Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Mapishi ya Tende Ya Kusonga Ya Lozi Na Cornflakes

VIAMBAUPISHI

Tende zilizotolewa kokwa – 1 Kilo

Cornflakes – 1 ½ kikombe

Lozi Zilokatwa katwa – 1 kikombe

Siagi – ¼ kilo

MANDALIZI

Mimina tende na siagi kwenye sufuria bandika motoni moto mdogo mdogo mpaka zilainike. Kwa muda wa dakika 10.
Isonge kidogo kwa mwiko au kuikoroga ichanganyike vizuri.
Changanya Cornflakes na lozi kwenye tende mpaka zichanganyika vizuri.
Pakaza treya au sinia mafuta au siagi kidogo.
Mimina mchanganyiko wa tende, zitandaze vizuri na ukate vipande saizi unayopenda. Zikiwa tayari kuliwa kwa kahawa.

Jinsi ya kupika Mkate wa sinia

Mahitaji

Unga wa mchele (rice flour 2 vikombe vya chai)
Sukari (sugar 3/4 ya kikombe cha chai)
Hamira (dried yeast 3/4 kijiko cha chakula)
Hiliki (cardamon powder 1/2 kijiko cha chai)
Ute wa yai 1(egg white)
Tui la nazi (coconut milk kikombe 1 na 1/2 cha chai)
Mafuta (vegetable oil)

Matayarisho

Changanya unga wa mchele, hamira, hiliki na tui la nazi pamoja katika bakuli la plastic kisha koroga vizuri. Ufunike na uwache katika sehemu ya joto mpaka uumuke.(ambayo inaweza kuchukua kama dakika 30-45. Ukisha umuka tia sukari na ute wa yai kisha ukoroge vizuri. Baada ya hapo washa oven katika moto wa 200°C kisha chukua chombo cha kuokea na ukipake mafuta na umimine mchanganyiko. Kisha utie katika oven na uoke kwa muda wa dakika 40. Hakikisha unaiva na kuwa rangi yabrown juu na chini. Na hapo mkate utakuwa tayari.

Jinsi ya kupika pizza ya mboga mboga na cheese

MAHITAJI

1 kilo unga wa ngano
240 ml maji ya vugu vugu
2 olive oil kijiko kikubwa cha chakula
2 asali kijiko kidogo cha chai
1 chumvi kijiko kidogo cha chai
1 hamira ya chenga kijiko kidogo cha chai

JINSI YA KUPIKA

Chukua bakuli weka maji ya uvugu vugu, amira ya chenga, asali na chumvi kisha koroga ichanganyike vizuri acha itulie kwa dakika 10.
Kisha chukua olive oil na unga wa ngao mimina kidogo kidogo changanya mpaka ichanganyike safi kabisa kisha anza kukanda kama mchanganyiko wa chapati au maandazi.
Baada ya mchanganyiko wako kua mgumu safi kabisa funika bakuli lako na mfuko wa plastiki au cling film kwa muda wa saa 1 katika joto la chumba na mchanganyiko wako utaumuka baada ya muda huo. kisha ukandamize mchanganyiko huo wa unga na kua flati kama mwanzo.
Kata mafungu matano hadi saba ya ujazo sawa inategemea na ukubwa wa piza unaopenda we mlaji kisha sukuma umbo la duara.
Tengeneza mchuzi mzito wa nyanya kisha weka juu ya kitako cha piza na kuitandaza vizuri kwenye pizza yako kama unavyopaka siagi kwenye mkate. Usisahau kuweka chumvi na sukari kidogo katika mchuzi wa nyanya ili kukata uchachu.
Katakata nyanya, kitunguu, pili pili hoho, na bilinganya na kuziweka juu ya pizza yako kwa mpangilio ukitanguliza biringanya, ikifuatiwa na pili pili hoho, kitunguu maji na nyanya.
Kisha chukua mozarella cheese ikwaruze katika mkato mdogo rahisi kuyeyuka kwa kutumia kwaruzo la karoti linafaa.
kisha chukua mkwaruzo wa mozarella cheese na unyunyizie juu ya hizo mboga.
Weka pizza yako kwenye sahani ya bati au pizza pan ili isaidie kuiva upande wa chini.
Weka pizza yako kwenye oven ambayo imeshawashwa na ina joto 400 – 450 F. Choma kwa dakika 20 hadi 25 iwe kaukau na rangi ya kahawia pia cheese itakua imyeyuka na kusambaa vizuri juu ya pizaa.

NB: Unaweza weka mchanganyiko wa nyama yeyote ile kama salami, nyama ya ngombe, nyama ya kuku au samaki kwa kufata maelekezo sawa sawa na hii piza ya mboga, tofauti yake itakua huweki mboga unaweka nyama.

Mapishi ya Wali Wa Nazi Kwa Mchuzi Wa Samaki Na Rojo La Bilingani Na Viazi/Mbatata

Wali Wa Nazi

Mpunga – 4 vikombe

Tui la nazi – 6 vikombe

Chumvi – Kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele kisha
Bandika tui jikoni likichemka tia mchele na chumvi.
Funika uchemke, tui likikauka wacha moto mdogomdogo hadi wali uive ukiwa tayari. Ikiwa unatumia mkaa unapalia juu yake.

Mchuzi Wa Samaki Nguru

Samaki – 4

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi – 2 viijiko vya supu

Kitunguu maji kilokatwakawa – 2 slice ndogo

Nyanya/tungule – 4

Nyanya kopo – 3 vijiko vya supu

Pilipili mbichi – 2

Kotmiri ilokatwakatwa – 3 msongo (bunches)

Bizari ya mchuzi (simba 2) – I kijiko cha chai

Ndimu – 1 kamua

Mafuta – ¼ kikombe

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Katakata samaki mkaange kwa kumtia viungo.
Weka mafuta katika sufuria, kaanga kitunguu. Vinapogeuka rangi thomu na tangawizi mbichi, nyanya, nyanya kopo, kitunguu na bizari ya mchuzi endelea kukaanga.
Tia maji kiasi na ndimu, pilipili mbichi ilosagwa kisha tia kotmiri.
Mwisho tia nusu ya samaki alokaangwa ukiwa tayari

Bilingani Za Kukaanga Na Viazi

Bilingani – 4 madogodogo

Viazi/mbatata – 3

Nyanya – 3

Majani ya mchuzi/mvuje/curry leaves – kiasi 6-7

Nnyanya kopo – 2 vijiko vya supu

Methi/uwatu ulosagwa – 1 kijiko cha chia

Rai/mustard seeds – 1 kijiko cha supu

Bizari ya manjano/haldi/turmeric – 1 kijiko cha chai

Chumvi – kiasi

Mafuta ya kukaangia – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

1. Weka mafuta ya kukaangia katika karai

2. Katakakata bilingani vipande vipande vya mraba (cubes) kaanga katika mafuta ya moto hadi yageuke rangi. Eupa weka kando.

3. Katakataka viazi/mbatata vipande vidogodogo vya mraba (cubes) Kaanga hadi viive epua weka kando.

4. Ondosha mafuta yote katika karai bakisha kidogo tu kiasi ya vijiko 2 vya supu.

5. Kaanga rai kisha majani ya mchuzi, na methi/uwatu kisha kaanga nyanya.

6. Tia nyanya ya kopo kisha changanya pamoja bilingani na viazi ikiwa tayari.

Mapishi ya Biriyani Ya Kuku

Vipimo

Mrowanishe kuku na viungo hivi kwa muda mdogo tu

Kuku (Mkate kate Vipande) – 4 LB

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi – 2 Vijiko vya supu

Chumvi – kiasi

Pilipili nyekundu ya unga – 1 Kijiko cha supu

Bizari ya manjano (Haldi au Tumeric) – 1 Kijiko cha chai

Bizari ya pilau ya powder (Jeera) – 1 Kijiko cha chai

Gilgilani powder (Dania) – 1 Kijiko cha chai

Ndimu – 1 Kijiko cha supu

Mchele na vitu vya Masala:

Mchele (Basmati mzuri) (rowanisha) – 7 cups

Mafuta ya kupikia – kiasi

Vitunguu Vilivyokatwa – 8

Nyanya iliyokatwa katwa – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) na Tangawizi – 1 Kijiko cha supu

Garam Masala -1 Kijiko cha supu

Hiliki powder – ½ Kijiko cha chai

Tomatoe paste – 1 Kijiko cha supu

Pilipili mbichi zipasue katikati – 4

Chumvi – kiasi

Mtindi – 4 Vijiko vya supu

Kotmiri iliokatwa (Chopped) – ½ Kikombe

Mafuta ya kunyunyuzia katika wali – 3 Vijiko vya supu

Zaafarani au rangi ya biriani – kiasi

Namna Ya Kutaarisha Na Kupika

Weka kuku aliyerowanishwa na viungo vyake katika Foil tray au chombo chocote utakachomwagia wali humo humo na kupikia biriani, kisha mchome (Bake) mpaka awive na awe mkavu kiasi.

Wakati kuku anapikika, kaanga vitunguu katika karai au sufuria mpaka viwe brown na epua nusu yake weka kando.

Punguza mafuta yabakie kiasi tu, ongeza Thomu na tangawizi, na viungo vyote vya hapo juu isipokuwa Mtindi na kotmiri, endelea kukaanga hadi tomatoe zilainike.

Ongeza chumvi, malizia mwisho kwa kutia mtindi, kotmiri na vile vitunguu ulivyoweka kando. Masala yako tayari.

Mwagia masala juu ya kuku uliyekwishmpika changanya vizuri.

Chemsha Mchele uwive nusu, chuja na mwagia juu ya masala.

Nyunyiza mafuta kidogo juu ya mchele na zaafarani au rangi ya biriani.

Bake katika moto wa 350 – 400 kwa muda wa 15 – 20 minutes. Biriyani imekuwa tayari kuliwa.

Mtindi wa kutolea Biriyani:

Mtindi – 1 kikombe

Pilipili mbichi – 1 ndogo

Kitunguu saumu(/galic) thomu – chembe mbili

Nanaa – kiasi

Chumvi – chembe tu

Weka kwenye Blender na uchanganye, kisha mimina katika bakuli

Mapishi ya Ugali, dagaa (wabichi) na matembele

Mahitaji

Dagaa wabichi (Fresh anchovies packet 1)
Unga wa ugali (corn meal flour 1/4 kilo) (unaweza kutumia unga wa choice uipendayo)
Matembele ya kukaushwa (dried sweet potato leaves, handful)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1)
Kitunguu maji (onion 2)
Limao (lemon 1/4)
Pilipili mbuzi nzima bila kukata (scotch bonnet pepper1, do not chop)
Chumvi (salt 1/2 ya kijiko cha chai)
Mafuta (vegetable oil)
Hoho (green pepper 1)
Kitunguu swaum (garlic 5 cloves)
Tangawizi (ginger 1 kijiko cha chai)
Binzari ya curry (Curry powder 1/2 kijiko cha chai)

Matayarisho

Safisha dagaa kwa kutoa vichwa na utumbo kisha waoshe na uwakaushe na kitchen towel na uwaweke pembeni. Baada ya hapo katakata, vitunguu na hoho kisha weka pembeni. Baada ya hapo weka sufuria jikoni na utie mafuta yakisha pata moto tia dagaa na uwakaange mpaka wawe wa brown, kisha tia kitunguu swaum,curry powder na tangawizi, kaanga kidogo kisha malizia kwa kutia vitunguu maji, hoho,pilipili,chumvi na ukamulie limao. Kaanga kwa muda wa dakika 3-4 na hakikisha vitunguu na hoho haviivi sana na hapo dagaa watakuwa tayari.

Baada ya hapo yaoshe na uyaloweka matembele (kama ni makavu) kwa muda wa dakika 15, Kisha yatoe na uyaweke kwenye sufuria pamoja na kitunguu, nyanya, chumvi ,kamulia limao kidogo, pilipili na maji kiasi. acha matembele yachemke kwa muda wa dakika 20 na uhakikishe yameiva kwa kuwa laini. Baada ya hapo yapike mpaka maji yote yakauke na mafuta yatok na hapo matembele yatakuwa tayari.

Ukisha maliza kupika dagaa na matembele andaa chungu cha ugali. Kwanza unatakiwa kuchemsha maji ya moto, kisha koroga pembeni unga kiasi katika maji ya baridi na utie kwenye maji yanayochemka, Fanya kama unatengeneza uji, uji wa ugali ukishachemka tia unga na uanze kuusonga mpaka ugali uive. Ukisha iva pakua na usevu na mboga tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About