Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Jinsi ya kupika vitumbua inavyotakiwa

Mahitaji

Unga wa mchele ( Vikombe 2 vikubwa)
Sukari (Nusu ya kikombe kikubwa)
Hamira ( Nusu ya kijiko cha chai)
Hiliki (Nusu ya kijiko cha chai)
Tui la nazi ( Kikombe kimoja kikubwa)
Unga wa ngano (Vijiko viwili vya chakula)
Mafuta ya kuchomea (Vegetable oil)

Matayarisho

Unachanga unga, sukari, hamira, hiliki, unga wa ngano na tui la nazi pamoja katika bakuli la plastiki. Kisha unaukoroga mpaka mchanganyiko unakuwa kama uji mzito. Kava bakuli lililokuwa na mchanganyiko kisha hifadhi katika sehemu yenye joto kwa muda wa masaa matatu.

Jinsi ya kupika

Weka chuma cha kuchomea vitumbua katika moto wa wastani, kisha weka mafuta kwenye chuma cha kuchomea ( Kijiko kimoja cha chai) mafuta yakisha pata moto tia uji wako (upawa mmoja) katika kila shimo la chuma cha kuchomea. Acha mpaka kitumbua kikauke kisha geuza na tia mafuta. Acha upande wa pili wa kitumbua mpaka uwe rangi ya kahawia na hapo kitumbua kitakuwa kimeiva utakitoa. Rudia hatua hizo kwa vitumbua vyote vilivyobaki.

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Chumvi

VIAMBAUPISHI

Unga – 3 Vikombe vya chai

Siagi – 250 gms

Baking powder – 3 Vijiko vya chai

Mayai – 2

Chumvi – 1 kijiko cha chai

Maziwa – 1/2 Kikombe

Pilipili manga ya unga 1 Kijiko cha chai

MAANDALIZI

Katika bakuli la kusagia (blender) au mashine ya keki, tia siagi, chumvi na mayai, piga mpaka iwe kama malai (cream).
Tia Unga, baking powder, pilipili manga.
Tia maziwa.
Kata usanifu (design) unayotaka na sokota au kunja kwa usanifu unaopenda.
Pika (bake) katika moto wa 350º C – usiviache vikawa rangu ya udongo (brown) sana.

Mapishi ya visheti vitamu

VIAMBAUPISHI

Unga – Vikombe 2

Samli au shortening ya mboga – 2 Vijiko vya supu

Maziwa ¾ Kikombe

Iliki – Kiasi

Mafuta ya kukarangia Kiasi

VIAMBAUPISHI :SHIRA

Sukari – 1 Kikombe

Maji ¾ Kikombe

Vanila ½ Kijiko cha chai

Zafarani (ukipenda) – Kiasi

JINSI YA KUPIKA

Katika kisufuria pasha moto maziwa na wakati huo huo chemsha Samli katika kisufuria kengine.
Tia unga katika bakuli na iliki, kisha mimina samli iliyochemka na huku unachanganya.
Tia maziwa na uwendele kuchanganya vizuri isiwe na madonge, ikiwa maziwa haitoshi ongeza maji kidogo.
Kisha uwache unga ukae mahali pa joto kwa muda wa dakika 10 hivi.
Halafu fanya viduara vidogo vidogo, kisha finyiza kwenye greta yenye vishimo vidogo ili upate umbo lake.
Kisha karanga kwenye mafuta yaliyopata moto hadi vibadilike rangi ya dhahabu, kisha viepue vichuje mafuta.
Chemsha shira, ikiwa tayari mimina visheti na upepete na kuzichanganya zipate shira kote.
Weka kwenye sahani na zitakuwa tayari kwa kuliwa na kahawa.

Mapishi ya Wali, Mchuzi Wa Nazi Wa Samaki Nguru

Mahitaji

Mchele – 3 vikombe

Samaki Nguru (king fish) – 5 vipande

Vitunguu – 2

Nyanya/tungule – 4

Mafuta – 3 vijiko vya supu

Tui la nazi zito – 2 vikombe

Pilipili mbichi – 5-7

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 7-9 chembe

Kotmiri – 1 msongo (bunch)

Bizari ya samaki – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 2-3

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha samaki, kata vipande kiasi weka kando.
Katakata kitunguu na nyanya vipande vidogo vidogo sana (crush) .
Katakata kotmiri weka kando.
Saga pamoja, pilipili mbichi, kitunguu thomu, ndimu na chumvi.
Changanya pamoja na bizari ya samaki kisha paka katika vipande vya samaki acha kidogo vikolee.
Weka mafuta katika sufuria au karai, kaanga vitunguu kidogo tu kisha tia nyanya/tungule endelea kukaanga hadi vilainike na kupondeka.
Tia kikombe kimoja na nusu cha tui la nazi, kisha tia vipande vya samaki na masala yake, acha mchuzi uchemke samaki aive. Ongeza chumvi, ndimu, pilipili ikihitajika.
Ongezea tui lilobakia acha motoni kwa daika chache tu.
Epua mwagia kotmiri mchuzi ukiwa tayari.

Pika wali wa maji/mweupe kama kawaida utolee na mchuzi.

Tofauti kati ya yai la kuku wa kienyeji na la kuku wa kisasa

Kilishe mayai yote ni sawa. Virutubishi vinavyopatikana kwenye yai la kuku wa kienyeji kama protini, vitamini A, madini ya chuma na virutubishi vya aina nyingine, ndivyo hivyo vinavyopatikana pia kwenye yai la kuku wa kisasa.

Tatizo linaweza kutokea pale ambapo wafugaji wa kuku wa kisasa hawafuati taratibu za ufugaji na pengine hawawapi kuku vyakula muhimu wanavyohitaji au wanawapa dawa na vyakula visivyo bora kiafya, hivyo wakati mwingine kiini cha yai la kuku wa kisasa huonekana kupungua rangi ya njano kuliko kiini cha yai la kuku wa kienyeji.

Mtu anashauriwa kula yai bila kujali ni la kuku gani, kwa kutegemea ni yai lipi linapatikana kwa urahisi. Lakini nivizuri kula mayai ambayo yapo salama.

Mapishi ya Ugali na dagaa

Mahitaji

Dagaa (dried anchovies packet 1)
Unga wa ugali (corn meal flour 1/4 kilo) (unaweza kutumia unga wa choice uipendayo)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1/2)
Kitunguu maji (onion 1)
Limao (lemon 1/4)
Pilipili mbuzi nzima bila kukata (scotch bonnet pepper1, do not chop)
Chumvi (salt 1/4 ya kijiko cha chai)
Mafuta (vegetable oil)
Hoho (green pepper)

Matayarisho

Chambua dagaa kwa kutoa vichwa vyao na utumbo, baada ya hapo waloeke katkika maji ya moto kwa muda wa dakika 5 na uaoshe tena katika maji ya baridi na uwakaushe uwaweke pembeni. Ukishamaliza katakata kitunguu na uandae nyanya tayari kwa upishi. Bandika sufuria ya kupikia dagaa jikoni na utie mafuta, yakishapata moto tia vitunguu pamoja na dagaa. Kaanga mpaka dagaa wawe light brown kisha tia nyanya, chumvi na pilipili. Pika nyanya mpaka ziive (ukitaka kujua kama nyanya zimeiva utaona zinatengana na mafuta) Baada ya hapo kamulia limao kidogo sana na tia pilipili hoho na zipike kama dakika mbili. kisha ipua.
Ukisha maliza kupika dagaa andaa chungu cha ugali. Kwanza unatakiwa kuchemsha maji ya moto, kisha koroga pembeni unga kiasi katika maji ya baridi na utie kwenye maji yanayochemka, Fanya kama unatengeneza uji, uji wa ugali ukishachemka tia unga na uanze kuusonga mpaka ugali uive. Ukisha iva pakua na usevu na mboga tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About