Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Samaki wa kupaka

Mahitaji

Samaki (Tilapia 2)
Nyanya ya kopo (Tomato tin 1)
Kitunguu (Onion 1)
Tangawizi (ginger kiasi)
Kitunguu swaum (garlic clove )
Mafuta (Vegetable oil)
Pilipili (scotch bonnet pepper 1)
Tui la nazi zito (coconut milk 2 vikombe vya chai)
Curry powder 1/2 cha kijiko cha chai
Binzari nyembamba ya unga (ground cumin 1/2 kijiko cha chai
Binzari manjano (turmaric 1/2 kijiko cha chai
Chumvi (salt)
Limao (lemon 1)
Giligilani (fresh coriander)

Matayarisho

Marinate samaki na chumvi, limao, kitunguu swaum, tangawizi kwa muda wa masaa 6 au zaidi. Baada ya hapo wakaange au waoke katika oven mpaka waive ila usiwakaushe sana. Baada ya hapo saga pamoja nyanya ya kopo, kitunguu maji, kitunguu swaum na tangawizi. Kisha bandika huo mchanganyiko jikoni na upike mpaka ukauke maji kisha tia mafuta, binzari zote, curry powder, chumvi na pilipili na upike kwa muda wa dakika 5. Baada ya hapo tia maji kidogo (kama 1/2 kikombe) pamoja na tui la nazi. Acha uchemke mpaka tui liive na mchuzi ubakie kiasi. Baada ya hapo waweke samaki kwenye sufuria ya kuokea na kisha umwagie huo mchuzi juu ya hao samaki na owaoke (bake) kwa muda wa dakika 20. Ukisha toa kwenye oven katakata giligilani na utie kwenye hao samaki na hapo watakuwa tayari kwa kuliwa. unaweza kuwala na wali, ugali au chapati

Mapishi ya Viazi, samaki na asparagus

Mahitaji

Viazi (potato 1/2 kilo)
Samaki (fish 2)
Asparagus 8
Kitunguu kilichokatwa (chopped onion 1)
Kitunguu swaum kilichosagwa (garlic 4 cloves)
Tangawizi iliyosagwa kiasi (ginger paste)
Limao (lemon 1)
Giligilani iliyokatwakatwa (chopped coriander)
Curry powder (kijiko 1 cha chai)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Safisha samaki na kisha uwamarinate na kitunguu swaum, tangawizi, limao na chumvi kwa muda wa nusu saa. Baada ya hapo wakaange na usiwakaushe sana kisha waweke pembeni. Chukua fry-pan kisha tia mafuta kidogo sana (kama 1/2 kijiko cha chai) kisha tia vitunguu maji na uvikaange kwa muda wa dakika 2 (kwani havitakiwi kuiva kabisa) kisha waweke samaki na uwachanganye na hivyo vitunguu. Kisha baada ya hapo tia giligilani iliyokatwa, kamulia limao na tia chumvi kidogo kisha geuzageuza ili kuchanganya vitu vyote na kisha ipua. Baada ya hapo menya na ukate viazi katika vipande vya wastani, na kisha uvichemshe kidogo na visiive kabisa. Baada ya hapo weka sufuria jikoni kwenye moto wa wastani na utie mafuta kidogo (kama vijiko 2 vya chakula) na kisha tia viazi na uanze kuvipika kwa kuvigeuzageuza mpaka viive na kuwa rangi ya brown kisha tia chumvi kidogo, curry powder na giligilani iliyokatwa.Vipike kwa muda wa dakika mbili kisha viipue. Na baada ya hapo malizia kwa kupika asparagus. Kwanza zioshe kisha zikate kati. Baada ya hapo weka mafuta kidogo kama 1/2 kijiko katika fry-pan yakisha pata moto tia kitunguu swaum, asparagus na chumvi.Zipike kwa kuzigeuzageuza kwa muda wa dakika 5 na hapo zitakuwa zimeshaiva na tayari kwa kuliwa pamoja na samaki na viazi. Unaweza kuvisevu kwa ketchup.

Mapishi ya Chapati za Kusukuma kitaalamu

Mahitaji

Unga wa ngano (plain flour 1/2 of kilo)
Siagi (butter vijiko 2 vya chakula)
Yai (egg 1)
Chumvi (1/2 ya kijiko cha chai)
Hiliki (ground cardamon 1/4 ya kijiko cha chai)
Maji ya uvuguvugu (warm water)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Weka unga wa ngano katika bakuli la kukandia, kisha tia chumvi na hiliki na uchanganye kwanza, baada ya hapo tia siagi na uichanganye vizuri na unga mpaka ipotee. Baada ya hapo tia tena yai na uchanganye vizuri. Mchanganyiko ukishachanganyika vizuri sasa unaweza kutia maji ya uvuguvugu kidogo, kidogo huku ukiwa unauchanganya ili kupata donge. Baada ya hapo anza kukanda hilo donge mpaka mabuje yote yapotee na unga uwe mlaini, ambapo itakuchukua kama dakika 15. Baada ya hapo tawanyisha unga katika madonge ya wastani (yasiwe makubwa sana au madogo sana) Ukimaliza hapo, andaa kibao cha kusukumia chapati kwa kukitia unga kidogo ili chapati isinatie kwenye kibao. Sukuma donge moja la chapati mpaka liwe flat na kisha weka kijiko kimoja cha mafuta na usambaze. ukisha maliza ikunje (roll). Fanya hivyo kwa madonge yote yaliyobakia.
Baada ya hapo andaa chuma cha kuchomea (fry-pan) katika moto wa wastani. Kisha anza kusukuma chapati (ni vizuri ukaanza na zile ulizozikunja mwanzo ili kuzipa nafasi zile za mwisho ziweze kulainika) ukiwa unasukuma hakikisha zinakuwa flat (na zisiwe nene sana au nyembamba sana) Ukishamaliza hapo tia kwenye chuma cha kuchomea. Acha iive upande mmoja then igeuze upande wa pili. Tia mafuta ama kijiko kimoja kikubwa upande wa chini wa chapati na uanze kuukandamiza kwa juu uku ukiwa unaizungusha. fanya hivyo uku ukiwa unaigeuza kuiangalia kwa chini ili isiungue. ikishakuwa ya brown, geuza upande wa pili na urudie hivyohiyvo mpaka chapati iive. Rudia hii process kwa chapati zote zilizobakia.

Siri ya chapati kuwa laini ni kutia siagi au mafuta ya kutosha kipindi unazikanda na pia kuzikanda mpaka unga uwe laini.

Mapishi ya Mseto wa choroko

Mahitaji

Mchele 2 vikombe vya chai
Choroko kikombe 1 na 1/2
Nazi kopo 1
Swaum 1 kijiko cha chakula
Kitunguu 1 kikubwa
Binzari nyembamba 1 kijiko cha chai
Chumvi
Mafuta

Matayarisho

Loweka choroko usiku mzima, pindi ukianza kupika loweka mchele nusu saa kisha katika sufuria kubwa, kaanga vitunguu vikianza kuwa vya brown tia swaum na binzari nyembamba kisha tia choroko, mchele, chumvi,nazi na maji mengi kiasi yakuivisha choroko pamoja na mchele. Pika mpaka vitu vyote viive na viwe vilaini kisha upondeponde kiasi.Baada ya mseto wako kuiva utakuwa unaonekana kama uji wa mchele vile. Na Baada ya hapo mseto wako utakuwa tayari kwa kuliwa na mboga yoyote uipendayo.Inapendeza zaidi kuliwa vile tu ukishamalizwa kupikwa

Jinsi ya kutengeneza Mkate wa mayai

Mahitaji

Slice za mkate 6
Mayai 3
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Vunja mayai yote katika sahani kisha tia chumvi kidogo sana na uyapige mpaka chumvi ichanganyike. Kisha chukua frying pan na utie vimafuta kidogo na uweke jikoni. Mafuta yakishapata moto kiasi,chovya slice za mkate katika hayo mayai na uzipike pande zote zikishaiva zitoe na uziweke katika kitchen towel ili kukausha mafuta.Na baada ya hapo mikate yako itakuwa tayari kwa kuliwa na chai.

Mapishi ya Mihogo ya nazi na kuku

Mahitaji

Mihogo kilo 1
Kidali cha kuku 1 kikubwa
Nyanya 1 kubwa
Kitunguu maji 1 cha wastani
Swaum/tangawizi i kijiko cha chai
Nazi kopo 1
curry powder 1 kijiko cha chai
Binzari manjano 1/2 kijiko cha chai
Limao 1/2
Pilipili 1
Chumvi kiasi

Matayarisho

Saga pamoja nyanya, kitunguu na swaum/ginger pamoja na vimaji kidogo. Kisha vitie kwenye sufuria isiyoshika chini na uvishemshe mpaka maji yote yakauke kisha tia mafuta na upike ktk moto mdogo mpaka viive.Baada ya hapo tia spice na uzipike kidogo kisha tia mihogo na kuku (kuku na mihogo vikatwe vipande vya wastani) vichanganye vizuri kisha tia nazi na vimaji kiasi,limao chumvi na pilipili na ufunike kisha punguza moto. Pika mpaka mihogo na kuku viive na ibaki rojo kidogo kisha ipua na mihogo yako itakuwa tayari kwa kuliwa

Jinsi ya kupika Biriani ya Nyama Ng’ombe Na Mtindi

Mahitaji

Mchele wa biriani – 5 gilasi

Nyama ya ngombe ya mifupa – 1 ½ kilo na nusu

Vitunguu – 2 kilo

Tangawizi mbichi – ¼ kikombe

Thomu (saumu/garlic) – 3 vijiko vya supu

Mtindi – 2 vikombe

Nyanya ilokatwakatwa (chopped) – 3

Nyanya kopo – 1 kikombe

Masala ya biriani – 2 vijiko vya supu

Hiliki ya unga – 2 vijiko vya chai

Pilipili mbichi ilosagwa – 3 kiasi

Kotmiri ilokatwakatwa – 1 msongo (bunch)

Rangi ya biriani ya manjano – ½ kijiko cha chai

Zaafarani au zaafarani flavour – 1 kijiko cha supu

Mafuta ya kukaangia

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata vitunguu ukaangae katika mafuta mpaka vigeuke rangi ya brown ilokoza.
Weka nyama iwe ilokatwakatwa katika treya au bakuli kubwa la oveni.
Chaganya pamoja na tangawizi, thomu, nyanya, nyanya kopo, mtindi, masala ya biriani, chumvi, pilipili.
Acha irowanike kwa muda wa masaa mawili takriban.
Funika kwa karatasi ya jalbosi (foil paper) utie katika oveni upike muda wa dakika 45 takriban mpaka nyama iwive na huku unachanganya changanya sosi. Ikiwa ina maji ongezea nyanya kopo iwe nzito.
Epua funua, kisha vuruga vitungu umwagie pamoja na kotmiri na umwagie mafuta ya moto kiasi.
Ongezea kutia masala ya biriani na hiliki ya unga.
Chemsha mchele nusu kiini, mwaga maji chuja, umwagie juu ya sosi ya nyama ukipenda kuchanganya au chemsha wali pekee.
Nyunyizia rangi ya biriani pamoja na zaafarani flavour au zaafarani yenyewe ukipenda.
Mimina mchele juu ya masala ya nyama, funika urudishe ndani ya oven upike muda wa kiasi ya dakika ishirini.
Epua upake kwa kuchota wali kwanza kisha masala uwekee juu yake, kiwa tayari.

Jinsi ya kupika Visheti

Viamba upishi

Unga 2 Vikombe

Samli au shortening ya mboga 2 Vijiko vya supu

Maziwa ¾ Kikombe

Iliki Kiasi

Mafuta ya kukarangia Kiasi

Shira

Sukari 1 Kikombe

Maji ¾ Kikombe

Vanila ½ Kijiko cha chai

Zafarani (ukipenda) Kiasi

Jinsi ya kupika na kuandaa

Katika kisufuria pasha moto maziwa na wakati huo huo chemsha Samli katika kisufuria kengine.
Tia unga katika bakuli na iliki, kisha mimina samli iliyochemka na huku unachanganya, kisha tia maziwa na uwendele kuchanganya vizuri isiwe na madonge, ikiwa maziwa haitoshi ongeza maji kidogo.
Kisha uwache unga ukae mahali pa joto kwa muda wa dakika 10 hivi.
Halafu fanya viduara vidogo vidogo, kisha finyiza kwenye greta yenye vishimo vidogo ili upate umbo kama kwenye picha.
Kisha karanga kwenye mafuta yaliyopata moto hadi vibadilike rangi ya dhahabu, kisha viepue vichuje mafuta.
Chemsha shira, ikiwa tayari mimina visheti na upepete na kuzichanganya zipate shira kote.
Weka kwenye sahani na zitakuwa tayari kwa kuliwa na kahawa.

Jinsi ya kutengeneza Fagi Ya Kumumunyuka Mdomoni

VIAMBAUPISHI

Maziwa mazito matamu (condensed milk) – 2 vibati

Sukari – 1 kikombe

Samli 1 ½ kikombe

Vanilla 2 kifuniko cha chupa yake

Hiliki ilosagwa – 2 vijiko vya chai

Sinia kubwa ya bati Paka samli

MAANDALIZI

Changanya maziwa, sukari na samli katika sufuria isiyogandisha chakula (non-stick) uweke katika moto.
Koroga huku ikipikika hadi ianze kugeuka rangi na kuanza kuachana. Usiache mkono kuroga isije kufanya madonge.
Tia hiliki na vanilla, endelea kuipika.
Itakapogeuka rangi vizuri mimina katika sinia na haraka uitandaze kwa mwiko huku ukiuchovya katika maji na kuendelea kuitandaza hadi ikae sawa kote.
Pitisha kisu kuikataka ili ikipoa iwe wepesi kuitoa vipande.

Kila inapozidi kupoa na kukaa ndipo fagi inakauka na kumumunyuka.

Mapishi ya Mitai

VIAMBAUPISHI

Unga wa ngano – magi 2 (vikombe vikubwa)

Hamira kijiko 1 cha chai

Sukari Vijiko 2 vya supu

Maziwa ¾ Magi

Siagi Vijiko 2 vya supu

Mafuta ya kukaangia kiasi

VIAMBAUPISHI:SHIRA

Sukari ¾ Kikombe

Maji ¾ Kikombe

Illiki ya unga kiasi

Zafarani kiasi

JINSI YA KUPIKA

Katika bakuli, changanya vipimo vyote pamoja na ukande unga usiwe mgumu wala laini sana uwe kiasi.
Kisha fanya donge moja na iache pahali penye joto mpaka iimuke.
Halafu weka mafuta ya kukaangia kwenye moto.
Sukuma donge hadi liwe duara sio nyembamba sana, kisha katakata kama maandazi.
Mafuta ya kisha pata moto choma mittai hukuunazigeuza hadi ziwive na kugeuka rangi.
Katika sufuria tia vipimo vya shira na iache ichemke isiwe nzito sana.
Mimina mitai kwenye shira na uzipepete, kisha weka kwenye sahani na zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika Wali Wa Sosi Ya Tuna

Viambaupishi

Sosi Ya tuna

Tuna (samaki/jodari) 2 Vikopo

Vitunguu (kata kata) 4

Nyanya zilizosagwa 5

Nyanya kopo 3 Vijiko vya supu

Viazi (vilivyokatwa vipande vidogo – cubes) 4

Dengu (chick peas) 1 kikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic)&Tangawizi iliyosagwa 1 Kijiko cha supu

Hiliki 1/4 kijiko cha chai

Mchanganyiko wa bizari 1 kijiko cha supu

Chumvi kiasi

Pilipili manga 1 Kijiko cha chai

Vipande cha Maggi (Cube) 2

Wali

Mchele 3 Vikombe vikubwa (Mugs)

Mdalasini 2 Vijiti

Karafuu chembe 5

Zaafarani kiasi

*Jirsh (Komamanga kavu au zabibu kavu -raisins) 1/2 Kikombe

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Kosha Mchele na roweka.

2. Kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi (brown) chuja mafuta uweke kando.

3. Kaanga viazi, epua

4. Punguza mafuta, kaanga nyanya.

5. Tia thomu/tangawizi, bizari zote, vipande vya Maggi, nyanya kopo, chumvi.

6. Mwaga maji ya tuna iwe kavu, changanyisha kwenye sosi.

7. Tia zaafarani kidogo katika sosi na bakisha ya wali.

8. Chemsha mchele pamoja na mdalasini na karafuu.

9. Karibu na kuwiva, chuja maji utie katika chombo cha kupikia katika jiko (oven)

10. Nyunyizia zaafarani, mwagia vitunguu, viazi, na dengu juu ya wali.

11. Mwagia sosi ya tuna na pambia jirshi (au zabibu).

12. Funika wali na upike katika jiko moto wa 450º kwa muda wa kupikika wali.

* Jirsh (komamanga) kavu zioshwe vizuri kutoa vumbi au tumia zabibu kavu (raisins)

Mapishi ya Pilau ya nyama ya ng’ombe na kachumbari

Mahitaji

Mchele (rice vikombe 3)
Nyama ya ng’ombe (beef 1/2 kilo)
Viazi mbatata (potato 3)
Vitunguu maji (onions 3)
Kitunguu swaum (garlic cloves 4)
Tangawizi iliyosagwa (ginger kiasi)
Hiliki nzima (cardamon 4)
Karafuu (clove 4)
Pilipili mtama (blackpepper 4)
Amdalasini (cirnamon stick 1)
Binzari nyembamba nzima(cumin seeds 1/2 ya kijiko cha chai)
Binzari nyembamba ya kusaga (ground cumin 1 kijiko cha chai)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)
Nyanya (fresh tomato 3)
Limao (lemon 1)
Pilipili (chilli 1)
Hoho (green pepper)

Matayarisho

Chemsha nyama na chumvi na nusu ya limao mpaka iive kisha weka pembeni. Baada ya hapo andaa vitu vya pilau kwa kuloweka mchele kwenye maji kwa muda wa dakika 10.Menya na kukatakata vitunguu na viazi kisha weka pembeni na pia chemsha maji ya moto na uweke pembeni. Baada ya hapo weka sufuri jikoni na tia mafuta kiasi . Yakisha pata moto tia vitunguu na uvikaange mpaka viwe vya rangi ya kahawia na kisha uitie nyama na ikaange mpaka ipate rangi ya bown pia. Baada ya hapo tia kitunguu swaum na tangawizi na uikoroge vizuri kisha iache ikaangike kwa muda wa dakika 2 kisha tia spice ambazo ni Binzari nyembamba ya unga, hiliki,karafuu, amdalasini na pilipili mtama na viazi. Baada ya hapo unatakiwa ugeuze geuze mpaka mchanganyiko uchanganyike vizuri kisha tia mchele na ugeuzege mpaka uchanganyike na viungo. Baada ya hapo tia chumvi na maji ya kutosha na ukoroge vizuri kisha funika na uache uchemke katika moto wa wastani. Maji yakikaribia kukauka tia binzari nyembamba nzima na ufunike uache mpaka maji yakauke kabisa. maji yakisha kauka ugeuze na ufunike tena na uuache mpaka uive.
Baada ya hapo andaa kachumbali kwa kukatakata vitunguu katika bakuli na kisha tia chumvi kwa ajili ya kuondoa ukali wa vitunguu. Baada ya hapo vioshe mpaka chumvi yote iishe. osha nyanya, Pilipili, hoho na kisha katakata slice nyembamba na uchanganye na vitunguu. Baada ya hapo tia chumvi, kamulia limao na uchanganye zote pamoja. Baada ya hapo chakula kitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kutengeneza Wali Wa Dengu Kwa Samaki Wa Kukaanga

Mahitaji

Mchele wa basmati – 3 Vikombe

Dengu – 2 vikombe

Viazi – 3 vikubwa

Kitunguu – 2 kubwa

Nyanya – 2

Pilipili mbichi kubwa – 3

Pilipilimanga – ½ kijiko cha chai

Garama Masala (bizari mchanganyiko) -1 kijiko cha chai

Supu ya vidonge (stock cubes) – 2 vidonge

Chumvi – kiasi

Mafuta – ¼ kikombe

Zaafarani – 1 kijiko cha chai

Samaki wa kukaanga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Dengu kama sio za tayari kwenye kopo, roweka na zichemshe hadi ziwive

Maandalizi ya Masala Ya Dengu:

Zaafarani – iroweke katika maji ya dafu dafu (warm) ya chini ya robo kikombe weka kando.
Osha mchele, roweka.
Menya viazi na vitunguu, katakata vitunguu, na nyanya , weka kando.
Katakata viazi vipande vidogo vidogo kwa umbo la mchemraba (cubes).
Katika sufuria tia mafuta yakipata moto, tia viazi ukaange kidogo kwa moto mdogo mdogo hadi kukaribia kuwiva, toa weka kando.
Kaanga vitunguu hadi vigeuka rangi ya hudhurungi isiyokoza (light brown) kisha tia nyanya ukaange kidogo.
Tia vidonge vya supu (stock cubes) uvivuruge katika mchanganyiko, katakata pilipili mbichi kwa urefu tia, uendelee kukakaanga. Tia bizari, chumvi.
Zima moto, changanya dengu na viazi katika mchanganyiko huo.

Mapishi ya Wali:

Chemsha mchele kama kawaida ya kupika wali mweupe, kiini kiwe kimewiva nusu yake.
Chuja maji kisha changanya katika mchanganyiko wa dengu.
Nyunyizia zaafarani, uchanganye wali na mchanganyiko kidogo tu.
Funika acha uive katika mtoto mdogo mdogo au tia katika oveni hadi uive kama kawaida ya kupika wali.
Pakua katiha sahani na tolea na samaki yoyote wa kukaanga.

Mapishi ya Chapati za maji za vitunguu

Mahitaji

Unga wa ngano (plain flour) 1/4
Kitunguu kikubwa (chopped/slice onion) 1
Yai (egg) 1
Chumvi (salt)
Mafuta (cooking oil)

Matayarisho

Tia unga, chumvi na maji kiasi katika bakuli kisha koroga mpaka madonge yote yaondoke. Baada ya hapo tia yai na vitunguu kisha koroga tena mpaka mchanganyiko wote uchanganyike vizuri. baada ya hapo choma chapati zako kama kawaida (jinsi ya kuchoma unaweza kuangalia kwenye recipe yangu ya chapati za maji katika older posts) na baada ya hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About