Dondoo za Mapishi na Lishe

Jinsi ya kupika Keki Ya Maboga

Viamba upishi

Unga wa ngano vikombe vikubwa 3
Boga lililopondwa kikombe 1
Baking powder vijiko vidogo
Sukari kikombe kikubwa 1
Blue band kikombe ½
Vanilla kijiko kidogo 1
Mayai 2
Maji kiasi/ maziwa
(kama nilazima)

Hatua

• Osha boga, Kata, ondoa mbegu, kisha kata vipande vikubwa, chemsha na maji mpaka vilainike.
• Kwangua boga la ndani ukiacha maganda na ponda sawasawa.
• Chekecha unga (kila kikombe 1, vijiko vidogo 2 vya baking powder) kwenye bakuli kubwa.
• Ongeza blue band na changanya sawasawa na vidole.
• Ongeza sukari na changanya.
• Ongeza mayai na koroga na mwiko.
• Ongeza boga lililopondwa na koroga njia moja mpaka ilainike.
• (Kama haikulainika ongeza yai /mayai au maziwa/ maji kidogo).
• Ongeza vanilla na koroga.
• Paka mafuta chombo cha kuokea au sufuria kisha chekecha unga kidogo wa ngano.
• Mimina rojo la keki kwenye sufuria au chombo cha kuokea.
• Oka kwenye oven au tumia sufuria na weka mkaa wa moto juu na chini moto kidogo mpaka iive.
• Jaribu kuchoma kisu katikati, kama ni kavu keki imeiva, epua, pozesha kata tayari kwa kula, kama kitafunio.

Mapishi ya Ndizi Mbichi Za Nyama Ng’ombe

Vipimo

Ndizi mbichi – 10

Nyama – kilo 1

Nazi ya kopo – 1

Chumvi – 1 Kijiko cha chakula

Ndimu – 1

Bizari ya manjano – 1 Kijiko cha chai

Pili pili mbichi – 3

Nyanya (tomatoes) – 2

Kitunguu maji – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi iliyosagwa – 1 Kijiko cha chakula

Namna ya Kutayarisha Na Kupika

Kata nyama vipande vipande na uisafishe.
Chemsha nyama weka chumvi, thomu, tangawizi na ndimu. Iache iwive.
Kata kata nyanya na kitunguu, kisha mimina kwenye nyama inayochemka, weka na bizari nusu kijiko. Wacha supu iwive kisha weka pembeni. Ukumbusho: Hakikisha supu inakuwa kiasi na si nyingi.
Menya maganda ndizi na uzikate vipande vipande vya kiasi.
Zikoshe ndizi na uziweke ndani ya sufuria.
Weka maji ndani ya sufuria kisha zichemshe ndizi mpaka ziwe laini kidogo.
Zimwage maji ndizi kisha mimina supu na nyama ndani ya ndizi.
Mimina nazi pili pili na bizari nusu kijiko ndani ya ndizi na uziweke kwenye jiko zichemke mpaka zibakie na urojo kiasi. Onja chumvi na uongeze kadri utakavyopenda.
Weka pembeni zipoe.
Pakua ndizi kwenye sahani au bakuli tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Kachori

Mahitaji

Viazi mbatata (potato 4 vya wastani)
Nyama ya kusaga (mince beef 1 kikombe cha chai)
Kitunguu (onion 1 cha wastani)
Carrot 1
Hoho (green pepper 1/2)
Kitunguu swaum (garlic)
Tangawizi (ginger )
Binzari nyembamba (ground cumin 1/2 kijiko cha chai)
Binzari manjano (turmeric 1/2 kijiko cha chai)
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Limao (lemon 1/2)
Pilipili ya unga (chilli powder 1/2 kijiko cha chai)
Giligilani (coriander kiasi)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)
Unga wa ngano kiasi

Matayarisho

Katakata vitunguu na hoho katika vipande vidogo vidogo na kisha kwangua carrot na uweke pembeni. Chemsha viazi na chumvi kidogo vikiiva viponde na uviweke pembeni, Baada ya hapo tia nyama limao, chumvi, kitunguu swaum na tangawizi ichemshe mpaka iive na uhakikishe maji yote yamekauka. Kisha Tia binzari zote, pilipili, curry powder, giligilani, vitunguu, hoho na carrot. Pika mchanganyiko huo kwa muda wa dakika 3 na kisha ipua. Baada ya hapo changanya na viazi kisha tengeneza maduara ya kiasi na uyaweke pembeni. Chukua unga wa ngano kiasi na uchanganye na maji kupata uji usiokuwa mzito au mwepesi sana. baada ya hapo chovya madonge katika huo uji na uyachome katika mafuta. Hakikisha zinaiva na kuwa rangi ya brown na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.Unaweza ukazisevu na chatney yoyote unayopendelea.

Mapishi ya Half cake (Keki)

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) kikombe 1na 1/2
Sukari (sugar) 1/4 kikombe
Barking powder 1/2 kijiko cha chai
Magadi soda (bicarbonate soda) 1 kijiko cha chai
Mafuta 2 vijiko vya chai
Mafuta ya kukaangia
Maji ya uvuguvugu kiasi

Matayarisho

Changanya unga na vitu vyote (kasoro mafuta ya kuchomea) kisha ukande (hakikisha unakuwa mgumu) Baada ya hapo sukuma na ukate shape uipendayo (hakikisha unakata vipande vinene kiasi na sio kama mandazi) Baada ya hapo ziweke sehemu yenye joto na uache ziumuke. Zikisha umuka zikaange katika moto mdogo ili ziive mpaka ndani. Zikisha iva zitoe na uziweke katika kitchen towel ili zichuje mafuta. Ziache zipoe na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika wali wa Tuna (samaki/jodari)

VIAMBAUPISHI VYA TUNA

Tuna (samaki/jodari) – 2 Vikopo

Vitunguu (kata kata) – 4

Nyanya zilizosagwa – 5

Nyanya kopo – 3 Vijiko vya supu

Viazi (vilivyokatwa vipande vidogo – cubes) – 4

Dengu (chick peas) – 1 kikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic)&Tangawizi iliyosagwa 1 Kijiko cha supu

Hiliki – 1/4 kijiko cha chai

Mchanganyiko wa bizari – 1 kijiko cha supu

Chumvi – kiasi

Pilipili manga – 1 Kijiko cha chai

Vipande cha Maggi (Cube) – 2

VIAMBAUPISHI VYA WALI

Mchele – 3 Vikombe vikubwa (Mugs)

Mdalasini – 2 Vijiti

Karafuu – chembe 5

Zaafarani – kiasi
Jirsh (Komamanga kavu au zabibu kavu -raisins) – 1/2 Kikombe

JINSI YA KUANDAA

Kosha Mchele na roweka.
Kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi (brown) chuja mafuta uweke kando.
Kaanga viazi, epua
Punguza mafuta, kaanga nyanya.
Tia thomu/tangawizi, bizari zote, vipande vya Maggi, nyanya kopo, chumvi.
Mwaga maji ya tuna iwe kavu, changanyisha kwenye sosi.
Tia zaafarani kidogo katika sosi na bakisha ya wali.
Chemsha mchele pamoja na mdalasini na karafuu.
Karibu na kuwiva, chuja maji utie katika chombo cha kupikia katika jiko (oven)
Nyunyizia zaafarani, mwagia vitunguu, viazi, na dengu juu ya wali.
Mwagia sosi ya tuna na pambia jirshi (au zabibu).
Funika wali na upike katika jiko moto wa 450º kwa muda wa kupikika wali. Epua upakue.

Jinsi ya kupika Mitai

VIAMBAUPISHI

Unga wa ngano 1 1/2 Kikombe

Baking powder 1 Kijiko cha chai

Baking soda ¼ Kijiko cha chai

Chumvi ½ kijiko cha chai

Sukari 1 kijiko cha supu

Hamira 1/2 Kijiko cha supu

Yai 1

Maziwa ½ Kikombe

Mafuta ya kukaangia

VIAMBAUPISHI:SHIRA

Sukari 1 Kikombe

Maji ½ Kikombe

Iliki au Mdalasini ¼ kijiko cha chai (ya unga)

MAANDALIZI NA JINSI YA KUPIKA

1. Kwenye bakuli, changanya pamoja unga, baking powder, baking soda, chumvi, sukari na hamira.

2. Katika kibakuli, piga mayai na maziwa pamoja.

3. Changanya mchanganyiko wa mayai na wa unga ; na ukande kama unga wa maandazi.

4. Ikisha fura, sukuma unga kama wa maandazi na ukate mitai .

5. Pasha moto mafuta na uchome hadi iwe rangi ya dhahabu, upande zote mbili.

6. Ipikie shira lakini isiwe nzito .

7. Tia mitai na upepete hadi sukari ienee kote na zitakuwa tayari kuliwa.

Mapishi ya Pilau Ya Nafaka Na Nyama Ya Kusaga

VIAMBAUPISHI

Mchele – 3 vikombe

Nyama ya kusaga – 1 LB

Mchanganyiko wa Nafaka upendazo; maharagwe, njegere, mbaazi n.k 1 mug

Vitunguu maji kata vipande vipande – 3 vya kiasi

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi – 2 vijiko vya supu

Mafuta – ½ Kikombe

Mchanganyiko wa bizari (Garam Masala) – 2 vijiko vya chai

Vipande vya supu (Maggi cubes) – 3

Maji (inategemea mchele) – 5

Chumvi – Kiasi

MAPISHI

Osha mchele na roweka.
Weka mafuta katika sufuria na kaanga vitunguu mpaka viwe brown.
Tia Thomu na tangawizi, kaanga kidogo.
Weka nyama ya kusaga, chumvi na garam masala, endelea kukaanga mpaka nyama iwive.
Mwaga maji yaliomo katika kopo la nafaka na utie nafaka pekee humo.
Tia maji na vipande vya supu (Maggi cubes) huku unavivuruga, koroga kidogo.
Tia mchele, koroga kidogo.
Funika na pika kwa moto mdogo mpaka karibu na kukauka ukikorogoka kidogo. (kama unavyopika pilau ya kawaida)
*Epua uipike katika moto wa oven 350-400 Deg kwa muda wa dakika 15.
*Kama sufuria uliyotumia sio ya kupikia katika oven, mimina katika chombo chochote kinachotumika kwa oven kama bakuli la pyrex au treya za foil.
Pakua katika sahani na iko tayari kuliwa.

Mapishi ya Pilau Ya Samaki Wa Tuna Na Mboga

Mahitaji

Mchele – 2 Mugs

Mboga mchanganyiko za barafu (Frozen veg) – Mug

Tuna (samaki/jodari) – 2 kopo

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi -2 vijiko vya supu

Garam masala – 1 kijiko cha supu

Nyanya – 2

Kitungu maji – 1

Mdalasini nzima – 2 vijiti

Karafuu – 6 chembe

Pilipili mbichi – 1

Chumvi – kiasi

Viazi – 3

Maji – 2 ½ Mugs

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Maandalizi

Osha mchele na uroweke kwa muda wa dakika 20
Tia mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu maji mpaka kigeuke rangi ya hudhurungi (brown).
Mimina viazi, thomu na tangawizi, bizari zote na kaanga.
Tia nyanya uliyokatakata ikaange mpaka iwive.
Tia tuna endelea kukaanga kidogo tu.
Tia maji, yatakapochemka tia mchele.
Punguza moto uwe mdogo funika kwa muda wa ½ saa hadi wali ukauke na uwive. Utakuwa tayari kuliwa.

Mapishi ya Viazi vitamu na kachumbari

Mahitaji

Viazi utamu 3
Nyanya 2 kubwa
Kitunguu
Tango
Limao
Chumvi
Pilipili
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Menya viazi na kisha vikate katika vipande. Tia mafuta kwenye chuma cha kukaangia, yakisha pata moto tia viazi nauviache vikaangike mpaka upande mmoja uwe wa brown na kisha geuza upande wa pili na upike mpaka uwe wa brown. Vikisha iva ipua na uweke kwenye kitchen towel ili vikauke mafuta.
Kachumbali: Katakata vitunguu katika bakuli na kisha tia chumvi kwa ajili ya kuondoa ukali wa vitunguu. Baada ya hapo vioshe mpaka chumvi yote iishe. osha nyanya, Pilipili tango na kisha katakata slice nyembamba na uchanganye na vitunguu. Baada ya hapo tia chumvi, kamulia limao na uchanganye zote pamoja .Baada ya hapo viazi na kachumbali vitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Chicken Curry

Leo wapendwa nitaenda kuzungumzia mapishi ya mchuzi wa kuku (chicken curry).

Mahitaji

Kuku mzima
Nyanya kubwa 3
Karoti mbili
Pilipili hoho
Kotmiri
Tangawizi
Kitunguu maji
Kitunguu saumu kidogo
Ndimu
Mafuta ya kupikia
Chumvi (pilipili ukipenda)

Matayarisho

1. Menya vitunguu saumu na tangawizi na uvitwange pamoja.
2. Katakata kuku vipande vidogo kisha ukamulie ndimu na kupaka mchanganyiko wa tangawizi na vitunguu saumu (kiasi tu).
3. Katakata vitunguu maji na pilipili hoho uweke pembeni.
4. Grind (Kwangua) kwenye grater nyanya na karoti pia uweke pembeni.
5.Katakata kotmiri vipande vidogo uweke pembeni.
6. Andaa kikaango na jiko.

Mapishi

1. Bandika kikaango jikoni na mafuta kiasi, yakishachemka weka vitunguu maji na kaanga hadi vimelainika na kuiva (hakikisha haviungui).
2. Weka pilipili hoho na karoti na endelea kukoroga hadi vyote viive na kulainika, Kisha weka chumvi.
3. Sasa weka vipande vya nyama koroga na funikia kwa dakika 3, kisha weka nyanya zako ulizo grind na koroga ili zichanganyike vizuri, vikishachanganyika weka kotmiri na pilipili kama utapenda. Acha vichemke kwa dakika 5. Hakikisha moto sio mkali sana.
4. Angalia kama nyama zimeiva vizuri kisha epua mchuzi wako.
5. Pakua kwenye bakuli na katakata kotmiri uweke kwa juu.
Unaweza kula kwa ugali, wali, ndizi rost au chipsi.

Mapishi – Mayai Mchanganyiko, Tosti na Soseji

Karibu tena jikoni, leo tunaandaa vitafunwa kwa ajili ya kifungua kinywa asubuhi.

Mahitaji

Mayai 3
Soseji 2
Mkate slesi 2
Mafuta ya kupikia vijiko 2
Chumvi

Matayarisho

Piga piga mayai vizuri kwenye bakuli na weka chumvi kidogo kisha weka kikaango kwenye moto na mafuta kidogo.

Kikisha pata moto miminia mchanganyiko wa mayai na uanze kukorogo pale tu unapomiminia, endelea kukoroga hadi uone yanakuwa magumu na kuanza kuiva. Pika kwa kiwango unachopendelea na kusha epua na weka kwenye sahani.

Weka mafuta kijiko kimoja kwenye kikaango na kisha weka soseji zako na uzipike kiasi pande zote kisha epua na weka pembeni.

Weka slesi za mikate kwenye toster na zikiwa tayari unaweza weka siagi ili kuongeza ladha na mvuto.
Andaa mlo wako pamoja na juice, maziwa au chai.

Mapishi ya Biriani Ya Samaki Nguru, Njegere Na Snuwbar (UAE)

Mahitaji

Mchele wa basmati – 4 cups

Samaki nguru (king fish) – 7 vipande au zaidi

Kitunguu – 5

Nyanya/tungule – 3

Njegere – 1 kikombe

Snuwbar (njugu za pine) – 1 kikombe

Viazi – 2 kata kata mapande makubwa

Tangawizi mbichi – 1 kijiko cha supu

Kitunguu saumu – 1 kijiko cha supu

Pilipili nyekundu – 1 kijiko cha chai

Bizari ya biriani/garama masala – 1 kijiko cha supu

Namna Ya Kupika:

Kaanga samaki mbali kwa viungo upendavyo umkoleze vizuri. Au choma (bake/grill) katika oveni ukipenda.
Weka mafuta katika sufuria, tia vitunguu kaanga hadi vigeuka rangi. Gawa sehemu mbili.
Sehemu moja bakisha katika sufuria kisha tia tangawizi mbichi na kitunguu thomu ukaange.
Tia nyanya kaanga kisha tia bizari zote endelea kukaanga, tia njegere, njugu za snuwbar na ndimu kavu.
Tia viazi ulivyokwishakaanga, na vitunguu vilobakia.
Tia mapande ya samaki, changanya na masala bila ya kumvuruga samaki.
Chemsha wali kisha mwagia juu yake, funika upike ndani ya oveni au mkaa hadi wali uive kama unavyopika kawaida ya biriani.
Epua pakua huku ukichanganya na masala ya samaki.

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Tende

MAHITAJI

Unga – 4 Vikombe vya chai
Sukari ya laini (icing sugar) – 1 Kikombe cha chai
Baking powder – 2 Vijiko vya chai
Mayai – 2
Siagi au margarine – 1 Kikombe cha chai
Vanilla -1 Kijiko cha chai
Maziwa ya kuchanganyia – kiasi
Tende iliyotolewa koko – 1 Kikombe
ufuta (sasame) kiasi 1/4 kikombe

MAANDALIZI

Changanya unga, siagi, baking powder, na sukari katika mashine.
Kisha tia mayai, vanilla na halafu maziwa kidogo kidogo hadi mchanganyiko ushikamane.
Gawanya madonge mawili na usukume kama chapati, lakini sio nyembamba sana.
Tandaza tende robo ya duara na unyunyize ufuta duara zima: kisha kunja hadi mwisho na ukate kate, kisha upange katika trei ya kuvumbika.
Vumbika (bake) moto wa 350°F kwa muda wa dakika 20 au hadi vigeuke rangi na viwive.
Zikisha iiva ziache zipowe na zitakuwa tayari kuliwa.

Jinsi ya kupika Biskuti Za Tende Na Ufuta

Viambaupishi

Unga 3 Vikombe vya chai

Baking powder 1 ½ Vijiko vya chai

Sukari 1 Kikombe cha chai

Siagi 1 Kikombe cha chai

Mayai 2

Maji kiasi ya kuchanganyia

Tende 1 Kikombe

ufuta ¼ kikombe

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Changanya unga, siagi, baking powder, na sukari katika bakuli

2. Tia mayai, na maji kidogo uchanganye vizuri.

3. Sukuma kiasi kama unavyosukuma chapati duara kubwa.

4. Tandaza tende juu yake halafu kunja hadi mwisho.

5. Paka mayai juu yake halafu mwagia ufuta kisha kata kata vipande kama katika picha.

6. Vipange kwenye treya ya oveni kisha choma(bake)moto wa 350°F kwa muda wa nusu saa takriban.

7. Ziepue katika moto naziache zipowe. Panga katika sahani.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About