Sala za Katoliki: Sala Muhimu Kwa Mkristu Mkatoliki

SALA YA KUWAOMBEA MAPADRE

Ee Bwana Yesu Kristo. Mkombozi wetu, kwa mapendo na tamaa yako ya kutaka kulinda vema Kanisa lako, ukachagua Mapadri wawe Wachungaji na Viongozi wa roho za watu. Nakuomba sana; ubariki nia na bidii inayowapasa Mapadri wote katika kazi zao. Uwaongezee Utakatifu.

Uwatie moyo mzuri wenye mapendo makubwa kwako na roho za watu. Hivyo wakiisha kupata wenyewe Utakatifu, waweze kuwaongoza vizuri watu walio chini ya ulinzi wao, katika njia ya Utakatifu na furaha ya milele. Uwajalie neema zote za hali ya Upadri. Uwajalie ili waonyeshe kila siku ya maisha yao mfano wa kila fadhila ya mapendo na ya uaminifu katika Kanisa, kwa Baba Mtakatifu na kwa Maaskofu.

Yesu mpendelevu, uangalie kwa mapendo kazi na mateso ya Mapadri wako; ubariki na ustawishe mafundisho yao; wanapowafundisha watoto, wanapowahubiria watu, wanapowatuliza wakosefu watubu na wanapowasaidia wagonjwa na wale wanaokaribia mauti, Ee Yesu uwe pamoja nao. Uwakinge na hatari zote za roho na za mwili.

Mwokozi Yesu, ulijalie Kanisa liwe na Mapadri wengi walio Watakatifu. Uwajalie watoto na vijana wengi wasikie wito wa Upadri, uwatie furaha na Utakatifu na roho za Mapadri waliokufa uzijalie punziko la amani.

Kwa mimi mwenyewe Ee Yesu mpendelevu, naomba unijalie roho ya imani na utii mnyenyekevu ili niwaheshimu Mapadri kama Mawakili wa Mungu. Niwatii katika njia zote za wokovu wa roho yangu. Amina.

SALA YA MTU ALIYEKABILIWA NA MATATIZO MBALIMBALI

Ewe Mtakatifu Yuda Tadei,/ mtume mtukufu na shahidi wa Kristo,/ umesifika pote kwa wepesi wako wa kutoa misaada/ kwa wanaokukimbilia katika matatizo yao mazito./ Pia ni mwombezi wa waliopondeka moyo./

Mimi ni mmoja wa hao./ Nakujia na moyo uliojaa shida na matatizo./ Nakusihi kwa moyo wote/ unisaidie kwa maombezi yako yenye nguvu/ kufikia utatuzi unaofaa kadiri ya mapenzi ya Mungu./ Maisha yangu yamejaa misalaba,/ siku kwa siku matatizo hayapungui./ Moyo wangu umekuwa bahari ya siki chungu sana./ Mapito yangu nayaona yamejaa miiba mikali./ Roho yangu imezama katika dimbwi la machozi na kite./ Nafsi yangu imezingirwa na giza nene./ Ghasia na kukatishwa tamaa ya kuishi/ hunyemelea roho yangu./ Maongozi ya Mungu na imani naviona vinanitoka kidogo kwa kidogo./

Nikielemewa na mawazo kama hayo/ najikuta sina nguvu za kuishi,/ na maisha kwangu ni msalaba mzito/ ninaouogopa hata kuunyakua./ Wewe unaweza kabisa kunitoa katika balaa hili./ Sitaacha kukusihi/ hadi hapo utakaponisaidia/ au kunijulisha mapenzi ya Mungu kwangu./ Natangulia kutoa shukrani kwa jibu liwalo lote.

SALA KWA BIKIRA MARIA KATIKA UKIWA WAKE

Nakusikitikia sana Mama Mtakatifu Maria kwa sababu ya ukiwa wako mkuu. Uchungu wako ulikuwa mkubwa sana ulipotazama mateso na kifo cha Mwana wako mpenzi. Muda ule uliweza kutuliz kidogo kwa sababu ya kumwona angali hai. Lakini je, baada ya kufa na kumzika? Sasa wewe ni mkiwa mkubwa mno! Uh, ukiwa wa pekee, uniombee mimi ninayempoteza mara nyingi kwa dhambi zangu. Unijalie nisimpoteze tena Yesu wangu kwa ubaya wa uvivu wangu, bali nimtumikie kiaminifu duniani hapa ili nimwone na kumfurahia milele mbinguni. Amina.

ROSARI YA BIKIRA MARIA MAMA WA MSAADA WA DAIMA

Namna ya kusali Rozari kwa Bikira Maria Mama wa Msaada wa Daima

(Tumia rosari ya kawaida)

Mwanzo, kwenye Msalaba:

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.

Kwenye chembe ndogo za awali:

K: Ee Mungu utuelekezee msaada W: Ee Bwana utusaidie hima
W: Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Kama mwanzo na sasa na siku zote na milele. Amina.

Maria ametusaidia,
Maria anataka kutusaidia,
Maria anaweza kutusaidia,
Maria atatusaidia.

KATIKA KILA FUNGU SALI SALA ZIFUATAZO:

Kwenye chembe kubwa:

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Kama mwanzo na sasa, na siku zote, na milele. Amina.

Maria ametusaidia,
Maria anataka kutusaidia,
Maria anaweza kutusaidia,
Maria atatusaidia.

Ee Maria Mama wa Msaada wa daima
Sikiliza maombi ya roho zetu
Unaweza kutusaidia katika mahitaji yetu
Ee Maria kwa matumaini twakuita wewe.

Kwenye chembe ndogo:

Kama unasali mwenyewe: โ€œEe Maria, utusaidie! (mara kumi)
Kama mnasali zaidi ya mmoja kwa pamoja: K; Ee Maria, W: Utusaidie. (mara kumi)

MWISHO SALI SALA ZIFUATAZO:

Salamu Maria

Salamu Maria, umejaa neema, Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu Mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa, na saa ya kufa kwetu. Amina. (mara tatu)

Tunaukimbilia

Tunaukimbilia ulinzi wako, ee Mzazi Mtakatifu wa Mungu, usitunyime tukiomba katika shida zetu, utuokoe siku zote, kila tuingiapo hatarini, ee Bikira Mtukufu na mwenye baraka,. Amina.

LITANIA YA KUWAOMBEA MAPADRE WOTE II

Kwa ajili ya Baba Mtakatifu wetu ..(N); Bwana, umpe moyo wako wa uchungaji mwema
Kwa ajili ya makardinali na maaskofu wakuu; Uwape moyo wa kichungaji ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wa majimbo; Uwajaze na Roho wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre watawa; Wakamilishe katika wito wao ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre walioko hatarini; Uwaokoe ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wenye udhaifu; Uwatie nguvu ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wenye hofu; Uwape amani ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre waliokata tamaa; Uwavuvie upya ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wakaao upweke; Uwasindikize ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wamisionari; Uwalinde ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wanaohubiri; Uwaangazie ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre na watawa waliokufa; Uwafikishe kwenye utukufu wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie hekima na ufahamu wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; Uwajalie elimu na shauri lako
Kwa ajili ya mapadre wako; wajalie wakuheshimu na wakuogope
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie subira na upendo
Kwa ajili ya mapadre wote; wajalie utii na upole
Kwa ajili ya mapadre wote; uwajalie hamu kuu ya kuokoa roho za watu
Kwa ajili ya mapadre wote; wape fadhila za imani, matumaini na mapendo
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie upendo mkuu kwa Ekaristi
Tunakuomba uwajalie mapadre wote; Waheshimu uhai na hadhi ya mtu ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote nguvu na bidii katika kazi zao ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote amani katika mahangaiko yao ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote upendo mkuu kwa Utatu Mtakatifu ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote upendo mkuu kwa Bikira Maria ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe mwanga wa Kristo ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wawe chumvi kwa ulimwengu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wajizoeze kujitoa sadaka na kujinyima ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wawe watakatifu kimwili, kiakili na kiroho ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe watu wa sala ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe kioo cha imani kwako ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wajali sana wongofu wetu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe waaminifu kwa wito wao wa kikuhani ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, ili mikono yao ibariki na kuponya ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawake moto wa mapendo yako ee Bwana
Uwajalie mapadre wote hatua zao zote ziwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wajazwe na Roho Mtakatifu na uwajalie karama zake kwa wingi ee Bwana.

Tuombe.
Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, usikie sala tunazokutolea kwa ajili ya mapadre wetu. Uwajalie wafahamu waziwazi kazi uliyowaitia kuifanya, uwape neema zote wanazohitaji ili waitikie wito wako kwa ushujaa, kwa upendo, na majitoleo yenye udumifu katika mapenzi yako matakatifu. Amina.

SALA KWA MAMA WA UCHUNGU KUOMBA NEEMA YA PEKEE

Ee Mama mbarikiwa na Bikira mwenye uchungu, Malkia wa Mashahidi, uliyesimama chini ya msalaba na uliyemtazama Mwana wako akifa, unitazame kwa huruma ya kimama ninayekusikitikia. Kwa sababu ya upanga uliochoma moyo wako, kwa mateso ya maisha yako nakuomba uniangalie kwa wema ukasikilize maombi yangu. Nakuomba, ee Mama, uniombee daima kwa Mwana wako, najua hawezi kukuvyima wewe kitu chochote. Basi, ufanye, Moyo wa Mwanao ukubali kunijalia ombi langu hili โ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆ(taja ombi lako).
Maana nitamkimbilia nani katika mahitaji na misiba yangu isipokuwa kwako, ee Mama wa huruma? Wewe hasa unaweza kutusaidia sisi tulio bado katika bonde la machozi kwa sababu ulishiriki mateso ya Mwanao kutukomboa. Umtolee Yesu tone moja la Damu yake takatifu. Umkumbushe ya kuwa wewe ni matumaini, furaha na maisha yetu ukanipatie jambo ninalokuomba kwa Yesu Kristo, bwana wetu. Amina.

SALA YA UHAI KWA MT. YOSEFU

(Sala hii inafaa sana kwa ajili ya kutetea uhai wa watoto wachanga wakiwa tumboni mwa mama zao, dhidi ya utoaji mimba au hatari nyingine dhidi ya uhai wa binadamu)

Ee Mt. Yosefu, wewe ni Mchumba safi na Mpenzi wa Bikira Maria, u Baba Mlishi wa Yesu, mlinzi na mtunzaji wa Familia Takatifu, na wa familia zote. Tuna imani kabisa katika uangalizi wako uliojaa upendo, juu ya uhai mpya, na uaminifu wako kwa familia.

Tunaweka jitihada zetu chini ya ulinzi wa sala zako. Utusaidie daima katika kutetea zawadi ya uhai wa binadamu, ili ukue hadi uzima wa milele ulioahidiwa na kujaliwa kwetu na Mwanao, Ndugu yetu, Yesu Kristu.
Amina.

SALA KWA MT. YOSEFU KUOMBA KUFAHAMU WITO WAKO

Ee uliye Mkuu, Mt. Yosefu, uliyatii kabisa maongozi ya Roho Mt. Unijalie neema ya kufahamu aina ya maisha ambayo Mungu anapenda mimi niishi. Usiniache nidanganyike katika jambo muhimu kama hili, ambalo furaha yangu hapa duniani inalitegemea, na hata pia wokovu wa roho yangu.

Unijalie, nikiangazwa na matakwa matakatifu na nikiwa mwaminifu katika kuyatimiza, nikumbatie aina ya maisha ambayo Mungu ameniandalia na yatakayoniongoza kwenye furaha ya milele.
Amina.

LITANIA YA MOYO MTAKATIFU WA YESU

Bwana utuhurumie Bwana utuhurumie
Kristo utuhurumie Kristo utuhurumie
Bwana utuhurumie Bwana utuhurumie
Kristo utusikie Kristo utusikilize
Baba wa mbinguni Mungu Utuhurumie
Mwana, Mkombozi wa dunia Mungu Utuhurumie
Roho Mtakatifu Mungu Utuhurumie
Utatu Mtakatifu Mungu mmoja Utuhurumie
Moyo wa Yesu Mwana wa Baba wa Milele Utuhurumie
Moyo wa Yesu uliotungwa na Roho Mtakatifu mwilini mwa Mama Bikira Maria Utuhurumie
Moyo wa Yesu ulioungana na Neno wa Mungu Utuhurumie
Moyo wa Yesu ulio na utukufu pasipo mfano Utuhurumie
Moyo wa Yesu, hekalu takatifu la Mungu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, hema la Yule aliye juu Utuhurumie
Moyo wa Yesu tanuru lenye kuwaka mapendo Utuhurumie
Moyo wa Yesu, nyumba ya Mungu na mlango wa Mbingu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, tanuru yenye kuwaka mapendo Utuhurumie
Moyo wa Yesu, chombo cha haki na upendo Utuhurumie
Moyo wa Yesu, unaojaa upendo na wema Utuhurumie
Moyo wa Yesu, kilindi cha fadhila zote Utuhurumie
Moyo wa Yesu, unaostahili sifa zote Utuhurumie
Moyo wa Yesu, unaotawala mioyo yote Utuhurumie
Moyo wa Yesu, zinamokaa hazina za hekima na elimu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, uliopendelewa na Mungu Baba Utuhurumie
Moyo wa Yesu, uliotuenezea maziada yake Utuhurumie
Moyo wa Yesu, mtamaniwa wa vilima vya milele Utuhurumie
Moyo wa Yesu, wenye uvumilivu na huruma nyingi Utuhurumie
Moyo wa Yesu, tajiri kwa wote wenye kukuomba Utuhurumie
Moyo wa Yesu, chemchemi ya uzima na utakatifu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, malipo kwa dhambi zetu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, ulioshibishwa matusi Utuhurumie
Moyo wa Yesu, uliovunjika kwa sababu ya ubaya wetu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, uliotii mpaka kufa Utuhurumie
Moyo wa Yesu, uliochomwa kwa mkuki Utuhurumie
Moyo wa Yesu, chemchemi ya faraja zote Utuhurumie
Moyo wa Yesu, uzima na ufufuo wetu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, amani na upatanisho wetu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, sadaka ya wakosefu Utuhurumie
Moyo wa Yesu, unamokaa wokovu wao wenye kukutumaini Utuhurumie
Moyo wa Yesu, matumaini yao wenye kuzimia kwako Utuhurumie
Moyo wa Yesu, sababu ya furaha ya watakatifu wote Utuhurumie
Mwanakondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za dunia Utusamehe Bwana
Mwanakondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za dunia Utusikilize Bwana
Mwanakondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za dunia Utuhurumie

Kiongozi: Yesu mwenye Moyo mpole na mnyenyekevu,
Wote: Ufanye mioyo yetu ifanane na Moyo wako

TUOMBE: (W) Ee Mungu Mwenyezi milele, uuangalie Moyo wa mwanao mpendelevu, pia na heshima na malipo aliyokutolea kwa ajili ya wenye dhambi, uridhike, uwaondolee wenye kuomba toba kwako kwa njia ya huyo Mwanao Yesu Kristo anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu milele. Amina.

KUJIWEKA CHINI YA ULINZI WA MT. YOSEFU

Ee Mt. Yosefu, Baba Mlishi wa Mwokozi wangu, na mchumba safi wa Mama wa Mungu, leo ninakuchagua wewe, kama mwombezi wangu kwa Mungu Mwenyezi, na pia kama mfano wangu, na mlinzi wangu, na baba yangu, katika bonde hili la ugenini.

Ee Mt. Yosefu, ambaye Bwana alikufanya mlinzi wa Familia yake, ninakuomba uwe mlinzi wangu mwema katika mambo yangu yote. Uniwashie moyoni mwangu moto wa mapendo makuu kwa Yesu, na uniwezeshe kumtumikia kwa bidii na kwa uaminifu kwa mfano wako. Nisaidie katika udhaifu wangu katika kumheshimu Mama Maria kama Mwombezi wangu.

Daima uwe kiongozi wangu katika njia ya fadhila na ibada, na unijalie, baada ya kukufuasa kwa uaminifu katika njia ya haki, nipate ulinzi wako wenye nguvu katika saa ya kufa kwangu.
Amina

Sala za kuheshimu Damu Takatifu ya Yesu

Tusali kila siku sala hizi, angalau kwa mwezi wa saba (Julai) kila mwaka, mwezi wa kuheshimu Damu Takatifu ya Mkombozi wetu.

Yesu alimwahidi Mt. Brigita wa Sweden kwamba wale watakaosali Baba Yetu 7 na Salamu Maria 7 kwa miaka 12 kwa kuheshimu damu yake takatifu na kutafakari juu ya Kutahiriwa kwake, jasho lake la damu, kupigwa kwake mijeledi, kuvikwa taji la miiba, kuchukua kwake Msalaba, kusuliwa kwake na kuchomwa ubavuni; watapata neema 5 zifuatazo: (1) Hawataingia toharani, (2) Yesu atawapa cheo cha mashahidi waliomwaga damu yao kwa ajili ya imani, (3) Yesu atawadumisha jamaa zake watatu katika hali ya neema, (4) Roho za jamaa zake zitakingwa na Jehanam mpaka kizazi cha nne, (5) Mwezi kabla ya kufa, Yesu atawajulisha. Wakifa kabla ya kutimiza miaka ile, watahesabiwa wamemaliza.

Ee Yesu, sasa ninataka kusali Baba yetu mara saba nikiungana na ule upendo ambao kwao uliitakasa sala hii katika Moyo wako. Uichukue kutoka mdomoni mwangu hadi moyoni mwako. Uiboreshe na kuikamilisha hivyo kwamba iupatie heshima na furaha kwa Utatu Mtakatifu kama vile Wewe ulivyoupatia kupitia sala hii wakati ulipokuwa bado hapa duniani. Utukuzwe ee Yesu, itukuzwe Damu Yako Takatifu sana uliyoimwaga kutoka katika Majeraha Yako Matakatifu.

1. Yesu anatahiriwa.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu โ€ฆ. Salamu Maria โ€ฆ. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea Majeraha ya kwanza, maumivu ya kwanza na Damu ya kwanza aliyomwaga Mwanao mpenzi, Bwana wetu Yesu Kristu, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu na dhambi za dunia nzima, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi ya kwanza ya mauti, hasa kati ya ndugu zangu.

2. Yesu anatokwa Jasho la Damu bustanini Gethsemane.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu โ€ฆ. Salamu Maria โ€ฆ. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea mateso na mahangaiko makali sana ya moyoni, ya Bwana wetu Yesu Kristu katika mlima wa mizeituni na kila tone la jasho lake la damu, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu za kimoyomoyo, na dhambi za namna hiyo zinazotendwa na dunia nzima, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi za moyoni na kwa ajili ya kueneza upendo wa kiMungu na wa kindugu.

3. Yesu anapigwa mijeledi.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu โ€ฆ. Salamu Maria โ€ฆ. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea majeraha elfu elfu aliyopata, maumivu makali sana na Damu Takatifu sana aliyomwaga, alipopigwa mijeledi, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu za tamaa ya mwili, kwa malipizi ya dhambi za tamaa ya mwili za wanadamu wote, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi za tamaa ya mwili, na kwa kulinda usafi wa moyo, hasa kati ya ndugu zangu.

4. Yesu anavikwa taji la miiba.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu โ€ฆ. Salamu Maria โ€ฆ. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea majeraha, maumivu na Damu Takatifu kutoka katika Kichwa Kitakatifu cha Yesu wakati alipovikwa taji la miiba, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu za rohoni, kwa malipizi ya dhambi za rohoni za wanadamu wote, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi za rohoni, na kwa ajili ya kueneza Ufalme wa Kristu hapa duniani.

5. Yesu anachukua Msalaba.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu โ€ฆ. Salamu Maria โ€ฆ. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea mateso ya njia ya Msalaba, hasa donda lake la begani na Damu Takatifu iliyomwagika, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu za ukaidi dhidi ya msalaba, na dhambi za ukaidi dhidi ya msalaba za wanadamu wote, malalamiko yote dhidi ya mipango yako mitakatifu na dhambi zote za ulimi, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya dhambi za ulimi na kwa ajili ya upendo wa kweli kwa Msalaba.

6. Yesu anasulibiwa.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu โ€ฆ. Salamu Maria โ€ฆ. Baba wa Milele, kupitia mikono safi ya Maria na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutolea Mwanao Msalabani, kupigwa kwake misumari na kuinuliwa kwake, madonda yake mikononi na miguuni na mifereji mitatu ya Damu yake Takatifu iliyomwagika kutoka katika majeraha haya, mateso yake makali sana ya mwili na roho, kifo chake kitakatifu, ukumbusho usio wa kumwaga wa damu wa kifo hiki katika Misa zote Takatifu ulimwenguni, kwa ajili ya majeraha yote yanayosababishwa na ukaidi wa nadhiri na kanuni katika madaraja matakatifu, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zangu zote na za ulimwenguni mzima, kwa ajili ya wagonjwa na wanaokufa, kwa ajili ya mapadre watakatifu na walei, kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu za kukarabati familia za kikristu, kwa ajili ya kuimarika kwa imani ya kikristu ulimwenguni, kwa ajili ya nchi yetu na muungano kati ya mataifa ndani ya Kristu na Kanisa lake, na kwa ajili ya wokovu wa dunia nzima.

7. Yesu anachomwa kwa mkuki moyoni.

Tafakari fupi (kimya kidogo). Baba Yetu โ€ฆ. Salamu Maria โ€ฆ. Baba wa Milele, ukubali kupokea, kwa ajili ya mahitaji ya Kanisa Takatifu na kwa ajili ya malipizi ya dhambi za wanadamu wote, Damu na Maji Takatifu vilivyomwagika kutoka jeraha la Moyo Mtakatifu wa Yesu. Utuhurumie. Damu Takatifu ya Yesu, tone lile la mwisho lililomwagika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu, unioshe mimi na wengine wote dhambi zetu zote! Ee Maji kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, unioshe na adhabu zote za dhambi zangu na uizime miale ya moto wa toharani kwa ajili yangu na kwa ajili ya roho zote zilizomo toharani. Amina.

Katika mwaka wa Kanisa wa kiliturjia, mwezi Julai ni wa kuiheshimu Damu Takatifu ya Yesu.

Shopping Cart
๐Ÿ  Home ๐Ÿ“– Reading ๐Ÿ–ผ๏ธ Gallery ๐Ÿ’ฌ AI Chat ๐Ÿ“˜ About