Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Jinsi ya kupika Magimbi Kwa Nyama Ya Ng’ombe

Vipimo

Majimbi (Eddoes) kiasi 6 au 7

Nyama ng’ombe ½ kilos

Tangawizi ilosagwa 1 kijiko cha kulia

Haldi (bizari manjano/turmeric) ½ kijiko cha chai

Tui zito la nazi vikombe 2

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha nyama kisha weka chumvi, bizari ya manjano, tangawizi mbichi, ukaushe kwanza katika sufuria kwa kukaanga kaanga.
Ikianza kukauka, weka maji funika uchemshe iwive.
Menya majimbi ukate kate na uweke katika sufuria nyengine.
Mimina supu na nyama katika majimbi uchemshe yawive majimbi.
Mwisho weka tui zito la nazi uchanganye vizuri kisha weka katika moto kidogo tu bila kufunika yakiwa tayari.

Jinsi ya kupika vitumbua inavyotakiwa

Mahitaji

Unga wa mchele ( Vikombe 2 vikubwa)
Sukari (Nusu ya kikombe kikubwa)
Hamira ( Nusu ya kijiko cha chai)
Hiliki (Nusu ya kijiko cha chai)
Tui la nazi ( Kikombe kimoja kikubwa)
Unga wa ngano (Vijiko viwili vya chakula)
Mafuta ya kuchomea (Vegetable oil)

Matayarisho

Unachanga unga, sukari, hamira, hiliki, unga wa ngano na tui la nazi pamoja katika bakuli la plastiki. Kisha unaukoroga mpaka mchanganyiko unakuwa kama uji mzito. Kava bakuli lililokuwa na mchanganyiko kisha hifadhi katika sehemu yenye joto kwa muda wa masaa matatu.

Jinsi ya kupika

Weka chuma cha kuchomea vitumbua katika moto wa wastani, kisha weka mafuta kwenye chuma cha kuchomea ( Kijiko kimoja cha chai) mafuta yakisha pata moto tia uji wako (upawa mmoja) katika kila shimo la chuma cha kuchomea. Acha mpaka kitumbua kikauke kisha geuza na tia mafuta. Acha upande wa pili wa kitumbua mpaka uwe rangi ya kahawia na hapo kitumbua kitakuwa kimeiva utakitoa. Rudia hatua hizo kwa vitumbua vyote vilivyobaki.

Mapishi ya Ugali Kwa Mchuzi Wa Nyama, Mchicha, Maharage Na Chatini Ya Pilipili Mbichi

Vipimo Vya Mchuzi Wa Nyama

Nyama ya ng’ombe vipande vidogo – 2lb

Nyanya – 1

Kitunguu Kilichoktwa katwa – 1

Mafuta – 2 vijiko vya supu

Paprika (bizari ya masala ya rangi) – ½ kijiko cha chai

Kidonge cha supu – 1

Chumvi – Kiasi

Ndimu – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha nyama kwa chungio ili itoke maji. Kwenye sufuria, weka mafuta na ukaange vitunguu mpaka viwerangi ya hudhurungi.
Kisha tia nyama na kidonge cha supu uwachie moto mdogo mpaka iwive.
Halafu tia nyanya na paprika ufunike sufuria na uiwache motoni mpaka ikauke, kamulia ndimu na itakuwa tayari.

Vipimo Vya Mboga

Mchicha ulio katwa katwa 400 gm

Nyanya 1

Kitunguu kilicho katwa 1

Nazi ya unga kiasi

Pilipili mbichi 2

Mafuta ½ kijiko cha supu

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha na Kupika

Osha mboga vizuri mpaka iwe haina mchanga.
Katika sufuria, kaanga vitungu hadi viwe laini.
Tia nyanya, mboga, pilipili na chumvi ikisha toa maji
Tia nazi na utaiwacha motoni mpaka ikauke kiasi na itakuwa
tayari kuliwa

Vipimo Vya Maharage

Maharage – 1 kopo

Kitunguu – 1

Nazi – 1 mug

Nyanya (itowe maganda) – 1 kiasi

Pilipili mbichi – 2

Mafuta – 1 kijiko cha supu

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na kupika

Tia mafuta katika sufuria na ukaanga vitungu mpaka vilainike.
kisha tia nyanya na pilipili na ukaange kidogo.
Tia chumvi, maharage na nazi uwachie
moto mdogo mpaka iwe nzito kiasi na itakuwa tayari.

Vipimo Vya chatini Ya Pilipili mbichi

Pilipili mbichi – 4/5

Kotmiri – 1 Kijiko cha supu

Ndimu – kiasi

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 chembe

Mafuta ya zaituni – 2 vijiko Vya supu

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha

Kwenye blender, tia vipimo vyote na sage isipokuwa chumvi tia mwisho kwa juu kwenye bakuli na itakuwa tayari kwa kuliwa.

Vipimo Vya ugali

Maji – 4 Vikombe kiasi inategemea na unga

Unga wa sembe – 2 vikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Tia maji kiasi katika sufuria, weka motoni, yakipata moto korogea unga wa sembe kiasi na ufanye uji mzito uache uchemke vizuri huku ukikoroga.
Chota kibakuli kimoja cha uji huo weka pembeni kisha mimina unga wote uliobaki upigepige uchanganyike vizuri kwenye uji huo mpaka ushikamane
Punguza moto anza kuusonga taratibu huku ukiongeza ule uji ulioweka pembeni kidogo kidogo mpaka uone sasa umeshikamana vizuri.
Endelea kusonga mpaka ulainike kisha mimina kwenye bakuli au sahani na itakuwa tayari kwa kuliwa na mchuzi wa nyama, maharage, mboga na chatini.

Mapishi ya Maharage

Mahitaji

Maharage (beans 2 vikombe vya chai)
Nazi (coconut milk kiasi)
Vitunguu maji (onion 1kikubwa)
Nyanya (fresh tomato 1)
Kitunguu swaum (garlic paste 1/4 kijiko cha chai)
Chumvi (salt kiasi)
Curry powder 1 kijiko cha chai
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Chemsha maharage mpaka yaive kisha yaweke pembeni. Kaanga vitunguu maji na mafuta mpaka vianze kuwa vya brown kisha weka kitunguu swaum,nyanya na curry powder. kaanga mpaka nyanya iive kisha tia maharage na chumvi kiasi. Geuza mpaka mchanganyiko uchanganyike vizuri. Baada ya hapo tia tui la nazi na ukoroge vizuri na uache lichemke mpaka liive. Baada ya hapo ipua na maharage yatakuwa tayari kwa kuliwa

Mapishi ya Pilau Ya Nyama ya Kusaga, Adesi Za Brauni Na Zabibu

Mahitaji

Mchele wa Par boiled au basmati – 5 vikombe

Nyama kondoo/mbuzi ya kusaga – 1 kikombe

Kitunguu – 2

Kitunguu saumu (thomu/galic) – 7 chembe

Adesi za brauni (brown lentils) – 1 kikombe

Zabibu – 1 kikombe

Baharaat/bizari mchanganyiko – 1 kijiko cha supu

Chumvi – kiasi

Pilipilii manga – ½ kijiko

Jiyra/bizari pilau/cummin – 1 kijiko cha chai

Supu ya nyama ng’ombe – Kiasi cha kufunikia mchele

Mafuta – ½ kikombe

Namna Ya Kutayarisha

Osha, roweka masaa 2 au zaidi.

Katakata (chopped)

Menya, saga, chuna

Osha, roweka, kisha chemsha ziive nusu kiini.

Osha, chuja maji

Namna Ya Kupika:

Tia mafuta katika sufuria, kaanga vitunguu hadi vianze kugeuka vyekundu.
Tia kitunguu thomu, kaanga, tia baharati/bizari zote kaanga.
Tia nyama uchanganye vizuri, ukaange iwive..
Tia mchele ukaange kidogo kisha tia supu, koroga kidogo, funika uivie mchele.
Karibu na kuiva, tia adesi, zabibu, changanya, funika uendelee kuiva kama unavyopika pilau.
Epua pakua katika chombo, ongezea zabibu kupambia ukipenda

Mapishi mazuri ya Wali Wa Kukaanga Kwa Kidari Cha Kuku

Vipimo vya Wali:

Mchele – 3 vikombe

*Maji ya kupikia – 5 vikombe

*Kidonge cha supu – 1

Samli – 2 vijiko vya supu

Chumvi kiasi

Hiliki – 3 chembe

Bay leaf – 1

Vipimo Vya Kuku

Kidari (chicken breast) – 1Kilo

Kitunguu – 1

Tangawizi mbichi – ½ kipande

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 7 chembe

Pilipili mbichi – 3

Ndimu – 2

Pilipilimanga – 1 kijiko cha chai

Mdalasini – ½ kijiko cha chai

Jira/Cummin ya unga – 1 kijiko cha chai

Maji – ¼ kikombe

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Wali:

Osha na roweka mchele kisha weka sufuria katika moto tia samli ipashe moto.
Tia hiliki, bay leaf, kaanga, kisha tia mchele ukaange kidogo.
Tia maji, chumvi na kidonge cha supu, upike wali kama unavyopika pilau.
*Maji kisia kwa kutegemea mchele ulivyo.
*Unaweza kutumia supu yoyote badala ya kidonge.

Kuku:

Katakata kidari cha kuku vipande vya kiasi, weka katika sufuria, tia ndimu, bizari zote, chumvi.
Katakata kitunguu vipande vidogodogo, pilipili, na kitunguu thomu (chopped), tia katika kuku.
Chuna tangawizi mbichi tia katika kuku. Changanya vitu vyote vizuri.
Tia maji kiasi ¼ kikombe tu kiasi cha kumkaushia kuku. Weka katika moto mpike huku unageuzageuza. Anapokaribia kukauka epua akiwa tayari kuliwa na wali (na saladi upendayo)

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About