Dondoo za Mapishi na Lishe

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Tende

MAHITAJI

Unga – 4 Vikombe vya chai
Sukari ya laini (icing sugar) – 1 Kikombe cha chai
Baking powder – 2 Vijiko vya chai
Mayai – 2
Siagi au margarine – 1 Kikombe cha chai
Vanilla -1 Kijiko cha chai
Maziwa ya kuchanganyia – kiasi
Tende iliyotolewa koko – 1 Kikombe
ufuta (sasame) kiasi 1/4 kikombe

MAANDALIZI

Changanya unga, siagi, baking powder, na sukari katika mashine.
Kisha tia mayai, vanilla na halafu maziwa kidogo kidogo hadi mchanganyiko ushikamane.
Gawanya madonge mawili na usukume kama chapati, lakini sio nyembamba sana.
Tandaza tende robo ya duara na unyunyize ufuta duara zima: kisha kunja hadi mwisho na ukate kate, kisha upange katika trei ya kuvumbika.
Vumbika (bake) moto wa 350°F kwa muda wa dakika 20 au hadi vigeuke rangi na viwive.
Zikisha iiva ziache zipowe na zitakuwa tayari kuliwa.

Mapishi ya Mitai

VIAMBAUPISHI

Unga wa ngano – magi 2 (vikombe vikubwa)

Hamira kijiko 1 cha chai

Sukari Vijiko 2 vya supu

Maziwa ¾ Magi

Siagi Vijiko 2 vya supu

Mafuta ya kukaangia kiasi

VIAMBAUPISHI:SHIRA

Sukari ¾ Kikombe

Maji ¾ Kikombe

Illiki ya unga kiasi

Zafarani kiasi

JINSI YA KUPIKA

Katika bakuli, changanya vipimo vyote pamoja na ukande unga usiwe mgumu wala laini sana uwe kiasi.
Kisha fanya donge moja na iache pahali penye joto mpaka iimuke.
Halafu weka mafuta ya kukaangia kwenye moto.
Sukuma donge hadi liwe duara sio nyembamba sana, kisha katakata kama maandazi.
Mafuta ya kisha pata moto choma mittai hukuunazigeuza hadi ziwive na kugeuka rangi.
Katika sufuria tia vipimo vya shira na iache ichemke isiwe nzito sana.
Mimina mitai kwenye shira na uzipepete, kisha weka kwenye sahani na zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Mlenda wa bamia na nyanya chungu

Mahitaji

Bamia (okra) 20
Nyanya chungu (garden eggs) 5
Magadi soda (Bicabonate soda) 1/4 ya kijiko cha chai
Nyanya (fresh tomato) 1
Chumvi (salt) kidogo
Pilipili 1/4

Matayarisho

Osha bamia, nyanya chungu na nyanya kisha vikatekate katika vipande vidogovidogo. Baada ya hapo vitie kwenye sufuria na vitu vyote vilivyobakia na kisha tia maji kidogo.Chemsha mpaka bamia na nyanya chungu ziive na vimaji vibakie kidogo sana. Baada ya hapo ziponde na mwiko kidogo kisha zikoroge na uipue na mlenda utakuwa tayari kwa kuliwa na ugali.

Mapishi mazuri ya Uji wa ulezi

Mahitaji

Unga wa ulezi (millet flour vijiko 3 vya chakula)
Maziwa fresh (milk 1/2 kikombe)
Sukari (sugar 1/4 ya kikombe cha chai)
Siagi (butter kijiko 1 cha chakula)
Maji (vikombe 4 vya chai) (serving ya watu wawili)

Matayarisho

Chemsha maji ya uji, Kisha koroga unga na maji ya baridi kiasi na uchanganye kwenye maji ya moto yanayochemka. Endelea kukoroga mpaka uchemke ili kuhakikisha uji haupatwi na madonge. Ukishachemka tia, maziwa, sukari na butter. Kisha acha uchemke kwa muda wa dakika 10 na hapo uji utakuwa tayari.

Mapishi ya Mandazi ya nazi

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour) vikombe 2 na1/2
Sukari (sugar) 1/2 kikombe
Hamira (yeast) 1/2 kijiko cha chai
Hiliki (cardamon powder) 1/4 kijiko cha chai
Tui la nazi (coconut milk) kiasi
Baking powder 1/4 kijiko cha chai
Siagi (butter)1 kijiko cha chakula
Mafuta ya kukaagia

Matayarisho

Changanya unga na vitu vyote kasoro tui la nazi na mafuta ya kukaangia. Ukisha changanyika vizuri tia tui la nazi na uanze kuukanda mpaka uwe mlaini. Baada ya hapo usukume na ukate mandazi katika shape uipendayo, Kisha uyawe katika sehemu yenye joto (warm place) ili yapate kuumuka.
Yakisha uumuka yakaange katika mafuta mpaka yaive kisha ipua na uyaache yapoe tayari kwa kuliwa. (Mafuta ya kukaangia yasiwe yamoto sana kwani yatayababua mandazi na hivyo ndani hayataiva vizuri.

Jinsi ya Kupika skonzi

Mahitaji

Unga wa ngano (self risen flour 2 vikombe vya chai)
Sukari (sugar 1/2 kijiko cha chakula)
Chumvi (salt 1/2 kijiko cha chai)
Hamira (yeast 1/2 kijiko cha chakula)
Baking powder 1/2 kijiko cha chai
Siagi (butter 1/4 ya kikombe cha chai)
Maziwa (fresh milk 3/4 ya kikombe cha chai)(unaweza kutumia maji badala ya maziwa)

Matayarisho

Pasha maziwa yawe ya uvuguvugu kisha weka pembeni, pia yeyusha siagi na uweke pembeni.Baada ya hapo tia kila kitu kwenye bakuli la kukandia kasoro maziwa, na uchanganye vizuri kisha tia maziwa kidogo kidogo katika mchanganyiko huo kisha ukande. Ukimaliza uweke kwenye sehemu ya joto na uache uumuke. Ukisha umuka utawanyishe katika madonge saba Kisha .pakaza mafuta au siagi katika chombo cha kuokea kisha yapange hayo madonge katika hicho chombo na uyaache yaumuke tena (kwa mara ya pili). Baada ya hapo pakaza mafuta juu ya hayo madonge na uyaoke (bake) katika oven (moto 200°C ) kwa muda wa dakika 25 na hapo scones au maskonzi yatakuwa tayari

Mapishi ya Ndizi Za Supu Ya Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi – 15 takriiban

Nayma ya ng’ombe – 1 kilo

Kitunguu maji – 1

Nyanya – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) kilosagwa – 1 kijiko cha supu

Tangawizi mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi ilopondwa – 2

Jira/cummin/bizari ya pilau ilosagwa – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 1

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chemsha nyama kwa ndimu, chumvi na tangawizi mbichi na kitunguu thomu.
Menya ndizi na zikatekate vipande kiasi, weka katika sufuria.
Katakata kitunguu na nyanya utie katika ndizi.
Tia jira na chumvi.
Nyama ikiwiva mimina pamoja na supu yake ufunike ndizi ziwive na kuwa tayari kuliwa.
Ukipenda tia pilipili mbuzi zichemke pamoja na ndizi.

Jinsi ya kupika Mishkaki ya kuku

Kidali cha kuku 1 kikubwa
Swaum,tangawizi 1 kijiko cha chai
Limao 1/2
Pilipili ya unga 1/2 kijiko cha chai
Curry powder 1/2 kijiko
Paprika 1/2 kijiko cha chai
Hoho jekundu 1/2
Hoho la njano 1/2
Kitunguu 1/2
Chumvi
Olive oil

Matayarisho

Katakata kuku ktk vipande vya mishkaki ya kawaida kisha vimarinate na vitu vyote, kasoro hoho na kitunguu.Ni vizuri kuziacha either usiku mzima au kwa masaa machache ili spice ziingie vizuri. Baada ya hapo katakata hoho na vitunguu vipande vya wastani kiasi. Baada ya hapo Taarisha vijiti vya mishkaki kisha tunga nyama pamoja na hoho na vitunguu kisha nyunyuzia mafuta na kisha uzichome kama mishkaki ya kawaida. Itakapoiva itakuwa tayari kwa kuliwa na chochote upendacho kama ndizi za kuchoma, viazi na n.k.

Jinsi ya kupika wali wa Tuna (samaki/jodari)

VIAMBAUPISHI VYA TUNA

Tuna (samaki/jodari) – 2 Vikopo

Vitunguu (kata kata) – 4

Nyanya zilizosagwa – 5

Nyanya kopo – 3 Vijiko vya supu

Viazi (vilivyokatwa vipande vidogo – cubes) – 4

Dengu (chick peas) – 1 kikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic)&Tangawizi iliyosagwa 1 Kijiko cha supu

Hiliki – 1/4 kijiko cha chai

Mchanganyiko wa bizari – 1 kijiko cha supu

Chumvi – kiasi

Pilipili manga – 1 Kijiko cha chai

Vipande cha Maggi (Cube) – 2

VIAMBAUPISHI VYA WALI

Mchele – 3 Vikombe vikubwa (Mugs)

Mdalasini – 2 Vijiti

Karafuu – chembe 5

Zaafarani – kiasi
Jirsh (Komamanga kavu au zabibu kavu -raisins) – 1/2 Kikombe

JINSI YA KUANDAA

Kosha Mchele na roweka.
Kaanga vitunguu hadi viwe rangi ya hudhurungi (brown) chuja mafuta uweke kando.
Kaanga viazi, epua
Punguza mafuta, kaanga nyanya.
Tia thomu/tangawizi, bizari zote, vipande vya Maggi, nyanya kopo, chumvi.
Mwaga maji ya tuna iwe kavu, changanyisha kwenye sosi.
Tia zaafarani kidogo katika sosi na bakisha ya wali.
Chemsha mchele pamoja na mdalasini na karafuu.
Karibu na kuwiva, chuja maji utie katika chombo cha kupikia katika jiko (oven)
Nyunyizia zaafarani, mwagia vitunguu, viazi, na dengu juu ya wali.
Mwagia sosi ya tuna na pambia jirshi (au zabibu).
Funika wali na upike katika jiko moto wa 450º kwa muda wa kupikika wali. Epua upakue.

Jinsi ya kupika Biskuti Za Kopa Za Kunyunyuziwa Sukari Za Rangi

MAHITAJI

Unga vikombe 2 ¼

Siagi 250g

Sukari kukaribia kikombe ½ (au takriban vijiko 10 vya kulia)

Baking powder ½ kijiko cha chai

Ute wa yai 1

Vanilla 1 kijiko cha chai

Sukari Ya Kunyunyizia na rangi mbali mbali.

MATAYARISHO

Kagawa sukari katika vibakuli utie rangi mbali mbali uweke kando.
Changanya siagi na sukari katika mashine ya kusagia keki upige mpaka ilainike iwe nyororo.
Tia ute wa yai vanilla uhanganye vizuri.
Tia unga na baking powder kidogo kidogo uchanganye upate donge.
Sukuma donge ukate kwa kibati cha shepu ya kopa.
Pakaza siagi katika treya ya kupikia kwenye oveni upange biskuti
Nyunyizia sukari za rangi rangi kisha pika katika oven moto mdogo wa baina 180 – 190 deg F kwa takriban robo saa.
Epua zikiwa tayari.

Mapishi ya Pilau Ya Nyama Na Mtindi

MAHITAJI

Nyama iliyokatwa vipande – 1 Ratili(LB)

Mchele Basmati – 2 Magi

Chumvi ya wali – kiasi

Kitungu kilichokatwa katwa – 1 kikubwa

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi – 1 kijiko cha supu

Mtindi (yogurt) – ½ kikombe

Mchanganyiko wa bizari ya pilau ya tayari – 2 vijiko vya supu

Mafuta kidogo yakukaangia

Rangi ya manjano (ukipenda)

NAMNA YA KUTAYARISHA NA KUPIKA

Osha mchele na roweka nusu saa .

Weka mafuta katika sufuria na kaanga vitungu mpaka viwe rangi ya hudhurungi (brown).

Tia thomu na tangawizi na ukaange kidogo.

Kisha weka bizari ya pilau halafu nyama huku unakaanga hadi nyama isiwe nyekundu tena.

Tia maji gilasi 1½- 2 ichemke mpaka nyama iwive na karibu kukauka.

Mimina mtindi na iachie moto mdogo ikauke kidogo.

Kwenye sufuria nyingine chemsha mchele pamoja na chumvi na mafuta kidogo mpaka uive.

Mimina wali juu ya nyama, kisha nyunyiza rangi (ukipenda) kama vile wali wa biriani na ufunike kwa dakika kumi hivi.

Changanya wali na nyama pamoja ikiwa tayari kuliwa.

Namna ya kutengeneza Visheti Vya Nazi Na Njugu (Sudani)

VIAMBAUPISHI

Unga – 3 mug za chai

Samli – ½ mug ya chai

Maziwa – 1¼ mug ya chai

Baking powder – 2 vijiko vya chai

VIAMBAUPISHI VYA MJAZO

Njugu zilizomenywa vipande vipande – 2 vikombe cha chai

Sukari – ½ kikombe cha chai

Iliki – 1 kijiko cha chai

Nazi iliyokunwa – 2 vikombe vya chai

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 2 vikombe vya chai

Maji – 1 kikombe cha chai

Ndimu – 1

JINSI YA KUVIANDAA

1-Changanya unga na samli kisha tia baking powder na maziwa. Ukande ulainike kisha

uwache kama dakika 5 uumuke.

2-Kwenye bakuli nyingine changanya njugu, sukari na iliki.

3-Kata madonge madogo dogo sukuma kila donge duara jembamba, kisha tia kijiko cha mchanganyiko wa njugu juu yake ifunikie juu yake na ibane pembeni.

4-Panga kwenye treya isiyoganda (non stick) kisha choma kwenye oven kwa moto wa chini

(bake) 350° C kwa dakika kama 15-20.

5-Chemsha maji na sukari katika sufuria ndogo kisha tia ndimu acha ichemke mpaka inatenate unapoigusa.

6-Kwenye sahani ya chali mimina nazi iliyokunwa.

7-Vibiskuti vikiwa tayari vya motomoto chovea kwenye shira kisha zungushia katika nazi iliyokunwa,

panga kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Ugali na dagaa

Mahitaji

Dagaa (dried anchovies packet 1)
Unga wa ugali (corn meal flour 1/4 kilo) (unaweza kutumia unga wa choice uipendayo)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1/2)
Kitunguu maji (onion 1)
Limao (lemon 1/4)
Pilipili mbuzi nzima bila kukata (scotch bonnet pepper1, do not chop)
Chumvi (salt 1/4 ya kijiko cha chai)
Mafuta (vegetable oil)
Hoho (green pepper)

Matayarisho

Chambua dagaa kwa kutoa vichwa vyao na utumbo, baada ya hapo waloeke katkika maji ya moto kwa muda wa dakika 5 na uaoshe tena katika maji ya baridi na uwakaushe uwaweke pembeni. Ukishamaliza katakata kitunguu na uandae nyanya tayari kwa upishi. Bandika sufuria ya kupikia dagaa jikoni na utie mafuta, yakishapata moto tia vitunguu pamoja na dagaa. Kaanga mpaka dagaa wawe light brown kisha tia nyanya, chumvi na pilipili. Pika nyanya mpaka ziive (ukitaka kujua kama nyanya zimeiva utaona zinatengana na mafuta) Baada ya hapo kamulia limao kidogo sana na tia pilipili hoho na zipike kama dakika mbili. kisha ipua.
Ukisha maliza kupika dagaa andaa chungu cha ugali. Kwanza unatakiwa kuchemsha maji ya moto, kisha koroga pembeni unga kiasi katika maji ya baridi na utie kwenye maji yanayochemka, Fanya kama unatengeneza uji, uji wa ugali ukishachemka tia unga na uanze kuusonga mpaka ugali uive. Ukisha iva pakua na usevu na mboga tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Kachori

Mahitaji

Viazi mbatata (potato 4 vya wastani)
Nyama ya kusaga (mince beef 1 kikombe cha chai)
Kitunguu (onion 1 cha wastani)
Carrot 1
Hoho (green pepper 1/2)
Kitunguu swaum (garlic)
Tangawizi (ginger )
Binzari nyembamba (ground cumin 1/2 kijiko cha chai)
Binzari manjano (turmeric 1/2 kijiko cha chai)
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Limao (lemon 1/2)
Pilipili ya unga (chilli powder 1/2 kijiko cha chai)
Giligilani (coriander kiasi)
Chumvi (salt)
Mafuta (vegetable oil)
Unga wa ngano kiasi

Matayarisho

Katakata vitunguu na hoho katika vipande vidogo vidogo na kisha kwangua carrot na uweke pembeni. Chemsha viazi na chumvi kidogo vikiiva viponde na uviweke pembeni, Baada ya hapo tia nyama limao, chumvi, kitunguu swaum na tangawizi ichemshe mpaka iive na uhakikishe maji yote yamekauka. Kisha Tia binzari zote, pilipili, curry powder, giligilani, vitunguu, hoho na carrot. Pika mchanganyiko huo kwa muda wa dakika 3 na kisha ipua. Baada ya hapo changanya na viazi kisha tengeneza maduara ya kiasi na uyaweke pembeni. Chukua unga wa ngano kiasi na uchanganye na maji kupata uji usiokuwa mzito au mwepesi sana. baada ya hapo chovya madonge katika huo uji na uyachome katika mafuta. Hakikisha zinaiva na kuwa rangi ya brown na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.Unaweza ukazisevu na chatney yoyote unayopendelea.

Shopping Cart
0
    0
    Your Cart
    Your cart is emptyReturn to Shop
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About