Sala za Katoliki: Sala Muhimu Kwa Mkristu Mkatoliki

Kumbuka ee Bikira Mwenye Rehema

KUMBUKA

Kumbuka ee Bikira mwenye rehema, haijasikika kamwe kwamba ulimwacha mtu aliyekimbilia ulinzi wako, akiomba msaada wako, akitaka umwombe.

Nami kwa matumaini hayo, nakukimbilia ee mama, mkuu wa mabikira, ninakuja kwako, ninasimama mbele yako,  nikilalamika mimi mkosefu ewe mama wa neno la mungu, usiyakatae maneno yangu, mbali uyasikilize kwa wema na unitimizie Amina.

LITANIA YA KUWAOMBEA MAPADRE WOTE II

Kwa ajili ya Baba Mtakatifu wetu ..(N); Bwana, umpe moyo wako wa uchungaji mwema
Kwa ajili ya makardinali na maaskofu wakuu; Uwape moyo wa kichungaji ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wa majimbo; Uwajaze na Roho wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre watawa; Wakamilishe katika wito wao ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre walioko hatarini; Uwaokoe ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wenye udhaifu; Uwatie nguvu ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wenye hofu; Uwape amani ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre waliokata tamaa; Uwavuvie upya ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wakaao upweke; Uwasindikize ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wamisionari; Uwalinde ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wanaohubiri; Uwaangazie ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre na watawa waliokufa; Uwafikishe kwenye utukufu wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie hekima na ufahamu wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; Uwajalie elimu na shauri lako
Kwa ajili ya mapadre wako; wajalie wakuheshimu na wakuogope
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie subira na upendo
Kwa ajili ya mapadre wote; wajalie utii na upole
Kwa ajili ya mapadre wote; uwajalie hamu kuu ya kuokoa roho za watu
Kwa ajili ya mapadre wote; wape fadhila za imani, matumaini na mapendo
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie upendo mkuu kwa Ekaristi
Tunakuomba uwajalie mapadre wote; Waheshimu uhai na hadhi ya mtu ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote nguvu na bidii katika kazi zao ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote amani katika mahangaiko yao ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote upendo mkuu kwa Utatu Mtakatifu ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote upendo mkuu kwa Bikira Maria ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe mwanga wa Kristo ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wawe chumvi kwa ulimwengu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wajizoeze kujitoa sadaka na kujinyima ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wawe watakatifu kimwili, kiakili na kiroho ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe watu wa sala ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe kioo cha imani kwako ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wajali sana wongofu wetu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe waaminifu kwa wito wao wa kikuhani ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, ili mikono yao ibariki na kuponya ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawake moto wa mapendo yako ee Bwana
Uwajalie mapadre wote hatua zao zote ziwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wajazwe na Roho Mtakatifu na uwajalie karama zake kwa wingi ee Bwana.

Tuombe.
Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, usikie sala tunazokutolea kwa ajili ya mapadre wetu. Uwajalie wafahamu waziwazi kazi uliyowaitia kuifanya, uwape neema zote wanazohitaji ili waitikie wito wako kwa ushujaa, kwa upendo, na majitoleo yenye udumifu katika mapenzi yako matakatifu. Amina.

LITANIA YA KUWAOMBEA MAPADRE WOTE 1

Kwa ajili ya Baba Mtakatifu wetu ..(N); Bwana, umpe moyo wako wa uchungaji mwema
Kwa ajili ya warithi wa Mitume; Bwana, uwape wawe na uangalifu uliojaa upendo kwa mapadre wao
Kwa ajili ya Maaskofu wako waliochaguliwa na Roho Mtakatifu; Bwana, uwabakishe karibu na kondoo wako
Kwa ajili ya wachungaji wako; Bwana, uwafundishe kutumikia kuliko kutafuta kutumikiwa
Kwa ajili ya waungamishi na washauri wa kiroho; Bwana, uwafanye kuwa vyombo visikivu kwa Roho wako Mtakatifu
Kwa ajili ya mapadre wanaotangaza neno lako; Bwana, uwawezeshe kushirikisha Roho wako na Uzima wako
Kwa ajili ya mapadre wanaosaidia utume wa walei; Bwana, uwatie moyo wa kuwa mifano bora
Kwa ajili ya mapadre wanaofanya kazi na vijana; Bwana, uwajalie wawakabidhi vijana kwako
Kwa ajili ya mapadre wanaofanya kazi kati ya watu fukara; Bwana, uwajalie wakuone na wakutumikie kupitia hao
Kwa ajili ya mapadre wanaoangalia wagonjwa; Bwana, uwajalie wawafundishe thamani ya mateso
Kwa ajili ya mapadre fukara; – Uwasaidie ee Bwana
Kwa ajili ya mapade wagonjwa; – Uwaponye ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wazee; – Uwapatie tumaini la raha ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wenye huzuni na walioumizwa; -Uwafariji ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wanaohangaishwa na wale wanaosumbuliwa; – Uwape amani yako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wanaodharauliwa na wanaonyanyaswa; – Uwatetee ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre waliokata tamaa; – Uwatie moyo ee Bwana
Kwa ajili ya wale wanaosomea upadre; – Uwape udumifu ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; – Uwape uaminifu kwako na kwa Kanisa lako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; – Uwajalie utii na upendo kwa Baba Mtakatifu na kwa maaskofu wao ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; – Uwajalie waishi katika umoja na maaskofu wao ee Bwana
Tunawaombea mapadre wote; – Wawe wamoja kama Wewe na Baba mlivyo wamoja ee Bwana
Tunawaombea mapadre wote; – Waishi na kuendeleza haki yako ee Bwana
Tunawaombea mapadre wote; – Washirikiane katika umoja wa ukuhani wako ee Bwana
Tunawaombea mapadre wote, wakiwa wamejawa na uwepo wako; – Waishi maisha yao ya useja kwa furaha ee Bwana
Tunawaombea mapadre wote; – Wajalie ukamilifu wa Roho wako na uwageuze wafanane nawe ee Bwana
Kwa namna ya pekee, ninawaombea mapadre wale ambao kwa njia yao nimepokea neema zako. Ninamwombea padre aliyenibatiza na wale walioniondolea dhambi zangu, wakinipatanisha na Wewe na Kanisa lako.
Ninawaombea mapadre ambao nimeshiriki Misa walizoadhimisha, na walionipa Mwili wako kama chakula. Ninawaombea mapadre walionishirikisha Neno lako, na wale walionisaidia na kuniongoza kwako. Amina.

Matendo ya Rozari Takatifu: Mchanganuo kwa siku zote za Saba za Juma

MATENDO YA FURAHA (Jumatatu na Jumamosi)

  1. Tendo la kwanza; Malaika Gabrieli anampasha habari Maria kuwa atakuwa Mama wa Mungu. Tumwombe Mungu atujalie unyenyekevu.
  2. Tendo la pili; Maria Mtakatifu anakwenda kumtembelea Elizabeti. Tumwombe Mungu atujalie mapendo ya jirani.
  3. Tendo la tatu; Yesu anazaliwa Betlehemu. Tumwombe Mungu atujalie moyo wa ufukara
  4. Tendo la nne; Yesu anatolewa hekaluni. Tumwombe Mungu atujalie usafi wa moyo.
  5. Tendo la tano; Maria anamkuta Yesu hekaluni. Tumwombe Mungu atujalie kuwatii wakubwa wetu.

MATENDO YA UCHUNGU (Jumanne na Ijumaa)

  1. Tendo la kwanza; Yesu anatoka jasho la damu kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie sikitiko la dhambi.
  2. Tendo la pili; Yesu anapigwa kwa mijeledi kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kuacha dhambi za uchafu.
  3. Tendo la tatu; Yesu anatiwa miiba kichwani kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kushinda kiburi.
  4. Tendo la nne; Yesu anachukua Msalaba kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kuvumilia taabu.
  5. Tendo la tano; Yesu anakufa Msalabani. Tumwombe Mungu atujalie kuwapenda Yesu na Maria.

MATENDO YA UTUKUFU (Jumatano na Jumapili)

  1. Tendo la kwanza; Yesu anafufuka. Tumwombe Mungu atujalie kugeuka watakatifu.
  2. Tendo la pili; Yesu anapaa mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kwenda mbinguni.
  3. Tendo la tatu; Roho Mtakatifu anawashukia Mitume. Tumwombe Mungu atujalie bidii katika dini yetu.
  4. Tendo la nne; Bikira Maria anapalizwa mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kufa vizuri.
  5. Tendo la tano; Bikira Maria anawekwa Malkia mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kudumu katika njia njema.

MATENDO YA MWANGA (Alhamisi)

  1. Tendo la kwanza; Yesu anabatizwa Mto Jordani. Tumwombe Mungu atujalie uaminifu kwa ahadi zetu za ubatizo.
  2. Tendo la pili; Yesu anageuza maji kuwa divai huko Kana. Tumwombe Mungu atujalie kuukoleza ulimwengu kwa chachu ya enjili.
  3. Tendo la tatu; Yesu anatangaza Ufalme wa Mungu. Tumwombe Mungu atujalie kupokea Ufalme wake kwa toba ya kweli.
  4. Tendo la nne; Yesu anageuka sura. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kuung’arisha ulimwengu kwa uso wa Yesu.
  5. Tendo la tano; Yesu anaweka Sakramenti ya Ekaristia. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine.

Karibu Vitatabu vya Kikatoliki

Shopping Cart