Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Jinsi ya kupika Biryani ya mbogamboga

Biriani ni miongoni mwa vyakula ambavyo ni nadra sana kupikwa katika familia nyingi tofauti na vyakula vingine. Inawezekana ni kutokana na watu wengi kutoelewa namna ya kuoika chakula hiki kutokana na kuhitaji viungo vingi ambavyo huwapa usumbufu wapishi.
Kuna aina mbalimbali za upishi wa biriani ambapo mara nyingi hutofautiana kutokana na viungo vinavyotumika katika upishi.
Biriani la mbogamboga ni miongoni mwa aina hizo za upishi. Chakula hiki kinaweza kuliwa na kila mtu hususan wale wasiotumia nyama wala samaki.

Mahitaji:

½ kg mchele wa basmati
Kitunguu maji kikubwa 1
Nyanya 1 kubwa
Karoti 1 kubwa
Njegere robo kikombe
Kiazi ulaya 1 kikubwa
Tangawizi za kusaga kijiko 1
Kitunguu swaumu cha kusaga kijiko 1
Karafuu kijiko 1
Majani ya kotimili fungu 1
Maziwa ya mtingi ¼ kikombe
Chumvi na pilipili kiasi
Unga wa dhani kijiko 1 cha mezani
Juisi ya limao kijiko 1 cha mezani
Mafua ¼ lita

Maandalizi:

Chemsha mchele na kisha weka pembeni
Osha mbogamboga zote isipokuwa vitunguu na nyanya
Changanya mtindi na tangawizi pamoja na kitunguu swaumu viache vikae kwa muda wa saa moja
Chukua sufuria weka mafuta na kisha kaanga vitunguu maji, weka nyanya, chumvi, kotimili na limao halafu weka karafuu na kanga hadi vichanganyike vizuri
Miminia mchanganyiko wa mtindi na baadaye weka pilipili na baadaye weka unga wa dhania
Chukua mchele uliochemshwa changanya na mchanganyiko huo
Palia moto juu ya chakula chako na acha kwa muda wa dakika 30
Baada ya hapo chakula chako cha biriani kitakuwa tayari kwa kuliwa

Mapishi ya wali Wa Nazi Kwa Mchuzi Wa Nyama Ng’ombe Na Mchicha

Wali Wa Mpunga

Mchele wa mpunga – 4 Vikombe

Tui la nazi – 6 vikombe

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mchele kisha

Bandika tui jikoni likichemka tia mchele na chumvi.

Funika uchemke, tui likikauka wacha moto mdogomdogo hadi wali uive ukiwa tayari. Ikiwa unatumia mkaa unapalia juu yake.

Mchuzi wa nyama Ng’ombe

Nyama – 1 kilo

Kitunguu saumu(thomu/galic) na tangawizi ilosagwa -2 viijiko vya supu

Viazi/mbatata – 2

Kitunguu maji kilokatwakawa (slice ndogo) – 2

Nyanya/tungule – 4

Nyanya kopo – 3 vijiko vya supu

Majani ya mchuzi/mvu – 3 msongo (bunches)

Bizari ya mchuzi (simba 2) – I kijiko cha chai

Ndimu – 1 kamua

Mafuta – ¼ kikombe

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Weka nyama katika sufuri, tia kijiko kimoja cha kitunguu thomu na tangawizi, chumvi, ndimu na chemsha nyama hadi iwive na ibakie supu yake kidogo.
Weka mafuta katika sufuri nyingine, kaanga kitunguu. Vinapogeuka rangi tia majani ya mchuzi endelea kukaanga hadi vigeuke rangi ya hudhurungi (golden brown)
Tia nyanya/tungule, viazi/mbatata, endelea kukaanga mpaka nyanya ziive.
Tia nyama na supu yake kisha tia nyanya ya kopo, kotmiri, bizari ya mchuzi, chumvi uache mchuzi kidogo katika moto hadi viazi viive vikiwa tayari.

Mboga Mchicha

Mchicha – 4 michano/vifungu

Kitunguu – 1

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 3

Nyanya/tungule – 2

Tui la nazi zito – 1 kikombe cha chai

Chumvi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Osha mboga iache ichuje maji.
Ikatekate kisha weka katika sufuria.
Katika kitunguu maji, kitunguu thomu kisage au kikatekate kidogodogo (chopped), nyanya.
Weka jikoni ipikike kwa maji yake na mvuke.
Tia tui endelea kuweka katika moto mdogomdogo hadi ikaribie kukauka ikiwa tayari.

Mapishi ya Ndizi Za Supu Ya Nyama Ya Ng’ombe

Mahitaji

Ndizi – 15 takriiban

Nayma ya ng’ombe – 1 kilo

Kitunguu maji – 1

Nyanya – 3

Kitunguu saumu(thomu/galic) kilosagwa – 1 kijiko cha supu

Tangawizi mbichi ilosagwa – 1 kijiko cha supu

Pilipili mbichi ilopondwa – 2

Jira/cummin/bizari ya pilau ilosagwa – 1 kijiko cha chai

Ndimu – 1

Chumvi – kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Chemsha nyama kwa ndimu, chumvi na tangawizi mbichi na kitunguu thomu.
Menya ndizi na zikatekate vipande kiasi, weka katika sufuria.
Katakata kitunguu na nyanya utie katika ndizi.
Tia jira na chumvi.
Nyama ikiwiva mimina pamoja na supu yake ufunike ndizi ziwive na kuwa tayari kuliwa.
Ukipenda tia pilipili mbuzi zichemke pamoja na ndizi.

Jinsi ya kupika vizuri Wali Wa Karoti Na Nyama

MAHITAJI YA WALI

Mchele – 3 Magi

Mafuta – 1/4 kikombe

Karoti unakata refu refu – 3

Vitunguu maji kata vikubwa vikubwa – 1 kikubwa

Pilipli manga – 1/2 kijicho chai

Hiliki – 1/2 kijiko chai

Karafuu ya unga – 1/4 kijiko cha chai

Mdalasini wa unga – 1/2 kijiko cha chai

Zaafarani (ukipenda) roweka katika maji – 1 kijiko cha chai

Zabibu kavu (ukipenda) – 1/4 kikombe

Chumvi kiasi

KUPIKA WALI

Kwenye sufuria tia mafuta na kaanga karoti kidogo.
Tia vitunguu kisha tia bizari zote.
Tia maji kiasi (kutegemea aina ya mchele) na chumvi
Tia mchele upike uwive.
Karibu na kuwvia tia zabibu ukipenda.
Funika endelea kuupika hadi uwive.

MAHITAJI KWA NYAMA

Nyama – 2 Ratili (LB)

Chumvi – Kiasi

Mafuta – 1/4 kikombe

Kitunguu (kata virefu virefu) – 1 Kikubwa

Pilipili mboga kubwa – 2 ukipenda moja nyekundu moja kijani unazikata vipande virefu virefu.

Figili mwitu (celery) kata vipande virefu virefu- Miche miwili.

KUPIKA NYAMA

Chemsha nyama hadi iwive
Ikaange kwa mafuta hadi iwe nyekundu
Weka vitunguu, pilipili mboga na figili mwitu
Kaanga kidogo tu kama dakika moja.
Tayari kuliwa na wali.

Jinsi ya kupika Wali Wa Kichina wa mboga mboga Na Mayai

Viambaupishi

  1. Mchele (Basmati) – 3 vikombe
  2. Mbogamboga za barafu (karot, njegere, spring beans na mahindi) – 1 kikombe
  3. Kuku Kidari – 1 LB (ratili)
  4. Mayai – 2 mayai
  5. Vitunguu (vikubwa) – 2 au 3 vidogo
  6. Pili pili manga – 1 kijiko cha chai
  7. Paprika – 1 kijiko cha chai
  8. Chumvi – Kiasi
  9. Mafuta – 1/3 kikombe cha chai
  10. Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha supu
  11. Tangawizi – 1 kijiko cha chai
  12. Kidonge cha supu – 1
  13. Soy sauce – 2 vijiko vya supu

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika Kuku

Kata kidari cha kuku vipande vidogo vidogo vya kiasi.

Tia mafuta kidogo katika wok (karai ya kichina)

Kisha mtie kuku, thomu, tangawizi, soy sauce, pilipilimanga, paprika chumvi.

Tia mboga za barafu, kidonge cha supu, kaanga kuku na mboga viwive yitu vyote na mchanganyiko ukauke.

Namna Ya Kutayarisha Na kupika Wali

Roweka mchele wa basmati kwa muda wa saa au zaidi.

Halafu chemsha mchele pamoja na chumvi

Wacha uchemke asilimia 70%

Chuja maji na weka kando

Katika sufuria, tia mafuta kidogo tu

Kisha tia mayai mawili ukaange haraka haraka (crumbled egg)

Changanya mchanganyiko wa kuku na mboga

Kisha tia wali changanye vizuri

Rudisha katika moto, funika upikike kidogo hadi uive

Kisha pakua katika sahani na tolea na mayai ya kuchemsha ukipenda.

MAANA YA MANENO YANAYOTUMIKA KATIKA MASUALA YA LISHE

1. Chakula

ni kitu chochote kinacholiwa au kunywewa na kuupatia mwili virutubishi mbalimbali Chakula huupatia mwili nguvu, kuulinda na kuukinga dhidi ya maradhi mbalimbali .Mfano wa chakula ni ugali, wali, maharagwe, ndizi, viazi, mchicha, nyama, samaki.

2. Lishe

ni mchakato unaohusisha hatua mbalimbali za jinsi mwili unavyokitumia chakula kilicholiwa, hatua hizi ni kuanzia chakula kinapoliwa, jinsi mwili unavyokisaga na kukiyeyusha, umetaboli, na hatimaye virutubishi kufyonzwa na kutumika mwilini.

3. Virutubishi

ni viini vilivyoko kwenye chakula ambavyo vinauwezesha mwili kufanya kazi zake, karibu vyakula vyote huwa na kirutubishi zaidi ya kimoja ila hutofautiana kwa kasi na ubora. Kila kirutubishi kina kazi yake mwilini na mara nyingi hutegemeana ili viweze kufanya kazi yake kwa ufanisi. Hakuna chakula kimoja chenye virutubishi vya aina zote isipokuwa maziwa ya mama kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto, ni mhimu kula vyakula vya aina mbalimbali ili kuwezesha mwili kupata virutubishi mchanganyiko vinavyohitajika.

4. Mlo kamili

ni ule ambao hutokana na chakula mchanganyiko kutoka katika makundi yote ya chakula na una virutubishi vyote muhimu kwa ajili ya lishe na afya bora. Mlo huu unapoliwa kwa kiasi cha kutosha kulingana na mahitaji ya mwili angalau mara tatu kwa siku huupatia mwili virutubisho vyote muhimu.

5. Ulaji unaofaa

hutokana na kula chakula mchanganyiko na cha kutosha (mlo kamili) ili kukidhi mahitaji ya mwili. Ulaji unaofaa pia huzingatia matumizi ya kiasi kidogo cha chumvi, mafuta, sukari, ulaji wa nyama nyekundu kwa kiasi kidogo. Ni muhimu kuzingatia ulaji wa mboga mboga, matunda, na vyakula vya jamii ya kunde kwa wingi ili kudumisha uzito wa mwili unaotakiwa na kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

6. Nishati- lishe

ni nguvu inayopatikana baada ya virutubishi (kabohaidreti, mafuta) kuvunjwa vunjwa mwilini. Mwili huitumia nguvu hiyo kufanya kazi mbalimbali Kama kulima, kutembea, kupumua, kuziweka seli za mwili katika hali inayotakiwa n.k.

7. Kalori au kilo kalori

ni kipimo kinachotumika kupima nishati -lishe

8. Makapi mlo

ni sehemu ya chakula ambayo mwili hauwezi kuyeyusha lakini ni muhimu katika uyeyushwaji wa chakula. Mfano wa vyakula venye makapi mlo kwa wingi ni mboga za majani, matunda( maembe, machungwa, mapera, machenza, mafenesi, unga usiokobolewa( dona) na vyakula vya jamii ya kunde.

9. Lehemu

ni aina ya mafuta yanayopatikana hasa kwenye vyakula vya asili ya wanyama na pia hutengenezwa mwilini. Lehemu inayotokana na vyakula ikizidi mwilini huleta madhara ya kiafya. Vyakula venye lehemu kwa kiasi kikubwa ni pamoja na maini, figo, mayai, nyama iliyonona kama nundu, nyama ya nguruwe yenye mafuta, mkia wa kondoo, samli, siagi, ngozi ya kuku n.k.

10. Utapiamlo

ni hali ya kupungua au kuzidi kwa baadhi ya virutubishi mwilini ambapo husababisha lishe duni au unene uliozidi.

11. Antioxidants

ni viini ambavyo vina uwezo wa kukinga seli za mwili zisiharibiwe na chembe chembe haribifu (free radicals) ambazo huweza kusababisha saratani. Viini hivyo huungana na chembechembe hizo haribifu na kuzidhibiti ili zisisababishe madhara. Mifano ya antioxidants ni pamoja na beta-carotene, lycopene, vitamin C, E, na A.

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About