Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Jinsi ya kuandaa Pilau ya sosi ya soya, nyama na mboga

Mahitaji

Nyama isiyokuwa na mifupa – 1 ½ Lb(ratili)
Mchele wa Basmati (rowanisha) – 3 Magi
Vitunguu maji – 2
Mchanganyiko wa mboga za barafu – 1 Magi
(karoti, mahindi, njegere)
Pilipili Mbichi – 3
Pilipili mboga kijani na nyekundu – 1
Pilipili manga – ½ kijiko cha chai
Chumvi – Kiasi
Sosi ya soya (soy sauce) – 5 Vijiko vya supu
Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi iliyosagwa – 1 Kijiko cha supu
Mchanganyiko wa bizari (garam masala) – 1 Kijiko cha supu
Kotmiri iliyokatwa – ½ Kikombe
Mafuta ya kukaangia – Kiasi

Namna Ya Kutaarisha

Ndani ya sufuria, tia mafuta yakipata moto kaanga vitunguu mpaka ziwe rangi ya hudhurungi.
Kisha tia nyama iliyokatwa vipande vidogo vidogo pamoja na maji ya kiasi na viungo vyote isipokuwa mchele, mboga zote na kotmiri. chemsha mpaka nyama iwive na maji yakauke.
Halafu changanya na mboga na iwache kwa muda wa dakika kumi kisha tia kotmiri na umimine kwenye bakuli au treya ya oveni na uweke kando.
Chemsha mchele na chumvi uwive kama kawaida ya kupika wali wa kuchuja, kisha umwagie juu ya ile treya ya nyama.
Nyunyizia mafuta na sosi ya soya na ipike katika oveni moto wa 350° kwa muda wa dakika 20 hivi.
Ukishawiva, uchanganye ukiwa tayari kwa kuliwa

Jinsi ya kutengeneza Keki Ya Mbegu Za Mchicha

Viamba upishi

Unga ngano vikombc 3
Unga mbegu za mchicha kikombe 1
Baking powder vijiko vidogo
Maziwa kikombe 1
Sukari kikombe 1
Blue band kikombe ½
Mayai 10-12

Hatua

• Chagua, osha, kausha mbegu za mchicha mweupe, kisha saga zilainike.
• Chekecha unga wa ngano, unga wa mbegu za mchicha na baking powder Kwenye bakuli kubwa.
• Ongeza sukari na changanya.
• Ongeza mayai kidogo, kidogo ukikoroga na mwiko kwenda njia moja mpaka ilainike.
• Kama rojo ni zito ongeza mayai, au maziwa ili iwe laini, ongeza vanilla na koroga.
• Paka mafuta kwenye chombo cha kuoka au sufuria na chekechea unga kidogo.
• Mimina rojo ya keki na oka kwenye oveni au kama ni sufuria funika, weka moto mwingi juu, chini weka moto kidogo.
• Ukinusia harufu nzuri ya vanilla, funua, choma kisu katikati ya keki, kama ni kavu epua, pozesha na pakua kama kitafunio.

Jinsi ya kutengeneza Fagi Ya Kumumunyuka Mdomoni

VIAMBAUPISHI

Maziwa mazito matamu (condensed milk) – 2 vibati

Sukari – 1 kikombe

Samli 1 ½ kikombe

Vanilla 2 kifuniko cha chupa yake

Hiliki ilosagwa – 2 vijiko vya chai

Sinia kubwa ya bati Paka samli

MAANDALIZI

Changanya maziwa, sukari na samli katika sufuria isiyogandisha chakula (non-stick) uweke katika moto.
Koroga huku ikipikika hadi ianze kugeuka rangi na kuanza kuachana. Usiache mkono kuroga isije kufanya madonge.
Tia hiliki na vanilla, endelea kuipika.
Itakapogeuka rangi vizuri mimina katika sinia na haraka uitandaze kwa mwiko huku ukiuchovya katika maji na kuendelea kuitandaza hadi ikae sawa kote.
Pitisha kisu kuikataka ili ikipoa iwe wepesi kuitoa vipande.

Kila inapozidi kupoa na kukaa ndipo fagi inakauka na kumumunyuka.

Jinsi ya kupika Donati

Viamba upishi

Unga
2 Magi (kikombe kibuwa cha chai)

Sukari
1/3 Kikombe cha chai
Mayai 5

Siagi 4 Vijiko vya chakula

Hamira 1 Kijiko cha chakula

Baking Powder 1 Kijiko cha chai

Vanilla 1 Kijiko cha chai

Hiliki zilizosagwa 1 Kijiko cha chai

Sukari ya laini ya unga

(icing sugar) 1 Magi

Jinsi ya kuandaa na kupika

Unavunja mayai, unatia sukari, hamira, baking powder, vanilla na hiliki ikisha unapiga kwa kutumia mchapo wa kupigia keki. Unapiga mchanganyiko kwa muda wa dakika tano.

Unatia siagi kwenye sufuria na unaiyayusha na kuipasha moto mpaka iwe moto ikisha unaimimina kwenye mchanganyiko na unapiga tena kwa dakika mbili tu.

Unatia unga kwenye sinia au bakuli kubwa ikisha unamimina ule mchanganyiko kwenye unga na unaukanda kutumia mkono, mpaka ulainike.

Ukiona unga mwingi basi ongeza maziwa kidogo mpaka uwe sawa, na ukiona unga mwepesi sana basi unaweza kuongeza unga kidogo pia mpaka ukae sawa mfano wa unga wa maandazi.

Sukuma na ukate madonge kama unavyoyaona hapo juu. Tumia kifuniko cha chupa kwa kukatia kiduara kidogo katikakti ya madonge.
Ukimaliza kukata madonge yote, yaweke kidogo yavimbe halafu teleka mafuta na uyachome.
Ukitoa kwenye mafuta yachuje moto na kabla ya kupoa yawe moto moto yarovye kwenye icing sugar na uhakikishe yote yameenea sukari juu.
Ukimaliza tia kwenye sahani acha zipowe na zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kutengeneza Slesi Za Chokoleti Na Karameli

VIAMBAUPISHI

Unga – 1 Magi (vikombe vya chai)

Sukari ya browni – ½ Magi

Siagi iliyoyayushwa – 125 g

Nazi iliyokunwa – ½ Magi

MJAZO WA KARMEL (Caramel filling)

Syrup – 1/3 kikombe cha chai

Siagi iliyoyayushwa – 125 g

Maziwa matamu ya mgando – 2 vikopo (condensed milk)

MJAZO WA CHOKOLETI (Chocolate filling)

Chokoleti – 185 g (dark chocolate)

Mafuta – 3 Vijiko vya chai

MAANDALIZI

Changanya unga, sukari, siagi na nazi iliyokunwa kwenye bakuli mpaka unga ushikamane.
Paka mafuta treya ya kuchomea kisha utandaze kwenye treya ya 20cm kwa 30 cm au (8 in kwa 12 in) unaweza kuweka karatasi ya kuchomea chini ukipenda.
Choma kwenye moto 325˚C kwa muda wa dakika 15 mpaka 18 au mpaka ibadilike kuwa rangi ya browni.
Kwenye sufuria ndogo tia syrup siagi na maziwa matamu ya mgando na changanya kwa moto mdogo mpaka uwe mzito kasha mimina juu ya keki uliyochoma na choma tena kwa muda wa dakika 20 mpaka karameli iwe rangi ya dhahabu.
Kwenye sufuria ndogo nyingine tia vipande vya chokoleti na mafuta na ukoroge kwa moto mdogo mpaka iyayuke kisha wacha ipoe kidogo mimina juu ya mjazo wa karameli kisha weka kwenye friji mpaka ishikamane.
Kata vipande weka kwenye sahani tiyari kwa kuliwa

Jinsi ya kuandaa Ndizi Mbichi Za Supu Ya Nyama Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi mbichi – Kisia

Nyama ng’ombe – ½ kilo

Pilipili ya kusaga – 1 kijiko cha chai

Tangawizi ya kusaga – 2 vijiko vya supu

Thomu (garlic/saumu) – 1 kijiko cha supu

Bizari mchuzi – 1 kijiko cha chai

Nazi ya unga (ukipenda kuongezea) – 2 vijiko cha supu

Chumvi – Kiasi

Ndimu – 1 kamua

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka nyama ng’ombe katika sufuria, tia tangawizi, thomu, pilipili mbichi, bizari, chumvi. Roweka kidogo ukipenda kisha ikaushe yenyewe kwa maji yake
Ongezea maji ya kiasi yasizidi mno, kisha funika na chemsha.
Menya ndizi, ukatekate.
Nyama ikikaribia kuiva, weka ndizi uendelee kupika mpaka viive vyote.
Tia nazi ya unga kidogo tu ukipenda. Koleza kwa bizari mchuzi, pilipili, na ndimu
Epua mimina katika chombo cha kupakulia zikiwa tayari.

Shopping Cart
2
    2
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About