Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Mandazi Matamu

Mahitaji

Unga wa ngano (nusu kilo)
Sukari (Kikombe 1 cha chai)
Chumvi (nusu kijiko cha chai)
Hamira (kijiko kimoja cha chai)
Yai (1)
Maziwa ya unga (vijiko 2 vya chakula)
Butter (kijiko 1 cha chakula)
Hiliki (kijiko1 cha chai)
Maji ya uvuguvugu ya kukandia
Mafuta ya kuchomea

Matayarisho

Tia unga kwenye bakuli kisha tia sukari, chumvi, yai, maziwa ya unga, butter na hiliki kisha uchanganye pamoja mpaka mchanganyiko wote uchanganyike vizuri. Baada ya hapo tia maji ya uvuguvugu kiasi na uanze kuukanda. Ni vizuri ukaukanda kwa muda wa dakika 15 ili kuhakikisha donge lote la unga limelainika vizuri.
Baada ya hapo Tawanyishaa unga uliokwandwa katika madonge 4. Tia unga wa ngano kidogo katika kibao cha kusukumia na uanze kusukuma donge moja katika shape ya chapati na hakikisha haiwi nyembamba sana wala nene sana yani inatakiwa iwe ya wastani.Ukishamaliza kusukuma unatakiwa ukate shape uipendayo na uyatandaze katika kitu kilichopo flat na kiwe kimenyunyuziwa unga wa ngano ili kuyazuia yasigandie. Rudia hiyo process kwa madonge yote yaliyobakia. Baada ya hapo yaweke mandazi katika sehemu iliyokuwa na joto ili yaweze kuumuka (inaweza kuchukua masaa 3 kuumuka). Yakisha umuka unatakiwa uweke mafuta katika karai la kuchomea. Yakisha pata joto la kiasi unatakiwa utumbukize mandazi na unaze kuyachoma mpaka yawe ya brown. Yakisha iva yaipue na uyaweke kwenye kitchen towel iliyakauke mafuta. Yakisha poa yatakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Chapati za Kusukuma kitaalamu

Mahitaji

Unga wa ngano (plain flour 1/2 of kilo)
Siagi (butter vijiko 2 vya chakula)
Yai (egg 1)
Chumvi (1/2 ya kijiko cha chai)
Hiliki (ground cardamon 1/4 ya kijiko cha chai)
Maji ya uvuguvugu (warm water)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Weka unga wa ngano katika bakuli la kukandia, kisha tia chumvi na hiliki na uchanganye kwanza, baada ya hapo tia siagi na uichanganye vizuri na unga mpaka ipotee. Baada ya hapo tia tena yai na uchanganye vizuri. Mchanganyiko ukishachanganyika vizuri sasa unaweza kutia maji ya uvuguvugu kidogo, kidogo huku ukiwa unauchanganya ili kupata donge. Baada ya hapo anza kukanda hilo donge mpaka mabuje yote yapotee na unga uwe mlaini, ambapo itakuchukua kama dakika 15. Baada ya hapo tawanyisha unga katika madonge ya wastani (yasiwe makubwa sana au madogo sana) Ukimaliza hapo, andaa kibao cha kusukumia chapati kwa kukitia unga kidogo ili chapati isinatie kwenye kibao. Sukuma donge moja la chapati mpaka liwe flat na kisha weka kijiko kimoja cha mafuta na usambaze. ukisha maliza ikunje (roll). Fanya hivyo kwa madonge yote yaliyobakia.
Baada ya hapo andaa chuma cha kuchomea (fry-pan) katika moto wa wastani. Kisha anza kusukuma chapati (ni vizuri ukaanza na zile ulizozikunja mwanzo ili kuzipa nafasi zile za mwisho ziweze kulainika) ukiwa unasukuma hakikisha zinakuwa flat (na zisiwe nene sana au nyembamba sana) Ukishamaliza hapo tia kwenye chuma cha kuchomea. Acha iive upande mmoja then igeuze upande wa pili. Tia mafuta ama kijiko kimoja kikubwa upande wa chini wa chapati na uanze kuukandamiza kwa juu uku ukiwa unaizungusha. fanya hivyo uku ukiwa unaigeuza kuiangalia kwa chini ili isiungue. ikishakuwa ya brown, geuza upande wa pili na urudie hivyohiyvo mpaka chapati iive. Rudia hii process kwa chapati zote zilizobakia.

Siri ya chapati kuwa laini ni kutia siagi au mafuta ya kutosha kipindi unazikanda na pia kuzikanda mpaka unga uwe laini.

Mapishi ya Ugali, dagaa (wabichi) na matembele

Mahitaji

Dagaa wabichi (Fresh anchovies packet 1)
Unga wa ugali (corn meal flour 1/4 kilo) (unaweza kutumia unga wa choice uipendayo)
Matembele ya kukaushwa (dried sweet potato leaves, handful)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1)
Kitunguu maji (onion 2)
Limao (lemon 1/4)
Pilipili mbuzi nzima bila kukata (scotch bonnet pepper1, do not chop)
Chumvi (salt 1/2 ya kijiko cha chai)
Mafuta (vegetable oil)
Hoho (green pepper 1)
Kitunguu swaum (garlic 5 cloves)
Tangawizi (ginger 1 kijiko cha chai)
Binzari ya curry (Curry powder 1/2 kijiko cha chai)

Matayarisho

Safisha dagaa kwa kutoa vichwa na utumbo kisha waoshe na uwakaushe na kitchen towel na uwaweke pembeni. Baada ya hapo katakata, vitunguu na hoho kisha weka pembeni. Baada ya hapo weka sufuria jikoni na utie mafuta yakisha pata moto tia dagaa na uwakaange mpaka wawe wa brown, kisha tia kitunguu swaum,curry powder na tangawizi, kaanga kidogo kisha malizia kwa kutia vitunguu maji, hoho,pilipili,chumvi na ukamulie limao. Kaanga kwa muda wa dakika 3-4 na hakikisha vitunguu na hoho haviivi sana na hapo dagaa watakuwa tayari.

Baada ya hapo yaoshe na uyaloweka matembele (kama ni makavu) kwa muda wa dakika 15, Kisha yatoe na uyaweke kwenye sufuria pamoja na kitunguu, nyanya, chumvi ,kamulia limao kidogo, pilipili na maji kiasi. acha matembele yachemke kwa muda wa dakika 20 na uhakikishe yameiva kwa kuwa laini. Baada ya hapo yapike mpaka maji yote yakauke na mafuta yatok na hapo matembele yatakuwa tayari.

Ukisha maliza kupika dagaa na matembele andaa chungu cha ugali. Kwanza unatakiwa kuchemsha maji ya moto, kisha koroga pembeni unga kiasi katika maji ya baridi na utie kwenye maji yanayochemka, Fanya kama unatengeneza uji, uji wa ugali ukishachemka tia unga na uanze kuusonga mpaka ugali uive. Ukisha iva pakua na usevu na mboga tayari kwa kuliwa.

Mapishi – Kisamvu cha Karanga

Mapishi yetu leo ni kisamvu cha kuchanganya na karanga. Karibu.

Mahitaji

Majani ya kisamvu
Karanga nusu kikombe
kitunguu kimoja
nyanya mbili
karoti moja
mafuta na chumvi kiasi

Matayarisho

1. Osha kisamvu chako vizuri kisha katakata vipande vidogo vidogo

2. Unaweza kutwanga kwa kutumia kinu au kuchemsha kidogo na kisha kusaga kwa kutumia mashine. Ukitumia mashine uwe makini usije ukasaga sana ukaharibu.

3. Kaanga karanga kidogo na kisha zisage ziwe unga unga.

4. Chemsha kisamvu chako hadi kiive.

5. Katakata kitunguu, karoti na na nyanya

6. Anza kuunga kisamvu kwa kukaanga vitunguu, weka karoti na kisha nyanya na vikishaiva weka kisamvu na koroga pamoja kisha weka karanga. Acha vichemke kwa muda na unaweza pia weka na nazi tui la kwanza.

7. Baada ya muda mfupi epua na kitakiwa tayari. Waweza kula kwa ugali, wali, chapati, makande n.k

Mapishi ya Biriani

Mahitaji

Mchele (rice 1/2 kilo)
Nyama (beef 1/2 kilo)
Vitunguu (onion 2)
Kitunguu swaum (garlic 1 kijiko cha chai)
Tangawizi (ginger 1 kijiko cha chai)
Maziwa mgando (yogurt 1 kikombe cha chai)
Hiliki nzima (cardamon 6)
Amdalasini nzima (cinamon stick 2)
Karafuu nzima (cloves 6)
Pilipili mtama nzima (black pepper 8)
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Binzari manjano (turmaric 1/2 kijiko cha chai)
Binzari nyembamba nzima (cumin 1/4 kijiko cha chai)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Kaanga vitunguu mpaka viwe vya brown kisha tia nyama na uikaange kwa muda wa dakika 10. baada ya hapo tia tangawizi, kitunguu swaum, hiliki(4), amdalasini (1), karafuu (4), pilipili mtama (5), Curry powder, binzari manjano, binzari nyembamba na chumvi. Kisha koroga. Baada ya hapo tia yogurt na uipike mpaka ikauke kisha tia maji kidogo, funika na upunguze moto na uache ichemke kwa muda wa nusu saa.Baada ya hapo nyama itakuwa imeiva na mchuzi kubakia kidogo.Kwahiyo itatakiwa kuiipua.
Loweka mchele kwa dakika 10. kisha chemsha maji mengi kidogo katika sufuria kubwa. baada ya hapo tia hiliki (2) amdalamsini (1) karafuu(2) pilipili mtama (3) chumvi na mafuta kiasi. acha ichemke kidogo kisha tia mchele.Hakikisha maji yameufunika mchele kabisa na uuache uchemke kwa muda wa dakika 8 tu (kwani hautakiwi kuiva kabisa) kisha uipue na uchuje maji yote katika chujio. baada ya hapo chukua sufuria ya kuokea (baking pot kama unayoiona kweye picha) Kisha weka wali nusu na uusambaze sawia kisha weka mchuzi nyama na mchuzi wake pia utandaze na umalizie kwa kuweka leya ya wali uliobakia. Baada ya hapo ufunike na uweke kwenye oven kwenye moto wa 200°C kwa muda wa nusu saa.na baada ya hapo biriani litakuwa tayari kwa kuliwa.

Bisikuti Za Kokoa (Cocoa Biscuits)

Viambaupishi

Siagi 100gm

Unga wa kaukau (cocoa powder) 2 Vijiko vya supu

Maziwa mazito (condensed milk) Moja kikopo (397gm)

Bisikuti za Mary 2 Pakiti

Njugu ½ Kikombe

Karatasi la plastiki

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Vunjavunja bisikuti zote packet mbili ziwe vipande vidogo vidogo.

2. Pasha moto siagi mpaka ipate.

3. Tia kwenya siagi imoto maziwa mazito na cocoa koroga vizuri.

4. Kisha tia kwenye mchanganyiko bisikuti zilizovunjwa na njugu na uchanganye kisha epua motoni.

5. Paka karatasi la plastiki mafuta kidogo halafu tia mchanganyiko kisha kunja (roll).

6. Tia kwenye freeza muda wa saa.

7. Halafu toa karatasi na ukate kate na panga kwenye sahani na itakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kuandaa Pilau ya sosi ya soya, nyama na mboga

Mahitaji

Nyama isiyokuwa na mifupa – 1 ½ Lb(ratili)
Mchele wa Basmati (rowanisha) – 3 Magi
Vitunguu maji – 2
Mchanganyiko wa mboga za barafu – 1 Magi
(karoti, mahindi, njegere)
Pilipili Mbichi – 3
Pilipili mboga kijani na nyekundu – 1
Pilipili manga – ½ kijiko cha chai
Chumvi – Kiasi
Sosi ya soya (soy sauce) – 5 Vijiko vya supu
Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 Kijiko cha supu
Mchanganyiko wa bizari (garam masala) – 1 Kijiko cha supu
Kotmiri iliyokatwa – ½ Kikombe
Mafuta ya kukaangia – Kiasi

Namna Ya Kutaarisha

Ndani ya sufuria, tia mafuta yakipata moto kaanga vitunguu mpaka ziwe rangi ya hudhurungi.
Kisha tia nyama iliyokatwa vipande vidogo vidogo pamoja na maji ya kiasi na viungo vyote isipokuwa mchele, mboga zote na kotmiri. chemsha mpaka nyama iwive na maji yakauke.
Halafu changanya na mboga na iwache kwa muda wa dakika kumi kisha tia kotmiri na umimine kwenye bakuli au treya ya oveni na uweke kando.
Chemsha mchele na chumvi uwive kama kawaida ya kupika wali wa kuchuja, kisha umwagie juu ya ile treya ya nyama.
Nyunyizia mafuta na sosi ya soya na ipike katika oveni moto wa 350° kwa muda wa dakika 20 hivi.
Ukishawiva, uchanganye ukiwa tayari kwa kuliwa

Jinsi ya Kupika skonzi

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour 2 vikombe vya chai)
Sukari (sugar 1/2 kijiko cha chakula)
Chumvi (salt 1/2 kijiko cha chai)
Hamira (yeast 1/2 kijiko cha chakula)
Baking powder 1/2 kijiko cha chai
Siagi (butter 1/4 ya kikombe cha chai)
Maziwa (fresh milk 3/4 ya kikombe cha chai)(unaweza kutumia maji badala ya maziwa)

Matayarisho

Pasha maziwa yawe ya uvuguvugu kisha weka pembeni, pia yeyusha siagi na uweke pembeni.Baada ya hapo tia kila kitu kwenye bakuli la kukandia kasoro maziwa, na uchanganye vizuri kisha tia maziwa kidogo kidogo katika mchanganyiko huo kisha ukande. Ukimaliza uweke kwenye sehemu ya joto na uache uumuke. Ukisha umuka utawanyishe katika madonge saba Kisha .pakaza mafuta au siagi katika chombo cha kuokea kisha yapange hayo madonge katika hicho chombo na uyaache yaumuke tena (kwa mara ya pili). Baada ya hapo pakaza mafuta juu ya hayo madonge na uyaoke (bake) katika oven (moto 200°C ) kwa muda wa dakika 25 na hapo scones au maskonzi yatakuwa tayari

Mapishi ya Koshari Na Sosi Ya Kuku

Vipimo Vya Koshari

Mchele – 2 vikombe

Makaroni – 1 kikombe

Dengu za brown – 1 kikombe

Vitunguu vilokatwakatwa (chopped) – 2

Nyanya ziilokatwakatwa (chopped) – 4

Nyanya ya kopo – 1 kijiko cha supu

Kitunguu saumu(thomu/galic) ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ya unga – 1 kijiko cha chai

Mdalisini kijiti – 1

Bizari ya pilau (cumin seeds) – 1 kijiko cha supu

Hiliki – 2 chembe

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Chumvi – kiasi

Vipimo Vya Kuku

Kuku – 3 LB

Kitunguu saumu(thomugalic) na tangawizi – 1 kijiko cha supu

Mtindi (yoghurt) – 1 kijiko cha supu

Pilipili ya masala nyekundu – 1 kijiko cha chai

Bizari upendazo – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 1

Vitunguu slesi vilokaangwa – 3

Namna Kutayarisha Kuku

Kata kuku vipande vikubwa kiasi, osha, weka kando achuje maji.
Changanya vipimo vya kuku pamoja katika kibakuli.
Changanya pamoja na kuku, roweka muda wa kiasi nusu saa au zaidi.
Mchome (grill) kuku hadi aive weka kando.

Namna ya Kutayarisha Koshari

Tia mafuta katika sufuria, kaanga vitunguu hadi viive kuwa rangi hudhurungi.
Tia thomu ,mdalisini, bizari ya pilau na hiliki kaanga tena kidogo.
Tia nyanya, pilipili zote, nyanya kopo, chumvi changanya vizuri ukaange kidogo.
Epua sosi acha kando.
Chemsha dengu pamoja na kidonge cha supu ziive nusu kiini na ibakie supu yake. Muda wa kuchemsha dengu inategemea aina yake.
Tia mchele uchanganyike, funika, pika hadi uive vizuri pamoja na dengu
Chemsha makaroni hadi yaive , epua chuja maji.
Changanya pamoja wali wa dengu na macaroni.
Pakua katika sahani, kisha weka juu yake kuku aliyechomwa, mwagia vitunguu vilokaangwa, kisha mwagia sosi.

Jinsi ya kuandaa Muhogo, Samaki Wa Kuchoma Na Bamia

Mahitaji

Mihongo 3 – 4

Tui – 1000 ml

Chumvi – 1 kijiko cha chai

Kitunguu maji kilokatwakatwa – 1

Nyanya mshumaa – 3-4

Pilipili mbichi ndefu – 2-3

Pilipili boga – 2

Namna Ya Kutayrisha Na Kupika

Menya mihogo kisha ikate kate vipande inchi tatu hadi nne, kila kipande kigawe kitoke vipanda vinne. Toa mzizi katikati
Osha mihogo ipange kwenye sufuria ya nafasi na yenye mfiniko, ili upate nafasi ya kutia viungo unavyoona pichani na utokotaji wa tui wahitaji nafasi.
Panga/tandaza kitunguu, nyanya mshumaa/tungule,pilipili mbichi na pilipili boga juu ya mihogo, tia chumvi na tui lote.
Funika sufuria kisha weka jikoni moto wa kiasi kuchemsha tui lipande juu. Hakikisha tui halifuriki na kumwagika kwa kuchungulia au kufunika nusu mfuniko
Kwa mda wa nusu saa hivi ukiona sasa tui linatokota chini chini fuinika mfiniko na upunguze moto mdogo kabisa tui likauke kidogo na liwe zito.
Toa muhogo moja ubonyeze ukiona umewiva zima jiko na wacha sufuria hapo kwa muda wa 10. Mihogo tayari kuliwa.

Kidokezo.

Tui lote huwa chini baada ya mihogo kuwiva unapopakuwa teka kutoka chini uweze kupata uzito wa tui umwagie juu.

Bamia/Mabenda

Bamia – robo kilo

Nyanya – 3

Kitunguu maji – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) ya unga au ilosagwa – 1 kijiko cha chai

Nyanya kopo (tomato paste) – 1 kijiko cha supu

Mafuta – 150 ml

Chumvi -1 kijiko cha chai

Pilipili boga – 1

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Kata vichwa vya bamia kisha zikate kate mara mbili zikiwa kubwa, ikiwa ni ndogo mno haina lazima kuzikata osha tu uweke kando.
Katika sufuria, katakata kitunguu, nyanya, pilipili boga tia ndani viungo hivi ongeza chumvi mafuta, thomu na nyanya kop
Washa moto mdogo mdogo huku umefunika sufuria kwa muda wa dakika 20 kisha ukiona mboga zimeshika kutokota ongeza bamia koroga.
Tia maji 200ml wacha kwa muda wa dakika 15 kupikika tena, ukionja utamu wa mboga na chumvi, hakikisha bamia pia zimewiva. Tayari kuliwa.

Samaki Wa Kuchoma

Samaki (dorado) au mikizi au una – 2 wakubwa (fresh)

Chumvi – 1 kijiko cha chai

Kitunguu saumu(thomu/galic) ya unga au iliyosagwa 1 ½ cha chai

Tangawizi mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Namna Ya Kutayrisha Na Kuchoma

Safisha samaki vizuri mchane chane (slit) kwa ajili ya kuweka masala.
Changanya viungo vyote na chumvi samaki kisha paka katika samaki kote na ndani ya sehemu ulizochanachana. Mroweke kwa muda wa robo saa hivi.
Weka karatasi ya jalbosi (foil paper) katika treya ya oveni. Muweke samaki kisha mpike (grill) kwa moto wa juu achomeke hadi samaki agueke rangi na awive.

Jinsi ya kupika Wali Wa Sosi Ya Tuna

Viambaupishi

Sosi Ya tuna

Tuna (samaki/jodari) 2 Vikopo

Vitunguu (kata kata) 4

Nyanya zilizosagwa 5

Nyanya kopo 3 Vijiko vya supu

Viazi (vilivyokatwa vipande vidogo – cubes) 4

Dengu (chick peas) 1 kikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic)&Tangawizi iliyosagwa 1 Kijiko cha supu

Hiliki 1/4 kijiko cha chai

Mchanganyiko wa bizari 1 kijiko cha supu

Chumvi kiasi

Pilipili manga 1 Kijiko cha chai

Vipande cha Maggi (Cube) 2

Wali

Mchele 3 Vikombe vikubwa (Mugs)

Mdalasini 2 Vijiti

Karafuu chembe 5

Zaafarani kiasi

*Jirsh (Komamanga kavu au zabibu kavu -raisins) 1/2 Kikombe

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Kosha Mchele na roweka.

2. Kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi (brown) chuja mafuta uweke kando.

3. Kaanga viazi, epua

4. Punguza mafuta, kaanga nyanya.

5. Tia thomu/tangawizi, bizari zote, vipande vya Maggi, nyanya kopo, chumvi.

6. Mwaga maji ya tuna iwe kavu, changanyisha kwenye sosi.

7. Tia zaafarani kidogo katika sosi na bakisha ya wali.

8. Chemsha mchele pamoja na mdalasini na karafuu.

9. Karibu na kuwiva, chuja maji utie katika chombo cha kupikia katika jiko (oven)

10. Nyunyizia zaafarani, mwagia vitunguu, viazi, na dengu juu ya wali.

11. Mwagia sosi ya tuna na pambia jirshi (au zabibu).

12. Funika wali na upike katika jiko moto wa 450º kwa muda wa kupikika wali.

* Jirsh (komamanga) kavu zioshwe vizuri kutoa vumbi au tumia zabibu kavu (raisins)

Mapishi ya Ndizi za nazi na utumbo

Mahitaji

Ndizi mshale 10
Utumbo wa ng’ombe 1/2 kilo
Nazi ya kopo 1
Nyanya 1
Kitunguu kikubwa 1
Tangawizi/ swaum 1 kijiko cha chakula
Olive oil kiasi
Limao 1
Chumvi
Curry powder 1 kijiko cha chai
Turmaric 1/2 kijiko cha chai
Coriander ya powder 1/2 kijiko cha chai
Pilipili ya unga 1/2 kijiko cha chai
Pilipili kali nzima (usiipasue)

Matayarisho

Safisha utumbo kisha uweke ktk pressure cooker pamoja na chumvi kiasi, limao, tangawizi, swaum na maji kiasi kisha uchemshe kwa muda wa nusu saa. Baada ya hapo menya ndizi kisha zikate vipande vidogo kiasi ili ziwahi kuiva, kisha ktk sufuria ya kupikia tia vitunguu na nyanya kisha ndizi kwa juu yake na supu ya utumbo kiasi chumvi kidogo na mafuta kiasi kisha bandika jikoni na uchemshe mpaka ndizi zikaribie kuiva. Zikisha karibia kuiva tia utumbo na spice zote, pilipili nzima na tui la nazi kisha changanya vizuri na uache vichemke mpaka ndizi na tui la nazi vitakapoiva na rojo ibaki kiasi. Baada ya hapo Ndizi zako zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Wali, mchicha wa nazi na nyama ya kukaanga

Mahitaji

Mchele (rice 1/2 kilo)
Mchicha uliokatwakatwa (spinach mafungu 2)
Nyama (beef 1/2 ya kilo)
Nyanya (tin tomato 1/2 ya tin)
Nyanya chungu ( garden egg 3)
Kitunguu swaum (garlic cloves 3)
Tangawizi (ginger)
Curry powder
Vitunguu (onion 2)
Limao (lemon 1)
Chumvi
Pilipili (scotch bonnet pepper )
Tui la nazi (coconut milk 1 kikombe cha chai)

Matayarisho

Kaanga kitunguu kikishaiva tia nyanya na chumvi. kaanga mpaka nyanya ziive kisha tia nyanya chungu,curry powder na pilipili 1 nzima, baada ya hapo tia mchicha na uuchanganye vizuri kwa kuugeuzageuza. Mchicha ukishanywea tia tui la nazi na uache lichemke mpaka liive na hapo mchicha utakuwa tayari.
Safisha nyama kisha iweke kwenye sufuria na utie chumvi, tangawizi, limao na kitunguu swaum. Ichemshe mpaka itakapoiva na kuwa laini. Baada ya hapo weka sufuria jikoni na mafuta kidogo yakisha pata moto tia vitunguu na nyama na uvikaange pamoja, kisha tia curry powder na ukaange mpaka nyama na viunguu vya brown. na hapo nyama itakuwa imeiva. Malizia kwa kupika wali kwa kuchemsha maji kisha tia mafuta, chumvi na mchele na upike mpaka uive. Baada ya hapo chakula kitakuwa tayari kwa kuseviwa.

Mapishi ya Wali maharage,mchuzi wa samaki na spinach

Mahitaji

Mchele (rice 1/2 kilo)
Maharage yaliyochemshwa (boiled red kidney beans 1 kikombe cha chai)
Samaki waliokaangwa ( 2 fried fish)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1/2 ya tin)
Vitunguu vilivyokatwa (onion 2)
Kitunguu swaum (garlic 3 cloves)
Tangawizi (ginger kiasi)
Limao (lemon 1/2)
Chumvi (salt)
Pilipili (scotch bonnet pepper 2)
Mafuta (vegetable oil)
Spinach
Tui la nazi (coconut milk 1 kikombe cha chai)

Matayarisho

Saga nyanya, kitunguu, tangawizi na kitunguu swaum pamoja. Tia kwenye sufuria na upike mpaka maji yakauke kisha tia curry powder, mafuta na chumvi na upike tena mpaka mchanganyiko uive kisha tia samaki na limao na maji kiasi na uache uchemke kiasi. Na hapo mchizi utakuwa tayari.
Osha na uzikate spinach kisha kaanga kitunguu na mafuta kiasi (hakikisha visiwe vya brown kisha tia spinach na chumvi. zipike kwa muda wa dakika 3-4 na hapo zitakuwa tayari zimeshaiva.
Wali: Chemsha maji kiasi kisha tia, chumvi, pilipili nzima(isikatwe) mafuta na tui la nazi. Baada ya hapo koroga na utie mchele na maharage na ufunike uache uchemke mpaka maji yakauke. Kisha geuza na ufunike tena na uuache mpaka uive. Baada ya hapo chakula chako kitakuwa tayari kwa kuseviwa.

Shopping Cart
21
    21
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About