Dondoo za Mapishi na Lishe

Jinsi ya kupika Biskuti Nyembamba (Wafer Bar) Za Chokoleti Na Njugu

MAHITAJI

Wafer Powder/gram wafer (unga wa biskuti uliosagwa wa tayari) – vikombe 2

Maziwa ya Mgando Matamu ya Kopo – 2 vikombe

Nazi iliyokunwa – ½ Kikombe

Chokoleti vipande vipande – 1 Kikombe

Njugu vipande vipande – ½ Kikombe

Siagi – 227 g

MAPISHI

Yeyusha siagi motoni kisha changanya na unga wa wafer acha kidogo motoni
Mimina katika treya unayochomea itandaze vizuri, kisha mimina maziwa juu yake pamoja na njugu vipande , nazi iliyokunwa na vipande vya chokoleti.
Choma (bake) kwenye oveni kwa moto wa 350ºC kwa dakika 20.
Katakata tayari kwa kuliwa

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Nazi Wa Nyanya Chungu/Mshumaa/Ngogwe Na Bamia, Mboga Ya Matembele Na Samaki Wa Kukaanga

Vipimo Vya Ugali

Unga wa mahindi – 4

Maji – 6 kiasi kutegemea na aina ya unga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka maji katika moto.

Tia unga kidogo katika kibakuli, koroga ufanye uji.

Maji yakichemka tia kwenye maji uwe uji.

Ujii ikiiva punguza kidogo tia unga kidogokidogo na usonge ugali. Ikiwa unga ni mgumu utaongeza maji ya ule uji ulopunguza usonge hadi uive ukiwa tayari.

Vipimo Vya Mchuzi Wa Nazi Kwa Nyanya Chungu/Mshumaa/Ngogwe Na Bamia

Nyanya chungu/mshumaa/Ngogwe – 7

Bamia – 10

Kitunguu maji – 2

Nyanya/tungule – 2

Tui la nazi jepesi – 2 viwili

Tui la nazi zito – 2

Chumvi – kiasi

Ndimu – 2 mbili kamua

Bizari manjano/haldi/turmeric – ½ kijiko cha chai

Pilipili mbuzi – 3

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata kitunguu maji na nyanya vipande vidogodogo sana kisha weka katika sufuria.

Iache ichemke kwa maji yake ya nyanya, ikishachemka tia maji kidogo kama robo kikombe.

Tia nyanya chungu, bamia na koleza ndimu, chumvi.

Iache ichemke. Inapokuwa tayari imeiva tia tui jepesi endelea kuacha katika moto huku unakoroga kidogo kidogo.

Tui jepesi likipungua kiasi chake, tia tui zito, kisha usiachie mkono koroga ikichemka kidog kiasi cha kuiva tui mchuzi tayari.

Vipimo Vya Mboga Ya Matembele

Matembele – 5 mafungu

Mafuta – ¼ kikombe

Kitunguu maji kilokatwakatwa – 1

Nyanya/tungule – 4

Chumvi – 1

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Punguza miche ya matembele kwa kuikata ncha kisha osha majani yake. Acha yachuje maji .
Weka mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu maji na nyanya hadi viivie.
Tia mboga, Iache ichemke kwa maji yake hadi iive. Ukiona bado haikuiva tia maji kidogo tu.
Ukipenda unatia ndimu kiasi cha kipande kimoja ukamue .

Samaki Wa Nguru Wa Kukaanga

Samaki Wa Nguru – 4 vipande

Kitunguu saumu(thom/galic) na tangawizi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi – 4

Ndimu – 2 kamua

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Mwoshe samaki kisha mtie kitunguu thomu, tangawizi ilosagwa, chumvi, pilipilimbichi ilosagwa, ndimu na bizari ya samaki.
Mwache akolee viungo kwa muda kidogo.
Makaange katika mafuta hadi aive akiwa tayari.

Mapishi ya chipsi na samaki wa kuchoma

Mahitaji

Viazi ulaya (baking potato 5 vya wastani)
Parprika 1 kijiko cha chai
Pilipili mtama ilyosagwa (ground black pepper 1 kijiko cha chai
Kitunguu swaum cha unga (garlic powder 1 kijiko cha chai)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)
Marination za samaki (angalia kwenye recipe ya samaki ya nyuma)

Matayarisho

Osha viazi na maganda yake kisha vikaushe na uvikate vipande vya wastani. Kwa kila kiazi toa vipande 6. Kisha vitie kwenye bakuli na utie parpika, pilipili mtama ya unga, kitunguu swaum cha unga, chumvi na mafuta kama vijiko 2 vya chakula. Changanya pamoja na kisha uvibake katika oven kwa muda wa dakika 25. Hakikisha vinakuwa rangi ya brown. Vikisha iva vitoe.
Wamarinate samaki, na uwaoke kisha wasevu na potato wedges tayari kwa kuliwa
(Jinsi ya kupika samaki, angalia katika recipe za nyuma)

Mapishi ya Biskuti Za Mayai

VIAMBAUPISHI

Unga 3 Vikombe

Sukari ya unga (icing sugar) 1 Kikombe

Siagi 250 gm

Mayai 3

Vanilla 2 Vijiko vya chai

Baking powder 1 Kijiko cha chai

JINSI YA KUPIKA

Koroga siagi na sukari katika mashine ya keki (cake mixer) mpaka iwe laini (creamy).
Tia mayai na vanilla koroga mpaka mchanganyiko uwe laini.
Tia unga na baking powder changanya na mwiko.
Tengeneza round upange kwenye tray utie nukta ya rangi.
Nyunyuzia sukari juu ya hizo round ulizotengeneza kabla huja choma.
Pika (bake) katika oven moto wa 350°F kama muda wa dakika 15 hivi huku unazitazama tazama.

Jinsi ya kupika Donati

Viamba upishi

Unga
2 Magi (kikombe kibuwa cha chai)

Sukari
1/3 Kikombe cha chai
Mayai 5

Siagi 4 Vijiko vya chakula

Hamira 1 Kijiko cha chakula

Baking Powder 1 Kijiko cha chai

Vanilla 1 Kijiko cha chai

Hiliki zilizosagwa 1 Kijiko cha chai

Sukari ya laini ya unga

(icing sugar) 1 Magi

Jinsi ya kuandaa na kupika

Unavunja mayai, unatia sukari, hamira, baking powder, vanilla na hiliki ikisha unapiga kwa kutumia mchapo wa kupigia keki. Unapiga mchanganyiko kwa muda wa dakika tano.

Unatia siagi kwenye sufuria na unaiyayusha na kuipasha moto mpaka iwe moto ikisha unaimimina kwenye mchanganyiko na unapiga tena kwa dakika mbili tu.

Unatia unga kwenye sinia au bakuli kubwa ikisha unamimina ule mchanganyiko kwenye unga na unaukanda kutumia mkono, mpaka ulainike.

Ukiona unga mwingi basi ongeza maziwa kidogo mpaka uwe sawa, na ukiona unga mwepesi sana basi unaweza kuongeza unga kidogo pia mpaka ukae sawa mfano wa unga wa maandazi.

Sukuma na ukate madonge kama unavyoyaona hapo juu. Tumia kifuniko cha chupa kwa kukatia kiduara kidogo katikakti ya madonge.
Ukimaliza kukata madonge yote, yaweke kidogo yavimbe halafu teleka mafuta na uyachome.
Ukitoa kwenye mafuta yachuje moto na kabla ya kupoa yawe moto moto yarovye kwenye icing sugar na uhakikishe yote yameenea sukari juu.
Ukimaliza tia kwenye sahani acha zipowe na zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Wali Wa Tambi Na Kuku Wa Sosi Ya Mtindi

Vipimo Vya Wali

Mchele – 3 vikombe

Tambi – 2 vikombe

Mafuta – ¼ kikombe

Chumvi

Vipimo Vya Kuku

Kuku kidari (boneless) aliyekatwa katwa vipande – 1 Kilo

Kitunguu maji kilichokatwa katwa – 2

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi iliyosagwa – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Paprika – 1 kijiko cha supu

Masala ya kuku (tanduri au yoyote) – 1 kijiko cha supu

Ndimu – 2 vijiko vya supu

Mtindi (yoghurt) au malai (cream) – 1 kikombe

Mafuta – ¼ kikombe

Majani ya kotmiri (coriander) – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Wali:

Osha Mchele, uroweke.
Tia mafuta katika sufuria, kaanga tambi zilizokatwakatwa hadi zigeuke rangi kuwa nyekundu.
Tia mchele endelea kukaanga kidogo.
Tia maji kiasi cha wali kupikika kama unavyopika pilau. Kiasi cha maji kinategemea aina ya mchele
Funika katika moto mdogo mdogo hadi uive ukiwa tayari.

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Kuku

Katika bakuli, changanya vitu vyote isipokuwa mtindi na kitunguu.
Tia mafuta katika karai, kisha tia kitunguu ukaange muda mdogo tu, usikiache kugeuka rangi.
Tia kuku na masala yake, endelea kukaanga, kisha tia mtindi au malai ufunike apikike na kuiva vizuri.
Nyunyuzia kotmiri iliyokatwakatwa ikiwa tayari kuliwa na wali wa tambi.

Mapishi ya Half cake (Keki)

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) kikombe 1na 1/2
Sukari (sugar) 1/4 kikombe
Barking powder 1/2 kijiko cha chai
Magadi soda (bicarbonate soda) 1 kijiko cha chai
Mafuta 2 vijiko vya chai
Mafuta ya kukaangia
Maji ya uvuguvugu kiasi

Matayarisho

Changanya unga na vitu vyote (kasoro mafuta ya kuchomea) kisha ukande (hakikisha unakuwa mgumu) Baada ya hapo sukuma na ukate shape uipendayo (hakikisha unakata vipande vinene kiasi na sio kama mandazi) Baada ya hapo ziweke sehemu yenye joto na uache ziumuke. Zikisha umuka zikaange katika moto mdogo ili ziive mpaka ndani. Zikisha iva zitoe na uziweke katika kitchen towel ili zichuje mafuta. Ziache zipoe na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya bagia na chatney ya machicha ya nazi

Mahitaji

Kunde (Ila mimi nilitumia Nigerian brown beans 1/2 kilo)
Vitunguu maji (onion 2)
Pilipili (scotch bonnet pepper 2)
Vitunguu swaum (garlic 4 cloves)
Chumvi (salt)
Barking powder (1/2 kijiko cha chai)
Machicha ya nazi (grated coconut 1 kikombe cha chai)
Limao (lemon 1)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Loweka kunde usiku mzima kisha ziondoe maganda na uzitie kwenye blender pamoja na vitunguu maji, vitunguu swaum, pilipili, chumvi,barking powder na maji kiasi. Visage vitu vyote mpaka viwe laini na kisha uutoe na kuweka kwenye chujio ili uchuje maji. baada ya hapo zikaange katika mafuta mpaka ziwe za brown na uzitoe na kuziweka kwenye kitchen towel ili zichuje mafuta.Baada ya hapo saga machicha ya nazi,limao, pilipili chumvi pamoja na maji kidogo na hapo chatney yako itakuwa tayari kwa kuseviwa na bagia.

Jinsi ya kupika Biriyani Ya Nyama Ng’ombe

Viambaupishi Vya Masala

Nyama vipande – 3 LB

Mtindi – ½ kopo

Kitunguu (thomu/galic) – 1½ kijiko cha supu

Tangawizi – 1½ kijiko cha supu

Nyanya – 2

Pilipili mbichi – kiasi

Nyanya kopo – 4 vijiko vya supu

Vidonge supu – 2

Pilipili nyekundu paprika – kiasi

Bizari zote saga – 2 vijiko vya supu

Viazi – 4

Mafuta – 2 mug

Samli – ½ kikombe

Vitungu – 6

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika masala

Kwenye sufuria tia nyama, saga nyanya na thomu, pilipili mbichi, tangawizi. Mimina kwenye nyama na mtindi, tia na nyanya kopo, bizari paprika, vidonge vya supu, chumvi kisha changanya vyote pamoja weka motoni.
Katika sufuria nyengine tia mafuta na samli kaanga vitungu mpaka viwe rangi ya hudhurungi toa weka pembeni.
Kanga viazi weka pembeni.
Chukua mafuta kidogo uliyokangia tia kwenye nyama acha katika moto wa kiasi mpaka nyama iwive na maji ya punguke.
Tia viazi na vitunguu vivunje vunje tia ndani ya nyama acha moto mdogo.

Vipimo Vya Wali

Mchele – 5 mug

Maji – kiasi

Chumvi – kiasi

Mafuta uliyokaanga vitungu – kiasi

Rangi ya biriani – ¼ kijiko cha chai

*Zafarani – ½ kijiko cha chai

*roweka rangi na zafarani

Namna Ya Kutarisha Na Kupika Wali

Osha mchele roweka muda wa saa.
Chemsha maji kama magi 10 hivi na chumvi tia mchele.
Uache uchemke ukishaiva kiini nusu, mwaga maji chuja.
Mimina juu ya nyama tia rangi na mafuta kwa juu funika.
Aacha kidogo katika oveni kwa muda wa dakika 20 hivi kisha epua ikiwa tayari.

Jinsi ya kuandaa biskuti za Siagi Na Jam

MAHITAJI

Unga – 2 Vikombe
Sukari ya icing – 1 Kikombe
Siagi – 250 gm
Yai – 1
Vanilla – 2 Vijiko vya chai
Baking powder -1 Kijiko cha chai
Jam – ¼ kikombe
Lozi – ¼ kikombe

JINSI YA KUPIKA

Koroga siagi na sukari katika mashine ya keki (cake mixer) mpaka iwe laini (creamy).
Tia yai na vanilla koroga mpaka mchanganyiko uwe laini kama sufi.
Tia unga na baking powder changanya na mwiko.
Chota mchanganyiko kwa mkono (kiasi cha kijiko kimoja cha supufanya duara kisha weka kwenye treya ya kupikia.
Bonyeza kila kiduara katikati kwa kidole, kisha weka jam na tupia lozi zilizomenywa na kukatwa katwa.
Pika (bake) katika oven moto wa 375° F kama muda wa dakika 15 hivi huku unazitazama tazama

Jinsi ya kutengeneza Wali Wa Dengu Kwa Samaki Wa Kukaanga

Mahitaji

Mchele wa basmati – 3 Vikombe

Dengu – 2 vikombe

Viazi – 3 vikubwa

Kitunguu – 2 kubwa

Nyanya – 2

Pilipili mbichi kubwa – 3

Pilipilimanga – ½ kijiko cha chai

Garama Masala (bizari mchanganyiko) -1 kijiko cha chai

Supu ya vidonge (stock cubes) – 2 vidonge

Chumvi – kiasi

Mafuta – ¼ kikombe

Zaafarani – 1 kijiko cha chai

Samaki wa kukaanga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Dengu kama sio za tayari kwenye kopo, roweka na zichemshe hadi ziwive

Maandalizi ya Masala Ya Dengu:

Zaafarani – iroweke katika maji ya dafu dafu (warm) ya chini ya robo kikombe weka kando.
Osha mchele, roweka.
Menya viazi na vitunguu, katakata vitunguu, na nyanya , weka kando.
Katakata viazi vipande vidogo vidogo kwa umbo la mchemraba (cubes).
Katika sufuria tia mafuta yakipata moto, tia viazi ukaange kidogo kwa moto mdogo mdogo hadi kukaribia kuwiva, toa weka kando.
Kaanga vitunguu hadi vigeuka rangi ya hudhurungi isiyokoza (light brown) kisha tia nyanya ukaange kidogo.
Tia vidonge vya supu (stock cubes) uvivuruge katika mchanganyiko, katakata pilipili mbichi kwa urefu tia, uendelee kukakaanga. Tia bizari, chumvi.
Zima moto, changanya dengu na viazi katika mchanganyiko huo.

Mapishi ya Wali:

Chemsha mchele kama kawaida ya kupika wali mweupe, kiini kiwe kimewiva nusu yake.
Chuja maji kisha changanya katika mchanganyiko wa dengu.
Nyunyizia zaafarani, uchanganye wali na mchanganyiko kidogo tu.
Funika acha uive katika mtoto mdogo mdogo au tia katika oveni hadi uive kama kawaida ya kupika wali.
Pakua katiha sahani na tolea na samaki yoyote wa kukaanga.

Jinsi ya kupika Mchuzi Wa Ngogwe Na Bamia

Viamba upishi

Ngogwe ½ kg
Kitunguu 2
Bamia ¼ kg
Karoti 2
Mafuta vijiko vikubwa 8
Maji vikombe 3 Mayai 2
Nyanya 2
Chumvi

Hatua

• Osha, menya na katakata nyanya na vitunguu.
• Osha, menya na kata karoti virefu virefu.
• Osha, kata ncha za bamia pande zote na kama ndefu sana kata
vipande viwili.
• Osha, kata vikonyo vya ngongwe, kama ni kubwa kata vipande viwili.
• Kaanga vitunguu, ongeza nyanya, korogoa mpaka zilainike.
• Ongeza ngogwe, karoti, bamia na chumvi, koroga mpaka
zionekane kukolea rojo.
• Ongeza maji vikombe 2 koroga na funikia kwa dakika 10-15 au
mpaka ziive. Punguza moto.
• Koroga mayai kwenye maji mpaka iwe kama maziwa, ongeza
kwenye mboga na koroga polepole usiponde ngogwe wala bamia
kwa dakika 5.
• Onya chumvi, pakua za moto kama kitoweo.

Mapishi ya Biriani Ya Tuna

MAHITAJI

Mchele Basmati – Mugs 2 ½

Vitunguu (Vikubwa kiasi) – 3

Tuna – Vibati 3

Carrot – 2 kubwa

Tomatoe paste – 1 kikopo

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 2 Vijiko vya supu

Tangawizi – 2 Vijiko vya supu

Uzile (Bizari ya pilau ya unga) (cummin powder )

(Jeera) – ½ Kijiko cha supu

Mdalasini – ½ Kijiko Cha supu

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Tuna carrots (grate) ziwe kama chicha weka kando.

Kaanga vitunguu 2 mpaka viwe brown weka pembeni.

Kaanga Kitunguu cha 3 halafu changanya na tangawizi, thomu, na tuna huku unakoroga.

Changanya na tomatoe, uzile (cummin powder) na mdalasini, koroga vizuri (hakikisha umeweka mtoto mdogo mdogo kwani ni rahisi kuungua)

Ikiwiva epua weka pembeni.

Chemsha wali wako kwa maji mengi na uuchuje kabla haujawiva vizuri na uugawe sehemu

Chukua trey au sufuria ambayo itaweza kuingia vitu vyote uilivyoandaa, tandaza fungu la kwanza la wali halafu utandaze carrot juu yake.

Tandaza fungu la pili la wali halafu utandaze vitunguu juu yake.

Tandaza fungu la tatu la wali halafu utandaze tuna (masalo) juu yake.

Mwisho tandaza fungu la nne la wali, ufunike vizuri na upike kwenye oven (bake) 350 Deg C kwa muda wa dakika 20

Epua ikiwa tayari kuliwa

Mapishi ya Borhowa

Mahitaji

Daal (lentils) nyekundu au/na kijani – 1 Kikombe kikubwa

Bizari ya manjano ya unga – 1/2 Kijiko cha chai

Pili pili ya unga – 1/2 kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Maji ya ndimu – 3 Vijiko vya supu

Kitunguu – 1 kiasi

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 Kijiko cha chai

Bizari ya unga (cummin powder) – 1 Kijiko cha chai

Mafuta ya kukaangia – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha daal kwa kutoa mawe ikiwa yapo, kisha osha na roweka dakika 15 hivi.
Kisha chemsha kwa kutia maji, bizari ya manjano, chumvi, pili pili ya unga na maji ya ndimu hadi iive na kuvurujika.
Halafu chukua kisufuria na kaanga kitungu, kisha thomu na mwisho tia bizari ya pilau.
Kisha mimina mchanganyiko wa kitunguu kwenye sufuria ya daal (iliyokwisha iiva)na uchanganye na iwache motoni kidogo itokote.
Ukipenda mimina mchanganyiko kwenye blenda na usage mpaka iwe laini.
Tia kwenye bakuli na itakuwa tayari kuliwa na wali na samaki ukipenda

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About