Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya viazi mbatata Vya Nazi Kwa Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Mbatata / viazi – 2 kilo

Nyama ng’ombe – ½ kilo

Kitunguu maji – 2

Tungule/nyanya – 2

Nazi /tui zito – 2 vikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic) ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Tangawizi mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

pilipili shamba/mbichi ilosagwa – kiasi

Mdalasini – 1 kipande

Bizari ya manjano – ½ kijiko cha chai

Bizari ya pilau/jiyrah/cummin – ½ kijiko cha chai

Ndimu/limau – 1

Namna Ya Kupika:

Chemsha nyama kwa kutia; chumvi, tangawizi, kitunguu thomu, mdalasini, na bizar zote.

Ipike nyama mpaka iwive na ibakishe supu yake kidogo.

Changanya tui la nazi pamoja na supu ilobakia.

Panga mbatata katika sufuria.

Tia nyama

Mwagia vitunguu na nyanya ulizotayarisha, tia pilipili.

Mwagia supu ulochanganya na tui

Funika upike mpaka viwive .

Tia ndimu

Mapishi ya Mlenda wa bamia na nyanya chungu

Mahitaji

Bamia (okra) 20
Nyanya chungu (garden eggs) 5
Magadi soda (Bicabonate soda) 1/4 ya kijiko cha chai
Nyanya (fresh tomato) 1
Chumvi (salt) kidogo
Pilipili 1/4

Matayarisho

Osha bamia, nyanya chungu na nyanya kisha vikatekate katika vipande vidogovidogo. Baada ya hapo vitie kwenye sufuria na vitu vyote vilivyobakia na kisha tia maji kidogo.Chemsha mpaka bamia na nyanya chungu ziive na vimaji vibakie kidogo sana. Baada ya hapo ziponde na mwiko kidogo kisha zikoroge na uipue na mlenda utakuwa tayari kwa kuliwa na ugali.

Mchemsho wa samaki na viazi

Mahitaji

Samaki mbichi (1)
Viazi mbatata (3)
Nyanya (1)
Kitunguu maji
Limao
Kitunguu saumu
Tangawizi
Chumvi
Pilipili
Vegetable oil

Matayarisho

Safisha samaki kisha mmarinate na tangawizi, kitunguu swaum, chumvi na limao kwa muda wa masaa mawili. Baada ya hapo menya viazi na uvikate vipande vidogo kisha vioshe na viweke kwenye sufuria yenye maji kiasi kwa ajili ya kuvichemsha. Viinjike jikoni na uviache vichemke kwa dakika 7. Vikisha chemka tia samaki, katia kitunguu,pilipili, chumvi, limao, vegetable oil na nyanya na uache supu ichemke mpaka samaki na viazi vitakapoiva. baada ya hapo supu itakuwa tayari kwa kuliwa.

Madhara ya nyama nyekundu kwa mtu mwenye VVU

Kuna nyama za aina mbili, nazo ni nyama nyeupe na nyama nyekundu.

Nyama nyeupe

Hizi ni nyama zitokanazo na samaki, kuku, ndege wa aina zote, bata, wadudu

Nyama nyekundu

Hutokana na ng’ombe, mbuzi, kondoo,nguruwe na wanyama wa porini.

Nyama ina virutubishi vingi muhimu kwa afya ya binadamu kama protini, vitamini na madini. Madini ya chuma yanayopatikana kwenye nyama ni rahisi sana kusharabiwa (kufyonzwa) mwilini na ni muhimu kwa kuongeza wekundu wa damu.
Uwezo wa miili ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kuyeyusha chakula na kusharabu (kufyonza) virutubishi hupungua. Utumiaji wa nyama nyekundu kwa wingi unaweza kuwaletea matatizo hasa katika uyeyushwaji tumboni kwani nyama nyekundu si rahisi kuyeyushwa ukilinganisha na nyama nyeupe.

Hata hivyo katika nchi yetu watu walio wengi wanatumia nyama kwa kiasi kidogo sana na mara chache. Si vyema watu hawa waache kabisa nyama nyekundu. Jambo la muhimu ni kutumia njia mbalimbali ili kuifanya nyama hii iyeyushwe kwa urahisi tumboni.

Namna ya kusaidia uyeyushwaji ni pamoja n a : –

• Kutafuna vizuri au kutumia nyama ya kusaga (kwa wanaoipata).
• Kupika nyama na viungo vinavyosaidia kulainisha kama vile papai bichi, limao, vitunguu saumu n.k.
• Kula nyama pamoja na papai

Kwa hiyo, kwa anayepata nyama nyekundu kwa wingi, kupunguza kiasi cha nyama hiyo na kuongeza kiasi cha nyama nyeupe. Na kwa yule asiyepata nyama nyeupe, apatapo nyama nyekundu asiache kutumia kwani ina umuhimu mwilini mwake.

Jinsi ya kupika Wali Wa Karoti Na Nyama

Viambaupishi: Wali

Mchele 3 Magi

Mafuta 1/4 kikombe

Karoti unakata refu refu 3

Vitunguu maji kata vikubwa vikubwa 1 kikubwa

Pilipli manga 1/2 kijicho chai

Hiliki 1/2 kijiko chai

Karafuu ya unga 1/4 kijiko cha chai

Mdalasini wa unga 1/2 kijiko cha chai

Zaafarani (ukipenda) roweka katika maji 1 kijiko cha chai

Zabibu kavu (ukipenda) 1/4 kikombe

Chumvi kiasi

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Kwenye sufuria tia mafuta na kaanga karoti kidogo.

2. Tia vitunguu kisha tia bizari zote.

3. Tia maji kiasi (kutegemea aina ya mchele) na chumvi

4. Tia mchele upike uwive.

5. Karibu na kuwvia tia zabibu ukipenda.

6. Funika endelea kuupika hadi uwive.

Viambaupishi kwa Nyama

Nyama 2 Ratili (LB)

Chumvi Kiasi

Mafuta 1/4 kikombe

Kitunguu (kata virefu virefu) 1 Kikubwa

Pilipili mboga kubwa 2

(ukipenda moja nyekundu moja kijani)

unazikata vipande virefu virefu.

Figili mwitu (celery) kata vipande Miche miwili

virefu virefu

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Chemsha nyama hadi iwive

2. Ikaange kwa mafuta hadi iwe nyekundu

3. Weka vitunguu, pilipili mboga na figili mwitu

4. Kaanga kidogo tu kama dakika moja.

Jinsi ya Kupika Kalmati

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour 2 vikombe vya chai)
Hamira (yeast kijiko 1 cha chai)
Sukari (sugar 2 vikombe vya chai)
Hiliki (cardamon 1/4 ya kijiko cha chai)
Maji kikombe1 na 1/2
Mafuta

Matayarisho

Changanya unga, hamira, maji na mafuta kijiko 1. Koroga vizuri mpaka upate uji mzito usiokuwa na madoge Baada ya hapo uache uumuke kisha zichome kalmati katika moto wa wastani. Baada ya hapo tia sukari, hiliki na maji 1/2 kikombe katika sufuria na ichemshe uku unakoroga mpaka iwe tayari.(ukitaka kujua kama iko tayari chovya mwiko kisha gusa na vidole utaona iko kama nta au gundi) Baada ya hapo tia kalmati na uzichange pamoja mpaka zikolee kisha zitoe na uziache mpaka zipoe tayari kwa kuliwa.

Kupima lishe au afya ya mtu

Njia za kupima Afya

Njia mbalimbali hutumika kupima hali ya lishe, njia hizi ni;

1. Vipimo vya umbile la mwili

2. Vipimo vya maabara

3. Kuchukua historia ya ulaji na maradhi

Vipimo vya umbile la mwili

Baadhi ya vipimo ambavyo vinaweza kutumika kutoa tahadhari kuhusu magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza ni;

1. Uwiano wa uzito na urefu au Body Mass Index (BMI).

2. Mzunguko wa kiuno.

3. Uwiano wa mzunguko wa kiuno na nyonga.

4. Kulinganisha uzito na umri.

Uwiano wa uzito na urefu au Body Mass Index (BMI).

Hiki ni kipimo kinachotumika kuangalia uwiano wa urefu na uzito wa mtu, ni muhimu kuchukua vipimo kwa usahihi.Uwiano wa uzito katika Kilogramu na urefu katika mita hupatikana kwa kutumia kanuni ifuatayo:

BMI= uzito (Kg)/Urefu2 (m2)

BMI huwa na viwango mbalimbali vilivyowekwa na shirika la Afya duniani (WHO) kutafsiri hali ya lishe ya mtu ambavyo ni

1. BMI chini ya 18.5 = uzito pungufu.

2. BMI kati ya 18.5 mpaka 24.9= uzito unaofaa.

3. BMI kati ya 25.0 mpaka 29.9 = unene uliozidi.

4. BMI ya 30 au zaidi = unene uliokithiri au kiribatumbo.

Mahitaji ya chakula mwilini hutegemea umri, jinsi, hali ya kifiziolojia (kama ujauzito na kunyonyesha), hali ya kiafya, kazi na mtindo wa maisha. Uzito wa mwili hutegemea na chakula unachokula, pamoja na shughuli unazofanya, mara nyingi unene hutokana na kula chakula kwa wingi.
Unene uliokithiri unachangia kwa kiwango kikubwa kupata magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, magonjwa ya moyo, shinikizo kubwa la damu, na saratani. Uzito uliozidi unapaswa kupunguzwa ili kuepuka magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza

Jinsi ya kupunguza unene uliozidi

1. Tumia mafuta kwa kiasi kidogo kwenye chakula

2. Epuka kula vyakula vyenye mafuta mengi hususani vinavyopikwa kwa kudumbukizwa kwenye mafuta, au vinavyokaangwa kwa mafuta mengi.

3. Epuka matumizi ya vinywaji au vyakula venye sukari nyingi

4. Epuka asusa zenye mafuta mengi au sukari nyingi kati ya mlo na mlo.

5. Ongeza vyakula venye makapi- mlo kwa wingi kama matunda, mboga mboga na nafaka zisizokobolewa.

BMI haitumiki kwa wanawake wajawazito, BMI haitumiki kwa watoto na vijana walio na umri chini ya miaka 18, BMI haitumiki kwa watu wasioweza kusimama vyema, waliovimba miguu, na wanawake wanaonyonyesha katika miezi sita ya mwanzo baada ya kujifungua.

Mapishi ya Wali, samaki wa nazi na kisamvu

Mahitaji

Mchele
Kisamvu kilichotwangwa
Samaki
Mbaazi
Nyanya chungu
Vitunguu
Nyanya ya kopo
Tangawizi
Kitunguu swaum
Vegetable oil
Curry powder
Tui la nazi (kopo 2)
Chumvi
Pilipili
Limao

Matayarisho

Safisha samaki kisha wamarineti na kitunguu swaum, tangawizi, pilipili, chumvi na limao kwa muda wa masaa 3.Baada ya hapo wakaange na usiwakaushe sana na uwaweke pembeni kwa ajili ya kuungwa.Katakata vitunguu maji, saga tangawizi na kitunguu swaum. Baada ya hapo injika sufuria ya mchuzi jikoni na mafuta kiasi ya kupikia, mafuta yakisha pata moto, tia vitunguu maji na vikaange mpaka viwe vya rangi ya brown. kisha tia kitunguu swaum na tangawizi.kaanga kidogo kisha tia nyanya ya kopo moja na ufunike. acha mpaka nyanya ziive. Kisha tia chumvi na curry powder na uache ikaangike kwa muda wa dakika 2 kisha tia samaki na nyanya chungu nakisha kamulia nusu ya limao. Geuza mpaka mchanganyiko uchanganyike vizuri kisha tia tui la nazi kopo moja na uache ichemke mpaka mchuzi uive.

Baada ya hapo chemsha kisamvu pamoja na mbaazi Kikisha iva, kaanga kitu na nyanya pembeni mpaka ziive kisha tia kisamvu. geuza mchanganyiko mpaka uchanganyike vizuri kisha tia tui la nazi na chumvi na aacha ichemke mpaka tui liive kisha ipua.malizia kwa kupika wali ambapo utachemsha maji kisha tia mafuta,chumvi na mchele na uupike mpaka uive kisha sevu na mboga ulizopika na mlo wako utakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Nazi Wa Nyanya Chungu/Mshumaa/Ngogwe Na Bamia, Mboga Ya Matembele Na Samaki Wa Kukaanga

Vipimo Vya Ugali

Unga wa mahindi – 4

Maji – 6 kiasi kutegemea na aina ya unga

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka maji katika moto.

Tia unga kidogo katika kibakuli, koroga ufanye uji.

Maji yakichemka tia kwenye maji uwe uji.

Ujii ikiiva punguza kidogo tia unga kidogokidogo na usonge ugali. Ikiwa unga ni mgumu utaongeza maji ya ule uji ulopunguza usonge hadi uive ukiwa tayari.

Vipimo Vya Mchuzi Wa Nazi Kwa Nyanya Chungu/Mshumaa/Ngogwe Na Bamia

Nyanya chungu/mshumaa/Ngogwe – 7

Bamia – 10

Kitunguu maji – 2

Nyanya/tungule – 2

Tui la nazi jepesi – 2 viwili

Tui la nazi zito – 2

Chumvi – kiasi

Ndimu – 2 mbili kamua

Bizari manjano/haldi/turmeric – ½ kijiko cha chai

Pilipili mbuzi – 3

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata kitunguu maji na nyanya vipande vidogodogo sana kisha weka katika sufuria.

Iache ichemke kwa maji yake ya nyanya, ikishachemka tia maji kidogo kama robo kikombe.

Tia nyanya chungu, bamia na koleza ndimu, chumvi.

Iache ichemke. Inapokuwa tayari imeiva tia tui jepesi endelea kuacha katika moto huku unakoroga kidogo kidogo.

Tui jepesi likipungua kiasi chake, tia tui zito, kisha usiachie mkono koroga ikichemka kidog kiasi cha kuiva tui mchuzi tayari.

Vipimo Vya Mboga Ya Matembele

Matembele – 5 mafungu

Mafuta – ¼ kikombe

Kitunguu maji kilokatwakatwa – 1

Nyanya/tungule – 4

Chumvi – 1

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Punguza miche ya matembele kwa kuikata ncha kisha osha majani yake. Acha yachuje maji .
Weka mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu maji na nyanya hadi viivie.
Tia mboga, Iache ichemke kwa maji yake hadi iive. Ukiona bado haikuiva tia maji kidogo tu.
Ukipenda unatia ndimu kiasi cha kipande kimoja ukamue .

Samaki Wa Nguru Wa Kukaanga

Samaki Wa Nguru – 4 vipande

Kitunguu saumu(thom/galic) na tangawizi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi – 4

Ndimu – 2 kamua

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha chai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Mwoshe samaki kisha mtie kitunguu thomu, tangawizi ilosagwa, chumvi, pilipilimbichi ilosagwa, ndimu na bizari ya samaki.
Mwache akolee viungo kwa muda kidogo.
Makaange katika mafuta hadi aive akiwa tayari.

Jinsi ya kuandaa Ndizi Mbichi Za Supu Ya Nyama Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi mbichi – Kisia

Nyama ng’ombe – ½ kilo

Pilipili ya kusaga – 1 kijiko cha chai

Tangawizi ya kusaga – 2 vijiko vya supu

Thomu (garlic/saumu) – 1 kijiko cha supu

Bizari mchuzi – 1 kijiko cha chai

Nazi ya unga (ukipenda kuongezea) – 2 vijiko cha supu

Chumvi – Kiasi

Ndimu – 1 kamua

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka nyama ng’ombe katika sufuria, tia tangawizi, thomu, pilipili mbichi, bizari, chumvi. Roweka kidogo ukipenda kisha ikaushe yenyewe kwa maji yake
Ongezea maji ya kiasi yasizidi mno, kisha funika na chemsha.
Menya ndizi, ukatekate.
Nyama ikikaribia kuiva, weka ndizi uendelee kupika mpaka viive vyote.
Tia nazi ya unga kidogo tu ukipenda. Koleza kwa bizari mchuzi, pilipili, na ndimu
Epua mimina katika chombo cha kupakulia zikiwa tayari.

Jinsi ya Kupika skonzi

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour 2 vikombe vya chai)
Sukari (sugar 1/2 kijiko cha chakula)
Chumvi (salt 1/2 kijiko cha chai)
Hamira (yeast 1/2 kijiko cha chakula)
Baking powder 1/2 kijiko cha chai
Siagi (butter 1/4 ya kikombe cha chai)
Maziwa (fresh milk 3/4 ya kikombe cha chai)(unaweza kutumia maji badala ya maziwa)

Matayarisho

Pasha maziwa yawe ya uvuguvugu kisha weka pembeni, pia yeyusha siagi na uweke pembeni.Baada ya hapo tia kila kitu kwenye bakuli la kukandia kasoro maziwa, na uchanganye vizuri kisha tia maziwa kidogo kidogo katika mchanganyiko huo kisha ukande. Ukimaliza uweke kwenye sehemu ya joto na uache uumuke. Ukisha umuka utawanyishe katika madonge saba Kisha .pakaza mafuta au siagi katika chombo cha kuokea kisha yapange hayo madonge katika hicho chombo na uyaache yaumuke tena (kwa mara ya pili). Baada ya hapo pakaza mafuta juu ya hayo madonge na uyaoke (bake) katika oven (moto 200°C ) kwa muda wa dakika 25 na hapo scones au maskonzi yatakuwa tayari

Jinsi ya kupika Biskuti Za Kopa Za Kunyunyuziwa Sukari Za Rangi

MAHITAJI

Unga vikombe 2 ¼

Siagi 250g

Sukari kukaribia kikombe ½ (au takriban vijiko 10 vya kulia)

Baking powder ½ kijiko cha chai

Ute wa yai 1

Vanilla 1 kijiko cha chai

Sukari Ya Kunyunyizia na rangi mbali mbali.

MATAYARISHO

Kagawa sukari katika vibakuli utie rangi mbali mbali uweke kando.
Changanya siagi na sukari katika mashine ya kusagia keki upige mpaka ilainike iwe nyororo.
Tia ute wa yai vanilla uhanganye vizuri.
Tia unga na baking powder kidogo kidogo uchanganye upate donge.
Sukuma donge ukate kwa kibati cha shepu ya kopa.
Pakaza siagi katika treya ya kupikia kwenye oveni upange biskuti
Nyunyizia sukari za rangi rangi kisha pika katika oven moto mdogo wa baina 180 – 190 deg F kwa takriban robo saa.
Epua zikiwa tayari.

Mapishi – Kisamvu cha Karanga

Mapishi yetu leo ni kisamvu cha kuchanganya na karanga. Karibu.

Mahitaji

Majani ya kisamvu
Karanga nusu kikombe
kitunguu kimoja
nyanya mbili
karoti moja
mafuta na chumvi kiasi

Matayarisho

1. Osha kisamvu chako vizuri kisha katakata vipande vidogo vidogo

2. Unaweza kutwanga kwa kutumia kinu au kuchemsha kidogo na kisha kusaga kwa kutumia mashine. Ukitumia mashine uwe makini usije ukasaga sana ukaharibu.

3. Kaanga karanga kidogo na kisha zisage ziwe unga unga.

4. Chemsha kisamvu chako hadi kiive.

5. Katakata kitunguu, karoti na na nyanya

6. Anza kuunga kisamvu kwa kukaanga vitunguu, weka karoti na kisha nyanya na vikishaiva weka kisamvu na koroga pamoja kisha weka karanga. Acha vichemke kwa muda na unaweza pia weka na nazi tui la kwanza.

7. Baada ya muda mfupi epua na kitakiwa tayari. Waweza kula kwa ugali, wali, chapati, makande n.k

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About