Sala za Toba
SALA YA KUUABUDU MOYO MTAKATIFU WA YESU KATIKA EKARISTI TAKATIFU
Kwa nguvu zangu zote za moyo wangu/ ninakuabudu ee Moyo Mtakatifu/ na Mwabudiwa sana,/ Moyo Mtakatifu wa Bwana wetu Yesu Kristu/ ambao ninataka kumpenda/ na kukusalimu kwa usikivu unaoendelea./ Kamwe nisikuudhi tena/ kwa sababu Wewe ni Mwema sana;/ Ee Mwema sana./ Ee Moyo Mtakatifu sana/ ninakupenda/ na ninataka kukupenda zaidi ya vitu vyote,/ kwa nguvu zangu zote/ na kwa uwezo wangu wote,/ ninatamani kuwa mali yako/ Wewe uliyejitoa Msalabani kwa ajili yangu/ kwa mateso makali./ Unionee huruma na udhaifu wangu/ na usiniruhusu kupotea./
Ninajitoa kabisa kwako/ ee moyo wa mapendo,/ kwa makusudi kuwa utu wangu,/ maisha na mateso yangu/ yalipie kukupenda,/ kukuheshimu/ na kukutukuza Wewe sasa na milele./ Ninakupenda ee Moyo Mwabudiwa wa Mwokozi wangu,/ ninakuomba kwako/ uamuru moyo wangu na kila kitu ndani yangu/ kikutukuze sasa na milele./ Amina.
(Na Mt Margareta Maria Alakoki)
SALA YA BWANA: SALA YA BABA YETU
Baba yetu uliye mbinguni
Jina lako litukuzwe
Ufalme wako ufike
Utakalo lifanyike
Duniani kama mbinguni
Utupe leo mkate wetu wa kila siku
Utusamehe makosa yetu
Kama tunavyowasamehe
Na sisi waliotukosea
Usitutie katika kishawishi
Lakini utuopoe maovuni.
Amina.
SALA YA MAOMBI KWA MOYO MTAKATIFU WA YESU
Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakukimbilia, ninakuja kwako katika mikono yako yenye huruma. Ndiwe tegemeo langu na tumaini langu dhabiti. Ndiwe mwenye dawa ya maovu yangu yote, malipizi ya makosa yangu yote. Waweza kunipatia haja zangu na neema ninazoziomba mimi na wengine. Wewe uko ili kutusaidia sote, ndiwe mwanga mkuu usiozimika, ndiwe chanzo cha nguvu, uvumilivu, amani na faraja. Nina hakika kuwa maombi yangu hayatakuchosha, nawe hutaacha kunisaidia, kunilinda, kunipenda, kwani, ee Moyo Mtakatifu , upendo wako hauna mwisho. Ee Moyo Mtakatifu, unihurumie, kwa ajili ya maombi yangu, kadiri ya huruma yako. Nawe katika sisi, na kwa ajili yetu, ufanye lolote unalolihitaji, kwani tunajitoa kwako kwa imani na uhakika thabiti kwamba kamwe hautatuacha, kwa milele. Amina.
Sala ya Usiku kabla ya kulala
Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.
SALA YA KUSHUKURU
Tunakushukuru, ee Mungu, kwa mapaji uliyotujalia leo. Amina.
Baba yetu …
Salamu Maria …
SALA YA IMANI
Mungu wangu, nasadiki maneno yote. Linayosadiki na linayofundisha Kanisa Katoliki la Roma. Kwani ndiwe uliyetufumbulia hayo. Wala hudanganyiki, wala hudanganyi. Amina.
SALA YA MATUMAINI
Mungu wangu, natumaini kwako, nitapewa kwa njia ya Yesu Kristo. Neema zako hapa duniani, na utukufu mbinguni. Kwani ndiwe uliye agana hayo nasi, nawe mwamini. Amina.
SALA YA MAPENDO
Mungu wangu, nakupenda zaidi ya chochote. Kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza. Nampenda na jirani yangu, kama nafsi yangu, kwa ajili yako. Amina.
KUTUBU DHAMBI
Tuwaze katika moyo wetu makosa ya leo tuliyomkosea Mungu kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo na kwa kutotimiza wajibu. (Husubiri kidogo ).
Nakuungamia Mungu Mwenyezi, nanyi ndugu zangu, kwani nimekosa mno, kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo, na kwa kutotimiza wajibu.
Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana. Ndiyo maana nakuomba Maria mwenye heri, Bikira daima, Malaika na Watakatifu wote, nanyi ndugu zangu, niombeeni kwa Bwana Mungu wetu.
Mungu Mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele. Amina.
SALA YA KUWAOMBEA WATU
Ee Mungu, nawaombea watu wa nchi hii, wapate kusikia maneno yako na kukupenda wewe Bwana Mungu wetu.
SALA KWA MALAIKA MLINZI
Malaika mlinzi wangu, unilinde katika hatari zote za roho na za mwili. Amina.
MALAIKA WA BWANA
(kipindi kisicho cha Pasaka)
Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria.
Naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
Salamu, Maria,…..
Ndimi mtumishi wa Bwana.
Nitendewe ulivyonena.
Salamu, Maria….
Neno la Mungu akatwaa mwili.
Akakaa kwetu.
Salamu, Maria….
Utuombee, Mzazi mtakatifu wa Mungu.
Tujaliwe ahadi za Kristu.
Tuombe:
Tunakuomba, Ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika kwamba Mwanao amejifanya Mtu kwa mateso na msalaba wake tufikishwe kwenye utukufu wa ufufuko. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. AMINA.
AU;
MALKIA WA MBINGU (kipindi cha Pasaka)
Malkia wa mbingu, furahi, aleluya.
Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.
Amefufuka alivyosema, Aleluya.
Utuombee kwa Mungu, Aleluya.
Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Alaluya.
Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.
Tuombe.
Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu, Mwanao, fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.
ATUKUZWE (mara tatu)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Kama mwanzo na sasa na siku zote na milele. Amina.
KUJIKABIDHI
Enyi Yesu, Maria na Yosefu nawatolea moyo na roho na uzima wangu!
Enyi Yesu, Maria na Yosefu mnijilie saa ya kufa kwangu!
Enyi Yesu, Maria na Yosefu mnijalie nife mikononi mwenu!
(Rehema ya siku 300).
WIMBO:
Kwa heri Yesu mpenzi mwema,
Naenda usiudhike mno.
Nakushukuru, nakupenda,
Kwa hizo nyimbo za mwisho.
Asubuhi nitarudi.
Yesu kwa heri.
Kwa heri Mama mtakatifu,
Sasa napita pumzika.
Asante kwa moyo na nguvu,
Leo umeniombea.
Asubuhi nitarudi.
Mama kwa heri.
Kwa heri Yosefu mnyenyekevu,
Kazi zatimilizika.
Kama mchana, leo usiku,
Nisimamie salama.
Asubuhi nitarudi.
Yosefu kwa heri.
Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.
KUOMBA ULINZI WA USIKU
Mungu wangu naenda kulala naomba malaika 14, waende nami, wawili juu, wawili chini, wawili upande wa kuume, wawili upande wa kushoto, wawili wanifunike, wawili waniamshe, wawili wanipeleke juu mbinguni. Mimi mtoto mdogo, roho yangu ni ndogo, haina nafasi kwa mtu yoyote ila kwa Yesu pekee. Amina.
Recent Comments