Upishi na Maandalizi ya Milo yenye Afya

Jinsi ya kutengeneza Biskuti Za Ufuta Na Jam

VIAMBAUPISHI

Unga vikombe 2

Sukari ya kusaga 1/4 Kikombe

Siagi 250 gms

Jam kisia

Ufuta kisia

Vanilla 1 kijiko cha chai

MAPISHI

Tia kwenye mashine ya kusaga (blender) au mashine ya keki, siagi, yai, sukari na vanilla uchanganye hadi ichanganyike vizuri.
Tia baking powder, na unga na changanya kwa mkono vizuri.
Paka siagi sinia ya kupikia ya oveni.
Tengeneza viduara vidogo vidogo.
Bonyeza kila kiduara katikati kwa kidole, kisha weka jam, halafu juu yake paka mayai na unynyuzie ufuta.
Pika katika moto wa chini 350ºF kwa muda wa dakika 20-25.
Tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika Magimbi Kwa Nyama Ya Ng’ombe

Vipimo

Majimbi (Eddoes) kiasi 6 au 7

Nyama ng’ombe ½ kilos

Tangawizi ilosagwa 1 kijiko cha kulia

Haldi (bizari manjano/turmeric) ½ kijiko cha chai

Tui zito la nazi vikombe 2

Chumvi kiasi

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

Safisha nyama kisha weka chumvi, bizari ya manjano, tangawizi mbichi, ukaushe kwanza katika sufuria kwa kukaanga kaanga.
Ikianza kukauka, weka maji funika uchemshe iwive.
Menya majimbi ukate kate na uweke katika sufuria nyengine.
Mimina supu na nyama katika majimbi uchemshe yawive majimbi.
Mwisho weka tui zito la nazi uchanganye vizuri kisha weka katika moto kidogo tu bila kufunika yakiwa tayari.

Mapishi ya Wali Wa Mboga Na Mchuzi Wa Kuku wa Tanduri

Vipimo vya Wali:

Mchele basmati – 3 magi (kikombe kikubwa)

Mchanganyiko wa mboga za barafu

(Frozen vegetables) – 1 ½ mug

Chumvi – kiasi

Mafuta – 3 vijiko vya chakula

Kitungu maji (kilichokatwa) – 1

Bizari ya pilau (nzima) – 1 kijiko cha chakula

Namna Ya kutayarisha na kupika:

Osha mchele uroweke kwenye maji muda wa dakika 20.
Chemsha maji kwenye sufuria kama magi 6.
Tia chumvi.
Yakisha kuchemka unatia mchele, chemsha usiive sana, uive nusu kiini. Mwaga maji na kuchuja wali.
Unamimina Yale mafuta kwenye sufuria unakaanga bizari ya pilau kidogo na kitunguu kabla ya kugeuka rangi ya hudhurungi (brown).
Tia mchanganyiko wa mboga za barafu.,
Mimina wali, changanya vizuri, ufunike na uweke katika moto mdogo kwa dakika 20.
Pakua tayari kwa kuliwa.

Vipimo Vya Mchuzi

Kuku – 2 Ratili (LB)

Chumvi – Kiasi

Mafuta – ¼ Kikombe

Nyanya Kata vipande – 4

Nyanya kopo – 2 vijiko wa chakula

Tangawizi – 1 kijiko ya chakula

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko ya chakula

Tanduri masala – 1 kijiko cha chakula

Kotmiri liliyokatwa – 3 vijiko vya chakula

Pilipili mbichi – 2

Pili masala – 1 kijiko cha chakula

Garam masala – ½ kijiko cha chakula

Bizari manjano – ½ kijiko cha chakula

Mtindi – 3 vijiko vya chakula

Pilipili boga (kata vipande virefu) – 1

Ndimu – 2 vijiko vya chakula

Namna ya kutayarisha na kupika:

Kwenye bakuli tia kuku na changanya vitu vyote pamoja isipokua mafuta.
Tia mafuta kwenye sufuria yakisha kupata moto mimina kuku umpike kwa muda ½ saa kwa moto kiasi.
Pakua kuku kwenye bakuli au sahani na ukate vitunguu maji duara na umpambie. Tayari kwa kuliwa.

JINSI YA KUANDAA VILEJA

MAHITAJI

Unga wa mchele – 500g

Samli – 250g

Sukari – 250g

Hiliki iliyosagwa – 1/2 kijiko cha chai

Arki (rose flavour) – 1/2 kijiko cha chai

Baking powder – 1 kijiko cha chai

Mayai – 4

Maji ya baridi – 1/2 kikombe cha chai

MAANDALIZI

Saga sukari iwe laini kiasi, changanya unga wa mchele, baking powder, hiliki na sukari.
Pasha moto samli mpaka iwe nyepesi kama maji mimina kwenye ule mchanganyiko wa unga wa mchele, kisha uchanganye pamoja na arki.
Ongeza mayai yaliopigwa endelea kuchanganya mpaka unga umeanza kuchanganyika vizuri.
Ongeza maji ya baridi sana kama nusu kikombe tu ili uchanganyike vizuri.
Kata kwa design unayotaka viwe vinene visiwe kama cookies za kawaida kama ilivyo kwenye picha na ukipenda utaweka kidoto kwa kutumia zaafarani katikati ya kileja kama inavyoonesha hapo juu.
Choma kwa moto wa baina ya 300F na 350F kwa dakika 15 mpaka 20 visiwe vyekundu toa na tayari kwa kuliwa.

Mapishi ya Sambusa za nyama

Mahitaji

Nyama ya kusaga (minced beef 1/4 kilo)
Vitunguu maji vilivyokatwakatwa(diced onion 2 vikubwa )
Kitunguu swaum/ tangawizi (garlic and ginger paste 1 kijiko cha chakula)
Chumvi (salt)
Pilipili iliyokatwakatwa (scotch bonnet 1)
Limao (lemon 1/2)
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Cinnamon powder 1/4 kijiko cha chai
Coriander powder 1/4 kijiko cha chai
Cumin powder 1/4 kijiko cha chai
Unga wa ngano (all purpose flour kidogo)
Manda za kufungia (spring roll pastry)
Giligilani (fresh coriander kiasi)
Mafuta ya kukaangia

Matayarisho

Changanya nyama na limao, chumvi, pilipili,kitunguu swaum, tangawizi na spice zote, kisha pika katika moto wa kawaida mpaka nyama iive na maji yote yakauke. Baada ya hapo kabla hujaipua nyama tia vitunguu na giligilani na uvipike pamoja kwa muda wa dakika 2 na uipue weka pembeni na uache viipoe. Baada ya hapo tia unga kidogo katika bakuli nauchanganye na maji kidogo kupata uji mzito kwa ajili ya kugundishia manda. Baada ya hapo tia nyama katika manda na kisha zifunge kwa kugundishia na unga wa ngano.Ukisha maliza kuzifunga zote zikaange mpaka ziwe za brown na uzitoe. Na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa.

Jinsi ya kupika Slesi Za Chokoleti Na Karameli

Viamba upishi

Unga 1 Magi (vikombe vya chai)

Sukari ya browni ½ Magi

Siagi iliyoyayushwa 125 g

Nazi iliyokunwa ½ Magi

Mjazo wa karameli (Caramel filling)

Syrup 1/3 kikombe cha chai

Siagi iliyoyayushwa 125 g

Maziwa matamu ya mgando 2 vikopo (condensed milk)

Mjazo wa chokoleti (Chocolate filling)

Chokoleti 185 g (dark chocolate)

Mafuta 3 Vijiko vya chai

Jinsi ya kuandaa na kupika

1. Changanya unga, sukari, siagi na nazi iliyokunwa kwenye bakuli mpaka unga ushikamane.

2. Paka mafuta treya ya kuchomea kisha utandaze kwenye treya ya 20cm kwa 30 cm au (8 in kwa 12 in) unaweza kuweka karatasi ya kuchomea chini ukipenda.

3. Choma kwenye moto 325˚C kwa muda wa dakika 15 mpaka 18 au mpaka ibadilike kuwa rangi ya browni.

4. Kwenye sufuria ndogo tia syrup siagi na maziwa matamu ya mgando na changanya kwa moto mdogo mpaka uwe mzito kasha mimina juu ya keki uliyochoma na choma tena kwa muda wa dakika 20 mpaka karameli iwe rangi ya dhahabu.

5. Kwenye sufuria ndogo nyingine tia vipande vya chokoleti na mafuta na ukoroge kwa moto mdogo mpaka iyayuke kisha wacha ipoe kidogo mimina juu ya mjazo wa karameli kisha weka kwenye friji mpaka ishikamane.

6. Kata vipande weka kwenye sahani tiyari kwa kuliwa

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About