Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Jinsi ya kutengeneza biskuti za Matunda Makavu Na Cornflakes

VIAMBAUPISHI

Unga – 4 Vikombe

Sukari – 1 Kikombe

Baking powder 1 kijiko cha chai mfuto

Siagi – 454 gms

Mayai – 2

Matunda makavu (tende, zabibu, lozi) – 1 Kikombe

Vanilla – 2 Vijiko vya chai

Cornflakes – ½ kikombe

JINSI YA KUANDAA

Changanya sukari na siagi katika mashine ya keki (cake mixer) mpaka iwe laini (creamy)
Tia yai moja moja huku unachanganya mpaka iwe laini kama sufi. (fluffy)
Tia unga, baking powder, matunda makavu, changanya na mwiko.
Chota mchanganyiko wa biskuti kwa mkono kama (kiasi cha kijiko kimoja cha supu) fanya duara na uchovye katika cornflakes iliyopondwa kwa mkono (crushed)
Zipange katika treya ya kupikia na zipike (bake) katika moto wa 375°F kwa muda wa kiasi dakika 15 huku unazitazama tazama.

Jinsi ya kupika Biskuti Nyembamba (Wafer Bar) Za Chokoleti Na Njugu

MAHITAJI

Wafer Powder/gram wafer (unga wa biskuti uliosagwa wa tayari) – vikombe 2

Maziwa ya Mgando Matamu ya Kopo – 2 vikombe

Nazi iliyokunwa – ½ Kikombe

Chokoleti vipande vipande – 1 Kikombe

Njugu vipande vipande – ½ Kikombe

Siagi – 227 g

MAPISHI

Yeyusha siagi motoni kisha changanya na unga wa wafer acha kidogo motoni
Mimina katika treya unayochomea itandaze vizuri, kisha mimina maziwa juu yake pamoja na njugu vipande , nazi iliyokunwa na vipande vya chokoleti.
Choma (bake) kwenye oveni kwa moto wa 350ºC kwa dakika 20.
Katakata tayari kwa kuliwa

Jinsi ya kupika Baklawa Za Pistachio Na Lozi

VIAMBAUPISHI

Philo (thin pastry) manda nyembamba – 1 paketi

Siagi – ¼ Kikombe cha chai

Baking powder – 2 Vijiko vya chai

Pistachio/ lozi – 2 vikombe vya chai

Mafuta – ½ Kikombe

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 2 Vikombe vya chai

Maji – 2 ½ Vikombe vya chai

ndimu – ½ kijiko cha chai

JINSI YA KUANDAA

Tafuta treya iliyokuwa sawa na ukubwa wa hizo manda nyembamba (philo) au zikate hizo manda kwa ukubwa wa treya (mraba au mstatili)
Kisha yeyusha siagi changanya na mafuta.
Kisha panga manda moja pakaza mafuta juu yake kisha weka manda nyingine juu yake kisha pakaza mafuta tena weka manda nyingine juu yake, endelea kufanya hivyo mpaka ziwe kama sita au saba kisha nyunyizia pistachio na lozi halafu panga tena manda na mafuta manda na mafuta tena sita au saba kisha nyunyizia tena pistachio na lozi.
Panga namna hivyo mpaka treya ijae inapofika manda ya mwisho kata vipande vya mraba vidogodogo humo humo kwenye treya kisha nyunyizia mafuta yaliyobaki.
Washa moto wa oven 350°F kwa muda wa dakika 20 au hadi rangi ibadilike kidogo (isikauke sana)
Chemsha syrup yako kama shira ya majimaji lakini isiwe nzito sana ikishakuwa tayari mwisho tia ndimu acha ipoe kidogo kisha miminia juu ya treya yote halafu malizia kunyunyizia pistachio na lozi zilizobaki.
Zikishakuwa tayari zipange kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

ANGALIZO

Ukishatoa treya kwenye oven wacha ipoe kidogo na syrup yako pia wacha ipoe kidogo kabla hujamimina, ukitia ya motomoto zitalainika.
Manda nyembamba za baklawa zinauzwa tiyari madukani kwenye pakiti.

Namna ya kutengeneza Visheti Vya Nazi Na Njugu (Sudani)

VIAMBAUPISHI

Unga – 3 mug za chai

Samli – ½ mug ya chai

Maziwa – 1¼ mug ya chai

Baking powder – 2 vijiko vya chai

VIAMBAUPISHI VYA MJAZO

Njugu zilizomenywa vipande vipande – 2 vikombe cha chai

Sukari – ½ kikombe cha chai

Iliki – 1 kijiko cha chai

Nazi iliyokunwa – 2 vikombe vya chai

VIAMBAUPISHI VYA SHIRA

Sukari – 2 vikombe vya chai

Maji – 1 kikombe cha chai

Ndimu – 1

JINSI YA KUVIANDAA

1-Changanya unga na samli kisha tia baking powder na maziwa. Ukande ulainike kisha

uwache kama dakika 5 uumuke.

2-Kwenye bakuli nyingine changanya njugu, sukari na iliki.

3-Kata madonge madogo dogo sukuma kila donge duara jembamba, kisha tia kijiko cha mchanganyiko wa njugu juu yake ifunikie juu yake na ibane pembeni.

4-Panga kwenye treya isiyoganda (non stick) kisha choma kwenye oven kwa moto wa chini

(bake) 350° C kwa dakika kama 15-20.

5-Chemsha maji na sukari katika sufuria ndogo kisha tia ndimu acha ichemke mpaka inatenate unapoigusa.

6-Kwenye sahani ya chali mimina nazi iliyokunwa.

7-Vibiskuti vikiwa tayari vya motomoto chovea kwenye shira kisha zungushia katika nazi iliyokunwa,

panga kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

JINSI YA KUANDAA VILEJA

MAHITAJI

Unga wa mchele – 500g

Samli – 250g

Sukari – 250g

Hiliki iliyosagwa – 1/2 kijiko cha chai

Arki (rose flavour) – 1/2 kijiko cha chai

Baking powder – 1 kijiko cha chai

Mayai – 4

Maji ya baridi – 1/2 kikombe cha chai

MAANDALIZI

Saga sukari iwe laini kiasi, changanya unga wa mchele, baking powder, hiliki na sukari.
Pasha moto samli mpaka iwe nyepesi kama maji mimina kwenye ule mchanganyiko wa unga wa mchele, kisha uchanganye pamoja na arki.
Ongeza mayai yaliopigwa endelea kuchanganya mpaka unga umeanza kuchanganyika vizuri.
Ongeza maji ya baridi sana kama nusu kikombe tu ili uchanganyike vizuri.
Kata kwa design unayotaka viwe vinene visiwe kama cookies za kawaida kama ilivyo kwenye picha na ukipenda utaweka kidoto kwa kutumia zaafarani katikati ya kileja kama inavyoonesha hapo juu.
Choma kwa moto wa baina ya 300F na 350F kwa dakika 15 mpaka 20 visiwe vyekundu toa na tayari kwa kuliwa.

Shopping Cart