SALAMU MARIA
Salamu Maria
Umejaa neema
Bwana yu nawe
Umebarikiwa kuliko wanawake wote
Na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa
Maria Mtakatifu
Mama wa Mungu
Utuombee sisi wakosefu
Sasa, na saa ya kufa kwetu.
Amina.
Salamu Maria
Umejaa neema
Bwana yu nawe
Umebarikiwa kuliko wanawake wote
Na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa
Maria Mtakatifu
Mama wa Mungu
Utuombee sisi wakosefu
Sasa, na saa ya kufa kwetu.
Amina.
Mungu wangu,
nakupenda zaidi ya cho chote,
kwani ndiwe mwema,
ndiwe mwenye kupendeza.
Nampenda na jirani yangu kama nafsi yangu,
kwa ajili yako.
Amina
Ee Mt. Yosefu, tunakuomba kwa ajili ya wale asio na ajira, kwa ajili ya wale wanaotaka kujipatia kipato chao na kulisha familia zao.
Wewe u Msimamizi wa wafanyakazi, tujalie kwamba pasiwepo kati yetu mtu asiye na ajira, na kwamba wale wote ambao wako tayari kufanya kazi waweze kuelekeza nguvu zao na uwezo wao katika kuwatumikia wanadamu wenzao na kujipatia kipato halali.
Wewe u Msimamizi wa familia, usiwaache wale wenye watoto wa kuwatunza na kuwalea wakose namna ya kufanya hivyo. Uwahurumie ndugu zetu waliokosa ajira na kugubikwa na umasikini kwa sababu ya magonjwa au mipango mibaya ya kijamii. Wasaidie viongozi wetu wa kisiasa na walioshika usukani katika nyanja mbalimbali za kiuzalishaji wavumbue suluhu mpya na za haki za jambo hili. Utujalie ili kila mmoja wetu apate kujipatia kipato halali na kufurahia fursa ya kushiriki kadri ya uwezo wake, katika maisha bora zaidi kwa wote. Utujalie ili wote tushiriki pamoja katika raslimali alizotujalia Mungu, na pia utujalie tuwe tayari daima kuwasaidia wale walio wahitaji kuliko sisi.
Amina.
(Sala hii inafaa sana kwa ajili ya kutetea uhai wa watoto wachanga wakiwa tumboni mwa mama zao, dhidi ya utoaji mimba au hatari nyingine dhidi ya uhai wa binadamu)
Ee Mt. Yosefu, wewe ni Mchumba safi na Mpenzi wa Bikira Maria, u Baba Mlishi wa Yesu, mlinzi na mtunzaji wa Familia Takatifu, na wa familia zote. Tuna imani kabisa katika uangalizi wako uliojaa upendo, juu ya uhai mpya, na uaminifu wako kwa familia.
Tunaweka jitihada zetu chini ya ulinzi wa sala zako. Utusaidie daima katika kutetea zawadi ya uhai wa binadamu, ili ukue hadi uzima wa milele ulioahidiwa na kujaliwa kwetu na Mwanao, Ndugu yetu, Yesu Kristu.
Amina.
Ee uliye Mkuu, Mt. Yosefu, uliyatii kabisa maongozi ya Roho Mt. Unijalie neema ya kufahamu aina ya maisha ambayo Mungu anapenda mimi niishi. Usiniache nidanganyike katika jambo muhimu kama hili, ambalo furaha yangu hapa duniani inalitegemea, na hata pia wokovu wa roho yangu.
Unijalie, nikiangazwa na matakwa matakatifu na nikiwa mwaminifu katika kuyatimiza, nikumbatie aina ya maisha ambayo Mungu ameniandalia na yatakayoniongoza kwenye furaha ya milele.
Amina.
Enyi Yesu na Maria na Yosefu,
nawatolea Moyo, na roho, na uzima wangu.
Enyi Yesu na Maria na Yosefu,
mnipokee saa ya kufa kwangu.
Enyi Yesu na Maria na Yosefu,
mnijalie nife mikoni mwenu.
Baba yetu uliye mbinguni
Jina lako litukuzwe
Ufalme wako ufike
Utakalo lifanyike
Duniani kama mbinguni
Utupe leo mkate wetu wa kila siku
Utusamehe makosa yetu
Kama tunavyowasamehe
Na sisi waliotukosea
Usitutie katika kishawishi
Lakini utuopoe maovuni.
Amina.
Novena ya Noeli (maarufu kama novena ya Mt. Andrea)
Husaliwa kuanzia tar 30 Nov hadi usiku wa Noeli, tar 24 Disemba. Inajulikana kama novena ya Mt. Andrea kwa sababu novena hii huanza kusaliwa katika siku ya kumbukumbu ya Mt. Andrea Mtume.
“IHESHIMIWE, NA IBARIKIWE, SAA ILE NA WAKATI ULE, AMBAO MWANA WA MUNGU, ALIZALIWA NA BIKIRA MBARIKIWA SANA, USIKU WA MANANE, KULE BETHLEHEM, WAKATI WA BARIDI KALI.
WAKATI HUO, UPENDE E MUNGU WANGU, KUSIKIA MAOMBI YANGU, NA KUNIJALIA YALE NINAYOYAOMBA KWAKO, KWA NJIA YA MASTAHILI YA MWOKOZI WETU YESU KRISTO, NA YA MAMA YAKE MBARIKIWA. AMINA. (Sali mara 15 kwa siku).
Inasadikika kuwa chochote uombacho kwa imani kwa sala hii utakipata mradi kipatane na mapenzi ya Mungu. Sali na watoto/ familia kuwatafakarisha na kuwaongezea matazamio juu ya sikukuu ya Noeli.
Isambaze sala hii kwa wengine.
Ufuatao ni mtiririko wa Novena ya Roho Mtakatifu kwa siku zote tisa.
Kusali novena hii unaanza nia wimbo/nyimbo kisha unasali sala ya kila siku na kumalizia na litania na Atukuzwe Baba….x3 kwa siku zote tisa.
/Njoo wangu Mfariji
Yako shusha mapaji
Roho Mungu njoo/
1. Hekima nishushie, Mungu nimfuatie, Roho Mungu njoo
2. Akili nijalie, imani nizidie, Roho Mungu njoo
3. Nieneze shauri, imani nizidie, Roho Mungu njoo
4. Nizidishie nguvu, nsifanye ulegevu, Roho Mungu njoo
5. Elimu nieleze, hakika niongoze, Roho Mungu njoo
6. Ibada niwashie, Peke nikupupie, Roho Mungu njoo
7. Uchaji nitilie, dhambi nizichukie, Roho Mungu njoo.
/Njoo Roho Mtakatifu, shusha mapaji (kweli) niwe imara x2
Leta nuru ya mwanga wako, ifikie moyoni mwangu x2/
1. Roho mwenye hekima, Roho wa shauri na nguvu
2. Nipatie elimu nitambue nafsi yako
3. Nipatie ibada nikusifu daima milele
4. Roho mwenye uchaji washa moto wako wa mapendo
1. Uje Roho Mtakatifu, tuangaze toka mbingu, roho zetu kwa mwangao
2. Uje Baba wa maskini, uje mtoa wa vipaji, uje mwanga wa mioyo
3. Ee Mfariji mwema sana, ee Rafiki Mwanana, ewe raha mustarehe
4. Kwenye kazi u pumziko, kwenye joto burudisho, u mfutaji wa machozi
5. Ewe mwanga wenye heri, uwajaze waumini, neema yako mioyoni
6. Bila nguvu yako Wewe, mwanadamu hana kitu, kwake yote yana kosa
7. Osha machafuko yetu, panyeshee pakavu petu, na kuponya majeraha
8. Ulegeze ukaidi, pasha moto ubaridi, nyosha upotovu wote
9. Wape waamini wako, wenye tumaini kwako, paji zako zote saba
10. Wape tuzo ya fadhila, wape mwisho bila hila, wape heri ya milele.
11. Amina aleluya, amina aleluya, amina aleluya.
1. Njoo Roho Mtakatifu, angalia zetu nyoyo, waletee neema nguvu, wakosefu viumbevyo.
2. Majina yako Mfariji, shina la uzima pendo, wake Mwenyezi upaji, mafuta ya roho moto
3. Ndiwe mnye mapaji saba, wa Mungu kuume mkono, mshika uhadi wa Baba, mtoa kwa ndimi maneno
4. Angalo litung’arie, moyo kwa pendo tushushe, nguvu neema tujalie, wanyonge wasabilitishe
5. Shetani mbali mkimbize, amani utupatie, tukufuate tuongoze, maovu utukingie
6. Baba Mungu tujulishe, pia Mwana tumkubali, Roho tukuungamie, mtokea wao wawili.
Yesu alipokuwa akiagana na mitume wake, kabla ya kupaa mbinguni, aliwaambia wasiondoke Yerusalemu mpaka hapo watakapokuwa wamempokea Roho Mtakatifu. Aliwaambia: “Wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni, mtajazwa nguvu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika nchi yote ya Yuda na Samaria, hata kwenye mipaka yote ya dunia.” (Mdo.1:8)
Waliendelea kusali pamoja toka hapo Yesu alipopaa mbinguni mpaka siku ya Pentekoste. Waliomba Roho Mtakatifu awashukie, awajaze na mapaji yake. Na baada ya siku tisa Roho Mtakatifu aliwashukia hao kundi dogo nao wakawa chanzo cha Kanisa lililopata kuenea duniani kote.
Siku hizo tisa za kusali zinaitwa NOVENA; na kila mwaka wakati huu, wakristu wakifuata mfano wa mitume, wanasali muda wa siku tisa kabla ya Sikukuu ya Pentekoste. Wanamuomba Roho Mtakatifu awashukie, awajaze nguvu na wingi wa mapaji yake.
Wakati huu wa NOVENA , Tunayo mengi ya kuliombea Kanisa na kujiombea sisi wenyewe. Kwa hiyo tumuombe Roho Mtakatifu atusaidie kusali vema na kuomba yale yote tunayohitaji kwa maslahi yetu ya roho na mwili.
Na kama mtume Paulo alivyowaambia wale waKristu wa kwanza, Roho Mtakatifu huja kutufatiji katika udhaifu wetu. Basi tumuombe atufariji kwa sala hizi za NOVENA, Atuwezeshe kusali na kuomba inavyotupasa kusali.
1. Ee Baba wa milele, tunakuomba umtume Roho Mtakatifu atushukie sisi taifa lako awashe ndani yetu moto wa upendo wako.
W. Twakuomba utusikie.
2. Ee Baba mwema, tunakuomba utujalie faraja ya Roho Mtakatifu sisi wana tulio katika dhiki na taabu nyingi mno hapa duniani.
W. Twakuomba utusikie.
3. Ulijalie Kanisa lako mapaji ya Roho wako Mtakatifu, liweze kutekeleza vema utume wake wa kuhudumia watu wote hapa duniani.
W. Twakuomba utusikie.
4. Utujalie sisi kudumu katika NOVENA hii mpaka mwisho kama Maria na mitume walivyodumu pamoja wakisali kabla ya Pentekoste ile ya kwanza.
W. Twakuomba utusikie.
5. Utujalie neema zote zinazohitajika ili tuweze kumshuhudia Kristu popote kwa mwenendo na matendo yetu ya kila siku, tukiongozwa na Roho Mtakatifu.
W. Twakuomba utusikie
6. Uzijalie familia zote za wakristu neema na nguvu za Roho Mtakatifu tupate kuendelea pasipo kuchoka katika sala na katika matendo mema siku zote.
W. Twakuomba utusikie
7. Ewe Roho Mtakatifu, uwajalie vijana wetu moyo wa ujasiri, wapate kulijenga kanisa lako na kueneza utawala wako katika jumuia zetu za Kikristu.
W. Twakuomba utusikie.
Ee Mungu, uliye muumba wa vitu vyote , tunakuomba utusikilize kwa wema sala zetu sisi taifa lako, utuongoze sote tufuate siku zote utaratibu wa mapenzi yako; naye Roho Mtakatifu atutegemeze mpaka mwisho wa novena hii. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu .
W. Amina.
“Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika utawala wa Mungu,” (Yn. 3:5).
Kanisa limepewa na Yesu ujumbe wa kuwaletea watu wote uzima mpya, uzima wa Mungu. Yesu aliwaambia mitume wake: “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Nendeni basi mkawafanye watu wa makabila yote kuwa wafuasi wangu. Wabatizeni kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Wafundisheni kuyashika maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku zote mpaka mwisho wa nyakati (Mt.28: 18-20).
Sisi tuliobatizwa tumepata kuwa viungo vilivyo hai vya Mwili wa Fumbo wa Kristu; kwa Kipaimara tumeimarishwa na kuthibitishwa na Roho Mtakatifu. Tumekuwa taifa teule. Tumeshirikishwa ule ukuhani wa Kristu. Tumepokea ujumbe wa kueneza utawala wa Mungu.
Tunapopokea Sakramenti, na hasa ile Sakmenti ya Ekaristi, tunalisha imani na kuongeza mapendo, ambayo ni msingi wa utume wowote ule. Mapendo yanatuhimiza kueneza utawala wa Mungu na kumpenda Yesu Kristu aliyekuja kuwakomboa wanadamu wote.
Kila aliyebatizwa anao wajibu wa kueneza imani ya Mungu na utawala wake. Kwa hiyo tumuombe Roho Mtakatifu atuwezeshe kutimiza wito huo.
1. Ee Baba wa mbinguni tunakuomba umpeleke Roho Mtakatifu aliangaze kanisa na kuliongoza, liweze kuwafikishia mataifa yote habari njema ya wokovu.
W. Twakuomba utusikie
2. Ee Yesu Mkombozi wetu, umtume Roho Mtakatifu awahimize wakristu wapate kutimiza wajibu wao wa kueneza neno lako popote duniani
W. Twakuomba utusikie
3. Ewe Roho Mtakatifu Mfariji, uamshe katika mioyo ya vijana wengi hamu ya kupenda kulitumikia kanisa lako na kulihudumia taifa lako kwa uaminifu.
W. Twakuomba utusikie
4. Ewe mwanga wa mataifa , uwajalie wanafunzi wasikie sauti yako mioyoni mwao, nawe unapowaita wasikose kuisikia sauti yako, wawe tayari kujitoa kwa ajili ya ndugu zao.
W. Twakuomba utusikie.
5. Uwasaidie wazazi wawalee vema watoto wao; uwatie moyo katika wito wao, wapate pia kuishiriki vema ile kazi ya kueneza neno lako kwa jirani zao.
W. Twakuomba utusikie
6. Ewe Roho Mtakatifu, uwasaidie wakristu wote kueneza habari njema ya wokovu, kwa sala, kwa sadaka na kwa mifano ya maisha yao ya uchaji.
W. Twakuomba utusikie
7. Ewe mpaji wa mema, uwajalie waumini mapaji yako saba, wasichoke kulieneza neno lako kwa hekima pasipo hofu.
W. Twakuomba utusikie.
Ee Mungu, unapenda watu wote waokoke, waifikie kweli yako. Tunakuomba uwapeleke wafanyakazi walio wengi na wema katika shamba lako. Uwajalie kulihubiri neno lako kwa imani kuu ili neno lako lienee na kupokewa na mataifa yote, wapate nao kukujua wewe peke yako Mungu wao, Mungu wa kweli. Tunaomba hayo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayeliongoza kanisa lako sasa na milele.
W. Amina
Bwana alisema kwa kinywa cha nabii Yoeli; “Katika siku zile za mwisho asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu, waume kwa wake, watautangaza ujumbe wangu; vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto….hata watumishi wenu watamiminiwa Roho wangu katika siku zile, nao watautangaza ujumbe wangu. (Mdo.2:17-21)
Siku ile ya Pentekoste, bada ya Roho Mtakatifu kulishukia kanisa, mitume waliwakumbusha watu maneno haya ya nabii Yoeli, na miaka mingi baadae, Petro aliwaandikia barua Wakristu wa kwanza akawaambia; kila mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine, kama vile wakili mwema wa zawadi mbali mbali za Mungu. Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumikia anapaswa kutumikia kwa nguvu aliyojaliwa na Mungu ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristu, ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele (Pet 4;10-11).
Mtaguso wa Pili wa Vatikano ulitukumbusha jambo hilo hilo uliposema; “Roho Mtakatifu anayetakasa taifa la Mungu kwa njia ya Sakramenti amewapa waumini mapaji ya pekee na kumjalia kila mmoja kadiri apendavyo. Kwa hiyo kila mmoja amgawie mwenzake kadiri ya vipawa alivyopewa, awe mgawaji mwaminifu wa neema ya Mungu, alijenge kanisa zima katika upendo.
Tunao wajibu wa kutumia vipawa tulivyojaliwa na Roho Mtakatifu kwa manufaa ya kanisa zima, na kwa faida ya watu wote. Tuunganike sote pamoja na wachungaji wote katika kazi hiyo ya utume. Tumuombe basi Roho Mtakatifu atusaidie kutumia vema vipawa vyake alivyotujalia.
1. Ewe Roho Mtakatifu uwape wakristu neema na nguvu za kutumia vema vipaji ulivyowajalia kwa ajili ya kujenga kanisa lako popote duniani, kwa ajili ya wokovu wa watu wote
W. Twakuomba utusikie
2. Utujalie sisi sote mapaji yako saba, tupate kukutumikia kwa uchaji
W. Twakuomba utusikie
3. Utujalie tuwe mitume wa kweli wa wenzetu, tushirikiane na wachungaji wetu katika huduma za kuwaongoza watu wote na kuwafikisha mbinguni
W. Twakuomba utusikie.
4. Utujalie hekima na nguvu za kuwahudumia watu wote kwa mapendo ya kweli yasiyo na kinyume
W. Twakuomba utusikie
5. Utujalie neema ya kumpenda Mungu kwa moyo wote na kuwapenda jirani zetu kama tunavyojipenda wenyewe
W. Twakuomba utusikie
6. Utupe neema ya kulisikia neno lako na kulifuata, nayo mawazo yetu na matendo yetu yafuate daima mwongozo wako mtakatifu
W. Twakuomba utusikie
7. Uwazidishie mapaji yako wale wote wanaotumia vyema vipawa vyao, uwarudishe na wale wanaotumia vibaya rehema zako
W. Twakuomba utusikie
=== TUOMBE;
Ewe Roho Mungu ndiwe uliyewapa waumini vipawa vyako kwa kadiri unavyotaka. Utujalie tuyapokee na kuyatumia vyema mapaji yako mengi kwa ajili ya utukufu wa Jina lako na kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu.
W. Amina
“Atakapokuja huyu Roho wa kweli , atawaongoza kwenye ukweli wote” (Yn 16:13)
Baada ya kusema hayo, Yesu aliinua macho yake kuelekea mbinguni akasema “Mimi nimekutukuza hapa duniani; nimeikamilisha kazi uliyonipa niifanye. Naomba ili wote wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba Wewe ulinituma (Yn 17:4,21).
Nasi twamuomba Mungu Mwenyezi alijalie kanisa lake umoja wa kweli, awaunganishe wakristu wa madhehebu yote katika zizi moja chini ya mchungaji mmoja.
Popote duniani watu wengi, makundi kwa makundi wanavutwa na neema hiyo ya kuungana na kuufikia umoja wa Kanisa. Hata ndugu zetu waliotengana nasi wanazidi kukubali mwongozo wa Roho Mtakatifu na kutaka kurudi katika nyumba ya Baba na kuwa kundi moja chini ya mchungaji mmoja. Isitoshe, hata sasa tena twaweza kuona kwamba kwa namna fulani wamejiunga nasi katika Roho Mtakatifu, naye Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani yao kumshuhudia hata kwa kumwaga damu yao.
Tena katika hao ndugu zetu waliojitenga, Roho Mtakatifu analisha katika mioyo yao ile ya imani inayowaunganisha wafuasi wote wa Kristu. Tumwombe basi Mwenyezi Mungu atujalie hima huo umoja wa Kanisa lake tunaouania mno.
1. Ee Yesu Bwana wetu wewe umetuombea kwa Mungu Baba tuwe itu kimoja kama Wewe ulivyo kitu kimoja na Baba. Utujalie huo umoja, ili ulimwengu uone na kukiri kwamba ndiwe Bwana na Mkombozi wa watu wote
W. Twakuomba utusikie
2. Ee Yesu utujalie moyo wa kulishika neno lako kwa uaminifu, wala usituache kufuata njia zetu sisi wenyewe na kufarakana.
W. Twakuomba utusikie
3. Ee Yesu uliye Mchungaji wetu mwema, ondoa ndani yetu ile tabia ya utengano, tupate kuwa sote kundi moja chini yako wewe uliye mchungaji wetu mmoja.
W. Twakuomba utusikie
4. Ee Yesu, uliye Mchungaji mkuu, uwajalie wachungaji wetu wawe siku zote na upendo wa Jina lako, wasichoke kulichunga vema kundi lako hapa duniani na kuliweka pamoja lisitengane
W. Twakuombaa utusikie
5. Ewe Roho Mtakatifu, uziangaze akili za watu wote, wapende siku zote kuishi kwa amani, umoja na mapendano
W. Twakuomba utusikie
6. Ee Mungu, utufungulie …… wa muungano wako wa kweli sisi tulio ndugu katika Bwana wetu Yesu Kristu.
W. Twakuomba utusikie
7. Utujalie mapatano na amani, tudumu tumeungana katika familia zetu, katika jimbo letu na katika nchi yetu yote.
W. Twakuomba utusikie.
Ee Mungu, utuunganishe sisi kondoo wako tuliotawanyika, tuwe chini ya Mwanao mpenzi, tupate sote kuushiriki ule utawala wako wa kweli na haki, utawala wa neema na amani, utawala wa upendo wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu
W. Amina
Walio wa Mungu watafuata yaliyo ya Mungu, na walio wa dunia hufuata yaliyo ya dunia,. Ni mauti kutosheka na mambo yaliyo ya dunia. Uzima na faraja ya kweli hupatikana tu katika mambo ya Mungu.
Kwa nguvu zetu sisi wenyewe hatuwezi kutenda lolote jema. Kuweza kwetu kwatoka kwa Mungu, kwatoka kwa Yeye anayetupa kujua, kupenda na kutenda.
Mtu anapotenda dhambi, hawezi kuongoka ila kwa msaada wa Roho Mtakatifu, ndiye anayempa mkosefu neema ya kutambua ubaya wa kosa lakena kuamua kuliacha. Ndiye anayempa pia mkosefu kutambua uzuri wa neema aliyoipoteza na kumrudishia neema hiyo. Ndiye anayempa nguvu za kuidumisha neema hiyo na kuiongeza.
Isitoshe, Roho Mtakatifu ndiye anayemuwezesha mtu kuwa na maendeleo katika fadhila na utakatifu. Ndiye anayemjalia imani iliyo msingi wa maisha ya kiKristu. Ndie anayetujalia akili ya kushika mafumbo ya dini yetu na kuishi imani yetu mpaka kufa.
Lakini imani peke yake haimtoshi mtu aokoke. Imani pasipo matendo haifai kitu; imani bila matendo imekufa (Yak 2:28) Roho Mtakatifu anamuwezesha mtu kumuamini Mungu na kumenda kuliko vitu vyote na kumpenda jirani kama kujipenda mwenyewe. Ndiyo maana Roho Mtakatifu huitwa chanzo cha matendo yetu yote yaliyo mema. Basi, tumuombe Roho Mtakatifu aitakase mioyo yetu sisi waumini wake, atuzidishie imani, atuwezeshe kutenda matendo yaliyojaa imani.
1. Ewe Roho Mtakatifu, utudumishie imani, uyatakase mawazo ya mioyo yetu yafuate daima maongozi yako na amri zako
W. Twakuomba utusikie
2. Uzigeuze nia zetu zipate kumuelekea daima Mungu
W. Twakuomba utusikie
3. Utuwezeshe kuelekea katika utakatifu na kutenda mema kwa imani siku zote za maisha yetu
W. Twakuomba utusikie
4. Utuzidishie imani matumaini na mapendo, tuweze kushika kwa moyo thabiti yale yote tunayofundishwa na kanisa lako takatifu
W. Twakuomba utusikie
5. Uiwashe mioyo yetu na moto wa mapendo yako, tupate kumpenda Mungu kweli na kumpenda jirani yetu pasipo unafiki.
W. Twakuomba utusikie
6. Utusaidie tuishi vema kwa imani na matumaini siku zote za maisha yetu
W. Twakuomba utusikie
7. Utujalie kudumisha mioyoni mwetu ile neema ya utakaso tuliyoipata mwanzo katika ubatizo wetu
W. Twakuomba utusikie
Ee Mungu, mbele yako mioyo yetu i wazi; wewe wayajua yote, wala hakuna siri iliyofichika mbele yako. Uyatakase mawazo ya mioyo yetu kwa kutupelekea Roho Mtakatifu, ili tuweze kukupenda na kukutukuza kama inavyostahili. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu
W. Amina
“Nitamuomba Baba , naye atawapelekea Mfariji mwingine atakaye kaa nanyi siku zote”. Katika maisha yenu hapa duniani tunahitaji mno kitulizo cha Mungu. Ni jambo la hekima kutafuta kitulizo hicho kwa Mungu wala si kwa viumbe; maana kitulizo kinachopatikana kwa viumbe hapa duniani hakidumu; bali kitulizo kitokacho kwa Mungu ni cha kudumu.
Roho Mtakatifu ndio kitulizo chetu cha kweli. Baba ndiye aliyetuumba, Mwana ndiye aliyetukomboa, Roho Mtakatifu ndiye aliyetutakasa mioyo yetu na kutufariji.
Kazi ya Roho Mtakatifu sio tu kuwatuliza wale walio na huzuni, bali pia kuwapa moyo wa kuvumilia taabu zozote kwa saburi.
Tunahitaji nguvu ya Roho Mtakatifu ili tuweze kuishi maisha mema ya kikristu. Katika juhudi zetu za kumtumikia Mungu mara nyingi tunakutana na shida; naye Roho Mtakatifu ndie anayetufariji kwa kutupa nguvu za kupambana na matatizo yote. Maisha yetu hapa duniani yamejaa misalaba. Na misalaba hiyo hatuwezi kuichukua kwa nguvu zetu wenyewe. Roho Mtakatifu ndie anayetupa nguvu za kuvumilia. Basi, tumuombe aje kutufariji na kutupa nguvu za kuchukua msalaba wetu kwa saburi kila siku.
1. Ee Yesu Bwana wetu, tunakusihi Wewe na Baba mumtume Roho Mtakatifu atufariji, awajalie kitulizo wale wote walio katika taabu na majonzi
W. Twakuomba utusikie
2. Ewe Roho Mtakatifu, uwafariji wale walio katika tabu za namna zozote ili waweze kuvumilia kwa saburi mateso yao kwa faida ya Roho zao na roho za ndugu zao.
W. Twakuomba utusikie
3. Uwafariji wale walio wagonjwa, uwajalie afya ya roho na ya mwili
W. Twakuomba utusikie
4. Uwasaidie yatima, wajane na wote walioachwa, wasikose kupata siku kwa siku mahitaji yao ya lazima
W. Twakuomba utusikie
5. Wajalie wale wote walio walegevu na wakosefu neema ya kuongoka na kurejea hima katika amani ya upendo wako
W. Twakuomba utusikie
6. Uwaimarishe wale walio wema, uwajalie neema ya kudumu wasilegee katika kutenda mema leo na kesho na siku zote za maisha yao.
W. Twakuomba utusikie
7. Utujalie nguvu za kutafuta na kudumisha amani ya kweli katika mioyo yetu na kati ya ndugu zetu katika jumuia zetu za kikristu
W. Twakuomba utusikie
Ee Bwana Mungu wetu, tunakuomba neema ya Roho Mtakatifu ituangaze akili na mioyo yetu na kutujaza nguvu ya upendo wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu.
W. Amina
Hekima tunayopewa na Roho Mtakatifu si sawa kama hekima inayopatikana katika ulimwengu huu.
Hekima ya Roho Mtakatifu ni ile Mtk. Paulo aliyowaambia Wakorintho ya kuwa; ni hekima ambayo watawala wa dunia hii hawakuielewa; maana kama wangaliielewa, hawangalimsulubisha Bwana wa utukufu. Lakini, ni kama yasemavyo maandiko; mambo ambayo jicho halijapata kuyaona wala sikio kuyasikia mambo ambayo binadamu hajapata kuyafikiria moyoni, hayo ndiyo Mungu aliyowatayarishia wale wampendao (1Kor 2;8-9).
Mtk. Paulo alisema kama vile roho ya mtu ndiyo yenye kufahamu na kutambua yaliyo ndani yake; hivyo pia Roho Mtakatifu ndiye anayefahamu mambo ya Mungu na kutufumbulia sisi mioyoni mwetu.
Katika Sikukuu hii ya Pentekoste tunatazamia kumpokea Roho Mtakatifu. Yeye aliye hekima ya Mungu atatufumbulia siri za Mungu na ukweli wake. Ndiye atakayeamsha ndani yetu mapendo ya Yesu Msulibiwa , Mkombozi wetu. Ni yeye atakayetuongoza kutenda mema na kuacha mabaya; tunahitaji sana Roho Mtakatifu katika maisha yetu ya kila siku, tupate hekima ya kuchagua na kutenda daima yaliyo mema. Katika novena hii tuzidi kumuomba Mungu atushushie Roho Mtakatifu, atujaze na hekima yake.
1. Ee Mungu, uwabariki viongozi wa dini na wasaidizi wao, wapate kutuongoza kwa hekima na mapendo
W. Twakuomba utusikie
2. Ewe Roho Mtakatifu, utujalie hekima ya kutambua Mambo ya Mungu na kuyatekeleza kwa uchaji
W. Twakuomba utusikie
3. Utujalie kuyajua mapenzi ya Mungu na kuyapokea kwa furaha
W. Twakuomba utusikie
4. Uamshe ndani yetu mapendo ya Yesu msulibiwa , utuwezeshe kutimiza vema wajibu wetu kama wafuasi wa kweli wa Kristu Bwana wetu
W. Twakuomba utusikie
5. Utuwezeshe kuchagua daima yaliyo mema na kuyatekeleza, tupate kulijenga na kulidumisha kanisa lako hapa duniani
W. Twakuomba utusikie
6. Utuepushe na mafundisho yoyote yaliyo na upotovu, utujalie hekima ya kuzidi kutambua ukweli wako na mafundisho yako yaletayo wokovu
W. Twakuomba utusikie
7. Hekima ya Roho Mtakatifu ituongoze katika satfari ya maisha yetu hapa duniani, tupate mwishowe kukurudi Wewe Muumba wetu uliye mwanzo wetu na mwisho wetu
W. Twakuomba utusiki
Ee Mungu, Baba wa utukufu, tunakuomba utupe Roho wako wa hekima, atuwezeshe kukufahamu vema, atuongoze kuishi maisha yenye kukupendeza. Utusaidie kupambana na matatizo ya maisha, tupate kuishi maisha mema hapa duniani na mwisho tupate tunzo la heri na furaha yako huko mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
Roho Mtakatifu anaangaza akili zetu tuweze kuona ukweli wa Mungu na kuufata. Bila Roho Mtakatifu akili zetu zimo katika giza nene, wala hatuwezi kuona njia ya kutuelekeza kwa Mungu.
Mungu alipoumba ulimwengu, dunia ilikuwa giza tupu, haina kitu. Mungu alisema; “Iwe nuru”, ikawa nuru, Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema (Mwa 1;3-4) vivyo hivyo akili ya binadamu bila nuru ya mwanga wa Roho Mtakatifu, ni tupu, ina giza, haiwezi kuona mambo yanayotuelekeza kwa Mungu. Tukiwa na nuru ya Roho Mtakatifu tunaona ukweli wa Mungu jinsi ulivyo.
Roho Mtakatifu anapoijia roho ya mtu, anaiangaza akili yake iweze kuona mambo yanayofaa kwa wokovu. Naye akiisha kuiangaza akili ya mtu huimarisha utashi wake na kumwezesha kuchagua daima yaliyo mema.
Roho Mtakatifu huiangaza akili iweze kuona ukweli. Kabla ya kuwaaga mitume, Yesu aliwaambia kuwa atawapelekea mfariji mwingine atakayekaa nao siku zote. Roho wa kweli ambaye dunia haiwezi kumpokea kwa sababu hawakumfahamu, lakini wao mitume watamfahamu kwa maana atakaa nao siku zote. Yesu ametuahidi pia sisi Roho huyo akae nasi
Leo hivi duniani kuna uwongo na udanganyifu mwingi; kuna dhuluma, vita, na maovu ya kila namna. Hii ni kwa sababu dunia haijamtambua bado Roho Mtakatifu na kumpokea Yeye aliye mwanga wa dunia na asili ya kweli yote.
Mtaguso wa Pili wa Vatikano watambua ya kuwa Roho Mtakatifu anakaa katika kanisa na katika mioyo ya waumini kama katika hekalu. Roho Mtakatifu analiongoza kanisa na kulifanya liwe na umoja; analipamba na mapaji yake mabalimbali.
Tumuombe Mungu Baba ampeleke huyo Roho Mtakatifu katika kanisa lake, aliongoze na kulilinda lisipate kutengana, bali lisaidie kueneza utawala wa Mungu popote duniani.
1. Ewe Roho Mtakatifu, utujalie kuona mwanga wa kweli yako na kuifuata
W. Twakuomba utusikie
2. Uwape waregevu neema ya kuirudia tena njia ya kweli yako
W. Twakuomba utusikie
3. Utuwezeshe sisi sote waamini wako tutembee siku zote katika nuru ya kweli yako na sheria zako
W. Twakuomba utusikie
4. Utuangazie akili ya mioyo yetu tuchague daima yale yanayakupendeza
W. Twakuomba utusikie
5. Uwape mwanga wako viongozi wetu wa dini na serikali, wapate kutuongoza kwa hekima na uchaji, wasisahau kamwe kwamba uwezo walionao unatoka kwa Mungu.
W. Twakuomba utusikie
6. Utupe mwanga wako tuwaone watu wote kama ndugu zetu. Tuishi kindugu na kusaidiana kindugu
W. Twakuomba utusikie
7. Ewe Roho Mtakatifu ndiwe mpatanishi wa mioyo,; tunakuomba uondoe udhalimu, uonevu, udanganyifu na maovu yote katika mioyo ya watu wote.
W. Twakuomba utusikie.
Ee Yesu Bwana wetu, uliyesema “Pasipo Mimi hamuwezi kitu” umpeleke Roho Mtakatifu atuangaze akili zetu, tupate kufahamu mapenzi yako na kuyatimiza kwa imani na uchaji. Roho Mtakatifu atuongoze katika mambo yote, yeye anayeishi na kutawala nawe pamoja na Baba daima na milele.
W. Amina
Maandiko Matakatifu yanatuambia ya kuwa, Roho Mtakatifu, Nafsi ya Tatu ya Utatu Mtakatifu, ndiye Upendo katika Baba na Mwana. Upendo hujieneza. Naye Roho Mtakatifu aliye pendo lenyewe la Mungu, hupenda kujieneza na kujishirikisha nasi, na kuwasha ndani yetu moto wa mapendo yake.
Roho Mtakatifu ndiye mwenye kutakatifuza roho zetu kwa neema ya utakaso. Neema hiyo ni uzima wa Mungu, ndio huo upendo wa Mungu tunaoshirikishwa. Roho isiyo na neema ya utakaso imetengana na Mungu, haina uzima wake, haina upendo wake, kwa hiyo haiwezi pia kuwa na mapendo ya kweli ya jirani.
Ingawa tunaona ishara nyingi za watu kupendana kidugu hapa duniani, mapendo hayo si mapendo ya kweli wala si kamili kama hayatokani na neema ya utakaso rohoni mwa mtu. Kama hakuna neema ya utakaso ndani yetu, Mungu pia hayupo kati yetu.
Roho Mtakatifu anatuunganisha na Mungu katika upendo. Pasipo na mapendo hapana mapatano, hapana masikilizano wala mwungano. Watu wanaopendana wanaungana na kulingana katika fikra zao na nia zao. Roho Mtakatifu anayetutia mapendo rohoni na kutuwashia moto wa mapendo, ndiye anayetuwezesha kuwa na mawazo ya namna moja na nia moja.
Watu wanaopendana hupenda kukaa pamoja, kuishi pamoja na kusaidiana. Roho Mtakatifu aliye chanzo cha mapendo ya kweli hutuweka pamoja katika Kanisa lake. Hukaa ndani yetu, hukaa katika Kanisa na kuwasha moto wa mapendo yake ndani yetu. Roho Mtakatifu anatuwezesha kukaa kwa amani nyumbani, kazini na katika jumuiya zetu. Basi, tumwombe sasa Roho Mtakatifu atuongezee hayo mapendo yake ndani yetu.
1. Ewe Roho Mtakatifu, uwashe mioyoni mwetu moto wa mapendo yako, tupate kuwapenda jirani zetu kama tunavyotaka kupendwa nao.
W. Twakuomba utusikie
2. Udumishe ndani yetu neema hiyo ya mapendo yako, tuwezeshe kuishi kwa amani leo na siku zote za maisha yetu.
W. Twakuomba utusikie
3. Utujalie neema na nguvu za kutekeleza mema yote tunayokusudia kuyatenda siku hii ya leo
W. Twakuomba utusikie
4. Uongoze nia zetu na maazimio yetu, yalingane na juhudi zetu za kutaka kuleta mafanikio ya roho na mwili kati yetu
W. Twakuomba utusikie
5. Utubariki, ili baada ya maombi haya, tuwe na juhudi ya kutimiza vema zaidi wajibu wetu wa kikristu kwa moyo mkuu
W. Twakuomba utusikie
6. Utuwezeshe kueneza mapendo na amani kati yetu na katika jumuiya zetu za kikristu
W. Twakuomba utusikie
7. Utuwezeshe kuwa kweli chachu ya wema na mapendano kati ya watu, ili nao wapate rehema zako kwa maombezi yetu.
W. Twakuomba utusikie.
Ee Mungu, tunakushukuru kwa neema ulizotujalia, hata tukaweza kuifanya ibada hii ya Novena takatifu mpaka mwisho. Utujalie mema yote tuliyoomba; utusaidie kutekeleza yote yale tuliyokusudia kutenda. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu.
W. Amina.
Ee Mungu Baba mwenye huruma tujalie Roho wako alete Mwanga kwetu ili apate kututakasa na kuingiza ndani ya mioyo yetu Baraka za kuweza kutenda yale yaliyo mema.
Tunaomba hayo kupitia kwa Mwanao Mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo, anbaye anaishi na kutawala pamoja nawe katika Umoja wa Roho Mtakatifu. AMINA
Ee Yosef mwenye heri, tunakimbilia kwako, katika masumbuko yetu, na kishaomba shime ya Mchumba wako Mtakatifu, tunaomba pia kwa matumaini usimamizi wako. Kwa ajili ya mapendo uliyompenda nayo Bikira Mtakatifu, Mzazi wa Mungu, na kwa ajili ya tunza ya Baba, uliyomtunza nayo Mtoto Yesu, tunakuomba sana, utuangalie kwa wema, sisi tuliokuwa fungu lake Yesu Kristo, tuliokombolewa kwa damu yake, utusimamie katika masumbuko yetu, kwa enzi na shime yako.
Ee Mlinzi amini wa Jamaa Takatifu, uwakinge watoto wateule wa Yesu Kristo, ee Baba uliyetupenda mno, utuepusha na kilema chochote cha madanganyo na upotevu. Ee kinga yetu mwezaji,utusimamie huko juu mbinguni ulipo, tunaposhindana na wenye nguvu wakaao gizani. Kama vile siku za kale ukamwokoa Mtoto Yesu katika hatari ya kuuawa, na leo hivi, ulikinge Kanisa Takatifu la Mungu katika mitego ya adui, na katika shida yote, mtunze daima kila mmoja wetu, tupate mfano wako, tusaidie kwa msaada wako, kukaa na utakatifu maisha, kufa kifo chema, na kupokelewa mbinguni makao ya raha milele. Amina
Ee Moyo Mtakatifu sana wa Yesu, chemchemi ya kila baraka, ninakuabudu, ninakupenda, na kwa majuto halisi ya dhambi zangu, nakutolea moyo wangu dhaifu. Nifanye mnyenyekevu, mvumilivu na safi, nikikubali na kuyatii kabisa mapenzi yako. Ee Yesu mwema, unijalie niishi nawe na kwa ajili yako. Unilinde niwapo katikati ya hatari, unifariji katika mateso, unipe afya ya mwili na msaada katika mahitaji ya mwili, Baraka yako juu ya kila nilifanyalo, na neema ya kifo chema. Amina.
Ee Yesu uliyesema “Kweli nawaambieni, ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtapata, gongeni nanyi mtafunguliwa”, tazama ninagonga, ninatafuta na kuomba …….. (Taja ombi lako)
Baba Yetu….., Salamu Maria …….., Atukuzwe Baba……..
Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutumainia kwa moyo wote!
Ee Yesu uliyesema “Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu mtapewa”, tazama kwa jina lako ninaomba ……. (Taja ombi lako)
Baba Yetu….., Salamu Maria …….., Atukuzwe Baba……..
Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutumainia kwa moyo wote!
Ee Yesu uliyesema “Kweli nawaambieni, mbingu na dunia zitapita lakini maneno yangu hayatapita kamwe”, tazama, nikitiwa nguvu na maneno yako ya kweli ninaomba …….. (Taja ombi lako)
Baba Yetu….., Salamu Maria …….., Atukuzwe Baba……..
Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutumainia kwa moyo wote!
Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambaye kwako ni kitu kimoja tu kisichowezekana, ambacho ni kutoacha kutowaonea huruma wenye huzuni, utuhurumie sisi wakosefu maskini na utujalie neema tukuombayo kwa njia ya Moyo Imakulata wa Maria, Mama yetu mpole.
Sali ‘Salamu Malkia’ na kuongezea, ‘Mtakatifu Yosefu Baba Mlishi wa Yesu, utuombee’.
P.S. – Sala hii ya Novena ilisaliwa kila siku na PADRE PIO kwa ajili ya kuwaombea wale wote waliomwomba msaada wa sala zake. Unaweza kuisali kwa namna tofauti tofauti. Mfano, kama Novena ya siku tisa, ambapo unasali sala hii mara moja au zaidi kila siku kwa siku tisa, au unaweza kuifanya kama Novena ya masaa, ambapo unasali sala hii kila baada ya saa moja kwa masaa tisa kwa siku hiyo hiyo, hasa kama kitu unachokiomba ni cha haraka au umesongwa moyoni. Vilevile unaweza kuifanya sala hii kama sehemu ya sala zako za kila siku katika mwezi Juni ambao ni mwezi uliotengwa na Kanisa kwa ajili ya kuuheshimu Moyo Mtakatifu wa Yesu, na hapo utaitumia kuwaombea watu waliokuomba msaada wa sala zako kama alivyofanya Mtakatifu Padre Pio. Pia unaweza kuitumia kama sala yako ya siku zote au ya mara kwa mara kwa ajili ya mahitaji mbalimbali.
Ewe Mtakatifu Yuda Tadei,/ mtume mtukufu na shahidi wa Kristo,/ umesifika pote kwa wepesi wako wa kutoa misaada/ kwa wanaokukimbilia katika matatizo yao mazito./ Pia ni mwombezi wa waliopondeka moyo./
Mimi ni mmoja wa hao./ Nakujia na moyo uliojaa shida na matatizo./ Nakusihi kwa moyo wote/ unisaidie kwa maombezi yako yenye nguvu/ kufikia utatuzi unaofaa kadiri ya mapenzi ya Mungu./ Maisha yangu yamejaa misalaba,/ siku kwa siku matatizo hayapungui./ Moyo wangu umekuwa bahari ya siki chungu sana./ Mapito yangu nayaona yamejaa miiba mikali./ Roho yangu imezama katika dimbwi la machozi na kite./ Nafsi yangu imezingirwa na giza nene./ Ghasia na kukatishwa tamaa ya kuishi/ hunyemelea roho yangu./ Maongozi ya Mungu na imani naviona vinanitoka kidogo kwa kidogo./
Nikielemewa na mawazo kama hayo/ najikuta sina nguvu za kuishi,/ na maisha kwangu ni msalaba mzito/ ninaouogopa hata kuunyakua./ Wewe unaweza kabisa kunitoa katika balaa hili./ Sitaacha kukusihi/ hadi hapo utakaponisaidia/ au kunijulisha mapenzi ya Mungu kwangu./ Natangulia kutoa shukrani kwa jibu liwalo lote.
Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.
Tunakushukuru, ee Mungu, kwa mapaji uliyotujalia leo. Amina.
Baba yetu …
Salamu Maria …
Mungu wangu, nasadiki maneno yote. Linayosadiki na linayofundisha Kanisa Katoliki la Roma. Kwani ndiwe uliyetufumbulia hayo. Wala hudanganyiki, wala hudanganyi. Amina.
Mungu wangu, natumaini kwako, nitapewa kwa njia ya Yesu Kristo. Neema zako hapa duniani, na utukufu mbinguni. Kwani ndiwe uliye agana hayo nasi, nawe mwamini. Amina.
Mungu wangu, nakupenda zaidi ya chochote. Kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza. Nampenda na jirani yangu, kama nafsi yangu, kwa ajili yako. Amina.
Tuwaze katika moyo wetu makosa ya leo tuliyomkosea Mungu kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo na kwa kutotimiza wajibu. (Husubiri kidogo ).
Nakuungamia Mungu Mwenyezi, nanyi ndugu zangu, kwani nimekosa mno, kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo, na kwa kutotimiza wajibu.
Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana. Ndiyo maana nakuomba Maria mwenye heri, Bikira daima, Malaika na Watakatifu wote, nanyi ndugu zangu, niombeeni kwa Bwana Mungu wetu.
Mungu Mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele. Amina.
Ee Mungu, nawaombea watu wa nchi hii, wapate kusikia maneno yako na kukupenda wewe Bwana Mungu wetu.
Malaika mlinzi wangu, unilinde katika hatari zote za roho na za mwili. Amina.
(kipindi kisicho cha Pasaka)
Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria.
Naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
Salamu, Maria,…..
Ndimi mtumishi wa Bwana.
Nitendewe ulivyonena.
Salamu, Maria….
Neno la Mungu akatwaa mwili.
Akakaa kwetu.
Salamu, Maria….
Utuombee, Mzazi mtakatifu wa Mungu.
Tujaliwe ahadi za Kristu.
Tuombe:
Tunakuomba, Ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika kwamba Mwanao amejifanya Mtu kwa mateso na msalaba wake tufikishwe kwenye utukufu wa ufufuko. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. AMINA.
Malkia wa mbingu, furahi, aleluya.
Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.
Amefufuka alivyosema, Aleluya.
Utuombee kwa Mungu, Aleluya.
Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Alaluya.
Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.
Tuombe.
Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu, Mwanao, fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.
ATUKUZWE (mara tatu)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Kama mwanzo na sasa na siku zote na milele. Amina.
Enyi Yesu, Maria na Yosefu nawatolea moyo na roho na uzima wangu!
Enyi Yesu, Maria na Yosefu mnijilie saa ya kufa kwangu!
Enyi Yesu, Maria na Yosefu mnijalie nife mikononi mwenu!
(Rehema ya siku 300).
Kwa heri Yesu mpenzi mwema,
Naenda usiudhike mno.
Nakushukuru, nakupenda,
Kwa hizo nyimbo za mwisho.
Asubuhi nitarudi.
Yesu kwa heri.
Kwa heri Mama mtakatifu,
Sasa napita pumzika.
Asante kwa moyo na nguvu,
Leo umeniombea.
Asubuhi nitarudi.
Mama kwa heri.
Kwa heri Yosefu mnyenyekevu,
Kazi zatimilizika.
Kama mchana, leo usiku,
Nisimamie salama.
Asubuhi nitarudi.
Yosefu kwa heri.
Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.
Mungu wangu naenda kulala naomba malaika 14, waende nami, wawili juu, wawili chini, wawili upande wa kuume, wawili upande wa kushoto, wawili wanifunike, wawili waniamshe, wawili wanipeleke juu mbinguni. Mimi mtoto mdogo, roho yangu ni ndogo, haina nafasi kwa mtu yoyote ila kwa Yesu pekee. Amina.
Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakukimbilia, ninakuja kwako katika mikono yako yenye huruma. Ndiwe tegemeo langu na tumaini langu dhabiti. Ndiwe mwenye dawa ya maovu yangu yote, malipizi ya makosa yangu yote. Waweza kunipatia haja zangu na neema ninazoziomba mimi na wengine. Wewe uko ili kutusaidia sote, ndiwe mwanga mkuu usiozimika, ndiwe chanzo cha nguvu, uvumilivu, amani na faraja. Nina hakika kuwa maombi yangu hayatakuchosha, nawe hutaacha kunisaidia, kunilinda, kunipenda, kwani, ee Moyo Mtakatifu , upendo wako hauna mwisho. Ee Moyo Mtakatifu, unihurumie, kwa ajili ya maombi yangu, kadiri ya huruma yako. Nawe katika sisi, na kwa ajili yetu, ufanye lolote unalolihitaji, kwani tunajitoa kwako kwa imani na uhakika thabiti kwamba kamwe hautatuacha, kwa milele. Amina.
Ee Mtakatifu Teresia wa mtoto Yesu, ulistahili kuitwa Msimamizi wa misioni katoliki za dunia yote. Kumbuka ile tamaa yako kuu uliyoonyesha huku duniani ya ” kusimika Msalaba wa Yesu Kristu, katika nchi zote na kuhubiri Injili mpaka mwisho wa dunia” . Twakuomba kwa ajili ya maagano yako, wasaidie mapadre, wamisionari, na kanisa zima.
Ee Mtakatifu Teresia wa mtoto Yesu ” Msimamizi wa misioni” UTUOMBEE
Recent Comments