Sala za Katoliki: Sala Muhimu Kwa Mkristu Mkatoliki

Sala kwa Mtakatifu Yosefu

Ee Yosef mwenye heri, tunakimbilia kwako, katika masumbuko yetu, na kishaomba shime ya Mchumba wako Mtakatifu, tunaomba pia kwa matumaini usimamizi wako. Kwa ajili ya mapendo uliyompenda nayo Bikira Mtakatifu, Mzazi wa Mungu, na kwa ajili ya tunza ya Baba, uliyomtunza nayo Mtoto Yesu, tunakuomba sana, utuangalie kwa wema, sisi tuliokuwa fungu lake Yesu Kristo, tuliokombolewa kwa damu yake, utusimamie katika masumbuko yetu, kwa enzi na shime yako.
Ee Mlinzi amini wa Jamaa Takatifu, uwakinge watoto wateule wa Yesu Kristo, ee Baba uliyetupenda mno, utuepusha na kilema chochote cha madanganyo na upotevu. Ee kinga yetu mwezaji,utusimamie huko juu mbinguni ulipo, tunaposhindana na wenye nguvu wakaao gizani. Kama vile siku za kale ukamwokoa Mtoto Yesu katika hatari ya kuuawa, na leo hivi, ulikinge Kanisa Takatifu la Mungu katika mitego ya adui, na katika shida yote, mtunze daima kila mmoja wetu, tupate mfano wako, tusaidie kwa msaada wako, kukaa na utakatifu maisha, kufa kifo chema, na kupokelewa mbinguni makao ya raha milele. Amina

SALA YA NOVENA YA SIKU TISA KWA MT. YOSEFU, YA ZAMANI, MIAKA 1900 ILIYOPITA

Ee Mt. Yosefu, ambaye ulinzi wako ni mkubwa, wenye nguvu na wa haraka mbele ya Kiti cha Enzi cha Mungu, ninakukabidhi nia na haja zangu zote. Ee Mt. Yosefu, unisaidie kwa maombezi yako yenye nguvu, na unipatie kutoka kwa Mwanao Mungu, baraka zote za kiroho, kwa njia ya Kristu Bwana wetu, ili nikishapata msaada wako wa mbinguni ningali bado hapa duniani, niweze nami kumsifu, kumwabudu na kumshukuru Mungu aliye Baba mwema kabisa kushinda wote. Ee Mt. Yosefu, sichoki kamwe kufikiri moyoni kwa upendo, jinsi Mtoto Yesu alivyokuwa amesinzia mikononi mwako. Akiwa amepumzika hivyo karibu na moyo wako, sithubutu kujongea, nisije nikamsumbua, bali nakuomba wewe umkumbatie na kumbusu kwa niaba yangu na kumwambia anipe busu lake nitakapovuta pumzi yangu ya mwisho.
Mtakatifu Yosefu Msimamizi wa wanaozimia roho; Utuombee.
Amina.

Sala hii ilipatikana katika mwaka wa hamsini wa Bwana na Mwokozi Wetu Yesu Kristu. Mnamo mwaka 1505 Baba Mtakatifu alimtumia sala hii Mfalme Charles wakati alipokuwa anaenda vitani. Yeyote atakayeisoma sala hii, au kuisikia ikisomwa, au kuibeba, hatakufa kifo cha ghafla,hatazama majini, hatadhurika kwa sumu, wala hataanguka katika mikono ya adui zake, au kuunguzwa katika moto wowote ule, au kushindwa katika vita.

Sali sala hii kwa siku tisa mfululizo, kwa kuomba jambo lolote unalolihitaji. Haijawahi kusikika kuwa sala hii imeshindwa jambo.

Sala ya Saa Tisa

✝⌚✝

Sala ya saa tisa🙏🏾

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. A mina

Yesu, ulikufa, lakini chanzo cha uhai kilitoka kwa ajili ya watu, na bahari ya huruma ilifunguka kwa ajili ya ulimwengu mzima. Ee chemchemi ya Uhai, huruma ya Mungu isiyo na mwisho, ikafunika ulimwengu mzima na ukajimwaga mwenyewe juu yetu.

❣✝❣

✝Ee Damu na Maji, yaliyotoka moyoni mwa Yesu kama chemchemi ya Huruma kwetu. Nakutumainia.

(Mara tatu)

🛐❣🛐

SALA YA MTU ALIYEKABILIWA NA MATATIZO MBALIMBALI

Ewe Mtakatifu Yuda Tadei,/ mtume mtukufu na shahidi wa Kristo,/ umesifika pote kwa wepesi wako wa kutoa misaada/ kwa wanaokukimbilia katika matatizo yao mazito./ Pia ni mwombezi wa waliopondeka moyo./

Mimi ni mmoja wa hao./ Nakujia na moyo uliojaa shida na matatizo./ Nakusihi kwa moyo wote/ unisaidie kwa maombezi yako yenye nguvu/ kufikia utatuzi unaofaa kadiri ya mapenzi ya Mungu./ Maisha yangu yamejaa misalaba,/ siku kwa siku matatizo hayapungui./ Moyo wangu umekuwa bahari ya siki chungu sana./ Mapito yangu nayaona yamejaa miiba mikali./ Roho yangu imezama katika dimbwi la machozi na kite./ Nafsi yangu imezingirwa na giza nene./ Ghasia na kukatishwa tamaa ya kuishi/ hunyemelea roho yangu./ Maongozi ya Mungu na imani naviona vinanitoka kidogo kwa kidogo./

Nikielemewa na mawazo kama hayo/ najikuta sina nguvu za kuishi,/ na maisha kwangu ni msalaba mzito/ ninaouogopa hata kuunyakua./ Wewe unaweza kabisa kunitoa katika balaa hili./ Sitaacha kukusihi/ hadi hapo utakaponisaidia/ au kunijulisha mapenzi ya Mungu kwangu./ Natangulia kutoa shukrani kwa jibu liwalo lote.

ROSARI YA BIKIRA MARIA MAMA WA MSAADA WA DAIMA

Namna ya kusali Rozari kwa Bikira Maria Mama wa Msaada wa Daima

(Tumia rosari ya kawaida)

Mwanzo, kwenye Msalaba:

Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.

Kwenye chembe ndogo za awali:

K: Ee Mungu utuelekezee msaada W: Ee Bwana utusaidie hima
W: Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Kama mwanzo na sasa na siku zote na milele. Amina.

Maria ametusaidia,
Maria anataka kutusaidia,
Maria anaweza kutusaidia,
Maria atatusaidia.

KATIKA KILA FUNGU SALI SALA ZIFUATAZO:

Kwenye chembe kubwa:

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Kama mwanzo na sasa, na siku zote, na milele. Amina.

Maria ametusaidia,
Maria anataka kutusaidia,
Maria anaweza kutusaidia,
Maria atatusaidia.

Ee Maria Mama wa Msaada wa daima
Sikiliza maombi ya roho zetu
Unaweza kutusaidia katika mahitaji yetu
Ee Maria kwa matumaini twakuita wewe.

Kwenye chembe ndogo:

Kama unasali mwenyewe: “Ee Maria, utusaidie! (mara kumi)
Kama mnasali zaidi ya mmoja kwa pamoja: K; Ee Maria, W: Utusaidie. (mara kumi)

MWISHO SALI SALA ZIFUATAZO:

Salamu Maria

Salamu Maria, umejaa neema, Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu Mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa, na saa ya kufa kwetu. Amina. (mara tatu)

Tunaukimbilia

Tunaukimbilia ulinzi wako, ee Mzazi Mtakatifu wa Mungu, usitunyime tukiomba katika shida zetu, utuokoe siku zote, kila tuingiapo hatarini, ee Bikira Mtukufu na mwenye baraka,. Amina.

Sala ya Malaika wa Bwana

Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria, naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Salamu Maria,….

Ndimi Mtumishi wa Bwana, nitendewe ulivyonena. Salamu Maria, ……
Neno wa Bwana akatwaa Mwili, akakaa kwetu. Salamu Maria, …..

Utuombee, ee Mzazi Mtakatifu wa Mungu, tujaliwe ahadi za Kristo.

Tuombe:

Tunakuomba ee Bwana, utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika, kwamba, Kristo Mwanao amejifanya mtu: kwa mateso na Msalaba wake, utufikishe kwenye utukufu wa ufufuko. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu, Amina.

Sala ya Kuombea Hali njema ya hewa na mvua

Ee Mungu Mwenyezi wa milele, mpaji wa mema yote, unayetusamehe na kutulinda. Utujalie sisi tunaokusihi, tufurahie hali njema ya hewa na mvua tunayoitamani na kuhitaji. Tutumie daima vipawa vya wema wako kwa ajili ya utukufu wa jina lako, na kwa ajili ya wokovu watu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana watu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele. Amina. `

`Baba Yetu………………. Salama Maria………… Atukuzwe Baba……….. `

K: `Bikra Maria mama wa msaada wa daima…. W: Utuombee na Utusaidie`

SALA YA MAOMBI KWA MOYO MTAKATIFU WA YESU

Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakukimbilia, ninakuja kwako katika mikono yako yenye huruma. Ndiwe tegemeo langu na tumaini langu dhabiti. Ndiwe mwenye dawa ya maovu yangu yote, malipizi ya makosa yangu yote. Waweza kunipatia haja zangu na neema ninazoziomba mimi na wengine. Wewe uko ili kutusaidia sote, ndiwe mwanga mkuu usiozimika, ndiwe chanzo cha nguvu, uvumilivu, amani na faraja. Nina hakika kuwa maombi yangu hayatakuchosha, nawe hutaacha kunisaidia, kunilinda, kunipenda, kwani, ee Moyo Mtakatifu , upendo wako hauna mwisho. Ee Moyo Mtakatifu, unihurumie, kwa ajili ya maombi yangu, kadiri ya huruma yako. Nawe katika sisi, na kwa ajili yetu, ufanye lolote unalolihitaji, kwani tunajitoa kwako kwa imani na uhakika thabiti kwamba kamwe hautatuacha, kwa milele. Amina.

SALA YA KUMWOMBA MTAKATIFU TERESIA WA MTOTO YESU

Ee Mtakatifu Teresia wa mtoto Yesu, ulistahili kuitwa Msimamizi wa misioni katoliki za dunia yote. Kumbuka ile tamaa yako kuu uliyoonyesha huku duniani ya ” kusimika Msalaba wa Yesu Kristu, katika nchi zote na kuhubiri Injili mpaka mwisho wa dunia” . Twakuomba kwa ajili ya maagano yako, wasaidie mapadre, wamisionari, na kanisa zima.

Ee Mtakatifu Teresia wa mtoto Yesu ” Msimamizi wa misioni” UTUOMBEE

LITANIA YA KUWAOMBEA MAPADRE WOTE II

Kwa ajili ya Baba Mtakatifu wetu ..(N); Bwana, umpe moyo wako wa uchungaji mwema
Kwa ajili ya makardinali na maaskofu wakuu; Uwape moyo wa kichungaji ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wa majimbo; Uwajaze na Roho wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre watawa; Wakamilishe katika wito wao ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre walioko hatarini; Uwaokoe ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wenye udhaifu; Uwatie nguvu ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wenye hofu; Uwape amani ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre waliokata tamaa; Uwavuvie upya ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wakaao upweke; Uwasindikize ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wamisionari; Uwalinde ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wanaohubiri; Uwaangazie ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre na watawa waliokufa; Uwafikishe kwenye utukufu wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie hekima na ufahamu wako ee Bwana
Kwa ajili ya mapadre wote; Uwajalie elimu na shauri lako
Kwa ajili ya mapadre wako; wajalie wakuheshimu na wakuogope
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie subira na upendo
Kwa ajili ya mapadre wote; wajalie utii na upole
Kwa ajili ya mapadre wote; uwajalie hamu kuu ya kuokoa roho za watu
Kwa ajili ya mapadre wote; wape fadhila za imani, matumaini na mapendo
Kwa ajili ya mapadre wote; Wajalie upendo mkuu kwa Ekaristi
Tunakuomba uwajalie mapadre wote; Waheshimu uhai na hadhi ya mtu ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote nguvu na bidii katika kazi zao ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote amani katika mahangaiko yao ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote upendo mkuu kwa Utatu Mtakatifu ee Bwana
Tunakuomba uwajalie mapadre wote upendo mkuu kwa Bikira Maria ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe mwanga wa Kristo ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wawe chumvi kwa ulimwengu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wajizoeze kujitoa sadaka na kujinyima ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, wawe watakatifu kimwili, kiakili na kiroho ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe watu wa sala ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe kioo cha imani kwako ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wajali sana wongofu wetu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawe waaminifu kwa wito wao wa kikuhani ee Bwana
Uwajalie mapadre wote, ili mikono yao ibariki na kuponya ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wawake moto wa mapendo yako ee Bwana
Uwajalie mapadre wote hatua zao zote ziwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu ee Bwana
Uwajalie mapadre wote wajazwe na Roho Mtakatifu na uwajalie karama zake kwa wingi ee Bwana.

Tuombe.
Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, usikie sala tunazokutolea kwa ajili ya mapadre wetu. Uwajalie wafahamu waziwazi kazi uliyowaitia kuifanya, uwape neema zote wanazohitaji ili waitikie wito wako kwa ushujaa, kwa upendo, na majitoleo yenye udumifu katika mapenzi yako matakatifu. Amina.

SALA KWA MT. YOSEFU KWA WASIO NA AJIRA WAPATE AJIRA

Ee Mt. Yosefu, tunakuomba kwa ajili ya wale asio na ajira, kwa ajili ya wale wanaotaka kujipatia kipato chao na kulisha familia zao.
Wewe u Msimamizi wa wafanyakazi, tujalie kwamba pasiwepo kati yetu mtu asiye na ajira, na kwamba wale wote ambao wako tayari kufanya kazi waweze kuelekeza nguvu zao na uwezo wao katika kuwatumikia wanadamu wenzao na kujipatia kipato halali.

Wewe u Msimamizi wa familia, usiwaache wale wenye watoto wa kuwatunza na kuwalea wakose namna ya kufanya hivyo. Uwahurumie ndugu zetu waliokosa ajira na kugubikwa na umasikini kwa sababu ya magonjwa au mipango mibaya ya kijamii. Wasaidie viongozi wetu wa kisiasa na walioshika usukani katika nyanja mbalimbali za kiuzalishaji wavumbue suluhu mpya na za haki za jambo hili. Utujalie ili kila mmoja wetu apate kujipatia kipato halali na kufurahia fursa ya kushiriki kadri ya uwezo wake, katika maisha bora zaidi kwa wote. Utujalie ili wote tushiriki pamoja katika raslimali alizotujalia Mungu, na pia utujalie tuwe tayari daima kuwasaidia wale walio wahitaji kuliko sisi.
Amina.

Litani ya Bikira Maria

  • Bwana utuhurumie
  • Bwana utuhurumie
  • Kristo utuhurumie
  • Bwana utuhurumie
  • Bwana utuhurumie
  • Kristo utusikie
  • Kristo utusikilize
  • Mungu Baba wa Mbinguni,…… Utuhurumie
  • Mungu Mwana Mkombozi wa dunia ……… Utuhurumie
  • Mungu Roho Mtakatifu …….. Utuhurumie
  • Utatu Mtakatifu Mungu Mmoja …….. Utuhurumie
  • Maria Mtakatifu ………. utuombee
  • Mzazi Mtakatifu wa Mungu …….. utuombee
  • Bikira Mtakatifu Mkuu wa Mabikira …….. utuombee
  • Mama wa Kristo ……… utuombee
  • Mama wa Neema ya Mungu ………….. utuombee
  • Mama Mtakatifu sana ……… utuombee
  • Mama mwenye usafi wa Moyo ……….. utuombee
  • Mama mwenye ubikira ……….. utuombee
  • Mama usiye na doa ……….. utuombee
  • Mama mpendelevu ………. utuombee
  • Mama mstajabivu ………. utuombee
  • Mama wa Muumba ………. utuombee
  • Mama wa Mkombozi ………….. utuombee
  • Mama wa Kanisa……….. utuombee
  • Bikira mwenye utaratibu ………….. utuombee
  • Bikira mwenye heshima ………….. utuombee
  • Bikira mwenye sifa ………….. utuombee
  • Bikira mwenye uwezo ………….. utuombee
  • Bikra mweye huruma ………….. utuombee
  • Bikra mwaminifu………….. utuombee
  • Kioo cha haki ………….. utuombee
  • Kikao cha hekima ………….. utuombee
  • Sababu ya furaha yetu ………….. utuombee
  • Chombo cha neema ………….. utuombee
  • Chombo cha kuheshimiwa ………….. utuombee
  • Chombo bora cha ibada ………….. utuombee
  • Waridi lenye fumbo ………….. utuombee
  • Mnara wa Daudi ………….. utuombee
  • Mnara wa pembe ………….. utuombee
  • Nyumba ya dhahabu ………….. utuombee
  • Sanduku la Agano ………….. utuombee
  • Mlango wa Mbingu ………….. utuombee
  • Nyota ya asubuhi ………….. utuombee
  • Afya ya wagonjwa ………….. utuombee
  • Kimbilio la wakosefu ………….. utuombee
  • Mtuliza wenye huzuni ………….. utuombee
  • Msaada wa waKristo ………….. utuombee
  • Malkia wa Malaika ………….. utuombee
  • Malkia wa Mababu ………….. utuombee
  • Malkia wa Manabii ………….. utuombee
  • Malkia wa Mitume ………….. utuombee
  • Malkia wa Mashahidi ………….. utuombee
  • Malkia wa Waungama dini ………….. utuombee
  • Malkia wa Mabikira ………….. utuombee
  • Malkia wa Watakatifu wote ………….. utuombee
  • Malkia uliyepalizwa Mbinguni ………….. utuombee
  • Malkia wa Rozari takatifu ………….. utuombee
  • Malkia wa amani ………….. utuombee

  • Mwanakodoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia,…………..Utusamehe ee Bwana.
  • Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia,…………..Utusikilize ee Bwana
  • Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za dunia,…………..Utuhurumie.

  • Utuombee, Mzazi Mtakatifu wa Mungu,…………..Tujaliwe ahadi za Kristo.

Tuombe

Ee Bwana Mungu, utujalie sisi watumishi wako afya ya roho na mwili siku zote; na kwa maombezi matukufu ya Maria Mtakaatifu Bikira daima, tuopolewe na mashaka ya saa, tupate na furaha za milele. Kwa Kristo Bwana wetu, Amina.

Shopping Cart
🏠 Home 📖 Reading 🖼️ Gallery 💬 AI Chat 📘 About