Karibu AckySHINE

Karibu AckySHINE

Chagua Unachotaka Kusoma Hapa

BURUDANI MAKALA DINI VITABU

Unahakikishiwa kusoma kitu kipya kizuri kila saa unapotembelea ukurasa huu.

Mapishi ya tambi za kukaanga

Kupika tambi ni kama ifuatavyo

VIAMBA UPISHI

Tambi pakti moja

Sukari ¾ kikombe cha chai

Mafuta ½ kikombe cha chai

Iliki kiasi

Maji 3 Vikombe vya chai

Vanilla / Arki rose 1-2 Tone

Zabibu Kiasi (Ukipenda)

JINSI YA KUPIKA TAMBI ZAKO

1. Zichambue tambi ziwe moja moja.

2. Mimina mafuta kwenye sufuria yakisha pata moto mimina
tambi,zigeuzegeuze mpaka zibadilike rangi na kuwa brown.

3. Punguza mafuta kwa kuyachuja na zirudishe jikoni.

4. Nyunyizia iliki zilizosagwa koroga kidogo na mimina maji na tia arki
na acha zichemke mpaka maji yakikaribia kukauka mimina sukari
koroga kidogo na punguza moto.
5. Kisha tia zabibu ukipenda, zifunike ili zikaukie vizuri.

6. Zikishakauka pakua kwenye sahani tayari kwa kuliwa

Kidokezi: Itategemea na aina za Tambi unazopika kwa kukisia maji, kama utaona hazijaiva unaweza kuongeza maji kidogo.

Mapishi ya Kidheri – Makande

Mahitaji

Nyama (kata vipande vidogodogo) – ½ kilo

Maharage – 3 vikombe

Mahindi – 2 vikombe

Kitunguu – 1

Nyanya – 2

Kabichi lililokatwa – 2 vikombe

Kitunguu saumu(thomu/galic) – 1 kijiko cha chai

Vidonge vya supu – 2

Chumvi – kiasi

Mafuta -1au 2 vijiko vya chakula

Namna Yakutayarisha

Chemsha mahindi mpaka yawive na maji yakauke kiasi.
Chemsha maharage pembeni nayo mpaka yawive na maji yakaukie kiasi.
Tia mafuta kwenye sufuria anza kukaanga vitunguu , thomu na vidonge vya supu koroga kiasi.
Kisha mimina nyama iliyokatwa vipande acha ikaangike kidogo na chumvi.
Nyama ikishakaangika tia nyanya funika kwa moto mdogo mpaka nyama iwive.
Kisha mimina mahindi na maharage yaliyochemshwa na maji yake kiasi koroga mpaka ichanganyike na mwisho mimina kabichi funikia mpaka kabichi iwive onja chumvi kama imekolea
Halafu malizia kukoroga mpaka ichanganyike na ikaukie kisha pakua kwenye sahani tayari kwa kuliwa.

Kwa ushauri huu jitambue upate mafanikio

Ukiona unalala masaa 9 wakati Donald Trump analala manne tu. Afu unaamka huna nauli na bado kesho unalala masaa manane tena.. Ujue unashabikia mafanikio.

Ukiona Bill Gates anasoma kitabu kimoja kwa wiki. Na wewe unasoma kimoja kwa miezi sita ujue nod maana kuna tofauti ya Bill Gates na wewe.

Ukiona unasema utakuwa successful siku moja afu huna DAILY GOALS. Yani hujui ukiamka ufanye nini na jioni utapimaje kama kweli umekifanya ujue hujaelewa vizuri maana ya kuwa successful.

Hard Work beats talent.

You must sleep less and work harder until you get what you want.

Ijue Ishara ya Msalaba

Ishara ya Msalaba ni tendo la mtu kugusa paji la uso, kifua na mabega kwa kutumia mkono wa kulia na kutamka ‘Kwa Jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu, Amina’.
Kugusa paji la uso tuna maana kukubali kwa akili, kugusa kifua maana yake ni kupokea na kuupenda msalaba moyoni na kugusa Mabega maana yake ni kuwa tayari kuubeba Msalaba kwa nguvu zetu zote.
Tunafanya njia ya Msalaba kwa nia ya kumkiri Mungu Mmoja katika Nafsi tatu. Pia Msalaba ni Ishara ya Ukombozi wetu.
Ishara ya Msalaba Juu ya Paji la uso, mdomo na kifua kabla ya injili:
Hii ina maana kwamba Niko tayari kulifahamu Neno la Mungu Kwa Akili yangu,
Nitalitangaza kishujaa kwa midomo yangu, na Nitalipenda na kulishika kwa Moyo wangu Wote.

Mambo muhimu kujua Kuhusu Uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke

Naamini umeshawahi kusikia kuhusu changamoto ya uvimbe kwenye kizazi kwa Wanawake yaani Fibroids. Uchunguzi unaonesha kuwa kati ya asilimia 30 mpaka 70 ya wanawake wapo kwenye hatari ya kupata tatizohili au wengine Tayari wameshalipata. Mpaka hivi sasa hakuna Sababu ya moja kwa moja ambayo inaelezwa kama chanzo cha tatizo hili.

JE NI NANI YUPO HATARINI ZAIDI KULIPATA UVIMBE KWENYE KIZAZI?

Ni Wanawake ambao wanakaribia kukoma hedhi (Menopause) hasa wa kati ya miaka ya 38-45.
Pia Wanawake wanene au wenye Matumbo makubwa (Obesity)
Pia wanawake wasiokuwa na watoto wapo kwenye hatari zaidi ukifananisha na wale wenye Watoto.

DALILI ZA UVIMBE KWENYE KIZAZI NI ZIPI

Tatizo hili linaweza kuwa na Dalili au Kutokuwa na Dalili kabisa. Lakini kwa mara nyingi Dalili zake ni hizi…

👉🏿Kutoka kwa Hedhi nzito pia kwa muda zaidi ya kawaida.
👉🏿Damu kutoka kipindi ambacho sio cha siku zake.
👉🏿Maumivu ya Sehemu za Kiuno.
👉🏿Maumivu ya Chini ya Mgongo.
👉🏿Kwenda haja ndogo mara nyingikwa hali isiyo ya kawaida.
👉🏿Maumivu wakati wa tendo la ndoa.

Sio lazima uwe na Dalili zote na mara nyingi hazitokei zote hasa ni moja au mbili.

Hivyo Kujikinga au kuepukana na Tatizo hili ni vyema kwa Mwanamke ukapungua Uzito hasa Kitambi au Tumbo kubwa.

Faida za kula tunda la apple (tufaa)

Tunda asili yake ni sehemu za Mashariki mwa Europe na pia Magharibi mwa Asia, na tunda hili linajulikana kwa miaka ya zamani mno katika miji ya Old China, Babulon na Egypt. Tunda hili hutumiwa na lina faida kubwa katika mwili wa mwanaadamu. Lina dawa ya maradhi tofauti:

Apple hutibu Anaemia

Apple lina wingi wa iron, arsenic na phosphorus, kwa mtu mwenywe ugonjwa huu inafaa kufanya juice ya apple iwe fresh. Ni vizuri kunywa juice hiyo glass moja kabla kula chakula (nusu saa kabla) na pia kabla ya kwenda kulala usiku.

Hutibu tatizo la kuharisha na kutapika

Mwenye kutokezewa na ugonjwa huu ni vizuri sana kutumia tunda hili (iwe bivu). Kila siku ale 2 pia kama yatapikwa au kuchomwa ni mazuri zaidi kwani hulainisha cellulose.

Hutibu matatizo ya tumbo.

Kuna matatizo tofauti ya tumbo, kwahivo tunda hili limekusanya matatizo yote ya tumbo na kuondoa matatizo hayo. Changanya apple, asali kidogo na ufura kidogo na kula kabla chakula hii husaidia kuondoa matatizo ya tumbo kama vile usagaji mdogo wa chakula na mengine.

Kuumwa na kichwa.

Tunda hili lina faida katika maradhi yote ya kichwa. Apple lilowiva limenye maganda yake, halafu ule kwa kutia chumvi kidogo kila siku asubugi kabla ya kula kitu chochote, na uendelee kufanya hivi kwa muda wa wiki 2.

Matatizo ya moyo

Apple ya wingi wa potassium na phosphorus lakini sodium inapatikana kidogo sana.Kwa wakai wa zamani watu walikuwa wakila matunda haya na asali, kwa ajili ya maradhi ya moyo na research imefanyika imeonekana kwa wale watu wanotumia vyakula venye potassium kwa wingi huepukana na maradhi ya moyo. Kwahili ni uzuri kula tunda hili pamoja na asali.

High Blood Pressure

Apple linasaidia katika kuongeza kutoa (secreation) mkojo ambayo hii inasaidia kurudisha blood pressure katika hali ya kawaida, pia inasaidia kupungua kwa sodium chloride katika figo..

Hutibu matatizo ya meno

Matunda ya maepo yanasaidia sana meno katika kuyasafisha na kuyaepusha na vijidudu na kuoza, kila baada chakula kula apple moja.

Faida na namna ya kutumia mafuta ya Zaituni Olive Oil kwenye nywele

Faida ya Mafuta Ya Zaituni Olive Oil kwenye nywele.

1. Yanasaidia kufanya mzunguko wa damu kufanya kazi vizuri kwenye ngozi ya kichwa na kupenyeza hadi kwenye shina ya nywele kisha kuifanya nywele inayoota kuwa imara

2. Yanasaidia kupambana na mba kwenye ngozi ya kichwa

3. Yanasaidia uzalishwaji wa mzizi au shina ya nywele

4. Yanasaidia uzalishwaji wa melanin ambayo inafanya kazi ya kutoa rangi ya nywele inayotakiwa.

5. Yanasaidia kuifanya nywele isiwe kavu sana.

NAMNA YA KUZIHUDUMIA NYWELE:

Unaweza kuchanganya na Mdalasini pamoja na Asali.

1. Olive oil vijiko 2 vya chakula

2. Asali kijiko 1 cha chakula

3. Mdalasini kijiko 1 cha chai

Pasha moto olive oil kisha changanya vyote kwa pamoja pakaa kwenye nywele acha kwa muda wa dakika 20 kisha osha nywele zako na upakae mafuta zikishakauka.

Ninashauri utumie mafuta haya kwenye nywele na ngozi ni mazuri sana. Ukiwa na mba pakaa kwenye ngozi mba itaisha na muwasho utaondoka.

Mafundisho ya Msingi kuhusu Roho Mtakatifu

Roho Mtakatifu ana nafasi gani katika sala?

Roho Mtakatifu ndiye Mlezi wa ndani wa sala ya Kikristo

Kusadiki kwa Roho Mtakatifu maana yake ni nini?

Kusadiki kwa Roho Mtakatifu maana yake ni kusadiki kwa nafsi ya Tatu ya Utatu Mtakatifu

Majina mengine ya Roho Mtakatifu ni yapi?

Roho Mtakatifu huitwa pia Mfariji wa kweli, Roho wa Bwana, Roho wa Kristu

Ni alama zipi zinawakilisha Roho Mtakatifu?

Alama zinazowakilisha Roho Mtakatifu ni hizi; Maji, Mpako wa mafuta, Moto, wingu, tendo la kuweka mikono, njiwa

Neno Manabii maana yake ni nini?

Neno Manabii maana yake ni waliovuviwa na Roho Mtakatifu waseme kwa jina la Mungu

Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume siku gani?

Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume siku ya Pentekoste, yaani siku ya hamsini toka Pasaka. (Mdo 2:1-4)

Roho Mtakatifu aliwafanyia nini Mitume?

Roho Mtakatifu aliwatia Mitume Mwanga wa nguvu ili waweze kuhubiri Injili na kueneza Kanisa kote duniani

Roho Mtakatifu anatufanyia nini sisi Wakristo?

Roho Mtakatifu anatufanyia haya;
1. Anatuangaza tufahamu mafundisho ya dini
2. Anatuimarisha tutende mema na kuacha mabaya
3. Anatutakasa na kutututia uzima rohoni mwetu
4. Analiongoza Kanisa. (Yoh 16:13-15)

Roho Mtakatifu anatutakasa kwa namna gani?

Roho Mtakatifu anatutakasa kwa;
1. Neema ya utakaso
2. Fadhila za Kimungu na vipaji vyake

Maandiko Matakatifu ndiyo nini?

Maandiko Matakatifu ndiyo vitabu vyote 73 ambavyo viliandikwa na watu kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu vikakusanywa na Kanisa kwa jina la “Biblia”, yaani “Vitabu”.
Hao “wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu” (2Pet 1:21).

Roho Mtakatifu ni nani?

Roho Mtakatifu ni upendo wa Mungu, nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu, mwenye Umungu mmoja na Baba na Mwana.
“Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rom 5:5).
Ametumwa kwetu atufanyie kazi pasipo kuonekana.
“Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho” (Yoh 3:8).
“Wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” (Rom 8:14).

Je, kazi zote za Roho Mtakatifu zinahusiana na Yesu?

Ndiyo, kazi zote za Roho Mtakatifu zinahusiana na Yesu na kulenga hasa kuandaa watu wampokee, wamfuate na kumshuhudia katika umoja wa kundi lake, Kanisa.
“Ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia. Nanyi pia mnashuhudia” (Yoh 15:26-27).

Kumpokea Roho Mtakatifu maana yake nini?

Kumpokea Roho Mtakatifu maana yake ni kuja kuongozwa naye badala ya kutawaliwa na shetani.
“Kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwetu, aliaye, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’ Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu. Lakini wakati ule, kwa kuwa hamkumjua Mungu, mliwatumikia wao ambao kwa asili si miungu… Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho” (Gal 4:6-8; 5:25).
“Ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake” (Rom 8:9).

Tukimpokea Roho Mtakatifu papo hapo tunapokea pia nini?

Tukimpokea Roho Mtakatifu papo hapo tunapokea pia adili kuu la upendo:
“Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rom 5:5).
Tena tunapokea vipaji vyake ambavyo Yesu alikuwa navyo kikamilifu.
“Roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana. Na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana” (Isa 11:2-3).
Mambo hayo, tofauti na karama, ni ya lazima kwa yeyote apate wokovu wa milele.

Je, tunaweza kuhakikisha neema ya utakaso?

Hapana, hatuwezi kuhakikisha neema ya utakaso kwa kuwa ni tukio ambalo linapita maumbile na kufanyika rohoni, hivyo halifikiwi na hisi zetu. Pengine Mungu anatokeza dalili fulani za badiliko hilo kama vile furaha ya ndani au karama ya nje, lakini hizo hazihitajiki wala hazitoshi kuthibitishia mtu amepata neema hiyo.
“Wengi wataniambia siku ile: Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri: Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu” (Math 7:22-23).
“Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu” (1Kor 13:1-3).

Je, karama ni zile za kushangaza tu?

Hapana, karama si zile za kushangaza tu, tena zile muhimu zaidi si hizo, bali zile zinazojenga zaidi Kanisa, kama zile za uongozi:
“Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha” (1Kor 12:28).
“Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema tuliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia, kwa bidii; mwenye kurehemu, kwa furaha” (Rom 12:6-8).

Karama nyingine muhimu zinatuwezesha kufanya nini?

Karama nyingine muhimu zinatuwezesha kuishi kwa useja kama Yesu na Paulo, au kwa ndoa:
“Nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi. Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane; ni heri wakae kama mimi nilivyo” (1Kor 7:7-8).
“Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa” (Math 19:11).
Tunavyoona katika historia ya watawa, mara nyingi karama ya useja inaendana na nyingine katika maisha ya sala, ya kijumuia na ya kitume. Hivyo Filipo “alikuwa na binti wanne, mabikira, waliokuwa wakitabiri” (Mdo 21:9).

Karama zinagawiwa vipi?

Karama zinagawiwa na Roho Mtakatifu jinsi anavyotaka, si kwa sifa au faida ya binafsi, bali kwa ustawi wa taifa la Mungu.
“Kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye… Je, wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?… Kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa… Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani” (1Kor 12:11,29-30; 14:12,33). Kwa ajili hiyo mitume walipambanua na kuratibu karama katika ibada na katika maisha ya jumuia zisije zikavuruga Kanisa.

Karama za kushangaza zina hatari gani?

Karama za kushangaza zina hatari mbalimbali, hasa zikitiwa maanani mno. Hapo ni rahisi zilete majivuno, kijicho na mafarakano.
“Ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je, si watu wa tabia ya mwili ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?… Mmekwisha kushiba, mmekwisha kupata utajiri, mmemiliki pasipo sisi. Naam, laiti mngemiliki… Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke” (1Kor 3:3; 4:8; 10:12).
Katika mambo yasiyothibitika ni rahisi kudanganyika kuwa yametoka kwa Mungu, kumbe sivyo. Kisha kudanganyika ni vigumu kuachana nayo hata yakiwa na madhara kwa mhusika au kwa Kanisa.
“Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani” (1Yoh 4:1).

Tunda la kuongozwa na Roho Mtakatifu ni lipi?

Tunda la kuongozwa na Roho Mtakatifu ni umoja wa Kanisa unaotokana na ustawi wa upendo na vipaji ndani ya waamini.
“Wote walijaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja” (Mdo 4:31-32).
“Tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria” (Gal 5:22-23).
“Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli. Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi, ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi; tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki” (Yak 3:14-17).
Madhehebu yanapozidi kufarakana ni lazima tujiulize kama kweli ni kazi ya Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu anatusaidiaje kusali?

Roho Mtakatifu anatusaidia tusali kama Yesu, akiwa mlezi wa ndani na kutumia vipaji vyake saba.
“Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’” (Gal 4:6).
“Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa… huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu” (Rom 8:26-27).
Ndiyo sababu Kanisa linatuhimiza tumtamani na kumualika kila mara, ‘Njoo, Roho Mtakatifu!’ yaani kumuomba Baba kwa njia ya Mwana amtume zaidi na zaidi ndani mwetu.

Roho Mtakatifu anaweza kutufikisha hadi wapi?

Roho Mtakatifu anaweza kutufikisha hadi muungano wa dhati na Mungu.
“Yeye awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake, katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu” (Ef 3:16-19).
“Huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote” (Yoh 16:13).
Safari hiyo inategemea sana sala isiyoishia katika maneno bali inalenga kupenya mafumbo kwa imani na upendo.

Sakramenti ya Kipaimara ni nini?

Ni Sakramenti yenye kumpa Mkristu Roho Mtakatifu na ukamilifu wa mapaji yake saba, kumfanya mkristu mkamilifu na kumwandika Askari hodari wa Yesu Kristo Mpaka Kufa

Nini maana ya Roho Mtakatifu?

Roho Mtakatifu ni nafsi ya Tatu ya Utatu Mtakatifu, ni Mungu Halisi sawa na Mungu Baba na Mwana. (Yoh 14:16-17,26)

Je, Roho Mtakatifu Katika mfano wa ndimi za Moto Maana yake nini?

Maana yake ni kupata nguvu ya Kuhubiri Injili, Neno la Mungu linalopenya kwenye Moyo Kama Moto.

Roho Mtakatifu anawafanyia Waamini nini?

Roho Mtakatifu anawafanyia Waamini haya.
1. Anawatakasa
2. Anawaangaza na kuwavuta ili waende kwenye uzima wa milele

Ni kwa namna gani Roho Mtakatifu Anatutakasa?

Roho Mtakatifu anatutakasa kwa njia ya Sakramenti, Visakramenti, Fadhila za Kimungu na vipaji vyake. (Yoh 16:8)

Ni kwa namna gani Roho Mtakatifu anatenda kazi zake?

Roho Mtakatifu anatenda kazi zake kwa njia hizi;
1. Anatuangaza kwa Mwanga wake tupate kuelewa mafundisho ya dini
2. Anatupatia neema za msaada za kutusaidia kutunza utakatifu wetu
3. Anatuvuta kwa mapendo yake tuzitumie Neema na kufika kwenye uzima wa milele.
4. Anatufariji katika shida zote. Ndio maana Roho Mtakatifu huitwa pia Mfariji

Kwa nini Sakramenti hii inaitwa Kipaimara?

Inaitwa Sakramenti ya Kipaimara kwa sababu inaimarisha na kukamilisha neema ya Ubatizo

Roho Mtakatifu anakuja kufanya nini rohoni mwetu kwa Kipaimara?

Anakuja kufanya yafuatayo;
1. Anakuja kutuongezea Neema ya Utakaso
2. Anatuletea pia ukamilifu wa mapaji yake saba na msaada wa kuungama imani yetu mbele za watu

Mapaji Saba ya Roho Mtakatifu ndio nini?

Mapaji saba ya Roho Mtakatifu ni msaada wake wa kuimarisha na kuzoesha akili na moyo wetu kwa mambo ya utumishi wa Mungu

Mapaji saba ya Roho Mtakatifu ni yapi?

Mapaji Hayo ni;
1. Hekima
2. Akili
3. Shauuri
4. Nguvu
5. Elimu
6. Ibada
7. Uchaji wa Mungu (Isaya 11:2)

Hekima ni nini?

Ni upendaji wa Mambo ya Mungu na Machukio ya Mambo ya Dunia

Akili ni nini?

Ni mwangaza wa Roho Mtakatifu wa Kutusaidia tumjue zaidi Mungu na Ukamilifu wake na kuwa na Hakika kwamba Mungu peke yake aweza kutuliza roho zetu

Shauri ni nini?

Ni utaratibu wa Kuchagua Siku zote mambo yenye kufaa kwa sifs ya Mungu na kwa Wokovu wetu

Nguvu ni nini?

Ni moyo wa kushika sana Amri za Mungu na mambo ya utumishi wake tusiogope watu, matukano, mateso wala kufa. (Rum 8:38-39)

Elimu ni nini?

Ni maarifa ya kutambua werevu na udanganyifu wa shetani; anaposhawishi mwenyewe au kwa kutumia vitu au watu. (1Pet 5:8-9)

Ibada ni nini?

Ni roho ya kupenda utumishi wa Mungu na yote yale yenye kumpa Mungu sifa na Heshima

Uchaji wa Mungu ni nini?

Ni hofu ya kumchukiza Mungu kwa Dhambi kama vile mtoto mwema aogopavyo kumchukiza mzazi au mlezi wake.

Roho Mtakatifu hutajwa wapi katika Rozari?

Roho Mtakatifu hutajwa katika fungu la tatu la Matendo ya Utukufu tusemapo; Aliyepeleka Roho Mtakatatifu. (Mdo 2:1-4)

Kabla ya Kupaa mbinguni Yesu aliwaahidi nini Mitume?

Kabla ya kupaa mbinguni Yesu aliwaahidia Mitume kuwapelekea Roho Mtakatifu; ndiye nafsi ya Tatu ya Utatu Mtakatifu. (Yoh 16:7)

Je, Yatupasa kumwomba Roho Mtakatifu?

Ndiyo, kwani twataka kwake maonyo na msaada. Tusipokuwa na neema yake hatuwezi kutenda jambo jema la kufaa kutuokoa. (Yoh 16:13)

Matunda ya kuongozwa na Roho Mtakatifu ni yapi?

Matunda ya Roho Mtakatifu ni;
1. Upendo
2. Furaha
3. Amani
4. Uaminifu
5. Uvumilivu
6. Utu wema
7. Fadhila
8. Upole
9. Kiasi
(Wagalatia 5:22, 23)

Biblia ni nini? Asili, Historia, waandishi na mipaka yake

Biblia ni mkusanyiko wa vitabu mbalimbali vinavyohusu kazi ya Mungu ya kuwakomboa mwanadamu kuanzia enzi za Mababu na manabii Wa Waisraeli, Enzi za Yesu na za Mitume wa Yesu.

Je, Biblia ilipatikanaje? Nini chanzo na asili ya Biblia.

Biblia iliundwa kwa kukusanya vitabu vya dini vya wakristo hapo awali na kuunda kitabu kimoja. Kwa maana hii, Biblia ni vitabu teule vya dini vilivyoonekana vinafaa kutumika kwa waumini Wakristo ili kusaidia Imani yao. Hivyo basi, kama Biblia ni vitabu teule tuu vipo vitabu vingine vya dini ambavyo havikuwekwa Kwenye Biblia.
Wakristo wa kwanza walichagua vitabu kadhaa na kuviweka pamoja na kisha kuvita Biblia. Biblia ni mkusanyiko wa vitabu muhimu tuu vya dini mpaka kufikia Enzi za Mitume.

Je, Biblia ndicho kitabu pekee cha neno la Mungu?

Hapana, Biblia sio kitabu pekee cha neno la Mungu isipokua Biblia ni kitabu kilichoidhinishwa rasmi kutumika Kama kitabu kikuu cha Wakristo. Hii ni kwa sababu Biblia imeundwa na vitabu muhimu tuu vilivyochaguliwa na wakristo wa kwanza vilivyoonekana vinafaa kwa kufundishia, Ibada na kukuza Imani. Kwa hiyo basi vipo vitabu vingine ambavyo haikuwekwa Kwenye Biblia ambavyo ni Maneno ya Mungu.
Hii ndiyo sababu kwa nini Wakatoliki wana vitabu vingi kuliko madhehebu Mengine. Yaani sababu ni kwamba madhehebu Mengine walivitoa vitabu vingine vilivyounda Biblia. Na Wakatoliki waliweka vitabu vingine vya dini Kwenye Biblia walivyoona vinafaa pia kutumika.

Je nje ya Biblia hakuna Neno la Mungu au Maandiko matakatifu?

Nje ya Biblia kuna Neno la Mungu na Maandiko Matakatifu. Hii Inamaanisha kuwa Biblia sio kitabu pekee cha neno la Mungu. Zipo nyaraka na Vipo vitabu vingine vingi ambavyo viliandikwa na Manabii na Mitume ambavyo havikuwekwa kwenye Biblia lakini ni mafundisho ya Mungu. Biblia ni mkusanyiko wa vitabu vikuu vya Mungu.
Kumbuka kuwa sio nyaraka zote za Mitume ziliandikwa Kwenye Biblia. Vile vile manabii walikuwa ni wengi kuliko waliowekwa Kwenye Biblia.

Je Biblia ndiyo mafundisho ya Mungu pekee?

Hapana, Biblia sio mafundisho pekee ya Mungu. Hii ni kwa sababu sio mambo yote aliyofanya na kusema Mungu yaliandikwa na vilevile Mitume hawakua watu wa Mwisho kupokea Roho mtakatifu na kupokea neno la Mungu.

Biblia inatuthibitishia yenyewe kuwa haijakamilika na Si mambo yote yameandikwa Kwenye Biblia

Biblia inatuthibitishia kuwa haijakamilika tunaposoma (Yohane 21:25)
Biblia inatuambia hivi…”Kuna mambo Mengine mengi aliyofanya Yesu, ambayo Kama yangeandikwa yote, moja baada ya jingine, nadhani hata ulimwengu wenyewe usingetosha kuviweka vitabu ambavyo vingeandikwa.”…Kwa mstari huu Biblia inatuthibitishia kuwa haikuandikwa vitu vyote.

Je Biblia ni mwisho wa Maandiko ya Mungu?

Biblia sio mwisho wa Maandiko ya Kimungu.
Biblia ni sehemu ya maneno ya Mungu mpaka miaka ya Mitume
Hata sasa Mungu anafanya kazi na watu wake kupitia Roho Mtakatifu na kwa kwa sababu hii Biblia sio mwisho wa kazi ya Mungu ya kusema na watu wake.
Mungu yu hai na anafanya kazi na watu wake mpaka sasa kwa kutumia vinywa vya watu Kama aliyofanya hapo awali.
Hata maneno unayohubiriwa sasa yanaweza kuwa ni kutoka kwa Mungu kwa maana hata waandishi wa Biblia walitumiwa na Mungu Kama wahubiri wa sasa. Mungu ni yule yule, Roho Mtakatifu ni yuleyule na Neno ni lile lile.
Kwa hiyo Biblia ni maneno yaliyochaguliwa mpaka enzi za Mitume. Vitabu vilivyofwata Baada ya Mitume japokuwa viliandikwa kwa Roho Mtakatifu havikuwekwa Kwenye Biblia.

Sababu ya Kanisa katoliki kutumia mapokeo na Maandiko ya Watakatifu

Kanisa katoliki linatumia mapokeo na Makala za watakatifu kwa Imani kuwa Mungu yule yule aliyefanya kazi tangu zamani anafanya kazi na watu wake mpaka sasa na hivyo Maandiko ya watu wa Mungu yanafaa kutumika kama yalivyotumika ya watu wa kale.

Yesu alituambia nini kuhusu Neno la Mungu na Mwendelezo wa kazi ya Mungu ya kusema na watu?

Yesu alituambia hivi katika (Yohane 16:12-15)..”Ninayo mengi ya kuwaambieni Ila kwa sasa hamuwezi kuyastahimili. Lakini atakapokuja huyo Roho wa Ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote. Maana hatasema kwa Mamlaka yake mwenyewe bali atasema atakayoyasikia na kuwajulisheni yatakayokuja. Yeye atanitukuza Mimi kwa kuwa atawajulisheni Yale atakayoyapata kutoka kwangu “…
Sasa basi,kama Roho Mtakatifu ni yuleyule na kazi zake ni Zile Zile za tangu Mitume, kwa nini hatukubali kuwa Anafanya kazi mpaka sasa kupitia watu wa Mungu? Kwa nini tunakataa mafundisho yao? Kwa nini tunashindwa kuelewa kuwa Biblia haikuwa mwisho wa Neno la Mungu? Kwa nini tunakana Mapokeo ya Watakatifu? Kwa nini hatuwaamini watumishi wake wa sasa?

Jinsi ya kujisaidia unapotokwa na damu Puani

Unapotokwa na damu puani fanya yafuatayo;
1. Simama wima na inamisha kichwa kwa mbele, kusimama itakusaidi kupunguza kasi na presha katika mishipa ya damu puani wakati unapoinamisha kichwa kwa mbele huzuia kumeza damu ambayo italeta shida tumboni.

2. Weka pamba au kitambaa chenye uwezo wa kufyonza damu nje ya pua na bana pua kwa muda wa dakika 15 huku ukitumia mdomo kupumua, kubana pua hurudisha damu katika mishipa ya pua na kuzuia kuvuja.

3. Kuzuia damu isitoke tena usichokonoe pua wala kuinamisha kichwa mbele kwa nguvu na kwa muda mrefu.

4. Kama damu inaendelea kutoka bana pua kwa kutumia kitambaa chenye ubaridi au barafu itasaidia kusinyaa kwa mishipa ya damu na kuzuia damu.

5. Nenda hosipitali kama damu puani inatoka na kuumia kichwani, haijakata kwa muda wa dakika 20 na kama pua imeumia au kuvunjika

KUMBUKA: Kutokwa na damu puani ni jambo la kawaida sana kwa kila mtu na mara nyingi huwa sio hatari sana isipokuwa kama linaambatana na dalili nyingine hatari. Tatizo ili huweza kusababishwa na kuumia ndani au nje ya pua, kuchokonoa pua mara kwa mara, shinikizo la damu, matumizi dawa za aspirini, ukosefu wa vitamini K, pombe kupita kiasi, na mabadiliko ya hormoni kwa wajawazito

Mapishi ya Mihogo ya nazi na kuku

Mahitaji

Mihogo kilo 1
Kidali cha kuku 1 kikubwa
Nyanya 1 kubwa
Kitunguu maji 1 cha wastani
Swaum/tangawizi i kijiko cha chai
Nazi kopo 1
curry powder 1 kijiko cha chai
Binzari manjano 1/2 kijiko cha chai
Limao 1/2
Pilipili 1
Chumvi kiasi

Matayarisho

Saga pamoja nyanya, kitunguu na swaum/ginger pamoja na vimaji kidogo. Kisha vitie kwenye sufuria isiyoshika chini na uvishemshe mpaka maji yote yakauke kisha tia mafuta na upike ktk moto mdogo mpaka viive.Baada ya hapo tia spice na uzipike kidogo kisha tia mihogo na kuku (kuku na mihogo vikatwe vipande vya wastani) vichanganye vizuri kisha tia nazi na vimaji kiasi,limao chumvi na pilipili na ufunike kisha punguza moto. Pika mpaka mihogo na kuku viive na ibaki rojo kidogo kisha ipua na mihogo yako itakuwa tayari kwa kuliwa

Tabia za kuepuka ili uweze kuwa tajiri

UKIWA NA HIZI TABIA 9, JIANDAE KUFA MASKINI…………
By Kashindi Edson

“Umasikini hauji kwa bahati mbaya kama ubaguzi wa rangi au ukoloni, umaskini hutokana na matendo ya kila siku ya mwanadamu” (Nelson Mandela, R.I.P)

“Kila mtu anataka kufanikiwa, lakini si kila mtu yuko tayari kushika majukumu na wajibu wa kumpeleka kwenye mafanikio”(Mwl Nyerere, R.I.P).

“Kile unahokifanya muda huu ndicho kinachoashiria na kutoa picha kamili ya baadae yako”(Mahatma Gandhi, R.I.P)

“Ukizaliwa maskini sio kosa lako, ila ukifa maskini hilo ni kosa”(Bill Gate, The richest man in the world).

Mwalimu wangu wa chuo aliwahi kuniambia kuwa, “mstari unaomtenganisha maskini na tajiri ni mwembamba sana, kwa hiyo ni rahisi sana kuwa tajiri pia ni rahisi sana kuwa maskini”. Mpaka leo sijaelewa alimaanisha nini.

Watu wote waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali za maisha, kwenye uongozi, biashara, kilimo, elimu, siasa, michezo, uandishi, muziki, afya, imani, utangazaji, nk huwa hawana hizi tabia 9 nilizokuandalia leo, kwa hiyo kama una kiu ya mafanikio kwa hicho unachopambania, achana na haya mambo 9 yafuatayo;

1. KUTOKUJARIBU.

Katika kutafuta mafanikio huwa kuna vitu viwili tu vya kuchagua. Tambua kuwa maisha ni vita. “Chagua kufa, au kupambana”. “Siogopi kufa, naogopa kutokujaribu'(Jay Z). Hakuna alie zaliwa anajua, jiamini, jaribu utafanikiwa.

2. KUTOKUJIFUNZA.

Che Guava mpaka anafariki library yake ilikuwa na vitabu zaidi ya 2000, mwenzangu na Mimi sijui hata kama una Biblia au Quran ghetoni kwako. Nkwameh Nkrumah library yake ilikuwa na vitabu zaidia ya 3000, Obama anakuambia kila akiamka asbuhi lazima asome kitu kipya. “JOSEPH=Jifunze, Ona, Soma, Elimika, Pitia, Hamasika.(Prof Jay)

3. WOGA & WASIWASI.

“Tunaweza tukamsamehe mtoto anayeogopa gizani, lakini sio mtu mzima anaeogopa mchana”(Plato, R.I.P). Kitu cha kuogopa katika maisha ni woga wenyewe. Kama hujiamini hutakuja kuwa mshindi katika jambo lolote. Fanya hicho unachofikiria kukifanya kwa moyo wa dhati, kama unaamini ni cha harali na kia manufaa kwako na familia yako, na jamii nzima. Acha tabia ya kuogopa kitu ambacho hakijatokea.

4. KUJILINGANISHA.

Kuna baadhi ya watu, huwa wangetamani kuwa kama watu Fulani. Kuwa wewe pia jiamini. Usitamani kuwa Magufuli, Kassim Majaliwa au Paul Makonda. Kila mtu ni wa pekee na maalumu. Jikubali kwanza afu wengine ndo watakukubali wewe. Weka nguvu kwenye ubora wako na sio kwenye madhaifu yako. Ukijilinganisha sana utakosa furaha ya nafsi maisha yako yote.

*5. KUWEKA VINYONGO.**

“Kuweka chuki na konyongo moyoni ni sawa na kunywa sumu ukidhani atakufa mtu mwingine”. Onesha upendo, sambaza upendo, hayo ndo mafanikio ya kweli.

6. UONGO

“Uongo utakupa ushindi wa siku moja, ukweli utaishi milele”(WEUSI), “Muongo hata akiongoea ukweli usimuamini”(FID Q). Ukiwa muongo huwezi kufanikiwa hata siku moja. “Unaweza ukawadanganya watu, lakini huwezi kuwadanganya watu wote, wakati wote”(Bob Marley). Ukweli kama jua, katika safari ya mafanikio huwezi kuvificha.

7. UVIVU & UZEMBE

“Nyumba yenye njaa ukisizi unapata zero”(Fid Q). Mafanikio huja kwa kupenda unachokifanya. Neno “kazi” katika biblia limeandikwa mara 600. Dangote analala masaa 3 tu kila siku, Mohammed Dewj anaamka saa 11 asbuhi kila siku. We kwepa majukumu tu, kesho utakula magodoro. “Uvivu unalipa muda huu, bidii & juhudi vinalipa baadae”.

8. STAREHE & ANASA KUPINDUKIA

Pombe, sigara, ngono, unga, bange, shisha, cocaine, nk vitu vibaya sana. Ni ngumu sana kufikia mafanikio makubwa kama una tabia kama hizi. “Sisi ni kile tunacho kula”. Mafanikio ya kwanza huanzia kwenye afya yako”. Afya ni utajiri. Pia starehe hupoteza muda sana. “Mavuno ya uzee, ni swaga za ujana, kwa ukila ujana kumbuka kula kiungwana”(Nikki Mbishi,).

9. LAWAMA & UMBEA

“Watu wenye uwezo mkubwa wa kufikiria hujadili kuhusu mawazo, uwezo wa kati hujadili kuhusu matukio na wale wenye uwezo wa chini, hujadili kuhusu watu” We upo kwenye kundi gani? Bora ukawa kundi la kati kuliko hilo la chini kabisa, hilo ni la “wachawi”. Tusilamike, tupambane,lawama hazisaidii chochote.Ukiweka malengo yako, vizuri na ukaacha hizo tabia hapo juu, muda si mrefu itazifikia ndoto zako

Mapishi ya Ugali, dagaa (wabichi) na matembele

Mahitaji

Dagaa wabichi (Fresh anchovies packet 1)
Unga wa ugali (corn meal flour 1/4 kilo) (unaweza kutumia unga wa choice uipendayo)
Matembele ya kukaushwa (dried sweet potato leaves, handful)
Nyanya ya kopo (tin tomato 1)
Kitunguu maji (onion 2)
Limao (lemon 1/4)
Pilipili mbuzi nzima bila kukata (scotch bonnet pepper1, do not chop)
Chumvi (salt 1/2 ya kijiko cha chai)
Mafuta (vegetable oil)
Hoho (green pepper 1)
Kitunguu swaum (garlic 5 cloves)
Tangawizi (ginger 1 kijiko cha chai)
Binzari ya curry (Curry powder 1/2 kijiko cha chai)

Matayarisho

Safisha dagaa kwa kutoa vichwa na utumbo kisha waoshe na uwakaushe na kitchen towel na uwaweke pembeni. Baada ya hapo katakata, vitunguu na hoho kisha weka pembeni. Baada ya hapo weka sufuria jikoni na utie mafuta yakisha pata moto tia dagaa na uwakaange mpaka wawe wa brown, kisha tia kitunguu swaum,curry powder na tangawizi, kaanga kidogo kisha malizia kwa kutia vitunguu maji, hoho,pilipili,chumvi na ukamulie limao. Kaanga kwa muda wa dakika 3-4 na hakikisha vitunguu na hoho haviivi sana na hapo dagaa watakuwa tayari.

Baada ya hapo yaoshe na uyaloweka matembele (kama ni makavu) kwa muda wa dakika 15, Kisha yatoe na uyaweke kwenye sufuria pamoja na kitunguu, nyanya, chumvi ,kamulia limao kidogo, pilipili na maji kiasi. acha matembele yachemke kwa muda wa dakika 20 na uhakikishe yameiva kwa kuwa laini. Baada ya hapo yapike mpaka maji yote yakauke na mafuta yatok na hapo matembele yatakuwa tayari.

Ukisha maliza kupika dagaa na matembele andaa chungu cha ugali. Kwanza unatakiwa kuchemsha maji ya moto, kisha koroga pembeni unga kiasi katika maji ya baridi na utie kwenye maji yanayochemka, Fanya kama unatengeneza uji, uji wa ugali ukishachemka tia unga na uanze kuusonga mpaka ugali uive. Ukisha iva pakua na usevu na mboga tayari kwa kuliwa.

Hizi ndizo faida za kiafya za kuota jua

Kuna mambo ambayo huwa tunayachukulia ya kawaida na wala hatuko tayari kufahamu umuhimu wake. Jua ni kitu mojawapo ambacho huwa tunakiona kila siku, lakini ni mara chache tumelichunguza.

Kwa hakika kuna umuhimu mkubwa wa jua kwa mimea na viumbe vingine akiwemo binadamu. Tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu wa afya, zimebaini kuwa kuna manufaa makubwa ya kuota jua angalau kwa kiasi fulani kila siku.

Kwa kuwa najua unapenda afya bora, basi fahamu faida 10 za kuota jua kiafya.

Kuua bakteria

Jua linaweza kutumiwa kuua bakteria mbalimbali katika majeraha na ngozi. Tiba hii iligunduliwa na mshindi wa tuzo ya Nobel Niels Finsen. Tiba hii ilitumiwa kuponya vidonda vya wanajeshi wa Kijerumani baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia.

Huondoa msongo wa mawazo

Inakadiriwa mtu anapokuwa kwenye jua hupata takriban kiasi cha kemikali ya lux kipatacho 100,000. Hivyo kukosa jua kunasababisha tatizo linalofahamika kama vile Seasonal Affective Disorder (SAD) ambayo ni aina fulani ya msongo.

SAD hutokea mara nyingi kwa watu wengi kipindi cha masika au kwa wale wanaokaa ofisini muda mrefu. Hivyo kuoata jua kutakuongezea kemikali ya lux na kukuepusha na tatizo la Seasonal Affective Disorder (SAD).

Huzuia shinikizo la damu

Utafiti uliofanyika katika chuo cha Edinburgh ulibaini kuwa kemikali ya nitric oxide ambayo hukabili shinikizo la damu, huingia kwenye damu pale mwili unapopigwa jua.

Watafiti waliendelea kueleza kuwa kutokana na utafiti huo ni wazi kuwa jua haliboreshi afya pekee, bali hurefusha maisha kwa kumwepushia mtu hatari ya kifo kinachoweza kutokana na shinikizo la damu.

Huimarisha mifupa

Inafahamika wazi kuwa jua ni chanzo cha upatikanaji wa vitamini D ambayo huuwezesha mwili kufyonza madini ya calcium na phosphorus yanayoimarisha mifupa.

Inaelezwa pia vitamini D3 inayozalishwa wakati wa uzalishaji wa vitamini D, husaidia kuzuia kuvunjika kirahisi kwa mifupa hasa kwa watu wenye umri mkubwa.

Huponya matatizo ya ngozi

Katika utafiti mmoja uliofanyika kwa watu wenye matatizo ya ngozi, ulibaini kuwa asilimia 84 ya magonjwa hayo yalipona baada ya kukaa kwenye jua kwa muda uliopendekezwa na daktari.

Inashauriwa kukaa kwenye jua kwa kiasi au kwa kutegemea ushauri wa daktari ili kuepusha madhara na kuhakikisha tiba hii inafanya kazi ipasavyo.

Huzuia baadhi ya saratani

Wakati watafiti wa saratani wakieleza kuwa zipo saratani hasa za ngozi zinazosababishwa na mionzi ya jua; kwa upande mwingine jua huzuia baadhi ya saratani.

Inaelezwa kuwa vitamini D inayozalishwa kutokana na jua, hupunguza aina mbalimbali za saratani kwa takriban asilimia 60.

Huboresha kinga ya mwili

Tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa kukaa kwenye jua la wastani huwezesha uzalishaji wa seli nyeupe za damu ambazo huukinga mwili dhidi ya maradhi.

Hupunguza lehemu (cholestrol)

Jua linapopiga ngozi ya mwanadamu hubadili lehemu iliyoko kwenye ngozi na kuifanya kuwa homoni ya steroid pamoja na baadhi ya homoni nyingine muhimu kwenye uzazi.

Hivyo kukaa kwenye jua hakupunguzi tu lehemu bali huzalisha pia homoni muhimu katika mwili wa binadamu.

Husaidia ukuaji wa watoto

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa jua ni muhimu sana hasa kwa ukuaji wa watoto wadogo. Hivyo kumweka mtoto nje ili apate angalau kiasi fulani cha jua kutaboresha afya na ukuaji wake.

Huongeza kiwango cha oksijeni mwilini

Jua linapoupiga mwili wako, linafanya seli nyekundu za damu kuweza kubeba na kusafirisha kiwango kikubwa zaidi cha oksijeni. Hili litapelekea kuwepo kwa kiwango kizuri cha oksjeni kwenye mwili wako.

Kumbuka! Kila kitu kinatakiwa kuwa cha kiasi ili kiwe na manufaa kwako. Kukaa muda mrefu sana kwenye jua kunaweza kukuletea madhara. Inashauriwa kukaa angalau dakika 10 hadi 15 ili upate manufaa kiafya.

Shopping Cart
1
    1
    Your Cart
    🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About