Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi – Saladi ya Matunda

Matunda ni mojawapo wa kundi la vyakula, ni muhimu sana kwa afya bora. Matunda yakitengenezwa vizuri yanavutia sana na yanakuwa ni chakula kizuri sana.

Mahitaji

Embe iliyoiva kiasi
Nanasi
Tango
Tikiti maji
Zabibu
Papai

Matayarisho

1. Ondoa maganda kwenye embe, nanasi, tango, papai na tikiti maji kisha kata kata vipande vidogo vidogo vya mraba

2. Changanya vipande vya matunda kwenye bakuli safikisha weka na zabibu zilizotolewa kwenye kikonyo chake.

3. Weka kwenye friji yapate ubaridi kidogo

4. Saladi yako tayari kwa kuliwa

Waweza kula saladi hii kama mlo wa kati au kama mlo kamili wa usiku.

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Cornflakes

MAHITAJI

Unga – 1 Kikombe

Sukari ya kusaga – 3/4 Kikombe

Siagi – 125 gms

Yai – 1

Baking powder – 1/2 kijiko cha chai

Zabibu kavu – 1/2 kikombe

Cornflakes iliyovunjwa (crushed) – 2 Vikombe

Vanilla – 1 kijiko cha chai

MAANDALIZI

Tia kwenye mashine ya kusaga (blender) au mashine ya keki, siagi, yai na vanilla uchanganye hadi ichanganyike vizuri.
Tia baking powder, zabibu na unga na changanya vizuri.
Paka siagi sinia ya kupikia ya oveni.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Weka cornflakes katika sahani ya chali (flat) na zungusha viduara humo kisha upange katika sinia ya oveni.
Pika katika moto wa 350ºF kwa muda wa dakika 20-25 hadi vigeuke rangi na viwive.

Jinsi ya kuandaa Pilau ya sosi ya soya, nyama na mboga

Mahitaji

Nyama isiyokuwa na mifupa – 1 ½ Lb(ratili)
Mchele wa Basmati (rowanisha) – 3 Magi
Vitunguu maji – 2
Mchanganyiko wa mboga za barafu – 1 Magi
(karoti, mahindi, njegere)
Pilipili Mbichi – 3
Pilipili mboga kijani na nyekundu – 1
Pilipili manga – ½ kijiko cha chai
Chumvi – Kiasi
Sosi ya soya (soy sauce) – 5 Vijiko vya supu
Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 Kijiko cha supu
Mchanganyiko wa bizari (garam masala) – 1 Kijiko cha supu
Kotmiri iliyokatwa – ½ Kikombe
Mafuta ya kukaangia – Kiasi

Namna Ya Kutaarisha

Ndani ya sufuria, tia mafuta yakipata moto kaanga vitunguu mpaka ziwe rangi ya hudhurungi.
Kisha tia nyama iliyokatwa vipande vidogo vidogo pamoja na maji ya kiasi na viungo vyote isipokuwa mchele, mboga zote na kotmiri. chemsha mpaka nyama iwive na maji yakauke.
Halafu changanya na mboga na iwache kwa muda wa dakika kumi kisha tia kotmiri na umimine kwenye bakuli au treya ya oveni na uweke kando.
Chemsha mchele na chumvi uwive kama kawaida ya kupika wali wa kuchuja, kisha umwagie juu ya ile treya ya nyama.
Nyunyizia mafuta na sosi ya soya na ipike katika oveni moto wa 350° kwa muda wa dakika 20 hivi.
Ukishawiva, uchanganye ukiwa tayari kwa kuliwa

UNYONYESHAJI BORA WA MAZIWA YA MAMA

• Maziwa ya mama pekee ndio chakula na kinywaji cha mtoto bora zaidi kwa watoto kwa miezi sita ya kwanza.
• Ni jambo la muhimu sana kunyonyesha watoto wachanga kwa muda wa miezi minne na uendelee kunyonyesha hadi mtoto atakapofikisha mwaka mmoja na kuendelea.

• Mtoto akifikisha miezi sita ndio wakati muafaka wa kumpa vyakula vya nyongeza vilivyotayarishwakatika hali ya usafi.

• Onana na mnasihi akushauri kuhusu muda na jinsi ya kumuanzishia mtoto wako vyakula vya nyongeza

• Vyakula vya ngogeza viwe ni vya mchanganyiko wa makundi yafuatayo ya chakula:- vyakula vya nafaka, venye asili ya nyama, mbogamboga na matunda, mafuta na sukari (kiasi). Lisha kila chakula kwa siku kadhaa kwa kufuatanisha kabla hujaaza chakula chengine kipya.

• Usimuachilie mtoto alale kama chupa ya maziwa ingali mdomoni, ili kuepukana na kuoza kwa meno na madhara ya.

• Watoto wanaopewa maziwa ya mama pekee hawaugui mara kwa mara, na wakiugua, makali ya ugonjwa hupungua na hupona mapema kwa sababu yale maziwa ya mwanzo ya njano yenye viini vingi vya kumkinga dhidi ya magonjwa.

Jinsi ya kupika Biskuti Nyembamba (Wafer Bar) Za Chokoleti Na Njugu

MAHITAJI

Wafer Powder/gram wafer (unga wa biskuti uliosagwa wa tayari) – vikombe 2

Maziwa ya Mgando Matamu ya Kopo – 2 vikombe

Nazi iliyokunwa – ½ Kikombe

Chokoleti vipande vipande – 1 Kikombe

Njugu vipande vipande – ½ Kikombe

Siagi – 227 g

MAPISHI

Yeyusha siagi motoni kisha changanya na unga wa wafer acha kidogo motoni
Mimina katika treya unayochomea itandaze vizuri, kisha mimina maziwa juu yake pamoja na njugu vipande , nazi iliyokunwa na vipande vya chokoleti.
Choma (bake) kwenye oveni kwa moto wa 350ºC kwa dakika 20.
Katakata tayari kwa kuliwa

Jinsi ya kupika Pilau ya Mpunga Na Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Mpunga – 4 vikombe

Nyama – 1 kilo moja

Kitunguu maji – 3

Mbatata/viazi – 7 vidogodogo

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi ilosagwa 3 vijiko cha supu

Bizari nzima/ya pilau/uzile/cumin – 3 vijiko vya supu

Mdalasini – 3 vipande

Hiliki – 7 punje

Pilipili manga nzima – 1 kijiko cha supu

Chumvi kiasi

Mafuta – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele weka kando
Katakataka vitunguu slice ndogo ndogo.
Weka mafuta katika sufuria kisha ukaange vitunguu pamoja na mdalasini, hiliki pilipilimanga.
Vitunguu vikigeuka rangi unatia kitunguu thomu na tangawizi.
Tia supu kidogo na nyama, kisha tia bizari ya pilau/uzile, na viazi/mbatata.
Maliza kutia supu yote, na ikiwa ni kidogo ongeze maji kiasi cha kuivisha mchele. kisha tia mchele ufunike hadi wali uwe tayari.
Ikiwa unatumia mkaa palia juu yake, ikiwa hutumii uache uive kwa moto mdogo mdogo.

Mapishi ya Wali Wa Kukaanga Kwa Kidari Cha Kuku (Chicken Breast) Wa Kukausha

Viambaupishi

Vipimo vya Wali:

Mchele 3 vikombe

*Maji ya kupikia 5 vikombe

*Kidonge cha supu 1

Samli 2 vijiko vya supu

Chumvi kiasi

Hiliki 3 chembe

Bay leaf 1

Viambaupishi: Kuku

Kidari (chicken breast) 1Kilo

Kitunguu 1

Tangawizi mbichi ½ kipande

Kitunguu saumu(thomu/galic) 7 chembe

Pilipili mbichi 3

Ndimu 2

Pilipilimanga 1 kijiko cha chai

Mdalasini ½ kijiko cha chai

Jira/Cummin ya unga 1 kijiko cha chai

Maji ¼ kikombe

Jinsi ya kuandaa na kupika

Wali:

Osha na roweka mchele kisha weka sufuria katika moto tia samli ipashe moto.

Tia hiliki, bay leaf, kaanga, kisha tia mchele ukaange kidogo.

Tia maji, chumvi na kidonge cha supu, upike wali kama unavyopika pilau.

*Maji kisia kwa kutegemea mchele ulivyo.

  • Unaweza kutumia supu yoyote badala ya kidonge.

Kuku:

Katakata kidari cha kuku vipande vya kiasi, weka katika sufuria, tia ndimu, bizari zote, chumvi.

Katakata kitunguu vipande vidogodogo, pilipili, na kitunguu thomu (chopped), tia katika kuku.

Chuna tangawizi mbichi tia katika kuku. Changanya vitu vyote vizuri.

Tia maji kiasi ¼ kikombe tu kiasi cha kumkaushia kuku. Weka katika moto mpike huku unageuzageuza. Anapokaribia kukauka epua akiwa tayari kuliwa na wali (na saladi upendayo)

Jinsi ya kupika Visheti Vya Kastadi Vya Shepu Ya Kombe

Viamba upishi

Unga wa ngano 1 Kilo

Siagi ¼ kilo

Mayai 2

Kastadi (custard) 3 vijiko vya supu

Baking powder 1 kijiko cha chai

Maziwa 1 ½ gilasi

Mafuta Ya kukaangia kiasi katika karai

Maandalizi na upikaji

Weka unga katika bakuli kubwa kisha changanya na unga wa kastadi na baking powder.
Tia siagi uchanganye vizuri.
Tia mayai, kisha maziwa ya baridi uchanganye vizuri usiukande sana.
Fanya madonge kisha kata vipande vidogovidogo kisha ubonyeze kwa kidole uvikwaruze kwenye chujio lenye tundu itokee shepu (design) yake.

5- Tia mafuta katika karai yakipata moto, kaanga visheti hadi viive. Usiache hadi vikageuka rangi sana.

6- Eupua, weka katika sufuria au chombo kikubwa kusubiri shira.

Vipimo Vya Shira

Sukari ½ kilo

Hiliki ilosagwa 1 kijiko cha chai

‘arki (rose flavor) 5 matone

Maji 1 gilasi

Namna Ya Kutyarisha

Changanya sukari na maji uipike hadi iwe nzito.
Ukiona mapovu yanatoka tia hilik na ‘arki .
Mwagia katika visheti uchanganye vizuri hadi vishike na sukari.

Mapishi ya Tende Ya Kusonga Ya Lozi Na Cornflakes

VIAMBAUPISHI

Tende zilizotolewa kokwa – 1 Kilo

Cornflakes – 1 ½ kikombe

Lozi Zilokatwa katwa – 1 kikombe

Siagi – ¼ kilo

MANDALIZI

Mimina tende na siagi kwenye sufuria bandika motoni moto mdogo mdogo mpaka zilainike. Kwa muda wa dakika 10.
Isonge kidogo kwa mwiko au kuikoroga ichanganyike vizuri.
Changanya Cornflakes na lozi kwenye tende mpaka zichanganyika vizuri.
Pakaza treya au sinia mafuta au siagi kidogo.
Mimina mchanganyiko wa tende, zitandaze vizuri na ukate vipande saizi unayopenda. Zikiwa tayari kuliwa kwa kahawa.

Jinsi ya kupika Roast ya biringanya na mayai

Mara nyingi biringanya hutumika kama kiungo cha nyongeza katika mchuzi. Hata hivyo, kiungo hiki kinaweza kupikwa chenyewe na kutoa mchuzi wenye ladha ya kipekee.

Baadhi ya wapishi wameweza kubuni aina hii ya upishi ambayo huweza kupikwa kwa dakika tano tu na kukupa chakula kitamu chenye ladha ya kuvutia.

Uzuri wa chakula hi ni kwamba kinaweza kuliwa wakati wowote na kwa chakula chochote kulingana na matakwa ya mlaji.

Kwa mujibu wa wataalamu wa maswala ya mapishi, biringanya ni miongoni mwa vyakula vyenye mapishi mengi kama ilivyo kwa mchele.
Hapa tutaenda kuona jinsi ya kupika roast ya biringanya na mayai.

Mahitaji:

Biringanya 2 kubwa
Nyanya 4 kubwa
Kitunguu maji kilichosagwa kijiko 1 cha mezani
Mayai 2
Mafuta ya mzeituni vijiko vitatu vya mezani
Chumvi kiasi
Pilipili 1 (kama unatumia)
Hoho 1
Karoti 1
Kitunguu swaumu kilichosagwa 1
Kotimili fungu 1

Maadalizi:

Chukua biringanya ioshe vizuri na kasha katakata vipande vidogo vidogo.
Osha na menya nyanya hapafu katakata. Fanya hivyo kw akaroti na hoho pia.
Weka mafuta kwenye sufuria na weka jikoni kwenye moto kiasi
Yakishachemka maji na kasha weka kitunguu maji na kasha swaumu huku ukikaanga taratibu.
Weka hoho na karoti huku ukiendelea kukaanga. Baada ya hapo weka nyanya na baadae chumvi. Funika hadi ziive kabisa na kasha weka majani ya kotimili.
Weka biringanya. Acha vichemke hadi viive. Koroga ili kuruhusu mchanganyiko wako uchanganyike vizuri.
Kwa kuwa biringanya ina majimaji huhitaji kuweka maji ya ziada, weka pilipili.
Acha kwa muda wa dakika tatu hadi dakika tano. Pasua mayai na kisha miminia huku ukikoroga taratibu. Fanya hivyo hadi yaive kabisa na kuwa mchuzi mzito. Roast yako ya biringanya iko tayari kwa kuliwa
Unaweza kula aina hii ya mboga na mikate, maandazi na hata ugali

Mapishi ya Wali maharage,mchuzi wa samaki na spinach

Mahitaji

Mchele (rice 1/2 kilo)
Maharage yaliyochemshwa (boiled red kidney beans 1 kikombe cha chai)
Samaki waliokaangwa ( 2 fried fish)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1/2 ya tin)
Vitunguu vilivyokatwa (onion 2)
Kitunguu swaum (garlic 3 cloves)
Tangawizi (ginger kiasi)
Limao (lemon 1/2)
Chumvi (salt)
Pilipili (scotch bonnet pepper 2)
Mafuta (vegetable oil)
Spinach
Tui la nazi (coconut milk 1 kikombe cha chai)

Matayarisho

Saga nyanya, kitunguu, tangawizi na kitunguu swaum pamoja. Tia kwenye sufuria na upike mpaka maji yakauke kisha tia curry powder, mafuta na chumvi na upike tena mpaka mchanganyiko uive kisha tia samaki na limao na maji kiasi na uache uchemke kiasi. Na hapo mchizi utakuwa tayari.
Osha na uzikate spinach kisha kaanga kitunguu na mafuta kiasi (hakikisha visiwe vya brown kisha tia spinach na chumvi. zipike kwa muda wa dakika 3-4 na hapo zitakuwa tayari zimeshaiva.
Wali: Chemsha maji kiasi kisha tia, chumvi, pilipili nzima(isikatwe) mafuta na tui la nazi. Baada ya hapo koroga na utie mchele na maharage na ufunike uache uchemke mpaka maji yakauke. Kisha geuza na ufunike tena na uuache mpaka uive. Baada ya hapo chakula chako kitakuwa tayari kwa kuseviwa.

Jinsi ya kupika Magimbi Kwa Nyama Ya Ng’ombe

Vipimo

Majimbi (Eddoes) kiasi 6 au 7

Nyama ng’ombe ½ kilos

Tangawizi ilosagwa 1 kijiko cha kulia

Haldi (bizari manjano/turmeric) ½ kijiko cha chai

Tui zito la nazi vikombe 2

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha nyama kisha weka chumvi, bizari ya manjano, tangawizi mbichi, ukaushe kwanza katika sufuria kwa kukaanga kaanga.
Ikianza kukauka, weka maji funika uchemshe iwive.
Menya majimbi ukate kate na uweke katika sufuria nyengine.
Mimina supu na nyama katika majimbi uchemshe yawive majimbi.
Mwisho weka tui zito la nazi uchanganye vizuri kisha weka katika moto kidogo tu bila kufunika yakiwa tayari.

Jinsi ya kupika Biriani Ya Nyama Mbuzi Ya Mtindi Na Zaafaraan

Vipimo – Nyama

Nyama mbuzi – 1 kilo

Kitunguu menya katakata – 1

Nyanya/tungule – 2

Thomu (kitunguu saumu/garlic) saga – 5 chembe

Tangawizi mbichi – kuna/grate au saga – 1 kipande

Pilipili mbichi saga – 2

Bizari ya pilau nzima (cumin seeds) – ½ kikombe cha kahawa

Mdalasini – 1 kijiti

Karafuu nzima – 5 chembe

Gilgilani/dania (coriander seeds) – ½ kikombe cha kahawa

Bizari ya mchuzi – 1 Kijiko cha supi

Chumvi – Kiasi

Mtindi – 1 glass

Hiliki ilopondwa – 2 vijiko vya chai

Vitunguu – menya katakata slices kwa ajili ya kukaanga- 7- 9

Mafuta – Kiasi ya kukaangai vitunguu

Vipimo – Wali

Mchele wa pishori/basmati – 4 glass

Zaafarani roweka katika kikombe cha kahawa – Kiasi

Mafuta – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katika sufuria, changanya nyama pamoja, kitunguu kimoja, tangawizi, thomu, nyanya, na viungo vyake isipokuwa mtindi, hiliki na vitunguu vilobakia.

Tia maji kisha funika ichemke mpaka iwive nyama na ikauke supu.

Tia mtindi na hiliki changanya pamoja.

Weka mafuta katika karai, kaanga vitunguu mpaka viwe rangi ya hudhurungi. Toa uchuje mafuta. Kisha viponde ponde kwa mkono uchanganye na nyama.

Chemsha mchele uive nusu kiini, mwaga maji.

Mimina katika nyama utie zaafarani, funika upike wali hadi uwive.

Epua ukiwa tayari.

Mapishi ya wali wa Kiafrika Mangaribi

Mahitaji

Mchele (rice vikombe 2 na 1/2)
Vitunguu (onion 2)
Nyanya ya kopo (tin tomato kopo 1)
Tangawizi (ginger paste kijiko 1 cha chakula)
Kitunguu swaum (garlic paste kijiko 1 cha chakula)
Paprika (kijiko 1 na 1/2 cha cha chai)
Pilipil (scotch bonnet pepper 1)
Curry powder (kijiko 1 cha chai)
Maggi cubes 3(unaweza kutumia yenye ladha ya chicken, beef au vegetable. Inategemea unasevu na mchuzi wa aina gani)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Loweka mchele kwa muda wa dakika 10.Katakata vitunguu kisha weka pembeni, saga pamoja nyanya ya kopo,pilipili, tangawizi na kitunguu swaum kisha weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu vikiiva tia curry powder, maggi cubes, chumvi na paprika na uchanganye vizuri. Kisha tia mchanganyiko wa nyanya na uupike mpaka uive. Baada ya hapo tia mchele na maji na uupike mpaka ukaribie kuiva kisha ugeuze na umalizie kwa kutia njegere na umalizie kuupika mpaka uive. baada ya hapo utakuwa tayari kuseviwa na mboga yoyote kama kuku, nyama, samaki au assorted meat (Mchanganyiko wa utumbo, makongoro na nyama), Hapo mimi nili-save na mchuzi wa kuku wa kienyeji.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About