Dondoo za Mapishi na Lishe

Jinsi ya kuandaa Vileja Vya Karanga

MAHITAJI

Mayai 5

Sukari 450gm (1 lb)

Unga wa Ngano 1 kg

Siagi 450gm (1 lb)

Baking powder ½ Kijiko cha chai

Unga wa Custard Vijiko 2 vya chakula

Karanga za kusaga 250gm

Jam ½ kikombe

MAANDALIZI

Chukua bakuli la kiasi, weka sukari na siagi.
Changanya sukari na siagi kwa kutumia mashine ya kukorogea keki (cakemixer), mpaka sukari ichanganyike na siagi.
Vunja yai moja moja na weka kiini chake kwenye mchanganyiko wa sukari na siagi, endelea kuchanganya mpaka ichanganyike vizuri. Hifadhi ute wa mayai ndani ya kibakuli.
Mimina unga wa ngano ndani ya mchanganyiko wako huku ukichanganya Changanya unga wa custard na baking powder.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Vichovye viduara ndani ya ute wa yai kisha zimwagie unga wa karanga na kuzipanga kwenye tray ya kuchomea.
Weka dole gumba kati kati ya kila kiduara na uweke jam.
Washa jiko (oven) 350F na uchome vileja vyako kwa dakika 20.
Toa vileja vyako vipoe na uviweke ndani ya sahani tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Kachori

Mahitaji

Viazi mbatata (potato 4 vya wastani)
Nyama ya kusaga (mince beef 1 kikombe cha chai)
Kitunguu (onion 1 cha wastani)
Carrot 1
Hoho (green pepper 1/2)
Kitunguu swaum (garlic)
Tangawizi (ginger )
Binzari nyembamba (ground cumin 1/2 kijiko cha chai)
Binzari manjano (turmeric 1/2 kijiko cha chai)
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Limao (lemon 1/2)
Pilipili ya unga (chilli powder 1/2 kijiko cha chai)
Giligilani (coriander kiasi)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)
Unga wa ngano kiasi

Matayarisho

Katakata vitunguu na hoho katika vipande vidogo vidogo na kisha kwangua carrot na uweke pembeni. Chemsha viazi na chumvi kidogo vikiiva viponde na uviweke pembeni, Baada ya hapo tia nyama limao, chumvi, kitunguu swaum na tangawizi ichemshe mpaka iive na uhakikishe maji yote yamekauka. Kisha Tia binzari zote, pilipili, curry powder, giligilani, vitunguu, hoho na carrot. Pika mchanganyiko huo kwa muda wa dakika 3 na kisha ipua. Baada ya hapo changanya na viazi kisha tengeneza maduara ya kiasi na uyaweke pembeni. Chukua unga wa ngano kiasi na uchanganye na maji kupata uji usiokuwa mzito au mwepesi sana. baada ya hapo chovya madonge katika huo uji na uyachome katika mafuta. Hakikisha zinaiva na kuwa rangi ya brown na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.Unaweza ukazisevu na chatney yoyote unayopendelea.

Jinsi ya kupika Biskuti Za Tende

Viamba upishi

Unga 4 Vikombe vya chai

Sukari ya laini (icing sugar) 1 Kikombe cha chai

Baking powder 2 Vijiko vya chai

Mayai 2

Siagi au margarine 1 Kikombe cha chai

Vanilla 1 Kijiko cha chai

Maziwa ya kuchanganyia kiasi

Tende iliyotolewa koko 1 Kikombe

ufuta (sasame) kiasi 1/4 kikombe

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Changanya unga, siagi, baking powder, na sukari katika mashine.

2. Kisha tia mayai, vanilla na halafu maziwa kidogo kidogo hadi mchanganyiko ushikamane.

3. Gawanya madonge mawili na usukume kama chapati, lakini sio nyembamba sana.

4. Tandaza tende robo ya duara na unyunyize ufuta duara zima: kisha kunja hadi mwisho na ukate kate, kisha upange katika trei ya kuvumbika.

5. Vumbika (bake) moto wa 350°F kwa muda wa dakika 20 au hadi vigeuke rangi na viwive.

6. Zikisha iiva ziache zipowe na zitakuwa tayari kuliwa.

Mapishi ya Wali maharage,mchuzi wa samaki na spinach

Mahitaji

Mchele (rice 1/2 kilo)
Maharage yaliyochemshwa (boiled red kidney beans 1 kikombe cha chai)
Samaki waliokaangwa ( 2 fried fish)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1/2 ya tin)
Vitunguu vilivyokatwa (onion 2)
Kitunguu swaum (garlic 3 cloves)
Tangawizi (ginger kiasi)
Limao (lemon 1/2)
Chumvi (salt)
Pilipili (scotch bonnet pepper 2)
Mafuta (vegetable oil)
Spinach
Tui la nazi (coconut milk 1 kikombe cha chai)

Matayarisho

Saga nyanya, kitunguu, tangawizi na kitunguu swaum pamoja. Tia kwenye sufuria na upike mpaka maji yakauke kisha tia curry powder, mafuta na chumvi na upike tena mpaka mchanganyiko uive kisha tia samaki na limao na maji kiasi na uache uchemke kiasi. Na hapo mchizi utakuwa tayari.
Osha na uzikate spinach kisha kaanga kitunguu na mafuta kiasi (hakikisha visiwe vya brown kisha tia spinach na chumvi. zipike kwa muda wa dakika 3-4 na hapo zitakuwa tayari zimeshaiva.
Wali: Chemsha maji kiasi kisha tia, chumvi, pilipili nzima(isikatwe) mafuta na tui la nazi. Baada ya hapo koroga na utie mchele na maharage na ufunike uache uchemke mpaka maji yakauke. Kisha geuza na ufunike tena na uuache mpaka uive. Baada ya hapo chakula chako kitakuwa tayari kwa kuseviwa.

Jinsi ya kupika Biskuti Za Kuchoveya Chokoleti

Viambaupishi

Unga 300gm

Siagi 225gm

Icing Sugar 60gm

Chokoleti iliyokoza (Dark Chocolate) 225gm

Vanilla 2 kijiko cha chai

Yai 1

Baking Powder ½ kijiko cha chai

Njugu za vipande ½ kikombe cha chai

Njugu zilizosagwa ¼ kikombe cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Piga sukari na siagi katika mashine ya keki mpaka iwe laini

2. Kisha mimina yai na vanilla koroga vizuri

3. Mwisho mimina unga na baking powder polepole mpaka ichanganyike.

4. Kata kata umbo (shape) lolote unavyopenda (kama nyota, pembetatu,duara, kopa n.k)

5. Panga kwenye treya na choma kwa moto wa 350°C , vikibadilika rangi kidogo tu vitoe

6. Yayusha chokoleti tia kwenye bakuli ndogo.

7. kisha paka kwa kijiko au chovyea upande mmoja mmoja wa biskuti kisha nyunyizia njugu za kipande na njugu ya unga.

8. Panga kwenye sahani tiyari kunywewa na chai ya maziwa au kahawa.

Jinsi ya kupika Labania Za Maziwa

Viamba upishi

Maziwa ya unga 2 vikombe

Sukari 3 vikombe

Maji 3 vikombe

Unga wa ngano ½ kikombe

Mafuta ½ kikombe

Iliki kiasi

Jinsi ya kuandaa na kupika

Paka sinia mafuta kabla ya kupika labania
Katika sufuria chemsha maji na sukari pamoja na iliki mpaka inate vizuri
Kisha mimina mafuta koroga
Halafu mimina unga wa ngano na ukoroge haraka haraka
Kisha tia unga wa maziwa, endelea kukoroga usiwe na madonge mpaka uwe rangi ya browni isiokoleza.
Kisha mimina mchanganyiko kweye sinia uliyoipaka mafuta, iwache ipoe na kata kata upendavo na itakuwa tayari.

Jinsi ya kuishi maisha marefu (Mambo ya kuzingatia ili uishi maisha marefu)

Kuishi ukiwa na afya na kuishi maisha marefu kunawezekana kwa kubadili hali ya maisha unayoishi inayoharibu afya yako mfano uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi,kutokufanya mazoezi na kutokula matunda na mbogamboga.

Mambo yanayoweza kukusaidia kuishi maisha marefu ni kama yafuatayo

  1. Kuuandaa mwili kwa maisha marefu kwa kufanya mazoezi
  2. Kuwa makini kutambua na kutibu matatizo ya kiafya
  3. Kuepuka mazingira na kufanya kazi kwa namna au kazi zinazoweza kudhuru maisha yako. Mfano kuendesha gari bila kufuata utaratibu, kutokuvaa vifaa vya kujikinga wakati wa kazi
  4. Epuka vitu vyenye sumu vinavyoweza kudhuru afya yako na kukuletea matatizo ya kiafya kama dawa za mimea na mifugo, zitumie kama inavyotakiwa
  5. Usinywe pombe, usivute sigara wala kutumia dawa za kulevya
  6. Kula mlo kamili
  7. Usile vyakula vyenye chumvi na mafuta mengi
  8. Kunywa maji mengi ili kusafisha mwili
  9. Epuka msongo wa mawazo

Mapishi – Fish Finger

Leo tunaangalia mapishi ya fish finger ( sijui kama unaweza kusema kidole cha samaki)!, Ni mlo mzuri hasa kuliwa kama kitafunio au mboga ya pembeni.

Mahitaji

500g Fileti ya samaki
120g Chenga za mkate
100g Unga wa ngano
Mayai 2
Ndimu 1
Kitunguu saumu 1
Kotmiri
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Menya vitunguu saumu kisha visage

Katakata fileti kwa muundo wa mraba (kama vidole) kisha paka mchanganyiko wa vitunguu saumu

Kata ndimu na kamulia kwenye fillet yako

Weka chenga za mkate kwenye bakuli kisha uchanganye chumvi kiasi na kata kata kotmiri majani 3 na uchanganye pamoja.

Kwenye bakuli lingine weka mayai na uyapigepige yawe kama uji mzito

Weka unga kwenye bakuli jingine.

Chukua kipande cha fillet kiweke unga kidogo kisha kizamishe kwenye yai na baada ya hapo kizamishe kwenye mchanganyiko wa chenga za mkate. Fanya hivyo kwa vipande vyote.

Weka mafuta kwenye kikaago na subiri yachemke kisha weka fillet zako vizuri na zikaange pande zote hadi zimekuwa rangi ya brown ( hakikisha moto sio mkali sana).

Epua na weka pembeni mafuta yote yakauke

Weka kwenye sahani tayari kwa kula.

Madhara ya soda

Soda ni kiburudisho ambacho si muhimu sana kwa afya.

Aina nyingi za soda zina kafeini ambayo huzuia usharabu (ufyonzwaji) wa madini ya chuma mwilini hasa yatokanayo na vyakula vya mimea Hata hivyo soda zinaweza kutumika kwa kiasi kidogo kama kiburudisho, ila tunapotaka ubora zaidi wa afya zetu inafaa kupunguza matumizi ya soda na badala yake kutumia vinywaji vyenye virutubishi muhimu kama vile maji ya matunda, maziwa, madafu au asusa kama vile matunda, karanga na aina mbalimbali za mboga mfano karoti.

Hii inasaidia pia kutumia fedha kidogo tuliyo nayo kwa vyakula muhimu, hasa ukizingatia badala ya soda moja unaweza kupata mayai matatu au nusu lita hadi lita moja ya maziwa.

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Samaki Wa Kuchoma

Vipimo Vya Ugali

Unga wa mahindi – 4 vikombe

Maji – 6 kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Tia maji kiasi katika sufuria wacha yachemke hasa

Tia unga kidogo kidogo huku ukikoroga mpaka ukamatane

Punguza moto huku ukiendelea kuusonga

Endelea kusonga kwa dakika kadhaa mpaka uanze kuchambuka

Kisha mimina kwenye bakuli au sahani na itakuwa tayari

Vipimo Ya Upishi Wa Mchuzi Wa Samaki Wa Kuchoma Wa Nazi

Samaki:

Samaki wa Nguru – kiasi vipande 5 – 6

Pilipili mbichi – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 5 chembe

Tangawizi mbichi – 1 kipande

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha supu

Pilipili nyekundu ya unga – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 3 kamua

Chumvi – kiasi

Ukipenda mkate samaki vipande kiasi.
Saga vipimo vyote vinginevyo katika mashine. Mchanganyiko ukiwa mzito ongezea ndimu
Changanya pamoja na samaki upake vizuri vipande vya samaki
Acha kwa muda wa nusu saa vikolee mchanganyiko
Panga samaki katika treya ya kupikia ndani ya oveni, kisha mchome (grill) samaki huku ukigeuza hadi viwive.
Epua weka kando.

Kuandaa Mchuzi:

Nyanya/tungule – 3

Kitunguu – 2

Bizari ya manjano/haldi – ¼ kijiko cha chai

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Tui la nazi zito – 3 vikombe

Chumvi – kiasi

Katakata vitunguu na nyanya vidogodogo (chopped) weka kando

Weka mafuta katika karai au sufuria, kaanga vitunguu hadi vianze kugeuka rangi

Tia nyanya kaanga pamoja na tia bizari ya njano/haldi .

Tia tui la nazi, chumvi koroga .

Mwishowe tia vipande vya samaki na rojo lake litakalobakia katika treya, mchuzi uko tayari

Mapishi ya Ndizi Mbichi Za Nyama Ng’ombe

Vipimo

Ndizi mbichi – 10

Nyama – kilo 1

Nazi ya kopo – 1

Chumvi – 1 Kijiko cha chakula

Ndimu – 1

Bizari ya manjano – 1 Kijiko cha chai

Pili pili mbichi – 3

Nyanya (tomatoes) – 2

Kitunguu maji – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi iliyosagwa – 1 Kijiko cha chakula

Namna ya Kutayarisha Na Kupika

Kata nyama vipande vipande na uisafishe.
Chemsha nyama weka chumvi, thomu, tangawizi na ndimu. Iache iwive.
Kata kata nyanya na kitunguu, kisha mimina kwenye nyama inayochemka, weka na bizari nusu kijiko. Wacha supu iwive kisha weka pembeni. Ukumbusho: Hakikisha supu inakuwa kiasi na si nyingi.
Menya maganda ndizi na uzikate vipande vipande vya kiasi.
Zikoshe ndizi na uziweke ndani ya sufuria.
Weka maji ndani ya sufuria kisha zichemshe ndizi mpaka ziwe laini kidogo.
Zimwage maji ndizi kisha mimina supu na nyama ndani ya ndizi.
Mimina nazi pili pili na bizari nusu kijiko ndani ya ndizi na uziweke kwenye jiko zichemke mpaka zibakie na urojo kiasi. Onja chumvi na uongeze kadri utakavyopenda.
Weka pembeni zipoe.
Pakua ndizi kwenye sahani au bakuli tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Supu ya makongoro

Mahitaji

Makongoro (miguu ya ng’ombe) kiasi
Limao 1 kubwa
Kitunguu swaum
Tangawizi
Chumvi
Pilipili

Matayarisho

Safisha makongoro kisha yatie kwenye pressure cooker. Kisha tia kitunguu swaum, tangawizi, chumvi,limao na maji kiasi. Baada ya hapo yachemshe mpake yaive na yawe malaini na pia ubakize supu kiasi inaweza kuchukua kama dk 45 au saa 1 hivi. Baada ya hapo yaipue na upakue supu yako kwenye bakuli katia pilipili kiasi kisha itakuwa tayari kwa kuliwa.

Note:
Ukiwa unanunua makongoro hakikisha unachukuwa yale yasiyokuwa na manyoya na pia
hakikisha usiyachemshe kupitiliza kwani yakiwa malaini sana utashindwa kuyaenjoy.

Jinsi ya kupika Eggchop

Mahitaji

Mayai yaliochemshwa 4
Nyama ya kusaga robo kilo
Kitunguu swaum
Tangawizi
Limao
Chumvi
Pilipili
Breadcrambs
Carry powder
Binzari nyembamba ya unga
Yai moja bichi
Mafuta

Matayarisho

Marinate nyama na pilipili, kitunguu swaum, tangawizi, limao, chumvi, carry powder, binzari nyembamba na breadcrambs pamoja. Kisha vunja yai moja bichi kwenye kibakuli na ulikoroge kisha tia kwenye mchanganyiko wa nyama.Gawanisha matonge manne kwa ajili ya kuzungushia kwenye mayai .Chemsha mayai kwa muda wa dakika 20. Yakisha iva acha yapoe na kisha yamenye maganda na uyaweke pembeni. Baada ya hapo chukua yai moja lililochemshwa na ulizungushie donge moja la mchanganyiko wa nyama. fanya hivyo kwa mayai yote yaliobakia. Baada ya hapo paka mafuta kwa nje ya hizo eggchop na kisha paka mafuta kwenye sinia la kuokea na uziokee kwenye oven kwa moto wa kawaida, kwa muda wa dakika 20.Na eggchop zako zitakuwa tayari kwa kuliwa

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About