Sala za Katoliki: Sala Muhimu Kwa Mkristu Mkatoliki

SALA YA KUANGUKA MIGUUNI PA BWANA YESU KATIKA EKARISTI

Ee Yesu Mfungwa wa Upendo wa Mungu,/ ninapofikiri Upendo wako na jinsi ulivyojitolea kwa ajili yangu,/ nashindwa kuelewa./ Unaficha Ukuu wako usiofahamika/ na kujidhihirisha kwa ajili yangu mimi mnyonge./ Ee Mfalme wa utukufu,/ unaficha uzuri wako,/ lakini jicho la moyo wangu/ linapenya pazia na kuona Majeshi ya Malaika/ wakikuimbia kwa heshima bila kukoma/ na nguvu zote mbinguni zikikusifu bila mwisho zikisema:/ โ€œMtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu..โ€/

Ni nani awezaye kufahamu Upendo wako/ na huruma yako isiyo na kipimo kwa ajili yetu!/ Ee Mfungwa wa Upendo,/ nafungia moyo wangu masikini/ kwenye Tabarnakulo hii/ ili niweze kukuabudu usiku na mchana bila mwisho./ Najua hakuna kizuizi/ na hata kama naonekana kukaa mbali,/ lakini moyo wangu u pamoja nawe/ katika ibada hii./ Hakuna kinachoweza kuzuia upendo wangu kwako./ Kwangu hakuna kizuizi chochote./

Ee Utatu Mtakatifu,/ Mungu Mmoja usiyegawanyika,/ utukuzwe kwa zawadi yako hii kuu/ na agano hili la huruma!/

Nakuabudu,/ Bwana na Muumba uliyefichika katika Sakramenti Takatifu!/ Ee Bwana,/ nakuabudu kwa kazi zote za mikono yako/ zinazonifunulia Hekima yako kuu,/ Wema wako na Huruma yako kuu./ Uzuri uliousambaza hapa/ Uzuri ulio nao Wewe mwenyewe/ ambaye U Uzuri usioelezeka;/ na ingawaje umejificha na kusitiri uzuri wako,/ jicho langu,/ kwa mwanga wa imani linafika kwako,/ na roho yangu inapata kumtambua Muumba wake/ aliye Uzuri usiopimika,/ ulio juu ya kila uzuri,/ na moyo wangu unazama kabisa katika sala ya kukuabudu./

Bwana wangu na Muumba wangu,/ wema wako wanitia moyo wa kuongea nawe,/ Huruma yako huondoa kiambaza/ kitenganishacho Muumba na kiumbe./ Furaha ya moyo wangu,/ ee Mungu, ni kuongea na Wewe./ Yote ambayo moyo wangu unayatamni nayapata kwako./ Hapa ndipo mwanga wako unaponiangaza akili yangu/ na kuiwezesha kukujua Wewe zaidi na zaidi/ โ€“ ndipo mikondo ya neema inapoutiririkia moyo wangu,/ ndipo roho yangu inapochota uzima wa milele./ Ee Bwana na Muumba wangu,/ licha ya mapaji yote haya,/ unajitoa mwenyewe kwangu,/ ili uweze kujiunganisha na kiumbe dhaifu na maskini./

Ee Kristu,/ nafurahi sana nionapo kwamba unapendwa/ na kwamba sifa na utukufu wako vinaongezwa/ hasa ya Huruma yako./ Ee Kristu,/ sitaacha kamwe kuutukuza wema wako na huruma yako,/ hadi dakika ya mwisho ya maisha yangu./ Kwa kila tone la damu yangu/ na kwa kila pigo la moyo wangu/ naitukuza Huruma yako./ Natamani kugeuzwa kabisa/ na kuwa utenzi wa utukufu wako./ Naomba siku ya kufa kwangu/ popote nitakapokuwa nimelala,/ pigo la mwisho la moyo wangu/ liwe utenzi mpendevu/ usifuo Huruma yako isiyo na kipimo./ Amina

(Na Mt. Faustina Kowalska).

SALA YA UHAI KWA MT. YOSEFU

(Sala hii inafaa sana kwa ajili ya kutetea uhai wa watoto wachanga wakiwa tumboni mwa mama zao, dhidi ya utoaji mimba au hatari nyingine dhidi ya uhai wa binadamu)

Ee Mt. Yosefu, wewe ni Mchumba safi na Mpenzi wa Bikira Maria, u Baba Mlishi wa Yesu, mlinzi na mtunzaji wa Familia Takatifu, na wa familia zote. Tuna imani kabisa katika uangalizi wako uliojaa upendo, juu ya uhai mpya, na uaminifu wako kwa familia.

Tunaweka jitihada zetu chini ya ulinzi wa sala zako. Utusaidie daima katika kutetea zawadi ya uhai wa binadamu, ili ukue hadi uzima wa milele ulioahidiwa na kujaliwa kwetu na Mwanao, Ndugu yetu, Yesu Kristu.
Amina.

SALA YA KUMWOMBA MT. YOSEFU MSAADA (SALA KUU KWA MTAKATIFU YOSEFU)

Ee Mt. Yosefu mwenye heri, tunakimbilia kwako katika masumbuko yetu, na kisha omba shime ya Mchumba wako Mtakatifu, tunaomba pia kwa matumaini usimamizi wako. Kwa ajili ya mapendo uliyompenda Bikira Mtakatifu Mzazi wa Mungu, na kwa ajili ya kumtunza Mtoto Yesu, twakuomba sana, utuangalie kwa wema sie tuliokuwa fungu lake Yesu Kristu, tukakombolewa kwa damu yake. Tusimamie katika masumbuko yetu kwa enzi na shime yako.

Ee Mlinzi amini wa jamaa takatifu, uwakinge watoto wateule wa Yesu Kristu.
Ee Baba uliyetupenda mno tuepushe na kilema chochote cha madanganyo na upotevu. Ee kinga yetu mwezaji, utusimamie huko juu mbinguni ulipo, tunaposhindana na wenye nguvu wakaao gizani. Kama vile siku za kale ukamwopoa Mtoto Yesu katika hatari ya kuuawa, na leo hivi likinge Kanisa Takatifu la Mungu katika mitego ya adui, na katika shida yote; mtunze daima kila mmoja wetu, tufwate mfano wako, ili tupate na msaada wako, kukaa na utakatifu maisha, kufa kifo chema, na kupata mbinguni makao ya raha milele.
Amina.

Shopping Cart