MASOMO YA MISA, JULAI 26, 2021 JUMATATU, JUMA LA 17 LA MWAKA

SOMO 1

Kut. 32:15-24, 30-34

Musa aligeuka akashuka katika mlima, na zile mbao mbili za mawe mikononi mwake; mbao ziliandikwa pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa. Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu, nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao.

Na Yoshua aliposikia kelele za watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, Kuna kelele ya vita maragoni. Akasema, Hiyo si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao nizo ninazozisikia mimi.

Hata alipyakaribia marago akaiona ile ndama, na ile michezo. Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima. Akaitwaa ile ndama walioifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli. Musa akamwambia Haruni; Watu hawa wamekufanyani hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao? Haruni akasema, Hasira ya bwana wangu isiwake; wewe unawajua watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya. Maana waliniambia, Katufanyie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata. Nikawaambia, Mtu yeyote aliye na dhahabu na aivunje; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu.

Basi asubuhi yake Musa akawaambia watu, Mmetenda dhambi kuu; na sasa nitakwenda juu kwa Bwana, labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu. Musa akarejea kwa Bwana akasema, Aa! Watu hawa wametenda dhambi kuu, wamejifanyia miungu ya dhahabu. Walakini sasa ikiwa utawasamehe dhambi yao – na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichokiandika. Bwana akamwambia Musa, Mtu yoyote aliyenitenda dhambi, ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. Basi sasa uende ukawaongoze watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekuambia habari zake; tazama, malaika wangu atakutangulia; pamoja na hayo siku nitakayowajilia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 106:19-23 (K) 1

(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.

Walifanya ndama huko Horebu,

Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.

Wakaubadili utukufu wao,

Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani. (K)

Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,

Aliyetenda makuu katika Misri.

Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,

Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu. (K)

Akasema ya kuwa atawaangamiza,

Kama Musa, mteule wake, asingalisimama,

Mbele zake kama mahali palipobomoka,

Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu. (K)

SHANGILIO

Efe. 1:17, 18

Aleluya, aleluya,

Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristu, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.

Aleluya.

INJILI

Mt. 13:31 – 35

Yesu aliwatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake.

Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia.

Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu awali.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Melkisedeck Leon Shine

Editor: Melkisedeck Leon Shine. About Me | Contact Me | LinkedIn | TikTok | WhatsApp

Read and Write Comments
Shopping Cart