Sala za Katoliki: Sala Muhimu Kwa Mkristu Mkatoliki

Kanuni ya imani

Nasadiki kwa Mungu, Baba Mwenyezi,/ mwumba mbingu na dunia./ Na kwa Yesu Kristu, Mwanaye wa pekee, Bwana wetu;/ aliyetungwa kwa Roho Mtakatifu,/ akazaliwa na Bikira Maria,/ akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato,/ akasulubiwa, akafa, akazikwa,/ akashukia kuzimu;/ siku ya tatu akafufuka katika wafu;/ akapaa mbinguni;/ amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi;/ toka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu,/ Kanisa takatifu katoliki,/ ushirika wa Watakatifu,/ maondoleo ya dhambi,/ ufufuko wa miili,/ uzima wa milele. Amina.

SALA MBELE YA SAKRAMENTI KUU I

Utukuzwe ee Bwana wangu Yesu Kristo./ Uliagua kifo chako./ Katika karamu ya mwisho ulitumia mkate wa kidunia/ ukafanya mwujiza na kuugeuza/ kuwa Mwili wako azizi./ Kwa mapendo ukawapa Mitume Mwili huo/ uwe kumbukumbu la mateso yako mastahivu./ Uliwaosha miguu kwa Mikono yako Mitakatifu./

Uheshimiwe, ee Bwana wangu Yesu Kristo./ Kwa kuhofu mateso na kifo,/ Mwili wako usio na kosa ulitoka jasho la damu/ badala ya maji./ Juu ya hayo uliutimiza wokovu wetu/ uliokuwa umetaka kuufanya./ Hivyo ulionyesha waziwazi mapendo yako/ uliyo nayo kwa wanadamu./

Utukuzwe, ee Bwana wangu Yesu Kristo./ Ulipelekwa kwa Kayafa,/ Wewe uliye Hakimu wa wote./ Ukaruhusu kwa unyenyekevu kutolewa kwa Pilato/ uhukumiwe naye./

Utukufu uwe nawe, Bwana wangu Yesu Kristo,/ kwa kuwa ulivumilia kuchekwa tena/ uliposimama huko,/ umevaa joho jekundu,/ umetiwa taji ya miiba mikali sana Kichwani,/ ukavumilia kwa saburi kubwa/ kutemewa mate katika Uso wako mzuri,/ kufumbwa Macho,/ na kupigwa mno na wajeuri/ ngumi na makofi Mashavuni na Shingoni./

Sifa iwe nawe, Bwana wangu Yesu Kristo,/ Kwa uvumilivu mkubwa ulikubali kufungwa nguzoni,/ kupigwa mijeledi kijeuri,/ kujaa damu na hivyo kusukumwa barazani kwa Pilato./ Ulionekana kama mwanakondoo asiye na kosa./

Heshima iwe nawe, Bwana wangu Yesu Kristo./ Umehukumiwa Mwili wako mzima/ Mtukufu wenye kutoka damu/ ufe msalabani./ Ulichukua msalaba kwa Mabega yako Matakatifu/ na kuumwa sana./ Kwa ghadhabu walikusukuma mbele/ mpaka mahali pa mateso,/ wakakunyangโ€™anya nguo zako./ Hivyo ulikubali kupigiliwa msalabani./

Heshima ya milele upate Wewe,/ Bwana wangu Yesu Kristo./ Ulipokuwa katika taabu kubwa hii,/ ulimkazia Mama yako mstahivu/ Macho yako ya hisani na mapendo/ na unyenyekevu,/ ndiye Mama yako asiyekosa hata mara moja/ wala kukubali dhambi yeyote./ Ulimweka katika ulinzi mwaminifu/ wa Mfuasi wako ili kumtuliza./

Milele utukuzwe, ee Bwana wangu Yesu Kristo./ Ulipokuwa mwenyewe taabani,/ uliwapa wakosefu wote/ matumaini ya kuondolewa dhambi/ kwa kumwahidia mnyangโ€™anyi aliyekuendea/ utukufu wa paradisi kwa huruma yako./

Sifa ya milele iwe nawe, Bwana wangu Yesu Kristo,/ kwa kila saa ulipovumilia uchungu/ na taabu kubwa mno msalabani kwa ajili yetu sisi wakosefu,/ maumivu makali sana/ yaliyotoka katika majeraha yako,/ yakapenya bila huruma Roho yako Takatifu./ Yakaingia kikatili katika Moyo wako Mtakatifu/ hata ukakatika,/ ukapumua Roho yako,/ ukainama Kichwa,/ ukaweka Roho yako mikononi mwa Mungu, Baba yako./ Na baada ya kufa uliacha nyuma Mwili baridi./

Utukuzwe, ee Bwana wangu Yesu Kristo,/ kwa Damu yako azizi na kwa kifo chako kitakatifu/ ulizifidia roho za watu,/ ukazitoa ugenini/ na kuzipeleka kwa hisani yako katika uzima wa milele./

Milele uheshimiwe, Wewe Bwana wangu Yesu Kristo./ Siku ya tatu ulifufuka katika wafu,/ ukajionyesha kwa wafuasi wako,/ ukapaa mbinguni/ mbele ya macho yao siku ya arobaini./

Shangilio na sifa ya milele upate Wewe, Bwana wangu Yesu Kristo,/ kwa kuwa umewapelekea wafuasi wako mioyoni mwao/ Roho Mtakatifu,/ ukawasha rohoni mwao mapendo makuu ya Mungu./

Pia, utukuzwe, usifiwe na kushangiliwa milele, Bwana wangu Yesu Kristo./ Umekaa katika ufalme wako wa mbinguni/ juu ya kiti cha enzi cha Umungu wako,/ ukaishi pamoja na Viungo vyako vyote Vitakatifu./ Na hivyo utakuja tena/ kuzihukumu roho za wazima na wafu wote./ Unaishi na kutawala/ pamoja na Baba na Roho Mtakatifu,/ milele. Amina.

(Na Mt. Birgita wa Sweden)

SALA MBELE YA KITI CHA ENZI CHA MUNGU

Sali Atukuzwe 7 kwa heshima ya Malaika 7 wateule ujipatie neema ya kuepa dhambi mbaya saba na kutujaza mapaji saba ya Roho Mtakatifu.

TUOMBE
Ee Mungu Mwenyezi wa milele, kwa wema na huruma yako ya ajabu, umetaka watu wako waokoke, ukamweka Malaika Mkuu Mikaeli kuwa Mkuu wa Kanisa lako, Utukinge na adui zetu, wasitusmbue saa ya kufa kwetu, bali tuongozwe naye kwenye utukufu wako Mkuu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana Wetu Yesu Kristo. Amina.

Utuombee Ee Mtukufu Mtakatifu Mikaeli Mkuu wa Kanisa la Yesu Kristo, tujaliwe ahadi za Kristo. Amina.

SALA YA KUMWABUDU BWANA YESU KATIKA SAKRAMENTI TAKATIFU

Ee Yesu Kristu,/ Bwana wangu na Mungu wangu/ ambaye ninasadiki kuwa upo hapa/ katika Sakramenti Takatifu ya Altare;/ pokea kitendo hiki cha kukuangukia kifudi fudi/ kama ishara ya tamaa niliyonayo ya kukuabudu Wewe/ bila kuchoka/ na kukushukuru kwa mapendo yako makubwa/ yasiyo na kipimo/ ambayo Moyo wako Mtakatifu sana/ unawaka katika Sakramenti Takatifu hii./ Siwezi kukushukuru vizuri zaidi/ kuliko kama ningetolea kwako/ matendo yangu yote ya kukuabudu/ unyenyekevu wangu/ uvumilivu na mapendo/ ambayo huu Moyo Mwabudiwa ulifanya,/ bado unafanya/ na utaendelea kufanya katika uzima wa milele mbinguni./ Ninaahidi kupitia Moyo huu,/ nitakupenda,/ nitakutukuza,/ na nitakuabudu kama nitakavyoweza./ Ninajiunganisha na hii Sadaka Takatifu/ ambayo unatoa kwa Baba Mungu/ na ninatolea kwako utu wangu./ Ninakuomba kuangamiza ndani yangu/ dhambi zote pamoja na majeraha yake/ na usikubali kunitenga nawe milele./ Amina.

(Na Mt. Margareta Maria Alakoki)

SALA YA KUUABUDU MOYO MTAKATIFU WA YESU KATIKA EKARISTI TAKATIFU

Kwa nguvu zangu zote za moyo wangu/ ninakuabudu ee Moyo Mtakatifu/ na Mwabudiwa sana,/ Moyo Mtakatifu wa Bwana wetu Yesu Kristu/ ambao ninataka kumpenda/ na kukusalimu kwa usikivu unaoendelea./ Kamwe nisikuudhi tena/ kwa sababu Wewe ni Mwema sana;/ Ee Mwema sana./ Ee Moyo Mtakatifu sana/ ninakupenda/ na ninataka kukupenda zaidi ya vitu vyote,/ kwa nguvu zangu zote/ na kwa uwezo wangu wote,/ ninatamani kuwa mali yako/ Wewe uliyejitoa Msalabani kwa ajili yangu/ kwa mateso makali./ Unionee huruma na udhaifu wangu/ na usiniruhusu kupotea./

Ninajitoa kabisa kwako/ ee moyo wa mapendo,/ kwa makusudi kuwa utu wangu,/ maisha na mateso yangu/ yalipie kukupenda,/ kukuheshimu/ na kukutukuza Wewe sasa na milele./ Ninakupenda ee Moyo Mwabudiwa wa Mwokozi wangu,/ ninakuomba kwako/ uamuru moyo wangu na kila kitu ndani yangu/ kikutukuze sasa na milele./ Amina.

(Na Mt Margareta Maria Alakoki)

SALA YA JIONI

TUNAKUSHUKURU, EE MUNGU KWA MAPAJI YOTE ULIYOTUJALIA LEO AMINA

BABA YETUโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆ.. SALAMU MARIAโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆ.

SALA YA IMANIโ€ฆโ€ฆ.YA MATUMAINIโ€ฆโ€ฆโ€ฆYA MAPENDO

SALA YA KUTUBU

TUWAZE KATIKA MOYO WETU MAKOSA YA LEO TULIYOMKOSEA MUNGU KWA MAWAZO,KWA MANENO, KWA VITENDO NA KWA KUTOTIMIZA WAJIBU (HUSUBIRI KIDOGO)
NAKUUNGAMIA MUNGU MWENYEZI,NANYI NDUGU ZANGU,KWANI NIMEKOSA MNO KWA MAWAZO,KWA MANENO,KWA VITENDO NA KWA KUTOTIMIZA WAJIBU,NIMEKOSA MIMI,NIMEKOSA SANA.NDIYO MAANA NAKUOMBA MARIA MWENYE HERI,BIKIRA DAIMA,MALAIKA NA WATAKATIFU WOTE,NANYI NDUGU ZANGU,MNIOMBEENI KWA BWANA MUNGU WETU.

MUMNU MWENYEZI ATUHURUMIE ATUSAMEHE DHAMBI ZETU,ATUFIKISHE KWENYE UZIMA WA MILELE.AMINA

SALA YA KUOMBEA WATUโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆ
KUSIFUโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆโ€ฆ

SALA KWA MT. YOSEFU KWA WASIO NA AJIRA WAPATE AJIRA

Ee Mt. Yosefu, tunakuomba kwa ajili ya wale asio na ajira, kwa ajili ya wale wanaotaka kujipatia kipato chao na kulisha familia zao.
Wewe u Msimamizi wa wafanyakazi, tujalie kwamba pasiwepo kati yetu mtu asiye na ajira, na kwamba wale wote ambao wako tayari kufanya kazi waweze kuelekeza nguvu zao na uwezo wao katika kuwatumikia wanadamu wenzao na kujipatia kipato halali.

Wewe u Msimamizi wa familia, usiwaache wale wenye watoto wa kuwatunza na kuwalea wakose namna ya kufanya hivyo. Uwahurumie ndugu zetu waliokosa ajira na kugubikwa na umasikini kwa sababu ya magonjwa au mipango mibaya ya kijamii. Wasaidie viongozi wetu wa kisiasa na walioshika usukani katika nyanja mbalimbali za kiuzalishaji wavumbue suluhu mpya na za haki za jambo hili. Utujalie ili kila mmoja wetu apate kujipatia kipato halali na kufurahia fursa ya kushiriki kadri ya uwezo wake, katika maisha bora zaidi kwa wote. Utujalie ili wote tushiriki pamoja katika raslimali alizotujalia Mungu, na pia utujalie tuwe tayari daima kuwasaidia wale walio wahitaji kuliko sisi.
Amina.

SALA YA NOVENA KWA MOYO MTAKATIFU WA YESU

Ee Moyo Mtakatifu sana wa Yesu, chemchemi ya kila baraka, ninakuabudu, ninakupenda, na kwa majuto halisi ya dhambi zangu, nakutolea moyo wangu dhaifu. Nifanye mnyenyekevu, mvumilivu na safi, nikikubali na kuyatii kabisa mapenzi yako. Ee Yesu mwema, unijalie niishi nawe na kwa ajili yako. Unilinde niwapo katikati ya hatari, unifariji katika mateso, unipe afya ya mwili na msaada katika mahitaji ya mwili, Baraka yako juu ya kila nilifanyalo, na neema ya kifo chema. Amina.

Ee Yesu uliyesema โ€œKweli nawaambieni, ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtapata, gongeni nanyi mtafunguliwaโ€, tazama ninagonga, ninatafuta na kuomba โ€ฆโ€ฆ.. (Taja ombi lako)
Baba Yetuโ€ฆ.., Salamu Maria โ€ฆโ€ฆ.., Atukuzwe Babaโ€ฆโ€ฆ..
Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutumainia kwa moyo wote!

Ee Yesu uliyesema โ€œKweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu mtapewaโ€, tazama kwa jina lako ninaomba โ€ฆโ€ฆ. (Taja ombi lako)
Baba Yetuโ€ฆ.., Salamu Maria โ€ฆโ€ฆ.., Atukuzwe Babaโ€ฆโ€ฆ..
Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutumainia kwa moyo wote!

Ee Yesu uliyesema โ€œKweli nawaambieni, mbingu na dunia zitapita lakini maneno yangu hayatapita kamweโ€, tazama, nikitiwa nguvu na maneno yako ya kweli ninaomba โ€ฆโ€ฆ.. (Taja ombi lako)
Baba Yetuโ€ฆ.., Salamu Maria โ€ฆโ€ฆ.., Atukuzwe Babaโ€ฆโ€ฆ..
Moyo Mtakatifu wa Yesu, ninakutumainia kwa moyo wote!

Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambaye kwako ni kitu kimoja tu kisichowezekana, ambacho ni kutoacha kutowaonea huruma wenye huzuni, utuhurumie sisi wakosefu maskini na utujalie neema tukuombayo kwa njia ya Moyo Imakulata wa Maria, Mama yetu mpole.

Sali โ€˜Salamu Malkiaโ€™ na kuongezea, โ€˜Mtakatifu Yosefu Baba Mlishi wa Yesu, utuombeeโ€™.

P.S. โ€“ Sala hii ya Novena ilisaliwa kila siku na PADRE PIO kwa ajili ya kuwaombea wale wote waliomwomba msaada wa sala zake. Unaweza kuisali kwa namna tofauti tofauti. Mfano, kama Novena ya siku tisa, ambapo unasali sala hii mara moja au zaidi kila siku kwa siku tisa, au unaweza kuifanya kama Novena ya masaa, ambapo unasali sala hii kila baada ya saa moja kwa masaa tisa kwa siku hiyo hiyo, hasa kama kitu unachokiomba ni cha haraka au umesongwa moyoni. Vilevile unaweza kuifanya sala hii kama sehemu ya sala zako za kila siku katika mwezi Juni ambao ni mwezi uliotengwa na Kanisa kwa ajili ya kuuheshimu Moyo Mtakatifu wa Yesu, na hapo utaitumia kuwaombea watu waliokuomba msaada wa sala zako kama alivyofanya Mtakatifu Padre Pio. Pia unaweza kuitumia kama sala yako ya siku zote au ya mara kwa mara kwa ajili ya mahitaji mbalimbali.

KUJIWEKA CHINI YA ULINZI WA MT. YOSEFU

Ee Mt. Yosefu, Baba Mlishi wa Mwokozi wangu, na mchumba safi wa Mama wa Mungu, leo ninakuchagua wewe, kama mwombezi wangu kwa Mungu Mwenyezi, na pia kama mfano wangu, na mlinzi wangu, na baba yangu, katika bonde hili la ugenini.

Ee Mt. Yosefu, ambaye Bwana alikufanya mlinzi wa Familia yake, ninakuomba uwe mlinzi wangu mwema katika mambo yangu yote. Uniwashie moyoni mwangu moto wa mapendo makuu kwa Yesu, na uniwezeshe kumtumikia kwa bidii na kwa uaminifu kwa mfano wako. Nisaidie katika udhaifu wangu katika kumheshimu Mama Maria kama Mwombezi wangu.

Daima uwe kiongozi wangu katika njia ya fadhila na ibada, na unijalie, baada ya kukufuasa kwa uaminifu katika njia ya haki, nipate ulinzi wako wenye nguvu katika saa ya kufa kwangu.
Amina

SALA YA KUWAOMBEA MAPADRE

Ee Bwana Yesu Kristo. Mkombozi wetu, kwa mapendo na tamaa yako ya kutaka kulinda vema Kanisa lako, ukachagua Mapadri wawe Wachungaji na Viongozi wa roho za watu. Nakuomba sana; ubariki nia na bidii inayowapasa Mapadri wote katika kazi zao. Uwaongezee Utakatifu.

Uwatie moyo mzuri wenye mapendo makubwa kwako na roho za watu. Hivyo wakiisha kupata wenyewe Utakatifu, waweze kuwaongoza vizuri watu walio chini ya ulinzi wao, katika njia ya Utakatifu na furaha ya milele. Uwajalie neema zote za hali ya Upadri. Uwajalie ili waonyeshe kila siku ya maisha yao mfano wa kila fadhila ya mapendo na ya uaminifu katika Kanisa, kwa Baba Mtakatifu na kwa Maaskofu.

Yesu mpendelevu, uangalie kwa mapendo kazi na mateso ya Mapadri wako; ubariki na ustawishe mafundisho yao; wanapowafundisha watoto, wanapowahubiria watu, wanapowatuliza wakosefu watubu na wanapowasaidia wagonjwa na wale wanaokaribia mauti, Ee Yesu uwe pamoja nao. Uwakinge na hatari zote za roho na za mwili.

Mwokozi Yesu, ulijalie Kanisa liwe na Mapadri wengi walio Watakatifu. Uwajalie watoto na vijana wengi wasikie wito wa Upadri, uwatie furaha na Utakatifu na roho za Mapadri waliokufa uzijalie punziko la amani.

Kwa mimi mwenyewe Ee Yesu mpendelevu, naomba unijalie roho ya imani na utii mnyenyekevu ili niwaheshimu Mapadri kama Mawakili wa Mungu. Niwatii katika njia zote za wokovu wa roho yangu. Amina.

Majitoleo kwa Bikira Maria

(Sala iliyotungwa na Mtk. Aloisi)
Bibi yangu mtukufu Maria, nakuwekea amana ya roho yangu na mwili wangu, nikikuomba uipokee amana yangu, kuitunzia ulinzi mwema ulinzi bora, ninakuaminia na kila neno langu, matumaini na kitulizo na kisongo chote, na masumbuko na uzima na ukomo wa uzima wangu: nitakayo ndiyo unifanyizie kwa maombezi na stahili zako, ili mambo yangu yote yapate kuongoka, yakiwa na kufuata mapenzi yako, pamoja na mapenzi ya Mwanao. Amina.

ROZARI YA MOYO MTAKATIFU WA YESU

Tumia tasbihi ya kawaida yenye chembe ndogo 53.

Kwenye Msalaba Sali:

โ€œEe Yesu tupe moyo wako kama amana ya upendo wako na kimbilio letu, ili tupate pumziko salama wakati wa maisha yetu na faraja tamu saa ya kufa kwetuโ€.
Baba Yetu โ€ฆโ€ฆ..
Salamu Maria โ€ฆโ€ฆ. (mara tatu)
Nasadiki โ€ฆโ€ฆโ€ฆ..

Kwenye chembe kubwa Sali (Badala ya โ€˜Baba Yetuโ€™):

โ€œNinakuabudu, ninakutukuza na ninakupenda, Ee Moyo wa Yesu wangu mpenzi, uliopenywa na huzuni nyingi kwa ajili ya dhambi, ambazo zimekuwa zikitendwa hata leo, dhidi ya Sakramenti Takatifu sana ya Altare. Ninakutolea hapo kwa kuridhika, moyo wa Mama yako mpendevu, na mastahili ya watakatifu. Aminaโ€.

Kwenye chembe ndogo sali (Badala ya โ€˜Salamu Mariaโ€™):

โ€œEe Moyo Mtakatifu wa Yesu, uwakao mapendo kwetu, washa nyoyo zetu kwa mapendo yako”

Shopping Cart
25
    25
    Your Cart
    ๐Ÿ  Home ๐Ÿ“– Reading ๐Ÿ–ผ๏ธ Gallery ๐Ÿ’ฌ AI Chat ๐Ÿ“˜ About