Masomo ya Misa

Kanisa Katoliki La Roma

MASOMO YA MISA, APRILI 4, 2022: JUMATATU, JUMA LA 5 LA KWARESIMA

SOMO 1

 

Dan.13:41-62

 

Palikuwa na mtu mmoja jina lake Yoakimu, akikaa Babeli, naye ameoa mke jina lake Susana binti Helkia, mwanamke mzuri sana na mcha Mungu. Wazee wake nao walikuwa wenye haki, pia wamemfundisha binti yao sawasawa na Torati ya Musa. Basi Yoakimu alikuwa mwungwana tajiri, na karibu na nyumba yake alikuwa na bustani nzuri; hivyo Wayahudi humwendea, maana alikuwa ni mwenye heshima kupita wengineo wote. Mwaka ule ule wakaamriwa wawili miongoni mwa wazee wa watu ili kuamua, watu wa namna ile ambao Bwana aliwanena, ya kama ufisadi ulitoka Babeli kwa wazee waamuzi waliohesabiwa kuwa wanatawala watu. Hao walikuwa wakienda mara nyingi kuzuru kwenye nyumba yake Yoakimu; na wote wenye mashtaka yoyote desturi yao wakawajia huko. Basi watu walipoondoka kwenda zao panapo saa sita, Susana huingia katika bustani ya mumewe ili kutembea. Nao wale wazee humwona kila siku anakwenda kutembea; hata wakawaka tamaa kwa sababu yake. Ndipo walipozipotosha nia zao, wakayageuza upande macho yao wasiweze kutazama mbinguni wala kukumbuka hukumu za haki. Ikawa walipongoja wakati wa kufaa, yeye aliingia bustanini kama ilivyokuwa desturi yake pamoja na wajakazi wawili, naye alitaka kuoga kwa sababu kulikuwa na joto. Wala hapakuwa na mtu yeyote isipokuwa wale wazee wawili, ambao wamejificha wakimvizia. Basi akawaambia wajakazi wake, Nileteeni mafuta na sabuni, mkaifunge milango ya bustani ili nioge . Mara wale wajakazi walipokwishas kutoka, wale wazee wawili waliondoka wakamwendea mbio, wakasema, Tazama, milango ya bustani imefungwa asiweze kutuona mtu yeyote nasi tunakupenda sana; haya! Basi, utukubali na ulale nasi. La! Hutaki tutakushuhudia ya kuwa hapa palikuwapo na kijana pamoja nawe, ndiyo sababu uliwaruhusu wajakazi wako. Basi Susana aliugua akasema, Nimesongwa pande zote, maana nikilitenda hilo ni mauti yangu; nisipolitenda siwezi kuokoka mikononi mwenu. Ni afadhali niangukie katika mikono yenu na kukataa, kuliko kutenda dhambi machoni pa Mungu. Mara Susana akapiga kelele kwa sauti kuu; nao wale wazee wawili wakampigia kelele pia. Kisha mmoja wao akakimbia, akaifungua milango ya bustani. Hivyo watumishi wa nyumbani waliposikia kelele bustanini, wao waliingia kwa kasi kwa mlango wa nyuma ili waone ni nini iliyompata. Lakini wale wazee waliisimulia hadith yao nao watumishi wakaona aibu kabisa, kwa maana Susana hakuchongelewa habari ya namna hiyo wakati wowote.

Ikawa kesho yake watu walipokusanyika kwa Yoakimu mumewe, wale wazee wawili wakaja nao, wamejaa kusudi lao ovu juu ya Susana la kumfisha. Wakasema mbele ya watu, “Mwiteni Susana binti Helkia, mkewe Yoakim, aje hapa”. Basi akaenda kuitwa; naye akaja pamoja na baba yake na mama yake, na watoto wake, na jamaa zake wote. Naye huyo Susana alikuwa mwanamke mwenye adabu, mzuri wa uso; basi hao watu wabaya waliamuru afunuliwe uso, maana alifunikwa utaji, ili washibe uzuri wake. Kwa hiyo rafiki zake na wote waliomtazama wakasikitika. Ndipo wale wazee wawili waliposimama katikati ya watu, wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. Naye akatoka machozi, akatazama juu mbinguni, kwa maana moyo wake ulimtumaini Mungu. Wale wazee wakasema, Sisi tulipokuwa tukitembea bustanini peke yetu, huyu aliingia pamoja na wajakazi wawili, wakaifunga milango ya bustani, naye mara akawaruhusu wajakazi. Kisha kukatokea kijana, ambaye amejificha humo, akamwendea akalala naye. Walakini sisi tungaliko pembeni mwa bustani, tuliona ubaya huo, tukamwendea mbio. Hata tukiwa tumewaona pamoja, yule kijana hatukuweza kumkamata, maana alikuwa mwenye nguvu kuliko sisi, akifungua milango akaepuka. Bali huyu tulimkamata, tukauliza yule kijana yu nani, asikubali kutuambia. Hayo basi, tunashuhudu. Basi waliohudhuria wakawasadiki, wakiwa wazee wa watu na waamuzi; hivyo wakahukumu auawe. Mara Susana akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Mungu wa milele, Wewe wajua yaliyositirika, wajua mambo yote yasijekuwako, Wewe wajua ya kwamba wananishuhudia uongo, na tazama, imenipasa kufa; walakini sikufanya mambo kama hayo, ambayo watu hawa wameyabuni juu yangu kwa ukorofi.

Naye Bwana akaisikia sauti yake. Kwa hiyo, alipochukuliwa huyo kwenda kuuawa, Mungu alimchocheleza roho kijana mmoja, jina lake Danieli; naye akapaza sauti akasema, Mimi simo; mimi sina hatia kwa habari ya damu yake mwanamke huyu. Mara wote wakamgeukia, wakasema, Maneno hayo uyasemayo, maana yake nini? Akasimama katikati, akasema, Enyi bani Israeli, mmekuwa wapumbavu, hata kumhukumu binti Israeli bila kuhoji wala kupata hakika ya kweli? Rudini hukumuni; mradi hao wanamshuhudia uongo.

Basi watu wote walirejea kwa haraka, nao wale wazee wakamwambia, Njoo uketi kati yetu, utujulishe habari hiyo, endapo Mungu amekupa wewe heshima yam zee. Hapo Danieli aliwaambia, Watu hawa wawili watengwe, nami nitawahoji. Basi wakiisha kutengwa, akamwita mmoja wao akamwambia, Ewe uliyepata kuwa mzee katika uovu, sasa dhambi zako zimekukalia, ulizozitenda zamani kwa kuhukumu isivyo haki, kumpatiliza asiye na hatia na kumwachilia mwovu; lakini Bwana asema, Asiye na hatia, mwenye haki, usimwue. Haya! Basi, wewe ulimwona kwa macho; useme; Chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, Chini ya msandarusi. Danieli akasema, Hakika umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana sas hivi malaika wa Mungu amepokea hukumu ya Mungu, akukate vipande viwili. akamtenga huyo tena, akaamuru kumleta yule mwingine, akamwambia, Ewe mzao wa Kanaani, wala si wa Yuda, uzuri umekudanganya, na tamaa imeupotosha moyo wako. Hivyo ndivyo ulivyowafanyia binti za Israeli, na kwa hofu walitembea nawe; bali huyu binti Yuda hakuweza kuustahimili uovu wako. Haya! Basi, nawe useme; Chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, Chini ya mkwaju. Danieli akamwambia, Hakika wewe nawe umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana malaika wa Mungu yu tayari, anakungoja mwenye upanga, akukate vipande viwili; ili awaangamize nyote wawili.

Mara hiyo makusanyiko yote wakapaza sauti kwa nguvu, wakamhimidi Mungu awaokoaye wamtumainio. Wakawaondokea wale wazee wawili, kwa maana Danieli ameuhakikisha ushuhuda wao wa uongo hata vinywani mwao wenyewe. Wakawatenda kwa Torati ya Musa kama vile walivyokusudia kwa ukorofi kumfanyia jirani yao; wakawaua; na mwenye damu isiyo na hatia aliokolewa siku ile.

 

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

 

WIMBO WA KATIKATI

 

Zab. 23 (K) 4

 

(K) Nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami.

 

Bwana ndiye mchungaji wangu,

Sitapungukiwa na kitu.

Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,

Kando ya maji ya utulivu huniongoza. (K)

 

Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza,

Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.

Naam, nijapopita kati aya bonde la uvuli wa mauti

Sitaogopa mabaya; kwa maana Wewe upo pamoja nami,

Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)

 

Waandaa meza mbele yangu,

Machoni pa watesi wangu.

Umenipaka mafuta kichwani pangu,

Na kikombe change kinafurika. (K)

 

Hakika wema na fadhili zinanifuata,

Siku zote za maisha yangu,

Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)

 

SHANGILIO

 

Yn. 6:64, 69

 

Maneno yako, Ee Bwana, ni roho, tena ni uzima, Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.

 

INJILI

 

Yn. 8:12-20

 

Yesu aliwaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.

Basi Mafarisayo wakamwambia, Wewe unajishuhudia mwenyewe; ushuhuda wako si kweli.

Yesu akajibu, akawaambia, Mimi ningawa ninajishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ndio kweli; kwa sababu najua nilikotoka na niendako; lakini ninyi hamjui nilikotoka wala niendako. Ninyi mwahukumu kwa kufuata mambo ya mwili; mimi simhukumu mtu. Nami nijapohukumu, hukumu yangu ni kweli; kwa kuwa mimi si peke yangu, bali ni mimi nay eye aliyenipeleka. Tena katika torati yenu imeandikwa kwamba, Ushuhuda wa watu wawili ni kweli. Mimi ndimi ninayejishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenipeleka ananishuhudia.

Basi wakamwambia, Yuko wapi Baba yako? Yesu akajibu, Mimi hamnijui, wala Baba yangu hammjui kama mngalinijijua mimi, mngalimjua na Baba yangu.

Maneno hayo aliyasema alipokuwa akifundisha hekaluni, katika chumba cha hazina; wala hakuna mtu aliyemkamata, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.

 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Biblia Takatifu

MASOMO YA MISA, JULAI 24, 2021: JUMAMOSI, JUMA LA 16 LA MWAKA

SOMO 1

Kut. 24:3-8

Musa aliwambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. Basi Musa akayaandika maneno yote ya Bwana, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli, akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng’ombe. Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 50:1-2, 5-6, 14-15 (K) 14 (K)

Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru. Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi, Toka maawio ya jua hata machweo yake. Tokea Sayuni,, ukamilifu wa uzuri, Mungu amemulika. (K)

Nikusanyieni wacha Mungu wangu, Waliofanya agano nami kwa dhabihu. Na mbingu zitatangaza haki yake, Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu. (K)

Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru; Mtimizie Aliye juu nadhiri zako. Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza. (K)

SHANGILIO

Zab. 8:15

Aleluya, aleluya,

Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao, hulisikia neno la Mungu na kulishika.

Aleluya.

INJILI

Mt. 13:24 – 30

Yesu aliwatolea makutano mfano akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala akaja adui yake akapanda magugu katikati ya agano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Biblia Takatifu

MASOMO YA MISA, JULAI 26, 2021 JUMATATU, JUMA LA 17 LA MWAKA

SOMO 1

Kut. 32:15-24, 30-34

Musa aligeuka akashuka katika mlima, na zile mbao mbili za mawe mikononi mwake; mbao ziliandikwa pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa. Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu, nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao.

Na Yoshua aliposikia kelele za watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, Kuna kelele ya vita maragoni. Akasema, Hiyo si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao nizo ninazozisikia mimi.

Hata alipyakaribia marago akaiona ile ndama, na ile michezo. Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima. Akaitwaa ile ndama walioifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli. Musa akamwambia Haruni; Watu hawa wamekufanyani hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao? Haruni akasema, Hasira ya bwana wangu isiwake; wewe unawajua watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya. Maana waliniambia, Katufanyie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata. Nikawaambia, Mtu yeyote aliye na dhahabu na aivunje; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu.

Basi asubuhi yake Musa akawaambia watu, Mmetenda dhambi kuu; na sasa nitakwenda juu kwa Bwana, labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu. Musa akarejea kwa Bwana akasema, Aa! Watu hawa wametenda dhambi kuu, wamejifanyia miungu ya dhahabu. Walakini sasa ikiwa utawasamehe dhambi yao – na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichokiandika. Bwana akamwambia Musa, Mtu yoyote aliyenitenda dhambi, ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. Basi sasa uende ukawaongoze watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekuambia habari zake; tazama, malaika wangu atakutangulia; pamoja na hayo siku nitakayowajilia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 106:19-23 (K) 1

(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.

Walifanya ndama huko Horebu,

Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.

Wakaubadili utukufu wao,

Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani. (K)

Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,

Aliyetenda makuu katika Misri.

Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,

Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu. (K)

Akasema ya kuwa atawaangamiza,

Kama Musa, mteule wake, asingalisimama,

Mbele zake kama mahali palipobomoka,

Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu. (K)

SHANGILIO

Efe. 1:17, 18

Aleluya, aleluya,

Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristu, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.

Aleluya.

INJILI

Mt. 13:31 – 35

Yesu aliwatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake.

Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia.

Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu awali.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Shopping Cart
Scroll to Top