Sala za Katoliki: Sala Muhimu Kwa Mkristu Mkatoliki

SALA YA KUUABUDU MOYO MTAKATIFU WA YESU KATIKA EKARISTI TAKATIFU

Kwa nguvu zangu zote za moyo wangu/ ninakuabudu ee Moyo Mtakatifu/ na Mwabudiwa sana,/ Moyo Mtakatifu wa Bwana wetu Yesu Kristu/ ambao ninataka kumpenda/ na kukusalimu kwa usikivu unaoendelea./ Kamwe nisikuudhi tena/ kwa sababu Wewe ni Mwema sana;/ Ee Mwema sana./ Ee Moyo Mtakatifu sana/ ninakupenda/ na ninataka kukupenda zaidi ya vitu vyote,/ kwa nguvu zangu zote/ na kwa uwezo wangu wote,/ ninatamani kuwa mali yako/ Wewe uliyejitoa Msalabani kwa ajili yangu/ kwa mateso makali./ Unionee huruma na udhaifu wangu/ na usiniruhusu kupotea./

Ninajitoa kabisa kwako/ ee moyo wa mapendo,/ kwa makusudi kuwa utu wangu,/ maisha na mateso yangu/ yalipie kukupenda,/ kukuheshimu/ na kukutukuza Wewe sasa na milele./ Ninakupenda ee Moyo Mwabudiwa wa Mwokozi wangu,/ ninakuomba kwako/ uamuru moyo wangu na kila kitu ndani yangu/ kikutukuze sasa na milele./ Amina.

(Na Mt Margareta Maria Alakoki)

ROZARI, MATENDO NA LITANI YA MAMA BIKIRA MARIA

Rozari ya Bikira Maria
Mwongozo wa namna ya Kusali Rozari Takatifu ya Mama Bikira Maria

Anza kusali Rozari kwa kuibusu miguu ya Bwana Yesu katika taswira (picha) yake Msalabani kisha fanya Ishara ya Msalaba ukiwa unasema “Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina”.

Taja kwa ufupi nia za Rozari hii. Tangaza nia hizo kwa sauti kama mnasali wengi kwa pamoja, Mfano, “Tusali kuombea amani katika nchi yetu na ulimwenguni kote, na tuunganishe nia hizo na nia zetu sisi wenyewe, nk).

Baada ya Sala ya Nasadiki pamoja na ya Baba Yetu, tunamwomba Mungu (Utatu Mtakatifu) fadhila za Imani, Matumaini na Mapendo, zikiambatana na Salamu Maria tatu.

Mojawapo ya maneno yafuatayo huweza kutumika:
“Mungu Baba utuongezee Imani. Salamu Maria, …… Mungu Mwana utuongezee matumaini, Salamu Maria, …… Mungu Roho Mtakatifu washa nyoyo zetu kwa mapendo yako, Salamu Maria, …..”

Au;

“Utuongezee Imani ee Bwana, Salamu Maria,…. Utuongezee matumaini ee Bwana, Salamu Maria,…. Uwashe nyoyo zetu kwa mapendo yako ee Bwana, Salamu Maria, …..” Au;
“Salamu e uliyechaguliwa na Mungu Baba, Salamu Maria,….. Salamu e Mama wa Mungu Mwana, Salamu Maria,….. Salamu e Mchumba wa Mungu Roho Mtakatifu, Salamu Maria,……”
Atukuzwe Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele, Amina.

Ee Yesu wangu, utusamehe dhambi zetu, utuepushe na moto wa milele, ongoza roho zote mbinguni, hasa za wale wanaohitaji huruma yako zaidi.
Tuwasifu milele, Yesu, Maria na Yosef.

Kisha endelea na sala zinazofuata kama mpangilio unavyoonyesha hapo juu.

Kila baada ya Tendo moja na makumi ya Salamu Maria…, “Atukuzwe..”, “Ee Yesu wangu…” na “Tuwasifu milele…” kama muda unatosha wimbo ufaao wa Bikira Maria uimbwe (kama muda ni mfupi basi angalau ubeti mmoja mmoja uimbwe kila baada ya makumi hayo). Baada ya Wimbo, Tendo linalofuata litangazwe kwa sauti pamoja na tafakari fupi au ombi linaloambatana na Tendo husika kama inavyoonyeshwa hapa chini.

MATENDO YA ROZARI TAKATIFU

MATENDO YA FURAHA (Jumatatu na Jumamosi)

Tendo la kwanza; Malaika Gabrieli anampasha habari Maria kuwa atakuwa Mama wa Mungu. Tumwombe Mungu atujalie unyenyekevu.

Tendo la pili; Maria Mtakatifu anakwenda kumtembelea Elizabeti. Tumwombe Mungu atujalie mapendo ya jirani.

Tendo la tatu; Yesu anazaliwa Betlehemu. Tumwombe Mungu atujalie moyo wa ufukara

Tendo la nne; Yesu anatolewa hekaluni. Tumwombe Mungu atujalie usafi wa moyo.

Tendo la tano; Maria anamkuta Yesu hekaluni. Tumwombe Mungu atujalie kuwatii wakubwa wetu.

MATENDO YA UCHUNGU (Jumanne na Ijumaa)

Tendo la kwanza; Yesu anatoka jasho la damu kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie sikitiko la dhambi.

Tendo la pili; Yesu anapigwa kwa mijeledi kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kuacha dhambi za uchafu.

Tendo la tatu; Yesu anatiwa miiba kichwani kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kushinda kiburi.

Tendo la nne; Yesu anachukua Msalaba kwa ajili yetu. Tumwombe Mungu atujalie kuvumilia taabu.

Tendo la tano; Yesu anakufa Msalabani. Tumwombe Mungu atujalie kuwapenda Yesu na Maria.

MATENDO YA UTUKUFU (Jumatano na Jumapili)

Tendo la kwanza; Yesu anafufuka. Tumwombe Mungu atujalie kugeuka watakatifu.

Tendo la pili; Yesu anapaa mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kwenda mbinguni.

Tendo la tatu; Roho Mtakatifu anawashukia Mitume. Tumwombe Mungu atujalie bidii katika dini yetu.

Tendo la nne; Bikira Maria anapalizwa mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kufa vizuri.

Tendo la tano; Bikira Maria anawekwa Malkia mbinguni. Tumwombe Mungu atujalie kudumu katika njia njema.

MATENDO YA MWANGA (Alhamisi)

Tendo la kwanza; Yesu anabatizwa Mto Jordani. Tumwombe Mungu atujalie uaminifu kwa ahadi zetu za ubatizo.

Tendo la pili; Yesu anageuza maji kuwa divai huko Kana. Tumwombe Mungu atujalie kuukoleza ulimwengu kwa chachu ya enjili.

Tendo la tatu; Yesu anatangaza Ufalme wa Mungu. Tumwombe Mungu atujalie kupokea Ufalme wake kwa toba ya kweli.

Tendo la nne; Yesu anageuka sura. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kuung’arisha ulimwengu kwa uso wa Yesu.

Tendo la tano; Yesu anaweka Sakramenti ya Ekaristia. Tumwombe Mungu atujalie neema ya kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine.

LITANIA YA BIKIRA MARIA

  • Bwana utuhurumie
  • Bwana utuhurumie
  • Kristo utuhurumie
  • Bwana utuhurumie
  • Bwana utuhurumie
  • Kristo utusikie
  • Kristo utusikilize
  • Mungu Baba wa Mbinguni,…… Utuhurumie
  • Mungu Mwana Mkombozi wa dunia ……… Utuhurumie
  • Mungu Roho Mtakatifu …….. Utuhurumie
  • Utatu Mtakatifu Mungu Mmoja …….. Utuhurumie
  • Maria Mtakatifu ………. utuombee
  • Mzazi Mtakatifu wa Mungu …….. utuombee
  • Bikira Mtakatifu Mkuu wa Mabikira …….. utuombee
  • Mama wa Kristo ……… utuombee
  • Mama wa Neema ya Mungu ………….. utuombee
  • Mama Mtakatifu sana ……… utuombee
  • Mama mwenye usafi wa Moyo ……….. utuombee
  • Mama mwenye ubikira ……….. utuombee
  • Mama usiye na doa ……….. utuombee
  • Mama mpendelevu ………. utuombee
  • Mama mstajabivu ………. utuombee
  • Mama wa Muumba ………. utuombee
  • Mama wa Mkombozi ………….. utuombee
  • Mama wa Kanisa……….. utuombee
  • Bikira mwenye utaratibu ………….. utuombee
  • Bikira mwenye heshima ………….. utuombee
  • Bikira mwenye sifa ………….. utuombee
  • Bikira mwenye uwezo ………….. utuombee
  • Bikra mweye huruma ………….. utuombee
  • Bikra mwaminifu………….. utuombee
  • Kioo cha haki ………….. utuombee
  • Kikao cha hekima ………….. utuombee
  • Sababu ya furaha yetu ………….. utuombee
  • Chombo cha neema ………….. utuombee
  • Chombo cha kuheshimiwa ………….. utuombee
  • Chombo bora cha ibada ………….. utuombee
  • Waridi lenye fumbo ………….. utuombee
  • Mnara wa Daudi ………….. utuombee
  • Mnara wa pembe ………….. utuombee
  • Nyumba ya dhahabu ………….. utuombee
  • Sanduku la Agano ………….. utuombee
  • Mlango wa Mbingu ………….. utuombee
  • Nyota ya asubuhi ………….. utuombee
  • Afya ya wagonjwa ………….. utuombee
  • Kimbilio la wakosefu ………….. utuombee
  • Mtuliza wenye huzuni ………….. utuombee
  • Msaada wa waKristo ………….. utuombee
  • Malkia wa Malaika ………….. utuombee
  • Malkia wa Mababu ………….. utuombee
  • Malkia wa Manabii ………….. utuombee
  • Malkia wa Mitume ………….. utuombee
  • Malkia wa Mashahidi ………….. utuombee
  • Malkia wa Waungama dini ………….. utuombee
  • Malkia wa Mabikira ………….. utuombee
  • Malkia wa Watakatifu wote ………….. utuombee
  • Malkia uliyepalizwa Mbinguni ………….. utuombee
  • Malkia wa Rozari takatifu ………….. utuombee
  • Malkia wa amani ………….. utuombee

  • Mwanakodoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia,…………..Utusamehe ee Bwana.
  • Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia,…………..Utusikilize ee Bwana
  • Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia,…………..Utuhurumie.

  • Utuombee, Mzazi Mtakatifu wa Mungu,…………..Tujaliwe ahadi za Kristo.

Tuombe

Ee Bwana Mungu, utujalie sisi watumishi wako afya ya roho na mwili siku zote; na kwa maombezi matukufu ya Maria Mtakaatifu Bikira daima, tuopolewe na mashaka ya saa, tupate na furaha za milele. Kwa Kristo Bwana wetu, Amina.

Karibu Vitatabu vya Kikatoliki

SALA YA KUMWOMBA MT. YOSEFU MSAADA (SALA KUU KWA MTAKATIFU YOSEFU)

Ee Mt. Yosefu mwenye heri, tunakimbilia kwako katika masumbuko yetu, na kisha omba shime ya Mchumba wako Mtakatifu, tunaomba pia kwa matumaini usimamizi wako. Kwa ajili ya mapendo uliyompenda Bikira Mtakatifu Mzazi wa Mungu, na kwa ajili ya kumtunza Mtoto Yesu, twakuomba sana, utuangalie kwa wema sie tuliokuwa fungu lake Yesu Kristu, tukakombolewa kwa damu yake. Tusimamie katika masumbuko yetu kwa enzi na shime yako.

Ee Mlinzi amini wa jamaa takatifu, uwakinge watoto wateule wa Yesu Kristu.
Ee Baba uliyetupenda mno tuepushe na kilema chochote cha madanganyo na upotevu. Ee kinga yetu mwezaji, utusimamie huko juu mbinguni ulipo, tunaposhindana na wenye nguvu wakaao gizani. Kama vile siku za kale ukamwopoa Mtoto Yesu katika hatari ya kuuawa, na leo hivi likinge Kanisa Takatifu la Mungu katika mitego ya adui, na katika shida yote; mtunze daima kila mmoja wetu, tufwate mfano wako, ili tupate na msaada wako, kukaa na utakatifu maisha, kufa kifo chema, na kupata mbinguni makao ya raha milele.
Amina.

SALA YA KUOMBEA FAMILIA

Ewe Mungu Mwenyezi, sisi kama familia tunakushukuru kwa zawadi ya Mama Kanisa Katoliki ambaye siku zote hutupatia malezi bora kwa ajili ya wokovu wetu. Kanisa halichoki kutuhimiza tutafakari na kuishi utakatifu wa familia ya Nazareti ya Yesu, Maria na Yosefu. Familia hii iliishi upendo uliojengwa kwa fadhila za imani, uaminifu, utii, uvumilivu na upole hata wakawa watakatifu. Tunapoadhimisha mwaka wa Familia, tunaiweka mbele yetu familia ya Nazareti iwe dira, baraka na mfano kwa familia zetu.

Tunakushukuru Baba kwa ajili ya familia zote zinazojitahidi kuishi fadhila hizo za Familia takatifu na tunakuomba uzidi kuwaimarisha wanandoa ili tupate kwao mifano mingi na bora ya kuigwa. Ee Bwana, tunaomba Roho Mtakatifu atuangazie tuweze: kutambua familia kuwa Kanisa la nyumbani na shule ya imani na upendo; kuimarisha familia kwa sala, sakramenti na tunu za kiinjili na kushirikiana kwa heshima katika familia kwa usitawi wa roho na wa mwili kwa wanafamilia wote.

Tunaziombea familia zetu na Jumuiya Ndogondogo za Kikristo ziwe bustani bora na salama za kuchipusha na kulea miito mitakatifu ya Ndoa, Utawa na Upadre. Tunawaombea vijana na watoto wetu Uchaji wa Mungu ili wawe na bidii ya kujitunza kwa kushika amri za Mungu na kuishi fadhila za kiinjili, wawe na roho ya kimisionari yaani walipende Kanisa na kuwa na moyo wa kueneza ufalme wako kwa matendo ya imani. Baba wa huruma, tunakukabidhi familia zenye misukosuko ya mafarakano, ulevi, ubinafsi, uregevu-dini, uvivu, ushirikina, hofu, magonjwa sugu na mengineyo yenye kuleta huzuni; kwa hisani yako uwape neema, mwanga na nguvu za kuanza maisha mapya yenye amani, waweze kufurahia upatanisho na uponyi wa pendo lako la kibaba kati yao.

Tunaomba toba na msamaha kwa ukatili, manyanyaso na hata mauaji katika familia zetu na uwaponye wote waliojeruhiwa kwa maneno, matendo na makwazo ya aina yeyote. Aidha tunakuomba uwe kitulizo na faraja kwa wagonjwa na wazee, pia tegemeo la yatima na wajane. Wenye matatizo ya kiafya au ya kijamii wasikate tamaa bali waunganishe hali zao na msalaba wa Mwanao na kukutumaini wewe Mweza yote. Jamii iwajibike nao kwa kuzijali haki zao na kuwapa misaada wanayohitaji.

Tunakuomba ubariki miradi na kazi zetu ili familia zipate usitawi na maendeleo; na utujalie hekima ya kukushukuru kwa maisha ya haki, amani na ukarimu na mwisho tukaimbe sifa zako pamoja na familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefuna jeshi lote la mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

Baba yetu… …..Salamu Maria….…Atukuzwe Baba………

Malkia wa Mbingu

Malkia wa mbingu, furahi, aleluya. Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya. Amefufuka alivyosema, Aleluya. Utuombee kwa Mungu, Aleluya. Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Alaluya. Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya. Tuombe. Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu, Mwanao: fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.

LITANIA YA KUWAOMBEA MAPADRE WOTE II

Kwa ajili ya Baba Mtakatifu wetu ..(N); Bwana, umpe moyo wako wa uchungaji mwema
Kwa ajili ya makardinali na maaskofu wakuu; Uwape moyo wa kichungaji ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wa majimbo; Uwajaze na Roho wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre watawa; Wakamilishe katika wito wao ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre walioko hatarini; Uwaokoe ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wenye udhaifu; Uwatie nguvu ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wenye hofu; Uwape amani ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre waliokata tamaa; Uwavuvie upya ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wakaao upweke; Uwasindikize ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wamisionari; Uwalinde ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wanaohubiri; Uwaangazie ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre na watawa waliokufa; Uwafikishe kwenye utukufu wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie hekima na ufahamu wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; Uwajalie elimu na shauri lako
Kwa ajili ya mapadre wako; wajalie wakuheshimu na wakuogope
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie subira na upendo
Kwa ajili ya mapadre wote; wajalie utii na upole
Kwa ajili ya mapadre wote; uwajalie hamu kuu ya kuokoa roho za watu
Kwa ajili ya mapadre wote; wape fadhila za imani, matumaini na mapendo
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie upendo mkuu kwa Ekaristi
Tunakuomba uwajalie mapadre wote; Waheshimu uhai na hadhi ya mtu ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote nguvu na bidii katika kazi zao ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote amani katika mahangaiko yao ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote upendo mkuu kwa Utatu Mtakatifu ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote upendo mkuu kwa Bikira Maria ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe mwanga wa Kristo ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wawe chumvi kwa ulimwengu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wajizoeze kujitoa sadaka na kujinyima ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wawe watakatifu kimwili, kiakili na kiroho ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe watu wa sala ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe kioo cha imani kwako ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wajali sana wongofu wetu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe waaminifu kwa wito wao wa kikuhani ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, ili mikono yao ibariki na kuponya ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawake moto wa mapendo yako ee Bwana
Uwajalie mapadre wote hatua zao zote ziwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wajazwe na Roho Mtakatifu na uwajalie karama zake kwa wingi ee Bwana.

Tuombe.
Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, usikie sala tunazokutolea kwa ajili ya mapadre wetu. Uwajalie wafahamu waziwazi kazi uliyowaitia kuifanya, uwape neema zote wanazohitaji ili waitikie wito wako kwa ushujaa, kwa upendo, na majitoleo yenye udumifu katika mapenzi yako matakatifu. Amina.

Sala ya Saa Tisa

✝⌚✝

Sala ya saa tisa🙏🏾

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. A mina

Yesu, ulikufa, lakini chanzo cha uhai kilitoka kwa ajili ya watu, na bahari ya huruma ilifunguka kwa ajili ya ulimwengu mzima. Ee chemchemi ya Uhai, huruma ya Mungu isiyo na mwisho, ikafunika ulimwengu mzima na ukajimwaga mwenyewe juu yetu.

❣✝❣

✝Ee Damu na Maji, yaliyotoka moyoni mwa Yesu kama chemchemi ya Huruma kwetu. Nakutumainia.

(Mara tatu)

🛐❣🛐

SALA YA MAJITOLEO KWA MAMA WA HUZUNI

Mama Mtakatifu, Mama wa Mungu na Malkia wa Mashahidi, leo nakuchagua Wewe uwe mfano wangu, mkingaji na mteteaji wangu. Naweka roho fukara katika moyo wako uliotobolewa na panga nyingi za mateso. Unipokee mimi niwe mtumishi wako wa pekee na mshiriki wa mateso yako. Nijalie nguvu niwe daima karibu na msalaba ule alikosulibiwa Yesu. Nakutolea nafsi yangu na mali yangu yote. Pokea kila tendo langu jema ukalisindikize kwa Mwanao, Mama, nifanye nistahili kuitwa mtumishi wa Maria, Simama karibu yangu katika matendo yangu yote ili yafanwe kwa sifa ya Mungu. Ulivyosimama karibu kabisa ya Mwanao alipokufa msalabani uwe karibu nami saa ya kufa kwangu. Nijalie niweze kutaja jina lako na la Mwana wako nikisema: “Yesu, Maria na Yosef mnisaidie saa ya kufa kwangu. Yesu, maria na Yosef, naomba nife kwa amani kati yenu!” . Amina.

ROZARI YA MATESO SABA YA BIKIRA MARIA

Tumia Rozari ya Mateso Saba ya Bikira Maria iliyo na mafungu 7 yaani mateso 7 yenye Salamu Maria saba kwa kila teso.

TESO LA KWANZA

Mzee Simeoni aliagua kuwa Moyo wa Mama Maria utachomwa kwa upanga.
Tuombe neema ya kuvumilia mateso.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA PILI

Maria na Yosefu walikimbilia Misri usiku ili kumficha Mtoto Yesu asiuawe na Herodi.
Tuombe neema ili miili yetu iwe kimbilio lake Yesu.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA TATU

Mama Maria aliona uchungu sana Mtoto Yesu alipopotea kwa siku tatu.
Tuombe neema ya kudumu na Yesu mioyoni mwetu.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA NNE

Mama Maria aliona uchungu sana alipokutana na Mwanae Yesu katika njia ya Msalaba.
Tuombe neema ya kudumu na Yesu siku zote.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA TANO

Mama Maria aliona uchungu sana alipomwona Mwanae Yesu akisulibiwa Msalabani.
Tuombe neema ya kufa mikononi mwa Yesu na Maria.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA SITA

Mama Maria aliona uchungu sana alipopakata maiti ya Mwanae Yesu baada ya kushushwa Msalabani.
Tuombe neema ya kutotenda dhambi.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

TESO LA SABA

Mama Maria aliona uchungu sana aliporudi nyumbani baada ya kumzika Mwanae Yesu
Tuombe neema ya kitulizo kwa Mama Maria.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.

ROSARI YA BIKIRA MARIA MAMA WA MSAADA WA DAIMA

Namna ya kusali Rozari kwa Bikira Maria Mama wa Msaada wa Daima

(Tumia rosari ya kawaida)

Mwanzo, kwenye Msalaba:

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.

Kwenye chembe ndogo za awali:

K: Ee Mungu utuelekezee msaada W: Ee Bwana utusaidie hima
W: Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Kama mwanzo na sasa na siku zote na milele. Amina.

Maria ametusaidia,
Maria anataka kutusaidia,
Maria anaweza kutusaidia,
Maria atatusaidia.

KATIKA KILA FUNGU SALI SALA ZIFUATAZO:

Kwenye chembe kubwa:

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Kama mwanzo na sasa, na siku zote, na milele. Amina.

Maria ametusaidia,
Maria anataka kutusaidia,
Maria anaweza kutusaidia,
Maria atatusaidia.

Ee Maria Mama wa Msaada wa daima
Sikiliza maombi ya roho zetu
Unaweza kutusaidia katika mahitaji yetu
Ee Maria kwa matumaini twakuita wewe.

Kwenye chembe ndogo:

Kama unasali mwenyewe: “Ee Maria, utusaidie! (mara kumi)
Kama mnasali zaidi ya mmoja kwa pamoja: K; Ee Maria, W: Utusaidie. (mara kumi)

MWISHO SALI SALA ZIFUATAZO:

Salamu Maria

Salamu Maria, umejaa neema, Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu Mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa, na saa ya kufa kwetu. Amina. (mara tatu)

Tunaukimbilia

Tunaukimbilia ulinzi wako, ee Mzazi Mtakatifu wa Mungu, usitunyime tukiomba katika shida zetu, utuokoe siku zote, kila tuingiapo hatarini, ee Bikira Mtukufu na mwenye baraka,. Amina.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About