MASOMO YA MISA, MACHI 26, 2022: JUMAMOSI, JUMA LA 3 LA KWARESIMA

SOMO 1

Hos. 5:15-6:6

Bwana asema: Katika taabu yao watanitafuta kwa bidii:

Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu. Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tuataishi mbele zake. Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyeshayo nchi.

Ee Efraimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema. Kwa sababu hiyo nimewakata-kata kwa vinya vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa change na hukumu yangu itatokea kama mwanga. Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 51:1-2, 16-19 (K) Hos. 6:6

(K) Ninavyotaka ni fadhili, si sadaka.

Ee Mungu, unirehemu,

Sawasawa na fadhili zako.

Kiasi cha wingi wa rehema zako,

Uyafute makosa yangu.

Unioshe kabisa na uovu wangu,

Unitakase dhambi zangu. (K)

Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,

Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.

Dhabihu za MUngu ni roho iliyovunjika;

Moyo uliovunjika na kupondeka,

Ee Mungu, hutaudharau. (K)

Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako,

Uzijenge kuta za Yerusalemu.

Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki,

Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. (K)

SHANGILIO

Eze. 18:3

Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa yote, asema Bwana, jifanyieni moy mpya na roho mpya.

INJILI

Lk. 18:9-14

Yesu aliwaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mpato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Shopping Cart