Sala za Katoliki: Sala Muhimu Kwa Mkristu Mkatoliki

ROZARI YA MATESO SABA YA BIKIRA MARIA

Tumia Rozari ya Mateso Saba ya Bikira Maria iliyo na mafungu 7 yaani mateso 7 yenye Salamu Maria saba kwa kila teso.

TESO LA KWANZA

Mzee Simeoni aliagua kuwa Moyo wa Mama Maria utachomwa kwa upanga.
Tuombe neema ya kuvumilia mateso.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA PILI

Maria na Yosefu walikimbilia Misri usiku ili kumficha Mtoto Yesu asiuawe na Herodi.
Tuombe neema ili miili yetu iwe kimbilio lake Yesu.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA TATU

Mama Maria aliona uchungu sana Mtoto Yesu alipopotea kwa siku tatu.
Tuombe neema ya kudumu na Yesu mioyoni mwetu.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA NNE

Mama Maria aliona uchungu sana alipokutana na Mwanae Yesu katika njia ya Msalaba.
Tuombe neema ya kudumu na Yesu siku zote.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA TANO

Mama Maria aliona uchungu sana alipomwona Mwanae Yesu akisulibiwa Msalabani.
Tuombe neema ya kufa mikononi mwa Yesu na Maria.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA SITA

Mama Maria aliona uchungu sana alipopakata maiti ya Mwanae Yesu baada ya kushushwa Msalabani.
Tuombe neema ya kutotenda dhambi.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA SABA

Mama Maria aliona uchungu sana aliporudi nyumbani baada ya kumzika Mwanae Yesu
Tuombe neema ya kitulizo kwa Mama Maria.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

SALA KWA BIKIRA MARIA KATIKA UKIWA WAKE

Nakusikitikia sana Mama Mtakatifu Maria kwa sababu ya ukiwa wako mkuu. Uchungu wako ulikuwa mkubwa sana ulipotazama mateso na kifo cha Mwana wako mpenzi. Muda ule uliweza kutuliz kidogo kwa sababu ya kumwona angali hai. Lakini je, baada ya kufa na kumzika? Sasa wewe ni mkiwa mkubwa mno! Uh, ukiwa wa pekee, uniombee mimi ninayempoteza mara nyingi kwa dhambi zangu. Unijalie nisimpoteze tena Yesu wangu kwa ubaya wa uvivu wangu, bali nimtumikie kiaminifu duniani hapa ili nimwone na kumfurahia milele mbinguni. Amina.

ROSARI YA BIKIRA MARIA MAMA WA MSAADA WA DAIMA

Namna ya kusali Rozari kwa Bikira Maria Mama wa Msaada wa Daima

(Tumia rosari ya kawaida)

Mwanzo, kwenye Msalaba:

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.

Kwenye chembe ndogo za awali:

K: Ee Mungu utuelekezee msaada W: Ee Bwana utusaidie hima
W: Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Kama mwanzo na sasa na siku zote na milele. Amina.

Maria ametusaidia,
Maria anataka kutusaidia,
Maria anaweza kutusaidia,
Maria atatusaidia.

KATIKA KILA FUNGU SALI SALA ZIFUATAZO:

Kwenye chembe kubwa:

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Kama mwanzo na sasa, na siku zote, na milele. Amina.

Maria ametusaidia,
Maria anataka kutusaidia,
Maria anaweza kutusaidia,
Maria atatusaidia.

Ee Maria Mama wa Msaada wa daima
Sikiliza maombi ya roho zetu
Unaweza kutusaidia katika mahitaji yetu
Ee Maria kwa matumaini twakuita wewe.

Kwenye chembe ndogo:

Kama unasali mwenyewe: β€œEe Maria, utusaidie! (mara kumi)
Kama mnasali zaidi ya mmoja kwa pamoja: K; Ee Maria, W: Utusaidie. (mara kumi)

MWISHO SALI SALA ZIFUATAZO:

Salamu Maria

Salamu Maria, umejaa neema, Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu Mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa, na saa ya kufa kwetu. Amina. (mara tatu)

Tunaukimbilia

Tunaukimbilia ulinzi wako, ee Mzazi Mtakatifu wa Mungu, usitunyime tukiomba katika shida zetu, utuokoe siku zote, kila tuingiapo hatarini, ee Bikira Mtukufu na mwenye baraka,. Amina.

Kumbuka ee Bikira Mwenye Rehema

KUMBUKA

Kumbuka ee Bikira mwenye rehema, haijasikika kamwe kwamba ulimwacha mtu aliyekimbilia ulinzi wako, akiomba msaada wako, akitaka umwombe.

Nami kwa matumaini hayo, nakukimbilia ee mama, mkuu wa mabikira, ninakuja kwako, ninasimama mbele yako,Β  nikilalamika mimi mkosefu ewe mama wa neno la mungu, usiyakatae maneno yangu, mbali uyasikilize kwa wema na unitimizie Amina.

Novena ya Noeli

Novena ya Noeli (maarufu kama novena ya Mt. Andrea)

Husaliwa kuanzia tar 30 Nov hadi usiku wa Noeli, tar 24 Disemba. Inajulikana kama novena ya Mt. Andrea kwa sababu novena hii huanza kusaliwa katika siku ya kumbukumbu ya Mt. Andrea Mtume.

“IHESHIMIWE, NA IBARIKIWE, SAA ILE NA WAKATI ULE, AMBAO MWANA WA MUNGU, ALIZALIWA NA BIKIRA MBARIKIWA SANA, USIKU WA MANANE, KULE BETHLEHEM, WAKATI WA BARIDI KALI.
WAKATI HUO, UPENDE E MUNGU WANGU, KUSIKIA MAOMBI YANGU, NA KUNIJALIA YALE NINAYOYAOMBA KWAKO, KWA NJIA YA MASTAHILI YA MWOKOZI WETU YESU KRISTO, NA YA MAMA YAKE MBARIKIWA. AMINA. (Sali mara 15 kwa siku).

Inasadikika kuwa chochote uombacho kwa imani kwa sala hii utakipata mradi kipatane na mapenzi ya Mungu. Sali na watoto/ familia kuwatafakarisha na kuwaongezea matazamio juu ya sikukuu ya Noeli.

Isambaze sala hii kwa wengine.

Sala fupi ya Asubuhi

Tuusifu Utatu Mtakatifu wa Mungu Mwenyezi, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, milele na milele, Amina.

Ee Utatu Mtakatifu wa Mwenyezi Mungu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, nasadiki kuwa upo hapa na mahali pote. Ee Mungu wangu, umeniumba, umenikomboa, umenifanya mkristo, umenizidishia neema zako hapa duniani, umenitayarishia makao yangu mbinguni, umenijalia na siku hii nikutumikie. Ee Mungu wangu! Nakuabudu, nakushukuru, nakuomba toba, nakupenda! Ee Mungu wangu, nakutolea roho yangu, na mawazo, na maneno, na kazi, na furaha, na mateso yangu: uyapokee unipe neema yako nisikutende leo dhambi!

SALA MBELE YA KITI CHA ENZI CHA MUNGU

Sali Atukuzwe 7 kwa heshima ya Malaika 7 wateule ujipatie neema ya kuepa dhambi mbaya saba na kutujaza mapaji saba ya Roho Mtakatifu.

TUOMBE
Ee Mungu Mwenyezi wa milele, kwa wema na huruma yako ya ajabu, umetaka watu wako waokoke, ukamweka Malaika Mkuu Mikaeli kuwa Mkuu wa Kanisa lako, Utukinge na adui zetu, wasitusmbue saa ya kufa kwetu, bali tuongozwe naye kwenye utukufu wako Mkuu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana Wetu Yesu Kristo. Amina.

Utuombee Ee Mtukufu Mtakatifu Mikaeli Mkuu wa Kanisa la Yesu Kristo, tujaliwe ahadi za Kristo. Amina.

SALA YA KUUABUDU MOYO MTAKATIFU WA YESU KATIKA EKARISTI TAKATIFU

Kwa nguvu zangu zote za moyo wangu/ ninakuabudu ee Moyo Mtakatifu/ na Mwabudiwa sana,/ Moyo Mtakatifu wa Bwana wetu Yesu Kristu/ ambao ninataka kumpenda/ na kukusalimu kwa usikivu unaoendelea./ Kamwe nisikuudhi tena/ kwa sababu Wewe ni Mwema sana;/ Ee Mwema sana./ Ee Moyo Mtakatifu sana/ ninakupenda/ na ninataka kukupenda zaidi ya vitu vyote,/ kwa nguvu zangu zote/ na kwa uwezo wangu wote,/ ninatamani kuwa mali yako/ Wewe uliyejitoa Msalabani kwa ajili yangu/ kwa mateso makali./ Unionee huruma na udhaifu wangu/ na usiniruhusu kupotea./

Ninajitoa kabisa kwako/ ee moyo wa mapendo,/ kwa makusudi kuwa utu wangu,/ maisha na mateso yangu/ yalipie kukupenda,/ kukuheshimu/ na kukutukuza Wewe sasa na milele./ Ninakupenda ee Moyo Mwabudiwa wa Mwokozi wangu,/ ninakuomba kwako/ uamuru moyo wangu na kila kitu ndani yangu/ kikutukuze sasa na milele./ Amina.

(Na Mt Margareta Maria Alakoki)

Sala ya Malaika wa Bwana

Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria, naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Salamu Maria,….

Ndimi Mtumishi wa Bwana, nitendewe ulivyonena. Salamu Maria, ……
Neno wa Bwana akatwaa Mwili, akakaa kwetu. Salamu Maria, …..

Utuombee, ee Mzazi Mtakatifu wa Mungu, tujaliwe ahadi za Kristo.

Tuombe:

Tunakuomba ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika, kwamba, Kristo Mwanao amejifanya mtu: kwa mateso na Msalaba wake, utufikishe kwenye utukufu wa ufufuko. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu, Amina.

Shopping Cart
🏠 Home πŸ“– Reading πŸ–ΌοΈ Gallery πŸ’¬ AI Chat πŸ“˜ About