Sala za Maombi

Majitoleo kwa Bikira Maria

(Sala iliyotungwa na Mtk. Aloisi)
Bibi yangu mtukufu Maria, nakuwekea amana ya roho yangu na mwili wangu, nikikuomba uipokee amana yangu, kuitunzia ulinzi mwema ulinzi bora, ninakuaminia na kila neno langu, matumaini na kitulizo na kisongo chote, na masumbuko na uzima na ukomo wa uzima wangu: nitakayo ndiyo unifanyizie kwa maombezi na stahili zako, ili mambo yangu yote yapate kuongoka, yakiwa na kufuata mapenzi yako, pamoja na mapenzi ya Mwanao. Amina.

SALA YA MAOMBI KWA MOYO MTAKATIFU WA YESU

Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakukimbilia, ninakuja kwako katika mikono yako yenye huruma. Ndiwe tegemeo langu na tumaini langu dhabiti. Ndiwe mwenye dawa ya maovu yangu yote, malipizi ya makosa yangu yote. Waweza kunipatia haja zangu na neema ninazoziomba mimi na wengine. Wewe uko ili kutusaidia sote, ndiwe mwanga mkuu usiozimika, ndiwe chanzo cha nguvu, uvumilivu, amani na faraja. Nina hakika kuwa maombi yangu hayatakuchosha, nawe hutaacha kunisaidia, kunilinda, kunipenda, kwani, ee Moyo Mtakatifu , upendo wako hauna mwisho. Ee Moyo Mtakatifu, unihurumie, kwa ajili ya maombi yangu, kadiri ya huruma yako. Nawe katika sisi, na kwa ajili yetu, ufanye lolote unalolihitaji, kwani tunajitoa kwako kwa imani na uhakika thabiti kwamba kamwe hautatuacha, kwa milele. Amina.

SALA KWA MAMA WA UCHUNGU KUOMBA NEEMA YA PEKEE

Ee Mama mbarikiwa na Bikira mwenye uchungu, Malkia wa Mashahidi, uliyesimama chini ya msalaba na uliyemtazama Mwana wako akifa, unitazame kwa huruma ya kimama ninayekusikitikia. Kwa sababu ya upanga uliochoma moyo wako, kwa mateso ya maisha yako nakuomba uniangalie kwa wema ukasikilize maombi yangu. Nakuomba, ee Mama, uniombee daima kwa Mwana wako, najua hawezi kukuvyima wewe kitu chochote. Basi, ufanye, Moyo wa Mwanao ukubali kunijalia ombi langu hili โ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆ(taja ombi lako).
Maana nitamkimbilia nani katika mahitaji na misiba yangu isipokuwa kwako, ee Mama wa huruma? Wewe hasa unaweza kutusaidia sisi tulio bado katika bonde la machozi kwa sababu ulishiriki mateso ya Mwanao kutukomboa. Umtolee Yesu tone moja la Damu yake takatifu. Umkumbushe ya kuwa wewe ni matumaini, furaha na maisha yetu ukanipatie jambo ninalokuomba kwa Yesu Kristo, bwana wetu. Amina.

ROZARI YA MATESO SABA YA BIKIRA MARIA

Tumia Rozari ya Mateso Saba ya Bikira Maria iliyo na mafungu 7 yaani mateso 7 yenye Salamu Maria saba kwa kila teso.

TESO LA KWANZA

Mzee Simeoni aliagua kuwa Moyo wa Mama Maria utachomwa kwa upanga.
Tuombe neema ya kuvumilia mateso.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu โ€ฆโ€ฆโ€ฆ Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba โ€ฆโ€ฆ
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA PILI

Maria na Yosefu walikimbilia Misri usiku ili kumficha Mtoto Yesu asiuawe na Herodi.
Tuombe neema ili miili yetu iwe kimbilio lake Yesu.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu โ€ฆโ€ฆโ€ฆ Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba โ€ฆโ€ฆ
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA TATU

Mama Maria aliona uchungu sana Mtoto Yesu alipopotea kwa siku tatu.
Tuombe neema ya kudumu na Yesu mioyoni mwetu.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu โ€ฆโ€ฆโ€ฆ Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba โ€ฆโ€ฆ
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA NNE

Mama Maria aliona uchungu sana alipokutana na Mwanae Yesu katika njia ya Msalaba.
Tuombe neema ya kudumu na Yesu siku zote.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu โ€ฆโ€ฆโ€ฆ Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba โ€ฆโ€ฆ
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA TANO

Mama Maria aliona uchungu sana alipomwona Mwanae Yesu akisulibiwa Msalabani.
Tuombe neema ya kufa mikononi mwa Yesu na Maria.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu โ€ฆโ€ฆโ€ฆ Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba โ€ฆโ€ฆ
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA SITA

Mama Maria aliona uchungu sana alipopakata maiti ya Mwanae Yesu baada ya kushushwa Msalabani.
Tuombe neema ya kutotenda dhambi.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu โ€ฆโ€ฆโ€ฆ Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba โ€ฆโ€ฆ
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA SABA

Mama Maria aliona uchungu sana aliporudi nyumbani baada ya kumzika Mwanae Yesu
Tuombe neema ya kitulizo kwa Mama Maria.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu โ€ฆโ€ฆโ€ฆ Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba โ€ฆโ€ฆ
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

SALA YA KUMWOMBA MTAKATIFU TERESIA WA MTOTO YESU

Ee Mtakatifu Teresia wa mtoto Yesu, ulistahili kuitwa Msimamizi wa misioni katoliki za dunia yote. Kumbuka ile tamaa yako kuu uliyoonyesha huku duniani ya ” kusimika Msalaba wa Yesu Kristu, katika nchi zote na kuhubiri Injili mpaka mwisho wa dunia” . Twakuomba kwa ajili ya maagano yako, wasaidie mapadre, wamisionari, na kanisa zima.

Ee Mtakatifu Teresia wa mtoto Yesu ” Msimamizi wa misioni” UTUOMBEE

SALA YA MAJITOLEO KWA MAMA WA HUZUNI

Mama Mtakatifu, Mama wa Mungu na Malkia wa Mashahidi, leo nakuchagua Wewe uwe mfano wangu, mkingaji na mteteaji wangu. Naweka roho fukara katika moyo wako uliotobolewa na panga nyingi za mateso. Unipokee mimi niwe mtumishi wako wa pekee na mshiriki wa mateso yako. Nijalie nguvu niwe daima karibu na msalaba ule alikosulibiwa Yesu. Nakutolea nafsi yangu na mali yangu yote. Pokea kila tendo langu jema ukalisindikize kwa Mwanao, Mama, nifanye nistahili kuitwa mtumishi wa Maria, Simama karibu yangu katika matendo yangu yote ili yafanwe kwa sifa ya Mungu. Ulivyosimama karibu kabisa ya Mwanao alipokufa msalabani uwe karibu nami saa ya kufa kwangu. Nijalie niweze kutaja jina lako na la Mwana wako nikisema: โ€œYesu, Maria na Yosef mnisaidie saa ya kufa kwangu. Yesu, maria na Yosef, naomba nife kwa amani kati yenu!โ€ . Amina.

Sala kwa Mtakatifu Yosefu

Ee Yosef mwenye heri, tunakimbilia kwako, katika masumbuko yetu, na kishaomba shime ya Mchumba wako Mtakatifu, tunaomba pia kwa matumaini usimamizi wako. Kwa ajili ya mapendo uliyompenda nayo Bikira Mtakatifu, Mzazi wa Mungu, na kwa ajili ya tunza ya Baba, uliyomtunza nayo Mtoto Yesu, tunakuomba sana, utuangalie kwa wema, sisi tuliokuwa fungu lake Yesu Kristo, tuliokombolewa kwa damu yake, utusimamie katika masumbuko yetu, kwa enzi na shime yako.
Ee Mlinzi amini wa Jamaa Takatifu, uwakinge watoto wateule wa Yesu Kristo, ee Baba uliyetupenda mno, utuepusha na kilema chochote cha madanganyo na upotevu. Ee kinga yetu mwezaji,utusimamie huko juu mbinguni ulipo, tunaposhindana na wenye nguvu wakaao gizani. Kama vile siku za kale ukamwokoa Mtoto Yesu katika hatari ya kuuawa, na leo hivi, ulikinge Kanisa Takatifu la Mungu katika mitego ya adui, na katika shida yote, mtunze daima kila mmoja wetu, tupate mfano wako, tusaidie kwa msaada wako, kukaa na utakatifu maisha, kufa kifo chema, na kupokelewa mbinguni makao ya raha milele. Amina

SALA YA UHAI KWA MT. YOSEFU

(Sala hii inafaa sana kwa ajili ya kutetea uhai wa watoto wachanga wakiwa tumboni mwa mama zao, dhidi ya utoaji mimba au hatari nyingine dhidi ya uhai wa binadamu)

Ee Mt. Yosefu, wewe ni Mchumba safi na Mpenzi wa Bikira Maria, u Baba Mlishi wa Yesu, mlinzi na mtunzaji wa Familia Takatifu, na wa familia zote. Tuna imani kabisa katika uangalizi wako uliojaa upendo, juu ya uhai mpya, na uaminifu wako kwa familia.

Tunaweka jitihada zetu chini ya ulinzi wa sala zako. Utusaidie daima katika kutetea zawadi ya uhai wa binadamu, ili ukue hadi uzima wa milele ulioahidiwa na kujaliwa kwetu na Mwanao, Ndugu yetu, Yesu Kristu.
Amina.

Sala fupi ya Asubuhi

Tuusifu Utatu Mtakatifu wa Mungu Mwenyezi, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, milele na milele, Amina.

Ee Utatu Mtakatifu wa Mwenyezi Mungu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, nasadiki kuwa upo hapa na mahali pote. Ee Mungu wangu, umeniumba, umenikomboa, umenifanya mkristo, umenizidishia neema zako hapa duniani, umenitayarishia makao yangu mbinguni, umenijalia na siku hii nikutumikie. Ee Mungu wangu! Nakuabudu, nakushukuru, nakuomba toba, nakupenda! Ee Mungu wangu, nakutolea roho yangu, na mawazo, na maneno, na kazi, na furaha, na mateso yangu: uyapokee unipe neema yako nisikutende leo dhambi!

Malkia wa Mbingu

Malkia wa mbingu, furahi, aleluya. Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya. Amefufuka alivyosema, Aleluya. Utuombee kwa Mungu, Aleluya. Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Alaluya. Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya. Tuombe. Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu, Mwanao: fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.

Shopping Cart
15
    15
    Your Cart
    ๐Ÿ  Home ๐Ÿ“– Reading ๐Ÿ–ผ๏ธ Gallery ๐Ÿ’ฌ AI Chat ๐Ÿ“˜ About