Sala za Maombi

KUJIWEKA CHINI YA ULINZI WA MT. YOSEFU

Ee Mt. Yosefu, Baba Mlishi wa Mwokozi wangu, na mchumba safi wa Mama wa Mungu, leo ninakuchagua wewe, kama mwombezi wangu kwa Mungu Mwenyezi, na pia kama mfano wangu, na mlinzi wangu, na baba yangu, katika bonde hili la ugenini.

Ee Mt. Yosefu, ambaye Bwana alikufanya mlinzi wa Familia yake, ninakuomba uwe mlinzi wangu mwema katika mambo yangu yote. Uniwashie moyoni mwangu moto wa mapendo makuu kwa Yesu, na uniwezeshe kumtumikia kwa bidii na kwa uaminifu kwa mfano wako. Nisaidie katika udhaifu wangu katika kumheshimu Mama Maria kama Mwombezi wangu.

Daima uwe kiongozi wangu katika njia ya fadhila na ibada, na unijalie, baada ya kukufuasa kwa uaminifu katika njia ya haki, nipate ulinzi wako wenye nguvu katika saa ya kufa kwangu.
Amina

Malkia wa Mbingu

Malkia wa mbingu, furahi, aleluya. Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya. Amefufuka alivyosema, Aleluya. Utuombee kwa Mungu, Aleluya. Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Alaluya. Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya. Tuombe. Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu, Mwanao: fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.

Kanuni ya imani

Nasadiki kwa Mungu, Baba Mwenyezi,/ mwumba mbingu na dunia./ Na kwa Yesu Kristu, Mwanaye wa pekee, Bwana wetu;/ aliyetungwa kwa Roho Mtakatifu,/ akazaliwa na Bikira Maria,/ akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato,/ akasulubiwa, akafa, akazikwa,/ akashukia kuzimu;/ siku ya tatu akafufuka katika wafu;/ akapaa mbinguni;/ amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi;/ toka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu,/ Kanisa takatifu katoliki,/ ushirika wa Watakatifu,/ maondoleo ya dhambi,/ ufufuko wa miili,/ uzima wa milele. Amina.

SALA YA KUOMBEA FAMILIA

Ewe Mungu Mwenyezi, sisi kama familia tunakushukuru kwa zawadi ya Mama Kanisa Katoliki ambaye siku zote hutupatia malezi bora kwa ajili ya wokovu wetu. Kanisa halichoki kutuhimiza tutafakari na kuishi utakatifu wa familia ya Nazareti ya Yesu, Maria na Yosefu. Familia hii iliishi upendo uliojengwa kwa fadhila za imani, uaminifu, utii, uvumilivu na upole hata wakawa watakatifu. Tunapoadhimisha mwaka wa Familia, tunaiweka mbele yetu familia ya Nazareti iwe dira, baraka na mfano kwa familia zetu.

Tunakushukuru Baba kwa ajili ya familia zote zinazojitahidi kuishi fadhila hizo za Familia takatifu na tunakuomba uzidi kuwaimarisha wanandoa ili tupate kwao mifano mingi na bora ya kuigwa. Ee Bwana, tunaomba Roho Mtakatifu atuangazie tuweze: kutambua familia kuwa Kanisa la nyumbani na shule ya imani na upendo; kuimarisha familia kwa sala, sakramenti na tunu za kiinjili na kushirikiana kwa heshima katika familia kwa usitawi wa roho na wa mwili kwa wanafamilia wote.

Tunaziombea familia zetu na Jumuiya Ndogondogo za Kikristo ziwe bustani bora na salama za kuchipusha na kulea miito mitakatifu ya Ndoa, Utawa na Upadre. Tunawaombea vijana na watoto wetu Uchaji wa Mungu ili wawe na bidii ya kujitunza kwa kushika amri za Mungu na kuishi fadhila za kiinjili, wawe na roho ya kimisionari yaani walipende Kanisa na kuwa na moyo wa kueneza ufalme wako kwa matendo ya imani. Baba wa huruma, tunakukabidhi familia zenye misukosuko ya mafarakano, ulevi, ubinafsi, uregevu-dini, uvivu, ushirikina, hofu, magonjwa sugu na mengineyo yenye kuleta huzuni; kwa hisani yako uwape neema, mwanga na nguvu za kuanza maisha mapya yenye amani, waweze kufurahia upatanisho na uponyi wa pendo lako la kibaba kati yao.

Tunaomba toba na msamaha kwa ukatili, manyanyaso na hata mauaji katika familia zetu na uwaponye wote waliojeruhiwa kwa maneno, matendo na makwazo ya aina yeyote. Aidha tunakuomba uwe kitulizo na faraja kwa wagonjwa na wazee, pia tegemeo la yatima na wajane. Wenye matatizo ya kiafya au ya kijamii wasikate tamaa bali waunganishe hali zao na msalaba wa Mwanao na kukutumaini wewe Mweza yote. Jamii iwajibike nao kwa kuzijali haki zao na kuwapa misaada wanayohitaji.

Tunakuomba ubariki miradi na kazi zetu ili familia zipate usitawi na maendeleo; na utujalie hekima ya kukushukuru kwa maisha ya haki, amani na ukarimu na mwisho tukaimbe sifa zako pamoja na familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefuna jeshi lote la mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

Baba yetu… …..Salamu Maria….…Atukuzwe Baba………

SALA YA KUMWOMBA MTAKATIFU TERESIA WA MTOTO YESU

Ee Mtakatifu Teresia wa mtoto Yesu, ulistahili kuitwa Msimamizi wa misioni katoliki za dunia yote. Kumbuka ile tamaa yako kuu uliyoonyesha huku duniani ya ” kusimika Msalaba wa Yesu Kristu, katika nchi zote na kuhubiri Injili mpaka mwisho wa dunia” . Twakuomba kwa ajili ya maagano yako, wasaidie mapadre, wamisionari, na kanisa zima.

Ee Mtakatifu Teresia wa mtoto Yesu ” Msimamizi wa misioni” UTUOMBEE

Sala ya Kuombea Hali njema ya hewa na mvua

Ee Mungu Mwenyezi wa milele, mpaji wa mema yote, unayetusamehe na kutulinda. Utujalie sisi tunaokusihi, tufurahie hali njema ya hewa na mvua tunayoitamani na kuhitaji. Tutumie daima vipawa vya wema wako kwa ajili ya utukufu wa jina lako, na kwa ajili ya wokovu watu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana watu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele. Amina. `

`Baba Yetu………………. Salama Maria………… Atukuzwe Baba……….. `

K: `Bikra Maria mama wa msaada wa daima…. W: Utuombee na Utusaidie`

SALA YA MAOMBI KWA MOYO MTAKATIFU WA YESU

Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakukimbilia, ninakuja kwako katika mikono yako yenye huruma. Ndiwe tegemeo langu na tumaini langu dhabiti. Ndiwe mwenye dawa ya maovu yangu yote, malipizi ya makosa yangu yote. Waweza kunipatia haja zangu na neema ninazoziomba mimi na wengine. Wewe uko ili kutusaidia sote, ndiwe mwanga mkuu usiozimika, ndiwe chanzo cha nguvu, uvumilivu, amani na faraja. Nina hakika kuwa maombi yangu hayatakuchosha, nawe hutaacha kunisaidia, kunilinda, kunipenda, kwani, ee Moyo Mtakatifu , upendo wako hauna mwisho. Ee Moyo Mtakatifu, unihurumie, kwa ajili ya maombi yangu, kadiri ya huruma yako. Nawe katika sisi, na kwa ajili yetu, ufanye lolote unalolihitaji, kwani tunajitoa kwako kwa imani na uhakika thabiti kwamba kamwe hautatuacha, kwa milele. Amina.

SALA KWA MT. YOSEFU KUOMBA KUFAHAMU WITO WAKO

Ee uliye Mkuu, Mt. Yosefu, uliyatii kabisa maongozi ya Roho Mt. Unijalie neema ya kufahamu aina ya maisha ambayo Mungu anapenda mimi niishi. Usiniache nidanganyike katika jambo muhimu kama hili, ambalo furaha yangu hapa duniani inalitegemea, na hata pia wokovu wa roho yangu.

Unijalie, nikiangazwa na matakwa matakatifu na nikiwa mwaminifu katika kuyatimiza, nikumbatie aina ya maisha ambayo Mungu ameniandalia na yatakayoniongoza kwenye furaha ya milele.
Amina.

SALA YA KUMWABUDU BWANA YESU KATIKA SAKRAMENTI TAKATIFU

Ee Yesu Kristu,/ Bwana wangu na Mungu wangu/ ambaye ninasadiki kuwa upo hapa/ katika Sakramenti Takatifu ya Altare;/ pokea kitendo hiki cha kukuangukia kifudi fudi/ kama ishara ya tamaa niliyonayo ya kukuabudu Wewe/ bila kuchoka/ na kukushukuru kwa mapendo yako makubwa/ yasiyo na kipimo/ ambayo Moyo wako Mtakatifu sana/ unawaka katika Sakramenti Takatifu hii./ Siwezi kukushukuru vizuri zaidi/ kuliko kama ningetolea kwako/ matendo yangu yote ya kukuabudu/ unyenyekevu wangu/ uvumilivu na mapendo/ ambayo huu Moyo Mwabudiwa ulifanya,/ bado unafanya/ na utaendelea kufanya katika uzima wa milele mbinguni./ Ninaahidi kupitia Moyo huu,/ nitakupenda,/ nitakutukuza,/ na nitakuabudu kama nitakavyoweza./ Ninajiunganisha na hii Sadaka Takatifu/ ambayo unatoa kwa Baba Mungu/ na ninatolea kwako utu wangu./ Ninakuomba kuangamiza ndani yangu/ dhambi zote pamoja na majeraha yake/ na usikubali kunitenga nawe milele./ Amina.

(Na Mt. Margareta Maria Alakoki)

SALA YA UHAI KWA MT. YOSEFU

(Sala hii inafaa sana kwa ajili ya kutetea uhai wa watoto wachanga wakiwa tumboni mwa mama zao, dhidi ya utoaji mimba au hatari nyingine dhidi ya uhai wa binadamu)

Ee Mt. Yosefu, wewe ni Mchumba safi na Mpenzi wa Bikira Maria, u Baba Mlishi wa Yesu, mlinzi na mtunzaji wa Familia Takatifu, na wa familia zote. Tuna imani kabisa katika uangalizi wako uliojaa upendo, juu ya uhai mpya, na uaminifu wako kwa familia.

Tunaweka jitihada zetu chini ya ulinzi wa sala zako. Utusaidie daima katika kutetea zawadi ya uhai wa binadamu, ili ukue hadi uzima wa milele ulioahidiwa na kujaliwa kwetu na Mwanao, Ndugu yetu, Yesu Kristu.
Amina.

Shopping Cart
19
    19
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About