Dondoo za Mapishi na Lishe

Jinsi ya kupika mkate wa sembe

Mahitaji:

Unga sembe glass 1
Unga ngano glass 1
Sukari glass 1 (unaweza kupunguza kidogo)
Maziwa glass 1
Mafuta 1/2 glass
Mayai 4
Iliki iliosagwa 2tbs
Bp 2tbs

Jinsi ya kupika:

Saga sukari yako uweke kwenye bakuli safi pamoja na mayai. Tumia mashine ya cake kusagia hadi ifure/ivimbe.
Weka mafuta saga, weka maziwa saga, weka unga wa ngano na bp(bp imix kwenye unga kabla kumimina kwenye mchanganyiko) changanya vizuri halafu malizia kwa kuweka unga sembe na iliki usage vizuri.

Chukua trey au sufuria safi weka baking paper Mimina mchanganyiko wako na uoke.

Ukiwiva utoe na uwache upoe. Mkate wa sembe utakua tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya tambi za mayai

Tambi za mayai ni moja kati ya vyakula ambavyo napenda kuandaa pale ninapokua ninaharaka au sina muda mrefu wakukaa jikoni.pishi hili huchukuca muda mfupi sana na nimlo uliokamilika.

Mahitaji

  1. Tambi ½ paketi
  2. Vitunguu maji 2 vikubwa
  3. Karoti 1
  4. Hoho 1
  5. Vitunguu swaumu(kata vipande vidogo) kijiko 1 cha chakula
  6. Carry powder kijiko 1 cha chai
  7. Njegere zilizochemshwa ½ kikombe
  8. Mafuta kwa kiasi upendacho
  9. Mayai 2
  10. Chumvi kwa ladha upendayo

Njia

1.Chemsha maji yamoto yanayotokota,ongeza chumvi na mafuta kidogo,weka tambi kwenye maji hayo chemsha adi ziive.Chuja maji yote ili kupata tambi kavu
2.Katika bakuli piga mayai kisha weka pembeni
3.Katika kikaango,weka mafuta,vitunguu maji ,vitunguu swaumu,hoho, karoti na carry powder,kaanga kwa pamoja katika moto mdogo kwa muda mfupi kwani mboga hazitakiwi kuiva.
4.Ongeza tambi na njegere katika kikaango,geuza kila mara ili kuchanganya .
5.Ongeza mayai kwenye tambi kisha geuza kwa haraka bila kupumzika adi mayai yaive na tambi ziwe kavu.Tayari kwa kula

Katika hatua hii ongeza moto uwe wa wastani,moto ukiwa mdogo mayai yatafanya tambi zishikane na kufanya mabonge.

Mapishi ya Wali Wa Karoti Na Kuku Wa Kukaanga

Vipimo Vya Wali

Mchele wa Basmati/Pishori – 1 kilo moja

Vitunguu maji – 3

Karoti – 2

Siagi – 3 vijiko vya supu

Kidonge cha supu (stock) – 1 kimoja

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Ósha mchele uroweke kama saa moja au mbili
Katakata vitunguu vipande vidogodogo (chopped) weka kando.
Kwaruza karoti (grate) weka kando.
Tia siagi katika sufuria ya kupikia wali, weka katika moto iyayuke
Kaanga vitunguu hadi vigeuke rangi kiasi tu.
Tia maji kiasi ya kupikia wali, changanya na kidonge cha supu.
Yakichemka tia mchele, koroga, funika uweke moto mdogo mdogo.
Kabla ya maji kukauka tia karoti changanya wali kisha funika uive kama unavyopika pilau.

Vipimo Vya Kuku Wa Kukaanga

Kuku alokatwakatwa – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi ilosagwa – 2 vijiko vya supu

Bizari ya mchanganyiko/garam masala – kijiko cha supu

Mtindi/Yoghurt – 1 kijiko cha supu

Ndimu – 1

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kukaangia – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Ukishamuosha kuku, mchuje atoke maji yote.
Changanya viungo vyote katika kibakuli kidogo.
Changanya pamoja na kuku kisha acha akolee viungo (marinate) kwa muda wa masaa mawili takriban.
Weka mafuta katika karai na kaanga kuku, akiwiva yu tayari kuliwa na wali.

Jinsi ya kupika Viazi Vya Nazi Kwa Nyama

Mahitaji

Viazi – 3lb

Nyama – 1lb

Kitunguu – 1

Nyanya – 2

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha chai

Manjano – ½ kijiko cha chai

Curry powder – ½ kijiko chai

Nyanya kopo – 1 kijiko cha chai

Pilipili ya unga – kiasi upendavyo

Chumvi – kiasi

Kidonge cha supu – 1

Tui la nazi – 1 kopoau zaidi

Mtindi ukipenda – 3 vijiko vya supu

Kotmiri – kiasi ya kupambia

Nazi ya unga – 4 vijiko vya supu

Mafuta – 2 vijiko vya supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Kata nyama vipande vipande kisha chemsha na chumvi mpaka iive.
Menya maganda viazi na ukate slice kubwa weka pembeni
Kata kata kitunguu kisha kaanga na mafuta mpaka vibadilike rangi
Tia thomu, bizari ya manjano, pilipili ya unga, nyanya kopo
Kata kata nyanya nzima vipande vidogo tia na kidonge cha supu.
Kisha tia viazi, nyama na tui la nazi finika mpaka viazi viwive lakini visiwe vikavu.
Tia mtindi na nazi ya unga kama vijiko 4 vya supu iache motoni kidogo kisha pakua, tupia kotmiri juu na itakuwa tayari kuliwa.

Mapishi ya wali Wa Nazi Kwa Mchuzi Wa Nyama Ng’ombe Na Mchicha

Wali Wa Mpunga

Mchele wa mpunga – 4 Vikombe

Tui la nazi – 6 vikombe

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele kisha

Bandika tui jikoni likichemka tia mchele na chumvi.

Funika uchemke, tui likikauka wacha moto mdogomdogo hadi wali uive ukiwa tayari. Ikiwa unatumia mkaa unapalia juu yake.

Mchuzi wa nyama Ng’ombe

Nyama – 1 kilo

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi ilosagwa -2 viijiko vya supu

Viazi/mbatata – 2

Kitunguu maji kilokatwakawa (slice ndogo) – 2

Nyanya/tungule – 4

Nyanya kopo – 3 vijiko vya supu

Majani ya mchuzi/mvu – 3 msongo (bunches)

Bizari ya mchuzi (simba 2) – I kijiko cha chai

Ndimu – 1 kamua

Mafuta – ¼ kikombe

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka nyama katika sufuri, tia kijiko kimoja cha kitunguu thomu na tangawizi, chumvi, ndimu na chemsha nyama hadi iwive na ibakie supu yake kidogo.
Weka mafuta katika sufuri nyingine, kaanga kitunguu. Vinapogeuka rangi tia majani ya mchuzi endelea kukaanga hadi vigeuke rangi ya hudhurungi (golden brown)
Tia nyanya/tungule, viazi/mbatata, endelea kukaanga mpaka nyanya ziive.
Tia nyama na supu yake kisha tia nyanya ya kopo, kotmiri, bizari ya mchuzi, chumvi uache mchuzi kidogo katika moto hadi viazi viive vikiwa tayari.

Mboga Mchicha

Mchicha – 4 michano/vifungu

Kitunguu – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 3

Nyanya/tungule – 2

Tui la nazi zito – 1 kikombe cha chai

Chumvi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mboga iache ichuje maji.
Ikatekate kisha weka katika sufuria.
Katika kitunguu maji, kitunguu thomu kisage au kikatekate kidogodogo (chopped), nyanya.
Weka jikoni ipikike kwa maji yake na mvuke.
Tia tui endelea kuweka katika moto mdogomdogo hadi ikaribie kukauka ikiwa tayari.

Mapishi ya Kidheri – Makande

Mahitaji

Nyama (kata vipande vidogodogo) – ½ kilo

Maharage – 3 vikombe

Mahindi – 2 vikombe

Kitunguu – 1

Nyanya – 2

Kabichi lililokatwa – 2 vikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha chai

Vidonge vya supu – 2

Chumvi – kiasi

Mafuta -1au 2 vijiko vya chakula

Namna Yakutayarisha

Chemsha mahindi mpaka yawive na maji yakauke kiasi.
Chemsha maharage pembeni nayo mpaka yawive na maji yakaukie kiasi.
Tia mafuta kwenye sufuria anza kukaanga vitunguu , thomu na vidonge vya supu koroga kiasi.
Kisha mimina nyama iliyokatwa vipande acha ikaangike kidogo na chumvi.
Nyama ikishakaangika tia nyanya funika kwa moto mdogo mpaka nyama iwive.
Kisha mimina mahindi na maharage yaliyochemshwa na maji yake kiasi koroga mpaka ichanganyike na mwisho mimina kabichi funikia mpaka kabichi iwive onja chumvi kama imekolea
Halafu malizia kukoroga mpaka ichanganyike na ikaukie kisha pakua kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika vitumbua inavyotakiwa

Mahitaji

Unga wa mchele ( Vikombe 2 vikubwa)
Sukari (Nusu ya kikombe kikubwa)
Hamira ( Nusu ya kijiko cha chai)
Hiliki (Nusu ya kijiko cha chai)
Tui la nazi ( Kikombe kimoja kikubwa)
Unga wa ngano (Vijiko viwili vya chakula)
Mafuta ya kuchomea (Vegetable oil)

Matayarisho

Unachanga unga, sukari, hamira, hiliki, unga wa ngano na tui la nazi pamoja katika bakuli la plastiki. Kisha unaukoroga mpaka mchanganyiko unakuwa kama uji mzito. Kava bakuli lililokuwa na mchanganyiko kisha hifadhi katika sehemu yenye joto kwa muda wa masaa matatu.

Jinsi ya kupika

Weka chuma cha kuchomea vitumbua katika moto wa wastani, kisha weka mafuta kwenye chuma cha kuchomea ( Kijiko kimoja cha chai) mafuta yakisha pata moto tia uji wako (upawa mmoja) katika kila shimo la chuma cha kuchomea. Acha mpaka kitumbua kikauke kisha geuza na tia mafuta. Acha upande wa pili wa kitumbua mpaka uwe rangi ya kahawia na hapo kitumbua kitakuwa kimeiva utakitoa. Rudia hatua hizo kwa vitumbua vyote vilivyobaki.

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Samaki Wa Kuchoma

Vipimo Vya Ugali

Unga wa mahindi – 4 vikombe

Maji – 6 kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Tia maji kiasi katika sufuria wacha yachemke hasa

Tia unga kidogo kidogo huku ukikoroga mpaka ukamatane

Punguza moto huku ukiendelea kuusonga

Endelea kusonga kwa dakika kadhaa mpaka uanze kuchambuka

Kisha mimina kwenye bakuli au sahani na itakuwa tayari

Vipimo Ya Upishi Wa Mchuzi Wa Samaki Wa Kuchoma Wa Nazi

Samaki:

Samaki wa Nguru – kiasi vipande 5 – 6

Pilipili mbichi – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 5 chembe

Tangawizi mbichi – 1 kipande

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha supu

Pilipili nyekundu ya unga – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 3 kamua

Chumvi – kiasi

Ukipenda mkate samaki vipande kiasi.
Saga vipimo vyote vinginevyo katika mashine. Mchanganyiko ukiwa mzito ongezea ndimu
Changanya pamoja na samaki upake vizuri vipande vya samaki
Acha kwa muda wa nusu saa vikolee mchanganyiko
Panga samaki katika treya ya kupikia ndani ya oveni, kisha mchome (grill) samaki huku ukigeuza hadi viwive.
Epua weka kando.

Kuandaa Mchuzi:

Nyanya/tungule – 3

Kitunguu – 2

Bizari ya manjano/haldi – ¼ kijiko cha chai

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Tui la nazi zito – 3 vikombe

Chumvi – kiasi

Katakata vitunguu na nyanya vidogodogo (chopped) weka kando

Weka mafuta katika karai au sufuria, kaanga vitunguu hadi vianze kugeuka rangi

Tia nyanya kaanga pamoja na tia bizari ya njano/haldi .

Tia tui la nazi, chumvi koroga .

Mwishowe tia vipande vya samaki na rojo lake litakalobakia katika treya, mchuzi uko tayari

Mapishi ya Pilau Ya Sosi Ya Soya Na Mboga

Viambaupishi

Kuku (mkate mkate vipande) 1

Mchele wa Basmati (rowanisha) 3 magi

Mdalasini 1 mchi mmoja

Vitunguu maji (vilivyokatwa vyembamba) 6

Mchanganyiko wa mboga za barafu 1 magi

(karoti, mahindi, njegere)

Kabichi (iliyokatwa katwa nyembamba) 1 magi

Pilipili mbichi (iliyosagwa) 3

Pilipili boga iliyokatwa vipande vidogo vidogo 1

Pilipili manga 1 kijiko cha chakula

Chumvi 1 kijiko cha chakula

Sosi ya soya (soy sauce) 5 vijiko vya chakula

Kotmiri iliyokatwa katwa 1 magi

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa 2 vijiko vya chakula

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Tia mafuta ndani ya karai. Yakipata moto kiasi, mimina vitunguu maji na mdalasini 1 mzima kaanga. Itachukua muda kidogo. Kaanga mpaka viwe rangi ya hudhurungi (brown). Viepue na uweke kando.

2. Ndani ya sufuria kubwa, mimina kuku, chumvi, thomu na tangawizi, sosi ya soya, pilipili manga, pilipili mbichi, chemsha mpaka kuku awive na maji yakauke.

3. Changanya vitunguu ulivyokaanga, kabichi, pilipili, mboga, kotmiri, mchanganyiko wa mboga za barafu na weka kwa muda wa dakika tano au kumi. Tia na mafuta kidogo uliyokaangia vitunguu .

4. Chemsha mchele na chumvi uwive kama kawaida ya kupika wali wa kuchuja. Ukishauchuja umwagie katika masala ya kuku.

5. Nyunyizia mafuta kidogo uliokaangia vitunguu.

6. Weka moto mdogo mpaka wali ukishawiva. Uchanganye ukiwa tayari kwa kuliwa.

KIDOKEZO:

Unaweza kuupika wali huo ndani ya jiko, yaani badala ya kutia masala kwenye sufuria ukayatia katika bakuli au treya ya jiko (oven), kisha ukamwagia wali uliouchuja humo na kuupika kaitka moto wa 400-450 Deg kwa muda wa dakika 15-20.

Mapishi ya Mitai

VIAMBAUPISHI

Unga wa ngano – magi 2 (vikombe vikubwa)

Hamira kijiko 1 cha chai

Sukari Vijiko 2 vya supu

Maziwa ¾ Magi

Siagi Vijiko 2 vya supu

Mafuta ya kukaangia kiasi

VIAMBAUPISHI:SHIRA

Sukari ¾ Kikombe

Maji ¾ Kikombe

Illiki ya unga kiasi

Zafarani kiasi

JINSI YA KUPIKA

Katika bakuli, changanya vipimo vyote pamoja na ukande unga usiwe mgumu wala laini sana uwe kiasi.
Kisha fanya donge moja na iache pahali penye joto mpaka iimuke.
Halafu weka mafuta ya kukaangia kwenye moto.
Sukuma donge hadi liwe duara sio nyembamba sana, kisha katakata kama maandazi.
Mafuta ya kisha pata moto choma mittai hukuunazigeuza hadi ziwive na kugeuka rangi.
Katika sufuria tia vipimo vya shira na iache ichemke isiwe nzito sana.
Mimina mitai kwenye shira na uzipepete, kisha weka kwenye sahani na zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Dagaa wa nazi, nyanya chungu na bamia

Mahitaji

Dagaa waliokaushwa (dried anchovy 2 kikombe cha chai)
Bamia (okra 5)
Nyanya chungu (garden egg 5)
Tui la nazi (coconut milk 1 kikombe cha chai)
Nyanya (fresh tomato 2)
Kitunguu (onion 1)
Curry powder 1/2 ya kijiko cha chai
Turmeric powder 1/2 kijiko cha chai
Limao (lemon 1/2)
Chumvi (salt kiasi)
Pilipili (scotch bonnet 1)
Mafuta (veg oil)

Matayarisho

Safisha dagaa na uwaweke pembeni. Baada ya hapo kaanga vitunguu vikianza kuwa vya brown tia dagaa wakaange kidogo kisha tia chumvi, pilipili, curry powder, turmeric, bamia na nyanya chungu, koroga vizuri mpaka mchanganyiko wote uchanganyike vizuri kisha tia nyanya na ufunike. Pika mpaka nyanya iive kisha kamulia limao,na pia hakikisha nyanya chungu na bamia zimeiva kidogo(usiache mpaka ziive sana manake zitavurugika pindi utakapotia tui la nazi) kisha malizia kwa kutia tui la nazi na uache lichemke mpaka rojo ibakie kidogo. Hakikisha nyanya chungu na bamia zimeiva ndo uipue. Na hapo dagaa wako watakuwa tayari kwa kuliwa na wali au ugali.

Jinsi ya kutengeneza juisi ya nyanya

Viamba upishi

Nyanya 1 kg
Maji Iita ½
Chumvi kijiko kidogo 1
Sukari

Hatua

• Osha nyanya, katakata na chemsha na maji mpaka zilainike.
• Chuja juisi.
• Pima juisi – vikombe 2 vya juisi kwa kikombe 1 cha sukari, weka
kwenya sufuria safi .
• Ongeza chumvi, chemsha ukikoroga mpaka ichemke.
• Mara ikichemka epua, pozesha na weak kwenya chombo safi kwa
kunywa.

Jinsi ya kupika Magimbi Kwa Nyama Ya Ng’ombe

Vipimo

Majimbi (Eddoes) kiasi 6 au 7

Nyama ng’ombe ½ kilos

Tangawizi ilosagwa 1 kijiko cha kulia

Haldi (bizari manjano/turmeric) ½ kijiko cha chai

Tui zito la nazi vikombe 2

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha nyama kisha weka chumvi, bizari ya manjano, tangawizi mbichi, ukaushe kwanza katika sufuria kwa kukaanga kaanga.
Ikianza kukauka, weka maji funika uchemshe iwive.
Menya majimbi ukate kate na uweke katika sufuria nyengine.
Mimina supu na nyama katika majimbi uchemshe yawive majimbi.
Mwisho weka tui zito la nazi uchanganye vizuri kisha weka katika moto kidogo tu bila kufunika yakiwa tayari.

Jinsi ya Kupika Kalmati

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour 2 vikombe vya chai)
Hamira (yeast kijiko 1 cha chai)
Sukari (sugar 2 vikombe vya chai)
Hiliki (cardamon 1/4 ya kijiko cha chai)
Maji kikombe1 na 1/2
Mafuta

Matayarisho

Changanya unga, hamira, maji na mafuta kijiko 1. Koroga vizuri mpaka upate uji mzito usiokuwa na madoge Baada ya hapo uache uumuke kisha zichome kalmati katika moto wa wastani. Baada ya hapo tia sukari, hiliki na maji 1/2 kikombe katika sufuria na ichemshe uku unakoroga mpaka iwe tayari.(ukitaka kujua kama iko tayari chovya mwiko kisha gusa na vidole utaona iko kama nta au gundi) Baada ya hapo tia kalmati na uzichange pamoja mpaka zikolee kisha zitoe na uziache mpaka zipoe tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About