Dondoo za Mapishi na Lishe

Mapishi ya Chapati za maji za vitunguu

Mahitaji

Unga wa ngano (plain flour) 1/4
Kitunguu kikubwa (chopped/slice onion) 1
Yai (egg) 1
Chumvi (salt)
Mafuta (cooking oil)

Matayarisho

Tia unga, chumvi na maji kiasi katika bakuli kisha koroga mpaka madonge yote yaondoke. Baada ya hapo tia yai na vitunguu kisha koroga tena mpaka mchanganyiko wote uchanganyike vizuri. baada ya hapo choma chapati zako kama kawaida (jinsi ya kuchoma unaweza kuangalia kwenye recipe yangu ya chapati za maji katika older posts) na baada ya hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Pilau Ya Adesi Za Brown Karoti Na Mchicha Kwa Samaki Wa Salmon

Vipimo

Mchele vikombe 3

Karoti 1 ikune (grate)

Mchicha katakata kiasi

Adesi za brown

Kitunguu katakata (chopped)

Supu ya kitoweo chochote upendayo au vidonge vya supu 2

Garama masala (bizari mchanganyiko) kijiko 1 cha kulia

Samli ¼ kikombe

Chumvi kiasi

Vipimo Vya Samaki Wa Salmon

Samaki wa Salmon vipande 4 vikubwa

Tangawizi mbichi ilosagwa kijiko 1 cha kulia

Thomu (garlic/saumu) kijiko 1 cha kulia

Chumvi kiasi

Bizari ya mchuzi kijiko 1 cha kulia

Ndimu 1 kamua

Nyanya 2 kata slice kubwa kubwa

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Samaki wa Salmon

Changanya viungo vyote upake katika samaki.
Weka katika treya na panga slice za nyanya juu yake.
Oka (grill/choma) katika oven umgeuze samaki upande wa pili.
Akiwa tayari epua.

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Wali

Roweka mchele kiasi kutegemea aina ya mchele. Tumia basmati (pishori)
Roweka adesi kisha zichemshe katika maji ya kiasi. Chuja maji adesi na maji yatakayobakia tumia katika kupikia pilau hii.
Kaanga vitunguu katika samli iliyoshika moto kwenye sufuria ya kupikia.
Vikianza kugeuka rangi tia karoti, mchicha, adesi, bizari mchanganyiko kisha kaanga kidogo.
Tia mchele ukaange kidogo kisha tia supu au maji pamoja na kidonge cha supu.
Tia chumvi ukoroge funika upike kama pilau.
Epua upakue katika sahani utolee kwa samaki wa salmon

Mapishi ya Chicken Satay

Mahitaji

Kidali cha kuku 1 (chicken breast)
Kitunguu maji 1/2 (onion)
Kitunguu swaum/tangawizi (garlic and ginger paste) 1 kijiko cha chai
Limao ( lemon)1/4 kijiko cha chai
Curry powder 1/4 kijiko cha chai
Pilipili ya unga kidogo (Chilli powder)
Coriander powder 1/4 kijiko cha chai
Soy sauce 1kijiko cha chai
Mafuta 2 vijiko vya chai.
Chumvi kiasi (salt)
Vijiti vya mishkaki

Matayarisho

Osha kidali kisha kikaushe maji na kitchen towel na ukate vipande(cubes) vidogodogo na uweke pembeni. Baada ya hapo changanya vitu vyote (kasoro vijiti )na utie vimaji kidogo kisha visage katika breda kupata paste nzito. Baada ya hapo changanya hiyo paste na kuku na uache zimarinate kwa muda wa saa moja. Baada ya hapo zitunge kuku katika vijiti vya kuchomea na uzichome katika oven mpaka ziive (inaweza kuchukua kama dakika 10). Baada ya hapo chicken satay yako itakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Viazi vya nyama

Mahitaji

Viazi (potato) 1 kilo
Nyama ya ng’ombe 1/2 kilo
Nyanya ya kopo iliyosagwa 1/2 tin
Vitunguu maji 2
Tangawizi/ swaum 1 kijiko cha chai
Hoho 1
Curry powder 1 kijiko cha chai
Pilipili ya unga 1/2 kijiko cha chai
Limao 1/2
Chumvi
Coriander
Mafuta ya kupikia

Matayarisho

Safisha na katakata nyama ktk vipande vidogovidogo kisha weka pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu mpaka viwe vya brown kisha tia nyama, swaum/ tangawizi, chumvi na limao. Ichanganye vizuri kisha funika na uipike mpaka iive na maji yote yakauke yani yabaki mafuta tu. Baada ya hapo tia viazi vilivyokatwa vipande vya wastani vikaange kwa muda wa dakika 10 kisha tia pilipili na curry powder na nyanya. Funika na punguza moto.Pika mpaka nyanya iive vigeuze kisha tia vimaji kidogo vya kuivishia viazi. Viazi vikikaribia kuiva(hakikisha vinabaki na rojo kidogo) tia hoho na upike kwa muda wa dk 5 kisha malizia kwa kutia coriander. Changanya vizuri kisha ipua na viazi vyako vitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya viazi mbatata Vya Nazi Kwa Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Mbatata / viazi – 2 kilo

Nyama ng’ombe – ½ kilo

Kitunguu maji – 2

Tungule/nyanya – 2

Nazi /tui zito – 2 vikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic) ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Tangawizi mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

pilipili shamba/mbichi ilosagwa – kiasi

Mdalasini – 1 kipande

Bizari ya manjano – ½ kijiko cha chai

Bizari ya pilau/jiyrah/cummin – ½ kijiko cha chai

Ndimu/limau – 1

Namna Ya Kupika:

Chemsha nyama kwa kutia; chumvi, tangawizi, kitunguu thomu, mdalasini, na bizar zote.

Ipike nyama mpaka iwive na ibakishe supu yake kidogo.

Changanya tui la nazi pamoja na supu ilobakia.

Panga mbatata katika sufuria.

Tia nyama

Mwagia vitunguu na nyanya ulizotayarisha, tia pilipili.

Mwagia supu ulochanganya na tui

Funika upike mpaka viwive .

Tia ndimu

Mapishi ya Kidheri – Makande

Mahitaji

Nyama (kata vipande vidogodogo) – ½ kilo

Maharage – 3 vikombe

Mahindi – 2 vikombe

Kitunguu – 1

Nyanya – 2

Kabichi lililokatwa – 2 vikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha chai

Vidonge vya supu – 2

Chumvi – kiasi

Mafuta -1au 2 vijiko vya chakula

Namna Yakutayarisha

Chemsha mahindi mpaka yawive na maji yakauke kiasi.
Chemsha maharage pembeni nayo mpaka yawive na maji yakaukie kiasi.
Tia mafuta kwenye sufuria anza kukaanga vitunguu , thomu na vidonge vya supu koroga kiasi.
Kisha mimina nyama iliyokatwa vipande acha ikaangike kidogo na chumvi.
Nyama ikishakaangika tia nyanya funika kwa moto mdogo mpaka nyama iwive.
Kisha mimina mahindi na maharage yaliyochemshwa na maji yake kiasi koroga mpaka ichanganyike na mwisho mimina kabichi funikia mpaka kabichi iwive onja chumvi kama imekolea
Halafu malizia kukoroga mpaka ichanganyike na ikaukie kisha pakua kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Mchemsho wa ndizi na nyama

Mahitaji

Ndizi mbichi 6
Nyama ya ng’ombe (nusu kilo)
Viazi mviringo 2
Kitunguu swaum
Tangawizi
Kitunguu maji
Nyanya 1 kubwa
Mafuta (vegetable oil)
Chumvi
Limao
Pilipili

Matayarisho

Chemsha nyama na limao, kitunguu swaum, tangawizi chumvi na maji kiasi mpaka nyama iive, Hakikisha unaiacha na supu kiasi kwa ajili ya kuwekea kwenye ndizi.Kisha katakata nyanya na vitunguu na uweke pembeni .Menya ndizi na viazi kisha zichemshe pamoja na vitunguu, nyanya, maji kidogo, mafuta na uhakikishe haziivi kabisa. Baada ya hapo tia nyama na supu yake, pilipili mzima na chumvi na uache uchemke mpaka ndizi na viazi viive.Na baada ya hapo mchemsho wako utakuwa tayari kwa kuliwa

Mapishi ya Wali, Mchuzi Wa Nazi Wa Samaki Nguru

Mahitaji

Mchele – 3 vikombe

Samaki Nguru (king fish) – 5 vipande

Vitunguu – 2

Nyanya/tungule – 4

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Tui la nazi zito – 2 vikombe

Pilipili mbichi – 5-7

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 7-9 chembe

Kotmiri – 1 msongo (bunch)

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 2-3

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha samaki, kata vipande kiasi weka kando.
Katakata kitunguu na nyanya vipande vidogo vidogo sana (crush) .
Katakata kotmiri weka kando.
Saga pamoja, pilipili mbichi, kitunguu thomu, ndimu na chumvi.
Changanya pamoja na bizari ya samaki kisha paka katika vipande vya samaki acha kidogo vikolee.
Weka mafuta katika sufuria au karai, kaanga vitunguu kidogo tu kisha tia nyanya/tungule endelea kukaanga hadi vilainike na kupondeka.
Tia kikombe kimoja na nusu cha tui la nazi, kisha tia vipande vya samaki na masala yake, acha mchuzi uchemke samaki aive. Ongeza chumvi, ndimu, pilipili ikihitajika.
Ongezea tui lilobakia acha motoni kwa daika chache tu.
Epua mwagia kotmiri mchuzi ukiwa tayari.

Pika wali wa maji/mweupe kama kawaida utolee na mchuzi.

Jinsi ya kupika Visheti Vya Kastadi Vya Shepu Ya Kombe

Viamba upishi

Unga wa ngano 1 Kilo

Siagi ¼ kilo

Mayai 2

Kastadi (custard) 3 vijiko vya supu

Baking powder 1 kijiko cha chai

Maziwa 1 ½ gilasi

Mafuta Ya kukaangia kiasi katika karai

Maandalizi na upikaji

Weka unga katika bakuli kubwa kisha changanya na unga wa kastadi na baking powder.
Tia siagi uchanganye vizuri.
Tia mayai, kisha maziwa ya baridi uchanganye vizuri usiukande sana.
Fanya madonge kisha kata vipande vidogovidogo kisha ubonyeze kwa kidole uvikwaruze kwenye chujio lenye tundu itokee shepu (design) yake.

5- Tia mafuta katika karai yakipata moto, kaanga visheti hadi viive. Usiache hadi vikageuka rangi sana.

6- Eupua, weka katika sufuria au chombo kikubwa kusubiri shira.

Vipimo Vya Shira

Sukari ½ kilo

Hiliki ilosagwa 1 kijiko cha chai

‘arki (rose flavor) 5 matone

Maji 1 gilasi

Namna Ya Kutyarisha

Changanya sukari na maji uipike hadi iwe nzito.
Ukiona mapovu yanatoka tia hilik na ‘arki .
Mwagia katika visheti uchanganye vizuri hadi vishike na sukari.

MAPISHI YA LADU

VIAMBAUPISHI

Unga – 6 vikombe

Samli – ½kikombe

Baking Powder – ½kijiko cha chai

Maziwa- 1 kikombe

Maji -Kisia kiasi kama unga bado mzito

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 5 vikombe

Maji – 2 1/2 vikombe

Vanilla – 2 vijiko vya chai

Rangi ya orange – 1 kijiko cha chai

Iliki ya unga – 1 Kijiko cha chai

MAANDALIZI

Changanya unga wa dengu, samli, baking powder pamoja na maziwa katika mashine ya keki (cake mixer).
Ukisha changanya angalia kama mchanganyiko wako umekua mwepesi kidogo kuliko wa keki, kama bado mzito basi ongeza maji kiasi.
Kisha weka mafuta kiasi kwenye karai,weka na samli kikombe kimoja, weka kwenye moto wa kiasi.
Mafuta yakisha pata moto, chukua kijiko kikubwa cha matundu chota mchanganyiko wako na kijiko cha kawaida tia kwenye kijiko cha matundu. Hakikisha kijiko cha matundu kiwe juu ya karai ili mchanganyiko wako uchuruzike ndani ya mafuta yalio pata moto.
Pika ndani ya mafuta mpaka iwive, ila usiache ikawa brown.
Toa mchanganyiko ulowiva tia ndani ya shira uliyo pika. Hakikisha shira iwe imepoa kabla ya kutia mchanganyiko huo.
Endelea kupika mchanganyiko wako mpaka uishe, kila ukitoa katika mafuta hakikisha unatia ndani ya shira.
Ukishamaliza wote kanda huo mchanganyiko ulokua ndani ya shira mpaka uone shira yote imekauka (yaani iwe imeingia ndani ya mchanganyiko).
Tupia zabibu kavu na lozi zilizo katwa, changanya na mkono.
Wacha mchanganyiko katika bakuli, funika na foil mpaka siku ya pili.
Siku ya pili chukua mchanganyiko kiasi katika mkono tengeneza mviringo (round).

MAANDALIZI YA SHIRA

Katika sufuria, tia sukari, maji, iliki, vanilla na rangi.
weka kwenye moto wacha ichemke mpaka itowe povu (bubbles) juu.
Kisha toa povu, wacha shira kwenye moto kama dakika 3.
Hakikisha shira yako iwe inanata kiasi kwenye vidole, lakini iwe nyepesi kidogo kuliko shira ya kaimati.

Vidokezo vya kukusaidia ule mboga za majani zaidi

Ulaji wa mboga za majani ni muhimu kwa sababu zina vitamini na madini mengi na viwango vidogo vya kalori. Ili uongeze mboga zaidi za majani katika milo yako, fuata vidokezi hivi vifuatavyo;

Gundua njia za kupika haraka

Pika mboga mpya za majani au zilizogandishwa kwa barafu katika wimbi mikro kwa mlo wa haraka na rahisi kuongeza kwa mlo wowote. Pika maharagwe ya kijani, karoti, au brokoli kwa mvuke katika bakuli na kiwango kidogo cha maji katika wimbi mikro kwa mlo wa haraka.

Kuwa mbele ya mambo

Katakata bechi ya pilipili hoto, karoti, au brokoli.Ziweke ili uzitumie wakati zimeadimika. Unaweza kuzifurahia kwenye saladi, na mboji au sandwichi ya mboga za majani.

Chagua mboga za majani zilizo na rangi nyingi

Ng’arisha sahani yako na mboga za majani zilizo na rangi nyekundu, ya machungwa, au kijani. Ziko na vitamini na madini. Jaribu boga ya tunda la muoka, nyanya cheri, viazi vitamu, au kale (sukuma wiki). Hazionji vizuri tu bali ni nzuri kwako pia.

Angalia mpangilio wa friza

Mboga za majani zilizogandishwa kwenye barafu hutumika haraka na kwa urahisi na ziko na lishe kama mboga mpya za majani. Jaribu kuongeza mahindi, dengu, maharagwe ya kijani, spinachi, au mbaazi barafu kwa milo yako kadhaa uipendayo au au ule kama mlo wa kando.

Weka mboga nyingi za majani

Mboga za majani za mkebe ni ongezo muhimu kwa mlo wowote, kwa hivyo weka nyanya, maharagwe mekundu, uyoga, na viazisukari vya mkebe tayari. Chagua zilizo na lebo kama “sodiamu iliyo punguzwa,” “sodiamu kidogo,” au “hakuna chumvi imeongezwa.”

Fanya saladi yako ya bustani ing’ae kwa rangi

Ng’arisha saladi yako kwa kutumia mboga za majani zilizo na rangi nzuri kama vile maharagwe meusi, pilipili hoho zilizokatakatwa, figili zilizokatakatwa, kabichi nyekundu iliyokatakatwa au wotakresi. Saladi yako haitapendeza tu lakini pia itaonja vizuri.

Kunywa supu ya mboga za majani

Ipashe moto na uile. Jaribu supu ya nyanya, boga kikazio, au mboga za majani za bustani. Tafuta supu iliyopunguzwa sodiamu au iliyo na kiwango cha chini cha sodiamu.

Ukiwa nje

Kama chakula cha jioni ni nje ya nyumbani, usijali. Unapoagiza, itisha mboga zaidi za majani au saladi zaidi badala ya mlo wa kawaida wa kando uliokarangwa.

Onja ladha ya mboga za majani za msimu

Nunua mboga za majani ambazo ni msimu wake kwa ladha ya kiwango cha juu kwa bei ya chini. Angalia bidhaa zilizo na bei maalumu katika duka kuu la karibu kwa ununuzi wa bei nafuu. Au tembelea soko la wakulima lililokaribu.

Jaribu kitu kipya

Huwezijua unachoweza kupenda. Chagua mboga mpya ya majani – iongeze kwa mapishi yako au tafuta mtandaoni jinsi ya kuipika.

Mapishi ya Viazi, samaki na asparagus

Mahitaji

Viazi (potato 1/2 kilo)
Samaki (fish 2)
Asparagus 8
Kitunguu kilichokatwa (chopped onion 1)
Kitunguu swaum kilichosagwa (garlic 4 cloves)
Tangawizi iliyosagwa kiasi (ginger paste)
Limao (lemon 1)
Giligilani iliyokatwakatwa (chopped coriander)
Curry powder (kijiko 1 cha chai)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Safisha samaki na kisha uwamarinate na kitunguu swaum, tangawizi, limao na chumvi kwa muda wa nusu saa. Baada ya hapo wakaange na usiwakaushe sana kisha waweke pembeni. Chukua fry-pan kisha tia mafuta kidogo sana (kama 1/2 kijiko cha chai) kisha tia vitunguu maji na uvikaange kwa muda wa dakika 2 (kwani havitakiwi kuiva kabisa) kisha waweke samaki na uwachanganye na hivyo vitunguu. Kisha baada ya hapo tia giligilani iliyokatwa, kamulia limao na tia chumvi kidogo kisha geuzageuza ili kuchanganya vitu vyote na kisha ipua. Baada ya hapo menya na ukate viazi katika vipande vya wastani, na kisha uvichemshe kidogo na visiive kabisa. Baada ya hapo weka sufuria jikoni kwenye moto wa wastani na utie mafuta kidogo (kama vijiko 2 vya chakula) na kisha tia viazi na uanze kuvipika kwa kuvigeuzageuza mpaka viive na kuwa rangi ya brown kisha tia chumvi kidogo, curry powder na giligilani iliyokatwa.Vipike kwa muda wa dakika mbili kisha viipue. Na baada ya hapo malizia kwa kupika asparagus. Kwanza zioshe kisha zikate kati. Baada ya hapo weka mafuta kidogo kama 1/2 kijiko katika fry-pan yakisha pata moto tia kitunguu swaum, asparagus na chumvi.Zipike kwa kuzigeuzageuza kwa muda wa dakika 5 na hapo zitakuwa zimeshaiva na tayari kwa kuliwa pamoja na samaki na viazi. Unaweza kuvisevu kwa ketchup.

Mapishi ya Bokoboko La Kuku

Mahitaji

Ngano nzima (shayiri) – 3 Vikombe

Kuku – ½ (3 LB takriban)

Thomu na tangawizi iliyosagwa – 1 kijko cha supu

Pilipili manga ya unga – ½ kijiko cha chai

Jiyrah (cumin/bizari ya pilau) – ½ kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Kidonge cha supu – 1

Samli ya moto – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Roweka ngano (shayiri) tokea usiku au muda wa masaa.
Katakata kuku mtie katika sufuria, tia maji kiasi viungo vyote. Mchemeshe awive na ibakie supu yake.
Toa kuku, toa mifupa na umchambue chambue vipande vidogo vidogo.
Chemisha ngano (shayiri) kwa kufunika sufuria hadi iwive na kukauka maji.
Tia supu ya kuku katika ngano (shayiri), na kuku uliyemechambua. Tia kidonge cha supu.
Tia samli nusu (bakisha nusu) kisha songa mchanganyiko uchanganye hadi ivurugike kuku na ngano (shayiri) vizuri.
Mimina katika sahani, mwagia samli imoto ilyobakia likiwa tayari.

Mapishi ya bagia na chatney ya machicha ya nazi

Mahitaji

Kunde (Ila mimi nilitumia Nigerian brown beans 1/2 kilo)
Vitunguu maji (onion 2)
Pilipili (scotch bonnet pepper 2)
Vitunguu swaum (garlic 4 cloves)
Chumvi (salt)
Barking powder (1/2 kijiko cha chai)
Machicha ya nazi (grated coconut 1 kikombe cha chai)
Limao (lemon 1)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Loweka kunde usiku mzima kisha ziondoe maganda na uzitie kwenye blender pamoja na vitunguu maji, vitunguu swaum, pilipili, chumvi,barking powder na maji kiasi. Visage vitu vyote mpaka viwe laini na kisha uutoe na kuweka kwenye chujio ili uchuje maji. baada ya hapo zikaange katika mafuta mpaka ziwe za brown na uzitoe na kuziweka kwenye kitchen towel ili zichuje mafuta.Baada ya hapo saga machicha ya nazi,limao, pilipili chumvi pamoja na maji kidogo na hapo chatney yako itakuwa tayari kwa kuseviwa na bagia.

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About