Sala za Maombi

SALA YA MAJITOLEO KWA MAMA WA HUZUNI

Mama Mtakatifu, Mama wa Mungu na Malkia wa Mashahidi, leo nakuchagua Wewe uwe mfano wangu, mkingaji na mteteaji wangu. Naweka roho fukara katika moyo wako uliotobolewa na panga nyingi za mateso. Unipokee mimi niwe mtumishi wako wa pekee na mshiriki wa mateso yako. Nijalie nguvu niwe daima karibu na msalaba ule alikosulibiwa Yesu. Nakutolea nafsi yangu na mali yangu yote. Pokea kila tendo langu jema ukalisindikize kwa Mwanao, Mama, nifanye nistahili kuitwa mtumishi wa Maria, Simama karibu yangu katika matendo yangu yote ili yafanwe kwa sifa ya Mungu. Ulivyosimama karibu kabisa ya Mwanao alipokufa msalabani uwe karibu nami saa ya kufa kwangu. Nijalie niweze kutaja jina lako na la Mwana wako nikisema: “Yesu, Maria na Yosef mnisaidie saa ya kufa kwangu. Yesu, maria na Yosef, naomba nife kwa amani kati yenu!” . Amina.

LITANIA YA KUWAOMBEA MAPADRE WOTE II

Kwa ajili ya Baba Mtakatifu wetu ..(N); Bwana, umpe moyo wako wa uchungaji mwema
Kwa ajili ya makardinali na maaskofu wakuu; Uwape moyo wa kichungaji ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wa majimbo; Uwajaze na Roho wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre watawa; Wakamilishe katika wito wao ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre walioko hatarini; Uwaokoe ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wenye udhaifu; Uwatie nguvu ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wenye hofu; Uwape amani ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre waliokata tamaa; Uwavuvie upya ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wakaao upweke; Uwasindikize ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wamisionari; Uwalinde ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wanaohubiri; Uwaangazie ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre na watawa waliokufa; Uwafikishe kwenye utukufu wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie hekima na ufahamu wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; Uwajalie elimu na shauri lako
Kwa ajili ya mapadre wako; wajalie wakuheshimu na wakuogope
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie subira na upendo
Kwa ajili ya mapadre wote; wajalie utii na upole
Kwa ajili ya mapadre wote; uwajalie hamu kuu ya kuokoa roho za watu
Kwa ajili ya mapadre wote; wape fadhila za imani, matumaini na mapendo
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie upendo mkuu kwa Ekaristi
Tunakuomba uwajalie mapadre wote; Waheshimu uhai na hadhi ya mtu ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote nguvu na bidii katika kazi zao ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote amani katika mahangaiko yao ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote upendo mkuu kwa Utatu Mtakatifu ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote upendo mkuu kwa Bikira Maria ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe mwanga wa Kristo ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wawe chumvi kwa ulimwengu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wajizoeze kujitoa sadaka na kujinyima ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wawe watakatifu kimwili, kiakili na kiroho ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe watu wa sala ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe kioo cha imani kwako ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wajali sana wongofu wetu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe waaminifu kwa wito wao wa kikuhani ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, ili mikono yao ibariki na kuponya ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawake moto wa mapendo yako ee Bwana
Uwajalie mapadre wote hatua zao zote ziwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wajazwe na Roho Mtakatifu na uwajalie karama zake kwa wingi ee Bwana.

Tuombe.
Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, usikie sala tunazokutolea kwa ajili ya mapadre wetu. Uwajalie wafahamu waziwazi kazi uliyowaitia kuifanya, uwape neema zote wanazohitaji ili waitikie wito wako kwa ushujaa, kwa upendo, na majitoleo yenye udumifu katika mapenzi yako matakatifu. Amina.

SALA KWA MAMA WA UCHUNGU KUOMBA NEEMA YA PEKEE

Ee Mama mbarikiwa na Bikira mwenye uchungu, Malkia wa Mashahidi, uliyesimama chini ya msalaba na uliyemtazama Mwana wako akifa, unitazame kwa huruma ya kimama ninayekusikitikia. Kwa sababu ya upanga uliochoma moyo wako, kwa mateso ya maisha yako nakuomba uniangalie kwa wema ukasikilize maombi yangu. Nakuomba, ee Mama, uniombee daima kwa Mwana wako, najua hawezi kukuvyima wewe kitu chochote. Basi, ufanye, Moyo wa Mwanao ukubali kunijalia ombi langu hili …………………(taja ombi lako).
Maana nitamkimbilia nani katika mahitaji na misiba yangu isipokuwa kwako, ee Mama wa huruma? Wewe hasa unaweza kutusaidia sisi tulio bado katika bonde la machozi kwa sababu ulishiriki mateso ya Mwanao kutukomboa. Umtolee Yesu tone moja la Damu yake takatifu. Umkumbushe ya kuwa wewe ni matumaini, furaha na maisha yetu ukanipatie jambo ninalokuomba kwa Yesu Kristo, bwana wetu. Amina.

SALA YA KUUABUDU MOYO MTAKATIFU WA YESU KATIKA EKARISTI TAKATIFU

Kwa nguvu zangu zote za moyo wangu/ ninakuabudu ee Moyo Mtakatifu/ na Mwabudiwa sana,/ Moyo Mtakatifu wa Bwana wetu Yesu Kristu/ ambao ninataka kumpenda/ na kukusalimu kwa usikivu unaoendelea./ Kamwe nisikuudhi tena/ kwa sababu Wewe ni Mwema sana;/ Ee Mwema sana./ Ee Moyo Mtakatifu sana/ ninakupenda/ na ninataka kukupenda zaidi ya vitu vyote,/ kwa nguvu zangu zote/ na kwa uwezo wangu wote,/ ninatamani kuwa mali yako/ Wewe uliyejitoa Msalabani kwa ajili yangu/ kwa mateso makali./ Unionee huruma na udhaifu wangu/ na usiniruhusu kupotea./

Ninajitoa kabisa kwako/ ee moyo wa mapendo,/ kwa makusudi kuwa utu wangu,/ maisha na mateso yangu/ yalipie kukupenda,/ kukuheshimu/ na kukutukuza Wewe sasa na milele./ Ninakupenda ee Moyo Mwabudiwa wa Mwokozi wangu,/ ninakuomba kwako/ uamuru moyo wangu na kila kitu ndani yangu/ kikutukuze sasa na milele./ Amina.

(Na Mt Margareta Maria Alakoki)

Sala ya Kuombea Hali njema ya hewa na mvua

Ee Mungu Mwenyezi wa milele, mpaji wa mema yote, unayetusamehe na kutulinda. Utujalie sisi tunaokusihi, tufurahie hali njema ya hewa na mvua tunayoitamani na kuhitaji. Tutumie daima vipawa vya wema wako kwa ajili ya utukufu wa jina lako, na kwa ajili ya wokovu watu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana watu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele. Amina. `

`Baba Yetu………………. Salama Maria………… Atukuzwe Baba……….. `

K: `Bikra Maria mama wa msaada wa daima…. W: Utuombee na Utusaidie`

Sala ya Saa Tisa

✝⌚✝

Sala ya saa tisa🙏🏾

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. A mina

Yesu, ulikufa, lakini chanzo cha uhai kilitoka kwa ajili ya watu, na bahari ya huruma ilifunguka kwa ajili ya ulimwengu mzima. Ee chemchemi ya Uhai, huruma ya Mungu isiyo na mwisho, ikafunika ulimwengu mzima na ukajimwaga mwenyewe juu yetu.

❣✝❣

✝Ee Damu na Maji, yaliyotoka moyoni mwa Yesu kama chemchemi ya Huruma kwetu. Nakutumainia.

(Mara tatu)

🛐❣🛐

Sala fupi ya Asubuhi

Tuusifu Utatu Mtakatifu wa Mungu Mwenyezi, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, milele na milele, Amina.

Ee Utatu Mtakatifu wa Mwenyezi Mungu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, nasadiki kuwa upo hapa na mahali pote. Ee Mungu wangu, umeniumba, umenikomboa, umenifanya mkristo, umenizidishia neema zako hapa duniani, umenitayarishia makao yangu mbinguni, umenijalia na siku hii nikutumikie. Ee Mungu wangu! Nakuabudu, nakushukuru, nakuomba toba, nakupenda! Ee Mungu wangu, nakutolea roho yangu, na mawazo, na maneno, na kazi, na furaha, na mateso yangu: uyapokee unipe neema yako nisikutende leo dhambi!

Majitoleo kwa Bikira Maria

(Sala iliyotungwa na Mtk. Aloisi)
Bibi yangu mtukufu Maria, nakuwekea amana ya roho yangu na mwili wangu, nikikuomba uipokee amana yangu, kuitunzia ulinzi mwema ulinzi bora, ninakuaminia na kila neno langu, matumaini na kitulizo na kisongo chote, na masumbuko na uzima na ukomo wa uzima wangu: nitakayo ndiyo unifanyizie kwa maombezi na stahili zako, ili mambo yangu yote yapate kuongoka, yakiwa na kufuata mapenzi yako, pamoja na mapenzi ya Mwanao. Amina.

Shopping Cart
2
    2
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About