Sala za Katoliki: Sala Muhimu Kwa Mkristu Mkatoliki

SALA KWA MT. YOSEFU KUOMBA KUFAHAMU WITO WAKO

Ee uliye Mkuu, Mt. Yosefu, uliyatii kabisa maongozi ya Roho Mt. Unijalie neema ya kufahamu aina ya maisha ambayo Mungu anapenda mimi niishi. Usiniache nidanganyike katika jambo muhimu kama hili, ambalo furaha yangu hapa duniani inalitegemea, na hata pia wokovu wa roho yangu.

Unijalie, nikiangazwa na matakwa matakatifu na nikiwa mwaminifu katika kuyatimiza, nikumbatie aina ya maisha ambayo Mungu ameniandalia na yatakayoniongoza kwenye furaha ya milele.
Amina.

SALA YA KUWAOMBEA MAPADRE

Ee Bwana Yesu Kristo. Mkombozi wetu, kwa mapendo na tamaa yako ya kutaka kulinda vema Kanisa lako, ukachagua Mapadri wawe Wachungaji na Viongozi wa roho za watu. Nakuomba sana; ubariki nia na bidii inayowapasa Mapadri wote katika kazi zao. Uwaongezee Utakatifu.

Uwatie moyo mzuri wenye mapendo makubwa kwako na roho za watu. Hivyo wakiisha kupata wenyewe Utakatifu, waweze kuwaongoza vizuri watu walio chini ya ulinzi wao, katika njia ya Utakatifu na furaha ya milele. Uwajalie neema zote za hali ya Upadri. Uwajalie ili waonyeshe kila siku ya maisha yao mfano wa kila fadhila ya mapendo na ya uaminifu katika Kanisa, kwa Baba Mtakatifu na kwa Maaskofu.

Yesu mpendelevu, uangalie kwa mapendo kazi na mateso ya Mapadri wako; ubariki na ustawishe mafundisho yao; wanapowafundisha watoto, wanapowahubiria watu, wanapowatuliza wakosefu watubu na wanapowasaidia wagonjwa na wale wanaokaribia mauti, Ee Yesu uwe pamoja nao. Uwakinge na hatari zote za roho na za mwili.

Mwokozi Yesu, ulijalie Kanisa liwe na Mapadri wengi walio Watakatifu. Uwajalie watoto na vijana wengi wasikie wito wa Upadri, uwatie furaha na Utakatifu na roho za Mapadri waliokufa uzijalie punziko la amani.

Kwa mimi mwenyewe Ee Yesu mpendelevu, naomba unijalie roho ya imani na utii mnyenyekevu ili niwaheshimu Mapadri kama Mawakili wa Mungu. Niwatii katika njia zote za wokovu wa roho yangu. Amina.

Sala za kuheshimu Damu Takatifu ya Yesu

Tusali kila siku sala hizi, angalau kwa mwezi wa saba (Julai) kila mwaka, mwezi wa kuheshimu Damu Takatifu ya Mkombozi wetu.

Yesu alimwahidi Mt. Brigita wa Sweden kwamba wale watakaosali Baba Yetu 7 na Salamu Maria 7 kwa miaka 12 kwa kuheshimu damu yake takatifu na kutafakari juu ya Kutahiriwa kwake, jasho lake la damu, kupigwa kwake mijeledi, kuvikwa taji la miiba, kuchukua kwake Msalaba, kusuliwa kwake na kuchomwa ubavuni; watapata neema 5 zifuatazo: (1) Hawataingia toharani, (2) Yesu atawapa cheo cha mashahidi waliomwaga damu yao kwa ajili ya imani, (3) Yesu atawadumisha jamaa zake watatu katika hali ya neema, (4) Roho za jamaa zake zitakingwa na Jehanam mpaka kizazi cha nne, (5) Mwezi kabla ya kufa, Yesu atawajulisha. Wakifa kabla ya kutimiza miaka ile, watahesabiwa wamemaliza.

Ee Yesu, sasa ninataka kusali Baba yetu mara saba nikiungana na ule upendo ambao kwao uliitakasa sala hii katika Moyo wako. Uichukue kutoka mdomoni mwangu hadi moyoni mwako. Uiboreshe na kuikamilisha hivyo kwamba iupatie heshima na furaha kwa Utatu Mtakatifu kama vile Wewe ulivyoupatia kupitia sala hii wakati ulipokuwa bado hapa duniani. Utukuzwe ee Yesu, itukuzwe Damu Yako Takatifu sana uliyoimwaga kutoka katika Majeraha Yako Matakatifu.

1. Yesu anatahiriwa.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu …. Salamu Maria …. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea Majeraha ya kwanza, maumivu ya kwanza na Damu ya kwanza aliyomwaga Mwanao mpenzi, Bwana wetu Yesu Kristu, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu na dhambi za dunia nzima, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi ya kwanza ya mauti, hasa kati ya ndugu zangu.

2. Yesu anatokwa Jasho la Damu bustanini Gethsemane.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu …. Salamu Maria …. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea mateso na mahangaiko makali sana ya moyoni, ya Bwana wetu Yesu Kristu katika mlima wa mizeituni na kila tone la jasho lake la damu, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu za kimoyomoyo, na dhambi za namna hiyo zinazotendwa na dunia nzima, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi za moyoni na kwa ajili ya kueneza upendo wa kiMungu na wa kindugu.

3. Yesu anapigwa mijeledi.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu …. Salamu Maria …. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea majeraha elfu elfu aliyopata, maumivu makali sana na Damu Takatifu sana aliyomwaga, alipopigwa mijeledi, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu za tamaa ya mwili, kwa malipizi ya dhambi za tamaa ya mwili za wanadamu wote, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi za tamaa ya mwili, na kwa kulinda usafi wa moyo, hasa kati ya ndugu zangu.

4. Yesu anavikwa taji la miiba.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu …. Salamu Maria …. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea majeraha, maumivu na Damu Takatifu kutoka katika Kichwa Kitakatifu cha Yesu wakati alipovikwa taji la miiba, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu za rohoni, kwa malipizi ya dhambi za rohoni za wanadamu wote, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi za rohoni, na kwa ajili ya kueneza Ufalme wa Kristu hapa duniani.

5. Yesu anachukua Msalaba.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu …. Salamu Maria …. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea mateso ya njia ya Msalaba, hasa donda lake la begani na Damu Takatifu iliyomwagika, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu za ukaidi dhidi ya msalaba, na dhambi za ukaidi dhidi ya msalaba za wanadamu wote, malalamiko yote dhidi ya mipango yako mitakatifu na dhambi zote za ulimi, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi za ulimi na kwa ajili ya upendo wa kweli kwa Msalaba.

6. Yesu anasulibiwa.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu …. Salamu Maria …. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea Mwanao Msalabani, kupigwa kwake misumari na kuinuliwa kwake, madonda yake mikononi na miguuni na mifereji mitatu ya Damu yake Takatifu iliyomwagika kutoka katika majeraha haya, mateso yake makali sana ya mwili na roho, kifo chake kitakatifu, ukumbusho usio wa kumwaga wa damu wa kifo hiki katika Misa zote Takatifu ulimwenguni, kwa ajili ya majeraha yote yanayosababishwa na ukaidi wa nadhiri na kanuni katika madaraja matakatifu, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu zote na za ulimwenguni mzima, kwa ajili ya wagonjwa na wanaokufa, kwa ajili ya mapadre watakatifu na walei, kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu za kukarabati familia za kikristu, kwa ajili ya kuimarika kwa imani ya kikristu ulimwenguni, kwa ajili ya nchi yetu na muungano kati ya mataifa ndani ya Kristu na Kanisa lake, na kwa ajili ya wokovu wa dunia nzima.

7. Yesu anachomwa kwa mkuki moyoni.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu …. Salamu Maria …. Baba wa Milele, ukubali kupokea, kwa ajili ya mahitaji ya Kanisa Takatifu na kwa ajili ya malipizi ya dhambi za wanadamu wote, Damu na Maji Takatifu vilivyomwagika kutoka jeraha la Moyo Mtakatifu wa Yesu. Utuhurumie. Damu Takatifu ya Yesu, tone lile la mwisho lililomwagika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu, unioshe mimi na wengine wote dhambi zetu zote! Ee Maji kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, unioshe na adhabu zote za dhambi zangu na uizime miale ya moto wa toharani kwa ajili yangu na kwa ajili ya roho zote zilizomo toharani. Amina.

Katika mwaka wa Kanisa wa kiliturjia, mwezi Julai ni wa kuiheshimu Damu Takatifu ya Yesu.

SALA YA NOVENA YA SIKU TISA KWA MT. YOSEFU, YA ZAMANI, MIAKA 1900 ILIYOPITA

Ee Mt. Yosefu, ambaye ulinzi wako ni mkubwa, wenye nguvu na wa haraka mbele ya Kiti cha Enzi cha Mungu, ninakukabidhi nia na haja zangu zote. Ee Mt. Yosefu, unisaidie kwa maombezi yako yenye nguvu, na unipatie kutoka kwa Mwanao Mungu, baraka zote za kiroho, kwa njia ya Kristu Bwana wetu, ili nikishapata msaada wako wa mbinguni ningali bado hapa duniani, niweze nami kumsifu, kumwabudu na kumshukuru Mungu aliye Baba mwema kabisa kushinda wote. Ee Mt. Yosefu, sichoki kamwe kufikiri moyoni kwa upendo, jinsi Mtoto Yesu alivyokuwa amesinzia mikononi mwako. Akiwa amepumzika hivyo karibu na moyo wako, sithubutu kujongea, nisije nikamsumbua, bali nakuomba wewe umkumbatie na kumbusu kwa niaba yangu na kumwambia anipe busu lake nitakapovuta pumzi yangu ya mwisho.
Mtakatifu Yosefu Msimamizi wa wanaozimia roho; Utuombee.
Amina.

Sala hii ilipatikana katika mwaka wa hamsini wa Bwana na Mwokozi Wetu Yesu Kristu. Mnamo mwaka 1505 Baba Mtakatifu alimtumia sala hii Mfalme Charles wakati alipokuwa anaenda vitani. Yeyote atakayeisoma sala hii, au kuisikia ikisomwa, au kuibeba, hatakufa kifo cha ghafla,hatazama majini, hatadhurika kwa sumu, wala hataanguka katika mikono ya adui zake, au kuunguzwa katika moto wowote ule, au kushindwa katika vita.

Sali sala hii kwa siku tisa mfululizo, kwa kuomba jambo lolote unalolihitaji. Haijawahi kusikika kuwa sala hii imeshindwa jambo.

SALA YA KUMWOMBA MTAKATIFU TERESIA WA MTOTO YESU

Ee Mtakatifu Teresia wa mtoto Yesu, ulistahili kuitwa Msimamizi wa misioni katoliki za dunia yote. Kumbuka ile tamaa yako kuu uliyoonyesha huku duniani ya ” kusimika Msalaba wa Yesu Kristu, katika nchi zote na kuhubiri Injili mpaka mwisho wa dunia” . Twakuomba kwa ajili ya maagano yako, wasaidie mapadre, wamisionari, na kanisa zima.

Ee Mtakatifu Teresia wa mtoto Yesu ” Msimamizi wa misioni” UTUOMBEE

SALA YA KUANGUKA MIGUUNI PA BWANA YESU KATIKA EKARISTI

Ee Yesu Mfungwa wa Upendo wa Mungu,/ ninapofikiri Upendo wako na jinsi ulivyojitolea kwa ajili yangu,/ nashindwa kuelewa./ Unaficha Ukuu wako usiofahamika/ na kujidhihirisha kwa ajili yangu mimi mnyonge./ Ee Mfalme wa utukufu,/ unaficha uzuri wako,/ lakini jicho la moyo wangu/ linapenya pazia na kuona Majeshi ya Malaika/ wakikuimbia kwa heshima bila kukoma/ na nguvu zote mbinguni zikikusifu bila mwisho zikisema:/ “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu..”/

Ni nani awezaye kufahamu Upendo wako/ na huruma yako isiyo na kipimo kwa ajili yetu!/ Ee Mfungwa wa Upendo,/ nafungia moyo wangu masikini/ kwenye Tabarnakulo hii/ ili niweze kukuabudu usiku na mchana bila mwisho./ Najua hakuna kizuizi/ na hata kama naonekana kukaa mbali,/ lakini moyo wangu u pamoja nawe/ katika ibada hii./ Hakuna kinachoweza kuzuia upendo wangu kwako./ Kwangu hakuna kizuizi chochote./

Ee Utatu Mtakatifu,/ Mungu Mmoja usiyegawanyika,/ utukuzwe kwa zawadi yako hii kuu/ na agano hili la huruma!/

Nakuabudu,/ Bwana na Muumba uliyefichika katika Sakramenti Takatifu!/ Ee Bwana,/ nakuabudu kwa kazi zote za mikono yako/ zinazonifunulia Hekima yako kuu,/ Wema wako na Huruma yako kuu./ Uzuri uliousambaza hapa/ Uzuri ulio nao Wewe mwenyewe/ ambaye U Uzuri usioelezeka;/ na ingawaje umejificha na kusitiri uzuri wako,/ jicho langu,/ kwa mwanga wa imani linafika kwako,/ na roho yangu inapata kumtambua Muumba wake/ aliye Uzuri usiopimika,/ ulio juu ya kila uzuri,/ na moyo wangu unazama kabisa katika sala ya kukuabudu./

Bwana wangu na Muumba wangu,/ wema wako wanitia moyo wa kuongea nawe,/ Huruma yako huondoa kiambaza/ kitenganishacho Muumba na kiumbe./ Furaha ya moyo wangu,/ ee Mungu, ni kuongea na Wewe./ Yote ambayo moyo wangu unayatamni nayapata kwako./ Hapa ndipo mwanga wako unaponiangaza akili yangu/ na kuiwezesha kukujua Wewe zaidi na zaidi/ – ndipo mikondo ya neema inapoutiririkia moyo wangu,/ ndipo roho yangu inapochota uzima wa milele./ Ee Bwana na Muumba wangu,/ licha ya mapaji yote haya,/ unajitoa mwenyewe kwangu,/ ili uweze kujiunganisha na kiumbe dhaifu na maskini./

Ee Kristu,/ nafurahi sana nionapo kwamba unapendwa/ na kwamba sifa na utukufu wako vinaongezwa/ hasa ya Huruma yako./ Ee Kristu,/ sitaacha kamwe kuutukuza wema wako na huruma yako,/ hadi dakika ya mwisho ya maisha yangu./ Kwa kila tone la damu yangu/ na kwa kila pigo la moyo wangu/ naitukuza Huruma yako./ Natamani kugeuzwa kabisa/ na kuwa utenzi wa utukufu wako./ Naomba siku ya kufa kwangu/ popote nitakapokuwa nimelala,/ pigo la mwisho la moyo wangu/ liwe utenzi mpendevu/ usifuo Huruma yako isiyo na kipimo./ Amina

(Na Mt. Faustina Kowalska).

KUJIWEKA CHINI YA ULINZI WA MT. YOSEFU

Ee Mt. Yosefu, Baba Mlishi wa Mwokozi wangu, na mchumba safi wa Mama wa Mungu, leo ninakuchagua wewe, kama mwombezi wangu kwa Mungu Mwenyezi, na pia kama mfano wangu, na mlinzi wangu, na baba yangu, katika bonde hili la ugenini.

Ee Mt. Yosefu, ambaye Bwana alikufanya mlinzi wa Familia yake, ninakuomba uwe mlinzi wangu mwema katika mambo yangu yote. Uniwashie moyoni mwangu moto wa mapendo makuu kwa Yesu, na uniwezeshe kumtumikia kwa bidii na kwa uaminifu kwa mfano wako. Nisaidie katika udhaifu wangu katika kumheshimu Mama Maria kama Mwombezi wangu.

Daima uwe kiongozi wangu katika njia ya fadhila na ibada, na unijalie, baada ya kukufuasa kwa uaminifu katika njia ya haki, nipate ulinzi wako wenye nguvu katika saa ya kufa kwangu.
Amina

SALA YA MAJITOLEO KWA MAMA WA HUZUNI

Mama Mtakatifu, Mama wa Mungu na Malkia wa Mashahidi, leo nakuchagua Wewe uwe mfano wangu, mkingaji na mteteaji wangu. Naweka roho fukara katika moyo wako uliotobolewa na panga nyingi za mateso. Unipokee mimi niwe mtumishi wako wa pekee na mshiriki wa mateso yako. Nijalie nguvu niwe daima karibu na msalaba ule alikosulibiwa Yesu. Nakutolea nafsi yangu na mali yangu yote. Pokea kila tendo langu jema ukalisindikize kwa Mwanao, Mama, nifanye nistahili kuitwa mtumishi wa Maria, Simama karibu yangu katika matendo yangu yote ili yafanwe kwa sifa ya Mungu. Ulivyosimama karibu kabisa ya Mwanao alipokufa msalabani uwe karibu nami saa ya kufa kwangu. Nijalie niweze kutaja jina lako na la Mwana wako nikisema: “Yesu, Maria na Yosef mnisaidie saa ya kufa kwangu. Yesu, maria na Yosef, naomba nife kwa amani kati yenu!” . Amina.

Majitoleo kwa Bikira Maria

(Sala iliyotungwa na Mtk. Aloisi)
Bibi yangu mtukufu Maria, nakuwekea amana ya roho yangu na mwili wangu, nikikuomba uipokee amana yangu, kuitunzia ulinzi mwema ulinzi bora, ninakuaminia na kila neno langu, matumaini na kitulizo na kisongo chote, na masumbuko na uzima na ukomo wa uzima wangu: nitakayo ndiyo unifanyizie kwa maombezi na stahili zako, ili mambo yangu yote yapate kuongoka, yakiwa na kufuata mapenzi yako, pamoja na mapenzi ya Mwanao. Amina.

ROZARI YA MOYO MTAKATIFU WA YESU

Tumia tasbihi ya kawaida yenye chembe ndogo 53.

Kwenye Msalaba Sali:

“Ee Yesu tupe moyo wako kama amana ya upendo wako na kimbilio letu, ili tupate pumziko salama wakati wa maisha yetu na faraja tamu saa ya kufa kwetu”.
Baba Yetu ……..
Salamu Maria ……. (mara tatu)
Nasadiki ………..

Kwenye chembe kubwa Sali (Badala ya ‘Baba Yetu’):

“Ninakuabudu, ninakutukuza na ninakupenda, Ee Moyo wa Yesu wangu mpenzi, uliopenywa na huzuni nyingi kwa ajili ya dhambi, ambazo zimekuwa zikitendwa hata leo, dhidi ya Sakramenti Takatifu sana ya Altare. Ninakutolea hapo kwa kuridhika, moyo wa Mama yako mpendevu, na mastahili ya watakatifu. Amina”.

Kwenye chembe ndogo sali (Badala ya ‘Salamu Maria’):

“Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, uwakao mapendo kwetu, washa nyoyo zetu kwa mapendo yako”

SALA YA UHAI KWA MT. YOSEFU

(Sala hii inafaa sana kwa ajili ya kutetea uhai wa watoto wachanga wakiwa tumboni mwa mama zao, dhidi ya utoaji mimba au hatari nyingine dhidi ya uhai wa binadamu)

Ee Mt. Yosefu, wewe ni Mchumba safi na Mpenzi wa Bikira Maria, u Baba Mlishi wa Yesu, mlinzi na mtunzaji wa Familia Takatifu, na wa familia zote. Tuna imani kabisa katika uangalizi wako uliojaa upendo, juu ya uhai mpya, na uaminifu wako kwa familia.

Tunaweka jitihada zetu chini ya ulinzi wa sala zako. Utusaidie daima katika kutetea zawadi ya uhai wa binadamu, ili ukue hadi uzima wa milele ulioahidiwa na kujaliwa kwetu na Mwanao, Ndugu yetu, Yesu Kristu.
Amina.

Malkia wa Mbingu

Malkia wa mbingu, furahi, aleluya. Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya. Amefufuka alivyosema, Aleluya. Utuombee kwa Mungu, Aleluya. Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Alaluya. Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya. Tuombe. Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu, Mwanao: fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.

LITANIA YA BIKIRA MARIA MAMA WA MATESO

Bwana utuhurumie Bwana utuhurumie
Kristo utuhurumie Bwana utuhurumie
Bwana utuhurumie Bwana utuhurumie
Kristo utusikie – Kristo utusikilize
Mungu Baba wa Mbinguni, Utuhurumie
Mungu Mwana, Mkombozi wa dunia Utuhurumie
Mungu Roho Mtakatifu Utuhurumie
Utatu Mtakatifu Mungu MMoja Utuhurumie
Maria Mtakatifu Utuombee (iwe kiitikio)
Mama wa Mkombozi wetu,
Mama mwenye mateso,
Malkia wa mashahidi,
Mama wa wenye uchungu,
Mfariji wa wenye taabu,
Msaada wa wenye shida,
Mlinzi wa wenye upweke,
Nguvu ya dhaifu moyoni,
Makimbilio ya wakosefu,
Afya ya wagonjwa,
Matumaini ya wanaozimia,
Kwa ajili ya ufukara wako ulioona pangoni Bethlehemu, – Utusaidie ee Mama wa mateso (iwe kiitikio)
Kwa ajili ya mateso yako uliyoona katika uaguzi wa Simeoni,
Kwa ajili ya taabu zako ulizopata katika safari ya Misri,
Kwa uchungu wako, Mwanao alipopotea,
Kwa ajili ya huzuni yako Mwanao alipodhulumiwa,
Kwa ajili ya hofu yako Yesu alipokamatwa,
Kwa ajili ya uchungu wako ulipokutana na Yesu katika njia ya Msalaba,
Kwa ajili ya mateso ya Moyo wako aliposulibiwa,
Kwa ajili ya mateso yako makali Yesu alipokufa,
Kwa ajili ya kilio chako juu ya Mwanao mpenzi,
Kwa ajili ya uchungu wako penye kaburi la Mwanao,
Kwa ajili ya upweke wako baada ya maziko ya Mwanao,
Kwa ajili ya uvumilivu wako katika shida zote,
Katika uchungu wetu wote,
Katika ugonjwa na mateso,
Katika huzuni na shida,
Katika umaskini na upweke,
Katika mahangaiko na hatari,
Katika vishawisho vyote,
Katika saa ya kifo chetu,
Katika hukumu ya mwisho,

Mwanakondoo wa Mungu, unayeondoa dhambi za dunia, Utusamehe ee Bwana.
Mwanakondoo wa Mungu, unayeondoa dhambi za dunia, Utusikilize ee Bwana.
Mwanakondoo wa Mungu, unayeondoa dhambi za dunia, Utuhurumie.
Kristo utusikie – Kristo utusikilize
Bwana utuhurumie – Kristo utuhurumie
Bwana utuhurumie.
Baba Yetu ….
Utuombee, ee Mama wa Mateso
Tujaliwe kupewa ahadi za Kristo.
TUOMBE: Ee Bwana Yesu Kristo, utusaidie sasa na saa ya kifo chetu msaada wa Bikira Maria Mama yako, ambaye moyo wake mtakatifu ulichomwa na upanga wa mateso ulipoteswa na kufa msalabani. Unayeishi na kutawala milele na milele. Amina.

Rozari ya Malaika Mkuu Mikaeli

Rozari ya Malaika Mkuu Mikaeli ni sala nzuri sana ya kumheshimu huyu Malaika Mkuu pamoja na makundi yote tisa ya Malaika. Kuendana na jinsi tunavyofunuliwa katika Maandiko Matakatifu, makundi haya tofauti tofauti ya Malaika hujipanga kuanzia karibu sana na Kiti cha Enzi alipo Mwenyezi Mungu, kwenda chini tulipo sisi wanadamu. Makundi hayo kuanzia juu kwenda chini ni Maserafi, Makerubi, Wenye Enzi, Watawala, Wenye Nguvu, Wenye Mamlaka, Wakuu, Malaika Wakuu na Malaika.

Asili ya Rozari hii ni maono aliyopata Mtumishi wa Mungu Antonia d’Astonac, ambaye alitokewa na Malaika Mkuu Mikaeli aliyemfundisha sala za Rozari hii kwa kumwelekeza kuwa anataka aheshimiwe kwa salamu tisa kufuatana na makundi tisa ya Malaika.

Mtakatifu Mikaeli Malaika Mkuu aliahidi kuwa yeyote anayefanya ibada hii kwa heshima, akaribiapo Meza Takatifu, atasindikizwa na Malaika tisa, mmoja kutoka kila kundi la Malaika. Zaidi ya hayo, kwa kusali rozari hii, aliahidi msaada wa daima, na kwamba Malaika watamsaidia mwenye kuisali duniani na kumtoa toharani akifariki, yeye pamoja na jamaa zake.

ROZARI YA MALAIKA MKUU MIKAELI

Ee Mungu unielekezee msaada, Ee Bwana unisaidie hima!
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele. Amina.

Sali Baba Yetu (mara nne) kwa heshima ya Malaika Wakuu, Mtakatifu Mikaeli, Mtakatifu Gabriel, Mtakatifu Rafaeli na Malaika Mlinzi.

1. Kwa heshima ya Malaika Mkuu Mtakatifu Mikaeli; Baba Yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, ufalme wako ufike, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni, utupe leo mkate wetu wa kila siku, utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi, lakini utuopoe maovuni. Amina
2. Kwa heshima ya Malaika Mkuu Mtakatifu Gabrieli; Baba Yetu, …..
3. Kwa heshima ya Malaika Mkuu Mtakatifu Rafaeli; Baba Yetu, …..
4. Kwa heshima ya Malaika Wangu Mlinzi; Baba Yetu, ……

Sali Baba Yetu moja na Salamu Maria tatu baada ya kila salamu katika tisa zifuatazo kwa heshima ya Makundi Tisa ya Malaika

Baba Yetu (mara moja, – tazama hapo juu)

Salamu Maria
Salamu Maria umejaa neema, Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu Mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu, Amina.

1. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya kundi la Serafin, Bwana awashe mioyoni mwetu moto wa mapendo kamili. Amina.
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

2. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Kerubin, Bwana atuwezeshe kuacha njia mbaya na kuenenda katika njia ya ukamilifu wa kiKristo. Amina.
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

3. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Wenye Enzi, Bwana atujalie roho ya unyofu na unyenyekevu wa kweli. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

4. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Watawala, Bwana atujalie neema ya kushinda maasi yetu na tamaa mbaya. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

5. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Wenye Nguvu, Bwana atukinge na vishawishi na mitego ya shetani. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

6. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Wenye Mamlaka, Bwana atukinge na mwovu wala tusianguke vishawishini. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

7. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Wakuu, Bwana atujalie kuwa na roho ya utii wa kweli. Amina
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

8. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Malaika Wakuu, Bwana atudumishe katika imani na katika kazi zote njema ili tujaliwe utukufu wa Milele. Amina.
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

9. Kwa maombezi ya Mtakatifu Mikaeli na ya Kundi la Malaika, Bwana atujalie ulinzi wao duniani hapa na baadaye watuongoze kwenye furaha za Mbinguni. Amina.
Baba Yetu (mara moja), Salamu Maria (mara tatu)

SALA MBELE YA KITI CHA ENZI CHA MUNGU

Sali Atukuzwe 7 kwa heshima ya Malaika 7 wateule ujipatie neema ya kuepa dhambi mbaya saba na kutujaza mapaji saba ya Roho Mtakatifu.

TUOMBE
Ee Mungu Mwenyezi wa milele, kwa wema na huruma yako ya ajabu, umetaka watu wako waokoke, ukamweka Malaika Mkuu Mikaeli kuwa Mkuu wa Kanisa lako, Utukinge na adui zetu, wasitusmbue saa ya kufa kwetu, bali tuongozwe naye kwenye utukufu wako Mkuu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana Wetu Yesu Kristo. Amina.

Utuombee Ee Mtukufu Mtakatifu Mikaeli Mkuu wa Kanisa la Yesu Kristo, tujaliwe ahadi za Kristo. Amina.

SALA KWA MTAKATIFU MIKAELI MALAIKA MKUU

Mtakatifu Mikaeli Malaika Mkuu, utulinde katika vita, uwe kinga yetu katika maovu na maoteo ya shetani, Mungu amtiishe, tunaomba sana, nawe Mkuu wa Majeshi ya Mbinguni kwa nguvu ya Mungu uwaangushe motoni shetani na pepo wabaya wengine wote, wanaozunguka duniani, ili kuzipoteza roho za watu.
Amina.

SALA KWA MALAIKA WAKO MLINZI

Malaika wa Mungu Mlinzi wangu mpenzi,
Ambaye upendo wake unanifanya niwepo hapa,
Uwe nami leo hii,
Kuniangaza na kunilinda,
Kunitawala na kuniongoza.
Amina.

SALA NYINGINE KWA MALAIKA WAKO MLINZI

Ee Malaika wangu Mlinzi, uliyewekwa na Mungu Mwema, naomba unilinde katika hatari zote za roho na za mwili. Amina

Sali mara kwa mara unapokumbuka, hasa asubuhi uamkapo na usiku kabla ya kulala, Atukuzwe mara saba, kwa heshima ya Malaika wako Mlinzi.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About