Dondoo za Mapishi na Lishe

Madhara ya nyama nyekundu kwa mtu mwenye VVU

Kuna nyama za aina mbili, nazo ni nyama nyeupe na nyama nyekundu.

Nyama nyeupe

Hizi ni nyama zitokanazo na samaki, kuku, ndege wa aina zote, bata, wadudu

Nyama nyekundu

Hutokana na ng’ombe, mbuzi, kondoo,nguruwe na wanyama wa porini.

Nyama ina virutubishi vingi muhimu kwa afya ya binadamu kama protini, vitamini na madini. Madini ya chuma yanayopatikana kwenye nyama ni rahisi sana kusharabiwa (kufyonzwa) mwilini na ni muhimu kwa kuongeza wekundu wa damu.
Uwezo wa miili ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kuyeyusha chakula na kusharabu (kufyonza) virutubishi hupungua. Utumiaji wa nyama nyekundu kwa wingi unaweza kuwaletea matatizo hasa katika uyeyushwaji tumboni kwani nyama nyekundu si rahisi kuyeyushwa ukilinganisha na nyama nyeupe.

Hata hivyo katika nchi yetu watu walio wengi wanatumia nyama kwa kiasi kidogo sana na mara chache. Si vyema watu hawa waache kabisa nyama nyekundu. Jambo la muhimu ni kutumia njia mbalimbali ili kuifanya nyama hii iyeyushwe kwa urahisi tumboni.

Namna ya kusaidia uyeyushwaji ni pamoja n a : –

• Kutafuna vizuri au kutumia nyama ya kusaga (kwa wanaoipata).
• Kupika nyama na viungo vinavyosaidia kulainisha kama vile papai bichi, limao, vitunguu saumu n.k.
• Kula nyama pamoja na papai

Kwa hiyo, kwa anayepata nyama nyekundu kwa wingi, kupunguza kiasi cha nyama hiyo na kuongeza kiasi cha nyama nyeupe. Na kwa yule asiyepata nyama nyeupe, apatapo nyama nyekundu asiache kutumia kwani ina umuhimu mwilini mwake.

Jinsi ya kupika kisamvu bila nazi

Kisamvu ni aina ya mboga ya majani inayopatikana kwa wingi na kwa urahisi katika mikoa takriban yote nchini Tanzania.
Pia aina hii ya mboga hupikwa katika mapishi ya aina mbalimbali kulingana na mahitaji ya mpishi.

Aina hii ya mboga kama zilivyo mboga zingine za majani ni nzuri na muhimu kwa afya ya binadamu. Aina hii ya mboga huleta virutubisho mbalimbali mwilini.
Hapa tunaenda kuona mapishi ya kisamvu kwa kutumia mafuta bila nazi kama ilivyozoeleka na wengi.

Mahitaji :

• Kisamvu kilichotwangwa na kuwa laini
• Kitunguu maji
• Kitunguu swaumu
• Kunde mbichi
• carrots
• Mafuta ya kula
• Chumvi kiasi

Maandalizi :

• Chemsha kisamvu ukiwa umechanganya na kunde mpaka uhakikishe vyote vimeiva. Baada ya kuiva weak pembeni.
• Chukua sufuria kavu, weak mafuta kasha weak katika jiko na yakipata moto weak kitunguu na koroga mpaka kibadilike rangi kasha weak kitunguu swaumu na endelea kukoroga kwa muda baada ya hapo weak carrots na kisha weka kisamvu chako ambacho kimechanganywana kunde.
• Endelea kukoroga kwa muda na kasha acha kichemke mpaka uhakikishe mboga yako imeiva vizuri.
• Mboga hii iko tayari kwa kulikwa na inaweza ikaliwa na wali au ugali.

Jinsi ya kupika Pilau ya Mpunga Na Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Mpunga – 4 vikombe

Nyama – 1 kilo moja

Kitunguu maji – 3

Mbatata/viazi – 7 vidogodogo

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi ilosagwa 3 vijiko cha supu

Bizari nzima/ya pilau/uzile/cumin – 3 vijiko vya supu

Mdalasini – 3 vipande

Hiliki – 7 punje

Pilipili manga nzima – 1 kijiko cha supu

Chumvi kiasi

Mafuta – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele weka kando
Katakataka vitunguu slice ndogo ndogo.
Weka mafuta katika sufuria kisha ukaange vitunguu pamoja na mdalasini, hiliki pilipilimanga.
Vitunguu vikigeuka rangi unatia kitunguu thomu na tangawizi.
Tia supu kidogo na nyama, kisha tia bizari ya pilau/uzile, na viazi/mbatata.
Maliza kutia supu yote, na ikiwa ni kidogo ongeze maji kiasi cha kuivisha mchele. kisha tia mchele ufunike hadi wali uwe tayari.
Ikiwa unatumia mkaa palia juu yake, ikiwa hutumii uache uive kwa moto mdogo mdogo.

Jinsi ya kupika Biskuti Ya Keki Kavu kwa kizungu Shortcake

Viamba upishi

Unga 2 Magi (vikombe vya chai)

Sukari iliyosagwa 2/3 Magi (kikombe cha chai)

Siagi   220 g

Unga wa mchele ½ Magi

Yai 1

Vanilla 1 kijiko cha chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Changanya vitu vyote hivyo kwenye bakuli mpaka unga ushikamane.

2. Paka mafuta treya ya kuchomea kisha utandaze kwenye treya ya 20cm kwa 30 cm au (8 in kwa 12 in)

3. Choma kwenye moto 325˚C kwa muda wa saa nzima au mpaka ibadilike kuwa rangi ya dhahabu.

4. Epua acha ipoe kisha kata vipande kama mstatili, weak kwenye sahani tayari kunywewa na chai.

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Tangawizi

MAHITAJI

Unga – 2 Vikombe

Cocoa ya unga – 1 Kijiko cha supu

Sukari ya hudhurungi – 1 Kikombe

Siagi – ¾ Kikombe

Yai – 1

Molasses – ¼ Kikombe

Baking soda – 2 vijiko vya chai

Mdalasini wa unga – 1 kijiko cha chai

Tangawizi mbichi – 1 kijiko cha supu

Karafuu ya unga – ½ kijiko cha chai

Chumvi ½ kijiko cha chai

Vanilla ½ kijiko cha chai

MAANDALIZI

Katika bakuli, chunga unga, baking soda, chumvi na cocoa. Weka kando.
Washa oven lipate moto huku unatayarisha biskuti.
Katika bakuli jengine, mimina siagi na sukari upige kwa mashini ya keki hadi mchanganyiko uwe laini kama dakika mbili.
Mimina molasses na yai ndani ya mchanganyiko wa siagi na sukari uchanganye vizuri.
Mimina unga kidogo kidogo huku unachanganya na mwiko hadi unga wote umalizike.
Mimina mdalasini, karafuu na tangawizi, changanya vizuri.
Weka mchanganyiko wako ndani ya friji kama masaa mawili. (Ukipenda unaweza kuhifadhi mchanganyiko wako ndani ya mfuko wa freezer na uoke siku nyengine.)
Tengeneza viduara vidogo vidogo.

Chovya kila kiduara katikati sukari, kisha panga kwenye treya ya kuoka

Rudisha viduara katika friji kama nusu saa.

Oka katika oven 350ºF kwa muda wa dakika 15.

Toa biskuti kwenye oven na uache zipoe kama dakika kumi.
Panga kwenye sahani tayari kuliwa.

Jinsi ya kupika Mchuzi Wa Ngogwe Na Bamia

Viamba upishi

Ngogwe ½ kg
Kitunguu 2
Bamia ¼ kg
Karoti 2
Mafuta vijiko vikubwa 8
Maji vikombe 3 Mayai 2
Nyanya 2
Chumvi

Hatua

• Osha, menya na katakata nyanya na vitunguu.
• Osha, menya na kata karoti virefu virefu.
• Osha, kata ncha za bamia pande zote na kama ndefu sana kata
vipande viwili.
• Osha, kata vikonyo vya ngongwe, kama ni kubwa kata vipande viwili.
• Kaanga vitunguu, ongeza nyanya, korogoa mpaka zilainike.
• Ongeza ngogwe, karoti, bamia na chumvi, koroga mpaka
zionekane kukolea rojo.
• Ongeza maji vikombe 2 koroga na funikia kwa dakika 10-15 au
mpaka ziive. Punguza moto.
• Koroga mayai kwenye maji mpaka iwe kama maziwa, ongeza
kwenye mboga na koroga polepole usiponde ngogwe wala bamia
kwa dakika 5.
• Onya chumvi, pakua za moto kama kitoweo.

Mapishi ya Kuku wa kukaanga

Mahitaji

Miguu ya kuku (chicken legs) 10
Kitunguu swaum na tangawizi (ginger & garlic paste) 1 kijiko cha chakula
Limao (lemon) 1
Pilipili iliyosagwa (ground scotch bonnet) 1/2
Giligilani iliyokatwakatwa (chopped coriander) kiasi
Chumvi (salt) kiasi
Mafuta ya kukaangia (veg oil)

Matayarisho

Safisha kuku kisha mtie kwenye sufuria na viungo vyote (kasoro mafuta na giligilani) kisha mchemshe mpaka aive na umkaushe supu yote. Baada ya hapo mkaange katika mafuta mpaka awe wa brown kisha mtoe na uweke katika kitchen towel ili kuchuja mafuta. Baada ya hapo weka katika sahani na umwagie giligilani kwa juu. Na hapo kuku wako atakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Wali, Mchuzi Wa Nazi Wa Samaki Nguru

Mahitaji

Mchele – 3 vikombe

Samaki Nguru (king fish) – 5 vipande

Vitunguu – 2

Nyanya/tungule – 4

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Tui la nazi zito – 2 vikombe

Pilipili mbichi – 5-7

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 7-9 chembe

Kotmiri – 1 msongo (bunch)

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 2-3

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha samaki, kata vipande kiasi weka kando.
Katakata kitunguu na nyanya vipande vidogo vidogo sana (crush) .
Katakata kotmiri weka kando.
Saga pamoja, pilipili mbichi, kitunguu thomu, ndimu na chumvi.
Changanya pamoja na bizari ya samaki kisha paka katika vipande vya samaki acha kidogo vikolee.
Weka mafuta katika sufuria au karai, kaanga vitunguu kidogo tu kisha tia nyanya/tungule endelea kukaanga hadi vilainike na kupondeka.
Tia kikombe kimoja na nusu cha tui la nazi, kisha tia vipande vya samaki na masala yake, acha mchuzi uchemke samaki aive. Ongeza chumvi, ndimu, pilipili ikihitajika.
Ongezea tui lilobakia acha motoni kwa daika chache tu.
Epua mwagia kotmiri mchuzi ukiwa tayari.

Pika wali wa maji/mweupe kama kawaida utolee na mchuzi.

Jinsi ya kupika Keki Ya Maboga

Viamba upishi

Unga wa ngano vikombe vikubwa 3
Boga lililopondwa kikombe 1
Baking powder vijiko vidogo
Sukari kikombe kikubwa 1
Blue band kikombe ½
Vanilla kijiko kidogo 1
Mayai 2
Maji kiasi/ maziwa
(kama nilazima)

Hatua

• Osha boga, Kata, ondoa mbegu, kisha kata vipande vikubwa, chemsha na maji mpaka vilainike.
• Kwangua boga la ndani ukiacha maganda na ponda sawasawa.
• Chekecha unga (kila kikombe 1, vijiko vidogo 2 vya baking powder) kwenye bakuli kubwa.
• Ongeza blue band na changanya sawasawa na vidole.
• Ongeza sukari na changanya.
• Ongeza mayai na koroga na mwiko.
• Ongeza boga lililopondwa na koroga njia moja mpaka ilainike.
• (Kama haikulainika ongeza yai /mayai au maziwa/ maji kidogo).
• Ongeza vanilla na koroga.
• Paka mafuta chombo cha kuokea au sufuria kisha chekecha unga kidogo wa ngano.
• Mimina rojo la keki kwenye sufuria au chombo cha kuokea.
• Oka kwenye oven au tumia sufuria na weka mkaa wa moto juu na chini moto kidogo mpaka iive.
• Jaribu kuchoma kisu katikati, kama ni kavu keki imeiva, epua, pozesha kata tayari kwa kula, kama kitafunio.

Mapishi ya Wali Wa Kichina Wa Kamba Na Kuku

MAHITAJI

Mchele wa pishori (basmati) – 4

Nyama ya kuku bila mafupa – 1 Lb

Kamba saizi kubwa – 1Lb

Mchanganyiko wa mboga – njegere, karoti,

mahindi, maharage ya kijani (spring beans) – 2 vikombe

Figili mwitu (Cellery) – 2 mche

Vitunguu vya majani (spring onions) – 4-5 miche

Kebeji – 2 vikombe

Pilipili ya unga nyekundu – 1 kijiko cha chai

Pilipili manga ya unga – 1 kijiko cha chai

Sosi ya soya – 3 vijiko vya supu

Mafuta – 1/4 kikombe

Chumvi – kiasi

MAPISHI

Osha na roweka mchele.
Tia kamba chumvi na pilipili nyekundu ya unga. Tia mafuta vijiko viwili katika kikaango (frying pan), kaanga kamba kidogo tu, weka kando.
Katakata kuku vipande vidogo vidogo, tia chumvi na pilipili manga. Kaanga kaTika kikaango (ongeza mafuta kidogo) Weka kando.
Katika karai, tia mafuta kidogo kama vijiko vitatu vya supu, tia kamba na kuku, tia mboga za mchanganyiko, sosi ya soya na chumvi, kaanga kidogo. (Kama mboga sio za barafu) itabidi uchemshe kidogo.
Katakata kebeji, figili mwitu (cellery) na vitunguu vya majani (spring onions) utie katika mchaganyiko. acha kwa muda wa chini ya dakika moja katika moto.
Chemsha mchele, tia mafuta kidogo au siagi, chumvi upikie uive nusu kiini, mwaga maji uchuje.
Changanya vyote na wali rudisha katika sufuria au bakuli la oveni, funika na upike kwa moto wa kiasi kwa muda wa dakika 15-20 takriban.
Epua na upakue katika sahani ukiwa tayari kuliwa.

Jinsi ya kuandaa Vileja Vya Karanga

MAHITAJI

Mayai 5

Sukari 450gm (1 lb)

Unga wa Ngano 1 kg

Siagi 450gm (1 lb)

Baking powder ½ Kijiko cha chai

Unga wa Custard Vijiko 2 vya chakula

Karanga za kusaga 250gm

Jam ½ kikombe

MAANDALIZI

Chukua bakuli la kiasi, weka sukari na siagi.
Changanya sukari na siagi kwa kutumia mashine ya kukorogea keki (cakemixer), mpaka sukari ichanganyike na siagi.
Vunja yai moja moja na weka kiini chake kwenye mchanganyiko wa sukari na siagi, endelea kuchanganya mpaka ichanganyike vizuri. Hifadhi ute wa mayai ndani ya kibakuli.
Mimina unga wa ngano ndani ya mchanganyiko wako huku ukichanganya Changanya unga wa custard na baking powder.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Vichovye viduara ndani ya ute wa yai kisha zimwagie unga wa karanga na kuzipanga kwenye tray ya kuchomea.
Weka dole gumba kati kati ya kila kiduara na uweke jam.
Washa jiko (oven) 350F na uchome vileja vyako kwa dakika 20.
Toa vileja vyako vipoe na uviweke ndani ya sahani tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Pilau Ya Nyama Ng’ombe Karoti Na Zabibu

Vipimo – Nyama

Nyama ng’ombe ya mifupa ilokatwa vipande – 1 kilo

Tangawizi na thomu (somu/garlic) ilosagwa – 2 vijiko vya supu

Bizari mchanganyiko/garama masala – 1 kijiko cha chai

Chumvi – Kiasi

Vipimo – Wali

Mchele – 4 glass

Mbatata/viazi menya katakata – 3 kubwa

Vitunguu katakata – 5

Kitunguu thomu kilosagwa (garlic/somu) – 1 kijiko cha supu

Hiliki ya unga – 1 kijiko cha chai

Bizari nzima ya pilau/cumin – 1 mti

Samli au mafuta – 2 Vijiko vya supu

Karoti zilokatwakatwa nyembamba – 6-7

Zabibu – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katika sufuria weka mafuta kijiko kimoja cha supu tia nyama na viungo vyake.
kaushe katika moto hadi ikaribie kukauka kisha tia maji kiasi cha kuivisha na kubakisha supu ya mchele.
Katika sufuria ya kupikia weka samli au mafuta ishike moto.
Tia mbatata/viazi kaanga, tia vitunguu kaanga kidogo.
Tia kitunguu thomu, hiliki, bizari ya pilau endelea kukaanga hadi viwe rangi ya brown kidogo.
Tia mchele kaanga kidogo, kisha mimina nyama na supu yake. Funika wali uwive.
Weka kikaangio katika moto, tia samli kijiko kimoja kisha tia karoti na zabibu, kaanga kwa sekunde chache tu kwa ajili ya kulainisha karoti na zabibu.
Utakapopakuwa wali, pambia juu karoti na zabibu.

Mapishi – Kisamvu cha Karanga

Mapishi yetu leo ni kisamvu cha kuchanganya na karanga. Karibu.

Mahitaji

Majani ya kisamvu
Karanga nusu kikombe
kitunguu kimoja
nyanya mbili
karoti moja
mafuta na chumvi kiasi

Matayarisho

1. Osha kisamvu chako vizuri kisha katakata vipande vidogo vidogo

2. Unaweza kutwanga kwa kutumia kinu au kuchemsha kidogo na kisha kusaga kwa kutumia mashine. Ukitumia mashine uwe makini usije ukasaga sana ukaharibu.

3. Kaanga karanga kidogo na kisha zisage ziwe unga unga.

4. Chemsha kisamvu chako hadi kiive.

5. Katakata kitunguu, karoti na na nyanya

6. Anza kuunga kisamvu kwa kukaanga vitunguu, weka karoti na kisha nyanya na vikishaiva weka kisamvu na koroga pamoja kisha weka karanga. Acha vichemke kwa muda na unaweza pia weka na nazi tui la kwanza.

7. Baada ya muda mfupi epua na kitakiwa tayari. Waweza kula kwa ugali, wali, chapati, makande n.k

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About