Masomo ya Misa ya Kanisa Katoliki

MASOMO YA MISA, JUNI 18, 2023: JUMAPILI, JUMA LA 11 LA MWAKA

SOMO 1 

Kut. 19 :2-6

Waisraeli walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; wakapiga kambi huko wakiukabili mlima. Musa akapanda kwa Mungu, na Bwana akamwita toka mlima ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya: Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi. Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu, nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI 

Zab. 100 :2-3, 5 (K) 3

(K) Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.

Mtumikieni Bwana kwa furaha;

Njoni mbele zake kwa kuimba. (K)

Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;

Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;

Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)

Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;

Rehema zake ni za milele;

Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)

SOMO 2 

Rum. 5 : 6-11

Wapendwa, hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyesha pendo lake veye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake, zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, am have kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANG1LIO 

Yn. 15 :15

Aleluya, aleluya, Ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.

Aleluya.

INJILI 

Mt. 9:36-10:8

Yesu alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza

magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye; Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti. Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, JUNI 11, 2023: SHEREHE YA MWILI NA DAMU TAKATIFU YA BWANA WETU YESU KRISTU

SOMO 1

Kum. 8:2-3;14-16

Musa aliwaambia makutano: Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako, aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu, kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo. Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana. Basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 147:12-15,19-20 (K) 12

(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.

Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;

Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.

Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,

Amewabariki wanao ndani yako. (K)

Ndiye afanyaye amani mipakani mwako,

Akushibishaye kwa unono wa ngano.

Huipeleka amri yake juu ya nchi,

Neno lake lapiga mbio sana. (K)

Humhubiri Yakobo neno lake,

Na Israeli amri zake na hukumu zake.

Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,

Wala hukumu zake hawakuzijua.

aleluya. (K)

SOMO 2

1Kor. 10:16-17

Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANG1LIO

Yn. 6:51

Aleluya, aleluya,

Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; asema Bwana; mtu akila chakula hiki, ataishi milele.

Aleluya.

INJILI

Yn. 6:51-58

Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Basi Wayahudi walishindana wao kwa wao wakisema, Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule? Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi. Hiki ndicho chakula kishukacho kutoka mbinguni; si kama mababa walivyokula, wakafa; bali akilaye chakula hicho ataishi milele.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, JUNI 04, 2023: SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU – Jumapili baada ya Pentekoste

MWANZO:

Asifiwe Mungu Baba na Mwana na Roho Mtakatifu; kwasababu ametufanyizia huruma yake.

SOMO 1

Kut. 34 : 4-6, 8-9

Musa aliinuka na mapema asubuhi, naye akakwea katika mlima wa Sinai, kama Bwana alivyomwamuru, akazichukua hizo mbao mbili za mawe mkononi mwake.

Bwana akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la Bwana. Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; Musa akafanya haraka, akainamisha kichwa chake hata nchi, akasujudu. Akasema, Ikiwa sasa nimepata neema mbele zako, Bwana, nakuomba, Bwana, uende kati yetu maana ni watu wenye shingo ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi yetu, ukatutwae tuwe urithi wako.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu

WIMBO WA KATIKATI

Dan. 3:52-56. (K) 52

(K) Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu:

Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu;

Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)

Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu;

Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako;

Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)

Umehimidiwa utazamaye vilindi, uketiye juu ya makerubi;

Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni

Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)

SOMO 2

2 Kor. 13 :11-14

Hatimaye, ndugu, kwaherini; mtimilike, mfariji- ke, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi. Sali- mianeni kwa busu takatifu. Watakatifu wote wawasalimu. Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu. na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

SHANG1LIO

Ufu. 1 :8

Aleluya, Aleluya,

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, Mungu ambaye yupo, aliyekuwako, na atakayekuja.

Aleluya.

INJILI

Yn. 3:16-18

Yesu alimwambia Nikodemu: Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhu- kumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.

Neno la Bwanaโ€ฆ Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MEI, 28, 2023: SHEREHE YA PENTEKOSTE

SOMO 1

Mdo. 2:1-11

Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.


Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Waparthi na Wamedi na Waelani, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu

WIMBO WA KATI KATI

Zab. 104:1, 24, 29-31, 34, (K) 30

(K) Waipeleka roho yako, Ee Bwana, Nawe waufanya upya uso wa nchi. au: Aleluya.

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wewe, Bwana, Mungu wangu,
Umejifanya mkuu sana;
Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
Dunia imejaa mali zako. (K)

Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
Na kuyarudia mavumbi yao,
Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
Nawe waufanya upya uso wa nchi. (K)

Utukufu wa Bwana na udumu milele;
Bwana na ayafurahie matendo yake.
Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake;
Mimi nitamfurahia Bwana. (K)

SOMO 2

1 Kor. 12 :3b-7, 12-13

Hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.

Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu

SHANGILIO

Aleluya, aleluya,
Uje Roho Mtakatifu, uzienee nyoyo za waamini wako uwatie mapendo yako.
Aleluya.

INJILI

Yn. 20 :19-23

Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.
Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

MASOMO YA MISA, MEI 24, 2023: JUMATANO YA 7 YA PASAKA

SOMO 1

Mdo 20 : 28-38

Paulo aliwaambia wakuu wa kanisa ya Efeso: Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwamwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu, wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao. Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi. Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa. Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea. Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote. Wakalia sana wote, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusu-busu, wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza hata merikebuni.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 68:28-29, 32-35 (K) 32

(K) Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu.
Au: Aleluya.

Ee Mungu, uziamuru nguvu zako;
Ee Mungu, uwe hodari uliyetufanyia makuu.
Kwa ajili ya hekalu lako Yerusalemu
Wafalme watakuletea hedaya. (K)

Enyi falme za dunia, mwimbieni Mungu,
Msifuni Bwana kwa nyimbo.
Apandaye mbingu za mbingu za tangu milele;
Aitoa sauti yake, sauti ya nguvu.
Mhesabieni Mungu nguvu; (K)

Enzi yake i juu ya Israeli;
Na nguvu zake zi mawinguni.
Mungu ni mwenye kutisha Kutoka patakatifu pako.
Ndiye Mungu wa Israeli;
Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo.
Na ahimidiwe Mungu. (K)

SHANGILIO

Yn. 14 : 26

Aleluya, aleluya,
Roho Mtakatifu atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
Aleluya.

INJILI

Yn. 17:11-19

Siku ile, Yesu alisali akisema: Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.

Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.

Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.

Shopping Cart