarani, uchanganye wali na mchanganyiko kidogo tu.
Funika acha uive katika mtoto mdogo mdogo au tia katika oveni hadi uive kama kawaida ya kupika wali.
Pakua katiha sahani na tolea na samaki yoyote wa kukaanga.

Jinsi ya kuishi maisha marefu (Mambo ya kuzingatia ili uishi maisha marefu)

Kuishi ukiwa na afya na kuishi maisha marefu kunawezekana kwa kubadili hali ya maisha unayoishi inayoharibu afya yako mfano uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi,kutokufanya mazoezi na kutokula matunda na mbogamboga.

Mambo yanayoweza kukusaidia kuishi maisha marefu ni kama yafuatayo

  1. Kuuandaa mwili kwa maisha marefu kwa kufanya mazoezi
  2. Kuwa makini kutambua na kutibu matatizo ya kiafya
  3. Kuepuka mazingira na kufanya kazi kwa namna au kazi zinazoweza kudhuru maisha yako. Mfano kuendesha gari bila kufuata utaratibu, kutokuvaa vifaa vya kujikinga wakati wa kazi
  4. Epuka vitu vyenye sumu vinavyoweza kudhuru afya yako na kukuletea matatizo ya kiafya kama dawa za mimea na mifugo, zitumie kama inavyotakiwa
  5. Usinywe pombe, usivute sigara wala kutumia dawa za kulevya
  6. Kula mlo kamili
  7. Usile vyakula vyenye chumvi na mafuta mengi
  8. Kunywa maji mengi ili kusafisha mwili
  9. Epuka msongo wa mawazo

Jinsi ya kupika Mishkaki ya kuku

Kidali cha kuku 1 kikubwa
Swaum,tangawizi 1 kijiko cha chai
Limao 1/2
Pilipili ya unga 1/2 kijiko cha chai
Curry powder 1/2 kijiko
Paprika 1/2 kijiko cha chai
Hoho jekundu 1/2
Hoho la njano 1/2
Kitunguu 1/2
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Katakata kuku ktk vipande vya mishkaki ya kawaida kisha vimarinate na vitu vyote, kasoro hoho na kitunguu.Ni vizuri kuziacha either usiku mzima au kwa masaa machache ili spice ziingie vizuri. Baada ya hapo katakata hoho na vitunguu vipande vya wastani kiasi. Baada ya hapo Taarisha vijiti vya mishkaki kisha tunga nyama pamoja na hoho na vitunguu kisha nyunyuzia mafuta na kisha uzichome kama mishkaki ya kawaida. Itakapoiva itakuwa tayari kwa kuliwa na chochote upendacho kama ndizi za kuchoma, viazi na n.k.

Jinsi ya kupika Pilau Ya Samaki WaTuna Na Mboga

Viambaupishi

Mchele 2 Mugs

Mboga mchanganyiko za barafu 1 Mug

(Frozen veg)

Tuna (samaki/jodari) 2 kopo

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi 2 vijiko vya supu

Garam masala 1 kijiko cha supu

Nyanya 2

Kitungu maji 1

Mdalasini nzima 2 vijiti

Karafuu 6 chembe

Pilipili mbichi 1

Chumvi kiasi

Viazi 3

Maji 2 ½ Mugs

Mafuta 3 vijiko vya supu

Jinsi ya kuandaa na kupika

Osha mchele na uroweke kwa muda wa dakika 20
Tia mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu maji mpaka kigeuke rangi ya hudhurungi (brown).
Mimina viazi, thomu na tangawizi, bizari zote na kaanga.
Tia nyanya uliyokatakata ikaange mpaka iwive.
Tia tuna endelea kukaanga kidogo tu.
Tia maji, yatakapochemka tia mchele.
Punguza moto uwe mdogo funika kwa muda wa ½ saa hadi wali ukauke na uwive. Utakuwa tayari kuliwa.

Jinsi ya kupika Mkate wa sinia

Mahitaji

Unga wa mchele (rice flour 2 vikombe vya chai)
Sukari (sugar 3/4 ya kikombe cha chai)
Hamira (dried yeast 3/4 kijiko cha chakula)
Hiliki (cardamon powder 1/2 kijiko cha chai)
Ute wa yai 1(egg white)
Tui la nazi (coconut milk kikombe 1 na 1/2 cha chai)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Changanya unga wa mchele, hamira, hiliki na tui la nazi pamoja katika bakuli la plastic kisha koroga vizuri. Ufunike na uwache katika sehemu ya joto mpaka uumuke.(ambayo inaweza kuchukua kama dakika 30-45. Ukisha umuka tia sukari na ute wa yai kisha ukoroge vizuri. Baada ya hapo washa oven katika moto wa 200°C kisha chukua chombo cha kuokea na ukipake mafuta na umimine mchanganyiko. Kisha utie katika oven na uoke kwa muda wa dakika 40. Hakikisha unaiva na kuwa rangi yabrown juu na chini. Na hapo mkate utakuwa tayari.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About